Watawala wa Wasukuma, Waha, Wahaya, Wazinza, Wanyamwezi na Wafipa walikuwa Wahima(Watutsi). Kuna ukweli kiasi gani?

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Jan 31, 2021
9,046
15,913
Haya yameandikwa katika kitabu Zamani Mpaka Siku Hizi. Inadaiwa Wahima(Watutsi ni Wahima walioelekea magharibi kwenye vilima vilivyoitwa Tutsi) Walipotoka kaskazini kwenye karne ya 14 walikuwa na nguvu na maarifa mengi. Hilo liliwafanya kila walikopita, kuanzia Uganda hadi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria walijiweka kuwa watawala.

HABARI ZA NCHI ZILIZO MAGHARIBI

Somo 1-Wahima

KATIKA sura ya kwanza tulisoma ya kuwa sisi Wabantu si watu wa asili wa nchi tunazokaa sasa maana tulitoka nchi nyingine tukawasukuma watu waliokuwa wakikaa huku au labda tulichanganyika pamoja nao. Hatuna hakika miaka mingapi imepita tangu tulipoanza kuhama kuja katika nchi hizi, lakini imedhaniwa inapata miaka 2,000 mpaka 3,000. Basi tukaja tuakenea pote tukatawanyika tukafanya makabila mengi na lugha vile vile iligawanyika ikafanya lugha nyingi.

Lakini hatukuachiliwa kukaa peke yetu, na baada ya miaka mingi, watu waliokuwa wakikaa kaskazini walianza kuingia katika nchi hizi kama sisi tulivyoingia zamani sana. Labda walikuwa wale wale waliosukuma babu zetu wakawafanya kuhama kutoka nchi zile walizokaa zamani katika kaskazini. Yaani sisi tulisukuma Watukoko na Wabilikimo tukakaa katika nchi yao, na halafu sisi tulianza kusukumwa na watu wengine. Watu hawa hawakuingia katika nchi hii, lakini wameacha alama za nguvu zao na kwa hiyo imetuhusu tujue habari zao. Hatuna maandiko wala sanamu zinazoweza kutusaidia kueleza habari zao wala kujua walikuja zamani gani, lakini pengine tumehadithiwa watawala wangapi waliotawala katika nchi fulani na hivi tunaweza kukisia tarehe.

Tena tunaweza kujifunza habari zao kidogo kwa habari walizozikusanya Wazungu wa kwanza waliokuja kusafiri katika nchi hizi.

*****

Basi katika sura hii tutasimuliwa habari za sehemu ya nchi iliyo katika magharibi ya kaskazini mwa Tanzania, yaani wilaya za Bukoba, Mwanza, Tabora na Kigoma.

Wenyeji wanaokaa katika sehemu hii ya nchi yetu ni wengi sana, jumla yao ni sehemu ya tatu kwa moja ya wenyeji wote wa Tanzania. Watu hao wote ni Wabantu ila kuna wachache wenye damu ya wageni, lakini watawala walio wengi si Wabantu ila ni wageni. Watawala hao waliojiweka juu ya wenzao ni Wahima, na asili yao wametoka katika taifa la wale watu waitwao Wahamiti waliotoka Kaskazini.

Labda zamani Wahima hao walifanana na Wamasai wanaokaa katika nchi yetu sasa, nao vile vile walitembeatembea wakitafuta malisho kwa makundi ya wanyama wao, lakini baadaye walifuata desturi ya kukaa mahali pamoja kama wanavyokaa Wabantu. Labda walipigana na Wabantu wakawashinda, au labda Wabantu walijiweka chini yao kwa hiari zao, hatuna habari.

Wahamiti hao wanakaa hasa katika nchi ya Ruanda, na hapo wanaitwa Watusi. Hata leo wanajulikana kwa kuwa ni watu warefu tena wembamba, na sura zao ni za kipanga, na rangi yao ni nyekundu kuliko ile ya Wabantu. Watu hao ndio walioleta ng'ombe wale wenye pembe ndefu sana kutoka kwao ambao tunaweza kuwaona Bukoba, na Ankole, na Ruanda na mahali pengine ambapo Watusi walipojiweka kuwa wakubwa wa nchi.

Watu wenye maarifa juu ya mataifa hukubali kuwa Wahima ni Wahamiti, na hudhani ni Wagala au taifa jingine lililo asili ya Wasegeju na Wamasai. Ni ajabu sana ya kuwa karibu kila mahali wanapokaa watu hao katika nchi yetu, lugha yao ya asili imewapotea na sasa hutumia lugha ya watu walioshindwa nao na hata wakitaka kutaja babu zao huwaita kwa majina ya Kibantu. Lakini wengine wanayo lugha ya Kihamiti hata sasa, kama vile Wamasai na wengineo.

Kama tulivyosema, hatuwezi kujua hakika Wahima hao walifika lini katika nchi hii mara ya kwanza, na kwa kuwa habari zao za zamani zimechanganyika sana na hadithi, hatuwezi kupambanua zilizo za kweli na zilizo hadithi tu. Lakini Padre mmoja wa Misioni ya Kikatoliki huko Uganda amezichungua sana, kwa hiyo tutafuata maneno yake katika kusimulia habari zao. (Père Julien Gorju, ndiye aliyetunga kitabu cha Kifaransa chenye habari za Wahima kiitwacho 'Entre le Victoria, l'Albert et l'Edouard'.)

Wahima wote wanajua asili yao walitokea nchi za kaskazini, na ya kuwa ufalme mkubwa ulisimamishwa na babu zao katika nchi ya Bunyoro, tena husema kuwa watawala wote wa Wahamiti walitokea ufalme huo. Bunyoro si katika nchi yetu ila ni katika nchi ya Uganda, lakini inatuhusu tujue habari hizi kwa sababu watawala waliotoka huko walijiweka katika nchi yetu pia. Ufalme huo uliitwa Kitara ukasimamishwa zamani kabla ya kusimamishwa ufalme wa Buganda unaoendelea hata sasa. Hatujui Kitara ulisimamishwa zamani gani, lakini tunajua kuwa ni zamani sana kwa sababu tunayo hakika kuwa wafalme 32 au pengine wanahesabiwa kuwa 36, wametawala katika ufalme wa Buganda, na kama tulivyosema, Kitara ulisimamishwa kabla hajaanza kutawala yule mfalme wa kwanza wa Buganda.

Watu waliosimamisha ufalme huo wa Kitara walikuwa Wahamiti. Lakini ufalme wa Kitara haukudumu miaka mingi sana ukaisha. Labda watu wa jamaa au ukoo mwingine walishindana ili kusudi wapate utawala, au labda waliugawanya ufalme sehemu nyinginezo.

Wakati huo Wahamiti walikuwa wakihama kutoka kaskazini wakitafuta nchi nyingine ili wapate mahali pazuri pa kukaa, au labda walikuwa wakisukumwa na watu wengine waliokuwa wakikaa kaskazini zaidi, hatuna hakika. Lakini huelekea kuwa kweli, maana kama ilivyo katika historia ya nchi za dunia ndivyo baba zetu walivyokuja wakawasukuma Watukoko na Wabilikimo, tena ndivyo Wahamiti walivyotusukuma sisi Wabantu tuliokaa kaskazini.

Basi miaka ikapita na zamani ya mwaka 1,300 hivi, watu wengi zaidi walihama kutoka kaskazini pamoja na mkubwa wao aliyeitwa Ndahura, wa jamaa ya Bachwezi. Ndahura alikuwa na nguvu, maana alisimamisha ufalme mkubwa sana ulioenea kutoka Ziwa Albert mpaka Ziwa Victoria, na ufalme huo uliitwa Kitara vile

****

vile. Ufalme huo ulisitawi sana na hasa wakati aliotawala mfalme mmoja aitwaye Wamala, lakini ndipo habari za jamaa hiyo ya Bachwezi zikakoma kabisa. Wengine husema kuwa jamaa ilitoweka, lakini sasa watu huhadithia kwamba watu wa jamaa hiyo waligeuka miungu! Imedhaniwa ya kuwa wakati huo ulikuwa katika miaka iliyo karibu na 1675.

Basi huku nyuma ufalme mwingine ulisimamishwa katika nchi ya Bunyoro na mtu jina lake Mpugu wa kabila moja la Wahamiti. Mpugu alianzisha jamaa ya Babito akaitwa Mpugu kwa sababu alikuwa mweupe kidogo, au labda alikuwa zeruzeru. Baba yake Mpugu alikuwa wa jamaa ya Bachwezi akaitwa Kyomya. Imehadithiwa kuwa Kyomya alitembeatembea sana mpaka alifika kilima kiitwacho Elgon katika nchi ya Kenya, na hapo alikutana na mwanamke chini ya mti unaoitwa Bito akakaa naye, na halafu yule mwanamke alizaa pacha. Mtoto mmoja aliitwa Mpugu na wa pili aliitwa Kintu.

Basi baadaye Mpugu alisafiri akafika mji mkuu wa Bachwezi akaushika ufalme, lakini wakati huo aliitwa kwa jina jingine, ndilo Wunyi. Mwingereza mmoja Baker alisafiri katika nchi hizi katika mwaka 1871 ili apeleleze habari za mito na milima na maziwa ya nchi, naye ameandika habari kuwa alikutana na mfalme mmoja aliyekuwa wa kumi na tatu kutawala tokea wakati ule aliotawala Wunyi.

Yule mtoto wa pili, Kintu, alisimamisha ufalme mwingine. Watu wengine husema kuwa Kintu alikwenda akashika ufalme wa Ntege aliyekuwa mkubwa wa Buganda wakati ule, lakini alimwacha atawale chini yake. Baadaye Kintu alitoweka na Ndahura aliyekuwa mfalme wa kwanza wa jamaa ya Bachwezi aliyetawala katika Bunyoro, alimwua Ntege, akampa mwanawe Kyomya ufalme wa Buganda kuutawala.

Ufalme mwingine ulisimamishwa Toro na mtu wa jamaa hiyo hiyo, na George David Kumurasi Rukidi III anayeitawala nchi hiyo sasa ni mfalme wa kumi na moja kutawala tokea uliposimamishwa.

Mpaka sasa tumesimulia habari kidogo za nchi zilizo jirani na nchi yetu ili tufahamu vizuri mambo yaliyotokea halafu katika nchi yetu. Basi sasa na tuache tukasimulia habari za Wahima waliokuja wakakaa katika nchi yetu ya Tanganyika.

Katika nchi ya Bukoba kwa upande wa kusini mwa mto uitwao Kagera kuna nchi inayoitwa Kiziba; huko ufalme ulisimamishwa na Kaganda, mtu wa taifa lile lile la Wahamiti. Katika hadithi ya Kibunyoro imesimuliwa kwamba Kaganda ni mwanawe Wunyi yule tuliyemtaja, naye ndiye aliyeusimamisha ufalme wa Babito katika Bunyoro. Lakini hadithi ya Kiganda inasimulia kuwa Kaganda ni mwanawe Kintu aliyekuwa mfalme wa kwanza wa Buganda. Basi Kaganda alitoka kwao Kyagwe akafika Buddu iliyo upande wa kaskazini mwa mto Kagera. Kutoka huko alisafiri mpaka Buyaga kando ya Ziwa Victoria, alipotoka huko alivuka kisiwa Sese. Kutoka Sese alisafiri tena mpaka Bwende katika ghuba iitwayo Sango, na mwisho alisafiri akafika Kyawa.

Tumetaja safari hizo kwa sababu zingali zinakumbukwa na watu wa huko, maana zinaonyeshwa katika desturi zinazoshikwa wakati wa kumweka mtawala mpya. Mtawala mpya huogeshwa kwa heshima kwa maji yanayoletwa kutoka Kibiro iliyo kando ya Ziwa Albert, tena hutiwa chumvi inayoletwa kutoka Kitunga iliyo katika nchi ya Buddu mahali alipokaa Kaganda kwa muda, na hapo ndipo alipowaacha wengine wa wafuasi wake. Mioto yote katika nchi huzimwa, na moto mwingine huletwa kutoka kisiwa cha Sese, kwa sababu yasemwa Kaganda alichukua moto unaoheshimiwa sana na Wanyoro akauacha Sese, na kwa hiyo alirudi huku kutoka Bwende ili aje auchukue.

Basi alipokuwa akitoka kaskazini, Kaganda alifika Kyowa, na hapo alikutana na mwana wa mfalme aliyekuwa amefukuzwa kutoka Kiziba, akafanya shauri naye la kumwua Ntumwa aliyekuwa mfalme wakati huo. Shauri lao likafanyika, na yule mwana wa mfalme aliushika ufalme, na Kaganda akawa waziri wake. Hatimaye yule mwana wa mfalme alikufa, na Kaganda alishika ufalme wa Kiziba akautawala. Basi hii ndiyo namna alivyopata ufalme wake. Lakini tendo hili la kuuliwa mfalme wao liliwachukiza sana wenyeji wa nchi kwa sababu walisadiki kuwa ni ishara mbaya itakayowaletea misiba na taabu. Basi tokea wakati huo walimwita Kaganda kwa jina la 'Kibi' na maana yake ni 'Kiovu' au 'Kibaya'. Imesemwa ya kuwa Kibi aliishi sana mpaka akawa mkongwe, akafa akazikwa mahali kaskazini mwa mto Kagera, yaani kukumbuka mahali alipotokea.

Kabla ya kufa kwake, Kibi aliusia kwamba mwanawe Samula awe mfalme baada ya kufa kwake, lakini jamaa ya yule Ntumwa mfalme aliyeuawa aliweza kuushika tena ufalme kwa muda, mpaka Samula alipata msaada wa mfalme wa Buganda wakamfukuza yule jamaa ya Ntumwa. Ndipo Samula alipopata jina la Nyakabinga' maana yake, 'Yule aliyefukuza.'

Samula hakupenda watoto wake wala wakubwa wa taifa lake wadhaniwe kuwa wenyeji, yaani Wabantu, hivi aliwaita kwa majina ili asili yao isisahauliwe, akawaita watoto 'Waziba' na wakubwa wa nchi aliwaita 'Wahima.' Tena hakupenda wachanganye damu na ile ya wenyeji, na kwa muda mrefu wana wa mfalme walioa watoto waliozaliwa na wale waliofuatana na Kaganda kutoka kwao. Hata sasa jamaa za watawala wanaheshimu sana miiko ya kabila la Babito, lakini mtawala mwenyewe hufuata desturi ya Kiganda, yaani hushika mwiko wa jamaa za mke wake ili kusudi kuwaheshimu. Desturi hiyo ililetwa na Kimera wa Buganda.

Hatujui tarehe alipoanza kutawala Kibi, lakini tokea wakati wake, wafalme kumi na watano wa jamaa yake wametawala ufalme wa Kiziba mpaka Mutahangarwa alipoanza kutawala. Mutahangarwa alikufa katika mwaka 1916.

Sasa tuchungulie kidogo habari za ufalme wa Wahinda. Kuna nchi nyingine inayoitwa Kiziba ya Kusini, na pengine inaitwa Ihangiro, lakini lazima tukumbuke ya kuwa ni mbali mbali na nchi ya Kiziba tuliyokwisha taja. Tulisimulia kuwa watu walidhani ukoo wa Bachwezi wa Bunyoro walitoweka kabisa wakageuka nchi nyingine wapate kuzishinda. Hadithi zinashuhudia kuwa miungu, lakini kwa kweli haikosi walihama kwenda kutafuta ufalme huu ambao tutasimulia habari zake sasa, ulisimamishwa zamani ya mwaka kama 1675, yaani wakati ule walipotoweka jamaa ya Bachwezi.

Imehadithiwa ya kuwa mtu aitwaye Ruhinda au Luhinda alihama kutoka kwake akaenda Buddu, kisha akaondoka akaenda Koki. Labda Bachwezi walishindwa au labda walihama kutafuta nchi nyingine, yaani walitoweka, na Ruhinda alikuwa mmojawapo waliohama. Basi alipofika Koki alikutana na mhunzi mmoja aliyetoka nchi ya Uzinza, ambayo ni nchi inayojulikana sana kuwa nchi ya wahunzi wa jamaa ya Warongo. Mhunzi huyo alianza kueleza habari za nchi ya Uzinza na Ruhinda aliposikia kuwa mfalme wa nchi hiyo ni mtu dhaifu, aliazimia kwenda huko. Alipofika, alijidai kuwa mganga mkubwa awezaye kuleta mvua, na baada ya kupita muda alipata nguvu akajifanya mtawala wa nchi ya Uzinza na Ihangiro na Karagwe na Urundi. Lakini halafu alipokuwa akisafiri kwenda Kagera kutoka Ihangiro alikufa katika kijiji kiitwacho Lwazi, na ule ufalme aliousimamisha ulivunjika ukagawanywa katika sehemu tatu, yaani Uzinza na Ihangiro, na Urundi na Karagwe.

Nchi ya Ankole iliyo jirani inatawaliwa na Wahima, nao hudai ya kuwa wametokea ukoo wa Ruhinda. Lakini yule Padre tuliyemtaja kuwa amechungua sana katika habari hizi, anadhani kuwa hawakutokea jamaa ya yule Ruhinda aliyetawala Uzinza na Karagwe na Ihangiro, ila labda ya Ruhinda mwingine.

Imesemwa kuwa Ruanda pia ilikuwa katika ufalme huo wa Wahinda, lakini hatuna habari safi juu ya hayo, na kwa kuwa Ruanda si sehemu ya Tanzania, basi habari zake hazituhusu sana. Yatosha kusema kuwa Watusi ambao ni kabila kuu la Ruanda, ni damu moja na Wahinda, yaani wale wanaoitwa pengine Wahima na pengine Wahuma. Tena imehadithiwa asili ya jina hilo Tusi ni jina la milima mirefu iliyo upande wa magharibi inayoitwa Ututsi na Warundi, na labda watu hawa Wahamiti walipewa jina hilo na wenyeji wa nchi hiyo.



Somo 2-Kuendelea na habari za Wahima

Ruhinda alipokufa, ufalme wake uligawanywa katika sehemu tatu, na wafalme wa Karagwe, yaani sehemu moja na ufalme, walitwaa majina ya Ruhinda na Ntare. Wa kwanza aliitwa Ruhinda na wa pili Ntare, na wa tatu Ruhinda na kuendelea hivi kwa vizazi kumi na moja. Wafalme kumi na wanane walitawala katika ufalme huo. Mwingereza mmoja jina lake Speke aliyesafiri katika nchi hizi kutafuta habari nyinginezo, alifika hapa katika mwaka 1861 akamkuta Rumanyika mwanawe Dagara akitawala nchi. Rumanyika alimpokea vizuri sana akamfurahisha kwa ajili ya akili na wema wake. Speke aliandika kitabu chenye habari za safari zake, na tukikisoma tutaona kuwa Rumanyika alikuwa mtu mwenye nguvu nyingi, na watawala wengine wa Kihinda walikubali kuwa yeye ni mkubwa wa jamaa yào, na mfalme wao.

Kwa muda kidogo ufalme huo wa Karagwe uliharibika, maana nchi ya Ihangiro ilitengwa ikawa ufalme wa peke yake ukatawaliwa na mtu aitwaye Sebahinda. Lakini baadaye uliunganishwa tena na Wadachi, na Kahigi aliyekuwa jamaa wa Sebahinda ambaye alipendwa sana na Wadachi, alipewa ufalme kwa sababu walitaka kumfurahisha. Kahigi alikufa katika mwaka 1916. Wahinda wanaotawala kisiwa cha Ukerewe walitoka Ihangiro, na Makaka aliyeanza kutawala katika mwaka 1895 ni mtawala wa kumi na nane tangu walipokiteka kisiwa.

Nchi ya Uzinza, yaani Usui iliyo katika wilaya ya Bukoba, na Uzinza katika wilaya ya Mwanza zilikuwa zikitawaliwa na mtawala mmoja wa Kihinda mpaka katika enzi ya Dagara wa Karagwe, ndipo alipotawala Rwona au Lwoma, na Dagara alimshauri kugawanya nchi na kufanya falme mbili. Basi watoto wa Rwoma, Suwarora na Ruhinda, walipewa kila mmoja sehemu yake. Suwarora alipewa nchi ya Usui na Ruhinda alipewa Uzinza iliyo upande wa Mwanza.

Baada ya kupita muda, Uzinza uligawanywa tena ukafanywa falme nne, ukakaa hivyo mpaka mwaka 1926, ndipo sehemu hizo zilipounganishwa kuwa ufalme mmoja ukatawaliwa na mtu mmoja aliyechaguliwa na wenyeji waliotoka Ukerewe.

Mhinda mmoja alisimamisha ufalme mwingine ulio mdogo, na nchi zilizokuwa katika ufalme huo ni Kiyanja na Kyamtwala na Bugabo, lakini hakuweza kuzishika, na Bankango wa Usui akaja akamnyang'anya nchi za Kyamtwala na Bugabo akamwachia nchi ya Kiyanja tu.

Haya ni majina ya utawala wa Uzinza na Ihangiro: Ruhinda; Ntare (huyu alifia kisiwa kiitwacho Kome); Kabambo Katobaa; Kabula; Nyamulasya (huyu alifanya Kome kuwa mji wake mkuu); Kyeda; Kinwa; Kabambo wa pili; Kabula wa pili; Kakalaza (huyu alifanya Butendwe kuwa mji wake mkuu akafia safarini wakati alipokuwa akienda Uha); Mwiyakabi; Ruhinda wa pili (huyu alipewa jina la Muhangakyaro baada ya kufa kwake).

Kabla hatujaacha kusimulia habari za nchi zilizo karibu na Ziwa Victoria na Ziwa Albert na Ziwa Tanganyika, inafaa tutazame kidogo dalili za utawala wa Wahamiti zinazoonekana pengine katika nchi hizo.

Nchi za Nera na Buhungukira na Usmao ni katika upande wa mashariki wa Uzinza katika wilaya ya Mwanza. Imesemwa kuwa nchi hizo zilikuwa ufalme mmoja ulioanzishwa na mtu mmoja jina lake Wile. Imehadithiwa kuwa huyu Wile alitoka Uzinza akaonana na mwanamke mmoja aitwaye Mhindi, na yeye vile vile alikuwa ametoka Uzinza. Basi walikaa pamoja wakashika nchi wakaitawala na walipokufa, mwana wao Solasi alirithi ufalme. Solasi alipokufa nchi iligawanywa sehemu tatu na nduguze wanawake walizirithi, ndipo zilipoitwa Nera, na Buhungukira na Usmao. Nchi hizi hazikuunganishwa tena mpaka mwaka 1927, ndipo alipoanza tena kutawala mtu mmoja.

Jina la nchi waliyotoka watu hao, yaani Uzinza, na jina la yule mwanamke Mhindi ambalo labda lilikuwa Mhinda yaonyesha dalili ya asili ya watawala hao. Tena mtawala wa Nera asema kuwa jamaa zake ni Watusi, na kwa hakika sura yake inaonyesha dalili ya kabila hilo. Dalili nyingine inayofaa kukumbuka ni ya kuwa tambiko na sadaka hufanyiwa babu zake Solasi, na mzee anayezitoa huitwa Mgabe, na jina hilo linatumika kuita watawala wa Uzinza.

Wasukuma husimulia habari za Mungu wa magharibi anayeitwa Luhinda, lakini labda hadithi zinachanganya jina la Luhinda na Mungu kwa sababu ya nguvu zake na namna alivyoanzisha utawala wa Kihinda. Kwa hakika haiwezekani kukanushwa kuwa ufalme huo wa Usukuma kwa asili yake ni wa Kihinda, tena imesemwa kuwa wenyeji wa Usmao walitoka Uzinza.

Tukizidi kwenda kuelekea upande wa mashariki tutawakuta Wabinza, na watu hawa husimulia habari za mtawala wao wa kwanza aliyeitwa Nkande. Husema kuwa alitokea upande wa magharibi ya kusini mwa Ziwa Victoria, yaani nchi iliyo upande wa mashariki ya Uzinza. Nkande aliwashinda watu wa Mwagala akatawala nchi yote iliyopakana nayo, lakini baada ya kupita miaka kadha wa kadha ufalme ulivunjika wala haukusimamishwa tena na kuwekwa chini ya mtawala mmoja mpaka mwaka 1927.

Basi kwa kadiri tujuavyo, falme hizo zilikuwa za mwisho katika upande huo wa mashariki wa magharibi zilizotawaliwa na Wahinda.

Turudi tena kwenda magharibi tuzidi kutazama dalili zilizopo za utawala wa Wahinda. Usambiro ni nchi iliyo upande wa kusini mwa Uzinza, na sehemu yake imo katika ufalme wa Uzinza wa siku hizi. Imesemwa kuwa wenyeji wa Usambiro walitoka Uzinza na watawala wao hudai kwamba walitoka Bunyoro. Kwa

****

pande zile za kusini kuna nchi ya Usumbwa na huko watawala wengine hudai kuwa ni kabila la Watusi au Warongo, yaani kabila la wahunzi waliofanana na kabila lile la wahunzi linaloitwa El Konono walio katika kabila la Wamasai.

Hatuwezi kusema kwa dhahiri kuwa watu wanaokaa upande wa kusini zaidi wana damu ya Wahamiti, lakini mtu mmoja aliyechungua sana habari hizo, asema kuwa watawala wa asili wa Unyamwezi wengi ni Wahima. Lakini habari hizo haziwezi kuhakikishwa sasa, tunaweza kubahatisha tu. Maana miaka mingi sana imepita na watawala wa Unyamwezi waliotawala katika miaka hiyo ni wengi mno, na hivi ni vigumu kuthibitisha jamaa au ukoo wa wale waliotawala kwa asili.

Kwa upande wa magharibi kuna nchi ya Uha, na watawala wa nchi hiyo kwa hakika ni Wahima, nao wanajua asili yao.
 
Mentality za kipuuzi kama hizi zinawafanya watutsi walio wachache kuona Wana haki ya Kutawala Wahutu walio wengi!
 
Sojasoma yote ila waha, wahutu,wahaya. Wasukuma ni wabantu na wana feature zote za wabantu.
Wanyamwezi na wasukumu asili yao kongo. Mnyamwe,i amemix sana na mmanyema na ndio maana Tabora ina wama yema wengi sana. Tabora ni mboka na Kongo nako kuna mboka manyema.
Ukija wafipa nao ni asili ya kongo mixer na wazambia na wamanyema. Kiasilia Wemba ni Bemba tribe lililopo kongo ambao wali migrate mpaka zambia na hatimae ufipa na mpaka tabora na wengine kigoma.
There is complexity of ad.ixturing btn these tribes
Lakini ushahidi wa kiutamaduni unajieleza moja kwa moja. Mfano ngoma ya maswezi.
Ngoma hii ukiichunguza utaiona imeeneo bonde lote la magharibi na kongo ila kongo .
Nakumbuka zamani miaka ya 80 kuna ngoma ya kutambika ilikuwa ikichezwa milima ya Vamia kwa sasa ni mjini ilihusisha kabila la walua(Luba in kongo).
Ngoma ile ilikuwa ni ya kipekee sana na imeshabihiana na ngoma ya maswezi ambayo huchezwa Tabora na ufipa.
Lakini jambo lingine ni Uchawi.
Kutoka usukumani mpaka ufipa na kigoma bonde lote linaashiria tabia inayofanana ya uchawi. Kongo nao ni vile vile. Sasa ukichunguza mambo haya hayana ufanano na UTUTSI.
Muha na mrundi na muhaya ni ndugu no daught na utamaduni nilioutaja haufani na wa wahaya,waha b
Na wahutu, mfano waha wanacheza usambere ni ngoma tofauti kabisa na hiyo niliyoitaja bila kusahau
Jambo la tatu ni Majina
Kongo hutumia majina ya wanyama kama Tembo, nk na hata ,Tabora Ufipa majina ni hayo hayo.
Nus7andike sana ila CHUO KIKUU NA WASOMI WA PHD wanajisahau sana kufanya utafiti juu ya mobility, migration and cultural and blood admixturing. Kuna haja serikali ifanye utafiti huu. Hata kupima DNA mbona wazungu wamepima huko North Africa na mafaraoh wa kale.
Historia hii ni ktk udadisi wangu na kujionea haijajikita kwenye kitabu chochote.
Historia ya Bantu people imekuwa ya kuchanganya sana.theory ni nyingi ila kupitia sisi wenyewe na babu zetu tunaweza pata mtiritiko. Nasikia South Sudan wamehifafhi kumbukumbu ya koo zao mpaka vizazi 25 nyuma na wametumia majina sisi tumedakia majina ya wazungu na warabu hivyo tumepoteza connection. Mfano mzaramo katoka wapi ? Sijui
 
Wafipa ukawaweke Kwa watusi hapana, labda Zambia na Congo, kwahiyo hao wazambia na wakongo wenyewe walitoka wapi?
 
Back
Top Bottom