Serikali Kuanza Ujenzi wa Daraja la Mkili na Mitomoni Mkoani Ruvuma - Waziri Bashungwa

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
2,588
1,190
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) ipo katika hatua ya kumtafuta Mkandarasi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa madaraja mawili ambayo ni Daraja la Mkili lenye urefu wa mita 20 pamoja na Daraja la Mitomoni lenye urefu wa mita 80 ambalo litaunganisha Wilaya ya Nyasa na Songea Vijijini.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi Wilayani Nyasa mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua barabara ya Mbinga – Mbamba Bay (km 66) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi Bilioni 122.76 Mkoani Ruvuma.

Waziri Bashungwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha inajenga na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo yote yasiyofikika ili kusaidia wananchi kupata huduma za kijamii, kibiashara na uwekezaji.

Ujenzi wa madaraja hayo unajili kufuatia ziara aliyoifanya Waziri Bashungwa mkoani Ruvuma Januari 26, 2024 ya kukagua miundombinu ya barabara kutokea Songea Mjini hadi kufikia Wilaya ya Nyasa kupitia barabara ya Likuyufusi - Mtomoni (km 124) inayoenda kujengwa sehemu ya kwanza Likuyufusi - Mkayukayu (km 60) kwa kiwango cha lami pamoja na kukagua madaraja ya Mkenda na Mitomoni.

Kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo hayo, Waziri Bashungwa alilazimika kutumia takribani saa tano kwa kutumia usafiri wa miguu, mitumbwi na pikipiki maarufu kama boda boda hadi kufikia vijiji hivyo.

Baada ya kukagua maeneo hayo, Waziri Bashungwa alitoa miezi miwili kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya usanifu wa kina na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa daraja la zege katika eneo la Mitomoni ili wananchi wa maeneo hayo waondokane na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii.

Ujenzi wa daraja hilo utaunganishwa na barabara ya Unyoni Mpapa - Liparamba - Mkenda pamoja na barabara ya Likuyufusi - Mkenda kupitia Mto Ruvuma.

MWISHO

WhatsApp Image 2024-09-27 at 15.15.13.jpeg
WhatsApp Image 2024-09-27 at 15.15.14.jpeg
WhatsApp Image 2024-09-27 at 15.15.34.jpeg
WhatsApp Image 2024-09-27 at 15.15.36.jpeg
WhatsApp Image 2024-09-27 at 15.17.51.jpeg
 
Back
Top Bottom