Shajara ya mwana Mzizima Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu na Alhaji Abdallah Tambaza

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,902
31,972
SHAJARA YA MWANA MZIZIMA
Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu
Na Alhaji Abdallah Tambaza



Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu Rais wa African National Congress

KAMWE asikuongopee mtu kwamba, eti utaweza kuwa umeelezea kikamilifu harakati za kuikomboa nchi ya Tanganyika kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza kama humtaji, humjui, au hukusikia chochote kuhusu simulizi za mwanamajumui huyo wa Kiafrika aliyetokea kupendwa hapa kwetu.

Jina lake akiitwa Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu. Alikuwa gwiji wa siasa za hapa kwetu aliyeupenda, kuupigania na kujivunia Uafrika wake vilivyo, hata ikabidi kukosana na kuachana na wenzake kwenye harakati na mapambano yakiwa ndio kwanza yanapamba moto; akiwamo hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Zuberi Mtemvu, alikuwamo kwenye siasa za enzi za AA, TAA na TANU siku nyingi nyuma kabla Nyerere wa Butiama hajaja Pugu Sekondari kufundisha. Mtemvu, si tu alikuwa rafiki mkubwa wa wanaharakati wengine wa siasa za nchi hii—akina Sykes, Tewa, Dossa Aziz na nduguze Ramadhan na Hamza, Iddi Simba na Ngombale Mwiru—lakini alicheza na kusoma pamoja na kundi hilo kutoka maeneo ya Gerezani mjini Dar es Salaam.

Kundi hilo lote, pamoja na baba mzazi wa mwandishi huyu, hayati Mzee Mohammed Saleh Tambaza, walisoma pamoja pale Al Jamiatul Islamiya fi Tanganyika kwa elimu ya madrassa halafu wakaenda pamoja shule za Mchikichini na Kitchwele wakati huo kwa elimu hiyo iitwayo ya ‘Kizungu’.

Wakati TANU ilipoanzishwa 1954, Mzee Mtemvu alikuwa katibu mkuu wake wa mwanzo na Mzee John Rupia akawa makamu mwenyekiti na mwenyekiti akawa Julius Kambarage Nyerere, msomi na mtoto wa chifu kutoka Butiama.

Nyerere, Mtemvu, Bibi Titi na John Rupia walizunguka nchi nzima hii ya Tanganyika kuelezea na kuhamasisha umma kujiunga katika mapambano haya mazito ya kuutokomeza ukoloni nchini mwetu. Kila walipoenda wasemaji wakubwa wakawa ni Nyerere, Mtemvu na Bibi Titi Mohammed, mwanamke pekee aliyejitoa mhanga kipindi hicho.


Kulia Zuberi Mtemvu, Julius Nyerere na John Rupia nyuma ni vijana wa
Bantu Group walinzi wa viongozi wa TANU na wahamasishaji


Msomaji, kumbuka kwamba wengi wa wananchi wakati huo tayari walikuwa wamekwisha kukata tamaa kwamba kamwe haitofika wakati eti mtu mweusi ndiye atakayekuwa kiongozi mkuu na Waafrika sisi kushika hatamu za kuongoza mambo mengine tupendavyo; kwa maana ya kwamba hali itabadilika na sisi kuchupa kutoka daraja la sifuri mpaka la mwanzo tukiwa juu ya Wahindi, Waarabu na Wazungu.

Kwa ufasaha na weledi mkubwa kabisa, Nyerere na wenzake waliwaeleza watu kwamba hiyo pia maana ni kwamba maeneo ya kuishi na nyumba za kuishi pia zitabadilika pale utukufu utakapotujia sisi na unyonge kutoweka—tutahamia magorofani kwa Wahindi na Oysterbay kwa Wazungu.

Watu wakafurahia sana ndoto hiyo na hivyo kuingia na kukikubali ‘chama cha tano’ (kilivyojulikana wakati huo) makundi kwa makundi wakiwamo wazee, vikongwe, vijana na wanawake pia. Kila walipoenda walipokewa vyema na Bibi Titi ndiye aliyekuwa kivutio kikubwa; kwamba lilikuwa ni jambo la kushangaza kuona mwanamke mno akiweza kupanda juu ya jukwaa na kuhutubia kwa kiwango kile na kuwashawishi wanawake wenziwe kujiunga na ‘uamsho ule mkuu.’

Mnamo miaka ya kuelekea kupatikana uhuru wetu, watawala wa Kingereza, walitengeneza mpango wa kufuatwa katika upigaji kura za kuchagua Wabunge na Rais wa nchi. Mpango huo ulioitwa wa ‘Kura Tatu’ haukukifurahisha hata kidogo chama cha TANU, kwa sababu ulipangwa kwamba kila mtu apige kura tatu atake asitake; yaani moja umchague mgombea Mzungu; nyengine mchague Muhindi; na ya tatu mchague Mwafrika.

Ilipangwa hivyo kwa sababu ilikuwa dhahiri kwamba chama cha TANU na Waafrika wangezoa viti vyote vya uwakilishi. TANU na watu wake hawakupenda ujanja huo utumike, hivyo kikatishia kususia uchaguzi wote kama utaendeshwa namna hiyo.

Nyerere, kwa upande wake akawa ameona mbali kwamba wakisusa itakuwa ni hasara kwao, hivyo ni bora kushiriki hivyo hivyo na kuwachagua hao Wazungu na Wahindi. Hali hiyo ikapelekea mvutano na mgawanyiko mkubwa ndani ya TANU baina ya wanaotaka na wasiotaka kushiriki uchaguzi ule.

Mmoja wa watu ambaye hakukubali hilo alikuwa ni Katibu Mkuu wa chama cha TANU Zubeir Mtemvu. Yeye Mtemvu, hakuona mantiki ya kuchagua mtu yeyote asiye Mwafrika ukizingatia kwamba wao hawakupenda hata kidogo kuishi na sisi kwa njia ya usawa. Mtemvu na Nyerere wakawa mbalimbali kwa hilo. Potelea mbali, hata mimi ningemuunga mkono Mtemvu, nikizingatia kwamba hawa jamaa hata kwenye biashara zao ukitaka kumlipa pesa, basi walikupa kopo utumbukize hiyo pesa ili tu msigusane mikono na wewe ‘mchafu.’ Sasa nimchague kwa lipi.

TANU ikaenda Tabora kufanya mkutano wake mkuu na moja ya ajenda ilikuwa kujadili na kutoa maamuzi kama washiriki au wasishiriki uchaguzi ule. Nyerere, kwa kumhofia Mtemvu, kwamba anaweza akawa na ushawishi mkubwa kwenye hilo, akambakisha ofisini Dar es Salaam ili aratibu mambo mengine muhimu ya chama wakati huo.

Walipofika Tabora, Mwalimu akampanga mjumbe kutoka Tanga, Mwalimu Kihere aje kuzungumzia umuhimu wa kushiriki na hasara za kususia uchaguzi ule. Mwalimu Kihere akaifanya kazi hiyo kwa ustadi mkubwa sana, na pale kura zilipopigwa upande wa Nyerere ukaibuka kidedea.

Akiwa ofisini Dar es Salaam, Mtemvu alitumiwa taarifa kwamba atangaze kuwa chama cha TANU kitashiriki Uchaguzi wa Kura Tatu. Mtemvu alichukizwa sana na hilo, hivyo akatuma ujumbe kwamba yeye anajiuzulu kutoka chama hicho na kwamba atatangaza kuanzisha chama chake mwenyewe.

Aliita waandishi na akatangaza kwamba kufuatia maamuzi ya Tabora, yeye hayumo tena TANU na kwamba ameanzisha chama kipya kilichojulikana kama Congress Party, kwa malengo yaleyale ya kupambana na utawala dhalimu wa Malkia wa Kiingereza mpaka atoe uhuru wetu.

Mtemvu, alikuwa hodari wa kuzungumza na kushawishi umma. Chama cha Congress kikavuma na kupata wafuasi wengi hasa kwenye maeneo ya Bukoba, Tabora na Mwanza kama takwimu za matokeo ya Uchaguzi Mkuu zilivyoonyesha.

Makao makuu yake yalikuwa pale Mtaa wa Nyamwezi na Faru alipochukuwa ghorofa nzima ya nchini kwenye nyumba iliyojengwa na Mzee Nassor Kiruka na sasa inamilikiwa na familia ya marehemu Mzee Masha, kada wa CCM kutoka Mwanza.

Mzee Mtemvu, aliyeng’oka na wanachama wengine shupavu wa TANU, akiwamo Said Chamwenyewe, Emmanuel Makaidi, Kassanga Tumbo, alikuwa tishio kwa Nyerere na TANU yake ingawa si kwa kiasi kikubwa, maana Nyerere na Bibi Titi, hiyo ilikuwa ni habari nyengine kabisa.

Chama cha Congress na Mtemvu ikawa ndio habari ya mjini. Alitembelea nchi nyingi duniani kwa mialiko ya vyama rafiki, hasa nchi zilizokuwa na siasa za mrengo wa kushoto. Amehutubia mikutano mingi ya kisiasa hapa kwetu na kwingineko duniani kuelezea kiu na kilio cha Watanganyika kutaka kujitawala wenyewe.

Kama walivyokuwa wakiitwa TANU linapokuja suala la kukutana na mawaziri mbalimbali wa serikali ya kikoloni ya Kingereza, na Mtemvu na Congress pia walipata nafasi hiyo hiyo kuelezea azma ya kuwa na serikali huru. Sasa vipi leo sisi tumsahau mtu wa namna hiyo? Aliyewakabili bila woga kwa niaba yetu Wazungu wale wafuga masharubu?

Nilimfahamu kwa kiasi fulani Mzee Mtemvu kwa kuelezewa kwenye mazungumzo nyumbani tukiwa na babangu mzazi. Baba akiishi kwao Upanga alikozaliwa na Mtemvu kwao kukiwa Gerezani. Baadaye wakakutana tena chuoni na shuleni.

Abdul Mtemvu, ni mdogo wa mwisho wa Mzee Zubeir Mtemvu. Kiumri, Abdul alikuwa kijana mdogo sana anayeweza kuzaliwa na Zuberi Mtemvu. Comrade Abdul na mimi tulisoma pamoja hapa kwetu Dar es Salaam kuanzia shule ya msingi pale Kitchwele Middle School na baadaye Sekondari ya Mtakatifu Joseph pale Forodhani.

Nyumba yao ilikuwa barabarani pale Mtaa wa Kitchwele na hivyo wakati wa kutoka shuleni nilipitia kwao mara kwa mara nikiongozana na Abdul kupata maji baridi ambayo wakati huo yalikuwa ni kitu adimu sana maana sisi wa daraja la tatu majumbani kwetu ilikuwa inatamba mitungi na kata zake. Hiyo ilikuwa ni fursa ya kumwona kwa karibu zaidi Mzee Mtemvu mwenyewe katika mazingira ya kinyumbani akiwa ametulia na gari yake TZM 1 ikiwa imepakiwa barazani.

Hapa mjini, aliendesha siasa zake kistaarabu sana akiranda kwa miguu huku na huku akiwa amevalia nguo rasmi za ‘migolole’ ya kisiasa ya kutoka Afrika Magharibi hasa kule Nigeria na Ghana, na usinga wake mkononi akisalimiana na kuongea na watu mbalimbali kuelezea mipango yake ya kujitawala wenyewe nchini.

Wakati mwengine alionekana akiwa amepiga suti zake nyembamba mwilini akiwa ndani ya gari lake zuri la kipekee, nadhani ilikuwa Ford Cortina hivi, yenye namba spesheli za usajili – TZM 1. T ikiwa na maana ya nchi yake Tanganyika; Z jina lake Zubeir; na M ni Mtemvu.

Hivyo ndivyo alivyokuwa akiwakoga watu Mtemvu na Cortina yake mpya.

Sasa wewe Mtanzania wa leo kwa nini basi usimtaje, usimjue, usimuenzi na kumtukuza mtu huyu shupavu ambaye alifanya kazi ileile kama Nyerere – kuelezea dunia – kwamba umefika wakati tupate uhuru wetu. Je, unafikiri madhumuni ya chama chake yalikuwa nini kama si hayo hayo?

Nyerere na TANU walishinda tu kwenye sanduku la kura wakapata ridhaa ya kuunda serikali, lakini hawa wengine nao wanastahili heshima kutoka kwetu. Hivi huoni kwamba kwenye uchaguzi ambao Zuberi Mtemvu alitokea wa pili, kama angeshinda yeye ndiye angekuwa rais wetu wa kwanza? Basi hujiulizi kwa nini watu wa Kanda ya Ziwa wakati ule wawe wamekipa kura nyingi chama cha Congress na Mtemvu?

Tubadilikeni jamani tutoe haki inapostahili; tuwe tunaelezana haya yanayohusu huko nyuma tulikotoka tulikuwaje; na kina nani hasa waliotufikisha hapa leo tunajivuna.

Simu:0715808864
 
Stori nzuri Sana nlichokua najua Mtemvu alikua mpinzani wa Nyerere Na hakuna habar zake nyingi katika historia ya taifa hili!
 
Tulisoma mashuleni kwamba ANC ilikuwa chama kilichoanzishwa ili kupunguza nguvu za TANU katika kudai uhuru. Hili ndilo tatizo la historia tulioisoma shuleni, haikuweza kudadavua utofauti wa kimtazamo kati ya TANU na vyama vingine vya kupigania Uhuru kama hiki cha Mtemvu.
 
Nikuite Mwalimu Mohamed Said au Maalim Mohamed Said?

Hebu nijuze kidogo... nimekuwa impressed na hizo nguvu za Mtemvu manake kama aliweza kuanzisha chama ambacho kiliitisha kidogo TANU basi bila shaka ushawishi wake ulikuwa mkubwa hasa ukizingatia TANU ilishaota mizizi.

Sasa ina maana hii Congress yake ni miongoni mwa vyama ambavyo vilivyokufa natural death baada ya Mwalimu kupiga ban mfumo wa vyama vingi?! Hivi Mwalimu alishawahi kuwashirikisha kwenye serikali ya Tanganyika huru wale magwiji ambao alitofautiana nao kisiasa au aliwaona threat mwanzo mwisho?

Mi ni miongoni mwa watu wanoamini kwamba, kwa big brain ya Nyerere, endapo angekuwa tayari kushirikiana na watu ambao hawakuogopa kumkosoa, basi Tanzania ingekuwa mbali sana.

NB: Tuwakumbushe watu kwamba Mtaa wa Kitwele ndio Mtaa wa Uhuru!
 
Historia nzuri sana, kuna haja wanaoandaa mitaala ya kufundishia hasa masomo yanayohusu historia ya Tanganyika na Zanzibar wakarudia kuandaa mitaala hiyo wakizingatia ukweli wa historia yenyewe. Hawa wapigania uhuru wanatakiwa watengewe topic mahususi kuwaelezea na hasa kuelezea michango yako.
 
Ndugu zangu makala hii sikuandika mimi kaandika Abdallah Tambaza.
pamoja na kuwa hukuandika makala hii unao uwezo wa kuandika kitabu kueleza harakati za uhuru kwa kuwapa nafasi sitahiki hawa mashujaa wetu bila kuwa tweza kama nilivyofundishwa kuwa wapinzani wa nyerere nia yao ilikuwa kuendeleza utawala wa mkoloni. uwe na siku njema mwl.
 
Sheikh Mohamed kumbe wewe ni mtoto wa Almaaruf Mzee Tambaza. Sikujua hilo. Asante kwa kumbukumbu nzuri ya mapambano yetu ya uhuru
 
pamoja na kuwa hukuandika makala hii unao uwezo wa kuandika kitabu kueleza harakati za uhuru kwa kuwapa nafasi sitahiki hawa mashujaa wetu bila kuwa tweza kama nilivyofundishwa kuwa wapinzani wa nyerere nia yao ilikuwa kuendeleza utawala wa mkoloni. uwe na siku njema mwl.
Alishaandika Toka 1988,"Maisha na nyakati za Abdullah Sykes"ameleza mengi,ingawa kilikumbwa na vizingiti mwanzo lakini sasa kinapatikana.Mleta mada ameleza kuwa Mzee Mtemvu alikuwa katibu wa kwanza wa TANU nadhani alikuwa katibu mwenezi wa kwanza.Vipi kuhusu mwanae Abdul Mtemvu alikuwa mdogo sana bado ama?
 
Alishaandika Toka 1988,"Maisha na nyakati za Abdullah Sykes"ameleza mengi,ingawa kilikumbwa na vizingiti mwanzo lakini sasa kinapatikana.Mleta mada ameleza kuwa Mzee Mtemvu alikuwa katibu wa kwanza wa TANU nadhani alikuwa katibu mwenezi wa kwanza.Vipi kuhusu mwanae Abdul Mtemvu alikuwa mdogo sana bado ama?
Balibaba...
Abdul Mtemvu ni mdogo wake Zuberi Mtemvu si mwanae.
 
Ndugu zangu makala hii sikuandika mimi kaandika Abdallah Tambaza.
Tena nilitaka kuhoji pale paliposema "baba mzazi wa mwandishi huyu, hayati Mzee Mohammed Saleh Tambaza... na ile sehemu iliyohusu Upanga kama makazi!"

Wengi wetu hatukuwa makini mwanzoni kabisa alipotajwa mwandishi....
 
Marhabaaa huwa makala kama hizi zinanifanya kuona uandishi kama movie hivi maana fikra zinarudi miaka 60 nyuma kumbe uko 2018
 
Back
Top Bottom