Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amefunguka sababu kubwa inayopelekea wasanii wengi kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na wasanii hao kuwa na majina makubwa lakini mfukoni hawana kitu.
Mhe. Nape Nnauye aliyasema haya kwenye kipindi cha Saturday Sports kinachorushwa na East Africa Radio.
Waziri alidai moja ya sababu kubwa inayowachanganya wasanii wengi ni kuwa na msongo wa mawazo kutokana na uhalisia ulipo, kuwa wana majina makubwa katika jamii lakini majina hayo hayafanani na uwezo wao kutatua matatizo, au changamoto za maisha yao ya kila siku.
“Unajua mfano wasanii wetu wengi wanaingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kuwa na majina makubwa lakini mfukoni hawana kitu, ndiyo maana mimi napigania kutengeneza mfumo ambao hata kama kesho sitakuwepo mimi watu waweze kunufaika na kazi zao.
Na hili tatizo ni mpaka kwa wachezaji unakuta tunawachezaji wana majina makubwa lakini hawana pesa, ndipo hapo mchezaji anatoka kucheza mechi anakwenda kula mihogo sababu ya kukosa fedha, hivyo huwa sipendi sana kufanya vitu kwa ajili ya kusherehekea siku moja bali nataka kutengeneza njia ili watu waweze kunufaika hata kwa baadaye.” Alisema Nape Nnauye
“Unajua hata kipindi kile Samatta anarudi watu wengi walikuwa wanataka tumfanyie shamra shamra lakini mimi siamini katika furaha ya siku moja ndiyo maana kama serikali tulifikiria na kuona kwamba tumpatie kiwanja ili ibaki kumbukumbu kwake na kuhamasisha watu wengine, vitu kama hivi vinamsaadia msanii au mchezaji kuliko hisho sherehe za siku moja” alisisitiza Nape Nnauye.
Source: Eatv