Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
(Kutoka kwa mwandishi wa stori za kusisimua zilizowahi kuchapishwa hapa JF za Taxi; Kizungumkuti!; Laiti Ningejua!; Hekaheka!; Hadi Lini! na nyinginezo)
Na Bishop Hiluka
0685 666964 | bjhiluka@yahoo.com
Kijasho Jepesi
Saa 12:15 asubuhi…
Wala sikujua kitu gani kilikuwa kimeukatisha ghafla usingizi wangu! Niliyafumbua macho yangu taratibu nikayatembeza mle chumbani kuangalia huku na kule, nikakutana na ukungu wa kiza chepesi machoni. Hali ile ikanifanya niyatulize vizuri mawazo yangu huku nikijaribu kufikiria pale nilikuwa wapi.
Hata hivyo, sikulipata jibu la haraka na hivyo niliamua kupeleka mikono yangu huku na kule nikijaribu kupapasa pale nilipokuwa nimelala. Sikuchukua muda kugundua kuwa nilikuwa nimelala juu ya kitanda chenye foronya laini na mto wa kuegemeza kichwa.
Kitanda kilikuwa kikubwa cha samadari cha futi sita kwa sita kilichokuwa katikati ya chumba kikubwa. Kwa kufanya vile taratibu fahamu zangu zikaanza kurejewa na uhai.
Niliweza kugundua kuwa nilikuwa nimelala kitandani chumbani kwangu ila sikuweza kukumbuka haraka muda huo ulikuwa ni wa saa ngapi, ingawa hisia zangu ziliniambia kuwa tayari kulikuwa kumeanza kupambazuka kutokana na kusikia sauti za majogoo waliokuwa wakishindana kuwika kwenye mabanda.
Pia niliweza kusikia, kwa mbali, sauti za ndege angani walioshindana kuimba nyimbo nzuri na kuruka huku na kule kwenye vilele vya miti mikubwa iliyokuwa nje ya ile nyumba na kandokando ya barabara ya mtaa ule wa Ng’ambo mjini Tabora, eneo la jirani kabisa na uwanja wa mpira wa Ali Hassan Mwinyi.
Nilikuwa nimelala peke yangu pale kitandani na nilipojichunguza nikagundua kuwa nilikuwa nimejifunika shuka lakini sikuwa nimevaa nguo yoyote mwilini mwangu hali iliyonistaajabisha sana! Sikuwa na kawaida ya kulala bila nguo hata kama ingekuwa ni wakati wa joto kali kiasi gani, bado nisingeweza kulala bila nguo.
Haraka nikataka niamke na kuketi pale kitandani lakini hilo halikufanikiwa kwani kichwa changu kilikuwa kizito mithili ya mtu aliyekuwa ametwishwa kiroba cha mchanga, hali hiyo ilinifanya niyafunge macho yangu taratibu na kuendelea kujilaza.
Nikiwa bado nimelala pale kitandani mawazo yalianza kupita kichwani kwangu mfano wa filamu, nilijaribu kukumbuka nilirudi vipi usiku pale nyumbani na nilikuwa na nani. Mara ikanijia picha ya usiku wa kuamkia siku hiyo. Nikakumbuka kuwa nilikuwa katika eneo la Chemchem mtaa wa Baruti mpaka majira ya saa saba za usiku.
Usiku huo nilikunywa pombe nyingi na kula nyama choma, na kama isingekuwa ushawishi wa rafiki yangu Majaliwa Nzilwa, haki ya nani nisingetia mdomoni pombe siku hiyo.
Majaliwa Nzilwa, jamaa fulani mfupi na mcheshi sana ambaye tulipenda kutaniana muda wote, alikuwa rafiki yangu wa muda mrefu tangu tukisoma katika Shule ya Msingi Gongoni iliyopo katika Manispaa ya Tabora.
Ukaribu wetu uliwafanya wengi kudhani tulikuwa ndugu kwa kuwa muda mwingi tulipenda kuwa pamoja hasa kila nilipotoka kazini, na licha ya urafiki wetu, Majaliwa pia alikuwa mshauri wangu mkubwa katika mambo yangu mbalimbali.
Hayo niliyakumbuka vema, na si akili ya pombe, picha ilikuwa inapita kichwani kwangu kama niliyekuwa naangalia filamu. Nilikumbuka kuwa Majaliwa alininunulia chupa kubwa ya pombe kali aina ya Grant’s Whisky nikaanza kugida kama maji, kisha alimwagiza Masawe mchoma nyama atuchomee ubavu mzima wa mbuzi. Baadaye tena alinunua chupa kubwa ya K Vant na chupa kadhaa za Savannah.
Usiku huo nilikunywa sana kwa kuwa sikuwa sawa kisaikolojia, nilikuwa nimevurugwa kwelikweli! Nilikumbuka pia kwamba baadaye Majaliwa alinitambulisha kwa msichana fulani hivi mwenye asili ya Kiarabu, aliitwa Rahma. Alikuwa msichana mzuri kwa sura na umbo, akiwa na macho mazuri yaliyojawa na haya alikuwa amevaa gauni fupi lililoishia juu kidogo ya magoti yake la rangi ya bluu lenye vidotidoti vyeupe vinavyong’aa.
Alikuwa mrefu na kifua chake kilibeba maziwa ya ukubwa wa wastani huku kiuno chake chembamba kikiwa kimebeba nyonga pana kiasi. Nywele zake zilikuwa nyingi ndefu nyeusi na zilikuwa zimeipendezesha sura yake ya kitoto. Nilikumbuka vyema kuwa Rahma alijitambulisha kwangu kwamba alikuwa mgeni pale Tabora na alitokea Singida. Hivyo tu!
Ni hivyo tu ndivyo nilivyovikumbuka kuwa vilitokea usiku huo, hakuna kingine isipokuwa kuwa na rafiki yangu Majaliwa eneo la Chemchem, kuja kwa huyo mwanamke wa Kiarabu aliyeitwa Rahma, tukala na kunywa, basi! Nilipojaribu kukumbuka mambo mengine kichwa changu kiligoma kabisa kuyakumbuka!
Nikiwa bado nipo kitandani, macho yangu bado nimeyafunga, nilihisi kuchoka mno na mawenge ya usingizi. Si hayo tu, bali pia uvivu ulinijaa na tumboni mwangu njaa ilikuwa inakereza mfano wa seremala aliyekuwa akiranda mbao. Vyote kwa pamoja vilikuwa vinanipa hali ya kutaka kuendelea kubadili uchago.
Akilini, niliutaka utulivu kwa gharama yoyote ile, japo nipate kukimalizia kipande cha usingizi kilichobakia, wala sikujua kingekwisha saa ngapi. Nilichotaka ni kulala tu mpaka pale ambapo mwili wangu ungeniruhusu kuamka. Niliuhisi uzito wa kichwa changu na nilikuwa nina mawenge ya usingizi, ukichanganya na uvivu uliokuwa umesababishwa na mning’inio mkali wa pombe nilizokunywa, vilinipa hali ya kutaka kuendelea kuuchapa usingizi.
Nilipanga nilale na nikiamka niende nikapate supu ya kongoro na chapatti kwa Mama Kashindye, aliyeishi upande wa pili wa barabara ya mtaa huo na baada ya hapo ndiyo nimtafute Majaliwa, huenda yeye angekuwa ana kumbukumbu nzuri ya kilichotokea usiku kuliko mimi.
Nilijiambia kuwa kwa muda huo sikupaswa kuumiza sana kichwa changu kwa hayo mambo ya usiku, sikufikiria kama yalikuwa na umuhimu wowote kwa muda huo, pindi nikiamka ningejua cha kufanya. Hivyo nilijigeuza kuelekea upande mwingine wa kitanda na kuendelea kulala. Sikujali sauti za kukera za majogoo waliokuwa wanashindana kuwika kwenye mabanda na juu ya mapaa. Nilijisemea kuwa kwa sababu nilikuwa nimeanza likizo basi wacha nilale mpaka usingizi ukate kabisa.
Jitihada zangu za kuutafuta usingizi zilikatishwa kikatili na sauti kali ya kitu mfano wa kengele iliyoanza kulia chumbani kwangu, sauti ile iligeuka kuwa kero kubwa masikioni mwangu. Niliposikiliza vizuri nikagundua kuwa ilikuwa ni simu yangu ya mkononi iliyokuwa sehemu fulani mle ndani. Nikawaza kuwa hakuna mtu mwingine ambaye angeweza kunipigia simu muda ule wa alfajiri zaidi ya mpuuzi mmoja tu, Majaliwa! Kwani Majaliwa na mimi tulipenda sana kutaniana na Majaliwa aliongoza kunikera. Kila nilipokasirika yeye aliona raha sana, na ili kukabiliana na hali hiyo ilibidi nimzowee.
Sikuwa na namna yoyote ya kufanya kwani sauti ya simu ilizidi kuniletea kero kubwa masikioni mwangu, na pia nilitambua kuwa kama mpigaji wa simu hiyo, kwa muda huo, angekuwa Majaliwa au mtu mwingine yeyote basi kungekuwa na tatizo na angeendelea kupiga hadi nipokee, hivyo nililitupa pembeni shuka nililojifunika, kisha kwa msaada wa swichi iliyokuwa kando ya kitanda changu nikawasha taa ya mle chumbani huku akili yangu ikiwa imeanza kupoteza utulivu.
Na hapo nikaziona nguo zangu zikiwa zimetupwa tupwa ovyo sakafuni mle chumbani, si hivyo tu niliona pia kifaa fulani kimoja kidogo cha kujipima virusi vya ukimwi ambacho kinauzwa kwenye maduka ya dawa na ki-sindano kidogo cha kutobolea ili kutoa damu. Vifaa hivyo vilikuwa vimetumika.
Kingine nilichokiona pale sakafuni ilikuwa ni mtapakao wa shanga za rangi mbalimbali zivaliwazo na wanawake kiunoni. Jambo hilo likanitia hofu kubwa huku mapigo ya moyo wangu yakianza kunienda mbio isivyo kawaida.
Itaendelea...