SoC03 Sitalisahau kaburi lako Madalitso

Stories of Change - 2023 Competition

saadala muaza

Member
May 12, 2023
38
37
SITALISAHAU KABURI LAKO MADALITSO

Mwandishi: Saadala Muaza

---
Ilikuwa ni saa kumi na mbili takribani na dakika arobaini na saba za jioni. Sauti yako ikapenyeza hadi kwenye ngoma za sikio langu na kunishtua toka usingizini ambako nilikuwa nimelala fo!fo!fo!

"Chima! Chima! Chima mme wangu tumbo linaniumaaa jamani" hapo hapo usingizi wote ukakata. Akili ikazidi kuchanganyikiwa zaidi pale nilipoangalia chini "Mungu wangu!" Zilikuwa ni damu zilizotapakaa sakafu nzima mithili ya anga pale linapokuwa jeupe pasina hata tone la wingu kujishikiza. Moyo ukaniruka kwa sekunde kadhaa. Macho yakanitoka kama bundi aliyeona mzoga na asiamini kilichotokea.

Akili yangu isingeweza kurudi katika hali yake ya kawaida kwa kelele zote ambazo madalitso mke wangu ulikuwa ukizitoa mpaka sasa."Tunafanya nini sasa mke wangu?" Ni swali ambalo nilijikuta nakuuliza wewe badala ya kujiuliza mwenyewe.

"Nipeleke hospitali chimaaa! Uwiiiiii jamaniìi nakufaaaa chimaaaa!" kelele hizi zilinifanya nikurupuke kutoka mikononi mwako na kutimka mbio kuelekea nje mpaka kwa mzee Majuto ambaye alikuwa ndiye jirani yetu wa pekee kijijini hapa."Baba! baba! Mke wangu ujauzito wake umetoka baba angu .Nisaidie baba! mke wangu anakufa".

Tukachukua baiskeli ya mzee Majuto na kukupeleka hospitali ili kuweza kuunusuru uhai wako. Tulitembea umbali mrefu sana ili kuipata hospitali ya Nzera ambayo ilikuwa ni zaidi ya kilometa kumi na tano mpaka kufika hospitalini hapo kutoka kijijini kwetu katoma wilayani Geita.

Nakumbuka vizuri kauli yako ya mwisho kabla ya kunyamaza kimya tukiwa bado tuko njiani. Ilikuwa yapata saa tatu za usiku. Usiku ambao ulitukataa na kukubali kulitandaza giza lake ili tusiweze kuona mbele. Barabara likatutupia mabonde kila tulipolikanyaga na kukufanya madalitso wangu uweze kulegea zaidi. Sura yako haikuwa yenye huzuni tena ulitabasamu kwa uchungu na kisha kunifuta machozi yangu. Uso wako ukiwa umelowa mvua ya machozi ambayo yalitiririka kwa kasi zaidi hata ya maporomoko ya maji.

"Nakupenda chima wangu" uliongea kwa sauti ya chini sana na kisha ukanyamaza. Sikuweza kugundua chochote mpaka pale tulipofika hospitalini na sasa yalikuwa yamekwisha pita zaidi ya masaa saba tangu tuanze safari yetu. Sikujua kama hii ndio itakuwa safari yetu ya mwisho tukiwa tumeshikana mikono. Kwani laiti ningelijua nisingelikubali kuuachia mkono wako mlaini na uliokuwa ukiyafuta machozi yangu kila nilipo lia.

Nayakumbuka pia macho yako laini yaliyoukonga moyo wangu kila nilipokutazama. Umbo lako lililonifanya niamini kabisa kuwa hakuna mwana mke mwingine yeyote duniani mzuri zaidi yako ukitoa Mama yangu mzazi.

Madakrati walikupokea na kukupeleka katika chumba cha wagonjwa mahututi ambako ilinichukua masaa kadhaa kabla ya kuipokea kwa masikitiko taarifa ya kifo chako. Ndio! madaktari walisema haupo tena nasi isipokuwa mtoto ametolewa salama katika tumbo lako la uzazi.

Ni miaka ishirini na tatu sasa imepita tangu upumzike ndani ya kaburi hili.Na huyu aliyeko mkono wangu wa kuume ndio binti yako uliyemuacha ambaye nilimpa jina la Vumilia.

Pokea maua yangu na uendelee kupumzika kwa amani huko uliko.

NAKUPENDA. Ni mimi kipenzi chako Chima.

Polish_20230517_095746845.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom