Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,961
- 13,732
Hayo yameelezwa Julai 13, 2024 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Mohammed Mang’una wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mpango wa NEST360 (Newborn Essential Solutions and Technologies) nchini Tanzania, uliofanyika kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ubungo.
Ambapo amesema katika Mkoa wa Dar kuna vituo vya Serikali vinavyotoa Huduma ya Uzazi 136 kati ya hivyo, vituo 30 vinatoa Huduma za Upasuaji, vituo saba (7) pekee ndio vinatoa Huduma ya Watoto Wachanga wenye matatizo mbalimbali.
Amesema "Kwa sasa huduma hizi zinatolewa kwenye Hospitali za Mikoa na Taifa hali inayopelekea kuwa na msongamano mkubwa katika vituo hivyo na kuhatarisha maisha ya Watoto wachanga."
Aidha, katika Taarifa ya NEST360 imeeleza kwamba "Kiwango cha sasa cha vifo vya Watoto Wachanga ni 24 kwa kila Watoto 1,000 wanaozaliwa wakiwa hai, huku zaidi ya vifo 46,000 vikiwa ni vya Watoto Wachanga."
NEST kupitia taarifa yao wameeleza katika kutekeleza malengo ya kimataifa ya kuboresha afya ya watoto wachanga, Wadau hao wamesema kuwa walianzisha kifurushi cha 'NEST360' kwa ajili ya kuboresha mifumo ya afya inayolenga kuleta mabadiliko na kuongeza utunzaji wa watoto wachanga kote Afrika.
Kupitia taarifa hiyo imeelezwa kuwa katika mpango huo awamu ya kwanza, (2019-2023), NEST360 na Wizara ya Afya walibuni kifurushi kulingana na matakwa husika ndani ya Nchi kwa ajili ya utunzaji wa watoto wachanga wanaoumwa.
"Hadi sasa Watoto 100,000 kila mwaka katika hospitali 68 Malawi, Tanzania, Kenya, Nigeria wamefaidika na mpango wa NEST360. Kwa ushirikiano wa mashirika 22 yaliyoko Afrika, Marekani na Uingereza, muungano huu wa NEST360 unachukua mbinu ya kimkakati inayotokana na takwimu ili kuboresha huduma za watoto wachanga Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kiwango hicho cha fedha kikiwa kinatarajiwa kutumika katika ukarabati wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba kuimarisha uwezo wa Wataalamu wa Afya na Wahandisi wa Vifaa Tiba na kuimarisha mifumo ya data nchini Tanzania.
Pia Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya. Dkt. Grace Magembe amesema kuwa huduma katika mpango huo zinasaidia kuokoa Watoto Wachanga ambao wangefariki au ambao wangepata ulemavu kutokana na ubongo wao kupata changamoto.
Amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kupunguza vifo kwa Watoto, ambapo amedai kwamba kwa Mwaka 2018 Nchi nzima ilikuwa na wodi za Watoto Wachanga 18 lakini hadi Mwaka 2024 tayari kuna jumla ya wodi 241.
Aidha, kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Ifakara Health Institute (IHI), Honorati Masanja amesema wanatarajia kuongeza wigo na kuzifikia hospitali 18 kwenye mpango wa pili kutoka hospitali saba kwenye mpango wa kwanza.
Baadhi ya hospitali zilizotajwa kunufaika ni kutokea Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, ambapo amesema katika utekelezaji huo wanatarajia kutumia zaidi ya Shilingi Bilioni 5 katika ununuzi wa vifaa na zaidi ya Shilingi Bilioni 4.5 katika ufanikishaji wa mafunzo kwa Wataalamu na uboreshaji wa Mifumo ya Taarifa.
Ambapo ameongeza kuwa katika mpango huo wanatarajia kufanikisha teknolojia bora ya utoaji wa huduma kusudiwa huku akitaja kuwa mafunzo hayo yatawagusa Wataalamu akiwemo madaktari, wauguzi sambamba na ufanikishaji wa teknolojia muhimu na bora zinazotunza Watoto Wachanga.
Mradi huo awamu ya pili umeelezwa unalenga kutekelezwa katika ngazi ya afya ya msingi (hospitali za Wilaya na Kituo cha Afya ) huku ukiwa unalenga kuboresha huduma kwa Watoto Wachanga kwa kupunguza magonjwa, ulemavu na vifo.
Itakumbukwa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi aliyoitoa mwanzoni mwa mwaka huu (2024 ) ikieleza kuwa tathimini ya Serikali inaonesha vifo vya Watoto vimepungua kwa 35%, kutoka vifo 67 kwa Watoto 1,000 mpaka kufikia vifo 43 kwa Watoto 1,000.
Aliongeza, kwamba vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua kwa 80%, kutoka vifo 556 kwa vizazi 100,000 mpaka kufikia vifo 101 kwa vizazi 100,000.
Vilevile, taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ya Mwezi Januari alinukuliwa akieleza takwimu za vifo vya Watoto Wachanga vinavyotokea kwenye Mikoa ya Kanda ya Kati.
"Takwimu zinaonesha kwa Kanda ya Kati vifo vya Watoto Wachanga vimepungua kutoka 1,929 Mwaka 2021 Hadi 1,630 Mwaka 2023, vifo vya Uzazi vimeongezeka kutoka 151 Mwaka 2021 hadi 165 Mwaka 2023."
Pia, Ripoti iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Benki ya Dunia ikiripotiwa kwenye kurasa zao, inakadiria takriban Watoto Milioni 4.9 walikufa kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano katika Mwaka 2022 ikiwa ni kiwango cha kihistoria cha vifo vya Watoto kuwa chini ya milioni tano kwa mara ya kwanza.