Mfungo wa Ramadhani na Sikukuu ya Eid mbali na nyumbani

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,796
31,809
MFUNGO WA RAMADHANI NA SIKUKUU YA EID MBALI NA NYUMBANI
Hii mbali na nyumbani nimemwibia gwiji wa fasihi, Shafi Adam Shafi.
Adam Shafi ameandika kitabu, ‘’Mbali na Nyumbani.’’

Ukisoma kitabu hiki utapata hisia mtu anakuwaje akiwa mbali na kwao.

Mombasa si mbali na Dar es Salaam kiasi cha kumtia mtu unyonge ikiwa ataifunga Ramadhani katika mji huo na sababu ni kuwa hawezi kujihisi upweke.

Miaka mingi nyuma nilifunga Mombasa.

Wakati wa kufungua mwadhini ulipokaribia nikawa njisogeza katika msikiti wa jirani kwa kufungua na kusali sala ya Maghrib kisha nitafute hoteli ya kwenda kufuturu.

Nilikuwa nakwenda Mombasa mara nyingi kiasi nikawa nafahamika katika barza moja Mwembetayari.

Barza hii ilikuwa barza ya wanachama wa chama fulani cha siasa na kila nikipita pale husimama kusalimiana na jamaa na wao wataniuliza habari za TZ kama jamaa wa Kenya wanavyopenda kuita Tanzania.

Basi nilipopita barzani jamaa wakanizuia wakaniambia nisubiri tufungue pamoja kisha sote tutaelekea msikitini.

Nilichoshuhudia pale siku ile kinilishangaza sana.
Nilikuwa sijaona popote pale.

Ilipopigwa adhana zikawekwa ‘’snacks’’ kilima cha sambusa, kababu, jelebi na mapochopocho mengine na chupa za juisi.

Kwa kweli vitu vilikuwa vingi kiasi nikajiuliza baada ya hawa jamaa kula kiasi hiki watakwenda kweli majumbani kwao kufuturu?

Niko Uingereza Ramadhani imenikuta katika nchi na mji ambao Waislam ni wachache sana.
Ilikuwa ikifika wakati wa kufungua naingia unyonge mkubwa sana.

Dar es Salaam Ramadhani ni ‘’funfair,’’ wakati wa kufungua na kabla yake.
Nakumbuka nyumbani.

Misikiti inakuwa na watu wengi na wafanya biashara hasa akina mama wanaleta kila aina ya vyakula kuuza nje ya misikiti kuanzia mishikaki, sambusa, kababu na kila aina ya juisi.

Hapa Uingereza hakuna kitu.
Wala huwezi kuhisi kuwa ni Ramadhani.

Nikawa nakumbuka nyumbani Msikiti wa Mtoro kuna darsa ya tafsiri ya Qur’an niliyokuwa sikosi kuhudhuria akisomesha Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo, mwanafunzi wa bingwa wa tafsir, Muft Sheikh Hassan bin Ameir.

Msikitini petu Uingereza hakuna darsa labda kwa kuwa msikiti ulikuwa ukisaliwa zaidi na wanafunzi.

Msikiti ulikuwa ukiendeshwa na Wapakistani na kwa kujua kuwa msikiti ule ni wa wanafunzi walikuwa wanatoa futari ya biriani matunda na juisi kila siku.

Wanafunzi kutoka kila pembe ya ulimwengu tunafuturu hapo.

Nyumbani nilikotoka biriani si futari lakini niliipenda futari ya biriani mchele wa basmati kwa nyama ya kondoo.

Siku ya Eid imefika.
Ikanijia hamu ya kwenda kusali Msikiti wa Regent Park London.

Natokea Cardiff.
Sikujua kuwa London kuna misikiti wamefunga tofauti na Cardiff.

Nikakuta msikiti lango kuu limefungwa na kuna tangazo kuwa siku hiyo si siku ya Eid wao watasali Eid siku ya pili, kesho yake.

Niliingiwa na majonzi.
Nilishangazwa kuona kuwa hata huku kuna tatizo la mwezi.

Nikiwa nimezubaa pale msikitini akatokea kijana mmoja wa Kinigeria akaniuliza kama ningependa kwenda msikiti mwingine kusali.

Yule kijana akaniambai kuwa White Chapel Mosque East London wanasali Eid.
Tukaondoka kuelekea East London.

East London ni sehemu ambayo kuna jamii kubwa sana ya Wahindi na wengi ni Waislam.

Basi letu lilipoanza kukaribia mitaa ya East London na ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kufika nikaanza kuona watu wamevaa kanzu na mavazi nadhifu ya Eid wakiashiria kuwa walikuwa wanaharakia misikitini kusali Eid watoto wadogo na wakubwa mitaa yote imepambika kwa shamra shamra za sikukuu.

Ilinijia kama vile niko Dar es Salaam mitaa ya Jamhuri karibu na misikiti ya Kitumbini, Sunni na Ibadh.

Nikasali sala ya Eid hapo White Chapel Mosque na baada ya sala sikufanya haraka ya kuondoka kurejea Cardiff nikawa natembea kuangalia mandhari ya East London.

Nikapata hoteli wanauza chai na sambusa na kabab na baadae mchana nilirejea hoteli ile kupiga biriyani.

Jioni jua linazama nikapanda treni kurudi Cardiff.
Stori hii ya sala ya Eid bado haijesha.

Nilirudi tena London mwaka unaofuata 1993 kuja kusali Eid Kubwa Regent Park Mosque bila ya kupanga nikitokea Le Havre, Paris nikakatiza English Channel na kuja London.

Allah ni mwingi wa rehema.
Itaendelea…

Nimefunga Ramadhani Harare, Zimbabwe mwaka wa 1993.
Naikumbuka safari hii vyema sana.

Nimepanda ndege ya alfajir ATC kuelekea Harare.

Uwanja wa ndege nimemkuta marehemu Dr. Buyuni Jahazi na yeye anaelekea Harare safari yetu moja.

Safari hii mimi na Dr. Jahazi ina mengi lakini In Shaa Allah hayo tutahadithiana siku nyingine ikitokea fursa.

Tulipofika Harare tunaelekea hotelini niko kwenye taxi moja na Dr. Jahazi nikamuomba dereva wa taxi anionyeshe msikiti na kusudio langu ni kuwa niwe nasali hapo sala ya tarwehe.

Tunazungumza Kiingereza na mimi namtajia ‘’mosque.’’

Ilipitika kazi labda kwa dakika mbili tatu dereva wa taxi hajaelewa ‘’mosque,’’ ni kitu gani wala neno ‘’masjid,’’ halikutusaidia kuelewana.

Nilipomwambia, ‘’the place where Muslims pray,’’ hapo haraka akanijibu, ‘’You mean Muslim church.’’

Hakika kusafiri peke yake ni elimu tosha.
Akanipitisha katikati ya mji wa Harare akanionyesha msikiti.

Mambo bado hayajesha.
Nimepanga Ambassador Hotel hoteli nzuri lau ya zamani toka 1950s.

Baada ya siku mbili hivi Meneja wa hoteli akanitafuta na sababu ni kuwa alikuwa hanioni kwenye kifungua kinywa asubuhi.

Nikamfahamisha kuwa mimi nafunga mfugo wa Ramadhani.

Yule bwana akaniambia kuwa atawaagiza watu wa jiko kuwa jioni waliniletee futari chumbani kwangu, yaani ‘’room service,’’ yote, ‘’on the house,’’ ‘’zero cost’’ silipi kitu.

Chef akaelezwa kuwa anitengenezee chai, juice, mikate, nyama, salads na mapochopocho mengine kila siku jioni hadi nitakapoondoka hotelini baada ya majuma matatu.

Jioni ile wakati wa kufungua umefika nikapiga simu Room Service hata dakika tatu hazijapita nagongewa mlango msichana anaingia na tray imefunikwa vizuri kwa makawa yale ya ‘’silver,’’ makubwa maarufu kwa kufunika vyakula katika mahoteli makubwa.

Haraka yule bint akanifunulia.
Hakika ilikuwa futari iliyokidhi viwango.

Binti kasimama ananiangalia.
Mimi jicho langu liko kwenye sahani za vyakula.

Kuna nyama nimeiona pale sura yake sijaizoea.
Nikamwuliza hiyo ni nyama gani?

‘’Bacon Sir.’’
‘’You mean pork?’’

‘’Yes Sir it is pork.’’

Mpishi kanitengenezea futari ya nyama ya nguruwe.
Siku ya pili asubuhi nikahama hoteli ile nikaenda hoteli nyingine inaitwa Holiday Inn.

Wenyeji wakanionyesha restaurant nzuri sana ya Waismailia hapo ndipo nikawa nakwenda kufuturu.

Nimefunga Ramadhani Muscat Oman mwaka wa 1999.
Muscat ya mwaka wa 1999 si Muscat ya hivi sasa.

Nilipokwenda Muscat mwaka wa 2016 nimeikuta Muscat nyingine kabisa iliyochangamka.

Nilikuwa nimefika Dubai mwaka huo huo kama miezi mitatu iliyopita ndipo nikaenda Muscat.

Tofauti niliyoiona nikifananisha na Dubai ilikuwa kubwa mno ni kama vile Muscat mji hauna watu.

Kwa mtu aliyefika Dubai na kushuhudia vurugu iliyopo Dubai ya watu walivyokuwa wengi mitaani na barabara zilizojaa watu na magari ataelewa ninachokisema.

Ramadhani ya Muscat ilikuwa imetulia sana.
Itaendelea In Shaa Allah.

Ilikuwaje nikarudi London mwaka wa 1993 na kusali Eid al Adha msikiti wa Regent Park?

Nilikuwa Le Havre mji Kaskazini ya Ufaransa nikaja Paris kisha London nikikusudia kwenda Cardiff.

Ikasadif kuwa Eid Kubwa imenikuta London ndipo nikaamua kwenda kusali msikiti wa Regent Park, msikiti ambao mwaka uliopita 1992 sikuweza kusali.

Allah ni muweza.
Kanirudisha London Regent Park Mosque kuja kusali Eid al Adha.

Baada ya sala nimesimama nje ya msikiti barabarani.
Najiuliza niende wapi?

London siku ya Eid na kama siku nyingine yeyote ya kazi.
Ghafla nasikia sauti inaita, ''Sidney, Sidney, Sidney...''

Nimeshtuka sana.
Nani analijua jina langu hili hapa London?

Hata hapo Dar es Salaam si wengi wanalijua jina hili ila wale waliokuwa karibu sana na mimi toka udogoni.

Nageuza shingo namuona anaeniita ni Shufaa Zialor mke wa rafiki yangu Yusuf Zialor yuko upande wa pili wa barabara na wanae na mama mkwe wake mama yetu Bi. Asha.

Ndugu zangu hawa kutoka Dar es Salaam lakini kwa miaka mingi wamehamia London na kwao nikienda wakati niko Cardiff.

Furaha yangu ilikuwa kubwa sana.
Mwaka uliopita 1992 nilisali Eid Kubwa Tilbury.

Huu mji ni bandari ndogo kilomita chache nje ya London.
Eid ilinikuta nikiwa katika mji huu.

Asubuhi mimi na wanafunzi wenzangu wote kutoka Nigeria tukaamua kwenda kusali Eid lakini toka kufika mji ule hatukupata kuona msikiti popote.

Tukatoka kuelekea mjini.

Tilbury ulikuwa mji uliohamwa kwa kuwa hekaheka za sera za uchumi za Margaret Thatcher ziliuathir sana.

Wakazi wake wakitegemea bandari na bandari ilikuwa inachechemea.
Mji ulikuwa mfano wa ''Ghost Town.''

Katika maisha yangu yote sijapatapo kuona mji kama huu.

Maduka ya mji yamefungwa unachokiona ni kufuli katika madirisha makubwa ya vioo ya maduka na milango yenye kufuli na nje matangazo ya biashara yaliyopauka.

Barabara nzima ukitembea unajikuta uko peke yako kisha wewe ni mgeni.
Mji hauna msikiti.

Tukiwa tunahangaika kutafuta msikiti akapita mzee mmoja wa Kihindi ndani ya gari na naamini kilichomfanya asimame ni yale mavazi ya Kinigeria waliovaa wenzangu.

Akatuuliza kama tulikuwa tunatafuta msikiti wa kusali Eid.

Alituchukua hadi kwenye shule ya msingi ambako ndani ya darasa moja ndipo sala ya Eid ilikuwa inasaliwa.

Hapa nataka niongeze kitu ingawa hakihusiani na Ramadhani wala Eid.
Nilikuja kusali kwenye darasa mara nyingine tena Washington DC, Maryland.

Nilikwenda Washington DC kumtembelea rafiki yangu Dr. Harith Ghassany mwaka wa 2011.

Ijumaa imefika akanichukua kwenda kusali.
Tulisali Sala ya Ijumaa John Hopkins University ndani ya darasa.

Itaendelea In Shaa Allah sehemu ya mwisho.
Kuhitimisha nakurudisheni Maputo mwaka wa 1990.

Nilisali Eid ya Mfungo Tatu Maputo.
Msumbiji Eid siyo sikukuu inayotambuliwa na serikali.

Waislam wako wengi tu lakini hiyo ndiyo hali.
Msikiti uko mjini kabisa na unajaa hadi nje.

Katika hali kama hii vuta hisia mathalan sala ya Eid Msikiti wa Ngazija ambao uko katikati ya mji na watu wanasali hadi nje wametandika mabusati lakini kwa kuwa ni siku ya kazi magari na watu wanapita pembeni watu wakisali wakiendelea na shughuli zao.

Hali kama hii ina raha yake kuishuhudia.

Mwaka wa 2011 nilikuwa Ujerumani kwa mwezi mzima na Ramadhani ikanikuta Berlin.
Berlin Waislam walio wengi ni Waturuki.

Jirani na nyumbani kwangu kuna mgahawa na kuna duka la vyakula na biashara zote hizi ni za Waturuki.

Katika mgahawa huu ndipo nilipokuwa nachukua chakula changu ''takeaway,'' ninapotoka ofisini kwangu nakwenda kula nyumbani.

Waturuki wanapika si mchezo.

Kama kesho Ramadhani nikauliza ratiba ya tarwehe kwenye msikiti wa jirani na mipango ya futari hapo mgahawani.

Katika nchi nilizojaaliwa kufika hakuna nchi ngumu kama Ujerumani.
Wajerumani muda wote sura zao kama jiwe.

Hawana tabasamu wala hawataki kusema Kiingereza wala vibao hawaweki tafsiri.
Ni juu yako wewe mgeni kujifunza lugha yao.

Mawasiliano yangu na Waislam wenzangu Waturuki yalikuwa ya shida sana lakini walipojua mimi ni ndugu yao walikuwa wakiniadhimisha sana ninapofika pale mgahawani au kwenye lile duka la vyakula.

Nimekwenda mgahawani kununua futari.
Mashaallah menu imeenea kazi kwako kuchagua.

Baada ya kuchukua futari yangu hapo sasa nakwenda kwenye lile duka la vyakula nikatafute vinywaji.

Rafiki yangu Mturuki kafunga tasbih mkononi lakini hasemi Kiingereza hili nalijua toka nilipofika dukani kwake siku ya kwanza.

Nikampa ishara kuwa nataka vinywaji.

Nikaelekezwa kwenye jokufu nadhifu lililosheheni kila aina ya vinywaji linamependeza ukiangalia kwa nje.

Kufungua nikapambana na kila aina ya ulevi na kila aina ya juisi.
Nikajiambia kheri nusu shari kuliko shari kamili.

Harare nililitewa nyama ya nguruwe kama futari.
Hizi chupa za juice kuwa pamoja na na chupa za ulevi jambo jepesi sana.

Ukishangaa ya Mussa utaona ya Firauni.

Mwezi wa Ramadhani niko ndani ya ndege narudi Dar es Salaam ndege inaelekea Cairo ''transit,'' kisha Dar es Salaam.

Wahudumu wanataka kuwajua abiria waliokuwa katika saum kabla ya kutoa vinywaji na chakula.

Tumetua Cairo Maghrib wakati wa kufungua.
Uwanja umejaa Waislam wako transit wanaelekea Makka kufanya Umra.

Viwanja vyote vya ndege duniani siku hizi zina msala yaani sehemu maalum ya kusalia wapita njia.

Baada ya kufungua na kuingia restaurant kutafuta futari nakutana na FM Station za Cairo zinapiga muziki utadhani mwezi wa kula mchana.

Madhari ile hakika ilikuwa tofauti na ihram nyeupe zilizojaa mle ndani za waumini waliokuwa wanakwenda Makka kufanya Umra.

PICHA:
Nje ya Msikiti Dar ul Isra, Cardiff (1993)
Nje ya Regent Park Mosque, London (1991)
Nje ya Msikiti wa Beldaware, Harare (1993)
Nje ya Grande Mosque, Paris (1993)
Tilbury Port (1992) kulia Omar Shariff (Egypt), kushoto Abdul Indabawa (Nigeria)
Maryland, Washington DC kulia ni Dr. Harith Ghassany (2011)
View attachment 2195616

Screenshot_20220422-070556_Facebook.jpg
 
Shukran sana sheikh, Dr.jahazi ni yule aliyekuwa muhimbili? akiishi kota za madaktari nyuma ya shule ya azania ?
 
Sheikh Mo Said
Dunia imeizunguka, na maisha umeyaona na hakuna majuto katika maisha yako.....
Sisi wengine tutaingalia tu kwenye mitandao...
 
Msumbiji Eid siyo sikukuu inayotambuliwa na serikali.
Kwani kuna tofauti na Tanzania?
Serikali inatambua jambo gani la Waislamu?

Eid inawezekana ikawa siku 9 hadi 10 zijazo utanisahihisha watoto wamefunga wiki moja na wamefungua Jumatano je watafunga tena wiki moja? 😝

Amini nakwambia Uislamu unatekelezwa Afrika Magharibi tu achana na wale wenye vinasaba na mtume wenu huku kwingine mnaigiza
 
Sheikh Mo Said
Dunia imeizunguka, na maisha umeyaona na hakuna majuto katika maisha yako.....
Sisi wengine tutaingalia tu kwenye mitandao...
Tek...
Usiseme hivyo ni vibaya.
Allah ni muweza wa kila kitu.

Nilikuwa na umri kiasi miaka 21 hivi nimemaliza kusali Maghrib msikiti wa Mtambani ule wa zamani.

Siku chache zilizopita nilimsikia Sheikh About Maalim Allah amrehemu Msikiti wa Manyema akituwaidhi akasema muombe Allah chochote utakacho.

Basi mimi siku ile pale Mtambani nilinyanyua mikono yangu nikaomba dua nikamwambia Allah nionyeshe dunia.

Yapo mengi mengine siwezi kueleza hapa.
Allah anaombwa na anatoa.
 
Gwiji la Uandishi
Mo Said

Umri umewatupa mkono, sasa ni jukumu letu sisi vijana katika ahli zetu kupita njia zenu ili kuandika vyenye kua'ngatika.
Da Vinci...
Hakika uzee umetufikia na ni jambo la kushukuru.

Muhimu sana ni nyinyi vijana kwanza tukuombeeni dua Allah awape umri tawil.

Pili sisi In Shaa Allah tukuachiani mema mtamani kutuiga.
 
Ama dunia mmeifaidi nyinyi wazee wetu mliokuta dunia na miji Kama Dar es salaam ikiwa bado inawaungwana amani ya kutosha...ananambiaga mzee wangu palipita watu mji huu mwanangu ungekuwepo ndio ungejua raha ya dunia stori za kina Alkhii shekh mzee comorian,mzee Abdallah Iddi chaurembo marehemu shekh Kassim bin jumaa bin Hamisi wachewa wallah natamani ningekuwepo enzi ya mzizima.
 
Ama dunia mmeifaidi nyinyi wazee wetu mliokuta dunia na miji Kama Dar es salaam ikiwa bado inawaungwana amani ya kutosha...ananambiaga mzee wangu palipita watu mji huu mwanangu ungekuwepo ndio ungejua raha ya dunia stori za kina Alkhii shekh mzee comorian,mzee Abdallah Iddi chaurembo marehemu shekh Kassim bin jumaa bin Hamisi wachewa wallah natamani ningekuwepo enzi ya mzizima.
Othi...
Nimeandika kitabu.

Hao uliowataja wamo ndani ya hicho kitabu.
View attachment 2196484
 
heshima yako Mohamed Said, hapo kwenye picha yako ya kwanza juu nimeona maandishi " DAR - US- ISLAM".. haya maneno yana maanisha nini?.. ndio asili ya neno Dar Es Salaam?
 
Sh Muhamed,

Kwanza, nikupe hongera kwa kipaji ulichonacho Mwenyeezi Mungu akuzidishie
Pili, nakupa hongera kwa kutokuwa mchoyo na kutokuchoka katika kuielimisha jamii

Ninawafahamu waandishi wachache wenye uwezo wa kuandika na msomaji akahisi kama na yeye yumo kwenye khadithi inayokhadithiwa na Sh Muhamed ni mmoja wao

Kuna magwiji wengi wa uwandishi waliopo Tanzania lakini jamii inafaidika na wachache

Yupo muandishi mmoja yupo Zanzibar, apatapo nafasi huandika khadithi fupifupi za maisha ya kila siku na nina imani munafahamiana kwani uandishi wenu unafanana sana

Sh Muhamed nakuomba usichoke kuandika na sisi wasomaji tunafaidika mengi

Hatuna la kukulipa ila Ahsante
 
Sh Muhamed,

Kwanza, nikupe hongera kwa kipaji ulichonacho Mwenyeezi Mungu akuzidishie
Pili, nakupa hongera kwa kutokuwa mchoyo na kutokuchoka katika kuielimisha jamii

Ninawafahamu waandishi wachache wenye uwezo wa kuandika na msomaji akahisi kama na yeye yumo kwenye khadithi inayokhadithiwa na Sh Muhamed ni mmoja wao

Kuna magwiji wengi wa uwandishi waliopo Tanzania lakini jamii inafaidika na wachache

Yupo muandishi mmoja yupo Zanzibar, apatapo nafasi huandika khadithi fupifupi za maisha ya kila siku na nina imani munafahamiana kwani uandishi wenu unafanana sana

Sh Muhamed nakuomba usichoke kuandika na sisi wasomaji tunafaidika mengi

Hatuna la kukulipa ila Ahsante
Wandugu,
Ahsante sana ndugu yangu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom