Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,187
- Thread starter
- #16,281


BASATA, iwapi taarabu yetu ya asili?
Juma Kasesa

Juma Kasesa

Leo katika Jamvi letu nataka nigusie kiduchu kuhusu muziki wa taarabu ambayo una asili ya utamaduni wa jamii ya watu wa pwani ya Afrika Mashariki, hapa nikizungumzia miji ya Mombasa, Tanga, Zanzibar, Kisumu na kwingineko.
Kimsingi hoja iliyonisukuma kuandika Jamvi hili ni baada ya kuutazama kwa jicho la pili muziki huo wapi ulikotoka na wapi unaelekea ambako ni ashirio kuwa anguko la utamaduni wa muziki wa pwani ya Afrika Mashariki.
Pengine kabla Jamvi hili halijaingia kwa undani katika kile ambacho kimelisukuma kuzungumzia muziki huu, ni vema msomaji ukafahamu muziki wa taarabu asili ya pwani ya Afrika Mashariki umeimbwa na waasisi wengi lakini kwa uchache naweza kukutajia Bi Kidude, Issa Matona, Mohamedi Kassim, Shakila Saidi, Sabaha Muchacho, Mwanahawa Ally, Juma Ballo na wengineo wengi.
Waasisi hao kwa nyakati tofauti waliweza kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali ambazo ziliitangaza pwani ya Afrika Mashariki na kupata umaarufu na nguvu za kiuchumi kutokana watalii wa ndani na wa kimataifa kwenda kutembelea baadhi ya miji na kujifunza masuala mbalimbali na utamaduni wa wakazi wa pwani hiyo.
Jamvi la Kulonga linakujulisha kuwa nyimbo nyingi za wakongwe hao ambao wengine wameshatangulia mbele ya haki, waliweza kutunga na kuimba nyimbo za kupigana vijembe ama kutambiana kulingana na ubora wa makundi yao, lakini wakitumia tafsida katika mashairi na ilikuwa ni kazi ngumu kutambua kijembe hicho kilikuwa kikililenga kundi gani kutokana na uficho wa maneno.
Pengine nikumbushe mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati mwimbaji nyota wa bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), Khadija Omary Kopa, alipotunga wimbo wa ‘TX wangu mpenzi', huu ulikuwa ni wimbo ambao kwa wachambuzi wa muziki wa taarabu ulikuwa na maneno mengi ya karaha na kuudhi na laiti Kopa angeamua kuyatumia bila tafsida usingefaa kusikilizwa katika jamii ya watu wastaarabu na waungwana lakini aliamua kumvika johoo la udaktari mtu ambaye alikuwa akimtaja kama mpenziwe akimsifia kwa namna alivyoweza kumtibu maradhi yake.
Lakini si Khadija pekee hata ilipofika katikati ya miaka ya tisini na mwanzoni mwa mwaka 2000, pale ambapo ndipo mapinduzi ya muziki huu yaliibuka yakiasisiwa na makundi hasimu ya taarabu ambayo yalikuwa ni TOT chini ya Kopa huku Muungano ikitamba na hayati Nasma Kidogo, bado kulikuwa staha katika nyimbo zao walizoimba ingawa hali ilikuja kubadilika baadae kutokana mashabiki kuwalazimisha kuimba bila tafsida.
Lakini ikiwa hiyo haitoshi ubora wa mashairi mengi ya wakati huo yalisaidia kuuutangaza muziki huo sambamba na ala zilizokuwa zikitumika katika kutia nakshi muziki huo, ambao kwa Tanzania, ni Zanzibar ndiko ambako bado hadi leo wanapiga kidogo muziki wa taarabu wenye asili ya Pwani yetu ya Afrika Mashariki.
Jamvi la Kulonga ni mmoja ya wadau wakubwa wa muziki wa Taarabu wenye asili ya Pwani, lakini kutokana na mabadiliko ya dunia na kuibuka kwa utandawazi, muziki huo umeonekana kupoteza muelekeo huku Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama chombo chenye dhamana ya kulinda utamaduni na sanaa ya Mtanzania kikiwa kimekaa kimya huku hali ikizidi kuwa tete.
Nikirudi katika hoja ya msingi iliyonisukuma kuandika Jamvi hili, ni wazi utagundua kuna tofauti kubwa ya muziki huo na huu wa sasa ambao unaitwa ‘Modern Taarabu' kutokana na kasoro nyingi ambazo zimeutawala muziki huo.
Swali ambalo Jamvi hili linajiuliza hivi kweli huu ndiyo muziki wa taarabu wa asili asili yetu? sitaki unipe jibu lakini kimsingi tumepotea njia na bahati mbaya hatuna wa kutoongoza kutokana waliopewa dhamana ya kulinda utamaduni na sanaa hiyo, ambao ni BASATA wamekumbwa na upofu, nani atamuongoza mwenzake?
Jamvi hili siyo kwamba linaikataa Modern Taarab, lakini kwa namna inavyozidi kuchakachuliwa ni wazi jahazi la muziki huo linaelekea mrama, kama si kuzama kabisa kutokana na muziki huo kuanza kumezwa na vionjo vingi vya Kikongo ambavyo vimekuwa vikiingizwa hapa, nikiwa nayazungumzia masebene na kutajana majina katika nyimbo hizo.
Mzee wa Jamvi la Kulonga anajiuliza, hivi kweli sisi tumekuwa watu wa kuiga kila kitu? Kama muziki wa dansi wenye asili ya Tanzania umemezwa na vionjo vya Kikongo tumeshindwa kuulinda sasa na huu wa taarabu nao? Hii ni hatari zaidi ya hatari na sitaki kuamini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kama kweli ina maofisa utamaduni ambao wameajiriwa kwa ajili ya kusimamia utamaduni na wakipokea mshahara ambao ni jasho la wanyonge huku wakilikalia kimya suala hili.
Kimsingi muziki wa taarabu ambao asili yake ni pwani ya Afrika Mashariki, ni ule pekee ambao mashairi yake yalikuwa na tafsida, lakini ukielimisha jamii kama ilivyo umuhimu wa muziki katika jamii, pia kwa wapenzi na mashabiki waliokuwa wakienda katika kumbi hizo za maonyesho walikuwa wakivaa mavazi ya kujistiri na wakitulia vitini, je, haya yanafanyika sasa?
Hofu ambayo imelizunguka Jamvi hili ni kwamba wanamuziki wa muziki wa taarabu wa sasa wakiambiwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya maonyesho ya muziki ni wazi hawawezi kuwa wawakilishi wazuri wa muziki huo kutokana na kupiga muziki ambao si wa asili ya Tanzania wala Pwani ya Afrika Mashariki.
Kwa mashabiki wenye kujua asili ya muziki huo, ambao waliwahi kutembelea pwani hii watagundua labda hawa ni Wakongo wanaoishi Tanzania, kutokana na kukosa ladha ile iliyozoeleka miaka mingi ya muziki huo.
Kwa leo nalikunja Jamvi lakini ni changamoto mpya kwa Baraza la Sanaa la Taifa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuanza kutathmini mwelekeo wa muziki wa Tanzania kwa ujumla ili kuepuka anguko ambalo linatunyemelea lakini lengo likiwa ni kulinda utamaduni na asili ya muziki wetu.

Tuwasiliane kwa barua pepe: jkasesa@hotmail.com, simu 0715-629298