Tanga: UWASA yazindua Hatifungani ya kwanza Afrika Mashariki ya Miundombinu ya Maji yenye thamani ya bilioni 53.12

Pfizer

JF-Expert Member
Mar 25, 2021
526
748
Tanga: Hatifungani ya kijani ya miundombinu ya maji yenye thamani ya Shilingi bilioni 53.12 imezinduliwa na Mamlaka ya Maji Tanga, taasisi ya serikali inayojitegemea. Hatifungani hii ya kwanza katika historia ya masoko ya mitaji nchini na ukanda wa Afrika Mashariki, inalenga kugharamia mradi wa uboreshaji miundombinu ya huduma ya maji safi na uhifadhi wa mazingira Tanga. Hatifungani hii itadumu kwa muda wa miaka 10, itaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, na itatoa riba ya asilimia 13.5% kwa mwaka, itakayolipwa kila baada ya kipindi cha miezi 6.

Mwaka 2021, Serikali ilizindua Mkakati wa Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa njia Mbadala (APF), ili kutanua wigo wa vyanzo vya fedha za kugharamia mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji, nishati, afya, kilimo na miradi mingine ya miundombinu. Hatifungani ya Tanga UWASA ni ya kipekee na inathibitisha kuwa kanuni na mifumo iliyopo inaweza kutumika na Halmashauri na taasisi nyingine za Serikali kupata fedha za miradi kupitia masoko ya mitaji na dhamana. Njia hii ya kibunifu inaweza kusaidia kuziba pengo kati ya uhitaji wa rasilimali fedha na zile zilizopo ili kufikia mipango ya maendeleo ya taifa na malengo ya maendeleo endelevu”.

Akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, mgeni rasmi Mhe. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema uuzaji wa hatifungani kama hii ya Tanga UWASA, ni njia mojawapo itakayosaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayozalisha kipato, itapunguzia Serikali Kuu mzigo wa bajeti ya miradi na kutoa nafasi ya kuweka mkazo kwenye maeneo mengine ya vipaumbele ambako haitokuwa rahisi kupata fedha kwa njia kama hizi.

Sambamba na hilo alisema “Nawaelekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kama msimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini na Waziri wa OR-TAMISEMI kama msimamizi wa Halmashauri, kuziandaa Taasisi za umma, Mashirika na baadhi ya Halmashauri zenye vigezo, kutumia utaratibu huu wa kujitafutia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kupitia uuzaji wa hatifungani.”

Akiongea katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande alieleza kuwa Serikali itahakikisha kuwa Mkakati wa Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa njia Mbadala (APF), unatekelezwa kama ilivyopangwa, na kwamba Taasisi za Serikali nazo pia zinatumia njia bunifu na mbadala katika kugharamia Miradi ya Maendeleo, badala ya kutegemea Serikali pekee, kama ambavyo inafanyika kwa mafanikio na Sekta Binafsi na Makampuni katika soko hilo hilo.

Kwa upande wake Mhe. Jumaa Aweso, Waziri wa Maji alisisitiza kuwa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha huduma ya Maji inafikia asilimia 95% kwa mijini na 85% kwa vijijini ifikapo Desemba 2025. Hadi sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi ni 88% kwa mijini na 77% kwa vijijini. “Ili kufikia malengo hayo, miongoni mwa mahitaji makubwa ni fedha ambazo upatikanaji wake unahitaji ubunifu mkubwa kama ilivyofanya Mamlaka ya Maji Tanga. Matokeo ya mradi huu yatasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji maji Jijini Tanga kutoka asilimia 96% hadi 100% na kwa saa 24, ifikapo Juni 2025.

Vilevile, kuongeza mtandao wa maji katika miji ya Muheza na Pangani toka asilimia 70% hadi zaidi ya 95% ifikapo Juni 2025. Kadhalika kusambaza maji ya kutosha kwa Wilaya ya Mkinga kupitia mradi unaoendelea kujengwa”, aliongeza.

Katika salamu zake, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji Tanzania (UNCDF) Bw. Peter Malika ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kufanikisha tukio hili la kihistoria kwa Tanga UWASA. Pia akasema “Jukumu la muhimu lililofanywa na UNCDF ni kushirikiana na Serikali na taasisi zake kuhamasisha maboresho ya sera na mazingira wezeshi yanayohusiana na masoko ya mitaji na dhamana.

Hatifungani ya Tanga UWASA inadhihirisha kuwa masoko ya mitaji yanaweza kutumika kupata fedha za kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa bila kuongeza deni la taifa. UNCDF itaendelea kutoa msaada wa kitaalam na kifedha kuhakikisha Hatifungani nyingine za taasisi nyingine za serikali pamoja na Halmashauri zinauzwa ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya fedha za miradi linalotokana na ukuaji wa miji, ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya tabia nchi.”

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Bw. Nicodemus Mkama alisema “Mamlaka imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mikakati ambayo imewezesha utoaji wa bidhaa bunifu zinazowezesha Kampuni na Taasisi kupata fedha za kuendeleza na kukuza biashara. Bidhaa hizo ni pamoja na hatifungani yenye mguso wa Jinsia; na hatifungani ya kijani iliyotolewa katika fedha mbalimbali ambazo zimeweka historia ya kuwa hatifungani za kwanza kutolewa katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara; pamoja na hatifungani zenye kukidhi misingi ya Shariah yaani Sukuk bond. Matokeo haya yameiweka Tanzania katika ramani ya masoko ya mitaji ulimwenguni yanayotoa bidhaa bunifu, zinazovutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Hatifungani ya Tanga UWASA ni hatifungani yenye ubunifu unaojumuisha vipengele vinavyogusa taasisi ya umma, ujenzi wa miundombinu ya huduma endelevu za maji, utunzaji wa mazingira na miradi yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara; na inaweka msingi madhubuti wa kuonyesha njia kwa Taasisi za umma; na Mamlaka za Serikali za Mitaa namna ya kupata fedha za kugharamia miradi yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara, kupitia masoko ya mitaji.”

Wadau wengine muhimu waliohusika na uandaaji wa hatifungani hii na maeneo yao ya kitaalam ni pamoja na Benki ya NBC (mshauri mwelekezi), FSD Africa (upatikanaji wa hati ya kijani), FIMCO na Global Sovereign Advisory (fedha na uwekezaji), ALN Tanzania (sheria), Innovex (uhasibu), Vertex International Securities (wakala wa soko la Hisa Dar es Salaam) and ISS Corporate Solutions (mtoa ithibati wa kimataifa). Ili kununua hatifungani hii, wawekezaji na watu binafsi wanashauriwa kutembelea wakala yeyote wa Soko la Hisa la Dar es Salaam mwenye leseni kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana au Tawi lolote la Benki ya NBC.
 
Back
Top Bottom