Ijue mifumo ya urekebishaji wahalifu

Fugwe

JF-Expert Member
Aug 21, 2008
1,676
656
Nchi nyingi duniani zina mifumo mikuu miwili ya urekebishaji wahalifu waliotenda makosa ya jinai. Mfumo wa kwanza ni ule wa kuwahukumu wahalifu kifungo gerezani (Custodial Corrections) na mfumo wa pili ni wahalifu kutumikia adhabu ndani ya jamii waliyoikosea (Community Corrections).

Mifumo yote miwili kama ilivyotajwa inafanya kazi hapa nchini Tanzania kwa kusimamiwa na Idara mbili tofauti. Idara hizo moja ni ile iliyozoeleka yaani Jeshi la Magereza na Idara ya pili ambayo inaonekana ngeni miongoni mwa watanzania wengi ni ile ya Probesheni na Huduma kwa Jamii (Department of Probation and Community Services). Idara zote hizi mbili ziko chini ya wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha nchi inakuwa salama na raia wanaishi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Tuangalie vifungo vya nje (Alternative sentences). Niseme tu kwamba, vifungo vya nje vipo vya aina nyingi, nitaje vichache tu: Onyo, kuachiliwa kwa sharti la kuendelea kuwa tabia njema na kujiepusha na uhalifu wa aina yoyote, faini, kuwekwa chini ya uangalizi wa Maafisa wa Probesheni (The Probation of offender's Act, Cap.247), kufanya kazi za kijamii bila malipo (The Community service Act, Cap.291), kuwekwa chini ya utaratibu wa parole (The Parole Boards Act, Cap.400) na kifungo cha nje maarufu kama Extra Mural Penal Employment (S. 73 of the Prisons Act, Cap.58). Vingine ni pamoja na utaifishaji mali, kukatazwa kutoka kwenye eneo Fulani na vingine vingi.

Hivi karibuni, Mawaziri wa zamani wa fedha (Bazil Mramba) na Nishati (Daniel Yona) waliamriwa na Mahakama kumalizia sehemu ya adhabu iliyobaki katika mojawapo ya vifungo vya nje (Community service Act,) kwa kufanya kazi kwa masaa manne (4) kila siku isipokuwa wikend na siku za sikuuu bila malipo. Kazi hizo lazima zifanyike kwenye taasisi ya umma ili walipie madhambi waliyoyafanya. Kifungo kama hiki kinaambatana na masharti mengine, ikiwemo kutojihusisha na uhalifu mwingine au kuambatana na makundi yanayotia shaka, kutoondoka kwenye eneo la kuishi bila ruhusa ya Afisa Probesheni, kuhudhuria vipindi vya urekebishaji tabia vinavyoendeshwa na maafisa Probesheni, kufanya kazi kwa kuzingatia viwango vya taasisi husika, kujiepusha na ulevi na matumizi ya dawa za kulevya, kutoshiriki ugomvi au uchochezi wa aina yoyote na mengine mengi.

Aidha, Kifungo hiki hakiwalengi baadhi ya watu Fulani bali kila mwenye sifa bila kuzingatia umaarufu wake anaweza kutumikia kifungo hiki. Katika mkoa wa Dar es salaam, wahalifu ni wengi wanaotumikia adhabu ya namna hii. Mfano, ni mabwawa ya maji taka ya Dawasco yaliyopo kurasini, tabata, lugalo, vingunguti na kitunda yanafanyiwa usafi na wafungwa wa namna hii. Katika zahanati, vituo vya afya, ofisi za watendaji wa kata na shule wafungwa hawa wapo wengi wakitumikia adhabu kwa kufanya kazi za kutunza mazingira. Katika baadhi ya mikoa wafungwa hawa wanashiriki katika ujenzi wa shule za kata wakisomba maji na tofari, wengine huchimba vyoo vya umma na wengine wanapanda miti. Kuna wengine wanafanya adhabu kwenye makazi ya wazee na watoto yatima hususan katika mkoa wa mbeya na moshi.

Katika nchi za wenzetu kasi ya matumizi ya vifungo vya namna hii ni kubwa, mfano Rais wa zamani wa Italia bwana Beruscon amewahi kutumikia adhabu kama hii, Mike Tyson na wengine engi maarufu.

Katika dhana ya urekebishaji, ni jambo la hatari kuchanganya wafungwa sugu na wasio sugu pamoja. Ukifanya hivyo utazalisha wahalifu wengi wenye uzoefu wa kutenda uhalifu kwa mbinu za kisasa zaidi. Wahalifu wasio sugu, waliotenda makosa ambayo si hatari sana kwa jamii ni bora watumikie vifungo nje ya magereza. Kwa kufanya hivyo utaikolea serikali gharama za kuendesha magereza, utapunguza msongamano wa uhalifu magerezani, jamii itanufaika na kazi wafanyazo wafungwa hao na wafungwa wenyewe watapata fursa ya kuendelea kushiriki katika kazi za maendeleo ya jamii. Nitaendelea siku nyingine
 
Back
Top Bottom