Serikali Ina Jukumu la Kuwekeza kwa Kiwango Stahiki Katika Elimu na Vipaji vya Wananchi Wake

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
747
2,115
Uwekezaji wa serikali kwa wananchi.jpg

Miongoni mwa mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele zaidi na serikali ni uwekezaji katika elimu na vipaji vya wananchi wake. Hii ina maana kwamba afya, elimu na lishe ni muhimu katika kukuza uchumi wenye nguvu, ushindani na unaostawi.

Hivyo basi, serikali inapaswa kuwekeza katika miundombinu ya maendeleo ya mtoto kuanzia ujauzito hadi kuanza shule rasmi, ikijumuisha lishe na afya ya mtoto, madarasa, na programu za elimu zinazofaa kimaendeleo.

Miaka mitano ya kwanza, kwa mfano, inaelezwa kuwa ni muhimu sana kwani ukuaji wa ubongo wa binadamu katika miaka hiyo huamua jinsi watakavyoweza kujifunza na kushughulikia kile wanachojifunza kwa maisha yao yote. Hivyo uwekezaji katika elimu unaweza kufeli ikiwa afya mbaya ya watoto haitawaruhusu kujifunza vizuri.

Zaidi ya hayo, serikali inapaswa kuhakikisha kuwa fursa za elimu iliyo bora zinapatikana kwa wananchi katika maisha yao yote. Kwa kuboresha afya na ujuzi wao, watu wanaweza kuwa na tija zaidi, wenye ubunifu, ushindani na uwezo wa kubadilika kutokana na mazingira (flexibility).

Serikali inayoamini katika vipaji na uwezo wa wananchi wake na kutoa sehemu kubwa ya mapato yake ya kodi kuwekeza kwao ili kuwasaidia kufikia uwezo huo ni msingi wa maendeleo endelevu.

Hata hivyo, ingawa ndio kichocheo kikuu cha ukuaji endelevu na kupunguza umaskini, watunga sera mara nyingi huona ugumu wa kutoa na kusimamia hoja kuhusu uwekezaji katika rasilimali watu. Udhaifu huu unaziacha nchi nyingi duniani zikiwa hazina utayari wa kwenda sambamba na mabadiliko yanayozidi kutokea kila uchao na katika kila nyanja.

Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu uchumi wa Tanzania mwaka 2019 ilisema ikiwa nchi hiyo inataka kuboresha nguvu kazi na kupata maendeleo endelevu inahitaji kufanya uwekezaji muhimu na wa haraka ili kuharakisha maendeleo katika afya na elimu ya wananchi wake, hasa vijana.

Pia, ilipendekeza kuwa ili kukabiliana na vikwazo vya nchi katika maendeleo ya rasilimali watu yake, Tanzania inahitaji kuongeza uwekezaji katika maeneo mengi kwa kutumia mbinu ya "serikali nzima" katika kutoa huduma bora.

Naye Bw. Quentin Wodon, Mchumi Kiongozi wa Benki ya Dunia na mwandishi mwenza wa Taarifa hiyo ya 12 ya Uchumi wa Tanzania, alisema kuna mengi ya kujifunza kwa Tanzania na nchi nyingine kutoka kwa nchi kama Singapore, Korea Kusini, Japan na Hong Kong ambazo mafanikio yake yametokana na uwekezaji kwa vijana kuwa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia elimu na ukuzaji ujuzi katika hatua zote za maendeleo yao.

Uwekezaji katika rasilimali watu unaweza kuleta faida kubwa; na mavuno hayo makubwa yanategemea uwekezaji uliobuniwa vyema. Ingawa kuwekeza kwa watu kunaweza kuchukua muda mrefu ili kuvuna matunda yake, lakini faida yake ni kubwa na endelevu.
 
Back
Top Bottom