Elton Tonny
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 412
- 3,059
MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Ysiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KWANZA
★★★★★★★★★★★★★
Maisha ni safari ndefu yenye kila aina ya changamoto, na hakuna mwanadamu yeyote azaliwaye kwenye sura ya dunia hii bila kuzipitia. Changamoto huja kwa nyuso tofauti-tofauti kwa kila mmoja, na kamwe haziwezi kufanana wala kuwa na uzito wa aina ile ile kwa watu wote wanaozipitia. Ikitegemea na hali, eneo, nyutu za watu, na mambo yanayowazunguka, sikuzote changamoto huwepo ndani ya maisha ya mtu kumsukuma awe na nia ya kupambana ili kujitoa ndani ya hizo na kuwa na maisha bora.
Tunaambiwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha bora lakini hata watu wenye elimu ya juu bado huhangaishwa na matatizo mengi yanayowakosesha amani. Kila mtu mmoja mmoja anatamani kufikia sehemu nzuri maishani kiasi kwamba hata wale waliozifikia sehemu hizo bado wanakuwa hawaridhiki. Ni tamaa yetu sote kuishi maisha yenye kuridhisha, lakini mivurugo ya maisha sikuzote huturudisha nyuma. Iwe ni kwa matajiri, au wenye hali za chini kiuchumi.
Kwa sababu ndivyo ambavyo sisi sote tumezaliwa na kukuta hali zikiwa namna hiyo tokea mwanaume wa kwanza alipoamua kumtandika ndugu yake mpaka akafa, imetubidi tuyaishi maisha kwa namna ambavyo yametutaka tuyaishi. Usione mtu anafanya jambo fulani ambalo linapingana na uasili wa kufanya mambo ukadhani hafai. La. Ni kwamba maisha ndiyo yamemfanya akaona kufanya jambo hilo kuwa sahihi. Analazimika kuishi kwa njia hiyo aidha kwa kupenda ama kusukumwa tu, maadamu aishi.
Hivyo kamwe huwezi kuhukumu maisha ya mtu kwa kumtazama tu bila kujua kiundani ni mambo yapi yaliyopelekea mpaka akafikia hatua za kuishi namna aishivyo. Kujenga taswira nzuri mbele ya jamii ni jambo la muhimu, lakini maisha yanapokulazimu kuishi kwa namna ambayo jamii itayahukumu vibaya, unachopaswa kufanya ni kula ugali wako na kuvuta shuka kulala, ili kesho uamkie mambo mengine na kuendelea kuishi. Basi!
Naandika haya mimi siyo chizi. Mimi siyo mtunga mashairi wala nini. Ila nimeona tu nijaribu kuzama zaidi ndani ya vina virefu visivyoelezeka kwa mapana sana kuhusu neno hili: maisha. Maisha hayawezi kufanana kwa kila mmoja. Hayawezi kuendana. Hayawezi kuingiliana kwa asilimia zote na kumfanya mtu wa hali ya chini aweze kuwa kama kiongozi wa nchi hii kwa ufanisi aupatao kutokana na jasho la huyo huyo "mtu wa hali ya chini."
Kila mtu ana kisa chake mwenyewe cha maisha. Alipo fulani sasa hakufika kwa muujiza, kuna sehemu amepita. Unaweza ukashangaa kwa nini watu wanahangaika sana kufatilia maisha ya watu maarufu zaidi. Ni kwa sababu tayari wameshajijengea umaarufu. Hawakuzaliwa nao, waliutafuta, wakaupata. Wanaoendelea kuwafuatilia tu wanaishia kuwa watu wa kutamani. Hata hao watu maarufu wamepitia changamoto nyingi maishani, lakini hakuna mtu hata mmoja aliyejisumbua kuzijua wala kuziulizia mpaka walipokuja kupata huo ufanisi na kuzigeuza changamoto hizo ziwe kitu cha kuwatia moyo wengine kupambana zaidi.
Hutajali saana kufatilia maisha ya ndani zaidi ya mwanamke abebaye sinia la karanga kichwani, akiwa amebeba mtoto mdogo mgongoni, sura yake ikiwa imechoka, akiziuza karanga hizo stendi ya mabasi na jua likiwa kali sana. Tayari tu una kitu ndani yako kinachojua kwamba ana changamoto zake, kama watu wote, kwa hiyo nawe utabaki kutulia na za kwako tu, si ndiyo? Angalau nunua hata hizo karanga basi, hata ya mia tu. Itampa faraja kuona kwamba hata kesho anaweza kujikwamua na kuendelea kupambana kuzivuka changamoto zake ili ajenge maisha mazuri kwa kiwango ambacho Mungu atambarikia kukipata.
Sina lengo la kuandika mahubiri ili muanze kutenga sura na mistari. Ni kwamba tu nimeangalia hata maisha yangu mwenyewe na kugundua kwamba kuna changamoto nyingi zilizo ngumu maishani mwa mwanadamu, na japo kwa wengi zinatofautiana, mapenzi ni suala lizushalo changamoto kwa KILA MTU. Kubali, kataa. Hakuna mtu apitaye upeo wa ujana bila kukumbwa na changamoto za jambo hilo. Kwa nini?
Kwa sababu hakuna lengo lolote la kuishi isipokuwa upendo. Ni kitu cha kiasili. Kila mtu anacho. Nazungumzia upendo wote, iwe ni wa kindugu, kirafiki, kishkaji, kihuni, vyovyote vile, ni lazima tu kuwe na changamoto nyingi sana. Sasa inapofikia kwenye ule upendo wa kijinsia ndiyo kabisaa! Watu mpaka wanauana kwa sababu ya kuumizwa na mapenzi.
Lakini kwa jinsi ambavyo mambo yamekuwa kufikia kipindi hiki, imeshaonekana kuwa jambo la kawaida sana kwa mapenzi kuwa kitu chenye kuumiza badala ya kutakiwa KUBAKI kuwa kitu chenye kuridhisha. Na kama nilivyosema mwanzoni, kwa sababu tumezaliwa na kuyakuta namna hiyo, basi ndiyo tunaendelea kuyaishi namna hiyo hiyo tu. Lakini kuyaishi namna hiyo hiyo tu si jambo linalofaa.
Ni muhimu kuishi kwa kusudi, na imenichukua visa vingi vilivyotokea katika maisha yangu mpaka kufikia sasa kutambua kwamba mapenzi ya kujifurahisha tu hayana faida yoyote. Yanapaswa kuwa na lengo. Lakini kwa wengi, hata MIMI, hutuchukua muda mrefu mpaka kuja kumpata mtu anayeweza kukufanya ulitamani sana lengo hilo, haijalishi ni changamoto za aina gani utakazopitia, maadamu akiwa na wewe, unajua yote unaweza kuyashinda....
★★★★
Ilikuwa ni kwenye siku ya Alhamisi, nikiwa ndani ya gari kuelekea eneo lingine la jiji la Dar es Salaam. Siku hii kama siku zingine tu ilionekana kuwa na ukawaida wa mambo mengi ya kutarajia kwa maisha tuliyozoea sisi wabongo, na ndani ya gari hili kulikuwa na kioja kilichochangamsha asilimia kubwa ya abiria waliokuwemo. Niliposema gari sikumaanisha nina gari hapa.
Hii ilikuwa ni ndani ya usafiri rahisi wa umma, ama daladala ndogo aina ya Costa, na kutokea nilipokuwa nimekaa siti ya pili kutokea mbele upande wa pembeni alikaa mwanamke mtu mzima kiasi, akiwa amevalia nguo ya batiki na kujifunga kiremba kichwani, masikioni kukiwa na vifaa vidogo vya kuunganisha sauti kutoka kwenye simu.
Bila shaka alifurahia muziki mzuri sana kiasi kwamba alikuwa akiimba kwa sauti ya juu kuufatisha, lakini ilionekana kwamba hakutambua sauti aliyotoa ilizidi kupanda. Watu kadhaa walimzungumzia, wakidhani angekuwa msukuma, walimcheka na kuendelea kumtazama tu, huku yeye akiendelea kuburudika na kudhani wanamfurahia sana kutokana na kuimba kwake.
Nilikuwa nimekaa upande wa kioo cha dirisha nikipulizwa zaidi na upepo uliokipisha kioo kilichokuwa wazi, mara kwa mara nikifungua simu yangu kutazama ujumbe ulioingia na kujibu, kisha kuifunga na kuendelea kutazama nje. Kuna jambo fulani kuhusu mimi ambalo sikuzote lilifanya watu wanitazame sana, na hata bila kujionyesha kwao kwamba wananitazama mno au mimi kutowaangalia, nilijua tu kwamba wangenitazama kwa wingi.
Sitaficha hili nikiwa ndiyo nimeanza kuelezea kisa changu. Sura niliyobarikiwa kuwa nayo ilipendeza. Wazungu huita wanaume wenye sura nzuri sana "handsome," na mimi kiukweli nilikuwa hendisamu. Siyo uzuri ule wa kujitahidi sana kuufikia, bali ule uzuri wa asili unaoonekana hata bila kujitengeneza baada ya kutoka kusinzia.
Labda kingine kilichozidishia jambo hilo utizami wa watu kunielekea ni kutokana na ngozi yangu kuwa nyeupe. Oh najua kuna watu huhangaishwa sana na rangi ya mwili, na ya kwangu ndiyo iliyoongeza utomato mtamu kwa sura yangu. Macho madogo yenye kope na nyusi nyingi kwa juu, pua ya kawaida na midomo yenye uwekundu isiyo ya denda nzito sana vilifanya nionekane kuwa kama mchina ama mwarabu kabisa!
Nywele zangu zikiwa ni laini, sikuzote nilipenda kuzichana vizuri huku pande za kichwa zikiwa zimepunguzwa kidogo sana kufikia nyuma ya usawa wa masikio yangu. Mwonekano wa kimwili ulikuwa wa kiume zaidi, lakini si ule uliopita kiasi. Nilifanya mazoezi kipindi cha nyuma kuujenga lakini kufikia hiki sikujihusisha na mazoezi kwa utaratibu kama ule wa kujenga mwili kuwa imara sana, kwa hiyo nilikuwa na mwili ambao ungeonwa kuwa mwembamba lakini mpana, na nilikuwa mrefu pia.
Kama ni jambo lingine lililoongeza hali ya mvuto kwangu na hata kwa watu niliopendelea kuchangamana nao, basi ilikuwa ni usafi. Kuanzia jinsi nilivyochonga ndevu zangu hafifu kutokea kwenye timba mpaka kidevuni, mavazi mpaka viatu, nilionwa kuwa mtanashati na bishoo, au sharobaro kwa watu wengi. Mwonekano wangu na jinsi nilivyojiweka tu mbele ya watu ilifanya kwa mtazamo wa kwanza yeyote afikiri nilikuwa mtu mwenye kujipa hadhi fulani ya juu, kama mtu mwenye kujisikia sana, na ni kitu ambacho nilikuwa nimeshazoea tangu zamani.
Hata sasa ndani ya safari hii, niligundua kuna watu ambao walipenda mwonekano wangu na kunitazama sana. Nilivalia T-shirt ya rangi ya zambarau iliyopauka yenye mikono mirefu, suruali nyeusi ya kardet, pamoja na viatu vyeupe miguuni. Manukato niliyojipulizia pia yaliongeza kiwango cha mvuto wa kiume niliokuwa nao, ila sikukazia fikira mno suala hilo na kuendelea kukaa kwa utulivu tu nikisubiri kufika kule nilikodhamiria kwenda.
★★
Gari liliendelea kutembea tu, likipita majengo na magari mengi ndani ya barabara pana kwenye jiji hili lililo na shughuli nyingi, na mara kwa mara msongamano wa magari ulifanya tukawizwe njiani kutokana na kusimama kwa muda mrefu barabarani. Joto likiwa kali mchana huu, angalau ndani ya daladala hii kioja cha mwanamke huyo kuimba kwa sauti ya juu kilifanya watu wafurahike zaidi, na alikuwa bize kweli kufatisha maneno ya kila wimbo alioufahamu.
Baada ya kutumia dakika nyingi sana gari likiwa limesimama sehemu moja tu, ikabidi dereva atumie akili nyingine. Akaliingiza gari kwenye barabara ya changarawe ambayo ingezungukia upande wa mbali kiasi ili kuweza kutokea mbele zaidi ya njia tuliyotumia kupita kwa ajili ya safari yetu. Hatukujua kilichosababisha foleni hiyo lakini lilikuwa ni jambo la kawaida sana kwa barabara za jiji hili.
Tukaendelea kusonga. Mdogo mdogo tu, huku mwanamke yule akikomaa kuimba "kekundu, kekunduuuu..." na baadhi ya wadau ndani ya gari wakiitikia pamoja naye, jambo lililofanya tabasamu hafifu liniponyoke midomoni mwangu maana ilikuwa ni kwaya moja ya kitambo kweli. Barabara hii ilifanya gari lipite kwenye kona zilizobanana sana kutokana na nyumba kadha wa kadha kukaribiana, kisha tukaingia sehemu yenye uwazi zaidi ambako miti mingi ilionekana na nyumba chache sana zilizoachana kwa umbali mfupi.
Baada ya dakika chache za mwendo huo wa gari kutembea kama linatubembeleza, likafika sehemu fulani yenye miti zaidi bila nyumba na kusimama baada ya kitu kama kishindo kusikika kutokea kule mbele kwa dereva. Watu wakawa wanauliza nini kimetokea, na sasa ikawekwa wazi kuwa gari liliharibika. Doh! Ikabidi wote tushuke na kusimama nje, huku kondakta na dereva wakijitahidi kulifanyia ukarabati ambao tulijua usingeleta matokeo ya haraka.
Nilikuwa nimebeba begi la mgongoni lililotuna kutokana na kuweka vitu vyangu vingi, nami nikawa nimesimama pembeni tu huku wengine wakijadili ya hapa na pale kuhusiana na jambo hilo. Angalau hata yule mama wa "kekundu" alipumzisha sauti yake wakati huu.
Ni magari machache sana yaliyoanza kupita usawa huu wa barabara, na yalikuwa yamejaa lakini abiria niliosafiri pamoja nao wakawa wanayapanda na kushonana hivyo hivyo ili yawaondoe sehemu hiyo upesi. Tukawa tunapungua tu, mpaka nikabaki mimi mwenyewe na dereva na konda.
Haikuonekana kuwa gari lingetengemaa, kwa hiyo wawili hao wakaanza kuondoka pamoja nami, tukitembea kuelekea mbele zaidi na kuomba kukutana na bodaboda maana magari yaliacha kupita; ikionekana labda foleni ile barabarani ilikuwa imekata.
Kweli tukawa tumepata bodaboda moja, na wawili hao wakanishauri nipande na kwenda zangu lakini mimi nikawaambia wapande tu kwa sababu nilitaka kutembea kidogo, na bila shaka ningepata tu bodaboda nyingine. Wakaridhia na kupanda pikipiki hiyo pamoja, fyuu wakaishia. Nilidhani ingekuwa rahisi tu kutoka ndani ya eneo hilo lakini muda si muda nikatambua kuwa nilikosea.
Njia hii tuliyopita haikuwa rasmi, si kama barabara rasmi za changarawe, na kwa kuwa huko mbele haikuja bodaboda nyingine tena, nikajikuta nimeachwa peke yangu eneo lililoonekana kuwa kama linaelekea kwa Mzee Tambitambi. Mh? Hapana. Kuwa mwanaume na mengi hakukumaanisha nifanye tu vitu bila kujali hali yangu nzuri, kwamba niende mbele tu kwa ujasiri na kujikuta nimeingia nisikokujua, hivyo kwa busara nikaamua kurudi kule nilikotoka.
Nikaenda tena mpaka pale ambapo tuliiacha Costa ile, nami nikajiketisha kwenye nyasi safi na laini chini ya mti wenye kivuli kizuri. Ilionekana kama vile siku hii niliamuliwa maana hakuna usafiri mwingine wowote uliopita tena upande huo. Dakika zikawa saa, saa zikawa masaa, na mchana ukaanza kugeuka kuwa jioni.
Nikajiuliza hii ilikuwa ni adhabu gani ya ghafla namna hii. Yaani from nowhere tu eti magari na pikipiki zikaacha kupita ndani ya eneo nisilofahamu vizuri, na hakuna hata nafsi moja iliyoonekana. Hapa pasingeendelea kukalika maana saa moja ilikuwa inaingia, hivyo wazo la kurudi na barabara tuliyokuja nayo kwa Costa likawa suluhisho zuri kwa wakati huu. Ningehitaji tu kufika eneo lenye makazi kiasi na kutokea hapo ningejua nini la kufanya kupata usafiri mwingine.
Taratibu nikaanza kutembea, begi likiwa mgongoni kwangu, simu ikiwa sikioni kuniruhusu nizungumze na msela wangu mmoja, ambaye alinicheka kwa kusema nimelaaniwa kukutwa na saibu hili, na bila shaka ningekutana na Basilisa huko mbele kwa hiyo eti angeandaa masufuria ya kuchemshia uji wa msiba wangu huko nilikotoka!
Nikiwa bado nasonga taratibu, sauti ya kuunguruma kwa pikipiki kutokea nyuma yangu ikanifanya nigeuke kuitazama, nami nikaingiwa na matumaini. Ilikuja upande wangu kutokea eneo hilo nilikoiacha ile Costa, nami nikaipungia mkono ili mwendeshaji asimame, lakini nikashangaa ananipita tu na kunyoosha mbele. Khh!
Nikatoa begi mgongoni na kusimama hapo. Giza lilikuwa limeshaingia kiasi, nami nilihisi njaa, na kwa kutazama taa za jiji mbele zaidi nikajiamulia kutakiwa kusonga tu ili nifikie sehemu yenye shughuli maana bahati nyingine isingekuja. Lakini Mungu si Athumani bwana, gari lingine dogo likaonekana likija kutokea huko nilikopaacha, nami nikapunga mkono lisimame lakini nalo likanipita tu. Kweli Mungu siyo Athumani!
Hali hii ikaniudhi, lakini nikaelewa vizuri upande wa pili wa mambo. Kikawaida, sehemu kama niliyokuwepo ilionekana kuwa na uhatari, labda wa vibaka, ukitegemea pia na muda, hivyo watu wasingekuwa wenye urafiki sana kwa mtu wasiyemjua na kusimamisha tu vyombo vyao kumsaidia; maana hofu ya kupatwa na madhara ilikuwepo kwa wote. Kwa hiyo ikanibidi nifikirie njia mbadala ya kujiondoa sehemu hii haraka kwa usafiri kabla usiku haujawa mzito zaidi.
Nilipopiga tu hatua zingine chache huku begi langu nikilining'iniza mkononi, gari lingine likasikika likija kutokea nyuma yangu. Sikugeuka. Nikaanza kutembea kwa kuyumba kiasi, kama mlevi, kisha nikaliangusha begi chini na kujishika kifuani, nikianza kuguna kwa sauti ya juu na kujiingiza barabarani kwa njia iliyoonyesha nakaribia kuanguka. Haya yalikuwa maigizo tu, na kama sikuwa nimeweka hili wazi mwanzoni, unapaswa kujua kwamba nina utundu fulani pia. Wengine huuita uhuni. Ila nilikuwa mhuni ilipohitajika tu.
Nilikuwa makini kutambua umbali ambao gari hilo lilifikia, na sasa likiwa karibu zaidi na nilipokuwa, nikajiangusha barabarani huku nikilinyooshea mkono lisimame maana nilikuwa na tatizo la kifua. Maigizo tu! Ikiwa aliyekuwa ndani ya gari hilo alikuwa na moyo mzuri, basi angenionea huruma na kushuka kuja kunipa msaada, hivyo ningeweza kupata lifti kwa wepesi. Akili mtu wangu!
Jaribio langu likazaa matunda mazuri pale gari hilo liliposimama, nami nikajisemea "Yes!" na kisha kuendelea kulia kwa maumivu makali chini hapo. Sikufumbua macho yangu na kuendelea kuigiza tu, nami nikasikia mlango ukibamizwa kidogo, kuashiria umefungwa baada ya kufunguliwa. Nikafungua jicho moja kiduchu na kuona kwamba kuna mtu alikuja upesi, nami nikafumba tena na kuendelea kulia.
"Oooh... aaah!"
Nikahisi shingo yangu ikishikwa kwa viganja na kunyanyuliwa kiasi ili kichwa changu kiwe juu, na sijui ni nini tu kilichofanya nisikazie fikira sana suala hili lakini mikono hiyo ilikuwa laini, na harufu ilikuwa nzuri sana.
"Kaka... nini tatizo?"
Sauti hiyo nyororo ikanifanya nifumbue macho yangu na kumtazama aliyeitoa, na kwa sekunde chache nikajisahau kwamba nilikuwa naumwa. Nilimtazama mwanamke huyo usoni kwa ufupi tu, lakini nilihisi ni kama nimemwangalia kwa muda mrefu. Alikuwa na sura nzuri. Mweupe, yaani mweupe. Mtu mzima kunipita hadi mimi kiumri, lakini kama angeamua kudanganya yeyote yule kwa kusema ana umri mdogo, hata mimi ningekubali.
Alikuwa na macho mazuri ya ufilipino fulani hivi na ya kungu kiasi, midomo laini na mizuri, na nywele zake zilikuwa zake, ndefu kufikia mabegani ambazo bila shaka alizilainisha zaidi kwa dawa. Uso wake mweupe wenye kujali sana ulionyesha huruma nyingi kunielekea, naye alikuwa anatumia kiganja kimoja kupima joto la mwili wangu kwa kukiweka kwenye shingo na paji la uso wangu.
Nikafumba macho yangu tena na kuendelea ku "Oooh... nakufaaa..." naye akanishika usoni kwa kiganja chake.
"Kaka... nini kinakusumbua?" akauliza hivyo.
Sauti yake ilikuwa tamu sana, kama ya mtoto mdogo vile ama ile ya Wema Sepetu anayobania puani.
"Aah... kifua dada... kifua kimekaza..." nikatoa lawama zangu.
"Pole sana. Naomba ujitahidi kusimama nikuingize kwenye gari tukatafute hospitali, hapo mbele tu, eti?" akaniambia.
Nikalibana tabasamu langu na kusema, "Sawa."
Kisha nikaanza kujinyanyua, naye akanipa egamio na kutembea nami mpaka upande wa mlango wa pili wa gari lake. Gari lake lilinishangaza kiasi. Ilikuwa ni zile pickup Toyota za zamani kweli ingawa ilikuwa safi, nyeupe, lakini haikuonekana kuwa gari iliyomfaa mwanamke mwenye uzuri wake. Kwa vyovyote vile hilo halingejalisha kwa kuwa sasa nilipata lifti.
Nikakalishwa siti ya upande wa mbele pembeni ya usukani, kisha mwanamke huyo akaniacha na kuelekea pale aliponitoa. Nikamwangalia na kuona akiliokota begi langu na kuanza kuja nalo upesi kwenye gari, naye akaingia pia kwenye usukani na kuliweka kwenye siti za nyuma. Akaingiza gia na kukanyaga mafuta, nalo gari likaanza kutembea tena huku bado nikiwa nimekaza sura na kuonyesha nina maumivu sana.
"Pole kaka. Una... unakaa wapi... umetokea wapi?" akauliza.
"Nilikuwa... natokea Bamaga kule..."
"Sinza?"
"Ndiyo... usafiri ukaharibikia hapo nyuma... ndiyo nikabaki mwenyewe mpaka oooOOH!" nikaendelea kujikata na wembe bandia.
"Pole... ngoja nikuwahishe hospitali ya karibu," akasema hivyo.
Nikafumbua jicho moja na kumtazama kwa chini, na alikuwa makini kweli kwenye uendeshaji akionekana kutaka kuharakisha kututoa huku. Nikaangalia upande wa nje na kutabasamu tu, kisha maigizo yakaendelea hadi tulipoanza kuzipita nyumba zile zilizokaribiana. Nikaelewa haingechukua muda mrefu kufikia barabara kuu, nami nikamtazama mwanamke huyo tena.
Isingekuwa ya mazingira tuliyokutana kuwa jinsi yalivyokuwa, basi angefaa sana kuwa rafiki mzuri. Alionekana kuwa mwenye kujali, nami nikawaza kuwa bila shaka angekuwa na watoto aliowatendea vizuri mno. Lakini kwa upande mwingine, kufanya naye urafiki ingekuwa ni jambo gumu maana tayari nilimdanganya kuumwa ili tu nitimize haja yangu ya kutoka eneo lile, kwa hiyo ningepaswa kuhakikisha namkimbia kwa spidi zote akishanifikisha huko mbele.
Kweli dakika si nyingi tukawa tumeingia barabara kuu za lami, naye akaonekana kupita kwenye njia ambayo ingetufikisha kwenye moja ya hospitali kwenye maeneo ya Buguruni. Nikiwa sitaki hilo kitokee, nikaanza kumpiga-piga taratibu kwenye mkono wake, naye akanitazama huku bado akiendesha.
"Nishushe dada..." nikamwambia hivyo huku bado nikiwa nimekunja sura.
"Wapi?" akauliza.
"Hapo tu hivi..."
"Lakini hali yako ni mbaya... unatakiwa kufika hospitalini kwanza..." akaongea kwa kujali.
"Hhh... nishushe... nahitaji hewa kidogo..."
"Upepo si unaingia vizuri hapo?"
Nikamtazama kwa konyezo na kuona jinsi alivyokuwa makini, nami nikasema, "Na juice..."
"Juice?"
"Ndiyo... huwa inatuliza moyo..."
"Ni... moyo au kifua?"
"Ah... vyote! Ooooh!" nikaendeleza uwongo wangu.
Akaonekana kujali zaidi hali yangu, naye akalipeleka gari sehemu ya kuegeshea barabarani ambako hakukuwa mbali na viduka vidogo vya bidhaa. Kwa upande aliosimamisha gari, ule wa pili ulikuwa na majengo ya makao makuu ya kampuni ya Azam, na magari mengi ya abiria yalipita na kusimama kushusha na kupakia abiria.
Mwanamke huyu akataka kushuka ili aende kunifatia juice lakini akashangaa baada ya mimi kuufungua mlango wa upande nilioketi na kutoka ndani ya gari. Akabaki kuniangalia mpaka nilipofungua mlango wa nyuma na kulitoa begi langu, kisha nikaufunga na kusogea hapo mbele; nikiinama kiasi kumchungulia.
"Asante sana dada. Mungu akubarikiii!" nikamwambia hivyo huku nikitabasamu.
Alikunja uso wake kimaswali kiasi, naye akasema, "Wewe... uko... uko..."
"Niko sawa," nikamalizia maneno yake.
"Kifua hakiumi tena?"
"Kimeacha sasa hivi tu. Niko poa kabisa. Endelea tu na safari dada na Mungu atakulipa kwa ukarimu wako. Mmmwah!" nikamwambia hivyo na kumrushia busu kwa kiganja.
Alionekana kushangazwa sana na hili, naye akaangalia pembeni kiasi na kusema, "Ulikuwa unadanganya."
"Oh... siyo kudanganya yaani... ni... ile ilikuwa ni njia ya kukuomba msaada maana hakuna aliyetaka kunisaidia hata lifti tu. Ila wewe una moyo mzuri sana dada yangu, yaani hadi ukanipima na joto... hahahah... msaada mdogo tu lakini nimefarijika sana. Utabarikiwa milele," nikamwambia kwa shauku.
"Kwa hiyo... umenipotezea muda wangu, nafikiri unaumwa kumbe..."
"Ona ninaweza kukulipa kama unataka," nikamkatisha.
"Nini?"
Nikatoa wallet yangu na kuchomoa pesa, kisha nikamnyooshea huku nikisema, "Time is money. Pole kwa kuchelewesha ulikokuwa unaenda ila chukulia hii buku mbili kama nauli ya kunibeba kulipia huo muda, mm? Shika."
Akanikazia macho yake na kuniuliza kwa sauti ya chini, "We' ni mjinga?"
"Aaa, usiwe hivyo sister. Huku ni kusaidiana tu. Eh? Nimesema asante na pole hii hapa nakupa. Chukua. Ama niendelee kuigiza nimenigwa kidogo? Eerrgh hahahah..." nikamwambia hayo na kumtania kidogo.
Akaniangalia kwa kutoamini fulani hivi, kisha akakanyaga mafuta na kuliondoa gari bila kuichukua elfu mbili niliyotaka kumpatia.
Nikaendelea kulisindikiza gari lake kwa macho, nami nikashusha pumzi na kusema kwa sauti ya chini, "Asante."
Aliistahili asante hiyo ingawa hangeisikia wala kuijali tena kwa sababu nilikuwa nimemkosea. Nikatoa kitambaa changu safi na kuanza kujifuta hapa na pale kwenye suruali yangu nyeusi ya kardet, iliyochafuka kiasi kutokana na kujilaza chini nilipomfanyia maigizo mwanamke huyo. Nikaangalia saa yangu kwenye simu na kukuta ni saa mbili kasoro sasa, nami nikasimama sehemu ambayo ingeleta daladala za kuelekea kule nilikodhamiria kufika kwa siku hiyo.
Daladala ikaja, nami nikapanda kwa kusimama pamoja na abiria wengine ambao kama kawaida wangenitazama mara kwa mara kuonyesha nilikuwa mtu mwenye utofauti fulani kutokana na sura yangu. Vuuu... gari likapita eneo moja baada ya lingine huku nikiwa nimebanwa kiasi na watu niliosimama pamoja nao, na hatimaye tukafika maeneo ya Rangi Tatu, huko Mbagala, nami nikashuka hapo.
Kwa jiji letu kufanya matembezi sehemu mbalimbali kipindi cha nyuma kulifanya niyajue maeneo mengi, lakini Mbagala ndiyo kati ya maeneo ambayo sikuwa na mazoea nayo kabisa. Hata safari hii fupi kutokea kule nilikoishi ilinibidi niwe nimefanya utafiti wa jinsi ya kufika huku, kwa sababu kuna sehemu hususa niliyokuwa nikielekea.
Isingekuwa kucheleweshwa kule kwa usafiri niliochukua mara ya kwanza basi ningewahi kufika nilikohitaji kufikia, kwa hiyo baada tu ya kushuka nikatafuta daladala nyingine ambayo ingenipeleka kwenye eneo la mbele zaidi lililojulikana kama Mzinga.
Mapema nikapanda gari za Toangoma na mwendo ukaanza. Sikuzote nilifurahia hali fulani ya ugeni nilipoingia kwenye maeneo ambayo sikuyafahamu vizuri, kwa hiyo nilikuwa makini kutazama mambo mengi ya maeneo haya. Hakukuwa na purukushani nzito kama maeneo ya Kariakoo ama maghorofa mengi na vitu maridadi mno, bali mwonekano wa hali ya kawaida ulioitofautisha Mbagala na maeneo mengine yaliyofanisika zaidi.
Dakika kama kumi tu nasi tukawa tumefika Mzinga, nami nikashuka pamoja na wale walioshukia hapo. Bila hata kusumbuka, bodaboda zikanikimbilia, nami nikachagua moja na kumpa maelekezo dereva anipeleke sehemu iliyojulikana kama Masai. Nikapanda, mwendo ukaanza.
Nadhani ni ugeni wa mtu kama mimi kwenye eneo hilo uliofanya wengi wa watu tuliowaopita wanikodolee sana, na upesi nikatambua kwamba vijora ndiyo vazi lililopendelewa zaidi na wanawake wa huko. Nilikuwa makini kukariri njia tuliyotumia kupita mpaka kufika Masai, ingawa ilikuwa giza. Hiyo Masai ilikuwa ni bar pana kiasi yenye ghorofa moja juu na vyumba vya wageni. Tayari kwa muda huu wa saa mbili palikuwa pameshachangamka, muziki ukiwa mnene, na wengi wa waliokuwemo kule ndani waliniangalia sana baada ya kuniona.
Nikamlipa boda, naye akatoweka. Nafikiri wengi walikuwa wanasubiri kuona nikienda pale aidha kunywa ama kuchukua chumba cha kupumzikia kutokana na kuwa sura mpya kwenye eneo lao na kubeba begi mgongoni. Lakini Masai haikuwa shabaha yangu. Nikasogea pembeni na kutoa simu, nami nikatazama ramani ndogo ya nyumba iliyokuwa karibu eneo la bar hii. Nilikuwa na mpango wa kufikia kwenye nyumba hiyo ambayo mwenye nayo alikuwa ametoa tangazo siku chache nyuma kuwa angepangisha mtu hapo.
Ilikuwa ni sehemu sahihi kwangu kutaka kufikia kwa sababu nilitaka mazingira mazuri ya unyumbani, siyo chumba cha kupanga, bali kama alivyoonyesha kwa tangazo lake nililoliona mtandaoni, ilikuwa ni sehemu ya kukaa kama nyumbani. Yaani, kungekuwa na sebule yenye vitu kama samani na makochi tayari, chumba chenye kitanda, bafu, choo, maji, umeme, mambo kama hayo. Na gharama yake ilikuwa nafuu kwa kila mwezi.
Tayari nilikuwa nimeshawasiliana na mwenye kutoa huduma hiyo kwa njia ya WhatsApp na kukubaliana naye kwamba ningekuja hapo siku si nyingi ili asije kumpa mteja mwingine nafasi hii niliyoitaka mimi, naye akawa ameridhia. Kwa hiyo baada ya kuona uelekeo ambao nyumba hiyo ilikuwa, nikaanza kuelekea huko taratibu.
Mtaa huo kwa usiku ulionekana kuwa kimya kiasi, na nyumba nilizozipita zilikuwa za kawaida sana, vijia vyenye uchochoro mwingi, yaani mwonekano sahihi wa uswahilini. Kidoti chekundu cha ramani kikanifikisha mbele ya nyumba hiyo, nami nikaiangalia kwa umakini.
Kutokea nje, ingeweza kuonekana kuwa kubwa kiasi, ikiwa imezungushiwa kuta iliyoitenganisha na nyumba nyingine pembeni lakini kwa ukaribu sana. Geti lilikuwa pana na jeusi. Ningeweza kuona madirisha mapana yaliyowekewa vioo vyeusi, ungo wa king'amuzi cha Azam huko juu, na taa nene ya nje iliyomulika vyema mpaka kufikia niliposimama. Bila shaka palikuwa ndiyo penyewe.
Kupiga jicho upande mwingine wa nyumba za waswahili, nikaona wanawake kadhaa wakiwa wamesimama, wengi wao wakijifunga mikhanga tu kuanzia kifuani, wakiniangalia kama hawanijui. Ah kweli walikuwa hawanijui.
Hivyo nikaenda zangu mpaka kwenye geti hilo na kuligonga kwa wepesi kiasi, nami nikabaki kusubiri. Sikuwa nimeona haja ya kumtafuta mwenye nyumba kwa simu tena maana alisema kuwa muda wowote ule ambao nilijisikia kufika kwenye nyumba hiyo basi ningeenda tu, na ndiyo muda wenyewe ukawa huu. Sauti ya kifungulio kidogo cha mlango wa geti ikasikika baada ya sekunde chache, nao ukafunguka.
Mbele yangu alisimama mwanamke mtu mzima vya kutosha kunizaa, labda hata mara mbili. Umri wake kwa kukadiria ungekuwa wa miaka 50 ya mwishoni na kuendelea, naye alikuwa na ufupi wa kadiri, mnene kiasi, mwenye ngozi yenye weupe uliofifia, na macho yake mazuri yalinitazama kwa umakini.
"Mama shikamoo..." nikampa salamu kwa heshima.
"Marahaba. Hujambo?" akaniitikia.
"Sijambo," nikamwambia.
Alinitazama kwa umakini sana, akiwa kama ananitafakari, nami nikawaza kwamba huenda ndiye aliyekuwa mwenye nyumba, hivyo ingenibidi nimweleze mimi ni nani.
"Pole kwa kuwa nimefika usiku mama, gari niliyokuja nayo iliharibikia njiani. Mimi ni...."
"Ndiyo wewe kumbe?" akanikatisha kwa kuniuliza hivyo.
Kwa kufikiri anamaanisha kile nilichowaza, nikamwambia, "Ndiyo mama, ni mimi."
Akanishusha na kunipandisha huku akitabasamu kiasi, nami nikatabasamu pia kirafiki.
"Umekuja mwenyewe?" akaniuliza.
Sauti yake ilikuwa yenye upole mwingi sana, nami nikasema, "Ndiyo, niko mwenyewe. Gari lisingeharibika nisingechelewa kufika, ila hata hivyo haukujua kama ningefika leo japo nilipanga kufika mapema."
"Ahah, hamna shida baba, nilijua unakuja. Sema... karibu ndani kwanza. Jamani! Utakuwa umechoka kweli..." akasema hayo huku akinipisha ili nipite.
Mh? Sikutarajia angefahamu kwamba nilikuwa nakuja leo lakini njia yake ya kunikaribisha ilikuwa nzuri sana, nami nikaingia tu na kusogea mbele kidogo. Akafunga mlango wa geti na kusogea usawa wangu.
"Pole baba jamani... karibu sana. Twende ndani upumzike kidogo," akaniambia.
"Asante," nikashukuru.
Akaniongoza kufikia ubaraza uliojengewa vigae sakafuni, nami nikaona viatu kadhaa chini hapo kunifanya nitambue kuwa huko ndani kulikuwa na watu wengine zaidi. Labda wengine wa familia yake ambao waliishi naye, na mimi ndiyo ningeongeza idadi kwa kuja kukaa hapo. Yote yalikuwa sawa kwangu, nasi tukaingia ndani ya nyumba hiyo pamoja. Alinisihi niingie na viatu tu nilipoashiria kutaka kuvivua, na baada ya kufika sebuleni akanikaribisha nikae kwenye sofa moja.
Sebule haikuwa pana sana lakini ilikuwa pana. Masofa yalikuwa matatu na marefu yaliyopangwa kwa njia ya ukuta uliozunguka meza ya duara yenye kioo cheusi na kizito hapo katikati. Sofa nililoketi lilinitazamisha moja kwa moja na TV ndogo tu ya flat screen ukutani, na juu kiyoyozi kilionekana kuzunguka na kuipa sebule ubaridi ulioleta ahueni kutokana na joto la jiji hili.
Upande wa nyuma wa sofa nililokalia kulikuwa na sehemu pana iliyokuwa ya lengo la kulia vyakula (dining), na hapo niliona meza ndefu kiasi ya mbao, iliyozungukwa na viti sita vilivyoibana kwa ukaribu. Pembeni na hapo kulikuwa na friji yenye urefu wa kadiri na yenye rangi ya njano, pamoja na sehemu yenye uwazi wa mlango usiokuwa na mlango, ambao ulionyesha uelekeo wa kwenda chumba cha jikoni kutokea hapo 'dining.' Kampangilio kalikuwa kazuri kweli, na safi sana.
Kwenye sofa la upande wa kulia alilala binti mwenye umri mkubwa kufikia miaka 20 hivi, akiwa makini tu kutazama runinga bila kujali kwamba kuna mgeni aliingia. Alivaa dera lililousitiri vyema mwili wake, na kwa kumwangalia haraka nikatambua alikuwa mweupe na mwenye sura nzuri. Alitulia kivyake tu akitazama tamthilia huku aking'atang'ata kucha moja ya kidole chake kiganjani.
Mwanamke yule aliyenikaribisha akasimama pembeni yangu na kusema, "Karibu sana baba'angu."
"Asante mama," nikamwambia.
"Ngoja nikuletee kitu cha kupoza koo kwanza, eti?" akaniambia.
Nikatabasamu na kusema, "Asante sana."
Angekuwa amefanya jambo la maana kwa kuwa sikuweka chochote kile tumboni tokea nilipokunywa chai asubuhi, kwa hiyo kama ni juice angeileta tu nami ningeishusha vizuri sana. Akaondoka na kwenda upande ulioonekana kuelekea jikoni, nami nikakaa kwa utulivu na kumtazama binti yule pembeni. Alionekana kutojali kabisa wageni, nami nikawaza huenda alikuwa mwenye nyodo kupita maelezo.
Sekunde chache kupita na mwanamke yule akawa amerejea tena, isipokuwa wakati huu akawa amekuja pamoja na mwanamke mwingine aliyeonekana kumzidi mpaka na yeye kiumri kiasi. Huyu hakuwa mweupe, bali mweusi wa maji ya kunde, naye alikuwa na nywele fupi zenye mvi kiasi kichwani kwake.
Yule aliyenipokea mara ya kwanza alibeba sinia lenye glasi iliyowekewa juice, bila shaka ya parachichi, pamoja na sahani yenye wali na nyama iliyoonekana kuungwa vizuri sana kutokana na namna ilivyonukia. Yaani vilitamanisha sana, na kwa njaa niliyohisi ningekula mpaka kusafisha sahani yote. Ni kama alijua!
Sikutegemea mapokezi yangu kwa hapo yangekuwa mazuri namna hiyo kutoka kwa watu wazima kama hao, lakini lilikuwa ni jambo la kawaida kwangu mimi kutendewa kwa njia nzuri na watu wengi. Siyo wote, ila wengi. Kwa hiyo sinia hilo likawekwa mezani, nayo ikavutwa mpaka kuifikia miguu yangu, na wanawake hao wakawa wamesimama pembeni huku wakinitazama kwa njia fulani ya... matumaini.
Nikatabasamu kidogo na kusema, "Asanteni sana. Shikamoo mama?"
Nilikuwa nikimsalimu yule mwanamke mwingine, naye akasema, "Marahaba kijana wangu. Karibu sana, jisikie umefika nyumbani."
Nikatikisa kichwa kukubali ukaribisho wake.
"Karibu chakula baba. Pole kwa safari," yule mwanamke mweupe akaniambia.
"Asante."
Kiukweli nilikuwa nimesema asante nyingi sana kwa jioni hiyo, nami nikaanza tu makamuzi taratibu huku wanawake hao wakiwa wamesimama tu na wakiniangalia. Niliona hilo kuwa ajabu kiasi lakini labda hawakuzoea sana ugeni wa wanaume, tena hasa kutokana na mwonekano wangu.
Oh, kwangu mimi sura niliyokuwa nayo ilikuwa kawaida sana, lakini kwa wengine ilikuwa kama vile kigezo fulani cha kuwafanya wanitendee kiyaiyai. Nilitamani kuwaambia watu hawa wazima wakae, lakini tena nikajizuia maana sikuona hilo kuwa adabu kutoka kwa mgeni aliyefika tu na kuanza kujifanya mjuaji. Wafanye vile walivyojisikia.
"Kwa hiyo... haukuja na Shadya?"
Swali hilo lilitoka kwa yule mwanamke mweupe aliyenipokea mwanzoni, nami nikamtazama machoni. Sikuelewa Shadya ilikuwa ni nini, ila nikadhani amemaanisha jina la gari la usafiri kama Mohammed Trans.
"Aa... hapana... sijaja na Shadya. Nilipanda tu daladala, nikaifata ramani ndiyo nikafika. Ni mara yangu ya kwanza," nikawaambia.
Waliangaliana kimaswali kiasi, mimi nisijue sababu, lakini nikaendelea zangu tu kula.
Yule mweusi kiasi akasema, "Tulifikiri ungekuja labda hata na... ndugu zako..."
"Ndugu? Hamna... ni mimi tu mama. Nimekuja kukaa huku peke yangu," nikasema.
"Umekuja... kukaa huku?" akauliza yule mwanamke mweusi.
"Ndiyo. Nafikiri tutaanza kuzungumza kuhusu gharama na kila kitu nimeshaandaa. Nimalize kwanza kula, eh?" nikawaambia.
Yule mweupe akatabasamu kwa furaha na kusema, "Sawa baba. Wewe kula tu. Tutaongea mengi zaidi Miryam akishafika."
Nikakunja uso kimaswali kiasi na kuuliza, "Miryam?"
"Ndiyo. Na yeye amekawia kidogo tu, ila amesema yuko karibu kufika," mwanamke mweupe akaniambia.
Nikaangalia pembeni kiufupi, nikiwa sijaelewa vizuri jambo hilo, na yule mwanamke mweusi alinitazama kwa umakini zaidi tofauti na yule mweupe ambaye aliniangalia kwa furaha zaidi.
"Miryam ndiyo... mwenye nyumba?" nikawauliza.
Wakaangaliana machoni kwa njia ya kuulizana jambo fulani, kisha wakanitazama tena na yule mwanamke mweusi akasema, "Eee... ndiyo... Miryam ndiyo... ndiyo mwenye nyumba."
"Mmmm... sawa basi, haina shida. Nitamsubiri ili tupangane vizuri. Nimepapenda sana hapa," nikawaambia hivyo.
Nikakirudia chakula changu na kuendelea kushuka nacho taratibu, nami nikamwona mwanamke yule mweusi akimpa kiashirio mwenzake kwa kumvuta ili waondoke hapo. Nikawaangalia, naye akasema wanaenda kuandaa mambo fulani kisha wangerudi tena, na mimi ningekuwa nani kuwazuia? Nikasema sawa, nao wakaishia kwenye kona upande mwingine ndani hapo.
Nikaendelea kula na kumwangalia binti yule tena, na bado alikuwa anatafuna tu kucha. Nilipomwangalia vizuri zaidi nikaanza kuona kwamba hali yake haikuwa sawa kwa asilimia zote, lakini nisingeweza kukisia haraka ikiwa alikuwa na tatizo fulani. Macho yake yaliielekea TV, lakini ni kama umakini wake haukuwa kwenye kile kilichoonyeshwa humo.
Nikataka nimsemeshe, lakini ndiyo hapa nikaanza kusikia maongezi baina ya wale wanawake wawili walioondoka muda mfupi nyuma. Nikatambua hawakuwa wameenda chumbani kabisa, bali walisimama nyuma ya ukuta uliowaficha kutokea hapo sebuleni.
Sauti ya chini ya mwanamke yule mweupe ikasikika ikisema, "Dada jamani, huyo kaka ni mzuri! Eh! Sijawahi kuona."
Sauti ya mwenzake ikasema, "Mbona kama mdogo sana?"
"Kinachofanya ufikiri ni mdogo nini?"
"We' humwoni? Anaonekana hadi kutakiwa kumwamkia Mimi."
"Mh? Hamna bwana. Halafu kwani kuna ubaya gani? Sema ni kasura kake tu ndiyo kanamfanya anaonekana mdogo, lakini hata Shadya alisema ni mkubwa. Sidhani kama alikosea. Mimi nimempenda sana jamani..."
"Ndiyo, ni mzuri ila, mbona kama haelewi-elewi mambo? Tunamuuliza hiki, yeye anajibu vingine, kama anavuta sijui..."
"Atakuwa amechoka tu, halafu anaonekana ana njaa, hajala muda huyo..."
"Lakini..."
"Acha hizo bwana. Kijana wetu amechoka tu, tumsubiri Miryam mengine tutajua. Dada nina furaha SANA!"
Mh? Hayo yote niliyasikia, nami sikuweza kuelewa kabisa maongezi hayo mafupi yalilenga suala gani haswa. Kulikuwa na ishu gani nyingine zaidi ya mimi kuja kupangishwa kwenye nyumba hii iliyomfanya mmoja wa wanawake hao afikiri kuwa sielewi mambo, ama navuta bangi? Shadya ndiyo alikuwa nani badala ya nini?
Ningehitaji kujua undani wa mambo hayo ili nisije kujikuta nadumbukia kwenye masuala mengine kabisa tofauti na yaliyonileta huku, na wao kuanza kuja tena kukanifanya nijiandae kuzungumza nao kwa kina kuhusu makazi yangu ya muda mfupi kwenye nyumba hii. Nilitaka kujua ningelala kwenye chumba kipi ndani hapo, na mambo ya kawaida ambayo ningeshiriki kufanya kama mwanajamii mpya katika eneo hilo. Basi.
Waliponifikia tena, walikuwa wakitabasamu tu, bila kujua kwamba mengi ya yale waliyozungumzia niliyasikia, nami pia nikatabasamu na kuigiza kutojua lolote. Tayari nilikuwa nimefuta wali wote na nyama, ikibaki tu juice ya kuendelea kushushia.
"Asanteni sana jamani," nikawaasante tena.
"Nikuongezee ubwabwa?" yule mwanamke mweupe akaniuliza huku akija kuchukua sahani.
"A... hapana. Nimeshiba. Asante..."
Asante nyingine tena? Nikaanza kuhisi naboa.
"Napenda kujua vitu vya kawaida, yaani shughuli za kawaida zifanyikazo hapa. Mmesema napaswa kusubiri mpaka Mariam aje ndiyo tuzungumze?" nikauliza.
"Abee..."
Hilo lilikuwa ni itikio kutoka kwa yule binti aliyelala kwenye sofa, nami nikageuka na kumtazama. Alikuwa ananiangalia sasa. Macho yake yakiwa na ukavu fulani hivi, ilikuwa kama vile sura yake si ngeni sana kwangu, ijapokuwa nilijua kabisa kwamba hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kukutana naye. Sikujua alikuwa ameitikia mwito kutoka kwa nani, lakini kuniangalia vile kukafanya nijue alidhani mimi ndiyo nimemwita.
"Hajakuita, endelea kuangalia sinema mama, eh?" yule mwanamke mweupe akamwambia hivyo binti, naye akaitazama TV tena.
Jambo hili lilinishangaza kiasi. Nikawatazama wanawake wale, wote wakiwa wamesimama, nami nikauliza, "Kwa nini anafikiri nimemwita?"
Mweupe akajibu kwa kuniambia, "Ulikuwa unataka kusema Miryam, jina la dada yake, ila ukasema hilo ulilolisema, ndiyo la kwake. Aka... akadhani umemwita."
Njia yake ya kuwasilisha taarifa hiyo kwangu ilikuwa kama vile hataki kuendelea kuzungumzia zaidi suala la binti huyo aliyelala kwenye sofa, naye akaondoka pamoja na sahani ile bila shaka kuirudisha jikoni. Nikamwangalia yule mwanamke mweusi, naye akaketi kwenye sofa la upande wa kushoto huku akiniangalia pia. Alionekana kuwa mtu makini, labda mkali kiasi pia, nami nikaendelea kuweka utulivu tu wa kiume.
"Hawajambo nyumbani?" akanisemesha.
Nikamwangalia na kutabasamu kiasi, nami nikasema, "Wazima kabisa. Sijui hapa?"
"Tunaendelea vizuri. Mungu anasaidia. Angalau mara moja moja tukipata wageni kama hivi... ni baraka," akaniambia.
Nilikuwa na kawaida ya kusugua magoti yangu kwa viganja taratibu hasa nilipozungumza na mtu niliyemheshimu sana, na wakati huu nikawa nikifanya hivyo, nami nikamwambia, "Ndiyo wageni huwa ni baraka. Hata sisi kule kwetu... angalau mgeni akifika tunafurahi maana mahanjumati na nyama ndiyo hupikwa kwa sana."
Kauli niliyotoa ikamfanya mwanamke huyo acheke, na yule mwanamke mweupe ndiyo alikuwa anarudi, naye akawa anacheka pia kuonyesha kwamba alinisikia.
Akakaa pembeni ya mwenzake na kusema, "Unasema kweli, maana siku hizi kila kitu ni mfumuko wa bei tu. Wengi kugusa nyama ni mara moja moja sana."
"Wee! Umeona?" nikamwambia hivyo, nasi kwa pamoja tukacheka kidogo.
"Napenda unavyoongea. Wewe ni kabila gani?" yule mwanamke mweusi akaniuliza.
"Ningesema mimi ni msukuma kwa upande wa mama, ila wa baba ni mpemba. Sivijui hivyo vikabila lakini, maana tupo kimjini-mjini zaidi..."
Nikawaambia hivyo, nao wakacheka kidogo.
"Ndiyo hivyo. Sisi ni wa Mwanza huko, ila hapa jijini ndiyo tumezamia kwa kipindi kirefu zaidi," nikawafahamisha.
"Hata sisi tumekaa huku muda mrefu pia. Sisi ni warangi, baba yao kina Miryam alikuwa mpemba pia kama wewe tu..." mwanamke mweupe akaniambia.
"Aaa kumbe..."
"Ndiyo. Tulikaa Tanga sana, then baadaye jiji likatuita. Ndiyo tuko na binti yetu hapa, tumemtunza-tunza na yeye sasa hivi anatutunza-tunza ahahah... Miryam amekua, na amekuwa mwanamke mzuri sana. Ana bidii, anatujali, anachapa kazi, ni mtu mmoja mpambanaji yaani kila mtu anampenda," mwanamke huyo akaniambia.
Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa, lakini nikijiuliza kwa nini angefikiria habari za huyo Miryam zingekuwa na umuhimu sana kwangu. Ila kwa kuwa nilijua kuna jambo lingine lililokuwa linaendelea lililomhusisha huyo mwenye nyumba, nikaona niulize tu.
"Kwa hiyo... Miryam ni mtoto wako?"
Wanawake hao wakaangaliana kimaswali kiasi, kisha wakanitazama kama vile hawakunielewa vizuri, na mimi singeweza kujua sababu ya kupewa itikio hilo.
Mwanamke yule mweusi akaniuliza, "Kwani mliongea nini na Shadya? Hakukuelezea mengi sana, au?"
Shadya ndiyo alikuwa nani? Dalali wa nyumba au? Mimi nilipata tu tangazo mtandaoni mpaka kufika hapa. Kiukweli hali hii ikaanza kunichanganya sasa. Nikashindwa kujua nitoe jibu lipi au niulize kipi kingine, na wanawake hao wakiwa bado wananitazama, sauti ya honi ya gari ikasikika kutokea nje ya geti, nami nilipowaangalia nikaona wakitabasamu kwa furaha.
Mweupe akaniangalia na kusema, "Amefika. Ngoja nikamfungulie."
Bila shaka alikuwa akimaanisha kwamba mwenye nyumba huyo, Miryam, ndiyo alikuwa amefika, naye akanyanyuka na kunipita kuelekea nje ili kufungua geti.
Nikaendelea kukaa kwa utulivu tu, bado nikiwa najiuliza kama kuna sehemu fulani akina mama hawa walijichanganya katika maongezi yao, ama labda mimi, na kwa nini mtu mzima kama mwanamke huyo mweupe ndiyo anyanyuke kwenda kufungua geti badala ya binti kijana aliyelala tu kwenye sofa hapo hapo. Ila mi' ningejua nini? Maisha yao yalikuwa yao.
Geti likasikika likifunguliwa, muungurumo wa gari ukaingia zaidi kuikaribia nyumba, kisha ukakata na geti likafungwa tena. Mwanamke yule aliyebaki akanisihi niendelee kunywa juice yangu kabla haijashuka kiwango cha ubaridi iliyokuwa nacho, nami nikaichukua glasi na kuanza kunywa tena. Bila shaka pale nje kuna maongezi mafupi yaliyofanywa baina ya mwanamke yule mweupe na mwenye nyumba aliyeingia, labda kumwambia kuhusu ujio wangu, nami nikajiweka tayari ili akifika mikakati zaidi iendeshwe.
Mlango ukafunguka, na wa kwanza kupita akawa ni yule mwanamke aliyenipokea, kisha akaingia mwanamke mwingine kumfatia. Nilikuwa tu ndiyo nimetoka kupiga fundo dogo la juice, na ile nimeshusha glasi na kumtazama mwanamke huyo, macho yangu yakashtuka kiasi kufuatisha na pigo la nguvu moyoni ndani ya kifua changu.
Ilikuwa ni yule mwanamke mweupe niliyekutana naye masaa machache yaliyopita jioni hiyo na kumdanganya kwamba niliumwa kifua ili tu anibebe kwa gari lake, naye baada ya kuwa ameniona, akasimama mlangoni hapo hapo na kuniangalia kwa mkazo sana ulioonyesha hasira kali kunielekea!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
SEHEMU INAYOFATWA
★★★★★★★★★
Full Story WhatsApp or inbox
Whatsapp +255 678 017 280