Uchaguzi 2020 Umuhimu wa Mawakala wa Wagombea Urais, Ubunge na Udiwani kupatiwa nakala za matokeo ya uchaguzi katika vituo vya kupiga kura

Matojo Cosatta

JF-Expert Member
Jul 28, 2017
234
390
KILA WAKALA WA MGOMBEA URAIS, UBUNGE NA UDIWANI KATIKA KITUO CHA KUPIGA KURA ANA HAKI YA KUPATIWA NAKALA YA FOMU YA MATOKEO YA UCHAGUZI WA RAIS, MBUNGE NA DIWANI.

SEHEMU 1: UTANGULIZI.


Makala hii inaangazia haki ya kisheria ya wagombea Urais, Ubunge na Diwani kupatiwa Nakala za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani kutoka kwa Wasimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura (Presiding Officers), Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi (Assistant Returning Officers) na Wasimamizi wa Uchaguzi (Returning Officers) pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Haki ya wagombea au mawakala wao kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi hiko wazi sana bila utata wowote katika ngazi ya Taifa, Jimbo la Uchaguzi na Kata lakini haki hii imezungukwa na utata mkubwa sana wa kisheria katika ngazi ya Kituo cha Kupiga Kura. Pamoja na ukweli kwamba haki ya wagombea Urais, Ubunge na Udiwani au mawakala wao kupatiwa nakala za fomu za matokeo katika Kituo cha Kupiga kura ina utata mkubwa wa kisheria, hatahivyo, magombea Urais na Ubunge au wakala wake ana haki ya wazi kabisa kupatiwa nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) na Mbunge (Fomu Na. 21 B) ya kila kituo cha kupiga kura kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi ambayo imejazwa "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura, hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 35 F (5) na 81 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343.

Kwa maneno mengine, Kifungu cha 35 F (5) na 81 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 kinaelekeza kwa lazima na kmshurutisha Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi kumpatia mgombea Urais na Ubunge au wakala wake nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) na Mbunge (Fomu Na. 21 B) ya kila Kituo cha Kupiga Kura ambayo imejazwa "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura.

Haki ya mawakala wa wagombea Urais, ubunge na udiwani ya kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi katika ngazi ya Kituo cha Kupiga Kura imezungukwa na utata mkubwa sana, hivyo, ufafanuzi wa kina unaitajika kuondoa utata huu.

Hivyo basi, makala hii itajikita zaidi katika swala la haki ya wagombea Urais, ubunge na udiwani kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi katika Kituo cha Kupiga Kura kutoka kwa Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura mara baada ya kumaliza kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani na kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi mara baada ya kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura na kujaza na kutia saini yake kwenye "Sehemu B" ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani. Msisitizo mkubwa utawekwa katika nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na unyeti wa ofisi hii tukufu.

Utangulizi huu umegawanyika katika Sehemu A na Sehemu B kama ifuatavyo hapo chini.


[ A. ] Umuhimu wa Nakala za Matokeo ya Uchaguzi Katika Uchaguzi Mkuu.

Mojawapo ya sifa ya Uchaguzi Huru na wa Haki ni uwepo wa mfumo wa uchaguzi ambao ni wa uwazi, unaodhibitishika, unaokagulika, unaowajibika, salama, sahihi, rahisi, aminifu na unaofikika yaani kwa Kiingereza tunasema Election System which is transparent, verifiable, auditable, accountable, secure, accurate, simple, reliable, and accessible.

Sifa hizi za Uchaguzi Huru na wa Haki zimekubalika kimataifa na ni za viwango vya kimataifa na pia sifa hizi zinatambuliwa na Katiba na sheria za nchi kadhaa duniani ikiwemo Ibara ya 81 (e) na 86 ya Katiba ya Jamhuri ya Kenya, 2010 kama ilivyotafsiriwa na Mahakama ya Juu ya Kenya (Supreme Court of Kenya) na Mahakama ya Rufaa ya Kenya katika kesi zifuatazo;

(i) Raila Odinga Vs Uhuru Kenyatta & Others, Petition No. 5 of 2013

(ii) Raila Odinga & Another Vs Uhuru Kenyatta & Others, Petition No. 1 of 2017

(iii) National Super Alliance (NASA) Vs IEBC, Attorney General & Jubilee Party, Civil Appeal No. 258 of 2017 (Mahakama ya Rufaa).

Pia, mwaka 2009, Mahakama ya Katiba ya Shirikisho la Ujerumani ya Seneti ya Pili (“Bundesverfassungsgericht") katika kesi ya muunganiko ya kikatiba (consolidated constitutional case) ambayo inafanyiwa rejea rasmi kama [BVerfG] 2 BvC 3/07 na 2 BvC 4/07 iliamua kuwa mfumo wa uchaguzi wa kielektroniki (Electronic Voting System) wa Ujerumani ni batili kisheria na kuupiga marufuku mfumo huo kutumika nchini Ujerumani kutokana na kukiuka Ibara ya 38, 20 (1) na 20 (2) ya Katiba ya Shirikisho la Ujerumani, 1949 ( Grundgesetz für die Bundesrepublik Deutschland ) kutokana na mfumo wa Uchaguzi wa kielektroniki kukosa sifa za kuwa na uwazi (transparency), uthibitishikaji (verifiability), kuaminika (reliability) na usalama (security) hususani usalama wa kimtandao (Cyber Security).

Ili mfumo wa uchaguzi uwe na uwazi , udhibitishike, ukagulike , uwajibike, uaminike, uwe salama na sahihi lazima wagombea wote wapatiwe nakala za matokeo katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kituo cha kupiga kura, ngazi ya kata, ngazi ya jimbo la uchaguzi na ngazi ya Taifa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hii ndo njia pekee inayoweza kufanya Election System kuwa transparent, verifiable, auditable, accountable, secure, reliable and accurate.

Swali ni je sheria za uchaguzi za Tanzania zinatoa haki kwa wagombea Urais, Ubunge na Udiwani kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi katika ngazi zote? Hili ndo swali muhimu sana ambalo litajibiwa na makala hii.


[ B. ] Haki ya Mgombea Kupatiwa Nakala za Matokeo ya Uchaguzi Katika Ngazi Zote.

Jibu ni ndio
, wagombea Urais, ubunge na udiwani wana haki ya kupatiwa nakala za matokeo ya uchaguzi katika ngazi zote kama ifuatavyo;

(a) Kila mgombea au wakala wa Mgombea wa nafasi ya Urais, ubunge na udiwani ana haki ya kupatiwa nakala ya za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani kutoka kwa Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura katika ngazi ya Kituo cha Kupiga Kura chini masharti ya Kifungu cha 79 A (1) (e) cha Sheria ya Uchaguzi waTaifa, Sura ya 343, Kanuni ya 63 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020, Kanuni ya 56 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani, 2020, Aya ya 9.19 (iv) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020, Aya ya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020 na Aya ya 8 (3) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na Wagombea, 2020.

(b) Kila mgombea Urais au wakala wake ana haki ya kupatiwa nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) ya kila kituo cha kupiga kura kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi ambayo imejazwa na kutiwa saini "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka kituo cha kupiga kura, hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 35 F (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343.

(c) Kila mgombea Ubunge au wakala wake ana haki ya kupatiwa nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa mbunge ya kila kituo cha kupiga kura kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi ambayo imejazwa "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka kituo cha kupiga kura, hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 81 (1) na 35 F (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343.

(d) Kila mgombea udiwani au wakala wake ana haki ya kupatiwa nakala ya fomu za matokeo ya uchaguzi wa diwani katika ngazi ya Kata kutoka kwa Msimamizi Msaadizi wa Uchaguzi chini masharti ya Kanuni ya 60 (1) (c) ya Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani, 2020 pamoja na Aya ya 10 (9) (iv) na (vi) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020.

(e) Kila mgombea ubunge au wakala wake ana haki ya kupatiwa nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa mbunge kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi katika ngazi ya Jimbo chini masharti ya Kanuni ya 69 (1) (c) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 na masharti ya Aya ya 10 (9) (vi) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020.

(f) Kila mgombea Urais au wakala wake ana haki ya kupatiwa nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi katika ngazi ya Jimbo chini masharti ya Kanuni ya 67 (1) (b) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 pamoja na masharti ya Aya ya 9 (5) (ii) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na Wgombea, 2020.

(g) Kila mgombea Urais au wakala wake ana haki ya kupatiwa nakala ya matokeo ya uchaguzi wa Rais ngazi ya taifa kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini masharti ya Kanuni ya 68 (4) (c) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020.


SEHEMU 2: MSIMAMO SAHIHI WA SHERIA.

(A) Msimamo wa Kisheria wa Kanuni na Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wagombea.


Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kila wakala wa mgombea Urais na ubunge alikuwa na haki ya kupatiwa nakala ya fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge. Sheria ilimtaka kwa lazima Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ( Presiding Officer ) kumpatia kila wakala wa mgombea Urais na ubunge nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge kwa mujibu wa Kanuni ya 60 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 (Tangazo la Serikali Na. 307 la 2015). Katika Kanuni za Uchaguzi Rais na Wabunge za mwaka 2015 haki ya wakala wa mgombea Urais na ubunge kupatiwa nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais nambunge ilikuwa wazi na bayana sana bila utata wowote.

Lakini kwa mtizamo wa juu juu bila kufanya uchambuzi wa kina wa sheria inaonekana katika Maelekezo ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na Wagombea, 2020 na Kanuni za Uchaguzi Rais na Wabunge za mwaka 2020 kuwa haki hii ya kupatiwa nakala za fomu za matokeo imepunguzwa makali kwa sababu kwa mtizamo wa juu juu bila kufanya uchambuzi wa kina wa sheria inaonekana kupewa nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge imefanywa kuwa hisani (privilege) kwa mujibu wa Kanuni ya 63 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 (Tangazo la Serikali Na. 402 la 2020) na kwa mujibu wa Aya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na Wagombea, 2020 ambapo kwa mtizamo wa juu juu bila kufanya uchambuzi wa kina wa sheria inaonekana Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura anaweza kumpatia au kukataa kumpatia wakala wa mgombea Urais na ubunge nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais na Mbunge iwapo atajisika kufanya hivyo kwa kuwa hashurutishwi na Kanuni au Maelekezo kutoa nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge. Hatahivyo, uchambuzi yakinifu ukifanyika majibu yanayopatikana ni kinyume chake ambapo inadhibitishwa kwa uwazi kabisa kuwa haki ya wagombea Urais na Ubunge au mawakala wao kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge ni haki ya lazima na Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura na Msimamizi wa Uchaguzi wanashuritishwa na sheria kwa lazima kuwapatia wagombea Urais na Ubunge au mawakala wao kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge katika nyakati na hatua tofauti.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2020, Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura "anaweza" kumpatia wakala wa mgombea Urais na Ubunge katika Kituo cha Kupiga Kura nakala ya fomu ya matokea ya uchaguzi wa Rais na mbunge "iwapo kuna nakala za kutosha za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge", hii ni kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 63 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 (Tangazo la Serikali Na. 402 la 2020) na Aya ya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na Wagombea, 2020.

Kutoka na matumizi ya neno "anaweza" (may) katika Kanuni ya 63 (2) na Aya ya 3 (8) tajwa hapo juu, kisheria inamaanisha kuwa Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ana hiyari (discretion) ya kumpatia au kukataa kumpatia wakala wa mgombea Urais na ubunge katika Kituo cha Kupiga Kura nakala ya fomu ya matokea ya uchaguzi wa Rais na mbunge.

Sababu ya hiyari (discretion) hii ya Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura inatokana na matumizi ya neno "anaweza" (may) katika sheria kwa msingi kwamba neno hili linapotumika katika sheria limaanisha kuwa mtu ana hiyari kufanya au hiyari ya kukataa kufanya kitu ambacho sheria inasema kifanyike (discretionary power), hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 52 (1) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1 kama kilivyotafsiriwa na Mahakama Kuu katika kesi ya Laula Edmund Vs Barke Ahmed Said, PC Civil Appeal No. 1 of 2020.

Kwa maneno mengine, ni kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya 63 (2) na Aya ya 3 (8) tajwa hapo juu, Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ana mamlaka ya hiyari (discretionary power) ya kukataa kumpatia wakala wa mgombea Urais katika Kituo cha Kupiga Kura nakala ya fomu ya matokea ya uchaguzi wa Rais na mbunge hata kama kuna nakala za kutosha za matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge.


(B) Ukinzano wa Sheria Kuu na Sheria Ndogo Ndogo.

Hatahivyo, masharti ya Kanuni ya 63 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 na mashartti ya Aya ya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na Wagombea, 2020 yanakinzana na masharti ya Kifungu cha 79 A (1) (e) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 ambacho kinaelekeza kwa lazima kwa kutumia kitenzi kisaidizi "ata" (shall) kuwa iwapo kuna nakala za kutosha lazima Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ampatie wakala wa mgombea Urais na mgombea ubunge katika Kituo cha Kupiga Kura nakala ya fomu ya matokea ya uchaguzi wa Rais na Mbunge.

Kwa maneno mengine, ni kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 79 A (1) (e) tajwa hapo juu, Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura analazimishwa na sheria bila hiyari yake kumpatia wakala wa mgombea Urais katika Kituo cha Kupiga Kura nakala yafomu ya matokea ya uchaguzi wa Rais na Mbunge iwapo kuna nakala za kutosha za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais au mbunge.

Kama kuna nakala za kutosha lazima Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ampatie wakala wa mgombea Urais au ubunge nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais na Mbunge kwa sababu kitenzi kisaidizi "ata" (shall) kinapotumika katika sheria kinamaanisha kuwa mtu au mtumishi wa umma hana kabisa hiyari bali ni lazima afanye kama alivyoelekezwa na sheria (mandatory duty), hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 52 (2) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1 kama kilivyotafsiriwa na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Shaaban Iddi Jololo and 3 others Vs Republic Criminal Appeal No. 200 of 2006.

Iwapo Sheria Ndogo Ndogo (subsidiary legislation) iliyotungwa na mamlaka iliyokasimishwa (delegated) mamlaka ya kutunga sheria na bunge "inakinzana" na Sheria Kuu (principal legislation) iliyotungwa na bunge lenyewe basi Sheria Ndogo Ndogo inakuwa batili tangia mwanzo (null et void ab initio) kwa kiwango ambacho Sheria Ndogo Ndogo inakinzana na Sheria Kuu iliyotungwa na bunge, haya ndo matakwa ya masharti ya Kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1 kama kilivyotafsiri na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Morogoro Hunting Safaris Ltd. Vs Halima Mohamed Mamuya, Civil Appeal No. 117 of 2011 na pia huu msimamo wa sheria uliwekwa na Mahakama zaidi ya miaka 80 iliyopita katika kesi ya Nanal Damodar Kanji Vs Tanga Township Authority [1940] 1 T.L.R. 239.

Kirai "Sheria Ndogo Ndogo" (subsidiary legislation) kimetafsiri na Kifungu cha 4 ya Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1, pamoja na mambo mengine kumaanisha Maelekezo, Tamko, Kanuni, na Notisi ambayo imetungwu au kutolewa chini ya mamlaka ya sheria iliyotungwa na bunge au mamlaka nyingine ya kisheria, hivyo, basi, kisheria Kanuni na Maelekezo ni sheria Sheria Ndogo Ndogo.

Tume ya Taifa Uchaguzi imekasimishwa (delegated) na bunge Mamlaka ya kutunga Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge na Maelekezo ya Uchaguzi chini ya Kifungu cha 124 na 126 cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 ambayo kisheria ni sheria ndogo ndogo.

Kwa msingi huu basi, iwapo Kanuni za Uchaguzi na Maelekezo ya Uchaguzi yaliyotungwa na Tume ya Taifa Uchaguzi vinakinzana na Sheria Kuu ya Uchaguzi iliyotungwa na bunge basi Kanuni za Uchaguzi na Maelekezo ya Uchaguzi ambayo yametungwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi vinakuwa batili tangia mwanzo (null et void ab initio) kwa kiwango ambacho vinakinzana na Sheria yaUchaguzi wa Taifa, Sura ya 343, haya ndo matakwa ya masharti ya Kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1.

Hivyo basi, msimamo sahihi wa sheria sio ule ambao umeelekezwa kwenye Kanuni ya 63 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 na Aya ya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na Wagombea, 2020 kwa sababu msimamo wa sheria ambao umeelekezwa na Kanuni ya 63 (2) na Aya ya 3 (8) tajwa hapo juu kisheria ni batili tangia mwanzo kwa kukinzana na Kifungu cha 79 A (1) (e) cha Sheria ya Uchaguzi waTaifa, Sura ya 343.


(C) Shuruti ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Vituo.

Pia, kuna baadhi ya Maelekezo ya Uchaguzi ambayo yametungwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya Kifungu cha 126 cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 ambayo yanashurutisha au yanaelekeza kwa lazima kuwa Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura lazima ampatie kila wakala wa mgombea Urais, Ubunge na Udiwani nakala ya Fomu ya Matokea ya Uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani ambayo ni Fomu Na. 21A, Fomu Na. 21B na Fomu Na. 21C kama inavyofafanuliwa kwa ufipi hapa chini;

(i) Aya 9 (19) (vi) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020 inaelekeza kwa lazima kwamba Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura baada ya kumaliza kujaza fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani sharti akumbuke kumpa kila wakala wa mgombea nakala moja ya matokeo ya Uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani bila sharti lolote na bila sharti la kwamba lazima kuwepo nakala za kutosha katika kituo cha kupiga kura.

(ii)Aya ya 3 (8) (iv) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020 pia nayo inaelekeza kwa lazima kwamba Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura baada ya kumaliza kujaza fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani sharti akumbuke kumpa kila wakala wa mgombea nakala moja ya matokeo ya Uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani bila sharti lolote na bila sharti la kwamba lazima kuwepo nakala za kutosha katika kituo cha kupiga kura .


(D) Shuruti ya Kupatiwa Fomu Na. 21 A na 21 B Ngazi ya Jimbo la Uchaguzi.

Magombea Urais na Ubunge au wakala wake ana haki ya kupatiwa nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) na Mbunge (Fomu Na. 21 B) kutoka katika Vituo vya Kupiga Kura mara mbili (2) katika ngazi mbili tofauti yaani ngazi ya Kituo cha Kupiga Kura kutoka kwa Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura mara tu baada ya zoezi la kuhesabu kura kukamilika na ngazi ya Kituo cha Kujumlisha Kura za Jimbo la Uchaguzi kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi mara baada tu ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura.

Magombea Urais na Ubunge au wakala wake ana haki ya wazi kabisa kupatiwa nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) na Mbunge (Fomu Na. 21 B) ya kila Kituo cha Kupiga Kura kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi ambayo imejazwa "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi mara tu baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura, hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 35 F (5) na 81 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343.

Kwa maneno mengine, Kifungu cha 35 F (5) na 81 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 kinaelekeza kwa lazima na kmshurutisha Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi kumpatia mgombea Urais, Ubunge na Udiwani au wakala wake nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) na Mbunge (Fomu Na. 21 B) ya kila Kituo cha Kupiga Kura ambayo imejazwa "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura.

(E) Hitimisho Dogo.

Hivyo basi, ipo misimamo sahihi wa sheria (correct positions of law) mitatu ifuatayo;

(i) Msimamo sahihi wa sheria wa kwanza (1) ni kama ulivyoelekezwa kwenye masharti ya Kifungu cha 79 A (1) (e) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 kwamba kama kuna nakala za kutosha "lazima" Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ampatie wakala wa mgombea Urais na mgombea ubunge nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge. Pia, muhimu kujua kuwa Aya ya 9 (19) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020 na Aya ya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020 zinaelekeza kwa lazima kuwa kila Kituo cha Kupiga Kura lazima kiwe na Kitabu cha Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais chenye "nakala 24" za fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ( Fomu Na. 21 A ) na kati ya nakala 24 tajwa hapo juu, nakala 21 ni kwa ajiri kuwapatia mawakala wa wagombea Urais ili wazipeleke kwa wagombea Urais na vyama vyao vya siasa ambavyo wanawakilisha katika Kituo cha Kupiga Kura na nakala 3 ni kwa ajiri ya matumizi ya Tume ya Uchaguzi. Hivyo basi, kutakuwepo na nakala za kutosha za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani.

(ii) Msimamo sahihi wa sheria wa pili (2) ni kama ilivyoelekezwa na Aya ya 9 (19) (iv) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020 na Aya 3 (8) (iv) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020 kwamba kwamba Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura baada ya kumaliza kujaza fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani sharti akumbuke kumpa kila wakala wa mgombea Urais, Ubunge na Udiwani nakala moja ya matokeo ya Uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani.

(iii) Msimamo sahihi wa sheria wa tatu (3) ni kama ilivyoelekezwa na Kifungu cha 35 F (5) na 81 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 kwamba lazima Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi kumpatia mgombea Urais na Ubunge au wakala wake nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) na Mbunge (Fomu Na. 21 B) ya kila Kituo cha Kupiga Kura ambayo imejazwa "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura.

Swali muhimu hapa ni je kutakuwepo nakala za kutosha za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, mbunge na Diwani katika Kituo cha Kupiga Kura? Ufafanuzi wa kina wa jibu la swali hili unapatikana sehemu inayofuatia hapo chini baada ya sehemu yaani Sehemu ya 3 na jibu ni ndio.


SEHEMU 3: JE KUTAKUWEPO NA NAKALA ZA KUTOSHA ZA FOMU ZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA RAIS, MBUNGE NA DIWANI KATIKA KITUO CHA KUPIGA KURA?

Jibu ni ndio.


Ndio kisheria lazima kuwepo na nakala za kutosha za Fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani katika Kituo cha Kupiga Kura kwa sababu ambazo nitazielezea hapa chini.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kutunga au kutengeneza Maelekezo ya Uchaguzi (Election Directives) yenye nguvu ya kisheria chini ya Kifungu cha 126 cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343. Vyama vya Siasa, wagombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiwemo Mwenyekiti na Wjumbe wa Tume ya Uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura na Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Kupiga Kura wanashurutishwa na Kanuni ya 75 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2020 kuheshimu Maelekezo ya Uchaguzi ambayo yametungwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitengeneza Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020 ambayo yanataja idadi ya nakala za matokeo ya uchaguzi wa Rais na mbunge ambazo zinapashwa kuwepo katika Kituo cha Kupiga Kura. Maelekezo ya Uchaguzi yanaishurutisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kwenye kila kituo cha kupiga kura kuna Nakala 24 za Fomu za Matokeo ya kila uchaguzi yaani uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani na kati ya hizo Nakala 24 za Fomu za Matokeo ya kila uchaguzi Nakala 21 ni kwa ajiri ya kuwapatia mawakala wa wagombea wa kila nafasi yaani nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani na Nakala 3 ni kwa ajiri ya Matumizi ya Tume ya Uchaguzi. Maelezo ya kina kuhusu utoshelevu wa nakala yametolewa hapa chini.


A. UTOSHELEVU WA NAKALA ZA FOMU ZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA RAIS.

Aya ya 9.19 ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020
na Aya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020 zinaelekeza kwa lazima kuwa kila Kituo cha Kupiga Kura lazima kiwe na Kitabu cha Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais chenye "nakala 24" za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ( Fomu 21 A ) ambazo zitagawiwa kama ifuatayo;

(1) Nakala ya Kwanza ya Fomu ya Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ambayo iko ukrasa wa 1 wa Kitabu cha Nakala za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais atapewa Msimamizi wa Uchaguzi (Returning Officer) ngazi ya jimbo la uchaguzi kwa ajiri ya kujumlishia matokeo ya uchaguzi wa Rais ngazi ya jimbo la uchaguzi. Nakala ya kwanza ni nakala halisi (original copy).

(2) Nakala ya Pili ya Fomu ya Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ambayo iko ukrasa wa 2 wa Kitabu cha Nakala za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais itabandikwa ukutani na Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura katika Kituo cha Kupiga Kura husika kwa ajiri ya kuwajulisha wapiga kura, wananchi au umma wa Watanzania matokeo ya Uchaguzi wa Rais katika Kituo cha Kupiga Kura husika. Nakala ya Pili sio nakala halisi bali ni nakala rudufu (photocopy) ambayo inarudufiwa kutoka katika nakala halisi yaani nakala ya kwanza.

(3) Nakala ya Kumi na Tatu (13) ya Fomu ya Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ambayo iko ukrasa wa 13 wa Kitabu cha Nakala za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais itapewa Tume Taifa ya Uchaguzi kwa ajiri ya matumizi yake ya kiofisi. Nakala ya 13 nayo ni nakala halisi (original copy).

(4) Kuanzia Nakala ya 3 na kuendelea (consecutively) mpaka Nakala ya 24 katika Kitabu cha Nakala za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ambazo ziko kuanzia ukrasa wa 3 na kuendelea mpaka ukrasa wa 24 wa Kitabu tajwa hapo juu watapewa mawakala wa wagombea Urais kulingana na idadi yao isipokuwa Nakala ya 13 ambayo itakuwa ni Nakala ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa kuwa kuna wagombea Urais 15, hivyo, basi mawakala wa wagombea Urais katika Kituo cha Kupiga Kura watapewa kuanzia nakala ya 3 mpaka ya nakala 18 isipokuwa nakala ya 13 ambayo itapewa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Pia, isipokuwa nakala ya 13, kuanzia Nakala ya 2 na kuendelea mpaka nakala ya 24 ni nakala zilizorudufiwa (photocopies) kutoka katika nakala halisi yaani nakala ya 1 na 13 na sio nakala halisi (original copy).

Nakala ya 3 kati ya nakala 24 ni kwa ajiri ya matumizi ya kiofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa maana ya Nakala ya 1, 2 na 13.

Fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais katika Kituo cha Kupiga Kura ambayo ni Fomu Na. 21 A iko kwenye umbo la kitabu ambacho kitakuwa na kurasa ishirini na nne (24) ambapo nakala 12 za awali zimetenganishwa na nakala 12 za mwisho kwa karatasi ngumu (separator). Nakala 12 za mwisho zinaanzia ukrasa wa 13 mpaka ukrusa wa 24 yaani ni kuanzia nakala ya 13 na kuendelea mpaka nakala ya 24.

Karatasi za Fomu Na. 21 A zimetayarishwa katika namna ambayo inawezesha kuandika na kutoa nakala rudufu (photocopies) bila kuweka karatasi ya kaboni (Carbon Papers) yaani ni "Self copying".

Hivyo basi, kila kituo cha kupiga kura kinatakiwa kuwa na nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais (Form 21 A ) zisizopungua Nakala 24 , basi kwa kuwa wagombea Urais ni watu 15 ambao watapewa nakala 15 za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais na Tume ya Taifa ya Uchaguzi itapewa nakala 3 za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi Rais, hivyo, zitabaki nakala 6 za fomu za matokea ya uchaguzi wa Rais za ziada kwa ajiri ya mawakala wa wagombea Urais ambazo hazitatumika.

Kutokana na uchambuzi wa hapo juu basi kisheria lazima zitakuwepo nakala 24 za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais katika Kituo cha Kupiga Kura ambazo zinatosha kabisa kuwapatia mawakala wote 15 wa wagombea Urais 15 wote katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.


B. UTOSHELEVU WA NAKALA ZA FOMU ZA MATOKEO YA UCHAGUZI WA MBUNGE NA DIWANI.

(a) Nakala za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Mbunge.


Utaratibu na masharti ya kisheria yanayotumika katika kutoa nakala za fomu za matokeo uchaguzi wa Rais kwa mawakala wa wagombea Urais katika Kituo cha Kupiga Kura unafanana karibu kwa kila kitu na utaratibu na masharti yanayotumika katika kutoa nakala za fomu za matokeo uchaguzi wa wabunge kwa mawakala wa wagombea ubunge na sheria inayotumika ni moja.

Hivyo basi, kutakuwepo na nakala 24 za fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa mbunge kwenye kila Kituo cha Kupiga Kura. Kati ya nakala 24 za Matokeo ya Uchaguzi wa mbunge, nakala 21 zitakuwa kwa ajiri ya kuwapatia mawakala wa wagombea ubunge katika Jimbo la Uchaguzi husika. Na nakala 3 zitakuwa kwa ajiri ya matumizi ya kiofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambapo nakala ya 1 ni ya Msimamizi wa Uchaguzi kwa ajiri ya kujumlishia matokeo ya mbunge ngazi ya jimbo na Nakala ya pili ni kwa ajiri ya kubandika ukutani kuwataarifu wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla matokeo ya uchaguzi wa mbunge na Nakala ya 13 ni kwa ajiri ya matumizi ya kiofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Hatahivyo, nakala za matokeo ya uchaguzi wa mbunge katika Kituo cha Kupiga Kura zitakuwa kwenye Fomu Na. 21 B.

(b) Nakala za Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Diwani.

Kwenye uchaguzi wa diwani sheria zinazotumika katika mchakato wa kutoa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa diwani katika Kituo cha Kupiga Kura kwa upande moja ni tofauti na sheria zinazotumika kwenye Uchaguzi Rais na mbunge kwa upande mwingine isipokuwa Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020 na Melekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020 ambayo yatumika katika uchaguzi wa madiwani pamoja na Uchaguzi wa Rais na wabunge.

Sheria zinazotumika kwa upande wa uchaguzi wa udiwani katika kutoka nakala za matokeo ya uchaguzi wa diwani ni hizi zifuatazo;

(i) Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292

(ii) Kanuni ya Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani, 2020

(iii) Aya ya 9.19 ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020.

(vi) Aya ya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020

Hatahivyo, pamoja na utofauti wa sheria bado utaratibu na masharti ya kisheria yanayotumika katika kutoa nakala za fomu za matokeo uchaguzi wa diwani kwa mawakala katika Kituo cha Kupiga Kura kwa upande mmoja unafanana karibu kwa kila kitu na utaratibu na masharti ya kisheria yanayotumika kwa wagombea wa nafasi ya Rais na nafasi ya mbunge kwa upande mwingine.

Isipokuwa nakala za matokeo ya uchaguzi wa diwani katika Kituo cha Kupiga Kura yanakuwa kwenye Fomu 21 C.


SEHEMU 4: NI LAZIMA MAWAKALA KUPATIWA NAKALA YA MATOKEO YA UCHAGUZI WA RAIS.

Kisheria ni lazima Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura na Msimamizi wa Uchaguzi ampatie kila wakala wa mgombea Urais nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais ambayo ni Fomu Na. 21 A kwa sababu nne zifuataza;

(1) Masharti ya Kifungu cha 79 A (1) (e) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 yanaelekeza kwa lazima kwamba iwapo kuna nakala za kutosha za fomu za matokeo ya Rais basi ni "lazima" Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ampatie kila wakala wa mgombea Urais nakala ya fomu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais ya Kituo cha Kupiga Kura.

(2) Aya ya 9 (19) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, 2020 na Aya ya 3 (8) ya Maelekezo ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura, 2020 zinaelekeza kwa lazima kuwa kila Kituo cha Kupiga Kura lazima kiwe na Kitabu cha Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais chenye "nakala 24" za fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ( Fomu Na. 21 A ) na kati ya nakala 24 tajwa hapo juu, nakala 21 ni kwa ajiri kuwapatia mawakala wa wagombea Urais ili wazipeleke kwa wagombea Urais na vyama vyao vya siasa ambavyo wanawakilisha katika Kituo cha Kupiga Kura.

(3) Kwa kuwa kisheria lazima ziwepo nakala 21 za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais kwa ajiri ya kuwapatia mawakala wa wagombea Urais ili wazipeleke kwa wagombea Urais na vyama vyao vya siasa basi kutakuwepo na nakala za kutosha kuwapatia mawakala 15 wa wagombea Urais 15 ambao wameteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea nafasi ya Rais katika uchaguzi mkuu wa 2020.

(4) Kwa kuwa kutakuwepo na nakala 21 za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais ambazo zinatosha kuwapatia mawakala 15 wa wagombea Urais 15 basi Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura lazima wawapatie nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais mawakala wote wa wagombea Urais kama inavyoelekezwa kwa lazima na masharti ya Kifungu cha 79 A (1) (e) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 kwamba iwapo kuna nakala za kutosha "lazima" Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura awapatie wakala wote wa wagombea Urais nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais.

(5) Kifungu cha 35 F (5) na 81 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343 kinaelekeza kwa lazima kwamba lazima Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo la Uchaguzi kumpatia mgombea Urais na Ubunge au wakala wake nakala ya Fomu ya Matokeo ya uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 21 A) na Mbunge (Fomu Na. 21 B) ya kila Kituo cha Kupiga Kura ambayo imejazwa "Sehemu B" na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kufanya uamuzi wa kura zenye mgogoro kutoka Kituo cha Kupiga Kura.

Pia, Kisheria ni lazima Msimamizi wa Kituo cha Kupiga Kura ampatie kila wakala wa mgombea Ubunge na udiwani nakala ya matokeo ya uchaguzi wa mbunge na diwani ambayo ni Fomu Na. 21 A na Fomu Na. 21 C mtawalia (respectively) kwa sababu tano (5) ambazo zimetajwa hapo juu kwa kufanya mabadiliko muhimu yanayotakiwa hapo juu (mutatis mutandis).


SEHEMU 5: HITIMISHO.

Wagombea wa nafasi ya Urais, ubunge na udiwani wana haki ya kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi katika ngazi zote za kiuchaguzi kuanzia ngazi ya kituo cha kupiga kura, ngazi ya Kata, ngazi na Jimbo la Uchaguzi mpaka ngazi ya Taifa kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Hivyo basi, ni raia yangu kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi pamoja na Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura kuheshimu sheria za Uchaguzi za nchi hii kwa kuwapatia Wagombea Urais, ubunge na udiwani au mawakala wao haki yao ya kisheria ya kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi Rais, Mbunge na Diwani katika ngazi zote za kiuchaguzi ili kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi Huru na wa Haki ambao una uwazi na unakagulika, unadhibitishika, unawajibika, sahihi na salama.

Kutoa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, wabunge na Madiwani kwa wagombea au mawakala wa wagombea katika Kituo cha Kupiga Kura na katika vituo vya kujumlisha matokeo ya uchaguzi katika ngazi ya Kata, Jimbo la Uchaguzi na ngazi ya Taifa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi utaondoa kwa sehemu kubwa tuhuma za wizi wa kura na tuhuma za hujuma za Uchaguzi Mkuu na kufanya matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2020 kuwa ya kuaminika, kuheshimike na kukubalika kwa wagombea wote, vyama vyote vya Siasa, wapiga kura wote, watazamaji wa ndani na wa kimataifa wote na wadau wote wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Imeandikwa na Matojo M. Cosatta, (Senior JF Member).
 
NEC ya CCM inasema si LAZIMA wakala kumpatia nakala....anaweza kupatiwa tu kama nakala zitatosha!!

Mmeona janja hiyo ....hapo kuna gepu la wizi... kwamba hata ujumlishaji wa kichama wa kura hauwezi kufanyika.

Soma mpaka mwisho utangundua kuwa kisheria ni lazima kuwapatia wagombea au mawakala wao nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi katika ngazi zote.
 
Soma mpaka mwisho utangundua kuwa kisheria ni lazima kuwapatia wagombea au mawakala wao nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi katika ngazi zote.
ni kweli wote tunajua hilo, ila bila kusisitiza hili, uhuni ni lazima utafanyika vituoni. Mkuu CCM hii unafikiri inaogopa sheria? angalia tu namna wagombea walivyoenguliwa kuhuni huni wakati sheria zipo wazi kabisa.
 
ni kweli wote tunajua hilo, ila bila kusisitiza hili, uhuni ni lazima utafanyika vituoni. Mkuu CCM hii unafikiri inaogopa sheria? angalia tu namna wagombea walivyoenguliwa kuhuni huni wakati sheria zipo wazi kabisa.

Kwenye eneo la mawakala kupewa nakala za fomu za matokeo katika vituo vya kupiga kura lina utata mkubwa sana wa kisheria ndo maana nimeamua kuandikia eneo hili ilikuondoa utata huu na kuwafanya wadau wote kuwa na uelewa wa pamoja (common understanding) kuhusu swala hili.
 
NEC ya CCM inasema si LAZIMA wakala kumpatia nakala....anaweza kupatiwa tu kama nakala zitatosha!!

Mmeona janja hiyo ....hapo kuna gepu la wizi... kwamba hata ujumlishaji wa kichama wa kura hauwezi kufanyika.

Kuna haja ya kwenda Mahakamani kupata tafsiri sahihi ya sheria.
 
Mkuu asante kwa maelezo yaliyoshiba, lakini najiuliza hakukuwa na njia rahisi ya kusema kila mhusika anatakiwa apatiwe copy husika. Hii ya kama zinatosha naona inatakiwa kutuchanganya sisi tusiojua haya mambo ya sheria na kuwanyima baadhi ya ma-ajenti hizo fomu.

Kwenye eneo la mawakala kupewa nakala za fomu za matokeo katika vituo vya kupiga kura lina utata mkubwa sana wa kisheria ndo maana nimeamua kuandikia eneo hili ilikuondoa utata huu na kuwafanya wadau wote kuwa na uelewa wa pamoja (common understanding) kuhusu swala hili.
 
Nani asiyejua kwamba CCM ni vibaka wazoefu wa kura? watanzania wote tunalifahami hilo..

Ongopa sana mwizi anatumia visheria vyake alivyotunga yeye mwenyewe!!

Mwaka huu ni bampa kwa bampa!! Weka wali weka mchuzi..weka ugoko weka chuma!!
 
Ndo maana nimeamua kutoa elimu ya sheria za Uchaguzi ili wagombea na mawakala wao wajue kuwa wana haki ya kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi wa Rais, mbunge na diwani.
 
Elimu iliyoambatana na uchochezi wa chuki dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sawa rudi kwa huyo aliyekutuma mwambie umeshafanya kazi uliyotumwa.
 
Ikumbukwe kwamba vyama vya Siasa ni wadau wakubwa wa NEC hushirikishwa katika utungaji wa Kanuni, Hivyo hata utolewaji wa Maoni na kupitishwa kwa kanuni hiyo ni Matokeo ya kikao cha NEC na wadau wake.

Andiko hili pamoja na mambo mengi. Lina mapungufu!!
 
Elimu iliyoambatana na uchochezi wa chuki dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sawa rudi kwa huyo aliyekutuma mwambie umeshafanya kazi uliyotumwa.

Nikuhakikushia kuwa sijatumwa na mtu bali nimeandika kwa utashi wangu na kwa hiyari yangu ni kawaida yangu kufanya uchambuzi wa maswala ya kisheria katika maeneo mbalimbali hata kabla ya uchaguzi.

Uchambuzi wangu ni wa kitaalamu na nimefanya uchambuzi wa sheria tu bila kutaja jina la mtu au jina la chama cha siasa ni uchambuzi wa maswala ya sheria na sio uchambuzi wa watu au vyama vya siasa.

Hakuna popote kwenye makala yangu nimeisema tume ya Uchaguzi kwa ubaya kwa lengo la kuleta chuki au uchochozi.

Makala yangu ililenga kutanua uelewa wa wadau wa uchaguzi kuhusu swala hili la wagombea na mawakala wao kupatiwa nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi ili kuwa na uelewa wa pamoja na unaofafana kuhusu swala hili na wadau hawa ni pamoja na wagombea, mawakala wa wagombea, wapiga kura, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Vituo vya Kupiga Kura na Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kama kweli unadhamila njema utakuwa umenielewa.
 
Ikumbukwe kwamba vyama vya Siasa ni wadau wakubwa wa NEC hushirikishwa katika utungaji wa Kanuni, Hivyo hata utolewaji wa Maoni na kupitishwa kwa kanuni hiyo ni Matokeo ya kikao cha NEC na wadau wake.

Andiko hili pamoja na mambo mengi. Lina mapungufu!!

Hili ni andiko au makala ya kitaalamu (scholarly article) ambayo ni matokeo ya utafiti wa kisheria, hivyo, kusema tu kuna mapungufu bila kutaja bayana mapungufu hayo na bila kuja na utafiti mwingine wa kisheria kupinga utafiti wangu kitaalumu na kitaaluma ni upuuzi wa kiwango cha juu kabisa.
 
Soma mpaka mwisho utangundua kuwa kisheria ni lazima kuwapatia wagombea au mawakala wao nakala za fomu za matokeo ya uchaguzi katika ngazi zote.
Kiongozi hapo tayari walisha chakachua hata hizo sheria zenyewe. Si unaona zinavyopingana. Matokeo yake vyama vitasimamia vifungu kudai nakala na wasimamizi watasimamia humo humo kutotoa nakala. Mwisho wa siku atakae pewa ama atakae nyimwa utaambiwa wote wako sahihi kwa mujibu wa sheria.
 
Ikumbukwe kwamba vyama vya Siasa ni wadau wakubwa wa NEC hushirikishwa katika utungaji wa Kanuni, Hivyo hata utolewaji wa Maoni na kupitishwa kwa kanuni hiyo ni Matokeo ya kikao cha NEC na wadau wake.

Andiko hili pamoja na mambo mengi. Lina mapungufu!!
Kuna maccm kama Polepole yana DHAMBI. Unafunga MIRIJA ya UCHUMI Nchi nzima. Wananchi wanalia NJA.

Wakisema vyuma vimekaza eti unawafunga badala kufungua mirija ya Uchumi.

Huu ujinga wote unafanywa ili uweze kuwaDHIBITI siku ya UCHAGUZI kwa kuwapa buku mbili wajaze viwanja.
 
Back
Top Bottom