SoC04 Tanzania tuitakayo: Serikali iboreshe mazingira ya biashara na kupunguza urasimu wa kisheria kwa maendeleo endelevu

Tanzania Tuitakayo competition threads
Nov 23, 2022
56
62
Utangulizi

Tanzania, kama nchi nyingine duniani, inakabiliwa na changamoto kadhaa linapokuja suala la kuanzisha biashara. Changamoto hizi zinajumuisha urasimu wa kisheria, upatikanaji wa vibali vya biashara, na mazingira magumu ya upatikanaji wa fedha na mitaji. Kwa bahati nzuri, kuna fursa nyingi za kuboresha mazingira ya biashara nchini, ambayo itasaidia kuchochea ujasiriamali na kukuza uchumi. Katika andiko hili, tutachambua changamoto kuu zinazowakabili wajasiliamali na wafanya biashara katika kuanzisha biashara nchini Tanzania na mapendekezo ya mabadiliko yanayoweza kufanywa na serikali ili kuweka mazingira wezeshi.

Changamoto 1: Urasimu wa Kisheria: Mchakato wa usajili wa majina, nembo au alama za biashara na huduma, kupata leseni na vibali vya biashara nchini Tanzania ni mgumu na unaweza kuwa changamoto kubwa katika mchakato wa kuanzisha biashara. Taratibu ndefu, na ukosefu wa uelewa wa sheria ni vikwazo vinavyoweza kuzuia ujasiriamali kwa vijana.

Utaratibu uliopo unamtaka Mtanzania kufanya yafuatayo ili aweze kuendesha biashara yake kihalali.

  • Kufanya usajili wa jina la biashara
  • Kufanya usajili wa alama za biashara (nembo) au huduma
  • Maombi ya leseni za biashara, na
  • Kuomba namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN).
Kila kipengele hapo juu kuna utaratibu wake wa kufanya maombi, suala hili linaweza kuwa ni kikwazo kwa Watanzania wengi na hivyo inaweza kusababisha uwepo wa biashara inayoendeshwa bila kusajiliwa.

Nini kifanyike?

Selikali ianzishe jukwaa la pamoja la usajili wa biashara ambapo mwombaji anaweza kukamilisha usajili wa biashara katika jukwaa moja lenye hatua tofauti. Mfumo huu pia utakuwa na mifumo ya malipo kwa kila hatua ambapo mwombaji atapokea namba ya malipo, afanye malipo ya hatua moja kabla ya kuendelea na hatua nyingine. Hatua hizo zinaweza kupangwa kama hivi;

Hatua 1: Usajili wa jina la biashara

Hatua 2: Usajili wa alama za biashara

Hatua 3: Maombi ya leseni ya biashara

Hatua 4: Maombi ya namba ya utambulisho wa mlipa kodi.

  • Serikali na mamlaka za udhibiti (regulatory agencies) watoe muda wa miezi sita (6) kwa biashara mpya kupata vibali na leseni za uendeshaji. Uwepo wa gharama za kusajili biashara na mahitaji ya leseni hizo zimekuwa ni kikwazo kwa wafanya biashara wenye mtaji wa wastani au kipato cha kati, hivyo suala hili linasababisha uwepo wa biashara nyingi ambayo haijasajiliwa kisheria na hivyo serikali hukosa mapato stahiki. Ikiwa serikali itatoa muda wa miezi sita tangu biashara ilipoanza, mfanya biashara anatakiwa kuwa amekamilisha usajili na kupata vibali na leseni husika katika kipindi hicho.
  • Serikali iangalie upya uwezekano wa kupunguza gharama za usajili wa biashara ikiwa ni pamoja na kuunganisha vipebngele tofauti katika hatua za usajili. Mfano, hatua ya kusajili jina la biashara pamoja na nembo au alama inaweza kuwa moja ili kupunguza gharama. Hii pia itasaidia wafanya biashara wengi kuweka nembo kwenye biashara zao uizingatia kuwa biashara nyingi kwa sasa haina alama/nembo. Kwa upande mwingine, serikali ipitie upya gharama za upatikanaji wa leseni kuu (principle license) na leseni ndogo (subsidiary license) ili kumsaidia mfanya biashara kupata unafuu wakati wa kuanzisha vitengo ndani ya biashara yake.
Changamoto 2: Upatikanaji wa Fedha na mitaji, kutokuwa na mtaji wa kutosha ni moja ya changamoto kubwa kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara. Benki na taasisi za kifedha zinahitaji dhamana au rehani kwa mikopo, ambayo mara nyingi vijana hawana. Aidha, bado kuna usimamizi duni wa asilimia kumi (10%) zinazotengwa na halmashauri za wilaya kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Nini kifanyike?

Kuwezesha Upatikanaji wa Fedha
: Serikali inaweza kuanzisha programu za mikopo yenye riba nafuu kwa vijana wajasiriamali, pamoja na kutoa mafunzo juu ya jinsi ya kuandaa mipango ya biashara na uwezeshaji wa kifedha. Kwa upande mwingine, serikali na halmashauri za wilaya ziongeze ufanisi katika usimamizi wa fedha zinazotengwa kwa ajili kuwezesha vijana.

Changamoto 3: Ukosefu wa Elimu na Maarifa ya biashara. Vijana mara nyingi wanakosa elimu na maarifa ya kutosha kuhusu ujasiriamali na mbinu za biashara. Hii inaweza kusababisha kushindwa kwa biashara zao. Ili kupata mikopo, ni muhimu zaidi kuwa na andiko la mpango wa biashara. Licha ya umuhimu wake, vijana wengi hawana elimu juu ya njia sahihi za kuandaa mpango wa biashara na hivyo hupelekea kukosa fursa ya kupata mikopo.

Nini kifanyike?

Elimu na Mafunzo ya Ujasiriamali
: Serikali inapaswa kuwekeza katika elimu ya ujasiriamali katika ngazi zote za elimu. Programu za mafunzo na ushauri kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara zinaweza kuwa muhimu.

Aidha, serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi wanaweza kuanzisha programu maalumu za mafunzo ya ujasiliamali na biashara ili kuinua uelewa na maarifa miongoni mwa vijana. Siku ya wafanya biashara inaweza kutanguliwa na wiki ya biashara nchini ambapo vijana watapata nafasi ya kujifunza na kuelewa taratibu mbalimbali zinazoongoza biashara nchini. Kwa kufanya hivyo, vijana watakuwa na elimu na maarifa sahihi juu ya biashara wanayofanya na hivyo ufanisi utakuwa ni mkubwa.

Changamoto 4: Upatikanaji wa ardhi kwa vijana. Katika upande mwingine, baadhi ya vijana wanatamani kuwekeza katika kilimo, lakini changamoto ya umiliki wa ardhi miongoni mwao hupelekea kuharibu mipango hiyo. Baadhi ya vikwazo hivyo ni Taratibu ngumu za kupata hati miliki ya ardhi pamoja na gharama kubwa za kupata arhi.

Nini kifanyike?

Serikali iwatazame vijana kwa jicho la pili na kuwapa nafasi ya kumiliki ardhi ikiwa ni pamoja na kupunguza Taratibu ngumu za kupata ardhi pamoja na kupunguza gharama za kupata hati miliki kwa vijana wenye nia ya kuwekeza kwenye kilimo.

Hitimisho

Kuanzisha mazingira wezeshi ya biashara ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi na kijamii nchini Tanzania. Kwa kushughulikia changamoto zilizotajwa hapo juu na kutekeleza mapendekezo ya mabadiliko, serikali inaweza kukuza ujasiriamali wa vijana na kuleta maendeleo endelevu. Ni muhimu kwa serikali kushirikiana na sekta binafsi na mashirika ya kimataifa ili kufanikisha mabadiliko haya na kuweka Tanzania kwenye njia ya maendeleo endelevu na ustawi.
 
Back
Top Bottom