Doctor Mama Amon
JF-Expert Member
- Mar 30, 2018
- 2,076
- 2,686
Freema Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Mbowe hajabainisha hoja ya kumwonesha Rais Samia kwamba kuna uharaka wa Katiba Mpya
Kazi mojawapo ya Kurasa za Mama Amon ni kutathmini siasa za kitaifa kwa kukusanya ushahidi kutoka vyanzo vya kuaminika, kuhakiki hoja za mfumo tawala na hoja za mfumo wa sekta ya kiraia, vikiwemo vyama vya ushindani wa kisiasa, na kisha kutoa mapendekezo kwa umma wa wasomaji.
Hivyo, nilikuwa njiani kufanya tathmini madai ya "Katiba Mbadala" kupitia programu ya "Operesheni Haki" ya Chadema mara tu baada ya mzunguko wao kukamilika.
Lakini, Juzi 01 JUlai 2021, Mdude Chadema alitoa kauli iliyonifanya niharakishe kusema jambo.
Awali ya yote, nataka niseme kuwa naungana na Mdude Chadema katika kupinga utekwaji, uteswaji na unyanyaswaji wa kisheria uliofanywa dhidi yake.
Naungana naye kwa kuwa, baadhi ya mambo aliyofanyiwa yanaanzia kwenye kanuni ya umachiaveli isemayo kuwa "lengo lolote linaweza kuhalalisha mbinu yoyote, bila kujali uharamu wa mbinu wala lengo husika."
Watu wote wenye kiu ya haki tumepinga, tunapinga na tutaendelea kupinga kanuni hii.
CHADEMA WANAPINGA UMAGUFULI KWA KUFANYA UMAGUFULI
Lakini sasa, Mdude ametuacha njia panda. Ametangaza wazi wazi kuunga mkono kanuni hii ya kimachiaveli kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo, ili aweze "kuacha alama" duniani baada ya kufa.
Mdude akiwa katika ukumbi wa Baracuda, Tabata, jijini Dar es Salaam, amerekodiwa akisema kwamba: "Kuna wakati ni lazima kutumia njia isiyo sahihi kuipata njia iliyo sahihi."
Huu ni Umagufuli. Na maneno haya aliyatamka mbele ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, na hakuna masahihisho yoyote yaliyofanywa na Mbowe.
Hivyo basi, kwa mujibu wa mawazo ya Mdude ambayo hayakupingwa na Mbowe:
- ni sahihi kupigana vita kama njia ya kupata utiifu kwa mtu anayekupinga kwa hoja,
- ni sahihi kufanya fujo kama njia ya kuleta utulivu,
- ni sahihi kusema uwongo kama njia ya kulinda ukweli,
- ni sahihi kuua mtu ili kupata utajiri,
- ni sahihi kubaka mtu ili kupata taarifa za siri alizo nazo na hataki kuzitoa,
- ni sahihi kumteka, kumtesa, kumtungia kesi bandia, na kumfunga mkosoaji wako ili kumziba mdomo asifichue tena madhaifu yako,
- na mifano mingine kama hii yenye kuongozwa na kanuni ya umachiaveli.
Ukishaanza kuitumia huwezi kujua ni lini utaachana nayo, na kwa kweli huwezi kupata sababu kuachana nayo. Huu ndio muzimu uliomtafuna hayati Magufuli.
Na sasa Mdude aameteleza kuelekea kwenye bonde la Umagufuli. Nadhani Mdude na wafuasi wake wanahitaji political mentorship ili waweze kutimiza ndoto yake ya "kuacha alama" chanya katika Taifa.
Mdude Nyagali Chadema (katikati) akiwa na vijana wenzake
Hivyo, napenda nitumie nafasi hii kuishauri Chadema kuhusu dhamira yao kusiana na suala la kampeni ya "Katiba Mbadala".
CHADEMA WANAKIUKA KANUNI YA PEMBETATU YA USIMAMIZI WA MIRADI
Kanuni muhimu ya usimamizi wa miradi inaitwa kanuni ya pembetatu ya usimamizi wa mradi (project management triangle).
Kanuni hii inahusisha ufuatiliaji wa vitu vinne ambavyo ni ubora, muda, bajeti na ukubwa wa vipaumbele vya mradi (quality, time, budget, scope).
Kanuni ya pembetatu ya usimamizi wa mradi
Kwa mujibu wa kanuni ya pembetatu ya usimamizi wa mradi , misingi mine inahusika.
- Mosi, ubora wa mradi ni kitu kimoja kisichobadilika (constant);
- Pili, muda, bajeti na ukubwa wa vipaumbele vya mradi ni vitu vitatu vinavyobadilika (variables) kulingana na matakwa ya meneja wa mradi.
- Tatu, ubora wa mradi unategemea kupatikana kwa fedha ya bajeti iliyopangwa, kupatikana kwa muda wa kutekeleza mradi na ukubwa wa vipaumbele unaoendana na bajeti na muda.
- Na nne, kwa lengo la kulinda ubora wa mradi, mabadiliko katika kibadilika kimojawapo yanapaswa kuambatana na mabadiliko katika vibadilika vingine viwili bila.
Kwa mfano, utekelezaji wa mradi utakamilika mapema ama kwa kuongeza bajeti au kupunguza ukubwa wa vipaumbele vya mradi.
Vivyo hivyo, kuongeza ukubwa wa vipaumbele vya mradi kunahitaji ongezeko la bajeti na muda. Na kupunguza najeti bila kuongeza muda wa kutekeleza mradi kunapunguza ubora wa mradi.
Kwa hiyo, kama “Katiba Mbadala” sio kipaumbele katika Mradi wa kuendesha nchi unaotekelezwa na serikali, kama serikali itakibeba kipaumbele hiki, maana yake ni kwamba ibadilishe bajeti yake na ratiba ya utendaji wa kazi zake. Uamuzi wa aina hii utategemea uharaka wa kipaumbele hiki.
Rais Samia anasema kuwa kwa sehemu kubwa, “Katiba ya Tuliyonayo” inamruhusu kutekeleza mradi wake wa kuendesha nchi kwa ufanisi.
Kwa hiyo, Rais Samia haoni uharaka wa kubadilisha vipaumbele vyake kwa kuongeza kipaumbele cha kutengeneza “Katiba Mbadala.” Lakini Chadema wanataka kumlazimisha.
CHADEMA WANAKIUKA KANUNI UMUHIMU NA UHARAKA
Wanachojaribu kufanya Chadema ni kuvunja kanuni ya umuhimu na uharaka katika kufanya menejimenti ya muda. Yaani, "importance and urgency principle".
Mara nyingi, kazi zenye umuhimu na uharaka mkubwa ni zile zinazohitajika ili kumwezesha memeja wa mradi kufanikisha malengo aliyonayo kwa mujibu wa mipango wa mradi wenye kuonyesha kazi gani ifanyike lini, nani aifanye, na kwa vipi.
Na mara nyingi, kazi zenye umuhimu na uharaka mdogo ni zile ambazo ziko nje ya mipango wa mradi wenye kuonyesha kazi gani ifanyike lini, nani aifanye, na kwa vipi. Zinaletwa na mtu baki kwa utaratibu wa dharula.
Jedwali la kanuni ya umuhimu na uharaka lifuatalo linaonyesha mahusiano kati ya mambo haya manne:
- umuhimu mkubwa,
- umuhimu mdogo,
- uharaka mkubwa, na
- uharaka mdogo.
Jedwali la kanuni ya umuhimu na/au uharaka
Kutokana na jedwali hili, ni wazi kuwa, kazi zote zinazofanyika hapa duniani zinaweza kugawanywa katika kundi mojawapo kati ya makundi manne yafuatayo bila kubaki, yaani:
- Kazi yenye umuhimu na uharaka, au
- Kazi yenye umuhimu lakini haina uharaka, au
- Kazi isiyo na umuhimu lakini ina uharaka, au
- Kazi isiyo na umuhimu wala uharaka.
Kwa hiyo, kwa upande mmoja, Rais Samia na Chadema wanakubaliana kuhusu kauli kwamba: "kazi ya kuunda Katiba Mbadala ni yenye umuhimu."
Na kwa upande mwingine, Rais Samia na Chadema wanatofautiana kuhusu kauli kwamba: "kazi ya kuunda Katiba Mbadala ina uharaka kuliko vipaumbele vingine vya Taifa"
Hivyo, hapa kuna majukumu mawili mbele ya viongozi wa Chadema na wanachama wao wanaotaka Katiba Mbadala iundwe haraka, kinyume na alivyopendekeza Rais Samia:
- Mosi, wanapaswa kuonyesha kwa nini kauli ifuatayo, kama inavyotolewa na Mwenyekiti wa Freeman Chadema (Mbowe), ni ya kweli:
- "Kwamba kazi ya kuunda Katiba Mbadala ina uharaka mkubwa kuliko vipaumbele vingine vya Taifa."
- Na pili, wanapaswa kuonyesha kwa nini kauli ifuatayo, kama ilivyotolewa na Rais Samia, sio ya kweli,
- Kwamba, vipaumbele baki vya Taifa vina uharaka mkubwa kuliko kazi ya kuunda Katiba Mbadala."
Na hata ndani ya Chadema, sioni kama wanaweza kujenga hoja ya kutetea madai kwamba "Katiba Mbadala" ndio kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza cha Chama.
Nitaeleza jambo hili kwa njia ya SWOT Analysis pamoja na TOWS Analysis inayoihusu Chadema na mazingira yake ya ndani na nje, kulingana na taarifa nilizo nazo mezani kwangu.
UCHAMBUZI WA UIMARA, UDHAIFU, FURSA NA CHANGAMOTO
Nimefuatilia program ya Chadema inayoitwa “Operesheni Haki” tangu mwanzo hadi sasa. Kwa uchache, nimegundua uimara, udhaifu, fursa na changamoto za Chadema. Nitaeleza kwa ufupi matokeo ya hii “SWOT Analysis” niliyoifanya:
Uimara wa ndani ya Chadema
- Uimara A. Kuna wanachama na wafuasi wa Chadema ambao bado ni waaminifu kwa sera na itikadi ya chama.
- Uimara B. Kwa ulinganisho, kinao wanachama na wafuasi wengi kuliko chama kingine cha ushindani.
- Uimara C. Chama kinaungwa mkono na wanaharakati wengi, watu wa azaki wengi, wanazuoni wengi, na wale wanaoona kuwa hawana matumaini ndani ya chama tawala.
- Uimara D. Chama kina cheti cha usajili, Katiba halali, kanuni, na miongozo, na hivyo haki ya kupigania mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
- Uimara E. Chama kinayo ilani nzuri ya uchaguzi mkuu wa 2020 inayoweza kutumika kama msingi wa mipango kivuli ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
- Uimara F. Chama kinaungwa mkono na mitandao ya kijamii, vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.
- Udhaifu G. Katika ngazi ya Kata, Wilaya, na Mkoa mabaraza ya vijana, wanawake, wazee na hamasa yamedhoofika sana. Baadhi hayajawahi kufanya AGM kwa miaka sita iliyopita.
- Udhaifu H. Chama hakijui kina wanachama wangapi hai kwa ujumla; na hakijui kina wanachama wangapi ambao ni Bavicha, Bawacha, au Bazecha.
- Udhaifu I. Chama hakina vitendea kazi kama vile Katiba, Kanuni, Ofisi za chama na pikipiki.
- Udhaifu J. Mpaka sasa chama kimeshindwa kubadilisha sera zilizomo katika ilani yake ya uchaguzi mkuu wa 2020 kuwa mikakati ya “Mpango Kivuli wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021-2026.” Yaani, “Shadow National Development Plan.”
- Udhaifu K. Chama hakina vyanzo vya mapato vya uhakiki, kwa kiwango kinachokiwezesha kutekeleza siasa zake kwa kasi na ushindani.
- Udhaifu L. Chama kinaonekana kushabikia siasa za mipasho zaidi kuliko siasa za hoja.
- Udhaifu M. Chama kimekuwa na historia ya kuvunja Katiba na kanuni zake waziwazi, bila kuchukua hatua za kukarabati hali hiyo.
- Udhaifu N. Chama kimeanza kupoteza taswira yake ya kutambuliwa kama mtetezi wa uhuru wa kweli, haki ya kweli na maendeleo ya kweli.
- Udhaifu O. Kwa kuwa Chadema sio chama tawala, hakina jeshi linaloweza kuisaidia kulinda maslahi yake.
- Fursa P. Chama kina wadau wengi ndani na nje ya nchi ambao wako tayari kuchangia utekelezaji wa mipango yake ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
- Fursa Q. Mipango ya maendeleo ya serikali kwa kipindi cha 2021-2025, kwa kila sekta, inayo mapengo yanayoweza kuzibwa kwa njia ya kuandaa mpango kivuli wa maendeleo wa kila sekta kwa kipindi cha 2021-2025.
- Fursa R. Wazo la kuandaliwa kwa Katiba Mbadala inayoweza kusawazisha uwanja wa siasa za vyama vingi bado lipo hai vichwani mwa wananchi tangu 2014.
- Fursa S. Tanzania inaye Rais ambaye hapingi ujio wa “Katiba Mbadala” na anayeunga mkono utawala wa sheria zinazoratibu uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kukosoana kwa hoja.
- Changamoto T. Katiba ya nchi iliyopo inaruhusu Rais wa nchi kuwa mwenyekti wa Chama tawala, na hivyo kutoa mwanya wa nchi kuwa na “Mgombea Urais wa kipindi kipya ambaye bado ni Rais wa kipindi kinachokwisha,” akiwa na mamlaka kamili juu ya vyombo vyote vya dola, vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama.
- Changamoto U. Katiba ya nchi iliyopo inaruhusu Rais wa nchi kuwa na madaraka makubwa kuliko Bunge na Mahakama, kiasi cha kuweza kuburuza mihimili hii kama akitaka.
- Changamoto V. Viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi huteuliwa na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama tawala.
- Changamoto W. Watumishi wa umma katika Mikoa na Halmashauri hugeuka watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mkuu .
- Changamoto X. Chama cha Mapinduzi kinayo ruzuku kubwa inayokiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa kasi kubwa na kwa ufanisi.
- Changamoto Y. Chama cha Mapinduzi kinao wataalam wengi wanaokisaidia kuweka sawa mipango yake, na hivyo kuwa chama imara katika suala la sera, utafiri na mipango ya maendeleo.
- Changamoto Z. Kwa kuwa CCM ni chama tawala, ina jeshi linaloweza kuisadia kulinda maslahi yake kwa kutumia mbinu za kimabavu.
- Changamoto Z. Wafuasi na wanachama wa Chadema kubaguliwa katika ajira za utumishi wa umma kwa sababu ya misimamo yao ya kiitikadi.
Kutokana na“SWOT Analysis” niliyoifanya hapo juu, nimefanya “TOWS Analysis” na kubaini makundi sita ya mikakati yafuatayo yanayoweza kufanyiwa kazi na Chadema, ili kujenga mazingira ya siasa chanya za upinzani hapa Tanzania:
- Mikakati inayotokana na uimara na udhaifu (SW strategies)
- Mikakati inayotokana na fursa na vitisho (OT strategies)
- Mikakati inayotokana na uimara na fursa (SO strategies)
- Mikakati inayotokana na udhaifu na fursa (WO strategies)
- Mikakati inayotokana na uimara na vitisho (ST strategies)
- Mikakati inayotokana na udhaifu na vitisho (WT strategies)
- Mikakati wa kwanza (SW strategy): Kutokana na Uimara A, Uimara B, Uimara C, na Udhaifu I Mkakati ufuatao unaopendekezwa: Kuhamasisha Kata, wilaya na mikoa kukusanya ada, michango na ruzuku kwa ajili ya kupata vitendea kazi kama vile Katiba, Kanuni, Ofisi na pikipiki.
- Mikakati wa pili (OT strategy) : Kutokana na Fursa S na Changamoto Z mkakati ufuatao unaopendekezwa: Kumwomba Rais asimamie utendaji wa serikali ili kuondoa kasumba ya kibaguzi iliyojengeka ndani ya nchi kwa miaka mitano iliyopita.
- Mkakati wa tatu (SO strategy one): Kutokana na Uimara E, Uimara C, na Fursa N mkakati ufuatao unaopendekezwa: Kuandaa na kutekeleza “Mpango Kivuli wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021-2026” kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo
- Mkakati wa nne (SO strategy two): Kutokana na Uimara D, Uimara C, na Fursa Q mkakati ufuatao unaopendekezwa: Kushirikiana na wadau kupigania ujio wa “Katiba Mbadala” kabla ya 2025.
- Mikakati wa tano (WO strategy): Kutokana na Udhaifu J na Fursa N mkakati ufuatao unapendekezwa: Kujenga uwezo wa kifedha wa chama kwa kuandaa andiko la kutafuta rasilimali fedha ndani na nje ya nchi.
- Mikakati wa sita (ST strategy): Kutokana na Uimara E, Changamoto R na Changamoto U mkakati ufuatao unaopendekezwa: Kutumia mitandao na vyombo vya habari kueleza ubaya wa Katiba ya sasa, likiwemo tatizo la urais wa kifalme, kuruhusu uwanja wa uchaguzi usio tambarare.
- Mikakati wa saba (WT strategy): Kutokana na Udhaifu O na Changamoto Z mkakati ufuatao unaopendekezwa: Kujenga mahusiano mema na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na kuunda vikosi vya kulinda mashai ya chama.
Kwa maoni yangu, huu ni mkakati ambao utekelezaji wake hauwezi kuwa na uharaka kuliko mikakati baki. Naona kuwa mkakati muhimu zaidi ni Mkakati namba tatu.
Chini ya Mkakati namba tatu Chadema wanatarajiwa kuibuka na angalau mradi mmoja kwa kila sera waliyoinadi jukwaani wakati wa kampoeni za 2000, watembeze bakuli ndani na nje ya nchi, na kutekeleza miradi hiyo. Kwa mfano:
- Sera ya elimu ya awali: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga shule ya awali moja kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Early Education Program";
- Sera ya elimu ya msingi: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga shule ya msingi moja kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Primary Education Program";
- Sera ya elimu ya sekondari: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga shule ya sekondari moja kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Secondary Education Program";
- Sera ya elimu ya ufundi: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Chuo cha ufundi kimoja kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Vocational Training Program";
- Sera ya elimu ya juu: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Chuo Kikuu kimoja kila Kanda na programu hii ikaitwa "M4C HIgher Education Program";
- Sera ya afya: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Chuo kimoja cha manesi kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Health Program";
- Sera ya habari: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Maktaba moja ya kisasa kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Infomatics Program";
- Sera ya kilimo: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Kituo Atamizi cha Kilimo-biashara kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Agribusiness Program";
- Sera ya masoko: Chadema yaweza kuweka mkakati wa kujenga Soko moja la kisasa kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Markets Program";
- Sera ya utalii na ukarimu: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Hoteli Moja kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Hotels Program";
- Sera ya Viwanda: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Kiwanda kimoja kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Industries Program";
- Sera ya Maji: Chadema waweza kuweka mkakati wa Kuchimba kisima kimoja kila kijiji na programu hii ikaitwa "M4C Water Program";
- Sera ya Nyumba na Makazi: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga Flat moja kubwa kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Habitat Program";
- Sera ya Fedha: Chadema waweza kuweka mkakati wa kuanzisha benki ya jamii na kuweka tawi lake kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Banking Program";
- Sera ya Biashara: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga fremu za biashara katika ploti moja kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Business Parks Program";
- Sera ya Ustawi wa Jamii: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga ukumbi wa matukio ya kijamii kama harusi na sherehe kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Cummunity Parks Program";
- Sera ya Ajira: Chadema waweza kuweka mkakati wa kuhuisha mnyororo wa ongezeko la thamani kwa zao moja la kilimo kila mkoa kama mkakati wa kuzalisha ajira kwa vijana na wanawake na programu hii ikaitwa "M4C Employment Program";
- Sera ya Usafiri: Chadema waweza kuweka mkakati wa kununua na kuendesha mabasi ya usafiri ndani na nje ya kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C Trans Program";
- Sera ya TEHAMA: Chadema waweza kuweka mkakati wa kujenga na kuendesha kuendesha Kituo cha TEHAMA ndani ya kila mkoa na programu hii ikaitwa "M4C ICT Program";
Na kama Chadema wakitekeleza programu hizi, watakuwa wameshiriki katika kazi ya kusukuma mbele gurumumu la haki, na hivyo kuifanya furaha kushinda huzuni kabla ya Chadema kushika dola.
Wakitaka kufanya mikutano ya hadhara kunadi miradi yao ya maendeleo hakuna mtu atakayewatilia shaka.
Kila mtu atakuwa anasema kimoyo moyo, "Chadema wanaweza." Wataonekana, wataaminika, na watajiamini.
HITIMISHO
Hivyo, matarajio yangu ni kwamba, kama Chadema watatekeleza mikakati hii saba, kati ya mingine mingi, watakuwa wamefanya siasa zenye ukomavu wa kiwango cha juu.
Hatimaye siasa za ushindani wa vyama vingi zitakuwa zimepata sura chanya. Hatimaye chama kitasonga mbele kwa kushirikiana na serikali bega kwa bega kama mdau wa kweli wa maendeleo aliye nje ya mfumo tawala.
Lakini, katika kufanya kazi hii, wakumbuka mwongozo huu: Katika kufanya kazi ya kutafuta uungwaji mono, kuna njia tatu zinaweza kutumika:
- Mosi, ni kulitamka jambo kwa sauti kubwa, na kwa kufoka foka, ili hofu inayotokea, ipofushe akili ya hadhira, na hivyo watu wakubali kinachosemwa kwa sababu ya hofu hiyo. Hii ni njia ya kubahatisha.
- Pili, ni kurudia rudia tamko mara nyingi, kusudi marudio yanayofanyika yaifanye hadhira isahau kuangalia upande wa pili wa mjadala, na hivyo kukubali kile kinachosemwa mara nyingi kupitia midomo ya watu wengi, kama ukweli kwa sababu hizo mbili. Hii ni njia ya kubahatisha pia.
- Na tatu, ni kutafuta ushahidi usiokanushika, na kuupangilia kimantiki, kwa upole na kwa umakini, kusudi sindano ya hoja umwingie msikilizaji taratibu, hadi aseme kwa hiari yake mwenye kwamba "hapo sawa, ni kweli aisee." Hii ni njia ya uhakika zaidi.