Haya tumekusikia.
SHANGWE, nderemo na vifijo vilitanda kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma kwa takribani dakika 10 wakati Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alipohudhuria akiwa miongoni mwa wageni huku wabunge wakitaja mambo tisa kuwa chanzo cha kumshangilia sana kiongozi huyo wa zamani wa nchi.
Kikwete, maarufu kama JK, aliingia bungeni asubuhi kushuhudia kiapo cha mkewe, Mama Salima Kikwete, aliyeteuliwa kuwa mbunge na Rais John Magufuli Machi mosi, mwaka huu.
Katika kikao hicho cha kwanza cha mkutano wa saba wa Bunge la 11, JK aliingia ukumbini saa 2:50 asubuhi na kutoka saa 3:20 baada ya kile kilichoonekana kuwa ni kuzidi kwa shangwe zilizokuwa zinaelekezwa kwake na wabunge waliokuwa chini ya uongozi wa Spika Job Ndugai. Kwa kiasi kikubwa, hali hiyo ilionekana kuathiri utulivu na ratiba ya kikao hicho.
Udhibiti wa safari za nje unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano tangu iingie madarakani na kuathiri pia ziara za mafunzo za wabunge; ukosefu wa kupungua kwa posho za vikao na pia madai ya kuingiliwa kwa kazi za kamati zao ni baadhi ya mambo yaliyotajwa na wabunge kuwa chanzo cha kushangiliwa sana JK, wakidai kukumbukia “neema” kadhaa wanazoamini kuwa sasa hawazipati kwa kiwango sawa na enzi za utawala wake wa awamu ya nne.
Baada ya kutoka ukumbini, JK alitumia dakika takribani tano kupiga picha na wabunge na watu mbalimbali waliokuwapo kwenye viwanja vya Bunge, kisha akaongozana na wasaidizi wake kuanza safari ya kutoka nje ya eneo hilo.
Kabla hajaingia kwenye gari, JK aliombwa kuongea na waandishi wa habari kuhusu kilichotokea bungeni lakini hakuwa tayari akisema: "Mimi si mbunge, siwezi kuzungumza hapa (bungeni)."
ILIVYOKUWA BUNGENI
Dalili za kushangiliwa kwa JK zilianza kuonekana mapema alipoingia ukumbini baada ya baadhi ya wabunge waliomuona kusikika wakisema 'tumekumiss JK' (tumekukumbuka JK).
Baada ya kupigwa kwa wimbo wa taifa na kuapishwa kwa Mama Salma, Spika Ndugai aliuliza kwa Katibu wa Bunge juu ya kinachofuata katika ratiba na kujibiwa kuwa ni kipindi cha maswali.
Hapo, Spika akasema kuwa kabla ya kipindi hicho kuanza, atambulishe kwanza wageni mashuhuri waliopo bungeni na ndipo akamtaja JK na kuamsha shangwe za wabunge zilizodumu takribani dakika 10.
Spika Ndugai alikiri kuwa haijawahi kutokea mgeni kushangiliwa kiasi hicho ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria katika kipindi chote cha ubunge wake.
"Waheshimiwa wabunge, mimi binafsi hiki ni kipindi cha nne nikiwa bungeni sijawahi kuona mgeni akipokelewa kwa kiwango hiki," alisema Ndugai.
Baadhi ya wabunge walisikika wakiomba JK aingizwe kwenye Ukumbi wa Bunge ili awasalimie huku Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT - Wazalendo), Zitto Kabwe, akiomba fursa ya kupatiwa nafasi ya kutoa hoja kupitia 'utaratibu' wa Bunge, ambayo hakupatiwa, hata hivyo.
Baada ya kuona Bunge zima linashangilia, Spika Ndugai aliwataka wabunge kumpa heshima zaidi JK kwa kumshangilia wakiwa wamesimama.
"Kwa makofi hayo, sasa naomba mumpe 'standing ovation' (heshima wanayoitoa watu waliokuwa wamekaa kwa kusimama na kumshangilia mtu aliyefanya jambo muhimu)," alisema Ndugai.
WABUNGE WATAJA MAMBO 9
Wakielezea sababu ya kuwapo kwa shangwe hizo ambazo Spika Ndugai alikiri kuwa hajawahi kuzishuhudia hapo kabla, baadhi ya wabunge walitaja mambo tisa kwa nyakati tofauti.
1. ni hali ya wabunge kukumbukia baadhi ya mambo wanayoamini kuwa yalikuwa mazuri enzi za JK lakini sasa hayapo. Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema kitendo cha JK kushangiliwa sana bungeni ndicho kinachoashiria jambo hilo.
"Haijawahi kutokea ndani ya Bunge mgeni kushangiliwa kiasi hiki.
Hii si mara ya kwanza marais wastaafu kuingia bungeni. Huu ni ujumbe kwa serikali iliyopo madarakani. Leo (jana) wabunge wamesema kwa vitendo kwa kumshangilia kupita kiasi rais aliyeondoka madarakani," alisema.
Aliongeza: "Kilichonishangaza kuliko vyote ni aina ya ushangiliaji. Wabunge wamepiga makofi, lakini pia wamesimama, na waliosimama ni mpaka Waziri Mkuu na mawaziri wengine.
"Na bado wametamka wazi kuwa wanaisoma namba, na wengine wanamwambia JK kwamba wamemkumbuka.
Ni ujumbe kwa serikali. Inapaswa kujitathimini. Na hawa si watu wa mtaani, ni wabunge,” alisema Selasini.
2. zuio la kurushwa moja kwa moja kwa matangazo ya Bunge kupitia vituo vya luninga. Hii ni sababu iliyotajwa pia na Selasini kuwa imesababisha wao kumkumbuka zaidi JK na kujihisi kuwa ‘wame-mmiss”.
" Kufunga Bunge 'live' ni tatizo, wabunge wanataka wanachokifanya bungeni kionekane kwa wananchi wao. Haya ni baadhi ya mambo yaliyofanya wabunge wamshangilie sana JK.
3. Aidha, Selasini alitaja jambo la tatu kuwa ni kucheleweshewa malipo yao na Serikali, jambo ambalo wakati wa JK lilikuwa nadra kutokea.
“Kuna wakati posho na mishahara inachelewa. Kipindi cha JK hatukuwahi kukosa pesa za uendeshaji wa Bunge," alisema Selasini.
4. kwa mujibu wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT), ni hisia za kutokuwapo kwa uhuru wa kutosha wa kuzungumza na demokrasia kulinganisha na ilivyokuwa wakati wa JK.
"Kikwete alitumia muda wake wa uongozi kutoa uhuru kwa watu kusema watakacho, na hata waliokuwa wanamtukana, yeye alikuwa kama mzazi, hakuchukua hatua zozote.
Aliachia vyama vya upinzani vifanye siasa bila shida yoyote. Kwa hiyo, watu wamekumbuka hayo ambayo kwa sasa hayapo. Ndiyo maana wakamshangilia," alisema Zitto.
5. ni kutofuatwa kwa sheria ya bajeti. Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alidai kusuasua kwa serikali kutekeleza miradi ya maendeleo ndicho kiini cha JK kushangiliwa kwa mbwembwe bungeni.
"Serikali inakiuka sheria za nchi. Bajeti haijatekelezwa na kuna pesa zimetumika bila idhini ya Bunge…hatukuwa na bajeti ya kuhamia Dodoma. Sheria zinakiukwa waziwazi. Wakuu wa wilaya leo wana ving'ora," alisema Msigwa.
6. kwa mujibu wa Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ni mchango ambao JK aliutoa katika kukuza siasa na demokrasia nchini, huku akiwataja baadhi ya wanasiasa walionufaika na hilo kuwa ni pamoja na yeye .
"JK ameshangilia kwa sababu wabunge wengi amewakuza kisiasa. Kina William Lukuvi (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na hata mimi binafsi. Kipindi cha Kikwete ndiyo nilikua kisiasa.
Amewagusa wabunge wengi. Kama alivyosema Nay wa Mitego -- 'waliommiss' (waliomkumbuka) JK wapo, ndiyo kama wabunge," alisema Bashe.
7. ni udhibiti wa safari za nje. Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alidai kuzuiwa kwa safari za nje za wabunge ni sababu mojawapo ya kushangiliwa sana JK kwa sababi enzi za utawala wake walipat fursa hizo.
8. ni hisia za baadhi ya wabunge kuwa Serikali ya sasa imekuwa ikiingilia majukumu ya Bunge mara kwa mara, na hasa kwa kuingilia utendaji wa kamati zake kiasi cha baadhi ya viongozi (wa kamati) kuamua kujiweka kando.
"Tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa kamati za Bunge wanajiuzulu kutokana na serikali kuingilia majukumu yao…kitu kama hiki hakikuwahi kutokea kwenye uongozi wa JK, " alidai Waitara.
9. kwa mujibu wa Waitara, ni miradi iliyopitishwa katika bajeti kutotekelezwa ipasavyo.
“Miradi mingi iliyoidhinishwa na Bunge haijatekelezeka, imekwama. Bajeti imekwama halafu serikali inaongeza bajeti,” alisema na kuongeza:
"Kikwete ameshangiliwa kwa mapenzi ya dhati ya watu… kwamba ni mtu ambaye wanamkumbuka."
SABABU ZAIDI
Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya Salum (CCM), alisema JK amepata mapokezi makubwa bungeni kutokana na mambo mazuri aliyoyafanya katika miaka 10 ya uongozi wake.
"JK alifanya makubwa sana kwa Tanzania kiuchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa. Aliimarisha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege.
Watu wanakubali mchango wake katika taifa hili ni mkubwa na ndiyo maana ukaona wabunge wanamshangilia. Hicho ndicho kiliwatokea wabunge leo (jana)," alisema.
John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), alisema uhuru wa Bunge umeminywa hivi sasa na ndiyo mana JK alishangiliwa sana.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM), alisema JK ameshangiliwa na wabunge kwa sababu alikuwa kiongozi wao kwa miaka 10 na hilo ndiyo kubwa.
"Tulikuwa tumemkumbuka kwa sababu muda mwingi hatujawa naye… ni hulka ya binadamu unapoona na mtu ambaye ulikuwa haujamuona kwa kipindi kirefu, unafurahi kwa kiasi kikubwa," alisema Aeshi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) .
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alidai JK amepata mapokezi makubwa bungeni kutokana na mwenendo wa serikali ya sasa kutowaridhisha baadhi yao.
"Taifa limemkumbuka JK kwa sababu matarajio ya serikali ya awamu ya tano imewakatisha tamaa wananchi. Hakuna Sh. milioni 50 kila kijiji, hakuna mafisadi waliosimama kwenye mahakama ya mafisadi…kilichopo ni kamatakamata tu," alidai Sugu.
Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Bungala, maarufu Bwege' (CUF), alisema kushangiliwa kwa shangwe kwa JK bungeni jana kulitokana na kitendo cha Rais Mstaafu huyo kuenzi demokrasia katika uongozi wake.
"JK alikuwa mtu ambaye yuko tayari kukosolewa. Ndiyo kitu ambacho watu wanafurahi. Kwa hiyo hata leo (jana) bungeni wabunge walifurahi kuona mtu aliyeenzi demokrasia tofauti na hali ilivyo kwa sasa. Kikwete alikuwa kiongozi, sasa tuna utawala," alidai Bwege.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Njombe, Lucia Mlowe (Chadema), alidai wabunge walimshangilia JK kutokana na kuwapa uhuru katika uongozi wake.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema JK alishangiliwa sana kwa sababu wananchi walimpenda na aliachia kila sehemu ikashamiri.
Chanzo: Nipashe