SoC03 Uhalisia katika utekelezaji wa dhana ya Utawala Bora nchini Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition
Nov 15, 2019
35
113
Dhana ya utawala bora
Utawala bora ni dhana jumuishi inayohusisha ufanisi wa kiutendaji katika kusimamia raslimali za umma bila kuathiri misingi ya utawala wa sheria na upatikanaji wa haki za binadamu kwa watu wote ndani ya jamii. Utawala bora ndio mhimili mkuu wa maendeleo ya nchi yetu. Hii ni katika yanja za kisiasa, kiuchumi na hata kijamii pia. Bila utawala bora nchi haiwezi kutawalika, na hata ikitawalika basi haki za wananchi wengi zitakuwa zinadidimizwa.

Nchini Tanzania, dhana ya utawala bora haijaanza leo bali imeanza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika. Tanganyika ilikuwa na wanaharakati wengi ambao walitetea dhana ya utawala bora ili waweze kujitoa kwenye mikono dharimu ya mkoloni (muingereza). Watanzania wengi kwa sasa tunapokuwa tunazungumzia utawala bora tunamtaja Hayati Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama mwanzilishi na mpiganaji pekee dhidi ya wakoloni, La Hashaa! asingeweza kupigana vita hivyo pekee yake bila kuwa na msaada wa kando. Historia ya utawala bora nchini Tanzania imebebwa na mashujaa wengi, hivyo basi hatuna budi kuuenzi utawala bora kama tunu ya taifa letu.

Wanawake nao hawawezi kuachwa nyuma katika historia ya utawala bora hapa nchini kabla na hata baada ya uhuru. Historia ya utawala bora Tanganyika ambayo ni Tanzania ya sasa haitakamilika bila kugusia mchango wa wanawake waliosimama imara katika kupigania uhuru wa taifa letu na kurejesha utawala bora mikononi mwa watanganyika ambao ni watanzania kwasasa. Wanawake hao ni Lucy Lameck Somi na Bibi Titi Mohamed ambao licha ya kupigania uhuru pia walijenga heshima katika mfumo wa siasa za nchi yetu ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mfumo dume ambapo matunda yake tunayaona kwasasa kupitia uwepo wa Rais wetu wa awamu ya sita mwenye jinsia ya kike Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan. Kiufupi, watanzania tunayo mambo mengi ya kujivunia kihistoria katika dhana nzima ya utawala bora, na ni wajibu wa kila mtumishi wa sekta ya umma, sekta binafsi na hata asasi za kiraia kuhakikisha anailinda na kuienzi tunu hii ya utawala bora kwa vizazi na vizazi.

Msingi wa kisheria wa utawala bora nchini
Nchini Tanzania katiba ya nchi ndiyo sheria mama ya sheria zote, na sheria yoyote inayokinzana na katiba ya nchi kwa namna yoyote sheria hiyo huamuriwa kuwa batili. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 chini ya ibara ya 129 imeanzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ambapo majukumu yake yamewekwa bayana chini ya ibara 130(1) ya katiba hii. Kwa mujibu wa katiba, tume hii imepewa majukumu kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, kufanya utafiti, kutoa na kueneza nchini elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora, kutoa ushauri kwa serikali na vyombo vingine vya umma na vya sekta ya binafsi kuhusu haki za binadamu na utawala bora, kama ikibidi, kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu au kurekebisha haki inayotokana na uvunjwaji huo wa haki za binadamu, au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Ni vigumu sana kuunga mkono hoja ya kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inafanya kazi ipasavyo kwa mujibu wa katiba na kwa mujibu wa sheria nyingine za bunge. Tume hii ipo kinadharia zaidi na utendaji kazi wake ni dhaifu ikilinganishwa na matakwa pamoja na uhitaji halisia uliopo uraiani kwa watanzania. Ni watanzania wachache sana wanaojua uwepo wa tume hii, na wengi kati ya hao wachache ni wasomi. Wananchi wengi wamekuwa wakipata shida sana katika upande wa utawala lakini wengi wao wamekuwa wakiishia kujilaumu na kuumia bila kujua wazi ni wapi waanzie katika kudai haki zao. Moja kati ya majukumu ya tume ya haki za binadamu na utawala bora ni kuhakikisha mwananchi anapata elimu jambo ambalo limekuwa halifanyiki kwa kiasi cha kuridhisha na hivyo kupelekea wananchi wengi kudhurumiwa haki zao.

Wahenga walishawahi kusema "akukanyagae mguu huwa ni bahati mbaya, lakini akukanyagae nyonga huyo kadhamiria kukuangusha." Kwa mantiki hiyo, ukimya wa serikali katika kutolea ufumbuzi matatizo yatokanayo na utawala mbovu hutoa picha ya wazi kuwa kipaumbele cha watawala ni nchi na siyo wananchi. Hilo haliwezi kuvumiliwa ilihali tunajua demokrasia, uwazi na uwajibikaji ndizo nguzo za utawala bora katika taifa lolote duniani. Viongozi wanapaswa kulisimamia sana kwa kuwa wanayo dhamana ya kuwahudumia watanzania wote kwa upendo na usawa bila kusahau kuwa mishahara yao inatokana na kodi za wananchi hao hao. Taasisi za umma na za sekta binafsi zifuatiliwe ili kubaini ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na hatimaye kupunguza kero kwa baadhi ya watumishi pamoja na wananchi.

Hali halisi ya utawala nchini
Licha ya kuwepo kwa sheria mbalimbali zinazosimamia masuala mazima ya utawala bora hapa nchini, hii ndiyo hali halisi ambayo watanzania wanaipitia kwasasa;-

Ubadhirifu
Hili limewekwa wazi kutokana na uthibitisho wa taarifa ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma. Hii hutokana na maamuzi mabaya ya viongozi wenye mamlaka ya kusimamia fedha katika ngazi ya serikali kuu hadi huku chini kwenye halmashauri zetu, hali inayopelekea wananchi kukosa imani na serikali yao. Katika hilo inakuwa vigumu kutaja uwepo wa utawala bora.

Rushwa
Vitendo hivi vinashuhudiwa katika halmashauri nyingi nchini hususani katika utoaji wa huduma za kijamii. Rushwa imekuwa ikitolewa waziwazi bila hofu na matokeo yake wananchi hukosa haki zao na hivyo kuathiri maana na dhana nzima ya utawala bora nchini.

Kutowajibika
Siku zote vitendo huongea zaidi kuliko maneno. Viongozi wengi wamekuwa wakiongea zaidi bila kutekeleza ahadi zao kwa wananchi na matokeo yake uwakilishi wao unakuwa mbovu na usio na mvuto wala tija na hivyo kuathiri dhana nzima ya utawala bora. Kiongozi mwajibikaji hujenga jamii shupavu na kinyume chake ni mzigo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Hitimisho
Utawala bora nchini utajengwa na nguvu ya hoja na siyo hoja ya nguvu, kupingana bila kupigana, kujikosoa na kukosoana bila kuleana pamoja na kujengeana uzalendo wa kweli wenye kuijali Tanzania na watanzania wote. Kupitia hilo hakika tutakuwa na taifa safi lenye maono chanya, maendeleo, mshikamano, upendo na amani.
 
Back
Top Bottom