KWELI Papa Francis alikataliwa ombi la kwenda Urusi kuzungumza na Rais Vladimir Putin kuhusu Ukraine

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Source #1
View Source #1
Source #2
View Source #2
Nimeona mtandaoni kuwa Papa Francis amepigwa stop kwenda Urusi kukutana na Putin Kwa ajili ya mazungumzo. Je, kuna ukweli wa taarifa hii?

Papa Francis.jpg
 
Tunachokijua
Mnamo Februari Mwaka 2022 Urusi iliivamia Ukraine katika mzozo ambao ulisababisha vita kati yao. Kufuatia vita hiyo Papa Francis amekuwa akionesha nia ya kutaka kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin ili waweze kufanya mazungumzo ya amani kuhusu Vita ya Urusi na Ukraine.

Lakini je, ni kweli Papa Francis amezuiwa kwenda Urusi kuzungumza na Rais Putin?
Mnamo 6, November 2023 kupitia mtandao wa Twitter, kurasa nyingi ikiwemo wa Megatron zilichapisha kuwa Papa alikuwa tayari kutembelea Urusi lakini alikataliwa na Lavrov (Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi) ambaye alimwandikia: "Asante, lakini hapana"

d68545bf223448149544816a4f1e620d.jpg

Picha: Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi tangu 2004
Katika uchunguzi wetu, JamiiForums imepitia vyanzo mbalimbali ikiwamo Gazeti la Serikali ya Vatican -L’Osservatore Romano - ambalo linafafanua kuwa Papa Francis kama miongoni mwa wachochea amani, alionesha nia ya kwenda Urusi muda mfupi baada ya vita hivyo kuibuka.

Akiwa katika mahojiano na mwandishi wa habari Gian Marco Chiocci kuhusu vita vinavyoendelea maeneo mbalimbali duniani, na hususani juhudi za Vatican kuleta amani nchini Ukraine, Papa Francis alisema ni muda wa kuwafikiria sana watu wa Ukraine kwani wamekuwa wakikutana na masaibu mengi, akigusia shida walizopata wakati wa utawala wa Joseph Stalin, ambaye alikuwa kiongozi wa Umoja wa Kisovieti kuanzia mwaka 1924 hadi 1953. Sera mbovu za Stalin zinaelezwa kuwa ziliwaua kwa njaa Waukraine takribani milioni nne kati ya mwaka 1932 na 1933.

Lakini ni katika mazungumzo haya Papa Francis anarudi nyuma kukumbuka hatua alizochukua siku chache baada ya vita ya Ukraine kuibuka ambapo anasema: "Siku ya pili ya vita nchini Ukraine, nilikwenda kwenye ubalozi wa Urusi. Nilihisi ni vyema kwenda huko na nilisema niko tayari kwenda kwa Putin ikiwa ingesaidia [kuleta amani]...”

Anaendelea kueleza kuwa alipofika alikuatana na Balozi (Aleksandr Avdeyev, ambaye sasa ni mstaafu) na alimpokea vizuri na kwamba tangu wakati huo alikuwa na mahusiano mazuri na ubalozi huo wa Urusi. Anaeleza kuwa mipango kadhaa ya kuwaachia wafungwa ilifanikiwa, lakini mazungumzo yaliishia hapo, na kuhusu suala la yeye kwenda kufanya mazungumzo na Rais Putin, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov alimwandikia: "Asante ikiwa unataka kuja, lakini hakuna haja." Papa anaeleza kuwa lengo lake ilikuwa ni kufanya mazungumzo na pande zote.

1699443507917-png.2807859

Kipande hiki kimenukuliwa kwenye aya ya nane (8) ya stori kama inavyosomeka kwenye L’Osservatore Romano, ambapo Papa anazungumzia kuhusu Vita ya Ukraine.

Jamiiforums pia imepata vyanzo vingine vilivyoandika taarifa hiyo na kujiridhisha kuwa ni kweli.

Hata hivyo, ingawa jambo hili limekuwa vichwa muhimu kwa baadhi ya vyombo vya habari kwa sasa, lakini si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kuieleza wazi dhamira yake ya kutaka kumaliza mgogoro huo kwa kufanya mazungumzo na Rais Putin.

Mwezi Mei 2022, Papa Francis alieleza utayari wake wa kusafiri hadi Moscow ili kukutana na Rais Vladimir Putin kujaribu kumaliza vita vya Urusi nchini Ukraine, na kueleza kuwa uvamizi huenda ulisababishwa na upanuzi wa ngome ya NATO kuelekea mashariki. Papa Francis alisema kuwa alitoa pendekezo hilo takriban wiki tatu baada ya uvamizi wa Urusi, kupitia Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, lakini bado hakuwa amepokea majibu.

Takribani miezi mitatu nyuma, vyombo vya habari vya kimataifa vilitangaza kuwa Papa Francis alienda kwenye ubalozi wa Urusi mjini Vatican kueleza wasiwasi wake kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kwa Balozi wa Moscow, jambo ambalo lilionekana kuwa ni tofauti na itifaki za kidiplomasia. Taarifa iliyotolewa baadaye na Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni, ilieleza kuwa Papa alitumia zaidi ya nusu saa kwenye ubalozi huo.

pope2.jpg

Picha: Papa Francis (Kusoto) na Vladmir Putin (Kulia)

Vatican imeendeleza nia yake hiyo kwani mnamo mwezi wa Aprili mwaka huu, Papa Francis alifafanua kwamba mipango ya kuleta amani inaendelea, ingawa bado haijawekwa hadharani.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo aliporejea Roma baada ya ziara yake ya siku tatu katika mji mkuu wa Hungary, Budapest. Wakati wa ziara hiyo, Francis alikutana na mwakilishi kutoka Kanisa la Kiothodoksi la Urusi lenye msimamo wa karibu na serikali, Metropolitan Hilarion.

Alipoulizwa ikiwa mikutano hiyo inaweza kuchangia amani, Papa Francis alisema: "Ninaamini kwamba amani huundwa kwa kufungua njia; amani haiwezi kamwe kuundwa kwa kufunga njia."

Baada ya kufanya mazungumzo kwa njia ya Zoom na kiongozi wa Kanisa la Kiothodoksi la Kirusi, Patriarch Kirill mwezi Machi 2022, katika mahojiano na vyombo vya habari mwezi mmoja baadaye, Papa Francis aliweka bayana mazungumzo aliyofanya na kiongozi huyo akisema: "Nilizungumza naye kwa dakika 40 kupitia Zoom... dakika 20 za kwanza alinisomea maelezo ya sababu za vita... nikasikiliza na kumwambia, sisi si makasisi wa serikali, hatuwezi kutumia lugha ya siasa bali ile ya Yesu."

Lakini pia Papa Francis alimuonya Patriarch Kirill asije akawa "kijana wa madhabahuni" (altar boy) wa Rais Putin, kwa sababu alikuwa akiunga mkono sababu [zisizo za msingi] za Urusi kuvamia Ukraine.

Baada ya kauli hiyo ya Papa Francis, Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi lilitoa taarifa ya kutofurahishwa na maneno ya Papa Francis na kusema ni jambo la kusikitisha kwamba mwezi mmoja na nusu baada ya mazungumzo na Patriarch Kirill, Papa Francis amechagua sauti isiyo sahihi kwa kufikisha maudhui ya mazungumzo hayo.

Taarifa ya kanisa hilo ilisema matamko kama hayo hayachangii katika kuanzisha mazungumzo yenye kujenga mahusiano mazuri kati ya Kanisa Katoliki la Roma na Kanisa la Kiothodoksi la Kirusi, ambayo ni muhimu sana wakati huu.

Tofauti na Vita ya Ukraine, Mapapa kwa miongo kadhaa wamejaribu kutembelea Moscow kama sehemu ya juhudi za muda mrefu za kurekebisha uhusiano na Kanisa la Kiothodoksi la Urusi, ambalo liligawanyika na Kanisa la Roma zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, lakini bado haijawezekana.
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom