Tuitazame Ilani ya ukomunisti(The communist manifesto)

Red Giant

JF-Expert Member
Mar 9, 2012
15,658
20,890
Pengine ukitoa Biblia na Quran, hakuna kitabu kingine kilichokuwa na impact kubwa katika maisha ya watu kama The communist manifesto. Miaka ya katikati ya 1800 wakomunisti ndiyo walikuwa magaidi wa enzi hizo. Basi katika mikutano yao ya siri wakampa kazi bwana Karl Marx kuandaa ilani yao ambayo itakuwa muongozo kwa wakomunisti wote. Basi Marx na mhisani wake, Friedrich Engels wakaandaa ilani hiyo.
Ni moja ya vitabu vilivyofasiriwa sana duniani. Nafikiri kwa nchi yetu ambayo tumetoka, au bado ni ya kijamaa tulitakiwa tuwe na fasiri ya kitabu hiki zamani sana. Maana hiki ndiyo msingi wa ujamaa duniani.
Kina sehemu nne. Si kirefu lakini pia najua watu humu si wavivu kusoma makala ndefu. Tusameheane kwa typing errors, tutakuja kuiweka sawa.

UTANGULIZI

Kitabu hiki ni fasiri ya kitabu(makala) “The Communist Manifesto” Kilichoandikwa na wanafalsafa wa kijerumani, Karl Marx na Friedrich Engels mwaka 1848. Kwa ufupi, kinazungumzia misuguano ya kitabaka katika jamii, matokeo yake, kukomeshwa kwake na nafasi ya ukomunisti katika hayo yote.
Kabla ya kuanza kusoma ni vizuri ukajua maneno/fasiri hizi.
  • Nguvu za uzalishaji(Productive forces)-Muunganiko wa njia za uzalishaji mali kama ardhi, mashine, miundombinu nk.
  • Zama za kati(Medieval/Middle ages)-Kipindi kutoka karne ya 5-15 A. D huko Ulaya.
  • Utawala wa wateule(Aristocracy)-Utawala wa wachache wanaosemwa kuwa ni wa uzao wa nasaba bora(Nobles). Aina hii ilifanyika sana kwenye zama za kati.
  • Ukabaila(Feudalism)-Mfumo wa uchumi ambao kunakuwa na mabwana na watwana. Ulikuwepo sana kwenye zama za kati.
  • Kazi ya ujira(Wage labour)-Kazi ya kibarua
  • Wahafidhina(Conservatives/Reactionaries)-Watu wanaopinga mabadiliko, Reactionaries wakiwa wahafidhina wenye msimamo mkali wakitaka mambo kurudi kama zamani.
  • Wanamageuzi(Reformists)-Watu wanaotaka mageuzi lakini si mabadiliko


ILANI YA UKOMUNISTI

ILANI YA CHAMA CHA KIKOMUNISTI​
KUNA PEPO linaisumbua Ulaya—Pepo la Ukomunisti. Mataifa yote yenye nguvu toka zamani katika Ulaya yameungana katika ushirika mtakatifu ili kulikemea na kulifukuza pepo hilo: Papa na Czar, Matternich na Guizot, wenye itikadi kali wa Ufaransa na mashushushu wa Ujerumani. Ni chama gani cha upinzani kimewahi pigiwa kelele na wapinzani wake walio madarakani kama chama cha kikomunisti? Wapi ambapo upinzani unarushiana shutuma na kukashfiana kuwa ni wakomunisti, dhidi ya vyama vingine vya upinzani na dhidi ya adui zao wa kihafidhina? Mambo mawili yanatokea kutokana na ukweli huo.

I. Tayari mataifa yenye nguvu ya Ulaya yanautambua ukomunisti kuwa nao ni chombo chenye nguvu.

II. Ni wakati muafaka kwa wakomunisti kutangaza waziwazi duniani maono yao, malengo yao, tabia zao, na kukabiliana nah ii hekaya ya kitoto juu ya Pepo la Kikomunisti kwa Ilni ya Chama chao.

Ili kufikia lengo hili, wakomunisti kutoka nchi mbalimbali wamekusanyika jijini London, na wameandika Ilani. Ilani hiyo itachapishwa katika lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kiitaliano, Ki-Flemish na Ki-Danish


I. MABEPARI NA MAKABWELA​

Historia yote ya jamii iliyopo ni historia ya misuguano ya kitabaka.

Watu huru na watumwa, watu wa tabaka la juu na wa tabaka la chini, mabwana na watwana, wataalamu wakuu na wasaidizi wao. Kwa lugha nyingine, wakandamizaji na wakandamizwaji wamekuwa wakikabiliana, wakipigana vita siku zote, wakati mwingine vya wazi na wakati mwingine vya siri. Vita ambayo mara zote imemalizika kwa mapinduzi yanayojenga jamii mpya, au maangamizi ya pamoja ya matabaka yanayopambana.

Katika nyakati za mwanzo za historia, tunaona kuwa karibu sehemu zote kulikuwa na mpangilio tata wa jamii katika vitengo mbalimbali, jamii ilipangwa katika madaraja mbalimbali. Katika dola ya kale ya Roma kulikuwa na tabaka la watu wa uzao bora, mashujaa, masikini na watumwa; katika nyakati za kati kulikuwa na makabaila, vibaraka, wataalamu wakuu, wasaidizi wa wataalamu, wanafunzi, watwana; na karibu ndani ya matabaka yote haya kulikuwa na madaraja zaidi.

Kwenye jamii ya kisasa ya kibepari ambayo ilitokana na mabaki ya mfumo wa ukabaila, misuguano ya kitabaka bado haijakoma. Ulichofanya ubepari ni kuanzisha matabaka mapya, mifumo mipya ya ukandamizaji na aina mpya ya mapambano mahali pa ile ya zamani.

Zama zetu hizi, zama za kibepari, zina sifa ya pekee sana: zimerahisisha misuguano ya kitabaka: jamii nzima inagawanyika kwa kasi sana kutengeneza kambi mbili kuu zinazokinzana watu wanakuwa katika matabaka mawili makubwa yanayokabiliana: Mabepari na makabwela.

Kutoka kwa watwana wa zama za kati, walitoka watu wa tabaka la kati walioishi kwenye miji ya mwanzo-mwanzo. Kutoka kwa watu hawa wa tabaka la kati ndipo ubepari wa mwanzo ulianza kuchipuka.

Kugunduliwa kwa bara la Amerika na meli kuweza kuzunguka kusini mwa Afrika, kulifungua maeneo mapya ya kukuza ubepari. Soko la India na China, ukoloni kwenye bara la Amerika, biashara na makoloni, kupanuka kwa namna ya kufanya biashara na kuongezeka kwa bidhaa kwa ujumla, kulivipa biashara, usafiri wa majini na viwanda msukumo ambao haujawahi shuhudiwa hapo kabla, na matokeo yake chachu za kimapinduzi zikapata kukua kwa kasi ndani ya jamii ya kikabaila iliyoanza kudhoofika.

Mfumo wa viwanda wa kikabaila, mfumo ambao uzalishaji viwandani ulihodhiwa na vikundi vya watu wachache, haukufaa tena kwa mahitaji makubwa ya masoko mapya. Mfumo mpya wa uzalishaji ukachukua mahali pake. Wataalamu waliohodhi uzalishaji walisukumwa pembeni na watu wa tabaka la kati walioanza uzalishaji; mgawanyo wa kazi ambao ulikuwepo kati ya vikundi vya wataalamu hao ulipotea mbele ya wazalishaji mmoja-mmoja.

Wakati huohuo, masoko yalizidi kukua. Hata wazalishaji hawa nao hawakuweza kutosheleza mahitaji yake. Hivyo basi, zikagunduliwa mashine za mvuke ambazo zilileta mapinduzi ya uzalishaji viwandani. Kazi ya uzalishaji ikachukuliwa na viwanda vikubwa vya kisasa, sehemu ya wazalishaji mmojammoja wa tabaka la kati ikachukuliwa na mamilionea wenye viwanda, viongozi wa jeshi lote la viwanda, mabepari wa kisasa.

Mfumo wa kisasa wa viwanda ndiyo umeanzisha soko la kidunia, na mwanzo wake ilikuwa ni kugunduliwa kwa bara la Amerika. Soko hili limesababisha ukuaji mkubwa sana wa biashara, usafiri wa baharini na mawasiliano ya nchi kavu. Na kadri biashara, usafiri wa majini na wa reli ulivyosambaa, ndivyo ubepari ulivyozidi kuendelea na mtaji wake ukiongezeka huku akisukumia mbali matabaka yote yaliyokuwepo toka zama za kati.

Kwa hiyo tumeona jinsi ambavyo ubepari wa kisasa nao ni zao la mambo yaliyotokea kwa kipindi kirefu, matokeo ya mapinduzi mengi juu ya mifumo ya uzalishaji mali na biashara.

Kila hatua ya ukuaji wa mabepari iliambatana na ukuaji wa nguvu za kisiasa za tabaka hilo. Tabaka lililokuwa likikandamizwa na mabwana wa kikabaila; wakiwatumikia makabaila na wafalme, na wakati mwingine wakitumiwa na wafalme waliotaka kujilimbikizia madaraka kuwadhibiti watu wa nasaba bora, na kiukweli wao ndiyo walikuwa msingi wa tawala kubwa za kifalme. Hatimaye mabepari, toka kuanzishwa kwa mfumo wa kisasa wa viwanda na soko la kidunia, wamefanikiwa kuteka nguvu za kisiasa za serikali za kisasa za kuchaguliwa. Serikali za kisasa si kitu kingine zaidi ya kamati tu za kusimamia masuala ya mabepari.

Kihistoria, mabepari ndiyo waliofanya mapinduzi makubwa zaidi.

Kila mara ubepari ulipopata nguvu, ulihakikisha umeikomesha mifumo ya uhusiano ya kikabaila. Bila huruma umevunja mfumo wa mahusiano wa hovyo wa kikabaila ambao mtu alijifunga kwa yule aliyemuona kuwa “Kiasili ni bora zaidi yake,” na uhusiano pekee uliouacha kati ya mtu na mtu ni uhusiano wa kimaslahi, uhusiano katili wa “Malipo taslimu.” Umezamisha hamu ya watu juu ya dini, utauwa, huruma na kuridhika ndani ya maji baridi ya kujikweza. Unapima thamani ya mtu kwa pesa, na mahali pa uhuru mwingi wa asili umeweka uhuru mmoja usiopatana na akili—Biashara Huria. Kwa maneno mengine, sehemu ya unyonyaji uliojivika kilemba cha dini na viini macho vya kisiasa, umeweka unyonyaji wa wazi, katili na usiojua aibu.

Ubepari umezivua vilemba vyake taaluma zote ambazo zimekuwa zikiheshimiwa na kuthaminiwa sana. Umewabadilisha wanasheria, madaktari, makuhani, washairi na wanasayansi kuwa wafanyakazi wa kulipwa mishahara.

Ubepari umevunja uhusiano wa kifamilia uliojengwa na hisia kuwa uhusiano wa kipesa tu.

Ubepari umeonyesha jinsi ulivyopita nguvu na ukatili vilivyokuwepo kwenye zama za kati, zama ambazo wapinga wabadiliko wanazihusudu sana, wakiona ni sifa jinsi walivyoishi kwa anasa na kizembe. Ubepari ndiyo umekuwa wa kwanza kuonyesha kile kinachoweza kutimizwa na binadamu. Umefanya maajabu ambayo yanaacha mbali mapiramidi ya Misri, mifereji ya Roma, na mahekalu ya kigothic; umefanya safari za uvumbuzi ambazo zinafanya uhamaji wote wa mataifa uliowahi kutokea hapo kabla kuwa si kitu.

Ubepari hauwezi kuwepo bila kuhakikisha kuwa muda wote unafanya mapinduzi ya nyenzo za uzalishaji, na hivyo uhusiano katika uzalishaji, na kwa ujumla uhusiano katika jamii. Kulinda njia za zamani za uzalishaji, bila kuzibadili, ilikuwa ndiyo kigezo cha kwanza cha uwepo wa matabaka ya uzalishaji ya kale. Mapinduzi katika uzalishaji yasiyokoma, kuvuruga hali za kijamii utakavyo, kutotabirika kwa wakati ujao na pilikapilika ndiko kunazitofautisha zama za ubepari na zilizopita. Kuhusiana kwao kusikobadilika, maoni yao, kunyanyaapaana na mambo yao mengine ya kale yamefagiliwa mbali. Na mapya yanayoundwa yanapitwa na wakati hata kabla hayajakomaa. Yote yaliyo imara yanayeyuka hewani, yote ambayo ni matakatifu yanadharauliwa, na hatimaye binadamu analazimika kukabiliana na hali halisi ya maisha yake na uhusiano wake na jamii yake.

Mahitaji ya bidhaa zake kwenye soko linalokua kila siku yameutawanya ubepari duniani kote, unalazimika kujishikiza kila sehemu, umetengeneza mtandao kila mahali.

Kwa kutumia soko la dunia, ubepari umefanya uzalishaji na utumiaji wa bidhaa kuwa sawa kwenye kila nchi. Wapinga mabadiliko wamepata aibu kubwa maana ubepari umetoa chini ya miguu yao utaifa ambao walikuwa wamesimama juu yake. Viwanda vyote vilivyoanzishwa na mataifa hapo zamani vimeuliwa au vinauliwa kila siku. Vinang’olewa na viwanda vipya ambavyo uwepo wake umekuwa suala la kufa na kupona kwa mataifa yote yaliyostaarabika, viwanda ambavyo havitumii tena malighafi za ndani, bali zilizotolewa kwenye maeneo ya mbali kabisa; viwanda ambavyo bidhaa zake zinatumika si tu nyumbani, bali kwenye kila pembe ya dunia. Badala ya mahitaji ya zamani yaliyotimizwa na uzalishaji wa nchi husika, tunapata mahitaji mapya, mahitaji yanayohitaji kutimizwa kwa uzalishaji unaofanyika kwenye nchi za mbali. Mahali pa nchi kujitenga na kujitegemea kumekuwa na mahusiano kuelekea kila upande, kutegemeana kwa mataifa ya dunia nzima. Kwenye bidhaa na kwenye ujuzi vilevile. Ujuzi uliozalishwa na nchi moja huwa mali ya wote. Na suala la nchi kuegemea upande mmoja linazidi kuwa gumu kila siku, na kutoka kwenye kazi za uandishi nyingi za kitaifa na kienyeji, yanaibuka maandiko ya dunia nzima.

Ubepari, kwa kuboresha njia za uzalishaji mali kwa kasi, kwa mifumo ya mawasiliano iliyoboreshwa sana, umezivuta nchi zote, hata zile za kishenzi kabisa, kwenye ustaarabu. Bei ya chini ya bidhaa zao ni mizinga mizito ambayo inapiga kuta zote za wachina, kwa kutumia hiyo, unazimisha chuki kali za washenzi dhidi ya wageni. Unalazimisha nchi zote, kwa kitisho cha maangamizi, kufuata njia za uzalishaji za kibepari; unazilazimisha kukubali kitu unachoita ustaarabu, yaani nazo kuwa za kibepari. Kwa maneno mengine: unaumba dunia kwa mfano wake.

Ubepari umeziweka nchi kwenye utawala wa miji. Umetengeneza majiji mengi, umeongeza wakazi wa mijini kwa kiwango kikubwa sana ukilinganisha na wale wa vijijini, na kwa namna hiyo, umeokoa sehemu fulani ya watu kutoka kwenye ujinga wa maisha ya vijijini. Kama tu ulivyofanya nchi itegemee miji, ndivyo ulivyofanya nchi za kishenzi na zile zilizostaarabika kidogo zitegemee zile zilizostaarabika, nchi za wakulima kutegemea za mabepari, Mashariki wategemee Magharibi.

Ubepari kila siku unazidi kukusanya pamoja, watu, njia za uzalishaji na mali. Umekusanya watu, na umeweka mali na njia za uzalishaji kwenye mikono ya wachache. Matokeo yasiyoepukika ya jambo hili yamekuwa ni wachache kuhodhi siasa. Mikoa huru au inayohusiana kwa kiasi fulani, yenye matakwa, sheria, serikali na mifumo ya kodi tofauti, inakusanywa pamoja kuwa nchi moja yenye serikali moja, sheria moja, na matakwa sawa ya kitaifa, mipaka na ushuru wa forodha mmoja.

Ubepari, ndani ya utawala wake wa miaka mia moja tu, umetengeneza nguvu kubwa ya uzalishaji kuliko vizazi vyote vilivyopita vikiwekwa pamoja. Utawala wa binadamu dhidi ya nguvu za asili, matumizi ya mashine, kutumia kemia kwenye viwanda na kilimo, usafiri kwa kutumia injini za mvuke, reli, telegraphs, kusafisha mabara mazima-mazima kwa ajili ya kilimo, kutanua na kujenga mito kwa ajili ya usafiri, jamii nzima ya watu imeamshwa kutoka usingizini—ni watu gani wa kale walikuwa hata na wazo kuwa nguvu kazi kubwa hivyo ya uzalishaji imelala kwenye mapaja ya jamii ya wafanyakazi?

Kwa hiyo tunaona kuwa: njia za uzalishaji na biashara, vitu ambavyo ubepari umejijenga juu yake, vilianzishwa wakati wa ukabaila. Katika hatua fulani ya kukua kwa njia hizi za uzalishaji na biashara, wakati ambao biashara, kilimo na uzalishaji wa viwandani vilifanyika chini ya mazingira ya kikabaila; ikatokea kuwa mazingira hayo hayaendani tena na nguvu za uzalishaji zilizokwisha endelea mbele, mazingira hayo yakawa ni kikwazo. Kukawa na uhitaji wa kukomesha ukabaila. Ukakomeshwa kabisa.

Sehemu yake ukatokea ushindani huru, ukiambatana na katiba ya kijamii na kisiasa ili kuendana nao, na uchumi na siasa zilizoegemea tabaka la mabepari.

Harakati kama hizo zinaendelea mbele ya macho yetu. Jamii ya kisasa ya kibepari, na uhusiano wake na uzalishaji, biashara na mali, jamii ambayo imeziita pamoja na kwa ukubwa sana njia za uzalishaji na biashara, imekuwa kama mchawi ambaye hawezi tena kudhibiti nguvu za kuzimu alizoziita. Kwa watu wengi, muongo mmoja wa viwanda na biashara si kitu bali historia ya uasi dhidi ya nguvu za kisasa za uzalishaji dhidi ya mazingira ya kisasa ya uzalishaji, dhidi ya suala la umiliki mali na sheria za kibepari, vitu ambavyo ni nguzo ya uwepo wake. Inatosha kutaja migogoro mikubwa ya kibiashara ambayo hujirudiarudia inavyouhukumu ubepari, na kila wakati ikizidi kutishia jamii nzima ya kibepari. Na kwenye migogoro hii, si tu bidhaa za sasa, bali hata nguvu za uzalishaji mali zilizotengenezwa huko nyuma huharibiwa. Kwenye migogoro hii huibuka gonjwa ambalo hapo zamani lingeonekana kitu cha ajabu sana—gonjwa la kuzalisha kupita kiasi. Ghafla, jamii inajikuta imerudishwa kwenye ushenzi kwa muda fulani; inakuwa kama vile janga la njaa au vita ya kidunia imekata njia zote za kijitegemea; uzalishaji na biashara huonekana kama vimekomeshwa; kwa nini? Kwa sababu kuna maendeleo kupita kiasi, kuna njia nyingi za kuendesha maisha kupita kiasi, viwanda vingi kupita kisai, biashara nyingi kupita kiasi. Nguvu za uzalishaji kwenye mikono ya jamii haziendelezi tena mazingira ya uwepo wa ubepari; kinyume chake, zimekuwa na nguvu sana hivyo haziwezi fanya kazi chini ya mazingira hayo, hivyo mazingira ya kibepari yanakuwa ni kikwazo, na mara tu zinapovishinda vikwazo hivyo, vurugu hutokea kwenye jamii ya kibepari, zikihatarisha mali za mabepari. Mazingira ya uwepo wa ubepari ni uwanja mdogo sana kuweza kumudu utajiri unaotengenezwa nao. Na ubepari unaishindaje migogoro hii? Njia moja ni kwa kuharibu nguvu nyingi za uzalishaji; na nyingine ni kwa kuteka masoko mapya na kwa kuhakikisha wanayashikilia yale ya zamani vilivyo. Hivyo tunaweza sema; unatatua migogoro kwa kutengeneza njia kwa ajili ya migogoro mingine mikubwa na mibaya zaidi, na kwa kupunguza njia za kuzuia migogoro hiyo.

Silaha ambazo ubepari ulitumia kuangusha ukabaila sasa zimewageuka.

Si tu kwamba ubepari umetengeneza silaha ambazo zinauua; lakini pia umekusanya watu wa kutumia silaha hizo—tabaka la wafanyakazi wa kisasa—makabwela.

Kadri ubepari unavyokua; mfano kimtaji, ndivyo tabaka la makabwela nalo linavyozidi kukua. Wafanyakazi wa kisasa—tabaka la vibarua, ni tabaka la watu ambao wanaishi iwapo tu wanaweza kupata kazi, na kazi zilizopo ni zile tu ambazo kwa kuzifanya wanaongeza mtaji. Vibarua hawa ambao wanajiuza polepole, ni bidhaa kama tu kitu kingine chochote cha kibiashara, na wanaathiriwa na kubadilikabadilika kwa ushindani na mabadiliko mengine yote ya soko.

Na sababu ya matumizi makubwa ya mashine na mgawanyo wa kazi, kazi za wafanyakazi zimepoteza upekee wake, matokeo yake furaha yote ya mfanyakazi imepotea. Amekuwa kama sehemu ya mashine. Na kazi anayotakiwa kufanya ni ile rahisi kupita zote, isiyohitaji ujuzi mkubwa na ya kujirudiarudia, hivyo ya gharama ya uzalishaji kwa kumtumia mfanyakazi inakuwa chini, chini hadi kwenye kiasi kinachomtosha kuishi na kuendeleza kizazi chake tu. Lakini gharama ya bidhaa na kwa hivyo gharama ya nguvu kazi, ni sawa na gharama ya kuizalisha. Kwa hiyo, jinsi kazi inavyochukiza, ndivyo mshahara wake unavyozidi kupungua. Na zaidi, kadri ambavyo matumizi ya mashine na mgawanyo wa kazi unavyoongezeka, ndivyo pia ugumu wa kazi kwa mfanyakazi huongezeka, iwe kwa kuongeza saa za kazi, kuongezeka kwa kazi inayotakiwa kufanywa kwa saa au kuongezaka kwa kasi ya mashine na njia nyinginezo.

Mfumo wa kisasa umebadilisha karakana ndogo ya mtu mwenye ujuzi kuwa kiwanda kikubwa cha bepari. Mamia ya wafanyakazi hujazana kwenye kiwanda, wakipangwa kama wanajeshi. Wakiwa kama makuruta wa jeshi la viwanda, chini ya usimamizi wa maofisa na masagenti. Si tu kuwa wafanyakazi ni watumwa wa tabaka la mabepari na nchi za kibepari; lakini kila siku na kila saa wanafanywa watumwa wa mashine, wa wasimamizi, na zaidi; wa bepari mwenye kiwanda. Na kadri ambavyo mfumo huu katili unavyoweka wazi kuwa lengo lake ni kuongeza mapato, ndivyo unavyokuwa mbaya zaidi, na ndivyo unavyozidi kuchukiza na kuudhi.

Kadri ambavyo ujuzi na nguvu ndogo vinapotumika kwenye kazi za mikono, kwa maneno mengine; kadri viwanda vinavyoboreka, ndivyo ambavyo kazi za wanaume zinavyochukuliwa na wanawake. Utofauti wa umri na jinsia hauna maana yoyote tena kwenye tabaka la wafanyakazi. Wote ni nyenzo za kazi, gharama zao zikitofautiana kulingana na jinsia na umri wao.

Na mara tu mfanyakazi anapokwisha kunyonywa na bepari, mara tu anapochukua mshahara wake, idara zingine za kibepari nazo humshukia, mwenye nyumba, muuza duka, dalali, nk.

Watu wa tabaka la kati la chini—wafanyabiashara wadogo, wauza maduka, mafundi na wakulima wadogo—hawa wote huzama polepole kwenye ukabwela, kwa sehemu ni sababu mitaji yao midogo haitoshi kumudu namna ambavyo shughuli za kisasa zinaendeshwa na huku wakiwekwa pamoja kushindana na mabepari wakubwa, na sababu nyingine ni kuwa, mbinu mpya za uzalishaji hufanya ujuzi wao kuwa si kitu tena. Kwa hiyo, makabwela hutoka kwenye matabaka yote ya watu.

Ukabwela hupitia hatua mbali mbali katika kukua kwake. Kuzaliwa kwake ndiyo mwanzo harakati zake dhidi ya ubepari. Mwanzoni, mapambano huendeshwa na kibarua mmojammoja, kisha na wafanyakazi wa kiwanda, baadaye na wafanyakazi wa idara moja kwenye eneo moja, dhidi ya bepari mmoja anayewanyonya. Wanalenga mashambulizi yao si kwa mazingira ya uzalishaji ya kibepari, bali dhidi ya nyenzo za uzalishaji; wanaharibu bidhaa zilizoingizwa kutoka nje ya nchi, wanavunja mashine vipandevipande, wanachoma moto viwanda, wakitaka kurudisha kwa nguvu hadhi iliyopotea ya mfanyakazi wa zama za kati.

Kwenye hatua hii, vibarua bado wanakuwa ni kundi tu lisiloeleweka, limetawanyika nchi nzima, likiwa limetenganishwa na ushindani wa wao kwa wao. Na kama kuna sehemu wamejiunga kutengeneza kikundi imara, basi si sababu ya kutaka kwao, bali sababu ya muungano uliofanywa na mabepari ambao ili kufikia malengo yao ya kisiasa, wanalazimika kuwahamasisha na kuwaleta pamoja makabwela, na kwa kipindi fulani wanafanikiwa katika hilo. Kwa hiyo, bado hatuwezi kusema makabwela wameungana, kwenye hatua hii, makabwela hawapigani na adui zao, bali adui wa adui zao, yaani mabaki ya watawala wa kifalme, wamiliki ardhi, mabepari wasio na viwanda na mabepari uchwara. Hivyo basi, harakati zote zinakuwa chini ya mabepari; ushindi wowote unaopatikana ni ushindi wa mabepari.

Lakini kadri ambavyo viwanda vinazidi kukua; si kwamba tu makabwela wanaongezeka, bali pia wanazidi kuwa pamoja, nguvu zao hukua, na wanaiona nguvu yao hata zaidi. Matakwa na hali ya maisha ya makabwela huzidi kufanywa kuwa ya aina moja kadri ambavyo mashine zinavyoua mgawanyo wa kazi, na karibu kila mahali zikishusha mishahara kuwa kima kimoja cha chini. Kukua kwa ushindani kati ya mabepari na migogoro ya kibiashara inayozalishwa nao, hufanya mishahara ya wafanyakazi ibadilikebadilike hata zaidi. Uboreshaji wa mashine usiokoma; zikizidi kuwa bora kwa kasi kila siku, kunafanya maisha ya makabwela kuwa ya mashaka hata zaidi. Migongano kati ya mfanyakazi mmoja na mwingine, na kati ya bepari na bepari, hatua kwa hatua huchukua sura ya mgongano wa kitabaka. Hivyo basi, wafanyakazi huanza kuunda umoja dhidi ya bepari; wanajiunga pamoja ili kuhakikisha wanapata mishahara mikubwa; wanaunda ushirika wa kudumu ili kuandaa migomo hiyo. Mara kwa kwa mara, hapa na pale, mizozo hii huibuka kuwa ghasia.

Kuna nyakati wafanyakazi huibuka washindi, lakini ni kwa muda tu. Matunda ya kweli ya mapambano yao hayapo kwenye matokeo ya mara moja bali kwenye umoja wa wafanyakazi unaokua kila uchwao. Umoja huu; kwa namna fulani unasaidiwa na njia nzuri za mawasiliano zilizoboreshwa na mfumo wa kisasa wa viwanda, hilo linawezesha wafanyakazi walio kwenye maeneo tofauti waweze kuwasiliana. Ni kuwasiliana huku tu ndiko kulihitajika ili kuleta pamoja harakati zinazofanana zilizokuwa zinaendelea kwenye maeneo mbalimbali kuwa harakati moja ya kitaifa kati ya matabaka. Lakini harakati zote za kitabaka ni harakati za kisiasa. Kilichowachukua wafanyakazi wa zama za kati; na barabara zao mbovu karne kadhaa kufanikisha, makabwela wa sasa, na hasa kwa msaada wa reli; wanafanikisha ndani ya miaka michache tu.

Kitendo cha makabwela kujiunga pamoja kutengeneza tabaka, na baadaye kuwa chama cha siasa, kinavurugwa bila kukoma na ushindani wa wafanyakazi wenyewe kwa wenyewe. Lakini mara zote wanaibuka tena, wakiwa na nguvu, uthabiti na na ukuu zaidi. Hilo hulazimisha matakwa fulani ya wafanyakazi kutambulika kisheria, hasa kwa kutumia fursa ya mgawanyiko baina ya mabepari. Hivyo ndivyo sheria ya saa kumi za kazi ilivyopitishwa Uingereza.

Na kwa ujumla wake, migogoro baina ya matabaka ya zamani kwa kiasi kikubwa inasaidia kusongesha mbele kukua kwa makabwela. Ubepari unajikuta muda wote ukiwa kwenye mapambano. Mwanzo kabisa, dhidi ya utawala wa wateule(Aristokrasi/makabaila); baadaye, dhidi ya kundi fulani la mabepari ambao maslahi yao yanapingana na kuendelea kwa mfumo wa viwanda; na muda wote, dhidi ya mabepari wa nchi zingine. Na katika mapambano yote haya ubepari unajikuta ukilazimika kukubaliana na makabwela, ukiomba msaada wao, na hivyo kuvuta makabwela kwenye uwanja wa siasa. Kwa hiyo, ubepari wenyewe ndiyo unawapa makabwela nyenzo zake za kisiasa na elimu, kwa maneno mengine; unawapa makabwela silaha za kupambana nao.

Zaidi, kama tulivyokwishaona, sehemu nzimanzima ya tabaka tawala, hasa kutokana na kukua kwa viwanda, wanaangukia tabaka la makabwela, au nafasi zao za sasa zipo kwenye kitisho. Hawa huwapatia makabwela maarifa na msukumo mpya.

Na mwisho, wakati ambapo misuguano ya kitabaka inapokaribia mwisho, zoezi la kuvunjika linakuwa linaendelea ndani ya tabaka tawala, ukweli ni kuwa linakuwa linaendelea kwenye jamii nzima, fikiria jinsi ukabwela utakavyokuwa baada ya sehemu fulani ya tabaka tawala kujitenga na kujiunga na tabaka la wanamapinduzi, tabaka ambalo ndilo linaamua mustakabali wa wakati ujao. Kama tu hapo mwanzo ambavyo sehemu ya tabaka la wateule ilivyoungana na mabepari, basi sasa sehemu ya mabepari inajitenga na kuungana na makabwela, na hasa sehemu ya mabepari ambao ni wanaitikadi, wale ambao wameweza kuelewa jinsi ambavyo harakati na historia huwa vinaenda.

Katika matabaka yote ambayo yanasimama dhidi ya ubepari leo, ni tabaka la makabwela pekee ndilo la kimapinduzi. Matabaka mengine yote hudhoofika na kupotea chini ya mfumo mpya wa viwanda; lakini makabwela wao ni zao muhimu na la kipekee la mfumo huo.

Watu wa tabaka la kati la chini, wazalishaji wadogo, wamiliki maduka, mafundi, wakulima wadogo nk, hawa wote wanapambana dhidi ya ubepari ili kulinda nafasi zao kwenye tabaka la kati. Hivyo si wanamapinduzi bali wahafidhina. Na hata zaidi, ni wapinga maendeleo, maana wanataka kurudisha nyuma gurudumu la historia. Na kama wametokea kuwa wanamapinduzi kwa bahati, wanafanya hivyo kwa sababu ya kuogopa uhamisho wa kwenda ukabwelani unaowakabili, kwa hiyo hawapigani kwa ajili ya hali yao ya sasa, bali kwa ajili ya manufaa yao ya baadaye. Wanaikimbia sehemu yao na kujiweka sehemu ya makabwela.

Watu hawa ni “tabaka hatari,” uchafu wa jamii, umati unaooza polepole na hivyo kutupwa nje kutoka matabaka ya chini kabisa la mfumo wa kijamii wa zamani. Hapa na pale wanaweza kusombwa na harakati za makabwela na hivyo kuingia kwenye mapinduzi; lakini hali ya maisha yao, inawaandaa kuwa chombo cha kuhongwa na hila dhidi ya mapinduzi.

Tunaweza kusema kuwa watu wengi wa jamii zilizopita tayari wameingia kwenye mazingira ya kikabwela. Kabwela hana mali yeyote, uhusiano wake kwa mkewe na watoto wake haufanani tena na ule wa bepari na familia yake; kazi za kisasa za viwandani na utumikishwaji chini ya mtaji, vimewaondolea makabwela sifa zote za kitaifa. Hali yao ipo vile vile katika Uingereza na katika Ufaransa, kama ilivyo Marekani ndiyo ilivyo Ujerumani. Kwake yeye; sheria, maadili na dini ni vitu tu vya kibepari, vitu ambavyo nyuma yake kuna maslahi ya mabepari yakivizia.

Matabaka yote ya juu katika historia yalihakikisha yanalinda hadhi yao kwa kuiweka jamii kwenye mazingira ya kunyonywa. Makabwela hawawezi kuwa mabwana wa nguvu za uzalishaji isipokuwa kwa kukomesha mfumo uliowanyonya, na hivyo kukomesha kila mfumo wa unyonyaji uliowahi pata kuwako. Hawamiliki kitu chochote cha kukilinda; kazi yao ni kuharibu mifumo yote iliyolinda umiliki mali binafsi.

Harakati zote za wakati uliopita zilikuwa ni harakati za walio wachache, au kwa ajili ya maslahi ya wachache. Harakati za makabwela ni harakati za wanaojielewa, harakati huru za walio wengi. Kwa ajili ya maslahi ya walio wengi. Makabwela, tabaka la chini kabisa la jamii yetu ya sasa, haliwezi kujiamsha bila ya tabaka lote la juu linalowakalia kurushwa hewani.

Mwanzoni harakati za makabwela dhidi ya mabepari huwa ni harakati za kitaifa. Ukabwela wa kila nchi unatakiwa kwanza kabisa kuweka mambo sawa na ubepari wake.

Katika kuonyesha hatua kuu za ukuaji wa makabwela, tulichunguza vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyojificha ikipamba moto ndani ya jamii ya leo, mpaka pale vita hivyo vinapokuwa mapinduzi ya waziwazi, na ambavyo kungo’lewa kwa ubepari kwa kutumia nguvu kunavyoweka msingi wa utawala wa makabwela.

Hata hivyo, na kama tulivyokwishaona, kila mfumo wa jamii umekuwa na upinzani wa kati ya tabaka la wanyonyaji na wanaonyonywa. Lakini ili kulinyonya tabaka fulani, hali fulani zinatakiwa kuwekwa ili walau liendelee kuishi katika maisha yao ya kitumwa. Mtwana wa wakati wa ukabaila, aliweza kujiinua na kuwa mshirika wa jumuia, kama tu ambavyo mabepari uchwara chini ya ukandamizaji wa ukabaila walivyoweza kuwa mabepari kamili. Lakini kibarua wa kisasa ni tofauti, badala ya kuendelea kadri ambavyo mfumo wa viwanda unavyoendelea, wao wanazidi kuzama chini, chini ya hali zinazowafaa kuishi. Anakuwa masikini wa kutupwa, na umasikini wa kutupwa unakua kwa kasi kuliko idadi ya watu na utajiri. Kufikia hatua hiyo kunakuwa na ushahidi usiyo na shaka, kwamba mabepari hawafai tena kuendelea kuwa tabaka tawala wala kuweka mazingira wayatakayo kwenye jamii kuwa sheria. Ubepari haufai kutawala kwa sababu hauna uwezo wa kuhakikisha maisha ya watumwa walio chini ya mfumo wake wa kitumwa yakiendelea, kwa sababu hauwezi kumsaidia asizame kwenye umaskini wa kutupwa, hauwezi kumlisha na badala yake unataka kulishwa naye. Jamii haiwezi tena kuendelea kuishi chini ya huu ubepari, kwa maneno mengine, uwepo wa ubepari hauendani tena na jamii.

Kigezo muhimu kwa uwepo, na utawala wa tabaka la mabepari ni kuundwa na kukuzwa kwa mtaji; na ukuzaji wa mtaji hutegemea uwepo wa kazi ya mshahara. Na uwepo wa kazi ya mshahara hutegemea ushindani kati ya wafanyakazi. Ukuaji wa viwanda ambao unachagizwa na ubepari, unaondoa utengano wa wafanyakazi unaoletwa na ushindani na kuwafanya washirikiane na kuungana kimapinduzi. Ukuaji wa mfumo wa kisasa wa viwanda unaondoa msingi chini ya miguu yake wenyewe, msingi ambao ubepari unazalisha na kupata mali. Hivyo basi, kitu ambacho ubepari unazalisha kuliko vyote ni kaburi lake wenyewe. Kuanguka kwake na ushindi wa makabwela haviepukiki.
 
Marx anasema, dini na sarakasi za siasa ni mifumo tu ya unyonyaji inayojivika vilemba ili ionekane mizuri. Lakini ubepari unanyonya bila aibu. "
Kwa maneno mengine, sehemu ya unyonyaji uliojivika kilemba cha dini na viini macho vya kisiasa, umeweka unyonyaji wa wazi, katili na usiojua aibu."
 
Red-Giant ni bepari ama mjamaa uliyekubuhu?
===
Asante kwa kumbukizi
Kulingana na Marx na walioanzisha ukommunisti(Tuite sawa na ujamaa) alisema kuwa haiwezekani kufikia ujamaa bila kupitia ubepari. Na kuna chapter alikemea sana wanaofikiri watafikia ujamaa bila ubepari, akiwaita waota ndoto. Mtu kama Nyerere, wakina Mao na wengineo, waliamini wanaweza kujenga jamii ya kijamaa hewani. Pengine ndiyo maana walishindwa. Alienda mbali hadi kuwaita wapinga mapinduzi, alisema kwa kupachika kwao ujamaa toka hewani wanaua harakati za makabwela.

Marx aliamini historia lazima ifuate mkondo wake. Kutoka ukabaila kuingia ubepari. Kutoka ubepari kuingia ukomunisti/ujamaa. Nchi za kujiita social democrats naona ndizo hasa zinaelekea kwenye ujamaa wa kweli.

Naamini katika mfumo mseto kama ule wa social democrats, nao unajengwa polepole kutoka kwenye ubepari. Ubepari kama wa kimarekani na ujamaa kama wa Nyerere ni tatizo.

Nikipata chance nitaedit na kutupia chapter zinazofuata.
 
Sura ya pili.

II. MAKABWELA NA WAKOMUNISTI​

Wakomunisti na makabwela wana uhusiano wa namna gani?

Wakomunisti hawaundi chama cha tofauti kikiwa dhidi ya vyama vingine vya tabaka la wafanyakazi.

Hawana maslahi mengine mbali na yale ya makabwela

Hawaundi kanuni zao wenyewe kwa kujitenga na kuongoza harakati za makabwela.

Wakomunisti wanajitofautisha na vyama vingine vya tabaka la wafanyakazi kwa vitu hivi pekee: (1) Katika harakati za kitaifa za makabwela wa nchi tofauti, wanaonyesha ufanano na kuleta maslahi ya makabwela wote pamoja bila kuangalia utaifa. (2) Katika hatua mbalimbali ambazo harakati za makabwela dhidi ya mabepari zinapitia katika kukua kwake, mara zote, na kila mahali wanasimamia maslahi au lengo kuu la harakati.

Kwa hiyo, kiuhalisia, kwa upande mmoja, wakomunisti ndiyo wenye msimamo thabiti na waliopiga hatua kubwa kati ya vyama vya wafanyakazi vya kila nchi, kikundi kinachowasukuma mbele wengine wote, kwa upande mwingine, kinadharia wao wanaelewa kwa usahihi kabisa harakati, hali na matokeo ya harakati za makabwela.

Malengo ya muda mfupi ya wakomunisti ni sawa na yale ya vyama vingine vya makabwela: kuwaunganisha makabwela kuwa tabaka moja, kupindua ubwana wa mabepari na makabwela kushika nguvu za kisiasa.

Nadharia za wakomunisti hazina msingi kwenye mawazo au kanuni zilizobuniwa au kugunduliwa na mtu fulani mwanamageuzi wa kidunia.

Wanachofanya wao ni kuonyesha tu uhalisia wa matokeo na uhusiano unaotokana na misuguano iliyopo ya matabaka, harakati kubwa zinazoendelea mbele ya macho yetu wenyewe. Kukomesha aina ya umiliki mali iliyopo si sifa kuu ya ukomunisti.

Mahusiano yote ya mali yaliyopita yalikutana na mabadiliko makubwa yaliyo sababishwa na mabadiliko makubwa ya mazingira ya kijamii.

Kwa mfano mapinduzi ya Ufaransa, yalikomesha ukabaila na kuleta ubepari.

Sifa pekee ya wakomunisti siyo kukomesha umiliki mali, bali umiliki mali wa kibepari. Lakini leo hii umilikaji mali wa kibepari, ndiyo mfumo wa juu kabisa wa kuzalisha na kupata mali ambao unategemea ukinzani wa matabaka, unaotegemea wachache kunyonya wengi.

Kwa mantiki hiyo basi, nadharia ya wakomunisti inaweza elezewa kwa sentensi moja tu: kukomeshwa kwa umilikaji binafsi wa mali.

Wakomunisti tumeshutumiwa kwa kutaka kukomesha haki ya mtu kuwa na mali ambayo ni matunda ya kazi yake, mali ambayo inasemwa kuwa ni msingi wa mtu kuwa huru, kufanya kazi na kujitegemea.

Mali iliyopatikana kwa jasho na nguvu za mtu mwenyewe! Unamaanisha mali za mafundi na wakulima wadogowadogo, umiliki mali kabla ya umiliki wa mali wa kibepari? Hakuna haja ya kukomesha umiliki wa aina hiyo; ukuaji wa viwanda, kwa sehemu kubwa umeshakomesha hilo tayari, na unaendelea kulikomesha kila siku.

Au unamaanisha umiliki mali wa kibepari?

Je, kazi ya ujira inazalisha mali yeyote kwa mfanyakazi? Hata kidogo. Inazalisha mtaji, yaani mali inayomnyonya, ujira ambao hauwezi kuongezeka isipokuwa hali zihitaji wafanyakazi wapya kwa ajili ya kuanza kuwanyonya. Mali, katika mfumo wake wa sasa, msingi wake ni ushindani kati ya mtaji na kazi ya ujira. Acha tuchunguze pande zote za ushindani huu.

Kuwa bepari, ni si tu kuwa na hadhi binafsi, bali pia hadhi ya kijamii kwenye uzalishaji. Mtaji ni zao la jumla, na ni kwa matendo ya watu wengi walioungana ndipo unaweza kuzalishwa.

Kwa hiyo basi, mtaji si mtu, ni nguvu ya kijamii.

Hivyo basi, mtaji unapobadilishwa kuwa mali ya wote, kuwa mali ya watu wote wa jamii husika, mali binafsi inakuwa haibadilishwi kuwa mali ya jamii. Ni sifa tu ya kijamii ya mali hiyo ndiyo inayokuwa imebadilika. Inapoteza sifa yake ya kitabaka.

Sasa na tuone kazi ya ujira.

Kiasi cha wastani cha kipato cha kazi ya ujira ni kima cha chini, yaani kiasi ambacho kinahitajika kwa kibarua kuishi kama kibarua. Kwa hiyo, kiasi ambacho kibarua anapata kutokana na kazi yake, kinatosha tu kumfanya kuishi na kuzaliana. Hatuna nia kabisa ya kukomesha upatikanaji wa mali wa namna hiyo, upatikanaji wa mali wa namna hiyo upo ili kumfanya mtu aishi na azaliane, ni uzalihaji ambayo hauzalishi ziada ambayo inaweza kutumika kuajiri nguvu kazi ya wengine. Kitu tunachotaka kukomesha ni unyonyaji huu mbaya, unyonyaji ambao mfanyakazi anaishi ili tu kuongeza mtaji, na anaruhusiwa kuishi kwa kadri tu maslahi ya tabaka tawala yanavyomhitaji.

Katika jamii ya kibepari, nguvukazi inayoishi, ni njia tu ya kuongeza nguvukazi. Kwenye jamii ya kijamaa, nguvukazi ni namna ya kupanua, kutajirisha na kuboresha maisha ya wafanyakazi.

Na mabepari wanaita ukomeshaji wa hali hii kuwa ni ukomeshwaji wa uhuru wa mtu binafsi na kujitegemea! Na wako sahihi, lengo ni ukomeshwaji wa uhuru wa mabepari, ubinafsi wa mabepari na kujitegemea kwa mabepari.

Kwa kusema uhuru, mabepari wanamaanisha; soko huria na uhuru wa kuuza na kununua uliopo chini ya ubepari.

Lakini iwapo kuuza na kununua kukitoweka, basi uhuru wa kuuza na kununua utatoweka pia. Haya maneno ya uhuru wa kununua na kuuza, na maneno mengine ya “Kishupavu” ya mabepari juu ya uhuru kwa ujumla wake, yanakuwa na maana iwapo yakilinganishwa na vikwazo vya kuuza na kununua vya wakati wa zama za kati, wakati wa ukabaila. Lakini yanakosa maana yanapolinganishwa na ukomeshwaji wa kuuza na kununua utaofanywa na wakomunisti, na ukomeshwaji wa mazingira ya uzalishaji ya kibepari, na ubepari wenyewe.

Unatishwa na nia yetu ya kukomesha umiliki binafsi wa mali. Lakini kwenye jamii yako leo, umiliki binafsi wa mali umekoma kwa tisa ya kumi ya watu; kuwepo kwake kwa wachache ni sababu ya kutokuwepo kwenye mikono ya hao tisa ya kumi. Kwa hiyo, unatushutumu kwa kunuia kukomesha mfumo wa mali ambao umeweka mazingira ambapo sehemu kubwa ya jamii haina mali!

Kwa neno moja, unatushutumu kutaka kukomesha mali zako. Sahihi kabisa; hiyo ndiyo nia yetu hasa.

Kutoka wakati ambao nguvu kazi haitabadilishwa kuwa mtaji, pesa, au kodi, yaani kuwa nguvu ya kijamii inayoweza kuhodhiwa, kutoka wakati ambao mali binafsi haitaweza tena kubadilishwa kuwa mali ya kibepari; kuwa mtaji, ndiyo unasema kutoka wakati huo uhuru binafsi unakuwa umetoweka?

Kwa hiyo basi, unatakiwa kukiri kuwa, unaposema “binafsi” unamaanisha si mtu mwingine zaidi ya bepari, si mwingine bali mtu wa daraja la kati anayemiliki mali. Ni kweli, mtu huyu anatakiwa kufagiliwa mbali na kufanya isiwezekane atokee tena.

Ujamaa haumnyimi mtu yeyote uwezo wa kujipatia mali; unachofanya ni kumnyima uwezo wa kutumia nguvu kazi ya wengine katika kujipatia huko mali.

Imepingwa na kusemwa kuwa, baada ya kukomesha umiliki binafsi wa mali, kazi zote zitakoma, na uvivu utaingia kwenye dunia nzima.

Kwa mantiki hii, jamii ya kibepari ingekuwa imeshatoweka sababu ya uvivu wa kupindukia; sababu watu wake wanaofanya kazi hawapati chochote, na wale wanaopata chochote hawafanyi kazi. Upinzani wote huu si kitu bali kuongea kitu kilicho wazi: kwamba, hakuwezi kuwa na kazi ya ujira iwapo uwepo wa mtaji utakoma.

Hoja zote zilizotolewa kupinga mfumo wa kikomunisti wa uzalishaji na umiliki mali, zimetolewa pia kupinga mfumo wa kikomunisti juu ya kuzalisha na kumiliki kazi za ubunifu. Kwa mabepari, kupotea kwa umiliki mali wa kitabaka, ni kupotea kwa uzalishaji mali kwa ujumla. Hivyo hivyo, wanaona kutoweka kwa tamaduni za kitabaka, kwake ni sawa na kupotea kwa utamaduni wote.

Utamaduni huo, ambao analia kuwa utapotea, ni utamaduni wa walio wengi kujifunza kufanya kazi kama mashine.

Lakini usibishane nasi kama unatumia viwango vyako vya kibepari juu ya uhuru, sheria, utamaduni nk, katika kupinga nia yetu ya kukomesha umiliki mali wa kibepari. Mawazo yako si kitu kingine bali zao la mazingira ya uzalishaji na umiliki mali wa kibepari, kama tu ambavyo sheria zako ambazo si kitu kingine bali matakwa ya tabaka lako yaliyofanywa kuwa sheria kwa wote, matakwa yanayotegemea mazingira ya kiuchumi ya uwepo wa tabaka lako.

Upofu uliotokana na ubinafsi ndiyo umekufanya ufanye ziwe sheria za asili taratibu za kijamii zilizotokana na mfumo wa sasa wa uzalishaji na umiliki mali—taratibu ambazo kwenye historia zinaibuka na kupotea kadri uzalishaji unavyobadilika—upofu huu uliwapata pia watu wote wa tabaka tawala waliopita kabla yako. Unachoona waziwazi kwenye mfumo wa umiliki mali wa kale, kile unachokubali juu ya ukabaila, umegoma kukubali juu ya mfumo wako wa umiliki mali wa kibepari.

Kukomeshwa kwa familia! Hata wenye itikadi kali hupagawa wasikiapo pendekezo hili la wakomunisti.

Je, familia ya sasa, familia chini ya ubepari ina msingi gani? Kwenye mtaji, kwenye maslahi binafsi. Kwenye hali yake iliyokomaa, familia hii inapatikana miongoni mwa mabepari tu. Na hali hiyo inaimarishwa zaidi na kutokuwepo kwa familia kati ya makabwela, na uwepo wa umalaya wa wazi.

Familia ya kibepari itatoweka siku ambayo kitu kinachoiimarisha kikitoweka, na vyote vitatoweka iwapo mtaji utatoweka.

Unatuhukumu kwa kutaka kukomesha wazazi kuwanyonya watoto wao? Kosa hilo tunakiri kulifanya.

Lakini utasema, tunaharibu uhusiano adhimu sana tunapoweka elimu ya kijamii na kuondoa elimu ya nyumbani.

Vipi kuhusu elimu yako? Si nayo ni ya kijamii pia, inayoamuliwa na hali za kijamii ambazo chini yake unatoa elimu, jamii ikiingilia elimu moja kwa moja au siyo moja kwa moja kwa kupitia shule nk? Wakomunisti siyo walioanzisha suala la jamii kuingilia elimu; wanachotaka ni kubadili tu namna ya uingiliaji huo, na kuiokoa elimu kutoka kwenye ushawishi wa tabaka tawala.

Ubwabwajaji wa mabepari kuhusu familia na elimu, juu ya uhusiano mtakatifu kati ya mtoto na mzazi, unazidi kuudhi kadri ambavyo matendo ya mfumo wa kisasa wa uchumi yanavyovunjilia mbali uhusiano wote wa kifamilia katika familia za makabwela, na watoto wao kuwa vitu vya kibiashara na nyenzo za kazi.

“Lakini nyinyi wakomunisti mtaanzisha jamii za wanawake,” wanapiga kelele mabepari wote kwa pamoja.

Bepari anamuona mke wake kuwa nyenzo ya uzalishaji tu. Anaposikia kuwa nyezo zote za uzalishaji zinatakiwa kutumika kwa pamoja, kiasili, kinachomjia akilini suala la kutumika kwa pamoja linahusu pia wanawake.

Hawazii hata kidogo kuwa lengo la kweli ni kuondoa hadhi ya mwanamke kuwa nyenzo ya uzalishaji tu.

Kwa mengine yote, hakuna cha ajabu kuliko kwa mabepari wetu kujidai kuchukia jamii ya wanawake ambayo wanadai itaanzishwa na wakomunisti. Wakomunisti hawana haja ya kuanzisha jamii ya wanawake; imekuwepo toka mwanzo wa ulimwengu.

Mabepari wetu hawaridhiki kuwatumia watakavyo wake na mabinti wa makabwela, na hapo bila ya kuongelea malaya wa kawaida, lakini bado wanatongozeana wake zao wao kwa wao.

Kiuhalisia, ndoa za kibepari ni mfumo wa wake wa pamoja, kwa hiyo, kile ambacho wakomunisti wanatakiwa kushutumiwa ni nia yao ya kuanzisha jamii ya wanawake ya wazi na ya kisheria badala ya hii ya kinafiki iliyofichwa. Kwa mengineyo yote, ni ukweli ulio wazi kuwa, kukomeshwa kwa mfumo wa sasa wa uzalishaji mali kutasababisha kukoma kwa jamii ya wanawake iliyotokana na mfumo huo, yaani, umalaya, wote-wa wazi na wa kisiri.

Hata zaidi, wakomunisti wanashutumiwa kwa kutaka kukomesha uwepo wa nchi na utaifa.

Wafanyakazi hawana nchi. Hatuwezi kuchukua kutoka kwao kitu ambacho hawana. Sababu makabwela wanatakiwa kwanza kupata utawala wa kisiasa, wanatakiwa kuwa tabaka linaloongoza kwenye taifa, wanatakiwa kujifanya kuwa taifa, kwa hiyo, makabwela tayari ni taifa, lakini si kwa namna wanayofikiri mabepari.

Tofauti za kitaifa na misuguano kati ya watu inapungua kila siku, na hili ni tokeo la kukua kwa ubepari, uhuru wa biashara, soko la kidunia, mfanano wa njia za uzalishaji mali na kufanana kwa hali za maisha kunakoambatana nako.

Utawala wa makabwela utafanya tofauti hizo zipungue kwa kasi zaidi. Hatua ya pamoja ya walau nchi zilizoendelea, ni jambo la kwanza katika kuelekea ukombozi wa makabwela.

Unyonyaji kati ya mmoja na mwenzake unapokomeshwa, unyonyaji wa kati ya taifa moja na jingine nao utakoma. Hivyohivyo, misuguano kati ya matabaka ndani ya taifa inapokoma, ndivyo uhasama kati ya nchi na nchi utakapokoma.

Shutuma dhidi ya ukomunisti zinazotolewa kwa mlengo wa kidini, kifalsafa, na yaani kiitikadi kwa ujumla, hazina haja ya kuzichunguza.

Kwani inahitaji uelewa mkubwa kutambua kuwa; mawazo na mtazamo wa binadamu, kwa lugha nyingine, uelewa wake wote, hubadilika kila mara hali ya maisha yake kiuchumi na kijamii zinapobadilika?

Historia juu ya mawazo inathibitisha nini zaidi ya kuwa mawazo hubadilika kulingana na kubadilika kwa uzalishaji wa vitu? Mawazo yaliyoongoza zama zote yalikuwa ni mawazo ya tabaka tawala.

Watu wanapoongelea juu ya mawazo yanayofanya mapinduzi kwenye jamii, wanaongelea ukweli ulio wazi, kuwa; jamii mpya huzaliwa kutoka kwenye ile ya zamani, na kuwa, kuondoka kwa mawazo ya zamani kunaenda sambamba na kuondoka kwa hali za zamani za maisha.

Wakati ulimwengu wa kale ulipokuwa katika hatua zake za mwisho, ukristo ukabadili mahali pa dini za kale. Na mawazo ya kikristo yaliposhindwa na mawazo ya wanazuoni katika karne ya 18, jamii ya kikabaila ikalazimika kupigana vita ya kufa na kupona dhidi ya mabepari wanamapinduzi wa wakati huo. Dhana za uhuru wa kidini na dhamira, zinaonyesha tu uwepo wa ushindani huru kwenye uwanja wa maarifa.

“Bila shaka,” itasemwa, “Mawazo juu ya dini, maadili, falsafa, na sheria, yamebadilika kadri historia ilivyobadilika. Lakini vitu vyenyewe, yaani dini, maadili, falsafa, sayansi ya siasa na sheria vimedumu bila kutoweka.

“Vitu hivyo ni vya milele, kama vile uhuru, haki nk vilivyo vya milele. Vipo katika jamii zote. Lakini ukomunisti unataka kuvikomesha, unakomesha dini na maadili yote badala ya kuviweka katika mtindo mpya; hivyo unaenda kinyume na yote yaliyotokea katika historia.”

Shutuma hizi zinatuonyesha nini? Historia ya jamii zote zilizopita zilikuwa kwenye misuguano ya kitabaka, misuguano iliyochukua sura tofauti katika zama tofauti.

Lakini haijalishi sura yake, kitu kimoja kimekuwepo kwenye nyakati zote, yaani sehemu moja ya jamii kuinyonya nyingine. Ndiyo maana haishangazi kuwa, uelewa wa jamii katika zama zilizopita, pamoja utofauti wao mwingi ulikuwa wa aina moja au wa mawazo yanayofanana, ambayo hayawezi kuondoka mpaka pale misuguano ya kitabaka itakapoondoka.

Mapinduzi ya kikomunisti ndiyo pigo kuu zaidi juu ya umiliki mali uliozoeleka; ndiyo maana si jambo la ajabu kukua kwake kunahusihsa mabadiliko makubwa sana juu ya mawazo yaliyozoeleka.

Lakini hebu tuachane na upinzani wa mabepari dhidi ya ukomunisti.

Tumeona huku juu kuwa; hatua ya kwanza katika mapinduzi ya wafanyakazi ni kwa makabwela kuwa tabaka tawala, kushinda vita ya demokrasia.

Makabwela watatumia utawala wao wa kisiasa kupokonya, polepole, mtaji wote kutoka kwa mabepari, kuleta pamoja njia zote za uzalishaji mali kwenye mikono ya serikali ya makabwela na kuongeza nguvu za uzalishaji kwa kasi kadri inavyowezekana.

Ni kweli kuwa mwanzoni hilo halitawezekana isipokuwa kwa kutumia njia za mabavu kuingilia haki ya umiliki mali na kuondoa mazingira ya uzalishaji ya kibepari; njia ambazo kwa kuzipima kiuchumi zinaonekana kuwa hazifai wala kuingia akilini, lakini kadri harakati zinavyoendelea, zitajionyesha uzuri wake na hivyo kufanya uondoaji wa mfumo wa zamani wa jamii uwe kitu cha lazima, na pia ni njia zisizoepukika kwenye kufanya mapinduzi ya mfumo mzima wa uzalishaji.

Njia hizo zitakuwa tofauti katika nchi tofauti.

Hata hivyo, kwenye nchi zilizoendelea sana, yafuatayo yanaweza kutekelezeka kwa urahisi.

  • Kukomesha umiliki binafsi wa ardhi na kuweka kodi kwenye ardhi yote kwa ajili ya manufaa ya umma.
  • kodi kubwa inayotegemea kipato.
  • Kukomesha haki zote kuhusiana na urithi.
  • Kutaifisha mali za wahamiaji na waasi wote.
  • Kuweka biashara ya ukopeshaji mikononi mwa serikali, kwa kutumia benki na mtaji wa taifa, benki hiyo ikihodhi biashara hiyo.
  • Kuweka njia za mawasiliano na usafirishaji mikononi mwa serikali.
  • Kupanua viwanda na nyenzo zingine za uzalishaji zinazomilikiwa na serikali; kuanza kulima maeneo yaliyokuwa tupu, kuboresha ardhi kulingana na mpango wa pamoja.
  • Uwajibikaji sawa wa wote katika kazi. Kuanzishwa kwa majeshi ya uzalishaji, hasa katika kilimo.
  • Kuunganisha kilimo na viwanda; kuondoa polepole tofauti ya mijini na vijijini, kwa kutawanya watu kwa usawa katika nchi.
  • Elimu bure kwa watoto wote katika shule za serikali. Kukomesha ajira za watoto viwandani kama ilivyo sasa. Kuhusianisha elimu na uzalishaji wa viwandani nk.
Ikitokea kuwa, wakati wa maendeleo ya mapinduzi tofauti za matabaka zimekoma, na uzalishaji mali wote upo mikononi mwa umoja wa taifa zima, nguvu za kisiasa zitapotea. Nguvu za kisiasa, na zimeitwa nguvu kwa usahihi kabisa—si kitu kingine bali mpango wa tabaka moja kukusanya nguvu ili kunyonya na kukandamiza lingine. Iwapo makabwela, katika mapambano yao na mabepari wakalazimika, kulingana na ulazima wa hali, kujipanga kama tabaka, ikiwa kwa mapinduzi wakawa tabaka tawala, na hivyo kufagilia mbali mazingira ya uzalishaji ya zamani, basi pamoja nazo, watakuwa wamefagilia mbali uwepo wa misuguano ya kitabaka na matabaka kwa ujumla, na kwa kufanya hivyo utajikomesha wenyewe kama tabaka tawala

Mahali pa jamii iliyopita ya kibepari, pamoja na matabaka na misuguano yake ya kitabaka, tutakuwa na umoja ambao ndani yake, mazingira ya kuendelea kwa mtu mmoja, ndiyo mazingira ya kuendelea kwa wote.
 
"Nguvu za kisiasa, na zimeitwa nguvu kwa usahihi kabisa—si kitu kingine bali mpango wa tabaka moja kukusanya nguvu ili kunyonya na kukandamiza lingine."
 
"Imepingwa na kusemwa kuwa, baada ya kukomesha umiliki binafsi wa mali, kazi zote zitakoma, na uvivu utaingia kwenye dunia nzima. Kwa mantiki hii, jamii ya kibepari ingekuwa imeshatoweka sababu ya uvivu wa kupindukia; sababu watu wake wanaofanya kazi hawapati chochote, na wale wanaopata chochote hawafanyi kazi."
 
Back
Top Bottom