- Thread starter
- #41
UTATA
Nakupa heri ya mwaka, Mola atujalie
Atujazie fanaka, mabaya tuyakimbie
Atupe zake baraka, wachawi watukimbie
Hakika nakuapia, Chama sina uduvi
Choveki nakutuma, Sindano nitafutie
Kwa Macheni amezama, asubuhi mdamkie
Mpe zangu karama, akili imfungukie
Hakika nakuapia, Chama sina uduvi
Chama hana utata, mtoto wa kiungwana
Jando amelipata, masomo walimshona
Akili ameipata, busara zipo bayana
Hakika nakuapia, Chama sina uduvi
Chama hana madhila, kajaa furaha tele
Ni mtu mwenye fadhila, hajipendei kelele
Usije ntia hila, kwa wivu uliotele
Hakika nakuapia, Chama sina uduvi
Chama mtu makini, hula kwa kuchagua
Hana umasikini, wa kushindwa kutambua
Mola kanipa dini, vya halali navijua
Hakika nakuapia, Chama sina uduvi
Chama namalizia, Kibaranga najiendea
Chelangwa nitamwambia, mjini kutembelea
Maneno kukupatia, utuondelee fedhea
Hakika nakuapia, Chama sina uduvi
Chama
Gongo la Mboto DSM
UUNGWANA NI VITENDO
Misifa wajisifia, wazidi kunishangaza
kwa mema wajipambia, tena wazi watangaza
watu walishasikia, sumu uliisambaza
uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
Na mema umepuuza, kwa jando ulopitia
Hili nimechunguza, mafunzo hukushikia
wabaki sasa kucheza, mjini wakusifia
Uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
Siwezi kuwa na wivu, kwa yako hiyo tabia
vipi mola nimuovu, mabaya kujisifia
Niombayo kwake hofu, ya shari kuyakimbia
uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
Uturi sasa wa nini, na hewa ulichafua
kuvisifu vya mjini, raha wajua tumbua
kila siku kwa macheni, vinyeo wavipangua
uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
Na mara umegeuka, eti wala kwa makini
wajua kweli zunguka, acha wako ufitini
Ni haya imekushika, umeacha vya gizani?
Uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
Fadhila unafadhili, wadai huna kelele
vipi upande wa pili, umeiacha misele?
Mtani mwendo badili, achana na misukule
Uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
Na iwapo nakukwaza, naomba unisamehe
Ila wacha kujikweza, punguza na starehe
Ya dunia hutoweza, uliza wako mashehe
uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
Ni mengi nimeyasema, kwa hapa ninasimama
Na mola mwenye rehema, akupe yenye karama
Azidishe ya neema, mola wetu yu karima
uungwana ni vitendo, twapima maneno yako
SMG