Shemsa Mohammed: Watumishi wa Afya Toeni Huduma Bora Ili Wananchi Waone Matunda ya Serikali ya CCM

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
2,583
1,189

Shemsa Mohammed: Watumishi wa Afya Toeni Huduma Bora Ili Wananchi Waone Matunda ya Serikali ya CCM.

WAKAZI wa Tarafa ya Laini, wilayani Itilima Mkoani Simiyu wamelalamikia kitendo cha watumishi wa Afya kwenye zahanati kuwatoza fedha ili wapate kadi ya watoto ya kliniki wakati huo hutolewa bure.

Wakizungumza jana kwenye mkutano wa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali, ulioitishwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed, wananchi hao wameeleza pia kutoridhishwa na utoaji wa huduma za matibabu kwenye zahanati za Sagata na Laini.

Wameeleza kuwa wajawazito wanapata shida kwenye zanahati wakati wa kujifungua ikiwemo kuombwa fedha za kununua kadi za kliniki kiasi cha shilingi 5,000.

Samwel Mbabani mkazi wa Sagata amesema katika zahanati ya Sagata wauguzi hawatoi huduma nyakati za usiku ikitokea mama mjamzito amekwenda kujifungua.

‘’Wamekuwa wakiomba shilingi elfu tano kwa ajili ya kadi la kliniki la watoto jambo siyo maelekezo ya serikali kupitia Ilani ya CCM, lakini tunalipa na ukienda kuhudumiwa hauna kadi hupati huduma.’’ Amesema Mbabani.

Kaimu Mwenyekiti wa Wazee Kijiji cha Laini Masumbuko Langa ameimboa serikali kusimamia maekeleza juu ya utoaji wa huduma bure.

Kaimu Mganga Mkuu wilaya hiyo Oswin Mlelwa amewaelekeza watumishi wa afya kuhakikisha wanatoa huduma muda wote ili wananchi waweze kupata huduma katika maeneo hayo.

Kuhusu kero ya wazee, Oswin amesema wazee wote wenye umri zaidi ya miaka 60 wanatakiwa kupata huduma bure lakini wazee wengi wanakwenda kwenye huduma bila barua za msamaha wa matibabu.

‘’Viongozi wa vijiji na kata watambueni wazee wanaostahili kupata matibabu bure, waandikieni barua za msamaha ili wakienda kupata huduma waweze kutibiwa bure…wazee nendeni mkapate huduma na zingatieni taratibu ili mpate huduma’’ amesema Oswin.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Itilima Anna Gidarya amekiri kuwepo kwa watoa huduma wa afya wenye changamoto licha ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya afya.

‘’Nimeshaongea na Mganga Mkuu wa wilaya, aniletee orodha ya wasiotekeleza wajibu kwa wananchi ili nilinganishe na upande wangu…ugonjwa hauchagui saa wala siku, ‘’ amesema.

Akitoa maelekezo yake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed amewaonya watumishi wa Afya kuhakikisha wanatoa huduma bora ili wananchi waone matunda ya serikali ya CCM.

Aidha amewataka kufanya kazi kwa bidii na kuacha mazoea ili kuondoa changamoto na malalamiko kwa wananchi juu ya ukosefu wa huduma kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali.

Amesema Ilani ya CCM ambayo wamefunga mkataba na wananchi 2020/2025 wakati wakiomba kura iliekexza watoto, wazee na wakina mama wajawazito wakapate huduma bure kwenye huduma za afya.

‘’Ninasikitika kuona wazee hawapewi huduma Itilima na wakina mama wanalipishwa kadi za kliniki, Mkuu wa wilaya najua umelipokea utalifanyia kazi…awamu nyingine nisisikie kero za wakina mama kulipisha kadi za kliniki, Wizara ya Afya inaelekeza ni bure’’ amesema.

Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia anataka na kuelekeza huduma zifike kwa wananchi kama inavyopaswa na siyo kulipisha wazee na wakinamama wajawazito.

‘’Wakati niko hapa leo, naambiwa zahanati ya Laini haifanyi kazi sababu watumishi wote wako msibani…hatukatai kushiriki na jamii basi abaki mmoja kuhudumia wananchi’’ amesema na kuongeza.

‘’Kwenye Mkoa wa Simiyu, mtumishi ambaye hawezi kutimiza wajibu wake wa kuhudumia wananchi anaacha wanajifungulia kwenye sakafu kwa shida zake binafsi, hatufai kwenye mkoa wetu…lengo la zahanati na kituo cha afya ni kuwapatia wananchi huduma bora’’.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Shemsa Mohammed anaendelea na ziara ya Tarafa kwa Tarafa ndani ya Mkoa wa Simiyu kuongea na viongozi wa matawi, mashina na kata kwenye zaira yake kwa lengo la kuimarisha na kukagua uhai wa chama.

MWISHO.
 

Attachments

  • DSC_4715.JPG
    DSC_4715.JPG
    108.7 KB · Views: 2
  • WhatsApp Image 2024-04-28 at 06.01.42.jpeg
    WhatsApp Image 2024-04-28 at 06.01.42.jpeg
    263 KB · Views: 4
  • WhatsApp Image 2024-04-28 at 06.01.46.jpeg
    WhatsApp Image 2024-04-28 at 06.01.46.jpeg
    216 KB · Views: 3
Back
Top Bottom