Kituo cha Uwekezaji kimesema kimesajili miradi 93 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.2 sawa na Sh trilioni 2.814 za Tanzania katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri ameeleza hayo katika ripoti ya uwekezaji ya kila mwezi ya TIC kwa mwezi Machi mwaka huu. Teri alisema idadi hiyo miradi iliyosajiliwa kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, inaifanya Tanzania kuwa eneo muhimu kwa shughuli za uwekezaji wa miradi.
Alisema katika kipindi hicho, Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.2 sawa na Sh trilioni 2.814 kwa miradi 93 inayotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 16,400.
"Thamani ya uwekezaji huo ni ongezeko la asilimia 48.9 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 787.4 (Sh trilioni 1.846) kwa mwaka uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 160 ikilinganishwa na uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 450.6 (Sh trilioni 1.056) kwa kipindi kama hicho mwaka 2021," alisema Teri.
Alisema sehemu kubwa ya uwekezaji huo wa Dola bilioni 1.2 za Marekani umetokana na uwekezaji wa ndani kwa Dola za Marekani milioni 887 (Sh trilioni2.079) sawa na asilimia 76 ya uwekezaji wote ulioidhinishwa.
Alieleza kuwa uwekezaji wa kutoka nje ulikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 276 (Sh bilioni
647.298) sawa na asilimia 24.
Kwa mujibu wa Teri, ukuaji huo wa uwekezaji katika robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha umechangiwa na ufanisi katika sekta ya ujenzi hasa majengo ya biashara uliovutia uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 333.2
sawa na Sh bilioni 781.509 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 2.3 (Sh bilioni 5.393) katika robo ya tatu ya mwaka 2021 / 2022.
Aidha, katika mwezi uliopita, TIC iliidhinisha na kusajili miradi 37 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 796.17 sawa na Sh trilioni 1.871. "Miradi hii inatarajiwa kuzalisha ajira 7,714 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita ambako TIC ilisajili miradi 35 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 361 (Sh bilioni 848.345) iliyotarajiwa kuzalisha ajira 6,681.
"Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 121 ya thamani ya miradi illiyoidhinishwa, asilimia 15 ya ajira zilizo-zalishwa na asilimia sita ya ongezeko la miradi iliyoid-hinishwa," alisema Mkuru-genzi Mtendaji wa TIC.
Alisema uwekezaii wa ndani (DI) ulikuwa asilimia 82 kwa uwekezaji wote uli-oidhinishwa mwezi uliopita au wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 648 (Sh tri-lioni 1.522) wakati uwekezaji wa kutoka nje (FDI) ulikuwa asilimia 18 au wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 148 (Sh bilioni 347.565).