Kumekuwepo na madai kuwa ulaji wa ugali hudumaza akili. Madai haya yana ukweli kiasi gani?
- Tunachokijua
- Ugali ni chakula kinachotumika sana Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa mujibu wa utafiti wa Onu Okpa et al (2019), “Sub-Saharan African Maize-Based Foods - Processing Practices, Challenges and Opportunities” mahindi huchangia 30% ya nishati za vyakula wanavyotumia watu wa ukanda huu kila siku.
Kwa mujibu wa utafiti huu, kila mtu anayepatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara hutumia wastani wa kati ya gramu 52-450 za mahindi kwa siku. Ni chanzo kikuu cha ugali unaotumika kila siku kwenye nchi hizi. Kwa Tanzania, 64% ya wananchi wake hula chakula hiki walau mara 5-7 kwa wiki.
Takwimu hizi zinaonesha kuwa ugali ni chakula kinachotumika sana, pengine kuliko aina nyingine za vyakula. Baadhi ya watu huutengeneza kwa kutumia unga wa mhogo, mtama, ulezi pamoja na aina zingine za nafaka.
Bila kujali tofauti ndogo za mgawanyiko wa virutubisho, nafaka zote husifika kwa kuwa na kiasi kikubwa cha nishati na wanga, pia kiasi kidogo cha madini na vitamini muhimu kwa afya.
Kuhusishwa na udumavu wa akili
Kitaalamu, udumavu wa akili husababishwa mambo mengi ikiwemo baadhi ya changamoto za kijenetiki mfano Down’s syndrome, kukosa hewa ya kutosha wakati wa kuzaliwa, maambukizi makali ya homa ya uti wa mgongo, utapiamlo, matumizi ya baadhi ya madawa na pombe wakati wa ujauzito pamoja na sababu zingine siziso wazi sana.
Kwa kurejea mgawanyiko wa virutubusho vinavyopatikana kwenye nafaka zinazotumika kutengenezea ugali, hakuna uhusiano wa moja kwa moja unaoweza kutajwa, au pia kuhusishwa na kusababisha udumavu wa akili kwa watu. Virutubisho na madini yake havina athari hasi kwenye afya ya ubongo.
Pia, JamiiForums imezungumza na wataalamu wa lishe ambao wamethibitisha kuwa chakula hiki ni salama, hakiwezi kusababisha madhara tajwa.
Hivyo, JamiiForums imebaini kuwa madai haya hayana ukweli uliojengwa kwa hoja za kisayansi. Ni uzushi usio na uthibitisho wa tafiti au takwimu.