Ajali iliyoua sita yakatisha ndoto za mwanafunzi

Kikwajuni One

JF-Expert Member
Mar 18, 2013
13,145
6,951
Ajali iliyoua watu sita na kujeruhi 16 imekatisha uhai wa mwanafunzi aliyekuwa akisoma Shahada ya kwanza ya Mipango Miji na Uhifadhi Mazingira katika Chuo Cha Mipango jijini Dodoma, Amani Matinde (24) ambaye alikuwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa vitendo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Julai 22, 2023 katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Sekou Toure jijini Mwanza, kaka wa marehemu, Baraka Magabe amesema mdogo wake alimaliza mafunzo kwa vitendo jana Ijumaa Julai 21 ,2023.

Baraka amesema baada ya kumaliza mafunzo hayo mdogo wake ambaye alikuwa anatarajia kuingia mwaka wa pili chuo kitakapofunguliwa aliamua kupumzika kwa siku kadhaa jijini Mwanza kwa mjomba wake kabla ya kwenda wilayani Tarime Mkoani Mara.

Amesema mdogo wake huyo ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto saba wa familia yao alikuwa na ndoto ya kufanya kazi serikalini atakapohitimu masomo hayo sambamba na kuendeleza kipaji chake katika riadha.

“Imeniuma mno, tunakamilisha taratibu za kuchukua mwili katoka Mochwari kwa ajili ya kuusafirisha kwenda nyumbani kwetu Tarime kwa ajili ya maziko,” amesema Baraka

Mwanafunzi aliyekuwa anasoma Shahada ya Mipango Miji na Uhifadhi wa Mazingira na Amani, Amon Faustine amesema atamkumbuka kwa nidhamu, ucheshi na uchangamfu wake na kuongeza kuwa alikuwa akijitoa kuwasaidia wanafunzi wenzake darasani.

"Alikuwa rafiki yangu ninayeishi naye chumba kimoja, ameniachia maumivu makubwa mno, ametuachia kumbukumbu nzuri ya kuishi vizuri na watu tunamuombea Mungu aipumzishe roho yake mahala pema," amesema Amon

Katika taarifa yake kuhusu ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya amesema watu sita wamefariki na 16 kujeruhiwa kutokana na ajali hiyo.

Msuya amesema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na msako wa kumtafuta dereva aliyekuwa akiendesha gari lililowagonga wanachama wa Klabu ya wakimbiaji ya Adden Palace. Ajali hiyo imetokea katika barabara ya Kiseke eneo la Lumala wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Makorongo Manyanda, Peter Fredrick, Shedrack Safari, Selestine Safari, Hamis Wariri na Aman Matinde (24).
 
Back
Top Bottom