SI KWELI Africa Cancer Foundation wanatoa Matibabu ya Bure ya Saratani ya Matiti kwa Wanawake

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
SARATANI YA MATITI PRESS RELEASE.jpg


Nimeona ujumbe wa WhatsApp unaotaka watu watume majina ya Wagonjwa wa Saratani ya Matiti kabla ya Machi 7 ili watibiwe bure.

Nina ndugu yangu ni mgonjwa. Naomba kufahamu kama tangazo hili lina ukweli ili nisitapeliwe bure.
 
Tunachokijua
Africa Cancer Foundation (ACF) ilianzishwa Aprili 6, 2011 kama Shirika la hisani, na kuzinduliwa rasmi Julai 12, 2011 huko Nairobi, Kenya. ACF inafanya kazi kuelekea Afrika isiyo na saratani kwa kukuza uzuiaji wa saratani na kutoa suluhisho kamili kwa watu walioathiriwa na saratani barani Afrika.

Katika kujitahidi kufanya hivyo, ACF hutafuta kuweka viwango bora vya utendaji na kukuza ubadilishanaji wa uzoefu na vituo vilivyopo vya ubora kote ulimwenguni na hivyo kupunguza pengo la maarifa kati ya ulimwengu ulioendelea na unaoendelea.

ACF pia huongoza utafiti wa saratani na uundaji wa miongozo ya uchunguzi, upimaji na matibabu ya saratani pamoja na kutetea serikali kuweka kipaumbele kwa ajenda ya saratani na kuongeza huduma za kinga, uchunguzi na matibabu ya saratani katika Bara la Afrika.

Madai ya kutoa Matibabu ya bure ya Saratani ya Matiti
Mapema Mwezi Februari 2024, taarifa zinazoihusisha taasisi hii kutoa matibabu ya bure kwa wanawake wanaougua saratani ya Matiti zilianza kusambaa kwenye mtandao wa Kijamii wa WhatsApp.

Ujumbe huo unasema:
"Wapendwa,
Tafadhali Kama unajua kuhusu mwanamke yeyote anayepambana na SARATANI YA MATITI kwa hatua yoyote tafadhali mshauri awasiliane na Dorothy@africacancerfoundation.org kabla ya tarehe 7 Machi, gharama zote za matibabu ni bure.

Tafadhali usiuweke kwako ujumbe huu, SHARE kwenye makundi na kuokoa maisha ya mwanamke huyo"


Ukweli wake upoje?
Baada ya kufanya ufuatiliaji wake, JamiiCheck imebaini kuwa taarifa hii si ya kweli.

"Ujumbe uliopo kuhusu upasuaji wa bure wa Saratani ya matiti si wa sasa. Tafadhali usiutilie maanani, kwani ulitumwa mwaka 2022 kwa wanawake 200 wenye kansa ya Matiti kwa ajili ya upasuaji wa bure. Upasuaji ulifanyika wakati huo, na hakuna ufadhili zaidi uliopo kuendelea na huduma hiyo" amesema Osita Chidoka, Afisa wa Taasisi hiyo.

Osita amewaasa watu kuacha kusambaza ujumbe huo kwani ACF haitoi Msaada wa upasuaji wa kansa ya matiti bure kwa mwaka 2024.

Aidha, barua rasmi ya Africa Cancer Foundation (ACF) iliyochapishwa Februari 5, 2025 ilikanusha pia madai hayo, ikibainisha kuwa tayari walikuwa wamepokea zaidi ya maombi 20,000 ya wagonjwa kutoka nchi za Tanzania, Burundi, Senegal, Canada, Zimbabwe, Senegal, Nigeria, Congo, Uganda, na Kenya wakiomba msaada huo.

"Kwa bahati mbaya hakuna upasuaji wa bure kwa wagonjwa wa Saratani utakaofanyika mwaka huu kwa kuwa hakuna fedha iliyotengwa kwa kazi hiyo. Ujumbe unaosambazwa sio wa sasa,na hauendani na hali halisi iliyopo wakati huu", inasema sehemu ya barua hiyo.

GFh_03kXcAAQc78

Barua rasmi ya ACF kukakusha uwepo wa huduma hii kwa mwaka 2024 (Chanzo: X)
"Habari potofu hii imeonyesha mzigo mkubwa wa matibabu ya kansa ambao wagonjwa wa kansa wanakabiliana nao kila mahali na maombi yanayoingia kwa uchunguzi, msaada wa uchunguzi, matibabu na usimamizi wa aina zote za kansa," anasema Wairimu Mwaura, Mratibu wa Programu.

Taasisi hiyo inaufahamisha umma kwamba wanatafuta kwa bidii fedha za kuendeleza programu hii lakini kwa sasa hakuna fedha zilizopo. Mara tu fedha zitakapopatikana watatoa taarifa rasmi kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom