Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 9,100
- 15,989
KUACHA KAZI
Baada ya kutoka Burma, siku moja, Utubora alisimama katika ofisi mbele ya tajiri wake kumwambia kuwa alitaka kuacha kazi. Kazi yake ilikuwa ukarani katika ofisi kubwa ya biashara ya karafuu. Mshahara wa Utubora ulikuwa simulizi karibu katika Unguja nzima; ilisemwa pia kuwa uliwatia wivu watu wengi sana. Alianza kazi kwa mshahara wa shilingi 100 kwa mwezi. Baada ya miaka mitano tu, alifikia mshahara wa shilingi 500 kwa mwezi kabla ya kwenda Burma. Aliporudi Unguja, alishika tena kazi yake kwa mshahara wa shilingi 1,000 kila mwezi. Hata katika ofisi za serikali hapakuwa na karani aliyekuwa anapata mshahara mkubwa kama huo.
Utubora alistahili sana ajira kubwa kama hiyo kwa sababu ya sifa alizokuwa nazo. Alikuwa mtu imara mbele ya telezi nyingi, kama vile hiana na mengine; mvumilivu mbele ya majaribu magumu, kama rushwa; hodari mbele ya mashaka mazito, mfano wa kushika amana au dhima kubwa; mwaminifu kama mchana; na msiri kama usiku. Kwa kushika majira alikuwa kama saa; na mahudhurio yake mema katika kazi hayakuwezekana kushindwa na watumishi wengine. Kila siku yeye alikuwa mtu wa kwanza kuhudhuria kazini, wakati wenziwe walipokuwa wamechelewa; na wa mwisho kuondoka kazini, wakati wengine walipotangulia kwenda zao. Kwa matendo haya ya sifa Utubora alikuwa kama pumzi ya maisha kwa tajiri wake ambaye alikuwa hana mtu mwingine bora wa kutegemea.
Laiti watumishi wote wangekuwa kama Utubora, ugumu katika mioyo ya matajiri ungalilainika. Tajiri ye yote mwingine angalipenda mtumishi kama alivyokuwa mtu huyu. Kazi nyingi sasa zimetokea katika maisha siku hizi; Lakini ni jambo la kusikitisha mno kwa kuwa mpaka sasa ulimwengu umewateua watu wachache tu kuwa kama Utubora. Watu wachache wenyewe kama yeye hukutani nao katika dunia katika kila hatua. Ukipishana naye mmoja, hukutani na mwingine ila labda baada ya muda mrefu sana.
Basi, tajiri mzee wa Utubora, ambaye moyoni alikuwa na nia ya kumfanya Utubora kuwa mshirika na mwongozi wa kazi yake siku moja, baada ya usemi wa Utubora, alituhumu kwa fadhaa kubwa kuwa yamkini karani wake alikuwa amerukwa na akili, akasema, “Lakini, Utubora, kwa hakika unatupa kazi iliyo njema sana. Sina haya ya kujipendekeza kwa njia yoyote; bali mimi na wewe twajua kwamba kazi hii ni bora ambayo huwezi kupata badala yake pahali po pote
Usemi huu ulipotoka kinywani mwa tajiri, sauti yake ilizuia kila onyesho la dalili ya kite. Maongezi haya yalihusu kazi tu kati ya bwana na mtumishi wake, na kama yalimchoma vingine, hilo lilikuwa shauri lake mwenyewe. Wakati ule palikuwa hapana uhusiano mkubwa baina ya watu wawili hawa zaidi ya ule wa bwana na mtumishi wake tu.
Utubora alijibu, “Najua hayo yote, Bwana Ahmed. Mimi sina nia ya kujaribu kutafuta kazi nyingine kama hii, bali kweli ni kuwa nimechoshwa sana na mji huu.”
Tajiri alisaili, “Kama naweza kunena bila ya kuwa fedhuli, tafadhali nambie wanuia kufanya nini baada ya kuondoka hapa?”
Utubora alicheka, lakini alijua kwamba tajiri wake alizoea maisha ya mjini utadhani kuwa alikuwa mwehu, kisha alijibu,
“Nakusudia kwenda Mrima nikakae shamba, Bwana. Nadhani haya ni matokeo ya vita yanayonizuia kuishi katika mji nikafanya kazi tena katika ofisi, kwa sababu najiona sina raha hapa Unguja. Nataka wasaa, hewa ya wazi, jua na makonde ya nyasi mbichi; nataka kusikiliza ndege wakiimba na ng’ombe wakiroroma. Yamkini, mimi mjinga bali hivyo ndivyo fikira yangu inavyoniongoza.” Baada ya kusema hivi, bubujiko la shauku yake mwenyewe lilimtahayarisha.
Ndipo tajiri alipozidi kusema, “Lazima niseme kuwa shauri lako la kuacha kazi halionyeshi faida, na kama laonyesha sioni aibu kuungama kuwa mimi siioni. Sauti za ndege na miroromo ya ng’ombe sivyo vitu vilivyoko Mrima tu. Kuna ngurumo za simba na mivumo ya chui vile vile ambayo hutisha pengine. Kama nilivyokuajibia wakati uliponiaga kwenda vitani, nafahamu kuwa wewe si mwoga, lakini kusema nijuavyo juu ya ghasia zilizoko Mrima, nadhani si vibaya. Nisingejaribu kuvuta akili yako kujua hali ya Mrima kabla hujaondoka hapa kama si kwa ajili ya manufaa yako mwenyewe. Tena sidhani kuwa Mrima hufaa kwa mtu aliyezoea maisha ya mji wa anasa na starehe kama Unguja. Ungechukua wakati wa kufikiri mambo haya kabla ya kufanya haraka ya kutimiza nia yako.”
Utubora alitoa kauli, “Naelewa kuwa shauri langu halionyeshi faida, na hiyo ndiyo haja yangu. Nia ya kupata faida sinayo. Nimechoshwa na kazi. Sitaki kuwa tajiri, wala fedha siijali. Ukiwa na fedha utajuta, ukiwa huna utajuta pia. Cha nini kitu kama hiki!
“Siwezi kubisha kuwa Unguja si mji wa anasa na starehe, bali kunradhi, Bwana, nikisema kuwa anasa na starehe hutosa watu pengine. Binafsi nimepata kutumbukia ndani yake. Nikijaliwa nataka kutoka sasa kabla kichwa changu kuzama vile vile katika gharika ya anasa na starehe.”
Utubora alijiona alikuwa fidhuli kidogo kwa tajiri wake mzee. Hakupenda kufidhulika kwake hata kidogo, lakini palikuwa hapana jingine la kusema isipokuwa kweli. Alishikwa na nguvu ya kweli.
Tajiri alieleza sasa, “Labda ni kweli kuwa hujali fedha, bali vitu vipatikanavyo kwa fedha vina manufaa pengine. Nasadiki pia kuwa anasa na starehe hupoteza mara kwa mara, bali kumbuka kuwa vitu hivi ni pepo ya dunia.”
Utubora alisema maneno machache, “Taibu, lakini haja zangu mimi si nyingi, kisha sina Makuu.”
Baada ya hayo palikuwa na kimya kidogo. Ahmed alikuwa anajaribu kugundua sababu iliyomshawishi mtumishi wake kuwa katika nia ile mpya. Aliwaza isije kuwa nia ile ilitokana na binti yake, Sheha, aliyechumbiwa na kijana huyu zamani! Alifahamu kuwa Sheha alitenda jambo la kuchukiza kwa sababu ya kuvunja ahadi aliyotoa mwenyewe baada ya kufikiri sana. Halafu alianza kusema tena, “Nadhani kuwa Sheha hahusiani na kusudi lako la kuacha kazi hii!”
Utubora alijibu kwa haraka, “La, nia yangu ya kuacha kazi hii haihusiani na Sheha hata kidogo, ingawa kama tungalioana nisingaliazimu kuacha kazi yangu, lakini upande huo wa maisha yangu imekwisha. Sheha aliponikataa, niliona kwanza kama dunia ilikoma kwenda, nikabaini dhahiri kuwa hapana mwanamke mwingine atayekuja katika maisha yangu, au kuwa kwangu hodari kama alivyokuwa yeye katika moyo wangu; lakini fadhaa ya vita ilinisaidia kupona: ilinifundisha kwamba yalikuwako mambo mengine ya kuangalia. Yeye alichagua mtu mwingine, basi mwisho wetu ulikuwa huo.”
Baba yake alitoa kauli kwa makini. “Nadhani kwamba Sheha alishawishika na kitu kingine kuliko yalivyokuwa mahaba yake,”
Kwa kuwa Utubora alikuwa amekwishajiingiza katika mazungumzo yale na bwana wake, moyo wake ulikuwa hauna hofu tena, kama ilivyo desturi ya mdogo kwa mkubwa wake akasema kwa kicheko, “Mimi sikutambua kama ni hivyo ulivyosema sasa.”
Ahmed alimkazia macho akanena, “Wadhani mama yako angalikubali kusudi lako kama angalikuwa mzima?”
Macho ya Utubora yalilengalenga machozi, yalifanya hivyo sikuzote kila alipofikiri habari za mama yake aliyempenda sana. Alikuwa na imani kubwa moyoni kuwa mauti yaliweza kuondoa wapenzi wa mtu machoni pake, lakini hayakuweza kuwafuta katika moyo wake. Kisha alijibu,
“Naam, kwa hakika, mama angalikubali; naona kuwa yu radhi huko aliko, hasa katika hali yangu ya sasa. Kwa kweli, laiti angalikuwa hai, nisingalifikiri habari ya kuacha kazi yangu, ingalinipasa kumsaidia na kumkimu; lakini kwa kuwa nimebaki peke yangu sasa, naweza kutenda nipendavyo bila ya lazima ya kufikiri habari za mtu ye yote mwingine.”
Ahmed ingawa aliguna, alitabasamu kidogo akasema, “Jambo unalokusudia naliona kama choyo, lakini hata hivyo, nafikiri kuwa ni kweli. Unajitawala mwenyewe, bali juu ya hayo, mimi siwezi kujizuia kufikiri kuwa utaishi mpaka siku ya kulijutia tendo lako la sasa, kama umekusudia hasa kutimiza nia uliyo nayo.”
Utubora alitikisa kichwa chake; na baadaye kidogo tajiri wake aliendelea kusema, “Tazama, kijana, mimi sitafikiri maneno usemayo leo asubuhi kuwa ndiyo ya mwisho. Nimekutana na vijana wengi waliotoka vitani wenye mawazo makubwa na ya ajabu. Sisemi kwamba vita vimewaharibu, lakini nadhani kuwa akili zao si timamu.”
Utubora alisema polepole, “Hivyo sivyo, Bwana, ila tulijifunza mambo mengi sana huko ambayo habari zake hatukuzifikiri zamani; miongoni mwa mambo hayo tulijifunza thamani za vitu vilivyo vya lazima kabisa katika maisha.”
Kwa uvumilivu mwingi Ahmed alitabasamu akanena, “Sifu jambo ulipendalo kwa sifa upendayo, lakini matokeo yake huwa mamoja sikuzote. Jambo niazimulo kutenda ni hili. Chukua mwaka mmoja wa mapumziko, katafute hayo mambo yaliyo ya lazima, na kwa muda huo wa kupumzika, nitakuwekea wazi nafasi ya kazi yako. Nasema shauri hili kwa sababu ya manufaa yangu mimi mwenyewe na yako wewe; Sijasahau pia urafiki wangu wa zamani na marehemu baba yako. Mimi na baba yako tulikuwa vijana pamoja. Sitaki uondoke katika maisha yangu. Maungano ya nikahi niliyotazamia zamani baina ya binti yangu na wewe hayakuwa. Sheha hakushinda jaribu lake kama anavyostahili mwanamke aliye bora, lakini mimi nilitazamia kustaafu na kukuacha wewe kazini kama mshiriki wangu sikuzote.”
Utubora aliingiwa na huruma kwa maneno haya akasema, “Ahsante sana, Bwana, nami sipendi kuonekana kama kwamba sioni wema wako, lakini kwa kweli sitarudi. Nina hakika kuwa sitarudi tena.” Ahmed alitamka, “Kama ni hivyo, vema! Kwa kila hali nitakupa ruhusa. Nadhani huna kusudi la kuondoka leo au kesho?”
Utubora alijibu upesi, “La, sivyo kabisa, lakini nitakuwa tayari kwenda zangu wakati wowote ambao utaweza kunipa ruhusa, Bwana.”
Ahmed aliposimama wima ili atoke afisi, saa saba ilikuwa inagonga Bet-el-Ajaibu. Motokaa yake ilikuwa inamngoja nje tayari, lakini mazungumzo yake na Utubora yalivunja kawaida yake ya sikuzote. Aliona mambo yamemkulia, akasema kwa huzuni,
“Nasikitika sana. Nadhani kuwa hutaniona kuwa mkavu wa macho nikisema kwamba mshahara wako nitauzidisha, lakini mwisho wa mwaka tutafikiri jambo hili.”
Alishikana mikono na Utubora wakaagana kwa furaha. Utubora na tajiri wake walikuwa marafiki sikuzote, na wakati Utubora alipomposa Sheha, urafiki halisi kati ya Ahmed na Utubora ulitokea.