Ripoti ya CAG, Kazi Inaendelea ya Kufuja Fedha za Umma

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
617
1,542
Maeneo kumi (10) muhimu katika Uchambuzi wa Ripoti ya CAG mwaka 2022/23.

Kama ambavyo tumekuwa tukifanya kila mwaka, uchambuzi wetu mwaka huu utajikita kwenye mambo kumi (10) ambayo tunaona ni muhimu Watanzania kuyatambua na tutayatolea mapendekezo ili yaweze kuchukuliwa hatua.

Katika uchambuzi wetu tumebaini CAG ameibua hoja nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi. Baadhi ya hoja hizo zitazingatiwa kwenye uchambuzi wa bajeti wa kila wizara ya Serikali utakaofanywa na Wasemaji wetu wa kisekta.

Kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali na hatari zake kwa Taifa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amefanya ukaguzi wa Akaunti ya Deni la Taifa na kuonyesha ukuaji wa kasi wa deni la taifa na viashiria vya hatari kwa deni la Serikali. CAG ameeleza kuwa Deni la Serikali hadi tarehe 30 Juni 2023 lilikuwa Shilingi trilioni 82.25 ambalo ni Ongezeko Shilingi trilioni 10. 94 sawa na 15% kutoka mwaka wa Fedha uliopita.

Uchambuzi wetu wa CAG kuhusu Mwenendo wa deni la Serikali ni kuwa kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali inatishia maendeleo ya watu, uwezo wa nchi kujihudumia na kusababisha ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na deni (debt driven growth).

Kasi ya ukuaji wa Deni ya Serikali ya awamu wa Sita chini ya Rais Samia kwa miaka miwili tumeshuhudia ongezeko ambalo halijawahi kutokea tangu kupata Uhuru katika Nchi yetu. Amekopa zaidi kwa shilingi trilioni 17.7 kutoka shilingi trilioni 64.52. Huku uchumi ukiendelea kuchechemea kwa ukuaji wa asilimia 5.2

Jedwali; Mwenendo wa Deni la Serikali kwa awamu mbalimbali za Serikali

JINA LA RAISIMIAKAKIASI KILICHOKOPWAKIASI CHA DENI LA SERIKALI.
Jakaya Kikwete10Trilioni 29.7Trilioni 33.5
John Mgufuli6Trilioni 31.3Trilioni 64.5
Samia Hassan2Trilioni 17.75Trilion 82.25
Athari za Mwenendo wa Deni la Serikali zinaangukia kwenye mabega ya wananchi. Mathalani kwa mwaka wa fedha 2022/23 Makusanyo ya Ndani ya kodi, yasiyotokana na kodi na makusanyo ya serikali za mitaa yalikuwa Sh. trilioni 26.515 huku matumizi kwa ajili ya kuhudumia deni la Serikali ilikuwa shilingi trilioni 9.1. Hii ina maana kuwa 34.3% ya kila tulichokuwa tunakusanya kilienda kulipa deni la Serikali.

Mwenendo wa kukua kwa deni linaathari zifuatazo;
Nchi inatumia sehemu kubwa ya makusanyo yake kwenda kuhudumia deni badala ya kutoa huduma kwa wananchi walalahoi. Ukitazama taarifa za Benki Kuu zinaonyesha kila mwezi tunatumia bilioni 900 kwa ajili ya kulipa deni la Serikali, kati ya fedha hizo deni la ndani ni wastani Bilioni 600.5

Ongezeko la mikopo ya Biashara yenye masharti ya muda mfupi Serikali inalazimika kuingia sokoni kukopa zaidi ili kulipa madeni (hatifungani) yaliyoiva.

Ukopaji wa Ndani; Serikali na Sekta binafsi kugombania fedha jambo linalopelekea kuiminya sekta binafsi kupata mikopo kutokana na taasisi zinaona zinafaidika kwa rahisi kuikopesha Serikali kuliko sekta binafsi

Ongezeko la utitiri wa kodi, tozo, ushuru kwa wananchi.

Kucheleweshewa kwa malipo ya mafao na pensheni za wastaafu ambao ni wanufaika/ wanachama kutokana na fedha nyingi ambazo Serikali haijazilipa kwa taasisi hizo

Jambo hili linaumiza sana wakati wananchi wakibebeshwa mzigo huo, tunashuhudia ubadhirifu na upotevu mkubwa wa fedha unaofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi bila kuchukuliwa hatua za kiuwajibikaji. Badala yake viongozi wanaendelea kulitafuna taifa kwa kujinunua magari ya kifahari, kujiongezea posho, safari za nje na mishahara.

Pili, kwa mujibu wa CAG Serikali bado ina orodha ya mikataba ya mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.6 bila kupokea fedha za mikataba hiyo. Hii ni hoja ambayo imekuwa ikijitokeza kila mwaka kwa muda mrefu.

Mapendekezo ya ACT Wazalendo;
Ili kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali, haswa Deni la Nje, kutokana na kushuka kwa mauzo yetu nje na kuporomoka kwa shilingi dhidi ya dola, tunapendekeza kuwa Serikali ifanye ‘hedging’ ya Deni la Nje ili kuwa na uhakika wa thamani ya fedha itakayotumika muda wote kuhudumia Deni hilo.

Serikali izibe mianya ya upotevu fedha na matumizi mabaya yanayongeza maumivu kwa wananchi.

Tunaitaka Serikali kufanya mapitio ya mikataba yote ya mikopo ili kufuta mikataba ambayo haitekelezeki na ile inayotekelezeka ipokee fedha na kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.

Madai ya wafanyakazi Sh. bilioni 36.47 na michango yao (sh. bilioni 856.78 kutowasilishwa kwenye Mifuko ya hifadhi ya Jamii.

Ripoti ya CAG ya mwaka 2022/2023 imeonesha madai ya shilingi bilioni 36.47 ya watumishi wa Umma katika halmashauri na serikali za mtaa 54. Madai hayo yanajumuisha malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi, stahiki za wastaafu na posho za kisheria. Mchanganuo wa madai ya watumishi hao ni ufuatao;

MADAIKIASI
Malimbikizo ya mishahara11,420,214,782
Madai mengine likizo, kujikimu, safari, uhamisho, posho za kisheria24,341,616,670
Wastaafu708,111,184
Kutokulipwa kwa madai haya kunaongeza ugumu wa maisha kwa wafanyakazi ikizingatia tayari gharama za bidhaa muhimu zinaendelea kupanda kila uchao.

Vile vile, ucheleweshwaji wa malipo ni kinyume na kanuni ya utumishi wa umma inayoelekeza mfanyakazi yeyote wa Serikali pale anapopandishwa daraja au kuteuliwa kwenye nafasi ya kiwango cha juu, alipwe malipo ya nyongeza ya mshahara yanayostahili.

CAG anathibitisha jinsi ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kuwathamini wafanyakazi wa umma nchini. Hii inapelekea kushusha morali ya watumishi na kuondoa ufanisi katika utendaji na kuwahudumia wananchi.

Aidha, CAG amebainisha kiasi cha Shillingi billion 856.78 cha michango ya wafanyakazi kutowasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSSF, PSSSF na WCF). Mifuko ya hifadhi ya jamii kushindwa kukusanya michango inadhofisha uwezo wake wa kuhudumia wanufaika. Mathalani kiasi cha shilingi milioni 708.1 ambacho ni madai ya wastaafu kimeshindwa kulipwa kwa zaidi ya miaka minne.

ACT Wazalendo tunaitaka hatua zifuatazo kuchukuliwa ili watumishi na wastaafu walipwe stahiki zao;

Tunaitaka Serikali na waajiri binafsi kuheshimu matakwa ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi.

Pia, tunaitaka Serikali kulipa malimbikizo ya madai yote ya watumishi na wastaafu.

Ubadhirifu na upotevu wa Shilingi Trilioni 3.14 fedha za umma.

Ripoti ya CAG mwaka 2022/23 imeendelea kuonesha uzembe mkubwa unaofanywa na Serikali uliosababisha upotevu wa makusanyo na mapato katika wizara, idara na taasisi za Serikali, Serikali za Mitaa, Miradi ya maendeleo na Mashirika ya umma.

Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG mwaka huu tumeona kwa mara nyingine vitendo au maamuzi yenye viashiria vya ubadhirifu wa fedha za umma katika utekelezaji wa miradi na majukumu mbalimbali ya wizara, taasisi za Serikali na Mashirika ya umma.

Hoja za ubadhirifu na upotevu wa fedha za makusanyo zina jumla ya thamani ya shilingi trilioni 3.14. Mchanganuo wa hoja na thamani yake ni kama ufuatao;

Serikali za Mitaa na Halmashauri zimeonesha upotevu wa shilingi bilioni 167.8

Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zina upotevu wenye thamani ya shilingi bilioni 103.32

Gharama zinazotokana na ucheleweshaji na kutelekezwa kwa miradi ya maendeleo zina jumla ya thamani ya shilingi bilioni 744.1

Dosari za kiusanifu za TANROADS kwenye miradi ya Barabara 6 wenye thamani ya shilingi bilioni 130.51

Mradi wa BRT shilingi Bilioni 28.05

Bwawa la kufua umeme la Mwl. Nyerere wenye thamani ya shilingi bilioni 327

Mashirika ya umma yana hoja zenye thamani ya shilingi trilioni 2.23

Taarifa ya CAG inathibitisha tena tatizo sugu la Serikali kuendelea kupoteza na kutumia vibaya fedha za umma bila hatua za uwajibishaji kuchukuliwa.

ACT Wazalendo tunataka

Watu wote waliohusika katika ubadhirifu na uzembe uliopelekea upotevu wa fedha za umma wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.

Tunatoa wito kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali. Bunge lisipotekeleza wajibu wake kikamilifu ndio maana nchi yetu inashuhudia matumizi mabovu na ufujaji wa fedha bila hatua kuchukuliwa kila mwaka.

Fedha kutumika bila kupitishwa Mfuko mkuu wa Hazina ni mwanya wa Ufisadi

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameendelea kubainisha ukaidi wa Serikali kutumia fedha kinyume na katiba ya nchi. Kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/18 tulionyesha kuna fedha za Serikali ambazo zimetumika bila kufuata utaratibu wa kikatiba, ambao unailazimu Serikali kupitisha mapato na matumizi yake kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina.

Katika Mwaka 2022/2023 Jumla ya Matumizi yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.2 yalifanyika bila kupita Mfuko Mkuu. Kwa mujibu wa maelezo ya CAG, sehemu kubwa ya fedha hizi zinatokana na fedha zilizopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutoka kwa wadau wa maendeleo. Fedha hizi za miradi zinaonekana katika vitabu vya Bajeti lakini CAG hazioni kuingia mfuko Mkuu na hivyo kutoka kwake ni kinyume cha Sheria

Matumizi ya aina hii licha ya kuwa ni kinyume na katiba na sheria za nchi, huwa ni kichaka cha kuficha ubadhirifu kwani kutumia fedha namna hii kunamnyima CAG kufanya kazi yake ya Udhibiti wa Fedha za Umma.

ACT Wazalendo tunamtaka Waziri wa Fedha na Mipango aheshimu Katiba na Sheria katika matumizi ya fedha ili kutotoa mwanya wa ufisadi kwa fedha za umma.

Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inafanya usuluhishi sahihi wa taarifa za fedha zilizotolewa kwa Wizara mbalimbali na fedha zilizopokelewa moja kwa moja kwenye maendeleo katika miradi. Hazina iweke mahesabu sawasawa ili kuhakikisha ‘credibility’ ya taarifa zake.

Mbolea ya ruzuku kutowafikia wakulima

CAG katika ripoti ya ufanisi wa usimamizi wa shughuli za kilimo ameonyesha kuwa wakulima wengi nchini hawajapata mbolea zenye ruzuku licha ya Serikali kutenga wastani wa shilingi bilioni 150 kila mwaka.

ACT Wazalendo tulitoa mapendekezo ya kukabiliana na hali ya kupanda kwa bei za pembejeo (mbolea) ikiwemo kuweka ruzuku ili kushusha bei na upatikanaji wake. Mpango wa ruzuku ulibeba matumaini makubwa kwa wakulima kwa matarajio ya kupunguziwa gharama na kuhakikishiwa urahisi wa upatikanaji.

CAG ameonesha kuwa wakulima milioni 2.55 kati ya milioni 3.4 waliosajiliwa katika mpango wa ruzuku (sawa na 75%) hawakupata wala kutumia mbolea kupitia mpango wa ruzuku licha ya kuwa na sifa ya kupata mbolea hiyo ya ruzuku.

Aidha, CAG amebainisha kuwa Wafanyabiashara 1,712 kati ya 4,346 waliosajiliwa (sawa na 41%) katika programu ya ruzuku hawakuuza wala kusambaza mbolea ya ruzuku .

Halmashauri 41 kati ya 181 hazikupata kabisa mbolea ya ruzuku, kitendo kilichosabisha usumbufu kwa wakulima kusafiri umbali mrefu kufuata mbolea.

ACT Wazalendo kwa hatua za uwajibikaji tunataka

Serikali itueleze fedha za ruzuku zimepelekwa wapi ikiwa wakulima hawajanuifa nayo?

Tunaitaka Serikali kuingiliakati mfumo wa uagizaji na usambaziji kwa kuiwezesha kibajeti Kampuni ya taifa ya Mbolea (TFC) kuagiza nje na kusambaza mbolea nchini. Kwaajili ya kuongeza uwezo wa usambazaji wa mbolea unaotokana na kulegalega kwa waagizaji na wasambazaji binafsi.

Tunaitaka Serikali irejeshe mfumo wa uagizaji wa Pamoja wa mbolea

Serikali illipe kwa wakati madai ya wasambazaji wa mbolea.

Kwa hatua ya kudumu, kuondoa utegemezi wa mbolea kutoka nje, kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili watu waweze kujenga viwanda vya kuzalisha mbolea nchini na kuimarisha uzalishaji kwa viwanda vilivyopo.

Tatizo la uagizaji, uingizaji na usambazaji wa mafuta nchini.
Kwa muda tumeshuhudia Changamoto ya Kupanda kwa gharama ya mafuta, uagizaji wa pamoja na usambazaji wa mafuta. Hii imepelekea kunaongeza sana Gharama za maisha, na Uchumi, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa Nauli za mabasi na Dalaladala nchini. CAG amefanya Ukaguzi wa ufanisi wa kiutendaji na uagizaji wa mafuta na hizi ni miongoni mwa hoja alizoibua;

Nchi haina hifadhi ya Taifa ya Petroli, CAG anaonesha kama Taifa kukosa hifadhi ya Petroli ya mkakati unaiweka nchi katika hatari ya kuwa na uhaba wa nishati wakati wa shida, CAG ameonesha kuwa Wizara haikuandaa mpango wa dharura wa Petroli kama unavyohitajika kisheria kwa takriban miaka 8 kutoka 2015-2023

Uwezo mdogo wa Miundombinu mafuta nchini, CAG anaonesha kwamba kuna Bomba Moja tu linalotumika kuingiza mafuta Tanga, mtwara na Dar es salaam na Bomba hilo moja ndio hutumika kusafirisha Petroli na Dizeli mtawalia, baada ya kusafirisha petrol linasafishwa ili kupitishwa Dizeli, Bomba hili limetumika kuanzia 2012 ambapo lilitumika kusafirishia Metric Tone 250,000 sasa linapitisha 650,000.

Serikali ya CCM inafanya mchezo na Suala hili nyeti, sisi tunaona ni lazima kuweka mkazo mkubwa sana kwenye eneo hili hasa ukizingatia mambo kadhaa yanaweza kuteteresha Usambazaji wa Mafuta Duniani kama vile, migogoro ya kieneo (vita mashariki ya kati), majanga, vikwazo vya kiuchumi kwa baadhi ya nchi, kupanda na kushuka kwa thamani ya dola na kuadimika kwa dola kunaweza kusababisha kupanda sana au kutopatikana mafuta kwa wakati na kuacha uchumi wetu mashakani.

ACT Wazalendo Tunataka Serikali ijenge uwezo wa Miundombinu ya kisasa na Usiamaizi wa hifadhi ya Mafuta nchini, tuwe na angalau hifadhi ya Mafuta ya Miezi mitatu.

kuelekeza nguvu hiyo katika Kuwekeza kwenye matumizi ya Gesi Asilia kama nishati mbadala.

Serikali iboreshe Miundombinu ya kupokelea, na kusambazia Mafuta nchini, ijenge Bomba kubwa na la kisasa la kupokelea Mafuta katika bandari zetu.

Serikali imepanga kuwanyima Fursa watoa huduma wazawa katika Miradi ya Gesi na Mfuta nchini (Local content)

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ilipaswa kufanya utafiti wa msingi wa uwezo wa soko la watoa huduma wa ndani na ushindani ambapo utafiti ulitakiwa kuwa umemalizika ifikapo tarehe 30 Juni 2023 lakini hadi sasa haukufanyika. utafiti huu ni kwa ajili ya kuwasaidia wazawa kupata nafasi ya kutoa huduma katika miradi ya Gesi asilia wa LNG na Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki.

ACT Wazalendo Tunazitaka mamlaka husika zifanye haraka utafiti huo haraka ili kuweka mazingira wezeshi kwa watanzania kupata nafasi ya kutoa huduma katika miradi husika, Tunaendelea kupigania Taifa la Wote, Maslahi ya wote, tunataka Rasilimali za Tifa hizi zinufaishe watu wote hivyo ni lazima watambulike.

Usimamizi mbovu wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi)

CAG amebaini kuwa kuna usimamizi mbovu kwa wakala wamabasi yaendayo haraka (DART)ambayo ipo chini ya OR-TAMISEMI, katika ripoti yake ametoa hoja tatu kubwa zinazothibitisha uzembe katika uendeshaji wa Mradi.

Kukamilika kwa miradi ya Awamu ya pili na kutotoa huduma, Mradi wa Bilioni 217.48 wa kutoka Katikati ya Jiji hadi mbagala umekamilika kwa 98.86% lakini hautoi huduma.

DART Kukalia bidhaa za Bilioni 3.43 za mifumo ya kukusanya Nauli, CAG ameonesha kuwa DART ilinunua Kadi janja (Smart cards) za Bilioni 1 na mifumo mingine ya TEHAMA ya kukusanyia nauli ya Bilioni 2.43 vimetelekzwa.

Utoaji wa Huduma usioridhisha, CAG ameonesha katika Mabasi 210 ya mkataba Mabasi 132 (63%) yalikuamabovu na hayatoi huduma na kwamba yanahitaji Bilioni 2.1 ya matengenezo.

Hoja zote alizotoa CAG ni hoja zinazotokana na Uzembe wa kiutendaji na kimenejiment na zina harufu ya Uhujumu Uchumi. Hii inasababisha kukosekana kwa thamani halisi ya fedha na kutotatua tatizo la usafiri jijini Dar es salaam.

Badala ya kurekebisha masuala tumemsikia Waziri wa OR-TAMISEMI ameona Suluhu ni mwekezaji Binafsi na ameipa miezi saba DART kupata mwekezaji binafsi, na tayari tumesikia kuwa tayari mwekezaji kutoka UAE ameshapatikana kuendesha huduma za mwendokasi. ACT Wazalendo tunaona uzembe na usimamizi mbovu wa mashirika ya Umma hauwezi kutatuliwa kwa kugawa miradi kwa watu binafsi, kufanya hivyo hakutatui matatizo.

Uchambuzi wetu unaona kuwa pesa iliyotumika kutengeneza mradi ni pesa za mkopo ambazo zinalipwa na watanzania wote, uzoefu unaonesha kuwa Nchi nyingi miradi ya usafiri ndani ya majiji zinaendeshwa na Majiji husika au serikali mfano ni Jiji la Berlin, Tokyo, Singapore, NewYork (NewYork City Depertment of Transportation), London (transport for London), Toronto (Toronto transit Commission) kutaja kwa uchache.

ACT Wazalendo Tunapendekeza yafuatayo;

Mfumo wa Kielekroniki wa kukusanyia nauli uliotelekezwa, ufungwe maramoja na uanze kutumika.

Bodi ya wakurugenzi ya DART ivunjwe yote na kuundwa upya, kwa kuzingatia wataalamu wa sekta ya hiyo ambayo itauendesha mradi kwa faida.

Waziri wa OR-TAMISEMI ajiuzulu kwa kushindwa kuisimamia DART na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa.

Tunamsihi DPP kufanya uchunguzi wa kijinai kubaini wote waliohusika kuhujumu Mradi wa mabasi ya mwendokasi Dart na kuwafikisha mahakamani.

Mradi wa Bwawa la kuzalishia umeme la Mwl. Nyerere
Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) limekuwa likiguswa na hoja za ukaguzi kila mwaka. Kuanzia mwaka wa fedha 2019/20, 2020/21, na 2021/22 zimejitokeza hoja kuanzia eneo la kitalaam masuala ya usanifu, ufuatiliaji wa sheria, udhaifu wa kiusimamizi, ulipaji wa gharama za ziada na masuala ya manunuzi.

Ripoti ya CAG 2022/23 imeendelea kuonyesha bado kutofanyiwa kazi hoja zake za huko nyuma na hasa kutotolewa kwa fedha za CSR shilingi bilioni 270 asilimia 3% ya fedha za mradi. CAG ameonesha mkandarasi wa bwawa la mwalimu Nyerere hajatoa fedha hizi zilizopaswa kupelekwa katika miradi ya kijiamii kwa wananchi wa Rufiji ambao mradi unajengwa katika eneo lao.

Aidha, hoja kubwa inayojirudia ni kuchelewa kwa Mradi kwa zaidi ya miaka miwili sasa kitendo kinachosababisha nchi yetu kumlipa Mkandarasi malipo ya ziada yenye thamani ya shilingi bilioni 327.

Ukiachilia, gharama tunayolipa kama taifa kutokana na ucheleweshwa huu. Tumeona katika siku za hivi karibuni kumekuwa na changamoto juu ya uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini. Katika mazingira ambayo bwawa limepokea maji ya kutosha (limejaa) lakini kinu cha kuzalishia umeme kilichofunguliwa ni 1 kati mitambo 9. Kwahiyo umeme unaozalisha ni Megawati 235 pekee kati ya Megawati 2115 zilizotarajiwa.

Katika hali hii ya mshangao, Wizara ya Nishati kupitia TANESCO imefungulia maji ambayo yameenda kusababisha maafa makubwa kwa wakazi wa Rufiji na Kibiti. Maji ambayo yangeweza kutusaidia kuzalishia umeme wa kutosha na kuzuia athari za mafuriko yamegeuka kuwa laana na majuto kwa wananchi wanaozungukwa na Mradi.

Hivyo basi, ucheleweshaji na uzembe mkubwa katika usimamizi wa Mradi huu umeligharimu taifa letu sio tu fedha zilizoteketea kwa kulipa ziada na maisha ya watu kutokana na mafuriko.

ACT Wazalendo tumeona udhaifu ulioibuliwa na CAG wa serikali kuamua kutoa ukandarasi wa usimamizi wa Ujenzi wa mradi wa bwawa la mwalimu Nyerere kwa taasisi ya serikali yenyewe umegharimu mali na maisha ya watu wa Rufiji. Tunaitaka serikali iwajibike kwa uzembe na iwalipe fidia wananchi waliopata hasara Rufiji kwa haraka.

Udhaifu katika Usimamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Unaweka rehani Afya za wanachama

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Serikali (CAG) kwa mara nyingine katika ukaguzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ameendelea kuonesha kasoro za usimamizi, kushindwa kukusanya madeni ya wanachama na deni la mkopo kwa Serikali.

CAG amezifafanunua hoja hizi kama zifuatazo kuhusu Mfuko wa NHIF;

Kasoro za usimamizi wa Mfuko, NHIF kama taasisi inaendaelea kugubikwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji ambazo zinadidimiza ufanisi wa mfuko kifedha na kudidimiza utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kutoa huduma bora kwa wanachama.

Kushindwa kukusanya madeni kwa huduma walizotoa, CAG ameonyesha hadi kufikia 30 Juni 2023 NHIF imekusanya shilingi bilioni 5.6 (12.6%) pekee kati ya shilingi bilioni 42.57 inazozidai taasisi za Serikali na binafsi ikiwa ni michango ya wanachama. Kati ya hiyo michango ambayo zinadaiwa Taasisi za Serikali ni shilingi bilioni 19.04 (45%) na shilingi bilioni 23.53 (55%) zinajumuisha madeni kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Serikali kushikilia shilingi bilioni 208 inayodaiwa na NHIF, CAG katika ripoti yake 2022/23 ameonesha Serikali inadaiwa na NHIF kutokana na fedha ilizokopa tangu mwaka 2020.

Ni dhahiri kuwa NHIF haiwezi tena kukidhi kulipa gharama za mafao ya huduma za matibabu kwani michango inayokusanywa ni kidogo kuliko gharama za kuhudumia wanachama na hivyo kulazimisha Mfuko kuuza mali zake ili kupata Fedha za kufidia nakisi. Kwa hali hii hapatakuwa na NHIF ndani ya miaka 3 inayokuja ni wakati wa Serikali sasa kuchagua mfumo sahihi wa uchangiaji wa wanachama ambao utaleta mapato ya kutosha kwa NHIF ili iweze kuhudumia watanzania kutokana na vipato vyao na kuwapa huduma stahiki.

ACT Wazalendo tunatoa wito kwa Mamlaka za uteuzi kufanyia mabadiliko Bodi na Menejimenti na kushughulikia madai yote ya watendaji wanaohujumu mfuko huu.

Pamoja na mapendekezo haya ya kimenejimenti, ACT Wazalendo tunaona mfumo mzima wa huduma za afya unapaswa kufanyiwa mabadiliko kwa kufungamanisha Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii.

Mapendekezo ya ACT kwenye mfumo mpya ni yafuatayo;

Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na PSSSF) iwe na Fao la Matibabu ambapo kila mwanachama wa Mifuko hiyo awe moja kwa moja mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (ulioboreshwa). 20% ya Michango ya Wanachama wa Mifuko hii itawasilishwa NHIF kila mwezi kwa ajili ya kugharamia Fao la Matibabu. Kwa Pendekezo hili NHIF itapata wanachama wapya milioni 1.9 waliopo kwenye mifuko kutoka sekta rasmi na makusanyo ya takribani shilingi bilioni 530 kwa mwaka.

Serikali itoe kivutio kwa watu waliopo sekta isiyo rasmi kama vile wafanyabiashara wadogo, wavuvi, wakulima, wafugaji, mamalishe nk kujiunga na Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwachangia theluthi ya mchango wa kila Mwezi yaani shilingi 10,000 (Matching Scheme). Moja ya chanzo cha fedha cha kivutio hiki ni 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri kama ilivyopendekezwa mwaka jana. Kwa Pendekezo hili takribani watu milioni 7.4 watakuwa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na hivyo wanachama wa NHIF na makusanyo ya Dola za kimarekani 266M kwa kugharamia Matibabu.​

Serikali iwalipie asilimia 100 wafaidika wa TASAF kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na hivyo kuwa wanachama wa NHIF. Kwa pendekezo hili takribani watu milioni 6.3 watapata fao la Matibabu na makusanyo ya Dola za Marekani 205M kwa Mfuko.

Ili kutekeleza mapendekezo yote hapo juu Serikali itenge kwenye bajeti ya kila mwaka asilimia 2.5 ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia matibabu na hivyo kuwezesha watu wazima Milioni 11 kuwa na Bima ya Afya pamoja na wategemezi wao. Kwa mfumo huu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hautakufa na ndoto ya Bima ya Afya kwa wote itafikiwa.

ATCL inaendelea kupata hasara kwa sababu ya kukodi ndege TGFA
Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) inaendelea kupata hasara kwa miaka sita mfululizo. Licha ya kupokea mabilioni ya fedha za walipa kodi kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji. Serikali inatoa imetoa ruzuku ya shilingi Bilioni 39 kwa ajili ya kugharamia mishahara ya wafanyakazi, mafunzo ya majaribio na miradi ya maendeleo. Katika Uchambuzi wetu wa mwaka wa fedha 2021/22 tulionesha makosa yanayofanywa yanayopelekea hasara kubwa na kuzorota kwa uendeshaji wa Shirika hili. Ikiwemo suala umiliki na kutokaguliwa kwa manunuzi Kwasababu ya kuwekwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu.

CAG katika ukaguzi mwaka wa fedha 2022/23 ameonesha kuwa ATCL ilipata hasara ya shilingi bilioni 56.64. Huku akitaja sababu za kupata hasara hiyo kuwa ni zile zile ikiwemo gharama kubwa za uendeshaji na gharama za ukodishaji wa ndege na Bima ya ndege Airbus A220-300 kutokana na ubovu wa Injini na kutu.

Uchambuzi wetu unaonyesha kwamba hasara inayopata ATCL kwa sehemu kubwa kunatokana na Mfumowa umiliki wa ndege, mfumo uliopo sasa ATCL haimiliki ndege. ndege zote zilizonunliwa na Serikali kwa kodi za wananchi zinamilikiwa na TGFA na kukodishwa kwa ATCL.

Aidha, kuendelea kuiweka TGFA chini ya Ofisi ya Rais kunazuia uwajibikaji kwa CAG kufanya ukaguzi na kuweka wazi kwa umma hasa kwenye masuala ya manunuzi ya ndege yanayoendelea kufanywa yanafanywa gizani. Kushindwa kukaguliwa na kuweka wazi ndio tunashuhuidia kununuliwa ndege mbovu zinazotengeneza hasara kwa ATCL.

Iwapo ATCL itamiliki ndege, gharama za ukodishaji zisingekuwepo kwenye vitabu vyake vya mahesabu hata hivyo kama ATCL ingemiliki ndege ingeshughulikia kwa wakati suala la ubovu wa ndege na CAG angeikagua.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iimilikishe ATCL ndege zote inazokodishiwa na kuirejesha TGFA chini ya wizara ya uchukuzi. Tunamtaka CAG Kufanya ukaguzi maalum wa manunuzi ya ndege tangu tulipoanza kununua ndege 2016 hadi sasa.

Hitimisho
Uchambuzi wetu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali umeangazia masuala 10 ambayo tumeyachagua kutokana na umuhimu wake. Hata hivyo Hoja za ukaguzi katika Ripoti nzima ni nyingi sana. Licha ya hoja mpya zilizojitokeza katika ukaguzi wa Mwaka huu, hoja nyingi ama zinajirudia rudia kutoka miaka ya nyuma au ni mwendelezo wa makosa ya nyuma.

Uchambuzi wetu unatuonyesha hoja nyingi zinazohusua uzembe, matumizi mabovu, ubadharifu na matumizi ya kinyume na sheria pamoja maamuzi yasiyozingatia maslahi mapana ya taifa. Hoja zenye thamani ya zaidi shilingi trilioni 6.6 zinaakisi Ubadhilifu, Fedha za Umma zimefujwa na Hakuna anaewajibika

Njia pekee ya kubadilisha haya ni kuiondosha CCM madarakani. Watanzania hatuwezi kuendelea kukamuliwa kodi kila siku ili fedha zetu zikafujwe namna hii na wajanja wachache waliopewa Madaraka. Wanatuambia Kazi inaenaendelea, kumbe ni kazi inayoendelea ni kupiga hela za Watanzania. Hali hii imechosha! Hali hii imetosha! Na sisi ACT Wazalendo tumedhamiria kuifikisha mwisho. Tutashirikiana na nyinyi Watanzania kuhakikisha tunaiondosha hali hii kwa kupigania kila senti ya fedha zenu zinazokusanywa kutokana na kodi zenu inatumika kujenga taifa la wote kwa maslahi ya wote.

Ahsanteni Sana.

ACT Wazalendo
Aprili 20, 2024
Dar es salaam.
 
Wizi, Ufisadi, Rushwa, Upendeleo ni Utamaduni ambao upo kwa Watawala Weusi wote waliopo Afrika na duniani kote. Hata nyinyi ACT-Wazalendo leo hii mkipewa Madaraka ya kutawala ktk nchi hii ya Tanzania, mtafanya mambo haya haya ambayo mnayapigia kelele leo hii.
 
Back
Top Bottom