Fikra Mbadala: Sababu Kumi (10) za Kwanini Tunakataa Hoja ya "Lazima Awe Kijana"...

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,485
40,014
Na. M. M. Mwanakijiji


Nina uhakika siko peke yangu nitakaposema kuwa sidhani kama Watanzania wana tatizo ikitokea kuwa mwaka 2015 Rais anayekuja atakuwa kijana. Sidhani kama wapo Watanzania wanaojua historia ya nchi yao ambao hawajui kuwa viongozi wetu wengi wa mwanzo walikuwa ni vijana au kwamba baadhi ya watendaji wa mwanzo mara baada ya uhuru walikuwa vijana. Sidhani kama kuna mtu ambaye anafahamu historia ya Jaji Warioba au Dr. Salim Ahmed Salim ambaye hajui kuwa wote walianza utumishi wa umma wakiwa vijana kweli kweli.


Baadhi yetu tunaopinga hoja ambayo inaonekana kurudi tena kwa nguvu kuwa Rais ajaye ni lazima awe kijana –pamoja na vigezo vingine vingi – siyo kwamba hatujui historia yetu au kwamba hatujui vijana wanaweza kushika majukumu mbalimbali ya kitaifa. Ni makosa kudhania kuwa tunaopinga hoja hii ya "lazima awe kijana" tunadharau mchango wa vijana au hatuamini kuwa wanaweza hata kuwa na Urais kwani tayari tunafahamu wapo vijana wengi tu wenye uwezo na wengine wameaminiwa kushika majukumu mbalimbali ya kitaifa – kwenye sekta ya umma au ya binafsi.


Tunaopinga hoja hii tunaipinga kwa sababu moja kubwa – ni hoja isiyopaswa kutolewa; ni hoja yenye makosa mengi ya kimantiki na kimtazamo kiasi kwamba tukiikubali tutakuwa tumekubali kulishwa mojawapo ya hoja mbaya sana na za hatari. Sidhani kama wenye kuitoa hoja hii wamefikiria kwa kina uzito wa wanachosema. Naomba nijaribu kuonesha ubovu wa hoja hii.


1. Ujana siyo kigezo cha kuwa kiongozi au cha uongozi bora .

Tutakuwa ni taifa la kwanza duniani ambalo katika kutafuta kiongozi wake wa kitaifa liliweka "awe kijana" kama mojawapo ya vigezo. Ujana ni hali ya mpito ya maisha ya kibailojia(transitionary biological state); siyo hali ya kudumu ambayo mwanadamu anayo. Kila mtu ambaye anaishi muda mrefu ni lazima atapitia hali ya ujana kwani ndivy mzunguko wa maisha unavyotaka na akiishi muda mrefu zaidi ni lazima ataishia kuwa mzee – hakuna njia nje ya hapo. Mtu hatokuwa kijana kama atakufa mtoto na hatokuwa mzee kama atakufa kijana – hakuna njia nyingine. Hivyo, kuweka kigezo ambacho mwanadamu hana uwezo nacho kukichagua ni kukosa hekima kulikopitiliza. Kimsingi ni kusema "vijana ni bora" kuliko watu wengine kwa sababu tu wao bado ni vijana. Msisitizo uko kwenye neno "bado". Hakuna uhusiano wowote (no correlation whatsoever) kati ya ujana na uongozi au uongozi bora; kwamba mtu akiwa kijana basi anaweza kuwa kiongozi mzuri zaidi au kuwa kiongozi anayefaa.


2. Ujana unaweza kuwa hoja inayofaa kwenye kazi inayohitaji zaidi matumizi ya misuli ya mwili kuliko akili.
Kama kiongozi tunayemtaka atakuwa na kazi ya kutumia misuli zaidi ya mwili basi ni wazi kuwa akiwa kijana itamsaidia sana. Kwa mfano, kama mojawapo ya majukumu ya Rais lingekuwa ni kushindana katika mashindano ya masumbwi au kunyanyua vitu vizito basi ni wazi kuwa yatupata tuchague mtu kijana na siyo kijana tu lakini kijana mwanamichezo maana siyo vijana wote wana misuli! Rais wa Tanzania atakuwa anabeba magunia wapi? Kikwete ni mzee wa miaka 63, lakini anasafiri, anasimamia miradi yake ya mananasi, wakati mwingine anahudhuria matukio makubwa sehemu mbalimbali nchini. Na hapo ni pamoja na matatizo ambayo amewahi kuwa nayo; lakini hatukusikia mwaka 2010 kwamba asingegombea kuwa ni mzee na hatusikii watu wakisema ajiuzulu nafasi yake sasa ampishe Makamu wake ambaye ni kijana zaidi! Dr. Ghaib Bilal ana miaka 69 lakini tujasikia wanaotaka Rais kijana wakisema kuwa ajiuzulu ili ampishe kijana! Sasa hawa wazee wawili wanaweza vipi kuendelea kuliongoza taifa wakati ndani ya chama chao kuna vijana wengi tu! Au hawatumii misuli ya mwili vizuri ndio maana taifa lina matatizo fulani fulani!?


3. Urais ni taasisi siyo mtu mmoja:
Hili la tatu linatokana na hilo la pili hapo juu; Rais mpendwa kijana atafanya nini zaidi akiwa Ikulu kuliko Rais wa makamu au mzee? Jambo moja ambalo wanaotaka Rais awe kijana – pamoja na sifa nyingine – wanalisahau ni kuwa Urais ni taasisi (the presidency is an institution); siyo kazi ya mtu mmoja. Urais siyo sawa na ukocha wa klabu ya mpira wa miguu – cha kushangaza makocha wa timu maarufu duniani siyo vijana! – ni taasisi. Maana yake ni kuwa Rais hafanyi mambo mengi yeye mwenyewe; amezungukwa na kundi la wasaidizi na washauri na watendaji wengi ambao wanatekeleza maagizo yake. Kimsingi Rais hutekeleza majukumu yake mengi kwa kupitia watendaji na wateule wake mbalimbali na hata kwenye kufanya maamuzi hushauriana na watu wengi sana. Ndio maana ni vizuri kukumbuka kuwa Rais hata hotuba haandiki mwenyewe labda awe na kipaji kama cha Nyerere na hata Nyerere alikuwa na wasaidizi wake katika mambo ya hotuba. Kama hili ni kweli, Rais kijana atakuwa anafanya kitu gani yeye mwenyewe ambacho Rais mzee au mtu wa makamu atashindwa kukifanya akizungukwa na misaada yote hiyo?

4. Tukiweka kigezo cha ujana kwanini tusiweke na vigezo vingine kama uzuri, urefu na ucheshi?
Kama nilivyosema hapo juu kuwa ujana ni hali ya mpito tu katika maisha na haihusiani kabisa na uwezo wa mtu kuongoza labda niirudie hili kwa namna nyingine. Ujana ni kama uzuri; vyote vinapita na ni vya muda. Unaposema unataka kuchagua mtu kuwa rais kwa sababu ni kijana ni sawa kwa namna fulani kusema unataka Rais ambaye ni mrefu, mzuri, au hata wa kabila fulani. Yaani, sifa ambazo kwa namna fulani zikikubalika zitawatenga watu wengine kwa sababu ambayo haziko ndani ya uwezo wao. Hivi ukisema Rais pia ni lazima awe kijana si maana yake ni kuwa watu wa umri wa makamo na wazee wasijitokeze kugombea? Au tunasema "wajitokeze lakini wasichaguliwe"? Lakini kwanini tusiseme basi huyo kijana pia awe mzuri? Kama uzuri unasaidia katika uongozi!


Sura nzuri katika mitazamo ya watu inaonekana ina ujana fulani, inavutia na ina ushawishi fulani. Mtu mwenye sura nzuri ni raisi kusikilizwa na hata kupata nafasi ya kusikilizwa. Wazuri ndio wanaonekana katika jamii wanapendeka kirahisi na wanakuwa na marafiki wengi. Rais mwenye sura nzuri anaweza kuwa ni mvuto kimataifa hasa katika ulimwengu huu wa wa mitandao ya kijamii ambapo watu wanapiga picha picha na watu maarufu.

5. Kiongozi mwenye kutukuza ujana atafanya nini na watumishi wazee serikalini?
Tukikubali kama namna fulani ni lazima kuwa Rais ajaye ni lazima awe kijana hatuna budi kuanza kujiuliza swali lisiloepukika – huyu Rais kijana atafanya nini na watumishi au watendaji wa umri wa makamo na wazee? atawalazimisha kustaafu ili awe na serikali ambayo watumishi wake hawana mvi? Au itabidi abadilishe umri wa kustaafu ili wazee wasiwe katika nafasi za juu bali wawaachie vijana wenye nguvu na wenye kujua teknolojia; kwa mfano kustaafu kuwa miaka 45!?

Hili swali haliepukiki kwa sababu kama taifa tutakubali ujana uwe kigezo tena cha msingi katika uongozi wa taifa ni lazima tukubali pia kuwa utumishi wa umma nao uangaliwe kwa kuwapa nafasi vijana zaidi. Na hili tulifikie hili tutafanya nini na hawa wazee ambao wanaelekea kustaafu? Lakini kama atawaacha waendelee katika utumishi wa umma atawaacha kwa sababu gani? Atateua mawaziri vijana watupu, wakuu wa mashirika vijana, wakuu wa jeshi vijana, n.k Hili swali halihitaji kuulizwa baadaye; ni vizuri kuwauliza wanaosema ni "lazima awe kijana" watujibu sasa hivi watafanya nini na hawa wazee wanaolitumikia taifa sasa hivi angalau watu waanze kujiandaa kugawana mbao! Watakapounda tume watachagua vijana tu; watakapofanya uteuzi watachagua vijana tu? Wasije kutuambia kuwa wataangalia vigezo vingine na ujana hautakuwa hoja!

6. Viongozi wa huko nyuma walikuwa vijana; hawakupewa nafasi kwa sababu ya ujana wao
Katika kusindikiza hoja hii ya "Rais ajaye lazima awe kijana" watoa hoja wanatuambia kuwa "mbona viongozi wengine wa nyuma walikuwa ni vijana"? Na mifano inatolewa; Nyerere alipokuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika alikuwa na miaka 39 hivi; na alipochukua uongozi wa TANU alikuwa katikati ya miaka ya thelathini. Dr. Salim Ahmed Salim alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Misri mwaka 1964 alikuwa na miaka 22 tu; Jaji Warioba alipokuwa mwanasheria wa jiji alikuwa na miaka 28 tu. Haya yote ni kweli lakini ukweli mwingine labda unafichika katika historia.

Wakati tunapata uhuru Tanzania haikuwa na wasomi wengi wazalendo na kwa hakika haikuwa na watu wengi wenye uwezo wa kushika nafasi mbalimbali ambazo kabla yake zilishikwa na wakoloni. Uhuru uliporudi mojawapo ya kazi ngumu sana zilizomkabili Nyerere na serikali yake ni kujaza nafasi mbalimbali; matokeo yake ni kuwa kila kijana ambaye alikuwa na usomi wa aina fulani aliangaliwa kama hazina kubwa sana ya taifa. Wapo ambao waliombwa toka wakiwa vyuoni na nakumbuka mmoja – tena mtu maarufu tu – aliitwa toka masomoni Canada kuja kutumikia taifa! Vijana kama kina Salim, Warioba, na vijana wengi walioingizwa katika serikali baada ya Uhuru na Muungano waliingizwa si kwa sababu walikuwa vijana; bali kwa sababu hakukuwa na uchaguzi mwingine na walikuwa na usomi unaohitajika katika taifa.

Ukifikiria sana tunaweza kusema kuwa baadhi ya watu waliongia katika utumishi wa umma wakati ule sidhani kama wangekuwa na nafasi leo hii katika taifa ambalo lina wasomi wengi wa nafasi mbalimbali! Leo hii tukisema tunaangalia "ujana" ni kana kwamba tunataka kusema kuwa tumeishiwa watu wenye uwezo kiasi kwamba tunaangalia vijana. Leo hii ziwa ambalo tunaweza kuvua samaki ni kubwa na lina samaki wengi kiasi kwamba kutaka samaki kijana tu ni kujinyima samaki wengine wengi wazuri!

7. Uzoefu una hoja na hatuwezi kupuuzia
Suala la uzoefu linakuja kwa namna nyingine. Watoa hoja hii wako sahihi kabisa wanaposema kuwa tusiwakatae vijana kwa sababu hawana uzoefu. Na wako sahihi kuwa uzoefu unakuja baada ya kupewa nafasi ya kutumika na baadhi ya vijana ambao wanaonekana wanautaka Urais sasa hivi tunaweza kusema wana uzoefu katika utumishi wa umma. Hata hivyo, hoja hii tuiangalie kwa namna nyingine.

Hakuna kitu muhimu katika uongozi wowote ule kama uzoefu na uzoefu unakuja ama kwa kufanya mambo fulani kwa mara nyingi au kufanya mambo fulani katika muda mrefu zaidi. Katika uongozi wa taifa naamini ni uzoefu mpana zaidi unahitajika na hili hauwezi kuliondoa. Rais wa nchi kama ya kwetu anahitai kuwa na uzoefu mpana na ikiwezekana katika mambo mengi na ya muda mrefu. Kwa sababu hii peke yake ni vigumu sana kuona jinsi gani leo tunaweza kumchagua mtu ambaye hajawa katika muda mrefu katika nafasi ya utendaji. Binafsi sijaona mahali popote ambapo kampuni au taasisi iliyofanikiwa ambayo imeweza kufanya hivyo bila kumweka mtu mwenye uzoefu mpana na wa muda mrefu katika kazi fulani.

Leo hii kampuni yoyote ikitangaza nafasi ya Mkurugenzi Mkuu au Afisa Mtendaji Mkuu sidhani kama kuna itakayosema kuwa mtu huyo awe ‘kijana' na asiwe na uzoefu wa kutosha katika fani au mambo fulani. Kila mkuu wa kampuni - hasa kampuni kubwa zilizofanikiwa – ni muhimu kuwa mtu ambaye ana uzoefu wa muda wa kutosha ama katika uongozi, fani, menejimenti , utawala n.k Na watu wanaoajiri hawa wanaangalia historia ya huyo mtu kwa kirefu na kuona mafanikio katika nafasi mbalimbali.

Katika uongozi wa taifa tunataka kumwajiri CEO wan chi. Yeye ndiye Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa utawala wan chi yetu na ambaye chini yake kutakuwa na vyombo vingi vyenye kugusa maisha ya Watanzania. Hivi kweli tunaweza kusema mtu huyo ni "lazima awe kijana"? Tukisema hivyo siyo kwamba tutajinyima sisi wenyewe watu wenye uzoefu na umahiri ambao unapatikana katika miaka mingi? Lakini kwa vile uzoefu siyo takwa la lazima kwenye katiba hatuwezi kusema vile vile kuwa ni lazima "awe na uzoefu mkubwa". Ujana na uzoefu siyo sifa za msingi sana.

8. Kuwa kijana haina maana kuwa mzalendo zaidi
Hoja nyingine ambayo inatolewa na sijui ni kwa kiasi gani imefikiriwa vizuri ni kuwa vijana wana uzalendo zaidi. Hivi hili tunalipima vipi? Mtu mmoja mmoja inawezekana anaweza kuonekana ni mzalendo lakini tunaweza vipi kuupima huu uzalendo kuwa unatokana na ujana? Ndio maana wengine hata tumepuuzia hoja kuwa uzalendo unaweza kufundishwa kwa nyimbo! Hivi kama vijana wana uzalendo zaidi kweli taifa letu lingekuwa hapa leo hii? Mbona tuna vijana wanafanya mambo ya ajabu kweli kweli kwenye uongozi na wengine wanaamini wanaongozwa na uzalendo huo huo. Wengine wanasema ati wazee ndio wamelifikisha taifa hapa na kuwa sasa tunahitaji vijana; hivi tunasahau kuwa hawa tunaowaita ‘wazee' na ambao wanaonekana hawana uzalendo au uadilifu na wenyewe waliingia katika utumishi huu huu wakiwa vijana.


Kwani baadhi ya watu ambao wanaonekana siyo viongozi wazuri au hata wale wenye chembe za wazi za ufisadi sin a wao waliingia katika utumishi wakiwa vijana? Sasa hawa vijana au wale wanaotaka kwa lazima kuwa Rais ajaye awe kijana watatupa uhakika gani kuwa wao watakuwa tofauti huko wanakozeeka – kwani watazeeka bila ya shaka. Au wao wakizeeka watakuwa tofauti? Maana nina uhakika hata hawa wazee ambao leo tunawaona hawafai walipoingia walipitia JKT, waliimba nyimbo za kizalendo na wengine kwa hakika walifanya mambo mengi ya kizalendo lakini mahali fulani huko mbeleni wengine ndio hivyo tena. Naweza kusema kabisa kuwa yawezekana wazalendo hasa hawako kwenye hizi nafasi za kuchaguliwa; wengi yawezekana wako kwenye utumishi wa umma. Watu ambao majina yao hayatajwi kwa sifa, hawaandikwi magazetini, hawafuatiliwi na vyombo vya habari wala nini lakini kila siku wanaamka alfajiri kuwahi kwenda kazini! Watu ambao kwa miaka ishirini au thelathini wamejitahidi kulisukuma hili gari letu bovu liende na linajikokota!



9. Kuwa kijana siyo lazima kuwa na maarifa, fikra au mitazamo mpya na bora!
Tatizo jingine la hoja hii ni kuwafanya watu waamini kuwa Rais kijana atakuwa na mawazo, fikra na mtazamo mpya kulinganisha na kama atakuwa na Rais wa makamo au mzee. Kosa hili linatokana na kudhani (presume) kuwa ujana = upya wa mawazo. Kwamba, mtu akiwa kijana basi moja kwa moja (automatically) anaweza kuwa na mawazo mapya. Hii ni fallacy (upotofu wa hoja) ya aina yake katika hoja. Upotofu huu unatokana na kudhania tena kwa makosa makubwa tu kuwa akili ya mwanadamu ni kama kaseti au santuri za kizamani ambazo ukisharekodi kitu basi huwezi kurekodi kitu kingine ndani yake; hivyo kikiwemo kitu cha zamani basi huwezi kuweka kitu kipya. Kwamba, mtu kijana ana uwezo wa kupokea maarifa na fikra mpya kuliko mtu wa makamo au mzee.

Hii si kweli. Siyo kweli kwa sababu elimu ya viumbe na hususan mwanadamu inatuonesha pasi ya shaka yoyote ile kuwa akili ya mwanadamu ina uwezo mkubwa wa kupata taarifa mpya hadi akiwa mzee sana. Na kama akili ina afya basi umri peke yake hautoshi kumfanya mtu kupoteza uwezo wa kujifunza, kufikiri au kubuni mambo mapya. Kama ingekuwa kweli kwamba mtu mzee hawezi kuwa na fikra mpya au hawezi kupata maarifa mapya makampuni au hata nchi nyingi duniani zisingekubali kuongozwa na watu wa makamo na wazee.

Watu wazima na hata wazee wa kizazi cha leo na ambao wanajifungua kujifunza na kuendelea kutumia akili yao vizuri wanaweza kabisa kushindana na kijana yoyote katika masuala ya elimu, ubunifu na kutumia maarifa mpya. Hivyo, kuwa mzee siyo hukumu ya kudumu ya kuwa mtu hawezi kufikiri na kuwa kijana siyo leseni ya kuwa mtu ana fikra mpya. Mara nyingi watu wanaosema "lazima awe kijana" wanataka tuamini kuwa mtu akiwa mzee basi moja kwa moja hawezi kufikiria au anaupungufu fulani kichwani. Ukweli ni kuw hili si lazima isipokuwa kama kweli mtu ni mzee sana na ana matatizo yanayotokana na uzee (kama dementia n.k). Lakini wazee wengi tu hadi miaka yao ya tisini bado wana uwezo wa kufikiria, kuandika na hata kujifunza mambo mapya. Ukweli wa hili unaonekana katika vyuo vikuu vingi na sehemu ambapo wazee bado wako kwenye utumishi. Kwa kadiri kwamba mtu anajiweka katika hali nzuri ya afya – ya kimwili na kiakili – basi uwezo wako haupungui kwa kiasi cha kushindwa kabisa.


Na kama suala ni afya vijana wana matatizo yao ya kiafya ambapo labda wazee hawahangaiki nayo sana. Pamoja na hayo vijana kutokana na uchangamfu wao wanaweza kuwa katika hali ya kuendekeza tabia ambazo zina madhara ya kihisia, kiakili hata kimwili. Ulevi, tamaa n.k vyote vinahusiana na ujana. Lakini hata hivyo, mtu akiwa kijana hadhaniwi tu moja kwa moja kuwa ana matatizo au tabia mbaya zinazohusishwa na ujana. Ndio maana huwezi kumkatalia kijana kuwa kiongozi ati kwa sababu "ni kijana". Kila kijana au mzee anapaswa kuhukumiwa kwa hali na matatizo yake siyo kuhukumiwa kwa ujumla (collective punishment).

Kwa hiyo ni kweli inawezekana kuwa kijana akaja na mawazo au fikra mpya lakini tuna uhakika gani zitakuwa ni fikra bora kuliko zinazoweza kutolewa na watu wengine? Siyo kwamba wakati mwingine vijana waliofikiri wana mawazo mapya (hasa ya kitaaluma) wamejikuta wakiabishwa na mawazo ya wazee yaliyojaribiwa katika Chuo Kikuu cha Muda Mrefu?

10. Siyo LAZIMA rais ajaye awe kijana
Tatizo la mwisho la hoja hii limejificha katika mantiki nzima ya "lazima awe kijana". Unaposema kitu ni "lazima" maana yake ni kuwa hakuna uchaguzi mwingine wowote isipokuwa hilo. Kwamba, mtu akisema ni "lazima upate leseni ili uweze kuendesha gari" basi hakuna jinsi nyingine kwani hilo ni jambo ambalo huna kingine cha kuchagua (option). Kwenye suala la Urais kusema "lazima awe kijana" ni hoja isiyo na mantiki kwani hakuna mahali popote katika Katiba yetu ambapo panasema hilo na sidhani kama kuna chama chochote kinaweza kusema hilo. Jambo pekee ambalo liko wazi na ni la lazima ni kuwa mtu huyo ni lazima atimize masharti ya kikatiba na kwenye suala la umri sharti la Katiba (Ibara ya 39:1b) iko wazi kuwa anayetaka kugombea ni lazima "awe amefikisha umri wa miaka arobaini". Kwa maneno mengine; mtu anaweza kusema Rais ajaye ni "lazima awe si chini ya miaka 40".

Kwa vile Katiba haijaweka kikomo cha umri wa juu kabisa na wala haisemi kuwa inapendekeza awe na umri unaokaribiana na miaka arobaini basi kudai kitu kingine chochote ni kutokuheshimu matakwa ya Katiba hii – pamoja na ubovu wake wote – na kujipa madaraka ambayo mtu mmoja mmoja hana. Tunapotaka Rais atakayeheshimu Katiba ni lazima aoneshe kuwa tayari anaheshimu Katiba.

Wenye kupendekeza kuwa Rais awe kijana wanaweza kufanya hivyo wakisisitiza tu kuwa hayo ni matamanio yao, ni mapendekezo yao lakini si matakwa ambayo watu wengine wanapaswa kuyakubali au hata kutumia lugha ya kuwa ni "lazima". Hakuna ulazima wowote – wa kimantiki au vinginevyo – wa kwanini Rais ajaye awe kijana.

Sasa naweza kuendelea na kuandika mengi lakini nimalize kwa kusema kuwa vijana wana nafasi; wana nafasi ya kulitumikia taifa na kutumia muda zaidi kujiweka katika mazingira ya kulitumikia taifa huko mbeleni. Ukiwa kijana huna haraka ya uongozi mkubwa wa namna hii kwani unaweza kukufikia tu. Na kama mtu ni kiongozi mzuri na anafaa wala haitaji kudai ujana wake kama kigezo kwani watu watamuona tu kuwa anafaa. Hii ndio sababu ya kwanini watu kama Nyerere na wengine ambao wamekuwa vijana waliaminiwa na watu wa vizazi vyao kuwaongoza. Obama alichaguliwa na watu wengi si kwa sababu alikuwa kijana zaidi; haikuwa hoja kwa Wamarekani. John F. Kennedy alipochaguliwa na Wamarekani kuwa Rais wao wa 35 alikuwa na miaka 46 wakati Obama alikuwa na miaka 47 alipochaguliwa. Kama hawa ni mifano ya vijana basi hoja ya kuwa Rais wetu awe chini ya miaka 40 haina msingi na sidhani kama kuna Mtanzania ana tatizo na Rais mwenye umri wa kati wa miaka juu ya 45!

Hoja hii ya "rais ni ajaye ni lazima awe kijana" ni hoja ya kuitupilia mbali. Ninaamini watu wanaotaka kuwa Rais wa Tanzania watajipambanua wenyewe kutokana na uwezo wao wa kuongoza, ushawishi wao, uadilifu wao, hekima na busara na kwa ujumla wake jinsi gani wanaweza kuongoza taifa la watu wenye tofauti nyingi kama la kwetu. Suala la umri wao siyo suala la lazima kama vile suala la jinsia zao, dini zao, makabila au mahali wanapotoka lisivyo suala la lazima. Ni sawasawa kabisa na watu watuambie ati Rais ajaye ni lazima "atoke Kusini" au "Atoke pwani"! Inavutia wasikilizaji lakini ni ya kipuuzi (an absurdity).

Watanzania wanahitaji kuwa na kiongozi mwenye maono, kiongozi mwenye ushawishi wa kuelekea maono hayo na ambaye atakuwa tayari kuwashawishi Watanzania wakubaliane na maono yake kwa taifa na kutoa uongozi kufikia maono hayo. Kama mtu huyo atakuwa kijana, mtu wa makamu au mzee haijalishi kabisa. Kama mtu huyo atakuwa Mhaya, Mmakua, Mndemba au Mchagga haipaswi kuwa hoja. Tunapokataa hoja hii ya "ujana" kwani inabagua watu kwa kitu ambacho hawana uwezo nacho tunakataa vile vile hoja ya kiongozi ajaye ni lazima awe Mkristu au awe Mprotestanti; tunakataa pia hoja ya kuwa kiongozi ajaye asitoke Kaskazini au ni lazima Atoke Kusini au kama wengine walivyosema ni lazima atoke Pwani!

Tukikubali hoja ya ni "lazima awe kijana" basi ni lazima tukubali pia ni lazima awe mzuri na itabidi tuangalie pia kabila lake, dini yake, na ikiwezekana tuangalie pia urefu wake! Vinginevyo, kwa mamlaka nilijipa mimi mwenyewe na ambayo hayana kukatiwa rufaa natangaza hoja ya ujana kufungwa rasmi. Tuzungumzie uwezo wa wagombe wetu bila kujali umri wao, dini, makabila, rangi, mahali wanakotoka, jinsia na hata familia wanazotoka. Tukiangalia kwa mapana hayo tunaweza kujikuta tunapata Rais mzuri kweli kweli, hata kama inatokea kuwa atakuwa ni kijana.

Ujana wenyewe siyo issue kama vile uzee au umri wa makamo siyo issue. Sasa kwanini tufanye issue kisicho issue?

Why make an issue a non issue?

Niandikie:
mwanakijiji@jamiiforums.com
 
Ninajua wanotangaza kutaka urais kwa karata ya ujana wanayajua haya, bali wanafanya ili wapate kutangazwa na kujitangaza kisiasa hasa kwa sasa hivi. Pia wanafahamu hawataupata huo urais.
 
Mzee MM kama main think tank ya JF tulianza kumiss vitu hivi hadhimu vya kufikirisha.......

Naamini wamekusikia.....hii najua hawatainukuu kwenye pages zao za FB lakini ujumbe umepenya vizuri.....Kudos Legendary .....Sina la ziada maana huu ni mjadala wa longtime na wewe pia una mabandiko kibao juu ya hili.....
 
Hatutafuti kijana wa kwenda kuchumbia magogoni,kama kuchumbia waende msoga!!

Hatutafuti kijana aende akabebe vyuma ikulu kwani ikulu sio kambi ya wapigana mieleka!!!

Hatutaki nyimbo zao za raisi kijana kwani hatutafuti raisi kijana wa kwenda jando!!

Vibaraka wa mafisadi waandae santuri nyingine ya kupigia chapuo la vimada wao wa kisiasa,hii ime-flop na haikubaliki kabisa kwa maslahi ya taifa na umma!!!
 
Mzee Mwanakijiji,
Ni kweli kabisa uyasemayo lakini kizazi kipya hawakubaliani na wewe wala mimi. Labda ebu nisaidie wewe kujibu maswali niloulizwa na mwanangu ya kwamba mbona miye sipendi nyimbo za Justine Bieber wakati anauza! Sipendi nyimbo za Diamond wakati ndiye kioo cha nchi? Kwao uzee ni sawa na kupitwa na wakati kifikra.

Na kaniuliza tena hivi kweli baba unaamini Quincy Jones na Babyface wanaweza kuandika na ku produce nyimbo leo na zikauzika kama kina Jay Z na Rehana ktk muziki wa kisasa!. Ati wakiwa na maana uchumi wa leo ni huo wa digital maneno yote kwenye keyboard sio kuja na magitaa sita, ngoma na kadhalika ili ipate muziki safi. Sisi wazee (above 40+) tutauweza wapi?. Nilibaki kukaaa kimya, wewe ungemjibu nini kuhusu hofu yake na wazee ktk uchumi wa leo.
 
Mzee Mwanakijiji

Shukrani kwa kukemea tabia hii inayoanza kuibuka ya kuwatenga wazee wetu. Inasikitisha na kuchefua sana kuona CCM wanakuwa vinara wa ubaguzi.
 
Unapokuja mjadala wa nani awe rais wa nchi yetu, hatuangalii umri, ukabila, jinsi, dini wala ukanda wake.

Tutatakiwa tujihoji tunamtaka mtu wa namna gani? Katiba imeweka sharti la kuanzia miaka 40 na kuendelea, na walioweka hawakufanya makosa.

Kimsingi kiongozi tunayemtaka ni lazima awe mzalendo na nchi yake, lazima awe mzalendo na wananchi, awe na uwezo wa kuongoza nchi yetu.

Asiwe kama kikwete anayesema sina ubia na mtu, huku akitofautiana na vitendo vyake. sijaona rais muhuni nchi hii kama kikwete
 
Mzee Mwanakijiji,
Ni kweli kabisa uyasemayo lakini kizazi kipya hawakubaliani na wewe wala mimi. Labda ebu nisaidie wewe kujibu maswali niloulizwa na mwanangu ya kwamba mbona miye sipendi nyimbo za Justine Bieber wakati anauza! Sipendi nyimbo za Diamond wakati ndiye kioo cha nchi? Kwao uzee ni sawa na kupitwa na wakati kifikra.

Na kaniuliza tena hivi kweli baba unaamini Quincy Jones na Babyface wanaweza kuandika na ku produce nyimbo leo na zikauzika kama kina Jay Z na Rehana ktk muziki wa kisasa!. Ati wakiwa na maana uchumi wa leo ni huo wa digital maneno yote kwenye keyboard sio kuja na magitaa sita, ngoma na kadhalika ili ipate muziki safi. Sisi wazee (above 40+) tutauweza wapi?. Nilibaki kukaaa kimya, wewe ungemjibu nini kuhusu hofu yake na wazee ktk uchumi wa leo.


Mkandara,with all due respect,tafadhali usihangaike kutafuta mifano ya kuhalalisha usanii wa hawa kijana wetu kadhaa ambao urefu wa kamba zao na mnunua kamba zao wanajulikana!!

Mfano wako wa Muziki- mziki ni aina moja wapo ya hoby,ndani ya hoby kuna migawanyiko kama ilivyo mziki ambapo kuna vanga,chakacha,bakurutu,salsa etc! Usilete hoja dhaifu ya mapenzi ya mziki na vizazi kwa kushahibisha na uongozi wa nchi au taasisi.

Uongozi ni kariba,kariba haipatikani kwa vijana tu na pia sio wazee tu ingawa naamini utakili kuwa kuishi kwingi/umri mrefu huongeza maarifa kwa hiyo hoja ya ujana kama nyenzo kuu ni mufilisi!!!

Uongozi ni busara,hekima na uapambanuaji wa mambo mujarabu kwa musitakabali wa uwaongozao,kwa ustawi wa leo na vizazi vijavyo,sifa za utambuzi wa hayo haupo mahsusi kwa vijana!!

Mfano wako wa uchumi na kizazi cha sasa cha digital,unajaribu tena kuhalalisha hoja mufilisi kwa hoja mfu!! Tusaidie kutuambia,katika kituo chako cha kazi ulisoma kabla ya kizazi cha digital,kwa nini hujapisha kisa we ni kizazi cha kale??!! Unahisi hoja na mfano wako una mashiko kweli kulingana na elimu na hadhi yako??!!

Mkandara,hivi theories za uchumi wa kidigital kama ulivyosema zinatofauti gani na kale??!! Law of demand and supply ya miaka 20/40 iliyopita ina utofauti na leo?!!

Me binafsi najua ni rafiki mkubwa wa kijana mmoja wapo kama mshauri wake pia,pengine ungetangaza maslahi yako na kutueleza kwa hoja mjarabu zenye mashiko kwa nini unamuunga yeye na tofauti na wengine,siyo kutu-drug kwa mifano ya mywpesi kwa kwa suala kubwa na nyeti linalogusa maskini,wasiojua kusoma na watu wa vijijini kwa hoja mufilisi za mifano ya watu wa kati waluovimberwa na fursa za kujuana!!
 
Mzee Mwanakijiji,

Unajua msimamo wangu kuhusu vijana kwenye mbio za urais maana miaka 2 iliyopita tuliijadili sana sana

Nakubaliana na wewe kama kuna kauli "Ni lazima awe Kijana".Huo ni ubaguzi.Lakini pia nikiri kuwa vijana wanaweza nao wasibaguliwe.Tuwe taifa la Fursa kwa wote.Tusibague watu

Ben Saanane, right on. Kimsingi haipaswi kabisa kusema "awe kijana" au "awe mzee". Katiba imeweka umri si chini ya miaka 40; period. Kusema "vijana wanaweza" ni sawasawa na kusema "wazee hawawezi"; suala la ujana au uzee siyo issue kabisa. Sidhani kama kuna mtu atabisha kuwa wapo vijana wenye uwezow a kuongoza nchi yetu hata kuwa Rais; na sidhani kama mtu anaweza kusema hakuna wazee wenye uwezo kama huo. Si vyema kutoa kauli za kijumla (generalization statements) wakati mtu anamzungumzia mtu mmoja mmoja. Tunachohitaji ni mtu mwenye uwezo wa kuwa rais na ambaye kama suala la umri linakuja asiwe chini ya miaka 40.
 
Mimi naona the biggest debate kuhusu uchaguzi ujao nijinsi waTanzania wengi walivyo choka hata kujadili hao wagombea.......wanahangaika kujitangaza but watu wengi wanajadili mpira na mengineyo.....watu wako so fed up na wanasiasa.....
 
Mzee Mwanakijiji,
... Kwao uzee ni sawa na kupitwa na wakati kifikra.

Na kaniuliza tena hivi kweli baba unaamini Quincy Jones na Babyface wanaweza kuandika na ku produce nyimbo leo na zikauzika kama kina Jay Z na Rehana ktk muziki wa kisasa!. Ati wakiwa na maana uchumi wa leo ni huo wa digital maneno yote kwenye keyboard sio kuja na magitaa sita, ngoma na kadhalika ili ipate muziki safi. Sisi wazee (above 40+) tutauweza wapi?. Nilibaki kukaaa kimya, wewe ungemjibu nini kuhusu hofu yake na wazee ktk uchumi wa leo.

Mzee mwenzangu huyu mtoto anaonekana ni mtu mwenye fikara sana. Hata hivyo ni vizuri kumsaidia kufikiri vizuri. Mojawapo ya matatizo ya watoto wetu na hata vijana ni kufikiri kwa makosa na katika kufikiria hivyo anafikia hitimisho lenye makosa. Umesema vizuri hapo juu kuwa "kwao uzee ni sawa na kupitwa na wakati kifikra". Hili ni suala la mtazamo wenye makosa tu ambao naamini unaweza kuusahihisha.

Uzee siyo sawa na kupitwa kifikra. Wapo wazee na watu wenye umri mkubwa ambao bado wanaandika na kutunga nyimbo nzuri na hata kazi nyingine za kisanii. Na hata leo wakifanya concerts bado wanajaza kushindana na kina Rihanna na hawa kina Diamond (labda siyo kwa Tanzania). Paul McCartney (72) ni mwanamuzi wa enzi za Beatles; lakini hata leo bado anavuma; Cher (68) naye yupo bado kwenye anga za muziki. Hata ukija kwenye Hip Hop kwani Snoop hajihuishi tena na muziki kwa sababu amepita miaka 40? Na hapo hatujawataja kina Mic Jagger, Bono na wengine. Hili la muziki ni rahisi kuwaelewesha watoto; suala la kipaji ni suala la kipaji na mtu mwenye kipaji hakiishi akiwa amepita miaka 40. Kitaisha au kitafifia kama hajiweki uptodate na maendeleo mengine ya sayansi ya muziki.

Lakini kwenye suala la uongozi ni rahisi zaidi kulielezea na kusahihisha mtazamo potofu kwani ndio kama huo wa mtoto; kwamba kwa baadhi ya hawa wanasiasa mtu akiwa mzee manake ni kuwa hata fikra zake zimezeeka au ni dhaifu. Tukikubali hili inabidi tujiulize kwanini basi wawepo watu wenye umri mkubwa kwenye vyuo vyetu vikuu wakifundisha wasiwaachie vijana wenye damu moto? Tujiulize kwanini watu wenye makampuni yao makubwa bado wanaendelea kuyasimamia badala ya kuwaachia vijana wadogo? Kwanini inaonekana ni watu waliona umri mkubwa tena wengi over 55 ndio wanaonekana kuendesha makampuni, kusimamia nchi n.k duniani? Vijana hawatali dunia; wanaweza kuchochea sana mabadiliko lakini hawatawali.

Angalia nchi zote ambapo kumetokea mapinduzi uone kama kuna kijana alipewa uongozi wa nchi. Madagascar walijaribu hili la kijana na alionekana mwenye uwezo tu. Andry Rajoelina alizaliwa mwaka 1974 na alianza kazi ya uDJ na mambo mengine na akiwa umri mdogo alikuwa Meya wa Antananarivo. Umaarufu wake ulimfanya aingie katika siasa na hatimaye kuwa Rais wa nchi hiyo. Ujana wake haukumzuia hata kidogo kufanya makosa aliyoyafanya kisiasa.

So, ni suala la kusahihisha mitazamo tu. Ukinisoma vizuri utaona kuwa sisemi na sijawahi kusema vijana hawafai au hawawezi kuongoza nchi yetu. La hasha, I'm not that presumptious.
 
Du yale aliyotukanya Nyerere bado kuna wapumbavu wameyashikilia , utawasikia "Mie safari hii namchagua huyu" wakiulizwa kwa nini ,wanajibu"ni kijana Aisee "

Hahaaaaaa kweli wanatuchekesha hawa !
 
Mkandara usilete mzaha ktk hili kwa kutumia hoja za mapenzi ya muziki kwa mambo makubwa na ya msingi.
 
toka zito kabwe alipokura njama za kuiua chadema kisa kapewa madaraka na ccm sina ham na vljana tena wao waendelee tu kusugua bench urais ubaki kwa akina lipumba slaa na wazee wengine sasa hatuwezi pata kijana kama alivyokua nyerere
 
toka zito kabwe alipokura njama za kuiua chadema kisa kapewa madaraka na ccm sina ham na vljana tena wao waendelee tu kusugua bench urais ubaki kwa akina lipumba slaa mbowe mbatia na wazee wengine sasa hatuwezi pata kijana kama alivyokua nyerere
 
Back
Top Bottom