Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,735
- 13,498
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita akiwa katika Jimbo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, kwenye ziara ya chama chake, ametoa kauli akimjibu Rais Samia, kufuatia hotuba aliyoitoa Rais Samia wakati wa maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi.
Kiongozi huyu wa ACT Wazalendo ameeleza kwamba kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), marehemu Mzee Ali Kibao, ni kifo na tukio la aina yake na lenye sura ya upekee; na hivyo kutokana na mazingira hayo haishangazi kuibua hisia kubwa katika jamii.
Hivyo, Mchinjita amesisitiza kwamba Rais Samia anapaswa kuliangalia na kulizingatia jambo hilo kwa aina na namna yake.
"Tukio hili [la Mzee Kibao] ni la aina yake. Watu wengine wote walienda kuchukua na kuteka Watu kwa siri. Hawa [waliomteka na kumuua Mzee Kibao] ni wauaji waliopata ujasiri wa kusimamisha basi la abiria. Ndani ya hilo basi kukiwa na askari wa usalama barabarani. [Watu hao] wakamchukua Mtanzania huyu anayejulikana na kesho [Mtanzania huyu] akakutwa ameuwawa. Hii inaonesha kilele cha ujasiri kwa wale wanaoua na kupoteza watu kwenye nchi yetu. [Mauaji haya] hayawezi kuwa sawasawa na matukio mengine ya kawaida."
Mchinjita aliendelea kusisitiza kwamba kelele zilizopo na zilizoibuka zinatokana na matukio ya utekaji kudumu na kuendelea kwa miaka nane sasa. Kiongozi huyo alieleza kuwa matukio haya yameanza mwaka 2016, huku akikumbushia kwamba kutokana na matukio haya kuwa mengi, Zitto Kabwe, Kiongozi Mstaafu wa ACT Wazalendo aliwasilisha hoja binafsi, katika bunge la awamu ya tano, akiliomba bunge kuunda tume ya uchunguzi, ili kuchunguza hali ya watu kupotea.
Pia soma ~ Rais Samia: Mauaji ya Kibao hayakubaliki. Uchunguzi umeanzishwa