Siri nzito,wimbo wa NIMWAGE RADHI wa Mrisho mpoto

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,209
4,406
JE!HUENDA MRISHO MPOTO (MJOMBA)ANAUSHANGILIA UTAWALA WA DKT.JOHN POMBE MAGUFULI KWA WIMBO WAKE MPYA WA "NIMWAGE RADHI"?.

Hivi karibuni Mwanamuziki Mrisho Mpoto(Mjomba)ametoa wimbo wake mpya akimshirikisha mwanamuziki mwingine kutoka WCB anayeitwa Hamornize.Wimbo huu umekwenda kwa jina la "Nimwage radhi" ambapo hasa maudhui yake makuu ni furaha yao waimbaji katika kuisherehekea "Ndoa" iliyofungwa ambayo ndani yake halikutajwa jina la bibi wala bwana arusi.Jambo lililoshughulisha vichwa vya watu wengi ni kwamba,kwa dasturi yake Mjomba katika nyimbo zake za kuwa na maigizo ndani yake sambamba na mafumbo ya kusugulisha bongo,je alichokimaanisha mjomba katika wimbo huu ndicho hichohicho?,au "arusi" hii inafumba jambo fulani lililomfurahisha MJOMBA MPOTO?.Ndipo nikaona nami niuthibitishe uhai wangu kama si kwa kutatua utata huu,basi kwa kuwachokoza wanaojua ili wapate kutujuza na MwenyeziMungu atawajaalia.

Binafsi,baada tu ya kuusikiliza wimbo wa MJOMBA MPOTO mara moja akili yangu ikakimbilia mwaka ~360KK/BC ambapo wachambuzi wa kazi za sanaa "Literary Works",wakisuguana kwa nadharia zao mbalimbali.

Mwaka huo kulikuwa na "dhana" ya "Moral Criticism: Drama Constructions" ambapo uundaji na uchambuzi wake ulijikita katika kuangalia maadili zaidi tena hasa ya jamii ya Kigiriki. Nikawakumbuka mwanafalsa Socrates, naye Plato na kitabu chake cha "Republic"aliposimamia hoja ya kwamba "Sanaa lazima ifikie katika kikomo kabisa cha wazi na nyoofu katika majukumu yake".Wao waliona kuwa,hapakuwa na haja ya kufumba fumba mambo katika sanaa bali sanaa ifundishe uchamungu na uvumilivu ndivyo vitavyosaidia kuipokea sanaa licha ya ukavukavu wake ambao itakuja nao.

Aristotle ni mwanafunzi wa akina Plato,lakini alipinga vikali kabisa nadharia hiyo. Yeye hakuona kama ni jambo la kheri kuishusha kazi ya Sanaa kwa ukavuukavu hata kidogo. Aliona kazi ya Sanaa tena kwa kutoa mifano ya ushairi "poetry" na michezo ya kuigiza "drama",lazima mwishowe vitowe na burudani licha ya maudhui yake ambayo inakuja nayo.Yeye aliona kuwa,lazima itazamwe lugha ya kutumia iwe na sanaasanaa ndani yake,viimbo na viliwazo nakadhaalika.Njia hii ilijaa mbinu nyingi ndani yake ambazo Aristotle alizipendekeza ambazo waandishi wengi waliokuja kuandika mambo mazito katika ufichouficho iliwasaidia sana.NA HAPA KATIKA VIATU VYA ARISTOTLE NDIPO NINAPOHOJI KUWA HUENDA MJOMBA MPOTO AMESIMAMIA?.

MJOMBA MPOTO kunasibisha wimbo wake na "Arusi" sikutaka kuona ni jambo dogo hata kidogo tena sikutaka kuishia palepale anapotupeleka kwamba anawapa mizungu bi rusi na bwana arusi tu basi.Mfano huu na historia ya MJOMBA MPOTO na kazi zake kisiasa nchini ilinipa hamu nipekuwe maktaba yangu na kutazama historia ya kazi za fasihi inaitazamaje "Arusi"?.Kwa hakika nilikuta mara nyingi wasanii wenye kariba ya MJOMBA MPOTO husema "Arusi" kwa kumaanisha mahusiano baina ya viongozi wa serikali hasa wakubwa kama Rais pamoja na serikali zao. Nitakupa mifano kadhaa.

1.Mwaka 1901 iliandikwa tamthiliya iitwayo "The Wedding" na Mpoli Stanistaw Wyspianski akikejeli "Ubwenyenye" wa karne ya 20 kwa kuwaita mabwenyenye hao wana ndoa na serikali zao.

2.Mwaka 1912,nchini Uingereza iliandikwa riwaya na H.G.Wells iliyoitwa "Marriage " pia alikuwa anakejeli "Mabwenyenye" waliojimilikisha tawala na kuzifanya kana kwamba wameumbiwa wao na wengine hawastahiki.

3.Mwaka 1926,nchini Ujerumani ilitoka kazi ya mchezo wa kuigiza"drama" mfupi tu ulioitwa "Respectable Wedding" uliotungwa na Bertolt Brecht ambao ulikuwa unakejeli pia jamii ya "Mabwenyenye" ambao walitaka kujifanya miungi watu,kama wale ambao mara zote MJOMBA MPOTO alikuwa akiwakemea kipindi cha nyuma kabla ya kumkaribisha "SIZONJE" katika jumba letu ambalo "Mabwenyenye" walikuwa wanapita madirishani na wakati milango ilikuwepo.

4.Mwaka 1977 nchini Kenya iliandikwa "play" ilojipatia jina la "Ngaahika Ndeenda" iloandikwa na Ngugi Wa Thiong'o na Ngugi wa Mirii iliyokuja kutafsiriwa katika Kiingereza baadae na ikawa inasomeka kama "I Will Marry When I Want" yaani "Nitaolewa Nikipenda",ambayo wengi huitafsiri sivyo kwamba "Nitaoa Nikipenda".Mchezo huu pia ulikuwa wakejeli mfumo wa elimu wa "Kibwanyenye" nchini Kenya baada tu ya Uhuru.Je!Kushangilia na kumwaga radhi kwa MJOMBA MPOTO,katika arusi ya nchini pake na kuwa tayari kwa lolote, SI KUSHANGILIA UTAWALA SAFI WA DKT.JOHN POMBE MAGUFULI?.

5.Mwaka 1980 nchini Tanzania,uliandikwa mchezo wa kuigiza ulioitwa "Arusi" na mwandishi Prof.Ebrahim Nurdin Hussein Al-shadhliy akikejeli mfumo wa vijiji vya "Ujamaa" na sera yenyewe yote kwa kutembelea mbinu ya changamoto za "Arusi".

6.Mwaka 1988 nchini Tanzania iliandikwa diwani iliyoitwa "Fungate ya Uhuru" na mwandishi Dkt.Muhammed Seif Khatib,akikemea na kusononeka juu ya "Ubwenyenye" wa wale waliooana na Serikali na kuifanya ni yao baada ya kuanza kuvuna matunda ya Uhuru."Fungate" ni masiku saba maalumu ya bibi na bwana arusi baada tu ya ndoa kufungwa.

7.Thomas A.R.Kamugisha nchini Tanzania ameandika riwaya ya "Harusi ya Wendawazimu " ambayo ilitahadharisha Tanzania kufungamana na baadhi ya mataifa kwa kuyafananisha na wanawake warembo warembo na kushauri kuwa hawafai kuolewa nao.Kitabu kinaeleza kuwa wanawake hao warembowarembo wamesababisha mataifa makubwa kuanguka akitoa mfano wa Dola ya Roma na viwanda kufa kwa walioolewa nao. Je!MJOMBA MPOTO anapomuonya bibi arusi kuchunga mashoga wambea na wachokonozi huenda anamtaka ajilinde dhidi ya mataifa haya pamoja na vibaraka wao nchini?.

Kwa ujumla arusi mmoja hawezi kuwa Rais wa nchi na chama chake,kisha serikali ndio ikawa bwana arusi?.Ikitazamwa video ya wimbo huu wa "NIMWAGE RADHI"itaonekana humo sare inayofanana na sare ya Chama cha Mapinduzi kwa kijani na njano ikiselebuka katikati. Lakini pia huonekana mtu mwingine aliyevaa kofia ya bendera ya taifa akila kuliko wote.Je!MJOMBA MPOTO anatabiri baraka ya chakula na faraja?.

Wimbo unamtaka arusi mmoja yaani siyo "serikali"?kumtunza arusi meingine yaani "Rais"?kwani anakubalika kusini kote?.Wimbo umetaja maeneo ya Ruvuma,Lindi na Mtwara. Kwanini kusini tu?.Mimi ninaona kusini mwa Tanzania ni sehemu ambayo imedhihirika miaka mingi kuwa chini kwa maendeleo ya kila aina.Kusini ndiko ambako wamefikia hatua ya kufanya mapigano makubwa dhidi ya serikali kwa kugoma nishati ya gesi kusafirishwa kwenda Kinyerezi.Je,kwa wimbo kuitaja kusini pekee tuamini kuwa Msanii ametaka kuonesha kukubalika kwa bi arusi kiasi kwamba hata jamii ile ya kusini imemkubali basi mwingine anayemkataa ni nani huyo.?.

Wimbo umeanza na Harmonize akitaarifu kuwa goma lipo uwanjani na akiuliza "KAIBIWA NANI?".Ndo tuamini kuwa ni utawala huu ambao hauna ufisadi unaoshangiliwa?Maarusi hawa wametandikiwa kapeti jekundu la viongozi na MAMLAKA .

Wimbo unamalizia kwa kusema kuwa "ANAOMBA AISHIE HAPA,TARISHI HUWA HAFUNGWI. ANAOMBA ACHAPE LAPA YALOBAKI NI YA MAKUNGWI,ALOWAKERA SAMAHANI,KUSEMA NI JUKUMU LAKE . ANAOMBA TUISHI KWA AMANI,HII NDIO FURAHA YAKE.

Je,kufurahika kwake ni dalili kuwa "arusi" hii si sawa na zile za "MABWENYENYE"?.WALLAHI KAMA NDIVYO ALIVYOMAANISHA BASI TANZANIA YOTE TUWE PAMOJA TUISHEREHEKEE ARUSI.

Mudhihiri Saidi Njonjolo.
Mtwara-Mjini.
22/5/2018.
0714-821926.
 
Mkuu kuna kitabu kiliandikwa na Ebrahim Hussein kinaitwa "ARUSI" na kingine kinaitwa "HARUSI" sijajua kimeandikwa na nani?
 
Kizazi cha bodaboda hii maada iko juu ya uwezo wao.Hii ilikua maada ya tafisida na akili ya hali ya juu.IQ ndogo haiwezi tambua chochote
 
Back
Top Bottom