Serikali kuanza kutumia ‘drone’ kwenye uchimbaji wa madini Kijiji cha Lemishuku

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
3,354
12,991
WhatsApp Image 2024-08-18 at 14.18.51_6f545f3d.jpg
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amefanya ziara kukagua shughuli za uchimbaji madini na kusikiliza changamoto za wachimbaji wadogo katika eneo la Lemishuku,Wilayani Simanjiro eneo ambalo ni maarufu kwa uchimbaji wa madini vito ya Green Garnet

Waziri Mavunde amepata nafasi ya kukagua uwekezaji uliofanywa katika uchimbaji wa madini katika Kijiji cha Lemishuku na kuahidi kwamba Serikali itafanikisha urushwaji wa ndege nyuki “drone” katika eneo hilo kwa ajili ya utafiti wa kina ili kuwaongoza vizuri wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha na kuongeza kuwa mwishoni mwa mwezi Desemba 2024 jengo la kituo cha ununuzi wa Madini litakuwa limekamilika ili kufanikisha urahisi wa Biashara ya madini.
WhatsApp Image 2024-08-18 at 14.18.55_19b24b39.jpg

WhatsApp Image 2024-08-18 at 14.18.50_8aaf2975.jpg

Aidha, Waziri Mavunde alieleza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia S. Hassan itatatuwa Changamoto zote za Maji, Umeme, Barabara na Zahanati ili kuchochea shughuli za ukuaji wa sekta ya madini ambapo katika ujenzi zahanati aliongoza harambee ambayo jumla ya matofali 4500, sarufi mifuko 183 na fedha Tsh 23m zimepatikana.

Akitoa salamu zake Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, amemshukuru Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kazi kubwa ya kuboresha huduma za kijamii katika eneo hilo la uchimbaji na kumshukuru Waziri Mavunde kwa kuwa Waziri wa kwanza kufika katika eneo hilo kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo (FEMATA), John Bina na Mwenyekiti wa Mabroka Tanzania(CHAMATA), Jeremiah Kituyo wameipongeza serikali kupitia wizara ya madini kwa mipango ya uendelezaji wa sekta ya madini na kusisitiza kwa wachimbaji wadogo kuzingatia sheria za nchi na pia kwa wafanyabiashara wa madini kuhakikisha wanakata Leseni ya biashara ya madini ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakhi Lulandala amewahakikishia wachimbaji wadogo wa eneo la Lemishuku kwamba Serikali ya ngazi ya Wilaya kupitia Taasisi mbalimbali zilizopo hapo zitahakikisha zinasimamia kwa ukaribu utekelezaji wa changamoto za wachimbaji ili kuweka mazingira mazuri ya uchimbaji katika eneo la Lemishuku.
 
Back
Top Bottom