Hii ndio hotuba ambayo serikali na Bunge hawakutaka kuisikia. Nimekikumbuka kitabu cha kivuli kinaishi. Nyeupe kuwa nyeusi
------------------------------------------- ----------------------
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI, MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Aprili, 2016.
______________________
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwa dhati namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema , nawashukuru pia Mke wangu Neema, Watoto wangu Allbless, Brilliant, Terrence na Precious Mawazo, pamoja na Wazazi wangu kwani wamekuwa msaada mkubwa sana kwangu katika shughuli zangu zote kwa maombi na sala . Kwani kufanya kazi ya Siasa za Mabadiliko Tanzania ni kazi ngumu na iliyojaa mateso, vitisho na hata kifo, lakini kwa ajili ya siku zao njema za baadae, ninapaswa kuendelea na kuvumilia katika kazi hii na wajibu huu muhimu ili kutafuta mwanga mpya wa Taifa letu katika siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, Namshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mhe. Freeman Aikael Mbowe kwa busara, ujasiri na maamuzi yake katika kuamua mambo yenye mwelekeo chanya katika Chama chetu na Nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Nawapongeza pia wale wote waliojiunga na Chama chetu na Ushirika wetu wa Ukawa katika mwaka ule wa Uchaguzi hasa katika hatua za mwisho, nampongeza Mhe. Edward Ngoyai Lowassa na mke wake Mama Regina Lowassa ambaye ni mfano wa kuigwa, Mhe. Fredrick Tulaway Sumaye ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati kuu wa CHADEMA na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na wengine wengi kwa ujasiri na maamuzi mazito waliyofikia.
Mheshimiwa Spika, nina washukuru wananchi wa jimbo la Arusha Mjini kwa imani yao kubwa kwa Chama chetu na kwangu kwa kuweza kutupa madiwani 24 kati ya 25 na kufanikisha kuongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha.
2.0 HALI YA USALAMA NA AMANI YA NCHI YETU
2.1 MAADILI YA FAMILIA
Mheshimiwa Spika, Taifa lolote Duniani msingi wake ni familia , hivyo njia sahihi ya Taifa kuwa na usalama wa kweli katika Jamii ni muhimu Serikali ikajua kuwa Jamii ni Familia, kuongelea hali ya usalama na amani ya Nchi yetu bila kuongelea maadili ya familia zetu ni kupotosha fikra zetu.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba familia yenye maadili, wajibu na inayomcha Mungu ni jamii bora itakayozalisha Raia wema wenye wajibu na tija kwa Taifa, hatuwezi kuwa na Nchi yenye nidhamu na ustawi pasipo kuwa na familia zenye wajibu katika malezi .
Mheshimiwa Spika, Wazazi wengi leo tukiwemo Waheshimiwa Wabunge na Jamii ya kada mbali mbali tunafikiri kuwa tumekosa nafasi ya kukaa na familia zetu, na hivyo tumeamua ku- out sourcemalezi ya Watoto wetu na familia zetu, hivyo watoto wengi wanao kuwa katika karne hii, ni watoto wanaolelewa ama na wasaidizi wa shughuli zetu majumbani, mitandao ya jamii, Shule, na makundi mengine tusiyoyajua, ambayo hayajui mila, utamaduni, desturi na maadili ya Jamii zetu.
Mheshimiwa Spika, hii ni hatari kwa usalama wa Taifa, unapokuwa na Taifa lenye familia ambazo hazina malezi mazuri ni ukweli usiopingika kuwa, ni lazima utegemee kizazi kisichokuwa na mwelekeo wa kimaadili. Hivyo ni muhimu Wazazi na Taifa likajua wajibu wa usalama na amani ya Nchi unaanzia kwenye malezi bora katika ngazi ya familia .
3.0 AMANI NI TUNDA LA HAKI.
Mheshimiwa Spika, hali ya Amani katika Nchi yetu iko katika mashaka makubwa na kwa bahati mbaya Serikali inaufahamu ukweli ila kwa sababu inazozijua yenyewe imeamua kupuuza ukweli huo wa kushindwa kutofautisha kati ya amani na utulivu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika , Taifa hili lina utulivu unaosabishwa na hofu inayojengwa kwa mabavu na silaha na sio amani, kuna mateso makubwa wanayoyapata wananchi wa Taifa hili kila siku, umasikini, njaa, ukandamizwaji, ubaguzi, uonevu, udhalilishwaji na mateso ya jinsi mbali mbali kutokana na kukosa uongozi unaojali maisha ya Watu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni baada ya uchambuzi na tathimini ya “Hali ya Usalama na Amani ya Nchi yetu” kabla wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015, tumebaini kuwa nadharia na mwenendo wa demokrasia ya vyama vingi hapa nchini iliwekwa kando, na badala yake sura nzima ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015, uligeuka kuwa “Military Operation”yaani “Operesheni ya Kijeshi” kwa kisingizio cha kulinda amani.
Mheshimiwa Spika, tarehe 25 Oktoba 2015 siku ambayo wananchi walipiga kura, Katika Jengo la Mlimani City, CCM na timu yao ya Kampeni ya Rais John Pombe Magufuli walifanya zoezi la kuhesabu kura za mawakala wao kutoka vituo mbalimbali nchini yaani “Parallel Voter Tabulation” bila kubughudhiwa na Jeshi la Polisi, wakati huo huo UKAWA wakifanya zoezi kama hilo la “Parallel Voter Tabulation” katika vituo vitatu vya ICT ndani ya Jiji la Dar es Salaam, na vituo vyote hivyo kuvamiwa na Jeshi la Polisi ambalo lilizuia zoezi hilo kufanyika, kuvunja na kuharibu baadhi ya vifaa vilivyotumika kama vile laptop, kuwanyang’anya simu na laptops vijana zaidi ya 160 waliokuwa wanajitolea kufanya zoezi hilo, kuwasweka rumande kwa muda wa siku tatu mfululizo bila kuwafungulia mashitaka, kuwatishia kuwa wanatuhumiwa kwa makosa ya kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu (human trafficking) na kuwafungulia mashitaka ambayo hayana msingi.
Mheshimiwa Spika, mnyonge anayelia moyoni kwa huzuni ya kuonewa ni hatari kwa usalama wa Nchi na Dunia , vikundi vingi vya uhalifu Duniani kwa asilimia kubwa vimesababishwa na utawala wa kibabe, uonevu na ukandamizwaji usiovumilika na huko ndiko tunakoelekea kama Taifa.
Mheshimiwa Spika , matendo mabaya haya yaliofanyika wakati wa uchaguzi mkuu uliopita Zanzibar na Tanzania bara ni ishara ya watawala kuelekeza Nchi yetu katika mapigano ya sisi kwa sisi katika siku za usoni .
Mheshimiwa Spika, unapokuwa na Jamii inayoamini kuwa mfumo wa demokrasia hauwezi kuwapa wananchi viongozi wanaowataka , maana yake ni dhahiri kwamba unaanza kuifundisha jamii hiyo kufikiri njia mbadala ya mabadilko katika Nchi .
Mheshimiwa Spika , kuwa na Tume ya Uchaguzi inayotiliwa mashaka na Jamii ni hatari kwa usalama wa Nchi yetu. Ni muhimu sasa kama Taifa kutafakari uwepo wa katiba ya wananchi na Tume Huru ya Uchaguzi itakayorudisha imani ya Wananchi katika Uchaguzi wa Kidemokrasia.
Mheshimiwa Spika , Mungu adhihakiwi apandacho Mtu ndicho avunacho, utulivu mnaouona Zanzibar na kwingine kokote kule kuliko na ukandamizaji ni nafsi zinazojadili mwelekeo mpya wa maisha yao katika utawala wa Nchi yao.
Mheshimiwa Spika , Zanzibar mmeshinda uchaguzi kwa hila na sio kwa haki, wekeni kumbu kumbu maneno ya Kambi Rasmi ya Upinzani leo kuwa, ipo siku Zanzibar itakuwa ni sehemu ngumu ya kuishi Binadamu kama hamtachukua hatua sasa ya kurekebisha mlichokifanya Zanzibar na Tanzania Bara katika uchaguzi uliopita .
Mheshimiwa Spika , kwani tunajiuliza maswali mengi , je tutarudi tena kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 kwa njia ya demokrasia ? au tutafakari njia nyingine mbadala, kwani demokrasia katika Taifa hili imethibitisha kuwa tunaweza kushinda uchaguzi lakini tukaporwa matokeo na tusitangazwe kuwa washindi.
4.0 MAUAJI YA VIONGOZI WA KISIASA.
Mheshimiwa Spika , Viongozi wa kisiasa hasa wale wa Upinzani wamekuwa wakiishi kwa kubaguliwa na kwa mateso makubwa sana hata wengine kuuwawa kwa sababu ya kazi na wajibu wao katika siasa na jamii.
Mheshimiwa Spika , nikianza kueleza wale wote waliopatwa na madhara ya vipigo , kusingiziwa kesi , na wengine kuuwawa , ninaamini kwamba hotuba hii haitoshi isipokuwa labda tuandike vitabu.
Mheshimiwa Spika ,Rafiki na ndugu yetu mpendwa Alphonce Chemu Mawazo, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita aliuawa kinyama kule Katoro- Busanda - Geita , mchana , hadharani , tena karibu na kituo cha Polisi.
Mheshimiwa Spika, sisi tulilia sana na kuhudhunika sana hata mpaka leo, na tulipohitaji kumzika kwa heshima anayositahili kama rafiki na Kiongozi wetu hatukuruhusiwa na Polisi , tulipigwa sana mabomu na wengine kama Mwenyekiti wetu wa Vijana Taifa Patrobas Katambi walipewa kesi ya kushambulia jambo ambalo ni la kutunga na uzushi.
Mheshimiwa Spika , Mwili wa Marehemu Alphonce Mawazo ulizuiwa kuagwa kwa ubabe na Jeshi la Polisi bila sababu za msingi mpaka Mahakama ilipotoa haki ya mwili kuagwa kule jijini kwao Busanda Geita.
Mheshimiwa Spika, Marehemu Mawazo ameacha Binti yake mzuri na mwenye akili nyingi Precious akiwa darasa la nne, Baba yake ameuwawa si kwa sababu alikuwa mwizi , bali aliamini katika siasa tofauti na demokrasia kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, wakati mioyo yetu ikilia ndani kwa huzuni, kwa dhuluma, uonevu, ukandamizwaji, vipigo hata vifo vya marafiki zetu na ndugu zetu katika kazi zetu za siasa tunazofanya, nyie mnaona mambo haya ni ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, hii ni hatari kwa usalama wa Taifa, kwani subira na uvumilivu vitakapoishiwa nguvu, kuna dalili ya mauaji ya ulipizaji visasi kuanza na itakapofika hapo usalama na amani ya Taifa letu utakuwa mashakani sana.
Mheshimiwa Spika, Kama Rais Magufuli anaweza kuanzisha Mahakama ya Mafisadi ambao wapo hai, Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa majawabu kwa nini mpaka dakika hii bado tume ya kimahakama ya kuchunguza vifo tata (Judicial Commission of Inquiry) haijawahi kuundwa, ili kutoa haki kwa Watanzania. Japo kuwa ilikuwa ni ahadi ya Waziri Mkuu katika katika Serikali ya awamu ya nne.
5.0 MIKATABA TATA YA JESHI LA POLISI.
5.1 Mkataba tata wa Lugumi na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali , ilihoji utekelezaji wa mkataba wenye utata wa vifaa vya Mfumo wa Alama za Vidole (AFIS) ulioingiwa kati ya Jeshi la Polisi Tanzania na Kampuni ya Lugumi Enterprises.
Mheshimiwa Spika, kumetokea majibishano na malumbano mengi kwenye vyombo vya habari na miongoni mwa wabunge wa Bunge lako tukufu, hasa pale walipoanza kuhoji utekelezaji wa mkataba huo hasa kuhoji juu endapo vifaa hivyo vinafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia majibishano na malumbano yaliyojaa utata ambao lazima upatiwe majibu yasiyo na shaka yoyote, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kutoa majibu ya moja kwa moja bila kupepesa macho. Tunataka Maswali yafuatayo yajibiwe hapa bungeni;
Mheshimiwa Spika,
1) Kwa kuwa mikataba ya serikali kwa mujibu wa sheria lazima ufuate sheria za manunuzi na kuthibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Je, Utaratibu huu ulifuatwa? 2) Je Mkataba huu wa LUGUMI ENTERPRISES na JESHI LA POLISI umetekelezwa ama haukutelezwa, na kama ulitekelezwa ni kwa kiwango gani, na ikiwa kulikua na tatizo la utekelezaji, Je, Jeshi la Polisi lilichukua hatua zipi?3) Je, ni kampuni ngapi ambazo zinahusika na hatua za utekelezaji wa Mkataba kati ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi, kwa kuwa kampuni ya INFOSYS ambayo mmoja wa wamiliki wake ni Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga inatajwa kufunga vifaa hivyo (AFIS). 4) Ni kwanini C.A.G katika ukaguzi wake hakuhoji kuhusu uhalali na ulinganishi wa thamani ya pesa ya manunuzi na faida ya vifaa hivyo?5) Kampuni ya INFOSYS (inayomilikiwa na Mhe. Kitwanga) imedai kulipwa na Jeshi la Polisi, takribani Dolla za Marekani 74,000, Je fedha hizi Kampuni ya Mhe. Kitwanga ililipwa kwa kazi ipi iliyofanya na Jeshi la Polisi? 6) Ni kwanini mpaka sasa , Rais Magufili hajachukua hatua dhidi Said Lugumi, na aliyekuwa IGP Said Mwema / Emmanuel Nchimbi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na kuwasimamisha kazi wale wote ambao bado wako kazini juu ya mkataba tata wa Lugumi ?7) Tunamtaka Rais , kutengua mara moja uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe na kumrudisha nchini mara moja , kwani alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na ni imani ya Kambi rasmi kuwa alijua mambo yote yanayoendelea ya mkataba wa Lugumi
Mheshimiwa Spika , Ni imani ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa Mhe.Waziri Charles Kitwanga, anazo taarifa za Mkataba huu na utekelezaji wake aidha kutoka kwenye Kampuni yake ambaye yeye ni Share holder ( Mbia ) ambayo ilifunga vifaa hivi au anazo taarifa ya utekelezaji wa Mkataba huu kutoka Jeshi la Polisi ambalo liko chini yake kwa kiwango chote kuhusu mambo yote ya Mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) , alinukuliwa na vyombo vya habari pale alipoulizwa kuhusu sakata la Lugumi na Mikataba yake na Jeshi la Polisi kutotekelezwa, alijibu majibu mafupi Katika gazeti la Raia Mwema la tarehe 27/04/2016 namnukuu “siyo kweli, watu wana ugomvi wao kibiashara, lakini nakueleza wazi kwamba, tembelea vituo vyote tulivyokubaliana, utakuta mashine zipo. Inawezekana zingine hazifanyi kazi kwa sababu ya kukosekana kwa internet” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, kulingana na maswali ambayo tumeuliza hapo juu na uchambuzi wetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika,
1. Kwa vile Waziri wa Mambo ya Ndani anahusika kwa karibu katika Mkataba huu kupitia Kampuni yake ya INFOSYS na vile vile Jeshi la Polisi liko chini yake , je ? haoni kuwa ni busara kwa yeye kujiuzulu ili kutoa nafasi ya Uchunguzi kuepusha mgongano wa maslahi ndani ya Jeshi la Polisi na kwenye Kampuni ambayo yeye ni mmoja wa wamiliki ?
Mheshimiwa Spika,
2. kwa vile inaonekana kupitia vyombo vya habari na kauli za viongozi mbali mbali kuwa upo uwezekano wa Polisi kuwa wametapeliwa na vifaa hivyo havijafungwa, Kambi ya Upinzani Bungeni inautaka uongozi wote wa juu wa Jeshi la Polisi kujiuzulu mara moja, kwani kama wao wameshindwa kujua ukweli wa vifaa vilivyofungwa kwenye vituo vyao vya Polisi ama vipo au havipo, watawezaje kuchunga na kulinda mali na usalama wa raia wengine?
Mheshimiwa Spika,
3. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka majibu yote yanayohusu Mkataba wa Lugumi na Jeshi la Polisi kuhusu utekelezaji wake uwekwe wazi hapa bungeni na wizara husika.
5.2 Sakata la Kuuzwa kwa ardhi ya Polisi Oysterbay
Mheshimiwa Spika, Sakata la Kuuzwa kwa ardhi ya Polisi Oysterbay limeleta mashaka makubwa ndani ya jamii na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi, pamoja na Rais Magufuli kutilia mashaka jambo hili.
Mheshimiwa Spika, Kwa vile kuna ukakasi na mashaka ya rushwa, tunaliomba bunge liazimie na kuitaka Serikali kuleta mara moja mkataba huu na mingine yote yenye sura kama hii ndani ya Bunge lako tukufu, ili ipitiwe na kufanyiwa tathimini endapo mikataba hiyo ilifuata utaratibu na ina tija kwa Taifa na hii iwe ni kwa mikataba yote iliyofanyika wakati wa Serikali ya awamu ya nne ya Mh Jakaya Kikwete , pamoja na ule wa ununuzi wa boti
( Mv Dar es salaam ) uliofanywa wakati Rais wa sasa Mh Dr Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi.
Mheshimiwa Spika samba samba na hilo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka pia Serikali kuleta mikataba ya uuzwaji wa Nyumba za Serikali kazi ambayo aliisimamia Rais Magufuli mwenyewe wakati huo .
Mheshimiwa Spika , kwa vile Rais wa sasa alihusika kuuza nyumba za Serikali ni imani yetu kuwa Kambi rasmi ya Upinzani itapata ushirikiano wa kutosha juu ya utata wa mikataba hii tete ya uuzaji wa nyumba hizi.
6.0 RUSHWA, SURA YA SERIKALI NA BUNGE TISHIO LA HALI YA USALAMA.
6.1 Rushwa na Bunge kutumika kuwalinda wahalifu nchini
Mheshimiwa Spika , Mh Andrew Chenge (MB) ametuhumiwa na imethibitika hapa Bungeni na katika taasisi za Uchunguzi za Kimataifa (SFO) kuwa alihusika kwa karibu na kwa ufanisi katika sakata la kashfa ya ununuzi wa rada ya Taifa.
Mheshimiwa Spika , Mwandishi Andrew Feinstein , Colonel .U.S. Army (retired) katika Kitabu chake “ THE SHADOW WORLD - Inside the Global Arms Trade, katika ukurasa wa 188-196, amefanya uchambuzi wa kina jinsi Andrew Chenge alivyofanikiwa kukwapua fedha za Wananchi kiasi cha pesa za Kimarekani dolari 1.2 milioni kupitia Kampuni yake ya Franton Investment Ltd Jersey na Kampuni hii ya Andrew Chenge ikampa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dr. Idrissa Rashid pesa za Kimarekani dolari $600,000 kupitia Kampuni ya Gavana huyu inayojulikana kwa jina la Langley Investment Ltd.
Mheshimiwa Spika, Lakini kwenye utawala huu wa utumbuaji majipu, Andrew Chenge ni Mkiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkiti wa Kamati ya sheria ndogo, jambo hili lina sura ya dharau na fedhea kwa Bunge lako tukufu na kwa jamii.
Mheshimiwa Spika, Wako wengi wenye sura hizi za Mh Chenge na wengine ni Mawaziri ambao wamekuwa na kashfa mbali mbali kwenye Serikali iliyopita lakini wameonekana kwenye madaraka tena katika Serikali hii ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais aneyeamini katika utumbuaji majipu , wakati kuna majipu mengine asiyoweza kuyatumbua ndani ya baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Spika , Taifa linapokuwa na huzuni juu ya utawala unaopuuza na kudharau Wananchi , kwa vyovyote vile hali ya amani na usalama inakuwa mashakani na kuwatia moyo watumishi wengine wa Umma katika masuala yanayohusu ufisadi, rushwa na ubadhirifu kwamba sio mambo mabaya. Ndio maana imekuwa ni vigumu kukemea rushwa katika ngazi mbalimbali za utawala wa nchi hii ikiwemo Jeshi la Polisi.
6.2 Kuingiliwa kwa Uhuru wa Bunge na Mhimili wa Dola
Mheshimiwa Spika , tishio lingine la hali ya usalama Nchini ni Serikali kuingilia Uhuru wa Bunge , ni ajabu kubwa kwamba chombo kinachopanga matumizi ya fedha za Serikali ni Bunge , lakini kwa wakati huu tumeona Serikali ikiondoa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kwa kisingizio cha kubana matumizi , kazi ambayo hata hivyo kama ingekuwa ni hoja basi jambo hilo lingefanywa na Bunge na sio Serikali.
Mheshimiwa Spika, Wananchi kupata habari na kujua wanachojadili wabunge wao ni hitaji la lazima la Kikatiba na sio hisani ya Serikali, malumbano yetu dhidi ya hoja mbali mbali ndani ya Bunge yalikuwa ni muhimu kwa ustawi wa usalama wa Nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Wananchi , walipotuona kupitia vyombo vya habari mbali mbali , tukilumbana juu ya maisha na maendeleo yao , jambo hili lilikuwa linasidia kupunguza tension na uchungu kwa jamii kwani walikuwa wanashuhudia tukipigana na kulumbana juu ya ustawi wa maisha yao , walipata matumaini waliposikia majibu ya Serikali hata kama yalikuwa ni uongo.
Mheshimiwa Spika , Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa na jinsi Bunge letu linavyoendelea kukosa nguvu na kuingiliwa na mihimili mingine ya dola kwa kuelekezwa ni kipi cha kufanywa na kipi si cha kufanywa. Ni wazi sasa bila chenga kuwa Bunge hili limeingiliwa na dola na sasa ni Bunge kibogoyo jambo linalohatarisha usalama na amani ya nchi, kwa kuwa Dola sasa inaweza kufanya chochote na isionekane kukemewa na Bunge ambalo kazi yake ni kuisimamia Serikali, badala yake sasa hivi Serikali ndio inalisimamia Bunge.
Mheshimiwa Spika , kisingizio cha gharama kubwa za kurusha matangazo ni uongo mkubwa ambao hata shetani anaushangaa, kwani hata vyombo vingine vya habari vilivyokuwa vinarusha matangazo ya “live” kwa gharama zao navyo vimezuiwa sio na Serikali bali na uongozi wa Bunge uliodhibitiwa na Serikali ya Dkt. Magufuli.
6.3 Tabia ya Rais Magufuli na Usalama wa Nchi.
Mheshimiwa Spika, wakati Taifa letu linapita kwenye changamoto nyingi Kama vile ukosefu wa sukari, umeme, umasikini, mizigo kupungua bandarini , madini ya Tanzanite kuanguka bei na ubadhirifu uliokithiri katika mfumo wa utawala. Rais mwenyewe ameonekana kufuatilia na kufanyia kazi habari za kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa tabia hii ya Rais Magufuli, kama Taifa tunahitaji maombi haraka, kwani Rais ataumiza watu wengi sana kwa kufuatilia maneno ya mitaani kwa njia mbali mbali , kwani kwa madaraka aliyonayo Rais bila shaka ataumiza watu wengi. Mfano, Sakata la Mke wa Waziri Mahiga na Trafiki barabarani. Ni jambo dogo sana na la karaha kuona linazingatiwa na Rais .
Mheshimiwa Spika, haikuwa busara Rais kukemea familia ya Waziri wake mbele ya vyombo vya habari na kuagiza askari huyu kupandishwa cheo bila kujua historia ya utumishi wake .
Mheshimiwa Spika , kwa nini mambo haya ni muhimu kuyasema na kwa nini ni hatarishi kwa usalama wa Nchi, tulipoonza vikao vya Kamati za Bunge, vyombo vya habari vilimnukuu Rais akielezea mpango wake wa kuanza kurekodi Mawaziri wake wanaolalamika juu ya staili yake ya uongozi. Kwa hiyo leo ukienda kwenye ofisi za Mawaziri, unaona, hofu, mashaka, kutokujiamini, mambo yatakayo punguza ufanisi, ubunifu na uhuru katika utendaji wao, jambo linalopeleka Taifa kuzorota katika Nyanja zote kwa utumishi wa umma jambo ambalo ni hatari kwa Taifa.
7.0 UGOMVI KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI
Mheshimiwa Spika, Ugomvi kati ya Wakulima na Wafugaji ni tatizo kubwa na ambalo lisipotatuliwa kwa makini na haraka , Nchi yetu itaendelea kushuhudia mauaji kwa raia wake .
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inashauri Serikali kutenga mara moja na kupima maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji , tatizo hili haliwezi kutatuliwa kwa bunduki na mabomu ya machozi isipokuwa mipango maalumu ya upimaji ardhi na ushauri wa kitalamu juu ya ufugaji wa kisasa na ukulima wa kisasa unaweza kuwa njia ya kupunguza tatizo na kuliondoa kabisa.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani inaishauri Serikali kuanzisha mfumo wa mauzo ya wanyama kwa kuzingatia vipimo vya uzito na kuuza kwa mizani yaani kilogramu na si kuuza kwa kutazama mifugo kwa macho na kupanga bei. Kwa kufanya hivyo wafugaji watajali zaidi na kuona tija ya kuwa na mifugo michache na kuwanenepesha kuliko kuwa na mifugo mingi isiyo na afya.
8.0 HALI YA UHALIFU NCHINI
Mheshimiwa Spika, Hali ya Uhalifu nchini bado ni mbaya na kasi ya kupunguza uhalifu hairidhishi, taarifa za Takwimu za Hali ya Uhalifu Januari-Juni, 2015 zilizotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi zimeonesha kuwa kuna ongezeko la asilimia 9.8 ya makosa ya jinai hapa nchini. Taarifa hiyo imeonesha kuwa matukio madogo ya makosa ya usalama barabarani yakiongezeka kwa asilimia 16.4 kutoka mwezi Januari – Juni, 2014 mpaka kufikia Januari – Juni, 2015.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa mara zote ndani ya muda wote wa Bunge la 10, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilikuwa ikiishauri Serikali juu ya hatua mbalimbali za kuchukua dhidi ya matukio ya ajali za barabarani ambazo zinagharimu maisha ya wananchi wa Taifa hili ambao ni nguvu kazi inayopotea, na kuwaacha vijana wengi wakipoteza wazazi wao na kubaki mayatima. Taarifa za Takwimu za Hali ya Uhalifu Januari-Juni, 2015 zimebainisha kuwa “Jumla ya watu 1,849 walifariki kutokana na ajali za barabarani ikilinganishwa na watu 1,777 waliofariki Januari hadi Juni, 2014. Hili ni ongezeko wa watu 72 sawa na asilimia 4.1”.
Mheshimiwa Spika, Ubunifu pekee wa Serikali katika Jeshi la Polisi ilikuwa na kuwapatia mashine za EFD ili wasiendelee kufanya kazi ya kuhakikisha usalama barabarani na badala yake “kudandia” kazi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kukusanya mapato. Ni aibu kubwa sana kwa Jeshi letu la polisi kujisifia kwa ukusanyaji wa mapato kutokana na makosa ya barabarani badala ya kutoa taarifa za namna gani Jeshi hilo limepunguza uhalifu wa makosa ya barabarani. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro alikaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa “Kikosi cha usalama barabarani kanda ya Dar es Salaam kimekusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kama faini za makosa ya barabarani kuanzia Februari 1 hadi 22, mwaka huu”
Mheshimiwa Spika, Itoshe tu kusema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijaridhishwa na mbinu na weledi hafifu unaotumiwa na Serikali ndani ya Jeshi la Polisi kupambana na uhalifu hapa nchini. Taarifa ya Hali ya UhalifuJanuari-Decemba, 2014 imeonesha ongezeko kubwa sana, (substantial increase) ya uhalifu nchini kwa asilimia 32.5, kutoka makosa milioni 1.2 mpaka makosa milioni 1.6.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuzingatia ushauri wote uliotolewa na Kambi kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe maelezo ya kina juu ya mpango mkakati wa kupunguza kiwango cha uhalifu hapa nchini na kueleza ni kwa kiwango gani wanafanya kazi ya Usalama wa Raia na Mali zao.
9.0 UKOMESHAJI BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA NCHINI
Mheshimiwa Spika, Ifahamike kuwa kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita Kambi Ramsi ya Upinzani Bungeni, imekuwa ikiishauri Serikali juu ya hatua za kuchukua katika kukomesha matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika , ushauri wetu juu ya jambo hili nikuitaka Serikali ikatafute ushauri wetu wote wa huko nyuma katika hansard na kuuzingatia mara moja , kwa ajili ya kuokoa Taifa letu.
10.0 HALI ZA MAHABUSU NA WAFUNGWA MAGEREZANI
10.1 Kuondoa adhabu ya Kifo iliyo kinyume na Katiba ya Tanzania
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2015, inakaridiwa kuwa watu 472 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa, kati ya hao wanaume ni 452 na wanawake 20, ambapo wafungwa 228 wanasubiria kunyongwa hadi wafe kwa mujibu wa sheria, na wafungwa 244 wanasubiria kusikilizwa kwa rufaa zao, hii ni kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu (LHRC, 2015).
Mheshimiwa Spika, adhabu ya kifo inakiuka misingi ya Kikatiba, ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa “Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika Jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa katiba hii” Lakini pia hajaanza kutumiza masharti ya katiba yetu kwa kuwa bado hukumu za vifo zinatolewa. Hata hivyo bado Serikali ya Tanzania haijatia saini makubaliano ya sehemu ya pili ya mkataba wa International Convention on Civil and Political Rights wa mwaka 1966, ambapo Second Optional Protocol to the International Convention on Civil and Political Rights, ya mwaka 1989 ambayo inataka nchi wanachama kukomesha adhabu ya kifo.
Mheshimiwa Spika, inaishauri Serikali kusaini na kuridhia mkataba wa Second Optional Protocol of the International Covenant on Civil and Political Rights, ili kuilinda katiba yetu na kutimiza matakwa ya kikatiba ya kulinda uhai wa kila Mtanzania.
10.2 MSONGAMANO WA MAHABUSU NA WAFUNGWA MAGEREZANI.
Mheshimiwa Spika, Kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kuchukua hatua ya kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu Magerezaji sambamba na kuboresha lishe na huduma za afya kwa Wafungwa na Mahabusu.
Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha 2015/2016, aliyekuwa Waziri wa mambo ya Ndani wakati huo, Mhe. Mathias Chikawe, alisema kuwa uwezo wa magereza yetu ni kubeba wafungwa 27,653, wakati mpaka kufikia mwaka 2015 mwezi machi magereza ilikuwa na wafungwa 33,027.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijaridhishwa na hatua ambazo Serikali ilizichukua kwa mwaka wa fedha uliopita katika harakati za kupunguza msongamano wa magereza. Hatua za Parole, Msamaha wa Rais na Kifungo cha nje bado hazitoshi kwa kuwa hatua hizo zinalenga kupunguza msongamano bila kuangalia hali ya mazingira ya mahabusu na wafungwa wanaobakia ndani ya magereza. Tuliendelea kuisisitiza Serikali kuwa huduma za afya, uchakavu wa miundombinu ya vyoo na mabafu, na ufinyu wa vyumba vya kulala, ukosefu wa matandiko na magodoro pamoja na lishe kwa mahabusu na wafungwa zimeendelea kuwa duni.
Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha 2015/2016, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliishauri Serikali kuwa ili kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani iandae utaratibu kwa Jeshi la Polisi kuwa kabla halijawakamata watu na kuwaweka mahabusu basi uchunguzi wa kina ufanyike, tofauti na sasa ambapo mtu anayehisiwa tu kuwa ni mhalifu anaweza kuwekwa mahabusu na kukaa huko hadi miaka zaidi ya mitano na baadae kuambiwa kuwa hana hatia, huu ni uvunjaji wa haki za Binadamu.
Mheshimiwa Spika , hata hivyo sababu nyingine mojawapo inayofanya mahabusu kujaa katika magereza zetu , zinachangiwa na matumizi mabaya ya Sheria ya mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 91 ambacho kinampa mamlaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kuondoa Shauri la jinai Mahakamani lakini kuondolewa kwa shauri hilo hakuzuii mamlaka kumshtaki tena kwa kosa lile lile mtuhumiwa.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi wamekuwa wakitumia vibaya masharti ya kifungu hiki ambapo mara baada ya mtuhumiwa/watuhumiwa kuachiwa wamekuwa wakikamatwa tena na Jeshi la Polisi mara nyingi ikiwa katika maeneo ya Mahakama.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani Bungeni inashauri mbali na uwepo wa parole, na vifungo vya nje ni vema magereza zikaimarisha na kuwa kitengo maalumu cha wafungwa watakao fanya kazi za huduma za jamii na Kitengo cha mazingira na upandaji miti hasa kwa kifungo chini ya mwaka mmoja au na zaidi ili kunusuru uharibifu wa mazingira unaohatarisha Taifa letu kuwa jangwa . Kazi yao kubwa iwe kuhudumia idadi miti kwa kuipanda na kuitunza adhabu zao ziwe na manufaa kwa jamii na sura ya Taifa.
11.0 HATIMA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yangu ya mwaka wa fedha 2015/16 nikiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, niiliitaka Serikali kutoa ukomo wa muda, ambapo kila raia wa Tanzania atapatiwa Kitambulisho chake cha Taifa na kuainisha gharama zilizotumika katika mchakato mzima wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Bwana Dickson E. MAIMU, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia, tarehe 25 Januari, 2016 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu tarehe 26 Januari 2016. Katika taarifa ile ilibainika kuwa “Taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni.”
Mheshimiwa Spika, Katika taarifa ile, Rais aliagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA. Sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kuliambia bunge hili tukufu kuwa ni lini inatarajia kuileta bungeni ripoti ya Ukaguzi Maalumu ulioagizwa kufanyika na Rais Magufuli, ili bunge sasa liweze kutimiza majukumu yake yaliyoanishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 ibara ndogo ya (2)
Mheshimiwa Spika, Ripoti hiyo ya uchunguzi maalumu wa NIDA itakapowasilishwa ndani ya Bunge hili, wabunge kwa niaba ya wananchi tutaweza kufahamu mbivu na mbichi na kujua hatma ya vitambulisho vya Taifa, hatma ambayo mpaka sasa Serikali imekosa majibu yake.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na masuala mengine kuhusu ushauri tuliotoa katika vitambulisho vya Taifa, bado tunaona kuwa mfumo mzima wa kuwatambua Watanzania upo “shaghala bagara” kutokana na kuwepo kwa vitambulisho vya aina nyingi kama vile Leseni za Udereva na Kadi ya Mpiga kura, hivyo kulifanya Taifa kuingia hasara kubwa ya kutengeneza vitambulisho kwa watu wale wale. Huku ni kukosa ubunifu.
Mheshimiwa Spika, Gazeti la Mtanzania la tarehe 2 Machi 2016, liliripoti kuwa “mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa unatarajiwa kuanza upya, kutokana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kukiri kuwapo kwa upungufu katika vitambulisho vya sasa.” Huu ni udhaifu mkubwa wa Serikali kukosa ubunifu, kitendo kinachopeleka hasara kwa Taifa bila watu kuwajibishwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuwa ni kwa sababu gani ilifanya uzembe mpaka vitambulisho vya Taifa vikaanza kutolewa huku kukiwa na udhaifu uliobainika baada ya zoezi la kuvigawa kuanza.
Mheshimiwa Spika, Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunaishauri Serikali kuunganisha mfumo wa vitambulisho vya Taifa na vitambulisho vya aina nyingine kama vile leseni za udereva, Utambulisho wa Namba ya Mlipa Kodi, Vitambulisho vya Bima za Afya, Hati za Kusafiria na Kadi za Mpiga kura ili kuwa na “National Database” ambayo inajumuisha taarifa zote za Watanzania, jambo ambalo litaepusha upotevu wa kumbukumbu na kurahisisha michakato ya kutoza kodi na kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa wapi wananchi wapo, wanafanya nini na wanaweza vipi kuisaida Serikali kutimiza majukumu yake kama vile ulipaji kodi kwa wakati na ufuatiliaji wa ulinzi wa Raia wetu wanasafiri nje ya nchi.
11.1 UKIUKWAJI WA TARATIBU ZA KUSITISHA AJIRA ZA WAFANYAKAZI 597 WA NIDA
Mheshimiwa Spika, Tarehe 7 Machi 2016, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa alisitisha ajira za vijana 597 waliokuwa wanafanya kazi kwa mkataba, bila kufuata taratibu za kusitisha ajira. Watumishi hao hawadai kurudishwa kazini, lakini wanachodai ni kulipwa stahiki zao kwa mujibu wa mkataba wao wa ajira.
Mheshimiwa Spika, waliokuwa watumishi wa NIDA waliositishiwa mikataba yao ya ajira wana madai ya zaidi ya bilioni 2.3. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA alitoa tangazo tarehe 11 April 2016, katika gazeti la Mwananchi ukurasa wa 16 kuwa NIDA itaanza kufanya malipo ya madai yao kuanzia Jumatano tarehe 13 April 2016 saa 3.00 asubuhi, lakini Mheshimiwa Spika, Taarifa zilizoifikia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kuwa mpaka dakika hii ninavyoongea hakuna fedha zozote zilizolipwa kwa waliokuwa waajiriwa hao 597 wa NIDA waliositishiwa ajira zao.
Mheshimiwa Spika, huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu wa kumfukuza mtumishi kinyume cha sheria kiholela na hatimaye kutomlipa stahiki zake ipasavyo jambo ambalo ni kinyume na misingi ya utawala bora.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa na imebaini kuwa mamlaka hiyo haikuwahi kupeleka makato ya wafanyakazi katika Mfuko wa Kijamii wa GEPF kuanzia mwezi Julai 2015 mpaka tarehe 7 Machi 2016 ambapo ajira zilisitishwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza bunge hili sababu za Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA kushindwa kulipa madai ya wafanyakazi wapatao 597 walioachishwa kazi tangu mwezi Disemba 2015 ambapo hawakulipwa stahiki zao kwa miezi mitatu mfululizo tangu mpaka ilipofika tarehe 7 Machi 2016 ambapo ajira zao zilisitishwa rasmi.
12.0 UMUHIMU WA JESHI LA POLISI KATIKA KUBORESHA MAISHA YAO.
Mheshimiwa Spika, Serikali yoyote makini Duniani inaweza kujenga ustawi wa maisha ya raia wake kwa kutambua umuhimu wa Ulinzi na Usalama katika Taifa. Lakini kuhitaji ulinzi kwa walinzi ambao huwapi ulinzi wa maisha yao kama mishahara bora na masilahi mengine ni sawa na kumeza dawa ya tumbo kwa kutumia konyagi.
Mheshimiwa Spika, Watumishi wote wa umma wanahitaji ungalifu bora kutoka Serikalini , lakini watumishi wetu wanaolinda amani na usalama wa raia wanahitaji upendeleo kwa kiwango fulani zaidi , kwani kazi ya ulinzi ni kujitoa maisha kwa ajili ya wengine .
Mheshimiwa Spika, mishahara ya Polisi na posho zao zote bado ni ni ndogo sana , na ndio maana kuondoa rushwa ndani ya jeshi la Polisi kwa kuendesha warsha , semina elekezi , kutoa miongozo , na vipeperushi ni jambo ambalo haliwezi kufanikiwa , katika sala ambayo Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake, kuna mahali sala hiyo inasema na nukuu “ USITUTIE MAJARIBUNI BALI UTUOKOE NA YULE MWOVU “
Mheshimiwa Spika , rushwa ndani ya Jeshi la Polisi imejengwa na utawala wa Serikali ambao umeshindwa kujali masilahi bora ya Walinzi wetu hawa ikiwa ni pamoja na Jeshi la Magereza , kwa hiyo Serikali ndiyo inayowatia Askari wetu majaribuni katika suala la kuomba na kupokea rushwa kwa kuwalipa fedha kidogo sana kwa ajili ya maisha yao .
Mheshimiwa Spika, hakuna Polisi wala Askari magereza anayeweza kujenga nyumba kwa mshahara na marupurupu anayopokea , wanaishi maisha magumu na ya taabu sana , ndio maana wakiona kosa wanaona fedha badala ya uwajibikaji na na kutenda haki.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kuwalipa walinzi wetu hawa vizuri ili kufanya kazi ya Jeshi la Polisi au Jeshi la Magereza / Zima moto na Uokoaji iwe ni kazi ya fahari kuanzia kwenye familia kama zilivyo kazi nyingine .
12.1 JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 pamoja na mambo mengine alipendekeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa majengo makubwa nchini ambayo ni chanzo cha mapato serikali ianzishe mamlaka ya kuyasimamia (Real Estate Regulatory Authority) kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inapata mapato na kusimamia uzingatiaji wa miundo mbinu na kanuni za kiusalama katika ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Aidha pamoja na masuala ya mapato tunaitaka serikali katika ihakikishe kuwa inatoa maelekezo kwa taasisi na watu binafsi ambao wanamiliki majengo au wanatarajia kuwa na majengo kuhakikisha kuwa wanajenga na kuweka visima kwa ajili ya maji ambayo yatatumika kama kutakuwa na janga la moto katika majengo yao au maeneo yao Hii itasaidia sana kuondoa tatizo la magari ya zima moto kuishiwa maji kila linapotokea janga la moto na hili ni kwa mujibu wa sheria ni bora sheria hii ikazingatiwa na kufuatiliwa.
Mheshimiwa Spika , Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inalitaka na kulishauri Jeshi la Uokoaji na zimamoto kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kuzipa mamlaka Halmashauri za Miji , Manispaa na Majiji uwezo wa kusimamia kikamilifu maeneo ya makazi na kuhakikisha kuwa kila nyumba inayoishi binadamu au anakofanyia kazi inakuwa na uwezo na miundo mbinu ya kuzima moto na kila nyumba iwe ni lazima kuwa na Mtungi wa kuzimia moto ( Fire extinguisher ) na kazi hizi ziachwe kwa Halmashauri za Miji , Manispaa , Majiji husika kwa kushirikiana na Jeshi la zima moto na uokoaji
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika kipindi chote cha Bunge la 10, tumekuwa tukiishauri Serikali kufanya maboresho makubwa ya Jeshi la Zima Mto na Uokoaji kwa kulipangia bajeti ya kutosha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ili jeshi hilo liendeshwe kisasa zaidi katika kukabiliana na majanga ya ajali za moto na matukio ya uokoaji.
Mheshimiwa Spika, Hata hizo bilioni 53 zilizoombwa na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji inaonesha kiasi gani Wizara yenyewe na Jeshi kwa ujumla halijatambua umuhimu wa kitengo hiki. Jeshi la Zima moto linahitaji Helkopta za kisasa zenye uwezo wa kuzima moto. Jeshi hili la zima moto linahitaji kuwa na uwezo wa kuzima moto kwenye misitu mikubwa kunapokuwa na janga la moto, milima inapopata majanga ya moto kama mlima Kilimanjaro, Jeshi hili linapaswa kuwa na uwezo wa kuzima moto, vile vile Jeshi linatakiwa kuwa na uwezo wa kuzima moto katika maeneo ya nchi ambayo magari hayawezi kufika kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona umuhimu wa Jeshi hili utathibitika baada ya Chama Cha Mapinduzi kuondoka madarakani, ili uongozi wenye maono mapana uje na kutazama Jeshi hili katika sura na mfano tulioeleza hapo juu. Bilioni 53 walizoomba inapaswa kuwa bajeti ya Jeshi la Zima moto ya kufanya dhifa ya nyama choma yaani (barbecue)
13.0 UHAMIAJI HARAMU NA USALAMA KATIKA MIPAKA YA NCHI
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeendelea kuishauri Serikali kuhusu usalama wa mipaka ya nchi yetu kuwa ipo hatarini dhidi ya matukio ya uhalifu wa kimataifa na matukio ya ugaidi, kutokana na ongezeko la wahamiaji haramu ambao wanaingia nchini kupitia mipaka yetu na wanakamatwa wakiwa ndani ya nchi tayari wakisafirishwa kwenda kwenye mataifa mengine kusini mwa jangwa la Sahara.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunaishauri Serikali kutumia mbinu za kisasa ili kuzuia wahamiaji haramu wanaotumia nchi yetu kama “transit gate” ya kuhamia kwenye mataifa mengine hasa kutoka mataifa ya Kaskazini mwa Afrika kwenda kusini mwaka bara la Afrika.
Mheshimiwa Spika , vile vile Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iangalie namna ya kuanzisha ofisi za uhamiaji kwenye maeneo muhimu yanayotumika kama matobo kwa wahamiaji haramu .
14.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Asilimia zaidi ya 50% ya wabunge waliomo ndani ya Bunge hili wengi ni wapya maana yake ni kwamba, michakato ya kura za maoni katika vyama vya siasa ni sehemu ya kubadilisha mwanasiasa na pia mfumo wa demokrasia unatoa uhuru wa jinsi hiyo katika uchaguzi.
Mheshimiwa Spika, Martin Niemoller alikua mchungaji wakati wa utawala wa Kinazi Ujerumani akiwa mstari wa mbele kupinga utawala wa mabavu , alichukuliwa mateka katika kambi (concentration camp) na alisema maneno yafuatayo;
“First they came for the Socialists, and I did not speak out—
Because I was not a Socialist.
Then they came for the Trade Unionists, and I did not speak out—
Because I was not a Trade Unionist.
Then they came for the Jews, and I did not speak out—
Because I was not a Jew.
Then they came for me—and there was no one left to speak for me.”
Mheshimiwa Spika, ni muhimu wabunge, viongozi wa vyama na serikali na watu wote wajue tunapoishauri Serikali juu ya sheria na sera za nchi ni busara na upendo wa hali ya juu kujua kwamba uamuzi tunaoufanya humu ndani leo ni kwa faida na maslahi ya watoto wetu na watoto wa watoto wetu. Kwa bahati mbaya itikadi za vyama vyetu zimenunua utashi, ukweli na utu wetu.
Mheshimiwa Spika, Rais Magufuli ana jambo muhimu la kufanya ili athibitishe anachokiita huruma yake kwa masikini nalo ni kuwapa masikini katiba yao (Rasimu ya Warioba) iliyobeba maoni waliyoyatoa katika Tume ya Warioba kabla ya kuchakachuliwa na Bunge la Katiba.
Mheshimiwa Spika, ni namma moja tu inaweza kumsaidia Rais kukabiliana na ufisadi , ubadhirifu wa mali za umma na mengineyo yenye sura hizi , na namna hiyo ni kuacha uhuru wa Bunge katika kazi zake za kuisimamia Serikali .
Mheshimiwa Spika, James Freeman Clarke alisema maneno haya “The difference between a politician and a statesman is that a politician thinks about the next election while the Statesman think about the next generation.” Sisi tunafikiria nini?
Mheshimiwa spika, tatizo la wanasiasa wengi wa Taifa hili kila wanapomaliza uchaguzi papo hapo, ndipo wanaanza kufikiria uchaguzi unaofuata. Ndio maana mawazo ya vikao vya vyama vyetu (Party Caucus) yanakuwa muhimu kuliko msingi wa siku za usoni za nchi yetu. Hili nalo ni tishio kubwa la usalama wa Taifa letu. Kwani wanaopaswa kushauri, kuelekeza na kusimamia wameukataa wajibu wao bila aibu.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema, zawadi pekee mbunge yoyote anayoweza akatoa kwa wazazi wake, watoto wake, familia yake na nchi yake ni yeye kuwa na uwezo wa kusimamia ukweli, demokrasia, utu na haki kwa gharama yoyote ile.
………………………………………..
Godbless Jonathan Lema (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Tarehe 16 Mei, 2016