SIMULIZI:VIFO VYA WAPELELEZI (By FADDY)

Nominee

JF-Expert Member
Sep 5, 2017
465
1,265
UTANGULIZI:

Ni jumapili ya tarehe 14/03/2010,Mida ya saa 10 jioni vinasikika vilio vya uchungu ndani ya nyumba kuukuu iliyopo maeneo ya uswahilini kata ya Mpambano wilayani Majita.Ni kilio hiki ndicho kinachowafanya majirani wasogee karibu na nyumba ya Mzee Mohammed kuangalia kuna nini kimetokea. "Eeeh mungu we....e...eee...we, nimekukosea nini mja wako hadi yote haya yanikute mimi tu, kwa niiii.....ni umeamua kunichukulia na huyu tena?, Baba Abdul amka,ooooooh mimi jamaaaani ntabaki na naaaaaani, amka mume wangu, amka, amka amka pliiiiiiz". Ni kilio cha kwiki na chenye kuhuzunisha cha mama huyu mjane ndicho kilichowashitua majirani hadi kusogea hapo. Mama Abdul alikuwa amepoteza mume wake kwa homa ya kupooza. Ni takribani wiki mbili zimepita tangu amzike mwanae mpendwa Abdul Mohammed, Mpelezi machachali ndani ya idara ya usalama wa taifa la BEIRAD kwa homa hiyohiyo ya kupooza. Ni huzuni kuu kupoteza wale uwapendao tena ndani ya wiki mbili tu. Mohammed Ismail almaarufu kama Mzee Mohammed ni miongoni mwa wazalendo ndani ya BEIRAD ambaye alilitumikia taifa kwa jasho na damu kuhakikisha kuwa usalama wa Raia na nchi kwa ujumla unalindwa dhidi ya mafedhuri wataka mali na umaarufu usio na maana. Akiwa chini ya uangalizi wa boss wake, Professor John Kluger anatumwa missions mbalimbali na zote anazikamilisha kwa ufanisi wa hali ya juu na hapo ndipo anapopewa fursa ya kumfundisha mwanae "Abdul Mohammed" ili aje kumrithisha fani yake.

JE,NINI KIMEWAKUMBA MTU NA BABA YAKE?. Usiikose simulizi hii kila siku za jumatatu, jumatano na jumamosi.
 
SIMULIZI:VIFO VYA WAPELELEZI(By FADDY)

SEHEMU YA KWANZA:

Mzee Mohamed au ukipenda muite MWAMBA WA CHUMA kama anavyojulikana katika ulimwengu wa Ushushushu alikuwa akisumbuliwa na HEMIPLEGIA (kupooza upande mmoja wa mwili, yaani mkono mmoja na mguu mmoja). Na baada ya siku chache homa ikazidi kuongezeka na kuwa kali zaidi, hapa haikuwa tena HEMIPLEGIA bali ilikuwa TETRAPLEGIA (yaani kupooza viungo vyote miguu na mikono). Kwa walio na macho ya kawaida kama yangu wanaweza kuongea pasi na shaka kuwa mipango ya Mungu tu ndio iliyofanya Nguli huyu wa USALAMA awe hivi alivyo sasa, ila usilolijua ni kama usiku wa kiza kinene, hujui nani mkweli na nani muongo. Katika hii dunia usije kumuamini mwanadam yeyote. Ni heri ucheke na simba, ila si mwanadam. Watu si wema, watu ni mashetani, watu ni wauaji. Kwa yaliyomtokea mzee Mohammed ,bila shaka aliapa juu ya mbingu na ardhi, hatokuja kuwa na urafiki na mwanaadamu yeyote,labda mama mzazi tu.

TURUDI NYUMA:

Ni miezi takribani 12 iliyopita, Mzee Mohammed akiwa na afya tele. Ndani ya ofisi za BISA(Beirad Intelligence and Security Agency) simu ya mezani inaita,
......."Hello,habari yako muheshimiwa".....
(sauti nzito ilisikika kutoka upande wa pili.)
...... "Salama, sijui nikusaidie nini".......
(mzee Mohammed aliitikia huku akiwa na shauku ya kutaka kumjua mpigaji ni nani)
......"Mi sina shida kubwa sana muheshimiwa, bali nimekupigia ili nikujuze tu kuwa kuna mzigo wako upo hapo ndani ya droo ya meza yako. Tafadhali angalia".......
(sauti ile iliongea na kukata simu).
Mzee Mohammed akabaki na kigugumizi, iweje mtu aongee haraka kiasi hicho na kukata simu?. Akainama chini ya meza yake na kuvuta droo ndogo aliyokuwa akiitumia kuweka vitu vidogo vidogo kama bahasha, mihuri na funguo. Alipoifungua akastaajabu kuona bahasha ya kaki iliyoandikwa kwa maandishi mweusi
........."KUTOKA KWA XYZ".........
Akaifungua kwa wasiwasi huku macho yake yakionesha mshangao wa dhahiri.
......."Kwako MWAMBA WA CHUMA, bila shaka unaendelea vyema na shughuli zako za kujenga taifa. Nina ombi moja kwako, naomba uache kunifatilia, hutoniweza. Ni wengi wamepotea bila kupewa onyo, ila kwako ni Yesu tu amekuokoa. Acha kufatilia mauaji ya DP HOTEL, ahsante"............
Ni maneno machache yenye ujumbe mzito ndio yalionekana katika barua hii. Mwamba wa chuma hakujua afanye nini, akatoka nje hadi katika ofisi ndogo ya Secretary wake kumuuliza ni nani aliyeileta ile barua.
....."Hivi James,mbona unaweka mizigo. yangu kwenye droo bila kunipa taarifa?"......
aliuliza mwamba wa chuma alipoingia tu ndani ya ofisi ya secretary.
...... "Aaah, Boss nsamehe sana, nilipitiwa. Ila nakumbuka asubuhi kuna Mama mmoja wa makamo alikuja hapa akiwa na bahasha akasema ikufikie wewe, ndo nikamwambia anipatie, nikaiweka mezani kwako ila nikasahau kukupatia Muheshimiwa, nsamehe sana".......
James alimueleza mwamba wa chuma huku akiomba msamaha kwa kosa la kuweka barua ofisini bila kumtaarifu. Mwamba wa chuma alitoka huku akighafirika. Alikuwa hajui nani ni mpigaji wa ile simu na namba aliitoa wapi. Ila ghafla akapata wazo la kwenda kitengo cha mawasiliano kilichopo hapohapo Idarani kuangalia ile namba inamilikiwa na nani na ikiwezekana basi hata mahali alipo mpigaji patambulike.
......."Muheshimiwa, mbona dialing code ya hii namba ni tofauti na yetu?, code ya hii namba ni +61 bila shaka ni ya Australia, yetu ni +999"............
(kijana anayehusika na masuala ya mitandao akawa anaongea huku akimuangalia Mwamba wa chuma usoni)
...."Duuh, basi sio mbaya. Ahsante sana".....
(Mwamba wa chuma alijibu huku akitoka nje huku sura ikionesha kukata tamaa)

Kesi iliyopewa Investigation code 12HDP ni miongoni mwa kesi nzito ambazo Mwamba wa chuma alipewa achunguze. Ni tukio la mauaji yaliyotokea ndani ya hotel ya nyota tano almaarufu kama DP HOTEL iliyopo katikati ya jiji la NAIPAD.
Ni siku ya jumamosi asubuhi mwezi wa 12, familia moja ya watu wanne walikuwa wamefika katika hotel hiyo wakitokea jiji la BINAS. Kwa muonekano wa haraka, ni dhahiri kuwa hii familia ni miongoni mwa familia chache zilizotunukiwa furaha, kwani nyuso zote zilionyesha hali ya kuchangamka tangu wakishuka ndani ya gari lao aina ya Bugatti chiron lenye thamani zidi ya dola milioni mbili na nusu za kimarekani. Ama hakika, kuna familia zimebarikiwa, sio kama zetu huku mwananyamala, baba na mama wananuniana ndani ya nyumba mwezi mzima utafikiri walifungishwa ndoa kwa mtutu wa bunduki.Yani mama hapo asijichanganye kusema anaomba hela ya vipodozi, hiyo kesi itakayozuka hapo ni mungu tu mwenyewe ndo anajua. Ila kwa familia ya watu hawa wanne ni tofauti kabisa na zile ninazozifahamu. Ila wahenga wanasema "Siri ya mtungi aijuae kata". Mida ya asubuhi siku ya pili ndipo kunatokea tukio la kusikitisha sana ambapo miili ya watu wa nne wa familia hii (Mke, mume na watoto wa kike mapacha wawili) ilikutwa ndani ya chumba kimoja cha hotel hiyo huku ikiwa haina vichwa. Ugumu si tukio la kukuta maiti, bali ugumu ni pale ujumbe unapokutwa kwenye karatasi chini ya dressing table ya chumba hicho ikisomeka "BADO SIJARIDHIKA,LAZIMA WAFE "

Je,nini kimeikumba familia hii?,
Ni nani alimpigia simu Mwamba wa chuma?

USIKOSE SEHEM YA PILI.
AHSANTE.




Pia naombeni radhi kwa usumbufu uliojitokeza.Ntakuwa najitahidi kutoa kila baada ya siku mbili.Ahsanteni.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SIMULIZI: VIFO VYA WAPELELEZI (By FADDY)

SEHEMU YA PILI

........................................................................

"Eti Da Doris wale wageni waliokuja Asubuhi wameshaondoka?" (ilikuwa ni sauti ya Anusiata, Dada mfanya usafi katika hotel ya DP akimuuliza mfanyakazi mwenzake wa mapokezi (Receptionist) mida ya saa moja usiku.

"Mmh, hapana, hawajaondoka, kwani vipi?" (Doris alijibu huku akiwa na mshangao wa lile swali la Anusiata).

"Si uliwapatia vyumba viwili?, kimoja ni cha wale mabinti pacha na kingine ni cha yule mke na mume? (Anusiata aliendelea kumtupia swali jingine Doris)

"We nawe acha umbea, sasa hayo ndo maswali gani!!!, ulitaka mke na mume walale vyumba tofauti au? (Doris alijibu kwa hasira huku akiendelea na shughuli yake ya kuchapa maneno kwenye tanakilishi iliyopo hapo mapokezi)

"Jamani Da Doris, sina nia mbaya, nilitaka tu kujua, maana nilipoenda kwenye chumba cha wale mabinti kubadilisha mashuka nikakuta chumba kipo wazi na watu hawapo. Ila kile chumba cha mke na mume ndo kimefungwa kwa ndani, nikipiga hodi hawafungui" (Anusiata alijitetea)

"Basi itakuwa wapo bize na wazazi wao wanapiga stori, we kama umeshabadilisha hizo shuka kwenye chumba cha mabinti basi inatosha, fanya mambo yako. Hayo mengine waachie wenyewe" (Doris alijibu kwa mkato huku akionekana kukereka kwa yale maswali ya Anusiata).

Anusiata aliondoka kiunyonge ingawa moyoni alihisi kama kuna kitu kisicho cha kawaida kinachoendelea hapo hotelini. Maana tangu ile Familia iingie pale hotelini mida ya asubuhi hakuwaona tena kutoka kama wateja wengine wanavyotokaga mfano kuelekea nje kupunga upepo au kwenda kwenye mgahawa mdogo uliopo Ground floor hapo hotelini. Ila akaamua kupotezea na kuelekea Chumba cha kufulia (washing room) ili aendelee na majukumu yake. Akiwa yupo bize na shughuli ya kuchambua nguo chafu ili aziingize kwenye mashine ya kufulia ghafla ana tahamaki baada ya kukiona kidole cha binadamu kilichoanguka kutoka kwenye zile shuka alizotoa chumba namba 123 (chumba cha wale mabinti). Akiwa bado anashangaa, ghafla anapigwa roba na kuzibwa mdomo na mtu alie nyuma yake.

"shiiiiiii, ole wako upige kelele nitakipasua hiki kichwa, haya niambie kule mapokezi ulikuwa unaongea nini na yule malaya mwenzako ulipotoka chumba namba 123 kuchukua mashuka?" (sauti nzito ya kukoroma ilisikika kutoka kwa huyu jamaa aliyemkaba roba Anusiata huku akimwachia mdomo Anusiata aongee)
"Ni...ni...ni...nilikuwa namuomba funguo za baadhi ya vyumba nikachukue mashukaaaa, pliiz u...uu...siniue" (Anusiata aliongea kwa kigugumizi huku haja ndogo ikianza kumtoka)

"Na ulipoingia chumba namba 123, ulishuhudia nini?" (yule jambazi akauliza kwa ukali huku akimpa nafasi Anusiata ajieleze)

"Ha...ha...hapaaana si...si..jaona chochote mimi,unaniua bure" (Anusiata aliongea kwa sauti ila kelele za mashine ya kufulia ikawa imefanya asisikike hata nje)

"Kelele zako hapa hazitasaidia kitu alafu nilikwambia utulie. Na hicho kidole umekitoa wapi" (yule jambazi aliendelea kuuliza huku akimtaka Anusiata aache kupiga kelele)

"Nisamehe sitasema chochote mie, nakuahidi, sitaongea mimi.Niache usiniue" (Anusiata alizidi kujitetea huku akiwa hana matumaini tena ya kubaki salama)

"Sasa nisaidie jambo moja, humu ndani nipo na wenzangu, tulikodi chumba namba 129. Tuna mzigo wetu tunataka kutoka nao.Tuelekeze mlango wa siri wa kutoka hapa,na mimi nitakuacha salama.ukijifanya kiburi basi nakuua hapahapa," (yule mtekaji aliongea kwa msisitizo)

"Sawa sitosema chochote, twendeni nikawaonyeshe" (Anusiata aliitikia haraka ili kunusuru maisha yake)

Walitoka wote kwenye chumba kile cha kufulia huku akipewa maelekezo ya kujifanya yupo kawaida. Walitembea kama marafiki ingawa kila mmoja alikuwa na lake moyoni. Walitembea kama hatua 20 ndipo wakakifikia kile chumba walichopanga wale majambazi.
"Haya ingia humu" (yule mtekaji akaongea taratibu huku akimuangalia Anusiata)
"Boss, tushamaliza kazi huku na mzigo upo tayari. Ila tumeamua tubebe vyote vinne." (mmoja kati ya majambazi watatu waliopo ndani alikuwa akiongea na simu muda ambao anusiata na yule mtekaji wake wakiingia)
"Safi sana makamanda. Huyo mpuuzi alinisumbua sana, akadhani hatoingia kwenye kumi na nane zangu, hongereni vijana. Vipi lakini CCTV Camera muliweza kuzi-control?" (upande wa pili wa simu uliuliza)

"Ndio Boss, wale wanaohusika na camera tumewamaliza, na CAMERA RECORDER tumeondoka nayo. (kijana alizidi kueleza)

"Basi poa, tukutane ofisini mkitoka huko" (upande wa pili wa simu uliongea na kukata simu)

Baada ya maongezi yale, wakatoka katika chumba kile wote wanne na huyu binti wa usafi ambaye kwa mda huu sasa ndo muongoza njia jumla watano. Wakapita katika mlango ulioandikwa "EMERGENCY DOOR" ambao uliwafikisha katika lift na kushuka na hiyo lift hadi chini ya lile ghorofa. Walipotua wakapita nyuma ya ile hotel hadi pale walipoukuta mlango mwingine tena ulioandikwa "EMERGENCY DOOR" ambapo Anusiata aliufungua kwa funguo zake na wakatokea nje kabisa ya hotel ile.

"Sasa wadau, huyu binti tumfanye nini?, maana ashatutoa nje ya hotel (Yule jambazi mtekaji aliyemshikilia anusiata akawauliza wenzake)

"Tumuue tu, maana ameshaziona sura zetu" (mmoja akadakia na hapohapo akachukua bunduki yake yenye kiwambo cha kuzuia sauti na kummiminia Anusiata risasi zaidi ya nne kwenye kifua chake upande wa moyo)
"Jamaa, unakosea, hukutakiwa kumuua huyu binti bila kutusikiliza wengine tunasemaje, huyu angetusaidia kwa mapishi na usafi kule kambini" (yule jambazi aliyemteka Anusiata kule washing room akaongea huku akionesha kuchukizwa na kitendo cha mwenzake kumuua huyu dada)

"Acheni kulaumiana, mtu ameshakufa bas, muacheni hapo tusepe.( Mwingine akadakia huku akiusukumizia mwili wa Anusiata mtaroni)
Wakaondoka pale kwa kupita njia za vichochoroni na hatimae wakalifikia gari lao walilolipaki mtaa wa pili na kuondoka eneo lile.

.............................................................................................................................................................

NYUMBANI KWA MWAMBA WA CHUMA.

Ni nyumba kubwa ya kisasa, iliyopendezeshwa kwa bustani nzuri ya maua ya kila aina huku sanamu za wanyama mbalimbali kama simba,tembo na chui zilizochongwa kwa udongo zikizidi kupafanya mahali hapa paonekane kama ikulu ndogo. Ama hakika Mwamba wa chuma alijipanga kimaisha. Mshahara wake aliutendea haki, tofauti na wafanyakazi wengi ambao muda mwingi hufikiria starehe tu na anasa za dunia huku wakisahau kuwa ajira ni za muda mfupi tu, ipo siku utaziacha. Mbali na nyumba hiyo Mwamba wa chuma pia alikuwa na nyumba nyingine mbili zilizopo katika jiji la NAIBAS pamoja na vitega uchumi vingine vingi kama magari ya abiria, nyumba za kulala wageni na mashamba makubwa. Ama hakika, huyu ni Mwamba wa chuma kweli kweli, si tu kwenye fani yake ya upelelezi bali hata kwenye maisha nje ya fani yake.
Abdul Mohammed ni mtoto wa kwanza na wa mwisho wa Mzee Mohammed(Mwamba wa chuma). Ni mtoto pekee kwenye familia hii ya mzee Mohamed na mke wake Bi Nusrat au ukipenda muite Mama Abdul. Ni matatizo ya uzazi yaliyokuwa yakimsumbua Bi nusrat ndio yaliyosababisha wawe na mtoto huyo mmoja tu. Abdul mohammed ni msomi wa shahada ya pili (shahada ya uzamili) aliyoipata katika chuo kikuu cha sheria Bloomsbury London,Uingereza. Ingawa bado alikuwa akiishi na wazazi ila haikumfanya kutokuwa mchapakazi kama baba yake, sifa iliyopelekea na yeye kuingizwa katika kazi ya ushushushu ndani ya idara ya usalama wa Taifa la Beirad (BISA). Akiwa na miaka michache tu ndani ya Idara, aliweza kufatilia matukio mbalimbali ya yanayohatarisha usalama wa nchi na kuzuia majaribio kazaa ya uharifu.

Ni asubuhi na mapema, simu ya Mwamba wa chuma inaita. Anakurupuka kutoka usingizini na kuangalia mpigaji ni nani.
"Habari za asubuhi kamanda" ( sauti ilisikika upande wa pili baada ya Mwamba wa chuma kuipokea ile simu)

"Salama mkuu,vipi kuna tatizo?, naona asubuhi sana" (Mwamba wa chuma aliuliza baada ya kuona mpigaji ni Boss wake, Professor John Kluger)

"Nenda DP hotel kuna tukio la mauaji limetokea. Waliouliwa ni Waziri wa Afya Mh. Charles Jaden na familia yake pamoja na wafanyakazi wengine wa hotel" (Professor aliongea na kukata simu)
Mwamba wa chuma alijiandaa haraka na kumuacha mkewe akiwa bado anamalizia usingizi wa asubuhi. Akatafuta funguo ya gari anapowekaga na kuelekea moja kwa moja parking kutoa gari. Akiwa ndani ya gari lake,anageuka siti za nyuma na kukuta bahasha iliyochanwa upande mmoja.

"Hii bahasha ni ya nani tena, mbona jana nilisafisha gari lote na makorokoro yote nilitoa" (Mwamba wa chuma alijiuliza peke yake huku akiisogelea ile bahasha na kuivuta barua iliopo ndani)

"Habari yako Nguli wa ujasusi, najua una kiherehere cha kutaka kufatilia kila jambo. Naomba kwa hili la DP hotel hebu lipotezee. Kina cha hii bahari ni kirefu hutokiweza. Utapotea bure. AHSANTE" .Mwamba wa chuma alishituka baada ya kuisoma barua ile na huku akitafakari bila kupata majibu ya nani aliyeiweka ile barua na alijuaje kama asubuhi ile atatoka. Akaamua kuipotezea ile barua na kuendelea na safari yake kuelekea DP HOTEL.


NINI KITAENDELEA,
NANI AMEMTUMIA BARUA MWAMBA WA CHUMA?,
USIKOSE SEHEM YA TATU. AHSANTE.









Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom