Melabon muuza embe za pilipili Kariakoo 1960s

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,820
31,847
MELABON MUUZA EMBE NA VITU VINGINE KIKAPUNI KWA WATOTO DAR ES SALAAM YA 1960

Alikuwa akiitwa Melabon na hadi leo sasa mimi ni mtu mzima sijaweza kulifahamu jina lake khasa.

Melabon ilikuwa dawa ya kichwa mfano wa Aspro na ikitangazwa radioni.

Vipi alikuwa na jina hili sijaweza kujua.

Nimekutana na picha hiyo hapo chini kwenye ''Magomeni Yetu Leo,'' picha ya embe mbichi zimekatwa na kunakshiwa na chumvi na pilipili kama alivyokuwa akituuzia Melabon katika mitaa ya Dar es Salaam ile ya 1960s.

Embe hizi zimenitia hamu.
Leo wapi mtu utazipata?

Bidhaa zake Melabon ameziweka kwenye kikapu nadhifu anapita mitaani kufanya biashara yake.

Akitua kikapu chake tu haupiti muda tushamzunguka. Mkono wake mwepesi kumenya na kunyunyuzia pilipili.

Utapenda kumtazama anvyomenya na kukata embe na embe inapokatwa ilikuwa ikitoa mlio fulani wa kupendeza masikio.

Lakini sehemu yake maarufu ni kwenye shule akivizia kipindi cha ''break,'' yaani mapumziko.

Soko lake kubwa lilikuwa Shule ya Mnazi Mmoja.

Kama vile namuona alikuwa mtu mwenye haiba ya upole na watoto wote tukimpenda.

Miaka hiyo Mtaa wa Lumumba barabara moja na pande zote mbili zina nyumba za makuti na nyuma ya nyumba hizi ndiyo uwanja wa Mnazi Mmoja.

Hizi ndizo zilikuwa sehemu za Melabon akifanya biashara yake.

Wakati mwingine hapo Mnazi Mmoja kunakuwa na mechi za mpira ambako watoto hatukosekani kuangalia club maarufu za mtaani zikicheza mfano Kahe Republic v na Liverpool.

Uwanja unafurika.

Hapo Melabon anaondoka kikapu chake chepesi sana na mfuko wake mzito.

Siku za utoto wetu.

Screenshot_20220731-120500_Facebook.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom