View attachment 1812671
Nimesoma petisheni dhidi ya Diamond Platnamz ili kumzuia kushiriki BET Awards lakini haina mashiko.
Naona petisheni inaratibiwa na mwanaharakati anayejitambulisha kwa jina la Liberatus Mwang'ombe, na kunadiwa mitandaoni na kupitia akaunti za twitter za Maria Sarungi, Hilda Newton, kigogo2014, Ansbert Ngurumo kupitia gazeti lake la Mtandaoni la Sauti Kubwa, na wengine kadhaa.
Kuna hoja sita zilizotajwa katika petisheni nazo ni hizi hapa:
- Kwamba, Diamond Platnamz hakupaza sauti wala kuonyesha mshikamano na wasanii kama vile Roma Mkatoliki, Nay wa Mitego na Idris Sultan, waliopinga utawala dhalimu wa hayati Magufuli.
- Kwamba, Diamond Platnamz alitumia bishara yake ya sanaa ya muziki kutakatisha ukatili wa hayati Magufuli na washirika wake kwa kuwajengea taswira chanya mbele ya jamii. Anatajwa kutunga wimbo wa "Magufuli Baba Lao," kupanda katika majukwaa ya kampeni za CCM mwaka 2015 na 2020, na kumfanya Paul Makonda Mlezi wa biashara zake, wakati Marekani tayari imetoa taarifa ya kusema kuwa Makonda anahusika katika kusababisha utendwaji wa uhalifu dhidi ya ubinadamu.
- Kwamba, Tuzo za luninga ya BET zimekuwa na heshima mbele ya Waafrika wengi kwa sababu ya kutambua kazi za wasanii ambao wanazo sifa za kuinuliwa kwa sababu wao ni mfano wa kuigwa katika jamii, wakati Diamond Platnamz hana sifa hiyo, kwani yeye ni mbinafsi, mchoyo, bendera fuata upepo, na mtu mwenye kufungamana na mifumo dhalimu.
- Kwamba, Diamond Platnamz alitumia bishara yake ya sanaa ya muziki kutakatisha ukatili wa Paul Makonda aliyetajwa na Marekani kuwa anahusika na makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kumjengea taswira chanya mbele ya jamii.
- Kwamba, Diamond Platnamz alitumia bishara yake ya sanaa ya muziki kutakatisha ukatili wa Paul Makonda aliyetajwa na Marekani kuwa anahusika na makosa ya uvunjaji wa haki za watu wenye jinsi tata (GLBITs) kwa kumjengea taswira chanya mbele ya jamii
- Kwamba ni mwanachama wa CCM chama kilichokuwa kinaongozwa na hayati Magufuli anayelaumiwa kwa udikteta
Ninazo sababu kadhaa za kupinga petisheni hii yenye msingi wake katika falsafa ya jino kwa jino. Nitaeleza kwa kifupi.
Mosi, kitendo cha mfanyabiashara kutafuta faida kwa kuuza huduma kwa mteja mwenye tabia tofauti na yake sio kosa kimaadili wala kisheria.
Pili, kuchagua kukaa kimya juu ya tabia mbaya ya mteja wako ili kukinda uteja kati yenu sio kosa kimaadili wala kisheria.
Tatu, kuchagua itikadi na sera za chama kinachoongozwa na watu wenye tabia mbaya sio kosa kimaadili wala kisheria.
Nne, matamko ya Marekani juu ya uchaguzi na Makonda yanatana makosa ya jumla (statements of offense) bila kutaja mchanganuo wa tuhuma (particulars of offense) na hivyo hayawezi kutumika kama msingi wa maamuzi huru.
Tano, kumshambulia Diamond kwa sababu zilizotajwa hapo juu ni sawa na kubomoa umagufuli kwa mkono wa kushoto na kuujenga kwa mkono wa kulia. Umagufuli unajumuisha tabia kama vile kutengeneza habari feki na kuzisambaza (disinformation), kusambaza in habari feki (misinformation), kusambaza habari binafsi bila ridhaa ya mhusika (malinformation), kujipa mamlaka ya kubadilisha ukweli kuwa uwongo na kinyume chake (constructivism), kuthamini matokeo bila kujali njia za kufikia matokeo hayo (machiavellism), kutumia neno lenye maana zaidi ya moja bila kubainusha maana kuaudiwa kwa makududi (equivocation), kutafsiri maneno ya mtu baki kinyume na maana aliyokusudia yeye (spinning), etc
Sita, Diamond Platnums ni mfanyabiashara anayeuza sanaa ya muziki kwa yeyote bila kujali itikadi ya kisiasa. Sanaa ni huduma inayonunuliwa kama bidhaa baki, kama vile nguo, mabango, vitabu, vipeperushi, fremu za biashara, magari ya abiria, na kadhalika. Walaji wa huduma hizi wanaweza kuwa na mitazamo tofauti na mitazamo ya muuzaji.
Na muuzaji anaweza KUTABIRI kuwa kwa kuwauzia huduma/bidhaa yake ILI APATE FAIDA wao wataweza kutumia bidhaa/huduma hiyo kuendeleza mitazamo yao, ambayo hata hivyo, muuzaji hazikubali, bali ANAZIVUMILIA tu.
Kwenye sayansi ya maadili hali hii inaelezeka vema kwa kutumia kanuni ya matokeo pacha (principle of double effect). Ni sawa na ambavyo, msanifu wa mipango mikakati ya habari, mwenye kuamini katika itikadi ya Chadema, ataajiriwa na chumba cha habari cha UHURU Media kuwafanyia kazi ya malipo.
Kazi atakayofanya itampa UJIRA na KUENDELEZA ITIKADI ASIYOIUNGA MKONO. Hili la pili ni matokeo yanayotabiriwa, na kuvumiliwa, japo hayachaguliwi moja kwa moja.
Na saba, kukataa kutumia kanuni ya matokeo pacha (principle of double effect) katika kisa cha Diamond Platnums, maana yake ni kwamba tusiitumie katika visa vingine pia, vyenye kufanana na kisa hiki. Kwa kuamua kutoitumia tutalazimika kuandika petisheni kwa kila kisa.
Nitatoa mifano michache ya visa vinavyofanana na kisa cha Diamond Platnums, lakini ambavyo havijaandikiwa petisheni.
Mfano wa kwanza: Julai 2020, Msajili wa Vyama, Jaji Mtungi, alitamka kuwa kanuni ya 6.5.2(d) ya Chadema ni batili kwa kuwa inapingana na ibara 5.2.4 ya katiba ya Chadema, toleo la 2019. Lakini Novemba 2020, Kamati Kuu ya Chadema ilitumia kanuni batili ya 6.5.2(d) kuwaadhibu kina Mdee, na hivyo kuvunja ibara 5.2.4 ya katiba ya Chadema.
Sasa hivi wajumbe wa Kamati Kuu wanazunguka nchi nzima kueneza chama, na wanapokelewa na wanachama wa Chadema. Kitendo cha wananchi kuwapokea wajumbe waliovunja Katiba ya chama kinamaanisha matokeo mawili: kuendeleza kazi za chama na kushirikiana na viongozi waliovunja Katiba.
Hili tokeo la pili linavumiliwa, kwa mujibu wa kanuni ya matokeo pacha, kwa kuwa chombo chenye mamlaka juu ya Wajumbe wa Kamati Kuu ni Baraza Kuu na sio wanachama wa ngazi za chini. Nje ya kanuni ya matokeo pacha wanachama wa mikoani wanapaswa kuwasusa wajumbe wa Kamati Kuu.
Mfano wa pili: Askofu Mkatoliki aliyekula kiapo cha useja anazaa mtoto na muumini wake. Habari zinasambaa kwa waumini. Lakini, jambo hili linavumiliwa na waumini, kwa mujibu wa kanuni ya matokeo pacha, kwani waumini wanaendelea kuhudhuria ibada zinazoongozwa na askofu huyo.
Kwa kitendo hiki waumini wanachagua ibada na kuvumilia uovu wa askofu, wakiwa wanasubiri mamlaka za juu kuchukua hatua stahiki. Nje ya kanuni ya matokeo pacha, waumini wanapaswa kumsusa askofu.
Mfano wa tatu: Kuna wafanyabiashara wengi ambao ni wanachadema wanafanya biashara zinazowahudumia vongozi wa CCM waliokuwa maswahiba wa Magufuli. Lakini hawa hawajaandikiwa petisheni.
Kwa hiyo, kama tunakubaliana na hoja kwamba tunapaswa kuepuka tabia ya kujipinga katika maamuzi yetu, basi, hatupaswi kusaini petisheni dhidi ya Diamaond Platnums. Naongelea kanuni ya
consistency ambayo ni kiashiria cha kanuni ya ukamilifu, yaani
integrity.
Kwa ujumla, umagufuli ni itikadi hatari kwa usalama wa nchi bila kujali kwamba inatekelezwa na wana CCM, wana CHADEMA, watu walio ndani ya nchi, watu walio nje ya nchi, au vinginevyo.
Na propaganda hasi zinazotegemea
fallacy of association ni mkakati wa kupakana matope bila uhalali. Ni vivyo hivyo kwa tamathali ya semi iitwayo satire.
Yaani, "the use of humour, irony, exaggeration, or ridicule to expose and criticize people's stupidity or vices, particularly in the context of contemporary politics and other topical issues."