Kwa mujibu wa mjadala wa bungeni; Wanafunzi vyuo vikuu piganieni haki yenu ya kupiga kura 25 Oktoba

Dec 11, 2010
3,321
6,328
Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2010 wengi wetu tukiwa vyuo vikuu hatukuweza kupata fursa ya kutumia haki yetu ya kidemokrasia naya kikatiba ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu huo, Serikali ya ccm ilifanya hila kwa kuhakikisha wanafunzi wengi wa vyuo vikuu hatupigi kura.

Mwaka huu kumeanza kuwa na dalili kama za mwaka 2010, sasa hivi wanafunzi wa vyuo vikuu maeneo wanayotoka tayari zoezi la kujiandikisha limesha kwisha fanyika, mathalani wanachuo wanao toka mkoa wa Njombe, Mtwara au Kagera huko tayari zoezi la kujiandikisha limesha fanyika. Wanafunzi walio maliza kidato cha sita nao wanapelekwa JKT wakiwa hawaja jiandikisha.

Bungeni leo yaliibuka maswali kuhusu swala hilo, ni matumiani yangu kuwa majibu ya maswali hayo yatawapa silaha wanafunzi wengi wa vyuo vikuu kuipigania haki yao kupiga kura.

Jisomee sehemu ya hansard ya Bunge la leo yenye majibu ya waziri mkuu kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura.

MAJADILIANO YA BUNGE

MKUTANO WA ISHIRINI
__________

Kikao cha Kumi na Mbili - Tarehe 25 Mei, 2015

(Kikao Kilianza Saa tatu Asubuhi)

DUA

Mwenyekiti (Mhe. Mussa A. Zungu) Alisoma Dua

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu

HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI:

Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na :-

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA:

Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha, 2015/2016.

NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:

Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha, 2015/2016.

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO:

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016.

MHE. MAUA ABEID ABDALLAH (k.n.y) MWENYEKITI WA KAMATI YA MAENDELEO YA JAMII:

Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2014/15 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha, 2015/2016.

MHE. MOSES J. MACHALI (k.n.y) MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO:

Taarifa ya Msemaji wa Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa Mwaka wa Fedha,2015/2016.

WAZIRI WA KAZI NA AJIRA:

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa Mwaka wa Fedha, 2015/2016.

MHE. AGNESS E. HOKORORO (k.n.y) MWENYEKITI WA KAMATI YA MAENDELEO YA JAMII:

Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa Mwaka wa Fedha 2014/15 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha, 2015/2016.

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI JUU YA WIZARA YA KAZI NA AJIRA

Taarifa ya Msemaji wa Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara ya Kazi na Ajira, kwa Mwaka wa Fedha, 2015/2016.

MWENYEKITI: Ahsante. Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri Mkuu amemteua Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu Kukaimu nafasi ya Uwaziri Mkuu, kwa hiyo sasa ndiyo atachukua nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Serikali Bungeni. Mambo yanaanza polepole, Katibu. (Kicheko)

MASWALI NA MAJIBU

Na. 78

Uhuishwaji wa Daftari la Wapiga Kura.

MHE. JOSEPH R. SELASINI Aliuliza:-

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeweka muda maalum wa kuhuisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, zoezi ambalo litaendelea wakati Walimu na Wanafunzi wako Vyuoni:-

Je, ni kwa nini Tume isiandae utaratibu utakaowezesha Walimu na Wanafunzi kujiandikisha katika maeneo watakayopigia kura;
Je, kama Tume haitafanya hivyo haioni kuwa ni sawa na kuwanyima wananchi hao haki ya kuchagua Viongozi wanaowataka


NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (k.n.y) WAZIRI MKUU Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge wa Rombo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kifungu cha 15 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina wajibu wa kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Uandikishaji unajumuisha kuhuisha Daftari ili sifa au kubadili taarifa zao. Tume ya Uchaguzi imekuwa ikihuisha Daftari la Kudumu la Mpigakura kama sheria inavyoelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za Uchaguzi zinamtaka mpiga kura kujitokeza mwenyewe kituoni kujiandikisha au kurekebisha taarifa zake inapotokea mahitaji ya kufanya hivyo. Wakati wa kupiga kura, kila mpiga kura anatakiwa aende kupiga kura katika kituo alichojiandikisha. Hata hivyo, vifungu 17, na 19 vya sheria ya uchaguzi vinatoa fursa na utaratibu kwa wapiga kura kuhamisha taarifa zao katika maeneo watakayoweza kupigia kura. Kwa utekelezaji wa vifungu hivi Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina utaratibu wa kutoa kipindi maalum kabla tarehe ya kupiga kura ili wale wanaotaka kuhamisha taarifa wafanye hivyo. Kwa mfano, katika uchaguzi Mkuu wa 2010, Tume ilitoa muda wa siku 30 kabla ya uchaguzi ili wapiga kura waliohitaji kuhamisha taarifa zao kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi nilioueleza katika sehemu (a), walimu, wanafunzi walioko vyuoni na wananchi wengine wenye mahitaji kama hayo watajiandikisha katika vituo walivyopo sasa na endapo wakati wa kupiga kura watapenda kupiga kura katika vituo tofauti na vile walikojiandikisha, utaratibu uliowekwa na Tume wa kuhamisha taarifa zao utatumika ili kuwapa haki ya kikatiba wananchi hao kushiriki katika uchaguzi


MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya hili swali yanachekesha na niseme kwa mara ya kwanza yanaudhi. Kwa sababu mimi sikuulizia wapigakura kwa ujumla wake, nimeuliza wanafunzi wa Vyuo Vikuu, wanafunzi wa Collages, wanafunzi wa Sekondari ambao hivi sasa zoezi hili likiendelea wapo mashuleni na wakati uchaguzi utakapokuwa unafanyika watakuwa majumbani. Je, hizo siku 30 zinazosemwa Vyuo vyote vitafungwa ili hawa Wanafunzi waende wakarekebishe hizo taarifa?

Swali la Pili, Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili linaendelea kwa teknolojia ambayo tunaamini ni ya kisasa, ni kwa sababu gani wanafunzi hawa wanapoandikishwa huko Vyuoni wasieleze vilevile maeneo wanapotoka ili taarifa zao zikahamishwa kwa mtandao kupelekwa kwenye maeneo ambayo wanategemewa kupiga kura, au hili linafanywa kwa maksudi mazima ili kuwanyima wanafunzi haki yao ya kupiga kura?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (k.n.y) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la msingi Mheshimiwa ameuliza wanafunzi, lakini pia na sisi tumeeleza kwamba katika muda muafaka na tukaeleza na mifano iliyotumika huko nyuma kwamba Tume kawaida kabla ya kwenda kwenye uchaguzi inatoa siku 30 za mwisho, wawe wanafunzi wa Vyuo Vikuu, wawe Watumishi wa Vyuo Vikuu, wawe Watanzania wengine wote wa kawaida, wanapewa fursa ya kubadilisha na kueleza nia yao kwamba ni wapi wangependa wapigie kura zao. Hili liko bayana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimweleze Mheshimiwa Selasini kwamba Serikali inajua kabisa kwamba Vyuo vyetu kwa sasa vina wanafunzi wengi na ambao kwa vyovyote vile hawawezi kunyimwa fursa ya kwenda kupiga kura katika maeneo ambayo wangependa kwenda kupiga kura. Hili tumeliweka bayana kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anasema kwamba tunatumia teknolojia ya kisasa kwanini wasieleze maeneo ambayo watapigia Kura. Haya mambo mengine ni masuala ya kuzungumza, ninaamini Tume wamesikia, na sisi kama Serikali tumeendelea kuzungumza na Tume. Lakini kwa sababu Tume wa Utaratibu wao, tumesema wakati mwingi siyo vizuri tukaingilia sana utendaji wa kazi wa Tume, maana itaonekana na sisi kama Bunge tunaingilia pia utendaji wa kazi wa vyombo vingine. Lakini kubwa zaidi tulilolisema ni kwamba tutahakikisha kwmaba wale wote wanapiga kura katika vituo ambavyo wangependa kupiga kura pamoja na kwamba wanaweza wakajiandikisha katika kituo chochote. Lakini tutahakikisha kwamba kama Serikali wanapiga kura bila kukosa na wala kuwa na kisingizio chochote.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri hebu subiri hapo hapo, kwa namna ya kuliweka sawa katika jibu lako la msingi la Serikali, hebu soma (b). ili Bunge lielewe msimamo mzuri wa Serikali.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (k.n.y) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuelewa. Tumejibu kwa msingi kwamba swali (b) linasema kama Tume haitafanya hivyo, haioni kuwa na kuwanyima wananchi hao haki ya kuchagua Viongozi wao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwenye majibu ya msingi…..

MWENYEKITI: No, no, no. mimi ninataka nikusaidie wewe katika jibu lako la msingi, jibu la Serikali soma kipengele cha (b) ili Mbunge aelewe Serikali imesema nini. Umenielewa?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (k.n.y) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawasawa. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi nilioueleza katika sehemu (a), Walimu, Wanafunzi walioko vyuoni na wananchi wengine wenye mahitaji kama hayo, watajiandikisha katika vituo walivyopo sasa na endapo wakati wa kupiga kura watapenda kupiga kura katika vituo tofauti na vile walikojiandikisha, utaratibu uliowekwa na Tume wa kuhamisha taarifa zao utatumika ili kuwapa haki ya kikatiba wananchi hao kushiriki katika uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye amesema wanafunzi tumeshaeleza. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, umeshajieleza. Mheshimiwa Paresso.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza:

Utaratibu wa kuandikisha mpiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR inahitaji mwananchi aweke alama za vidole, na maeneo mbalimbali wananchi wamekuwa wakilalamika zile mashine zinakuwa hazichukui alama za vidole kwa maana ya finger print. Kuna akina mama wanaenda mara mbili mpaka mara saba alama hiyo ya vidole haiwezi kuchukuliwa, Je, watu hawa ambao wanaathirika kwa namna moja ama nyingine watakosa haki yao ya kupiga kura na kujiandikisha. Nini kauli ya Serikali?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (k.n.y) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni lazima tukubali kwamba hii ni teknolojia ya kisasa ambayo inatumika katika uandikishaji na mashine zile kwa kawaida kama vidole vile, wote tunajua dole gumba zina alama fulani kama kontua. Sasa zinapokuwa zimepotea vyovyote vile mashine zile hazirekodi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watalaam wetu wanaendelea na kuhakikisha hakuna mtu kwa sababu hiyo atakayeshindwa kujiandikisha. Wameendelea kurudia na wengine wamefanikiwa. Mpaka sasa hata maeneo ambayo yameandikishwa hatujasikia kwamba kuna mtu au mpigakura yeyote au mwandikishaji yeyote ambaye amshindwa kujiandikisha kwa sababu hiyo. Baada ya marekebisho waliyofanya kufanyika wakarudia, na tuseme wote hakuna ambaye ameshindwa na wote kimsingi amejiandikisha na tutahakikisha kwamba wote wanaendelea kujiandikisha.

MHE. SAID A. ARFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Kwa kuwa zoezi hili la uandikishaji linafanyika katika Mkoa wa Katavi pia katika Jimbo la Mpanda Mjini. Lakini mashine zilizopelekwa hazitoshelezi. Kumekuwa na msongamano mkubwa na taabu kwa wananchi wanalala kwenye vituo kwa sababu ya kuandikishwa; Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba ndani ya muda huu mdogo wa wiki moja uliowekwa wananchi wote wanaandikishwa na kuwaondolea hiyo bugdha.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (k.n.y) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunaeleza hapa Bungeni kwamba ni kweli mashine zile zilianza kuja kwa awamu na ninataka nimhakikishie Kaka yangu Said Arfi kwamba mashine hizi zinaendelea kuja, na mwisho wa mwezi huu tunapokea hizi BVR 1550, na katika maeneo yale yote ambayo yanaonekana yana mapungufu tutahakikisha kwmaba vifaa hivi vinaongezwa, lakini kubwa zaidi ambalo ningependa nimhakikishie Kaka yangu Arfi ni kwamba hakuna mwananchi yeyote kwa muda tulioweka ambaye atashindwa kujiandikisha kwa sababu tu inawezekana vifaa hivi vitakuwa vichache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo nataka niwahakikishie Wabunge wote lakini pia niwahakikishie na Watanzania wote kwamba Tume itahakikisha kwamba kwa muda uliowekwa wananchi wote ambao wana sifa za kujiandikisha basi wanajiandikisha katika daftari la kupiga kura.

MH MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwa kuwa, kujiandikisha moja ya takwa la kisheria la Kikatiba ni kuwa Mtanzania na mtu mwenye umri wa miaka 18, na kwa kuwa, katika Jimbo langu la Iringa Mjini kwa sababu ya uelewa mdogo watu wengine wamekuwa wamezuiwa kuandikishwa wakitumia sheria ile ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwalazimisha wananchi wajiandikishe wale tu wanaotoka katika ule mtaa kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Je, Serikali itakuwa tayari kutangazia Watanzania kwamba wale wote wenye umri wa miaka 18 na ambao ni Watanzania wana haki ya kujiandikisha mahali pale wanapotaka?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (k.n.y) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena naomba niwahakikishie Watanzania wote kwamba wote watajiandikisha katika kudumu la Mpiga Kura kwa Mtanzania yeyote mwenye sifa, kwa maana ya kuanzia miaka 18 pamoja na sifa nyingine. Lakini hili la kwamba wajiandikishe mahali popote, tumeweka utaratibu kwmaba ni lazima watu hawa watambuliwe na vyama vyote. Huwezi ukampeleka mpigakura yeyote katika kila eneo hata pale ambapo wenyewe wa eneo hilo hawamtambui. Inawezekana Chama kimoja kikasema kinamtambua lakini wengine wa eneo lile kuna Viongozi wetu tuliowachagua kwenye mitaa, kwenye vitongoji, hao wanatusaidia sisi. Lakini tukisea kila mtu aende hata pale ambapo anashindwa kutambuliwa akajiandikishe tunaweza tukalivuruga zoezi zima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme kwamba, watu wote watajiandikisha na kutambuliwa na Viongozi katika maeneo hayo, lakini tukiruhusu vinginevyo tutakuwa tunaleta fujo na vurugu katika maeneo ya uandikishaji.(Makofi)
 
wana chuo mwaka huu watapiga kura ya kumchagua rais ubunge na mdiwani?
mwaka 2010 wanafunzi wengi wa vyuo vikuu walinyimwa haki yao ya kupiga kura je mwaka huu watapata furusa ya kupiga kura?
hivi ni kwanini serekali inawanyima watanzania wenzetu kushiriki uchaguzi wa kuchagua viongozi wao? ni rai yangu mwaka huu wanafunzi watapewa furusa ya kupiga kura na kuchagua viongozi wao wanaowapenda
 
Mwaka wa mabadiliko ni huu mbinu zote chafu za ccm zitafeli tu!!
 
lendila.waliomaliza six mwaka huu wanaenda jkt wakitoka daftar lilishafungwa.hapo inakuwaje!!
 
Ni hivi popote mlipo haki haiombwi bali inatafutwa kwa kila hali.Sasa ni hivi, kila mlipo kama ni majumbani, mnajioganaizi mnapitisha bakuli mnapata nauli na pesa za kujikimu.

Beben masufulia vikombe nk, mrudi mashuleni wekeni kambi hadi mjiandikishe na huko vile vile ombeni michango watu watawapa tena pesa nyingi mno maana wanapenda mabadiliko.Vingnevyo hamtapewa haki, idaini haki yenu.

Asanteni.
 
Mkuu kuna watu wa aina mbili wanaolengwa kunyimwa haki yao ya kupiga kura,

:Wanafunzi wa sekondari-Hawa wao walitakiwa wawe wameshajua shule walizopangiwa kwa kidato cha tano na sita.Wanabakizwa ili wajiandikishe huku uraiani ili October wawe shule washindwe kuvote.

:Wanafunzi wa elimu ya juu- Hawa watajiandikishia vyuoni na October itawakutia likizo hivyo hataweza kuvote

Hiyo solution ni kwa kundi lipi?
 
Wapendwa wakubwa naomba kujua hivi hawa wasomi wetu wao wamewekwa kundi gani maana wamemaliza mitihani Yao wamerudi majumbani kwao baadhi ya mikoa watu walishajiandikisha kupiga Kura sasa je wao serikali imewaweka kundi lipi?
 
wana chuo mwaka huu watapiga kura ya kumchagua rais ubunge na mdiwani?
mwaka 2010 wanafunzi wengi wa vyuo vikuu walinyimwa haki yao ya kupiga kura je mwaka huu watapata furusa ya kupiga kura?
hivi ni kwanini serekali inawanyima watanzania wenzetu kushiriki uchaguzi wa kuchagua viongozi wao? ni rai yangu mwaka huu wanafunzi watapewa furusa ya kupiga kura na kuchagua viongozi wao wanaowapenda
JIBU LAKE RAHISI. INAJULIKANA KARIBU WANFUNZI WOTE MKIJIANDIKISHA HAMTAICHAGUA CCM. Kwa hiyo ni afadhali kuwapotezea. au kuweka mazingira magumu na chenga za hapa na pale kupunguza idadi yenu kujiandikisha.
mfano. wengi hawajajiandikisha wakijua muda huo hawatakuepo. sasa chenga ya mwili ni kuwa lazima wawe wamejiandikisha kwanza ndio taarifa zao zihamishwe. MPO HAPO.
Kwa nini taarifa hii au utaratibu huu usifafanuliwe mwanzoni.
WASOMI MPAKA HAPO MMENISOMA
 
jamani haya manyanyaso yataendelea mpaka lini ikiwa idadi kubwa ya watanzania tena wasomi wenye uchungu na nchi yao kukosa tena haki ya kupiga kura ikiwa mahali walipojiandikishia ni vyuoni na mpaka xaxa uchaguzi vyuo vitakuwa havijafunguliwa.
mwaka 2010 ilijitokeza lakini na sasa inajirudia, kifanyike nini mwaka huu ili watu hawa waweze kupiga kura ambayo ni haki yao ya msingi.
 
Back
Top Bottom