Tusome sanaa ya vita (The art of war) cha Sun Tzu

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Jan 31, 2021
8,459
14,939
UTANGULIZI

Toka kilipoandikwa mwishoni mwa karne ya 6KWK, sanaa ya vita ni moja ya vitabu vya kale na maarufu sana kuhusu mbinu za kivita. Kitabu hiki kiliandikwa na Sun Tzu, huyu alikuwa alikuwa jenerali na mwanazuoni wa ufalme wa Wu. Mbinu zilizomo kwenye kitabu hiki hazitumiki tu jeshini bali kwenye nyanja nyingine kama biashara na michezo.

Sun Tzu alikuwa ni mwenyeji wa nchi ya Chi. Kitabu chake, sanaa ya vita kilifanya mfalme wa Wu, Ho Lu amtafute. Ho Lu akamwambia Sun Tzu "nimesoma sura 13 za kitabu chako kwa makini sana. Naweza kufanya jaribio ili kuona iwapo nadharia yako ya kuongoza jeshi inafanya kazi?".
Sun Tzu akajibu "bila shaka"
Ho Lu akauliza" naweza jaribu kwa kutumia wanawake".
Sun Tzu akajibu "unaweza"

Wakaletwa masuria 180 wa mfalme. Sun Tzu akawagawa katika makundi mawili. Akateua masuria wawili wanaopendwa sana na mfalme kuwa wakuu wa kila kikosi. Akawapa masuria wote mikuki kisha akasema "nadhani wote mnajua tofauti ya mbele na nyuma, kushoto na kulia"
Wale masuria wakajibu "ndiyo"

Sun Tzu akaendelea, "Nikisema macho mbele mnatakiwa kuangalia mbele kwa kunyooka. Nikisema kushoto geuka mnatakiwa kugeuka na kuangalia kushoto. Nikisema kulia geuka, mnatakiwa kugeuka na kuangalia kulia. Nikisema nyuma geuka, mnatakiwa kugeuka na kuangalia nyuma". Akawauliza kama wameelewa, wakasema wameelewa.

Baada ya maelezo hayo akaanza kuwaongoza kwenye mazoezi ya kijeshi, ngoma ikapigwa kisha akasema " kulia geuka". Wale masuria badala ya kugeuka kulia wakaangua kicheko. Sun Tzu akasema , "iwapo amri haileweki vizuri na haiko wazi, jenerali ndiye anatakiwa kulaumiwa". Akawaeleza tena wanachotakiwa kufanya na kuanza kuwaongoza tena "kushoto geuka", masuria wakaangua kicheko tena. Sun Tzu akasema. "Iwapo amri haiko wazi na haieleweki ni kosa la jenerali. Lakini ikiwa amri iko wazi na inaeleweka lakini wanajeshi hawaitii kosa ni la maofisa wao".
Baada ya kusema hayo akaamrisha wale masuria wawili waliokuwa viongozi wakatwe vichwa.

Mfalme wa Wu alikuwa anaangalia mambo yote hayo kutoka kwenye kibaraza cha juu. Alipoona masuria wake wapendwa wanataka kuuwawa akaingiwa na kiwewe. Akatuma ujumbe kwa Sun Tzu ukisema " sasa tumeridhika na uwezo wako kama jenerali na uwezo wako wa kuongoza jeshi. Ukiua hao masuria siku yetu itaharibika, tunaomba wasiuwawe".

Sun Tzu akajibu. "Baada ya kupewa jeshi la mfalme, kuna amri za mfalme sipaswi kuzitii". Akawachinja wale masuria wawili na kuchagua wengine wawili kuwa mbadala wao. Ngoma ikapigwa na akaanza kuwaongoza tena kwenye mazoezi.

Wale masuria walifanya kama walivyoelekezwa. Waligeuka kulia, kushoto, walisogea mbele na kurudi nyuma, walipiga magoti na kusimama kwa usahihi mkubwa.
Sun Tzu akatuma ujumbe kwa mfalme.

"Wanajeshi wako wako tayari na wana nidhamu, unaweza kuwakagua. Unaweza kuwatumia upendavyo. Waamrishe kupita kwenye maji na moto nao hawatakaidi".

Mfalme akajibu "Mwambieni jenerali wetu asitishe mazoezi na arudi kambini, hatuna hamu ya kuja kukagua kikosi".

Sun Tzu akasema "mfalme anapenda maneno matupu lakini hawezi kutekeleza kwa vitendo".

Kuanzia siku hiyo Ho Lu akajua kuwa Sun Tzu ndiye anajua jinsi ya kuongoza jeshi. Akamteua kuwa jenerali wa jeshi lake.
 
I: MIPANGO

1. Sun Tzu alisema: Sanaa ya vita ni muhimu sana kwa nchi.

2. Hili ni jambo la kufa na kupona, ni barabara inayoweza kuelekea kwenye usalama au kwenye kifo na uharibifu. Hivyo ni jambo linalotakiwa kuchunguzwa kwa umakini bila kupuuzwa hata kidogo.

3. Sanaa ya vita huuongozwa na vitu vitano ambavyo vinapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa iwapo utataka kuelewa mambo yanavyokwenda kwenye uwanja wa vita.

4. Mambo hayo ni.

i. Uhuru na amani.

ii. Mbingu.

iii. Sura ya nchi

iv. Kamanda

v. Mbinu na nidhamu


5,6. Sheria za maadili/amani na uhuru hufanya watu wawe pamoja au washikamane na kiongozi wao. Hufanya wamfuate hata maisha yao yakiwa hatarini.

7. Mbingu huwakilisha usiku na mchana, baridi na joto, nyakati na majira.

8. Sura ya nchi huwakilisha umbali, ukubwa na udogo wa vitu. Hatari na usalama, uwanda mpana wa vita na njia nyembamba za kupita. Uwezekano wa kufa au kupona.

9. Kamanda ni kiongozi na anatakiwa kusimama kama mtu mwenye maadili, busara, mkweli, mwenye kujali na shujaa asiyeogopa wala kuyumba.

10. Mbinu na nidhamu huhusisha kupanga jeshi kwenye vikosi, kupanga wanajeshi kwa vyeo, kurekebisha na kutengeneza barabara ambazo mahitaji ya jeshi hupita, kupanga na kuangalia matumizi ya jeshi.

11. Mambo haya matano yanatakiwa kueleweka vizuri na jenerali wa vita. Anayeyajua ataibuka mshindi vitani, asiyeyajua atashindwa.

12. Kwahiyo, ukitaka kujua uwezo wa jeshi, angalia mambo yafuatayo.

13.
i. Nchi ipi raia wake wanaishi kwa uhuru na amani.

ii. Nchi ipi ina jenerali mwenye uwezo zaidi.

iii. Nchi ipi inafaida za kidunia na kimbingu.

iv. Jeshi lipi lina nidhamu zaidi.

v. Jeshi lipi lina nguvu zaidi.

vi. Jeshi lipi ambalo lina wanajeshi na maofisa wenye mafunzo ya hali ya juu.

vii. Jeshi lipi ambalo adhabu na zawadi hutolewa vinapohitajika.

14. Kwa kuangalia haya mambo saba ninaweza kutabiri ushindi au kushindwa.

15. Jenerali atakayesikiliza ushauri wangu na kuufanyia kazi ataibuka na ushindi. Huyo ndiyo anafaa kuongoza jeshi. Jenerali ambaye hasikilizi ushauri wangu wala kuufanyia kazi huyo atashindwa vitani na wala hafai kuongoza jeshi.

16. Pamoja na kufuata ushauri wangu, inatakiwa pia kutumia fursa zote zitakazokusaidia kufikia ushindi.

17. Kwasababu kama hali zinaruhusu na kubadili mbinu kuna faida basi mtu anatakiwa kubadili mbinu.

18. Vita zote hutegemea udanganyifu.

19. Kwa hiyo. Pale tunapoweza kupigana tunatakiwa kuonekana kama hatuwezi, pale wanajeshi wanapotumika waonekane kama hawatumiki, tukiwa karibu tunatakiwa kumfanya adui aone kama tuko mbali. Tukiwa mbali tumuaminishe tupo karibu.

20. Tuweke mitego kumnasa adui, tujifanye hatujajipanga ili anase tummalize.

21. Kama adui kajipanga kila idara basi ujipange kupambana naye. Kama amekuzidi sana nguvu basi muepuke.

22. Kama mpinzani wako ni mtu wa kukasirika haraka, mchokoze. Jifanye dhaifu ili apatwe na kiburi na kujikweza.

23. Adui akiwa ametulia mchokoze asipumzike. Kama jeshi lake limeungana litawanye.

24. Mvamie sehemu ambayo hajajiandaa, tokea sehemu ambazo hatarajii.

25. Ili zikupe ushindi, mbinu hizi zinatakiwa kufanywa kwa usiri mkubwa.

26. Kwa hiyo, jenerali anayeshinda pigano hufanya mipango na hesabu kwa umakini kabla ya vita kupiganwa. Anayeshindwa vita hufanya hesabu na mipango yake bila umakini. Kwa hiyo kufanya hesabu na mipango kwa umakini huleta ushindi na kukosa umakini huleta kushindwa. Ninaweza kutabiri mshindi wa vita kwa kuangalia mipango na hesabu vilivyofanyika.
 
Nasikia kitabu hiki ni zuga, hakiiaandikwa na wachina au kuhusu Mchina ni code za shirika moja maarufu la kidinijasusi duniani na kimeandikwana wazungu tu.

Ila kikao Vzri katika mbinu za biashara
 
Nasikia kitabu hiki ni zuga, hakiiaandikwa na wachina au kuhusu Mchina ni code za shirika moja maarufu la kidinijasusi duniani na kimeandikwana wazungu tu.

Ila kikao Vzri katika mbinu za biashara
Lolote linawezekana mkuu. Lakini kihistoria wazungu walikitafsiri kwenda kwenye kiingereza mwanzoni mwa miaka ya 1900.
 
II: KUPIGANA VITA

1. Sun Tzu alisema: kwenye vita kunaweza kuwa na magari ya vita 2000, wanajeshi laki moja na vitu vya kutosha safari ya kilomita 600. Ukijumlisha na burudani kwa wanajeshi, vitu vidogovidogo kama gundi na rangi, gharama za magari ya vita na mavazi, matumizi yanaweza kufika jumla ya kilogramu 28 za fedha kwa siku. Hiyo ndiyo gharama ya kuhudumia jeshi la wanajeshi 100,000.

2. Kwahiyo, kama vita ni ya muda mrefu basi silaha zitaharibika na mori(mzuka) wa wanajeshi utapoa. Iwapo utazingira mji basi ujue utajimaliza nguvu.

3. Pia kama vita ni ya muda mrefu mali za nchi zinaweza kushindwa kuhimili matumizi.

4. Ikitokea silaha zako zimeharibika , mori umeshuka, nguvu zimepungua na hela umeishiwa, nchi zingine zinaweza kuona fursa na kukuvamia. Hakuna mtu anaweza kuepuka kushindwa katika hali kama hiyo.

5. Kwa hiyo, japo tumewahi ona watu wakiingia vitani harakaharaka na kijinga, kujipanga kwa muda mrefu kupita kiasi hakumaanishi ni akili.

6. Hakuna nchi imewahi faidika kwa kupigana vita kwa muda mrefu.

7. Ni yule tu anayeelewa madhara ya vita ndiye ataelewa namna ya kuendesha vita kwa faida.

8. Mwanajeshi mzuri ni yule asiyesababisha watu kutozwa kodi mara mbili. Ni yule ambaye haombi vifaa vya vita zaidi ya mara mbili.

9. Beba vifaa vyako vya vita kutoka nyumbani lakini mahitaji mengine chukua kwa adui wako. kwa njia hiyo jeshi lako litakuwa na chakula cha kutosha.

10. Hazina ya nchi ikiwa haina kitu husababisha gharama za jeshi kutolewa kwa michango. Kuendesha jeshi kwa michango husababisha raia kuwa maskini.

11. Kwa njia nyingine, uwepo wa jeshi karibu husababisha gharama za maisha kupanda. Kupanda kwa bei ya bidhaa husababisha wananchi kuwa maskini.

12. Raia wanapokuwa hawana kitu ile kodi wanayotozwa inakuwa kubwa sana kwa wao kuhimili.

13, 14. raia watapoteza 30% ya mali zao, nyumba zao zitabaki tupu. Wakati huohuo matumizi ya serikali kwenye kurekebisha magari yaliyoharibika, kutibu farasi, kurekebisha mavazi ya vita, mishale na pinde, mikuki na ngao, zinaweza kufika asilimia 40 ya mapato yake.

15. Kwa hiyo, jenerali mzuri ni yule ambaye anahamasisha kuchukua mali za adui. Ujazo wa toroli moja wa mali za adui ni sawa na toroli ishirini za mali yako mwenyewe.

16. Ili kuua adui, wanajeshi wanatakiwa kujazwa morali. Kuaminishwa kwamba kutakuwa na faida ya kumpiga adui, kuna zawadi watapata.

17. Kwa hiyo, kwenye mapigano ya magari vita, na magari kumi au zaidi yakatekwa basi magari hayo yanatakiwa kupewa wale waliyoyateka kwanza. Bendera zetu ziwekwe kwenye magari hayo na yatumike sambamba na magari yetu. Wanajeshi waliotekwa wanatakiwa kutunzwa vizuri.

18. Hii ni ili kuwatumia mateka kujiimarisha.

19. Kwa hiyo, kwenye vita lengo lako kuu liwe ushindi na si vita ya muda mrefu.

20. Inatakiwa kujulikana kuwa, kiongozi wa jeshi ameshikilia mustakabali wa maisha ya watu. Mtu ambaye nchi inamtegemea ili iwe na amani au iangamie.
 
III. MBINU ZA UVAMIZI.

1. Sun Tzu alisema: Kwenye vita, jambo zuri ni kuteka nchi ya adui bila kuiharibu. Kuiharibu si vyema. Vivyohivyo, ni vema kuliteka jeshi kuliko kuliangamiza.

2. Kwa hiyo, kuvamia na kumshinda adui kwenye vita zako zote siyo uhodari. Uhodari unahusisha kumteka au kuvunja upinzani wa adui bila kupigana.

3. Kwa mantiki hiyo, ujenerali mzuri nikukwamisha mipango ya adui. Njia ya pili ni kuzuia vikosi vya adui kuungana, Inayofuata ni kuvamia vikosi vya adui kwenye uwanja wa vita. Mbinu mbaya kabisa ni kuzingira miji yenye kuta.

4. Sheria ya vita ni kutozingira miji yenye ngome iwapo hilo linaweza kuepukwa. Maandalizi ya kutengeneza mashine za kuzingira na makazi yanaweza kuchukua miezi mitatu. Kuweka kifusi ukutani kwa ajili ya kupanda ukuta inaweza chukua miezi mitatu mingine.

5. Jenerali asiye na subira anaweza kuamrisha wanajeshi wake wavamie mji kama kundi la siafu. Hili linaweza sababisha theluthi moja ya wanajeshi wake kuangamia na bado mji ukawa bado haujatekwa. Madhara kama hayo yanaweza kutokea ukizingira mji.

6. Kwa hiyo, kiongozi hodari anamdhibiti adui bila hata kupigana. Anateka miji yao bila kuizingira na anaangusha falme zao bila ya kupigana kwa muda mrefu.

7. Bila jeshi lake kuathirika atapambana na kuangusha falme. Bila kupoteza wanajeshi atapata ushindi. Hii ndiyo njia ya kuvamia kwa mbinu.

8. Hii ni sheria ya vita, kama jeshi letu ni mara kumi ya adui, tutamzingira. Kama ni mara tano ya adui basi tutamvamia. Kama ni mara mbili yake basi tutagawanya jeshi letu mara mbili.

9. Kama jeshi letu lipo sawa na jeshi la adui tunaweza kupambana naye Lakini tukiwa pungufu kidogo tunaweza kumuepuka. Tukiwa wachache sana tutamkimbia tukiweza.

10. Japo jeshi dogo linaweza kupigana kishujaa na jeshi kubwa, mwisho wa siku litashindwa na jeshi kubwa.

11. Kwa hiyo, jenerali ni kama ukuta wa ulinzi wa nchi. Ukuta ukiwa imara sehemu zote za nchi zitakuwa salama. Ukuta ukiwa dhaifu nchi itakuwa dhaifu.

12. Kuna njia tatu ambazo mtawala anaweza kusababisha jeshi likashindwa vitani.

13.
i. Kuamuru jeshi lisonge mbele au lirudi nyuma bila kujua kwamba jeshi haliwezi kumtii. Hii ni kukwamisha jeshi.


14. ii. Kujaribu kuongoza jeshi kama vile anavyoongoza nchi bila kujua hali halisi ya jeshi. Hili linaweza kuchanganya wanajeshi.

15. iii. Kwa kushindwa kuweka watu sahihi kuongoza jeshi lake. Kwa kutojua kuwa vitani kila hali inahitaji aina fulani ya ofisa, ataharibu imani ya wanajeshi.

16. Jeshi lisipokuwa na utulivu na lisipojua wa kumuamini matatizo lazima yatatokea kutoka kwa machifu wanaounda ufalme. Hili huleta machafuko jeshini na kusababisha kushindwa vita.

17. Kwa hiyo, tumejua kuwa kuna vitu vitano muhimu kwa ushindi.

i. Atashinda yule anayejua wakati wa kupigana na wakati wa kutopigana.

ii. Atashinda yule anayejua jinsi ya kupigana na jeshi bora na jeshi dhaifu.

iii. Atashinda yule ambaye wanajeshi wake wa vyeo vyote wana mori uleule.

iv. Atashinda yule ambaye amejitayarisha, akisubiri kumvamia adui ambaye hajajitayarisha.

v. Atashinda yule ambaye jeshi lake halitaingiliwa na watawala.

18. Hivyo kuna usemi, ukimjua adui wako na ukijijua wewe mwenyewe huna haja ya kuogopa mapambano mia moja. Ukijijua lakini usimjue adui, kwa kila ushindi mmoja utakaopata, utashindwa mmoja. Kama hujijui wewe mwenyewe na humjui adui wako, utashindwa kwenye kila pambano.
 
Tuendelee na sura ya nne.


IV: KUVIZIANA

1. Sun Tzu alisema: Wapiganaji hodari wa kale walijilinda kwanza dhidi ya kupigwa na kisha wakasubiria fursa ya kumshinda adui.

2. Suala la kujilinda tusipigwe liko mikononi mwetu lakini fursa ya kumpiga adui na kumshinda hutolewa na adui mwenyewe.

3. Kwa hiyo, mpiganaji mzuri anaweza kujilinda asipigwe na kushindwa lakini hawezi kuwa na uhakika wa kumshinda adui.

4. Hivyo kuna usemi; mtu anaweza jua jinsi ya kushinda vita bila kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

5. Usalama dhidi ya kupigwa na kushindwa unahusisha mbinu za kujilinda. Uwezo wa kumpiga adui unahusisha mbinu za kuvamia.

6. Kujilinda kunaonyesha uwezo mdogo. Kuvamia kunaonyesha uwezo mkubwa sana.

7. Jenerali mwenye ujuzi wa kujilinda hujificha kwenye sehemu za siri na zilizo ngumu kufikiwa. Yule mwenye ujuzi wa kuvamia hutokea sehemu za juu kabisa za mbingu. Kwahiyo upande mmoja tuna uwezo wa kujilinda na ule mwingine tuna ushindi ulio kamili.

8. Kuona ushindi ambao kila mtu ameuona siyo uhodari.

9. Wala siyo uhodari unapovamia na kushinda na kisha nchi yote ikaona ulivyoshinda na kusema "hongera sana, kazi nzuri"

10. Kunyanyua unyoya si ishara ya nguvu, kuona jua na mwezi siyo ishara ya uwezo mzuri wa kuona. Kusikia muungurumo wa radi siyo ishara ya uwezo mzuri wa kusikia.

11. Wale ambao zamani waliitwa wapiganaji hodari hawakushinda tu vita bali walishinda kirahisi.

12. Ushindi wao haukuwaletea sifa ya busara wala ushujaa.

13. Walishinda vita zao bila kufanya makosa. Kutofanya makosa ndiko huhakikisha ushindi kupatikana, kunamaanisha kumshinda adui aliyekwisha shindwa.

14. Kwa hiyo, mpiganaji hodari hujiweka kwenye nafasi ambayo haitawezekana kumpiga. Pia hapotezi nafasi yoyote ile ya kumpiga adui.

15. Kwenye vita, washindi hupata kwanza ushindi ndipo huenda kupigana . Yule anayeshindwa, hupigana kwanza ndipo hutafuta ushindi.

16. Kiongozi mzuri hutilia mkazo suala la maadili na haki kwanza ndipo anasimamia nidhamu kikamilifu. Nguvu za kuongoza kwenye ushindi zipo chini yake.

19. Ukilinganisha jeshi la ushindi na na lile la kushindwa ni sawa na kuweka jiwe kwenye mzani dhidi ya punje moja ya nafaka.

20. Mwendo wa jeshi la ushindi ni sawa na maji yanayoruka toka kwenye kisima kipya.
 
V. NGUVU

1. Sun Tzu alisema: Kanuni za kuongoza jeshi kubwa ni sawa na zile za kuongoza jeshi dogo. Ni suala la kugawanya jeshi kwenye makundi madogomadogo.

2. Kupigana ukiwa na jeshi kubwa hakuna tofauti na kupigana ukiwa na jeshi dogo. Ni suala la kuweka matumizi ya alama na ishara.

3. Kuhakikisha jeshi lako linasimama dhidi ya adui bila kutetereka, inatakiwa kujua jinsi ya kujipanga na kushambulia kwa mbinu zinazoweza kumchanganya adui.

4. Nguvu ya jeshi lako inatakiwa kuwa kama kuponda yai kwa jiwe la kusagia. Hii inatokana na sayansi ya kujua sehemu imara na dhaifu.

5. Kwenye mapigano yote, mbinu za moja kwa moja zinatumika kwenye mapambano ya uso kwa uso. Mbinu zisizo za moja kwa moja zinahitajika ili kukuletea ushindi.

6. Mbinu zisizo za moja kwa moja zikitumika ipasavyo ni nyingi kama mbingu na ardhi. Hazina mwisho kama mtiririko wa mito na vijito. Kama vile jua na mwezi vinavyozama na kuibuka tena. Kama vile majira ya mwaka ambavyo huisha na kuanza tena.

7. Hakuna zaidi ya nota tano za muziki lakini muunganiko wake unaweza kutoa ala zisizohesabika.

8. Rangi za msingi hazizidi tano(bluu, njano, nyekundu, nyeusi na nyeupe) lakini muunganiko wake hutokeza rangi zisizo na idadi.

9. Hakuna ladha zaidi ya tano( chungu, tamu,chachu, chungu na chumvi) lakini muunganiko wake huleta ladha zisizo na idadi.

10. Kwenye vita hakuna mbinu zaidi ya mbili za kupigana (Mbinu za moja kwa moja na mbinu zisizo za moja kwa moja) lakini muunganiko wa mbinu hizi hutokeza mbinu zisizo na idadi.

11. Mbinu za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja hutegemeana. Ni kama kuzunguka duara, huwezi kufika mwisho. Zinaweza kuunganishwa na kutokeza mbinu nyingi sana.

12. Jeshi likianza kupigana liwe kama mafuriko. Maji ya mafuriko hukusanya nguvu na kwa wakati muafaka hushuka kwa nguvu inayoweza kubiringisha hata mawe makubwa.

13. Maamuzi yanatakiwa yawe kama kushuka kwa kipanga, hushuka kwa wakati muafaka na kuvunja mgongo wa windo lake.

14. kwa hiyo mpiganaji mzuri huanza polepole na kwa wakati muafaka hushambulia kwa kasi na nguvu kubwa.

15. Nguvu inafananishwa na kuvutwa kwa upinde na maamuzi kama kuachiliwa kwa mshale.

16. Katikati ya vurugu za vita kunaweza kuonekana kama hakuna mpangilio lakini kunakuwa (kunatakiwa kuwe) na mpangilio. Katikati ya vurugu na machafuko jeshi lako linaweza onekana halina mpangilio lakini halitaweza kushindwa.

17. Kujifanya hamna mpangilio kunaonyesha nidhamu ya hali ya juu. Kujifanya mnaogopa kunaonyesha ushujaa wa hali ya juu. Kujifanya dhaifu kunaonyesha nguvu.

18. Kuficha jinsi mlivyojipanga kwa kujifanya hamna mpangilio ni suala la kugawanya jeshi tu. Kuficha ushujaa kwa kuonyesha uoga ni mbinu ya kuvizia, kuficha nguvu kwa kujifanya dhaifu ni kuweka chambo.

19. Kwa hiyo, mpiganaji mjanja atakuwa na muonekano wa kudanganya ambao adui atajiingiza kichwakichwa. Atakubali kupoteza kitu ambacho adui atakivamia kwa pupa.

20. Kwa kuweka chambo atamfanya adui azifuatilie. Hapo akiwa na wanajeshi wake atajificha amvizie.

21. Mpiganaji mwenye akili anategemea zaidi nguvu ya pamoja na si mtu mmoja mmoja. Anauwezo wa kutumia nguvu ya jeshi zima na ya mtu mmojammoja.

22. Akitumia nguvu ya pamoja, wapiganaji wake huwa kama kuporomosha gogo au jiwe. Gogo au jiwe hutulia tuli kwenye sehemu tambarare na huporomoka likiwa kwenye mteremko. Kama lina umbo la mraba basi litaporomoka kidogo na kutulia, lakini kama ni mviringo, litaporomoka mpaka chini.

23. Kwahiyo nguvu ya wapiganaji hodari ni kama ya jiwe la mviringo lililoporomoshwa toka mlima wa futi 1,000. Hayo ndiyo yahusuyo nguvu.
 
VI: SEHEMU DHAIFU NA IMARA

1. Sun Tzu alisema: Yule anayewahi kwenye uwanja wa vita na kumsubiria adui atakuwa tayari zaidi kwa pambano. Yule anayekuja kwa kuchelewa na kulazimika kuharakisha kufika, atafika amechoka.

2. Kwa hiyo, mpiganaji hodari anamchagulia adui sehemu ya kupigana na si yeye kuchaguliwa na adui.

3. kwa kuweka chambo anaweza mfanya adui amkaribie, kwa kumdhuru anaweza mfanya adui akae mbali naye.

4. Kama adui ametulia basi atamchokoza na kumsumbua. Kama ana chakula cha kutosha atahakikisha anapatwa na njaa kama ametulia kambini atamlazimisha aondoke.

5. Vamia sehemu ambayo adui atalazimika kujiandaa harakaharaka kujilinda. Nyatia sehemu ambazo hatarajii.

6. Jeshi linaweza kutembea umbali mrefu iwapo linatembea sehemu ambapo hakuna adui.

7. Utakuwa na uhakika wa ushindi iwapo tu utavamia sehemu zisizolindwa. Utakuwa na uhakika wa usalama iwapo utakaa kwenye sehemu zisizoweza kuvamiwa.

8. Kwa hiyo, jemedari mzuri ni hodari wa kuvamia kwa mbinu ambazo adui hajui jinsi ya kujilinda na ni hodari wa kujilinda kwa mbinu ambazo adui hajui jinsi ya kuvamia.

9. Jinsi ilivyo vema kuwa msiri. Usiri utakufanya usionekane wala usisikike.

10. Utasonga mbele bila pingamizi iwapo utapita sehemu ambazo adui yako ni dhaifu. Utakuwa salama ukimbizwapo iwapo utakuwa na kasi kuliko adui.

11. Kama tukitaka kupigana basi adui atalazimishwa kupigana nasi hata kama kajilinda ndani ya ukuta imara au kajificha kwenye mahandaki marefu. Tunachotakiwa kufanya ni kuvamia maeneo yake mengine ambayo atalazimika kuyalinda.

12. Kama hatutaki kupigana basi tunaweza kumzuia adui asitulazimishe kupigana hata kama jeshi letu lipo kwenye uwanja wa vita au kambi yetu haina kuta wala mahandaki ya kuilinda. Tunachotakiwa kufanya ni kufanya kitu kitakachomtoa kwenye lengo au kitakachomchanganya hadi atoke kwenye lengo(tumpige mkwara).

13. Kwa kujua jinsi alivyojipanga na tukiendelea kujificha tunaweza fanya jeshi letu liwe limeungana sehemu moja huku lile la adui likiwa limegawanyika.

14. Tutakuwa na jeshi kubwa lililoungana wakati lile la adui likiwa limegawanyika. Kwahiyo itakuwa jeshi kubwa dhidi ya vikosi vidogovidogo. Hivyo tutakuwa wengi dhidi ya adui wachache.

15. Na tukiweza kupambana tukiwa na jeshi lenye nguvu dhidi ya jeshi dhaifu, adui yetu hawezi kusimama.

16. Sehemu tuliyopanga kuvamia haitakiwi kujulikana. Kwa hiyo adui inabidi ajitayarishe dhidi ya uwezekano wa kuvamiwa sehemu nyingi. Jeshi lake likiwa limegawanyika kwenye sehemu nyingi, tutakutana na upinzani kidogo tutakapovamia.

17. Adui akiimarisha jeshi lake mbele, atalifanya kuwa dhaifu nyuma. Akiimarisha nyuma basi litakuwa dhaifu mbele. Akiimarisha kushoto basi kulia atakuwa dhaifu. Akiimarisha kulia, kushoto atakuwa dhaifu. Kama akipeleka vikosi vyake kila sehemu basi atakuwa dhaifu kila sehemu.

18. Udhaifu wa kuwa na vikosi vidogovidogo unatokana na kujiandaa dhidi ya kuvamiwa. Uimara wa kuwa na kikosi kikubwa unatokana na kumlazimisha adui kujiandaa dhidi ya uvamizi wetu.

19. Tukijua sehemu ya pambano tunaweza kusanya wanajeshi toka sehemu za mbali kwaajili ya pambano.

20. Kama sehemu ya pambano haijulikani basi jeshi letu la kushoto halitaweza kulisaidia la kulia na lile la kulia halitaweza kulisaidia lile la kushoto.

21. Kwa makadirio yangu, wanajeshi wa Yueh wametuzidi kwa wingi lakini hilo halitawasaidia kitu kwenye suala la ushindi. Nasema ushindi unaweza kupatikana.

22. Adui anaweza kuwa na jeshi kubwa lakini tunaweza kumzuia asipigane. Peleleza ili kujua mipango yake na uwezekano wa kufanikiwa kwake.

23. Mchokoze ili afunue mbinu zake za vita. Mlazimishe ajionyeshe ili ujue udhaifu wake.

24. Linganisha kwa makini jeshi lako na jeshi la adui ili ujue wapi kuna uimara na wapi kuna udhaifu.

25. Unapofanya mipango kitu bora zaidi cha kufanya ni kuificha. Ficha mipango yako na utakuwa salama dhidi ya upelelezi, hata dhidi ya wapelelezi hodari na majasusi wenye akili nyingi.

26. Watu wengi hawaelewi jinsi ya kupata ushindi kupitia mbinu za adui.

27. Watu wengi wanaweza kuona jinsi ninavyovamia na kuteka lakini wengi hawawezi kuona mipango iliyoleta ushindi.

28. Usirudie mbinu ambazo zimekupa ushindi bali mbinu zako ziwe zikibadilikabadilika kulingana na hali na mazingira yanavyobadilika.

29. Mbinu za vita ni kama maji. Kiasili maji hutoka sehemu za juu kwenda sehemu za chini.

30. Kwa hiyo, vitani, kanuni ni kuepuka maeneo sehemu ambazo ni imara na kuvamia zile ambazo ni dhaifu.

31. Maji hutengeneza njia kulingana na sehemu yanakopita. Mwanajeshi anapigana na kushinda kulingana na adui anayepigana naye.

32. Kwa hiyo, kama ambavyo maji hayana njia ya kudumu, kwenye vita hakuna mbinu za kudumu.

33. Yule anayeweza kubadili mbinu kulingana na upinzani na hivyo kupata ushindi ndiye ataitwa jemedari wa majemedari

34. Maji, moto, miti, chuma na ardhi hupatikana kwa kiwango tofautitofauti duniani. Misimu minne ya mwaka hutokea kwa kupokezana. Kuna siku zenye mchana mrefu na siku zenye mchana mfupi. Mwezi una siku za kuangaza na siku za kuwa gizani.
 
VII: KUJONGEA KWA MBINU

1. Sun Tzu alisema: Jenerali hupokea amri kutoka kwa watawala.

2. Akishakusanya jeshi lake anatakiwa kuliunganisha kuwa kitu kimoja kabla ya kuweka kambi.

3. Baada ya hapo anatakiwa kusonga mbele kwa mbinu, kitu ambacho ni rahisi tu.

4. Tupite njia ndefu ya mzunguko na kumfanya adui atoke njia kuu. Japo tumeanza safari kwa kuchelewa, tufike eneo la vita kabla yake. Huko ndiko kuonyesha ujuzi wa kujongea.

5. Kujongea na jeshi kuna faida, ukijongea na umati usio na nidhamu ni hatari.

6. Ukitaka kufika uwanja wa vita kabla ya adui yako ukiwa na vitu vyote vya jeshi lako utafika kwa kuchelewa. Itakupasa utume kikosi kinachokwenda haraka lakini itakibidi kiache nyuma baadhi ya mahitaji yake.

7. Kwahiyo, ikiwa umeamuru jeshi lako kusonga bila kusimama, watembee mara mbili ya umbali wa kawaida kwa siku. Ukiwaambia watembee kilomita 50 ili wafike uwanja wa vita mapema, viongozi wa vikosi vyako vitatu wataangukia mikononi mwa adui.

8. Wanajeshi wenye nguvu watakuwa mbele na wale wadhaifu nyuma. Kwa njia hii ni moja ya kumi tu ya wanajeshi ndiyo itafika kwa wakati.

9. Kama ukitembea kilomita 25, ili kumzidi adui basi utapoteza kiongozi wa kikosi chako cha kwanza na ni nusu tu ya wanajeshi wako ndiyo watafika kwa wakati.

10. Ikiwa utatembea kilomita 15 kwa lengo lile lile, basi ni theluthi mbili tu ya wanajeshi wako ndiyo watafika kwa wakati.

11. Tunaelewa kuwa jeshi bila magari yake ya mizigo halitafaa kitu. Bila mahitaji yake na vituo vya kutolea mahitaji hayo halitafanikisha kitu.

12. Hatuwezi kuingia kwenye ushirikiano mpaka pale tatakampomjua vizuri yule tunayeshirikiana naye.

13. Hatuwezi kuamuru jeshi kusonga mbele isipokuwa tuwe na uelewa kuhusu maeneo tutayopita. Milima yake, misitu yake, mabwawa yake nk.

14. Hatutaweza kutumia vizuri sura ya nchi ya eneo isipokuwa tukitumia wenyeji wa maeneo hayo kutuongoza.

15. Ili kufanikiwa kwenye vita inatakiwa kuwa msiri.

16. Uamuzi wa ikiwa jeshi lako litapigana pamoja au utaligawa kwenye vikosi unatakiwa kufanywa kulingana na hali.

17. Kasi yako iwe kama upepo na umoja wako kama msitu.

18. Kwenye kuvamia na kupora uwe kama moto. Imara usiyetikiswa kama mlima.

19. Mipango yako iwe myeusi na iliyojificha kama usiku wa giza. Unapovamia uwe kama radi.

20. Kama jeshi lako likipora sehemu basi mali iliyoporwa igawanywe kwa wanajeshi wako. Kama ukiteka nchi mpya basi igawanye kwa wanajeshi wako.

21. Fikiri kwa kina kabla hujatenda jambo.

22. Atashinda na kuteka yule anayejua sanaa ya kujongea kwa mbinu.

23. Kitabu cha uongozi wa jeshi kinasema. Kwenye uwanja wa vita sauti haiwezi kufika mbali ndiyo maana zimewekwa ngoma na ngoma za chuma. Pia vitu vya kawaida ni ngumu kuonekana hivyo zimewekwa bendera na vitambaa vya ishara.

24. Ngoma, ngoma za chuma, bendera na vitambaa vya ishara vinasaidia macho na masikio ya jeshi kukazia fikira sehemu moja.

25. Kwa hiyo, jeshi likiwa kitu kimoja haitawezekana kwa wanajeshi shupavu kusonga mbele peke yao wala wale waoga kikimbia nyuma peke yao. Hii ndiyo sanaa ya kuongoza jeshi kubwa.

26. Kwa mapambano ya usiku tumia moto na ngoma kutoa ishara. kwa mchana tumia bendera na vitambaa vya ishara kama njia za kuelekeza macho na masikio ya jeshi lako.

27. Jeshi lote linaweza kushushwa mori. Jenerali anaweza kufanywa achanganyikiwe.

28. Mori wa wanajeshi huwa juu wakati wa asubuhi. Kufika mchana unakuwa umeanza kushuka. Jioni akili yao huwa inawaza kurudi kambini tu.

29. Jenerali mwenye akili ataepuka kuvamia jeshi iwapo mori wa wanajeshi wa adui upo juu. Atamvamia mori wake ukiwa chini. Hii ndiyo sanaa ya kusoma mori wa adui.

30. Akiwa mtulivu na mwenye nidhamu atasubiri mvurugano utokee katikati ya adui yake. Hii ndiyo sanaa ya kujizuia.

31. Kuwa karibu na lengo wakati adui yako yuko mbali. Kusubiri kwa utulivu wakati adui anahangaika kufika na kujipanga. Kushiba wakati adui akiteseka kwa njaa. Hii ndiyo sanaa ya kukusanya nguvu.

32. Kujizuia kupambana na adui ambaye bendera zake zimepangwa vizuri. Kujizuia kupambana na jeshi lililotulia kwa mpangilio mzuri. Hii ndiyo sanaa ya kusoma hali.

33. Ni sheria ya vita kutopanda muinuko ili kwenda kupigana na adui. Haitakiwi kumzuia adui anayeshuka mteremko.

34. Usimkimbize adui anayejifanya kukimbia. Usimvamie adui ambaye mori wake upo juu

35. Usimeze chambo za adui. Usizuie jeshi linalorudi nyumbani.

36. Ukizingira jeshi acha nafasi ya kutokea. Usilishambulie jeshi lisilo na pa kukimbilia kwa nguvu zote.

37. Hiyo ndiyo sanaa ya vita.
 
Zamani walikuwa wanatumia ngoma na bendera kuelekeza wanajeshi cha kufanya. Wanajeshi walikuwa wanajua mlio fulani unamaanisha tufanye kitu fulani. Nawaza kama huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa haya maonyesho ya magwaride ya siku hizi? Kwamba wanaonyesha wameiva na wanaweza fuata maelekezo?!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom