Mashimo ya Mfalme Suleiman

Je, nyinyi Bwana Good na Quatermain, mwasemaje?’
Bwana Good akasema, ‘Waweza kumwambia ya kuwa mimi nipo tayari kabisa kumsaidia, lakini neno moja nalitaka, nalo ni kuruhusiwa kuvaa suruali zangu.’


Basi nikatafsiri maneno hayo yote, na Ignosi ambaye ndiye Umbopa akasema, ‘Vema rafiki zangu, nawe Makumazahn wewe utakuwa pamoja nami? Maana wewe ni mwindaji wa zamani mwenye uerevu kupita ule wa nyati aliyejeruhiwa.’


Nilifikiri kwanza nikajikuna kichwa, kisha nikasema, ‘Umbopa au Ignosi, mimi sipendi vita, ni mtu wa amani na tena ni mwoga kidogo (na hapo Umbopa akacheka) lakini napenda kuambatana na rafiki zangu.


Wewe ulitusaidia sisi, nami nitakusaidia wewe. Lakini mimi ni mfanyabiashara na kwa hiyo, ikiwa tutapata almasi, basi nakubali ahadi yako. Na tena, kama ujuavyo, sisi tulikuja kumtafuta ndugu yake Bwana Henry aliyepotea; lazima utusaidie kumtafuta.’

Basi Ignosi akajibu, ‘Nemekubali, lakini wewe, Infadus, apa kwa alama hii ya nyoka iliyochanjwa kiunoni mwangu kisha uniambie kweli. Mtu mweupe yeyeto ameingia katika nchi hii?

Akajibu, ‘Hapana, Ignosi.’
Ignosi akasema, ‘Mtu mweupe angalionekana au habari za mtu mweupe zingalivuma, wewe ungalipata habari?’ Akajibu, ‘Hakika ningalipata habari.’


Akamwambia Bwana Henry, ‘Umesikia, Inkubu, hakufika katika nchi hii.’ Bwana Henry akasikitika akasema, ‘Basi, basi, ni hivyo. Naona hakufika hata hapa, masikini, masikini! Tumefanya safari ya bure. Lakini ndiyo Mungu alivyo panga.’


Basi nikaona afadhali kumtoa katika fikira za huzuni, nakasema, ‘Haya, sasa tufanye kazi.

Ni vizuri kuwa mfalme wa haki, Ignosi, lakini utafanya nini upate kuwa mfalme kweli?’ Akajibu, ‘Hayo mimi sijui; je, Infadus unalo shauri linalofaa?’

Mjomba wake akajibu, ‘Ignosi, Mwana wa Umeme, usiku wa leo itakuwapo ngoma kuu ya kutambulisha wachawi. Wengi watatambuliwa na kuuawa, na wengi zaidi watajaa huzuni na masikitiko na hasira juu ya mfalme Twala.


Ngoma itakapokwisha nitasema na wakubwa, na ikiwa nitaweza, wao watasema na watu walio faraghani, nami nitawaleta kwako wapate kushuhudia kuwa kweli wewe ni mfalme. Nadhani kabla ya jua kuchomoza kesho utakuwa na mikuki ishirini elfu tayari kutii amri zako.

Na sasa lazima niende nikafikiri na kusikiliza na kuweka yote tayari. Baada ya ngoma kwisha ikiwa nita kuwa hai, tukutane hapa hapa, tutaweza kuongea zaidi. Lakini haikosi kutakuwa na vita.’


Basi hapa mazungumzo yetu yalivunjika kwa kuwa matarishi wa mfalme walikuja. Tukakaribia mlangoni na tukawapa ruhusa kuingia, kisha watu watatu waliingia na kila mtu alikuwa kachukua nguo za minyororo ya chuma iliyong’aa na iliyofumwa, na shoka zuri la vita.

Wakasema, ‘Hizi ni zawadi kutoka kwa mfalme, za watu weupe waliotoka katika nyota.’ Nikajibu, ‘Tunamshukuru mfalme.’ Basi wakatoka wakaenda zao nasi tukazitazama nguo zile. Kazi yake ilikuwa nzuri mno kupita zote tulizoona.

Nikamuuliza Infadus, ‘Je, hizi nguo zina tengenezwa hapa kwenye hii nchi?’
Akajibu, ‘Hapana, bwana wangu, tumezirithi kutoka kwa mababu zetu.

Hatujui ni nani aliyezitengeneza, na sasa zimebaki chache tu. Waana wa mfalme tu ndio wanaoruhusiwa kuzivaa. Zina nguvu kama zile za uchawi na mkuki hauwezi kuzipenya. Mtu akivaa nguo hizi katika vita yu salama.


Mfalme amependezwa sana, au ameogopa sana, maana asingewaleteeni nguo hizi. Mabwana zangu, afadhali mzivae usiku wa leo.’

Basi tulipumzika siku ile tukaongea juu ya mambo yaliyotokea. Jua lilipotua tuliona mwangaza wa mioto mingi na katika giza tulisikia vishindo vya nyayo za watu wengi na vya mikuki yao, vikosi vilipokuwa vikipita na kujipanga katika utaratibu wa kujitayarisha kwa ngoma kuu ya usiku.


Baadaye kidogo mwezi ulitoka ukaangaza nchi yote, tukasimama na kutazama mbalamwezi; akaja Infadus amevaa nguo zake nzuri za vita, amefuatana na askari ishirini, kutupeleka kwenye ngoma.

Tulikuwa tumekwisha vaa zile nguo za minyororo ya chuma kama alivyotushauri, na juu yake tukavaa nguo zetu za kila siku.

Tukajifunga bastola zetu, tukachukua mikononi mashoka yale ya vita aliyotupa mfalme, tukaondoka.

Tulipofika kwenye jumba kuu tuliona mahali palipojaa watu kiasi elfu ishirini waliopangwa kwa vikosi.

Vikosi hivyo viligawanywa katika makundi, na katikati ya kila kundi na kundi waliacha njia ili kusudi wale watakaotambulisha wachawi wapate nafasi ya kupita.
 
Ikawa shani ya kustajabisha kabisa. Wote walisimama kimya kabisa, na mwezi ukawaangaza wakawa kama mwitu wa mikuki, na manyoya yao ya vichwani yalipepea katika upepo.

Popote tulipotazama tuliona mistari kwa mistari ya mikuki inayong’aa.
Nikamwambia Infadus, ‘Jeshi zima limehudhuria?’ akajibu, ‘La, Makumazahn, hii ni theluthi tu. Maana ni theluthi tu huudhuria kwenye ngoma kuu kila mwaka.

Theluthi nyingine imewekwa nje tayari kukomesha matata ikiwa yatatokea wakianza mauaji, elfu kumi hulinda nje ya mji wa Loo, na waliobaki wametawanywa katika miji ya nchi.’

Bwana Good akasema, ‘Wamekaa kimya kabisa.’ Infadus akauliza, ‘Je, Bwana anasema nini?’ Nikamtafsiria, akajibu, ‘Wanaokabiliwa na mauti huwa kimya.’
Nikamuuliza, ‘Wengi watakufa?’ Akajibu, ‘Wengi sana.’

Nikawaambia wenzangu nao wakasikitika kabisa . Nikamuuliza Infadus, ‘Je, waonaje, tutakuwa katika hatari?’ Akajibu, ‘Sijui, mabwana zangu, lakini natumai mtakuwa salama. Maana askari wananung’unika juu ya mfalme.’

Basi wakati huo tulikuwa tukisogea tufike katikati ya nafasi tuliona viti vimewekwa tayari. Tulipokuwa karibu tuliona kuwa wengine wanatoka katika jumba la mfalme, na Infadus akasema, ‘Ni mfalme Twala na mwanawe Skraga na kizee Gagula; na pamoja nao ni wale wauaji.’

Akaonyesha kundi dogo la watu wakubwa sana wenye sura za ukali na ukatili, kila mtu ana mkuki katika mkono mmoja na rungu katika mkono wa pili. Mfalme akakaa katika kiti chake katikati, na Gagula akajikalisha chini penye miguu yake, na wengine walisimama nyuma.

Mfalme Twala akasema, ‘Karibuni, mabwana weupe, kaeni msipoteze wakati wenye thamani, usiku ni mfupi sana na kazi iliyo mbele yetu ni kubwa. Mmekuja wakati unaofaa sana, maana mtaona mambo mkuu sana.

Tazameni, mabwana, nyota zaweza kuwaonyesha shani kama hii? Tazameni namna wanavyotetemeka kwa uovu wao, wale wote wenye uovu katika mioyo yao wanaihofu hukumu ya mbinguni.’

Gagula akalia, ‘Anzeni! Anzeni! Fisi wanaona njaa, wanalilia chakula chao. Anzeni! Anzeni!’

Kwa muda kidogo ikawa kimya kabisa. Mfalme akainua mkuki wake na mara ile miguu ishirini elfu ikainuliwa kama mguu wa mtu mmoja, ikakanyaga chini tena kwa kishindo kimoja.

Mara tatu walifanya hivi, na nchi ilitetemeka kwa kishindo.
Ndipo mbali palipo watu sauti moja ikaanza kuimba wimbo kama wa kusikitika na wengine wakaitika.

Maneno ya wimbo yalikuwa haya: Nini ajali ya mtu azaliwaye…? Na sauti za wote zikaitikia, Mauti…?

Kwa taratibu wimbo huo ulishikwa na watu wote katika kila kikosi mpaka wote walikuwa wakiimba. Sikuweza kusikia maneno yote ya wimbo ila nadhani yalikuwa yakisimulia habari za mambo yanayowapata wanadamu, kama vile tama zao na hofu zao na furaha zao.

Kwanza yalionyesha mapenzi, halafu yakawa ya vita, halafu yakawa maneno ya kusikitikisha sana ya mauti.

Walipokwisha kuimba kukawa kimya tena, na mfalme akainua tena mkono wake, na mara tulisikia nyayo za watu wanakuja na katika kundi la watu tuliona watu wa kutisha sana wanatoka.

Walipotukaribia tuliona kuwa ni wanawake wazee na nywele zao nyeupe zilifungiwa vibofu vidogo vilivyotolewa katika matumbo ya samaki, vikipeperuka nyuma yao.

Nyuso zao zimetiwa rangi nyeupe na ya kimanjano; na nyuma walifunga ngozi za nyoka na kiunoni walijifunga mifupa ya wanadamu, na kila mtu alishika fimbo yenye meno matatu nchani mkononi mwake.

Jumla yao ilikuwa kumi, na mmoja wao alimwonyesha Gagula kwa mkono wake akasema, ‘Mama, mama mzee, tupo hapa.’ Yule Gagula akaitikia, ‘Vema! Vema! Vema! Macho yenu makali? Nyinyi watambuzi, nyinyi mnaweza kuona gizani?’ Wakajibu, ‘Mama, ‘Ni makali.’

Akasema, ‘Vema! Vema! Vema! Masikio yenu yamefumbuka, nyinyi watambuzi, nyinyi mnasikia maneno yasiyotamkwa kwa ulimi?

Wakajibu, ‘Mama, yamefumbuka.’ Akaitikia, ‘Vema! Vema! Vema! Pua zenu zinaweza kusikia harufu, nyinyi watambuzi? Mnaweza kusikia harufu ya damu, manaweza kusafisha nchi yetu kwa kuwaondoa wale wanaomfanyia maovu mfalme na jirani zao?

Mpotayari kuhukumu kwa haki za mbinguni? Nyinyi niliowafundisha, mliokula mkate wa busara zangu na kunywa maji ya uwezo wangu?’ Wakaitikia, ‘Mama, tunaweza.’
Basi akasema, ‘Vema, nendeni.

Msikawie, nyinyi tai; mwaona wauaji?’ (Akawaonyesha wale waliosimama tayari kuua.) ‘Haya fanyeni mikuki yao kuwa mikali; watu weupe waliotoka mbali wana hamu ya kuona, nendeni!’
 
Basi wale watu wakalia kwa sauti kuu wakatawanyika pote, na mifupa waliyofunga ikagongana walipokuwa wakienda ; wakaenda kila mahali katika kundi lile la watu.

Hatukuweza kuwatazama wote, basi tulimtazama Yule aliyekuwa karibu. Alipopita karibu na askari wale waliosimama, kisha akaanza kucheza na kuruka ruka, akizunguka zunguka kwa upesi sana, na akisema maneno kama haya:

‘'Nasikia harufu yake, mtenda maovu! Yu karibu, Yule aliyempa sumu mama yake! Nasikia mawazo maovu aliyemwazia mfalme!’'

Akazidi kucheza upesi upesi mpaka akawa kama mwenye wazimu na povu likamtoka kinywani na macho yakawa kama yanatoka kichwani, na mwili wake ulitetemeka. Mara akasimama akakaza mwili kama mbwa anayesikia harufu ya nyama porini, akanyosha fimbo yake na akaanza kuwaendea pole pole wale askari.

Na sisi tulimfuata kwa macho yetu kama tumepagawaa. Basi akafanya hivi mpaka alipofika mbele yao karibu, ndipo aliposimama akanyosha fimbo yake, akatambaa mbele kidogo tena. Mara mambo yalikwisha.

Kwa kilio kikuu aliruka akamgusa askari mmoja kwa fimbo yake. Mara Yule askari alishikwa na wenzake wawili akaletwa mbele ya mfalme. Hakufanya ukaidi, lakini tuliona kuwa walipokuwa wakimleta alikuwa kama amepooza, na vidole vilikuwa kama vidole vya maiti, na mkuki ulimponyoka.

Alipofika karibu, wauaji wawili wakatoka mbele, wakamtazama mfalme ili kupewa amri. Mfalme akasema, ‘Muueni!’
Na Gagula akalia, ‘Muue!’
Na yule Skraga akacheka akasema, ‘Muue!’

Basi kabla hawajamaliza kusema, mauaji yalikwisha tendeka. Mtu mmoja akamchoma mkuki wa moyo, na Yule mwingine akampiga rungu la kichwa. Mfalme Twala akahesabu, ‘Mmoja.’ Na maiti ilichukuliwa ikalazwa pale pale.

Mara tuliona mtu mwingine analetwa kama ng’ombe anayeletwa kuchinjwa. Mtu huyu alikuwa mwenye cheo, maana alikuwa kava ngozi ya chui. Tena tulisikia maneno yale yale ya kikatili na Yule mtu akaanguka amekufa. Mfalme akahesabu, ‘Wawili.’


Basi vivyo hivyo mchezo wao ukaendelea mpaka maiti mia moja walilazwa kwa safu. Mara moja tulisimama tukajaribu kumzuia mfalme, lakini alitukanya kwa ukali, akasema, ‘Acheni sheria iendelea, nyinyi watu weupe. Mbwa hawa ni wachawi na watenda maovu; kufa ni haki yao.


Ilipopata saa nne na nusu, mambo yakasita kidogo, na wale waliokuwa wakichagua wachawi wakajikusanya pamoja, tukafikiri kuwa wamechoka.

Lakini sivyo, maana tuliona ajabu Gagula alipojiinua akajikongoja kwa fimbo yake akaja katikati. Ikawa ajabu kumwona, Alikuwa karibu kupinda kabisa, lakini alipata nguvu akaanza kwenda mbio huku na huko kama walivyo fanya wanafunzi wake.


Haku na huko alikwenda mbio huku akiimba, mpaka akamrukia mtu mrefu aliyekuwa kasimama mbele ya kikosi kimoja, akamgusa. Alipofanya hivi, watu wakikosi chake wakaguna. Lakini wawili wao wakamshika wamlete mbele ya mfalme auawe.


Baadaye tulikuja kujua kuwa ni mwenye cheo kikubwa naye ni tajiri sana, tena ni mjukuu wa mfalme mwenyewe. Aliuawa, na mfalme akahesabu mia moja na tatu. Tena Gagula akaruka huku na huko, akaanza kutukaribia sisi.

Bwana Good akasema, ‘Lo! Nadhani anatujia sisi.’ Bwana Henry akasema, ‘Upuuzi! Hathubutu!’ na mimi nilipoona kuwa Yule afiriti anatukaribia, nilikata tamaa kabisa. Nikageuka nikatazama safu zile za maiti, nikatetemeka.


Gagula akakaribia, akakaribia zaidi na macho yake yakang’aa kwa uovu. Akaja karibu, karibu, na kila mtu hadharani alimkodolea macho.

Mwisho akasimama, akanyosha fimbo yake, na mara akamrukia Umbopa, yaani Ignosi, akamgusa begani, akasema, ‘Nasikia harufu yake.

Muue, muue, amejaa uovu; muue mgeni huyu kabla damu haijamwagika kwa ajili yake. Ee mfalme, muue!’

Hapo ikawa kimya kidogo, nami nikasimama nikasema, ‘Ewe mfalme, mtu huyu ni mtumishi wa wageni wako. Yeyote atakaye mwaga damu yake anamwaga damu yetu. Kwa ajili ya ukarimu wako, naomba asidhuriwe.’ Mfalme akasema, ‘Gagula, mama wa watambuzi wa wachawi, amemchagua; lazima afe.’


Nikajibu, ‘Hafi kabisa. Atakayejari kumgusu ndiye Atakayekufa.’
Twala akasema kwa sauti kubwa. ‘Haya, mkamateni’ Na wale wauaji waliopaka damu ya wale waliowaua, wakaja mbele, lakini walisita. Ignosi alishika mkuki wake, akawa tayari kupigania maisha yake.


Nikasema, ‘Rudini nyinyi! nyinyi, mbwa! Mkitaka kuona mwangaza wa jua kesho, rudini! Mkigusa hata unywele mmoja wa kichwa chake, basi mfalme wenu atakufa.’

Nikaelekeza bastola yangu kwa mfalme, Bwana Henry na Bwana Good vile vile wakatwaa bastola zao, na Bwana Henry akamwelekezea Yule muuaji wa mbele, na Bwana Good akamwelekezea Gagula Yule kizee.


Twala alipoona bastola imewekwa sawa na kifua chake akajikunja, nikasema, ‘Je, Twala, utafanya nini?’ Akasema, ‘Haya wekeni mianzi yenu ya ajabu, umeomba kwa ajili ya ukarimu na kwa ajili hiyo nitamwacha, wala si kwa kuhofu vitendo vyenu. Nendeni kwa amani.’


Nikajibu, ‘Vema, tumechoka kuona mauaji. Tunataka tukalale. Je, ngoma imekwisha?’
Twala akajibu, ‘Imekwisha,’ Akageuka akaonyesha maiti wale akasema, ‘Mizoga ya mbwa hawa itupiwe fisi na tai mwituni.’ Akainua mkuki wake.


Mara vikosi vikaanza kutoka kwa taratibu na kwa kimya kabisa, wachache tu walibaki ili kuchukua maiti. Tukaondoka tukamuuaga mfalme tukaenda nyumbani, naye hakutaka hata kututazama .


Tulipofika nyumbani tukawasha taa za Kikukuana, yaani, uzi kidogo uliowekwa kwenye mafuta ya kiboko, na Bwana Henry akasema, ‘Mimi naona kama nataka kutapika.’
Na Bwana Good akasema, ‘Kama nilikuwa na shaka katika shauri la kumsaidia Umbopa katika kumpiga vita Yule Twala, basi sasa limeondoka kabisa.

Nilijizuia kwa nguvu walipokuwa wakiwaua wale watu. Nilijaribu kufumba machoyangu, lakini ikawa kila mara nilipoyafumbua ukawa wakati usiofaa! Je, yupo wapi Umbopa.


Ehe rafiki yangu, nadhani yafaa kutushukuru sana, wewe ulikuwa karibu na kufa leo.’ Umbopa akajibu, ‘Ndiyo, kweli, nawashukuru sana.

Sitaweza kusahau mambo ya usiku huu. Infadus atakuja baadaye, lazima tumngojee.’ Basi tukatia tumbako katika viko vyetu, tukakaa tukivuta na kumngoja.
 
SURA YA KUMI NA MOJA


Kwa muda mrefu, kadiri ya saa mbili tulikaa kimya. Tulikuwa tumeshindwa kuondosha fikra za vitisho tulivyoviona usiku ule. Baadaye tuliona ni usiku sana tukafikiri kwenda kulala, na mara tulisikia kishindo cha miguu ya watu.

Tukasikia sauti ya mtu aliyekuwa akilinda zamu, na mara tukasikia nyayo zinakaribia; na baada ya muda kidogo Infadus akaingia ndani pamoja na watu warefu sita.

Infadus akasema, ‘Mabwana zangu, nimekuja kama nilivyoahidi. Mabwana zangu na Ignosi, mfalme wa haki wa Wakukuana, nimewaleta watu hawa walio wakubwa wetu, na kila mmoja ni mkubwa wa skari elfu tatu.

Askari hao huwatii kufanya wanavyoamrishwa chini ya mfalme. Nimewaeleza niliyoyaona na kusikia. Sasa waonyeshe nyoka mtukufu aliyochajwa kiunoni mwako, Ee Ignosi, wapate kukata shauri kama watakusaidia kupingana na Mfalme Twala.’

Ignosi akavuta tena ukanda wake akawaonyesha Yule nyoka aliyochanjwa kiunoni mwake. Kila mkubwa akamtazama kwa mwangaza wa taa, kisha bila ya kusema neno, kila mmoja akapita akasima kando.

Sasa Ignosi akavaa tena ukanda akawaeleza habari zile alizosimulia asubuhi.
Kisha, Infadus akasema, ‘Sasa nyinyi wakubwa mmesikia, mnasemaje? Mtamsaidia mtu huyu ajipatie ufalme wa baba yake?

Nchi inalalamika kwa sababu ya ukatili wa Twala, na damu za watu zinamwagika kama mto wakati wa masika. Mmeona usiku huu huu. Walikuwapo wawili wengine niliotaka kusema nao, na sasa wako wapi? Fisi wanapigania maiti zao sasa.

Na nyinyi mtakuwa kama walivyo wao msipojipigania upesi. Basi ndugu zangu chagueni.’
Yule mkubwa katika wale sita akasimama mbele akasema, ‘Infadus, maneno yako niya kweli; nchi inasikitika.

Ndugu yangu mimi ameuliwa usiku huu huu; lakini jambo hili ni kubwa mno nalo ni vigumu kuamini.

Tutajuaje ya kuwa tukipigana kwa ajili ya mtu huyu hatumpiganii mwongo? Nasema ni jambo kubwa na mwisho wake haujulikani.

Kwa hakika damu itamwagika kama mito kabla ya kumalizika jambo hilo; wengi watamfuata mfalme; na watu weupe hawa waliotoka katika nyota, kweli uwezo wao ni mkubwa, nao Ignosi yu chini ya ulinzi wao.


Ikiwa kweli ni mfalme wa haki, basi na watuonyeshe ishara, na watu waonyeshwe ishara ili wote waione. Hivyo watu wataambatana nasi wakijua kuwa nguvu za watu weupe ziko upande wetu.’

Nikajibu, ‘Mmeona ishara ya nyoka.’ Akasema, ‘Bwana wangu, haitoshi. Inawezekana kuwa ile alama ilichanjwa baada ya utoto wake. Tuonyesheni ishara, Hatuwezi kufanya kitu bila kupata ishara.’

Wale wengine wakasema hivyo hivyo, nikawa katika shida, nikawageukia Bwana Henry na Bwana Good nikawaeleza mambo yote.

Bwana Good akacheka, akasema, ‘Nadhani nimepata shauri la kufaa. Waambie watupe nafasi kidogo tupate kufikiri.’

Nikawaambia, wakajitenga mbali kidogo. Bwana Good akafungua kasha lake la dawa zake, akatoa kitabu chake chenye takwimu.(Yaani hesabu ya miezi na miaka na habari za mwezi na nyota.)

Akasema, ‘Sasa tazameni rafiki zangu, kesho ni siku ya nne katika mwezi wa Juni sivyo?’ Tulikuwa tukiweka hesabu kila siku, tukamwambia ndiyo. Akasema, ‘Vema, hapa imeandikwa kuwa siku ya nne katika mwezi wa June mwezi utapatwa kwenye saa mbili na robo.

Basi ndiyo ishara yetu. Waambie kuwa tutafanya mwezi kutoweka usiku wa kesho.’ Shauri likawa ni jema sana, na hatari iliyopo ni labda habari zilizoandikwa katika kitabu ya kuwa zitatokea si kweli.

Maana tukitangaza ishara ya namna hiyo nayo isipotokea, nguvu zetu mbele ya Wakukuana zitakwisha kabisa, na tena tutashindwa kumweka Ignosi katika kiti cha ufalme wa Wakukuana.
 
Basi tukafanya hesabu yetu, tukaona kuwa kwa mahali tulipo, mwezi utapatwa saa nne ya usiku wa kesho, nao utaachiliwa tena saa tisa na nusu.

Yaani kwa muda wa saa moja na nusu itakuwa giza tupu. Bwana Henry akasema, ‘Basi, afadhali tubahatishe.’

Nikamtuma Umbopa kuwaita wale Wakubwa, na walipokuja nikawaambia, ‘Watu wakubwa wa Wakukuana na wewe Infadus, sikilizeni. Hatupendi kabisa kuonyesha kabisa nguvu zetu, maana kufanya hivi kunaweza kubadili mwendo wa mambo ya asili, napengine kutia dunia katika hofu na fadhaa.


Lakini kwa kuwa ni jambo kubwa, na kwa kuwa tumemkasirikia Mfalme Twala kwa ajili ya mauaji tuliyoyaona, na kwa sababu ya vitendo vya Yule Gagula ambaye alitaka kumuua rafiki yetu Ignosi, tumenuia kuonyesha ishara ambayo watu wote wataiona. Njooni.’


Nikawaongoza mlangoni nikawaonyesha mwezi uliokuwa ukishuka, nikasema, ‘Mnaona nini huko juu?’ Wakajibu, ‘Twaona mwezi unaotua.’


Nikajibu, ‘Kweli. Na sasa niambieni, je, yuko mtu yeyote anayeweza kuushusha mwezi kabla haujafika wakati wa kushuka, na kufunikiza nchi yote kwa pazia la giza usiku?’ Yule mkubwa aliyekuwa msemaji wao akacheka kidogo akasema, ‘Hayupo, bwana wangu, hapana mtu anayeweza kufanya hivi.

Mwezi una nguvu nyinyi kuliko wale wanaoutazama, wala hauwezi kubadili majira yake.’
Nikajibu, ‘Wewe unasadiki hayo, lakini nakwambia ya kuwa usiku wa kesho saa nne tutafanya mwezi kuliwa kwa muda wa saa moja na nusu.


Ndiyo, giza tupu litafunika nchi na itakuwa ishara kuonyesha kuwa Ignosi ndiye mfalme halisi wa Wakukuana.

Tukifanya hivi mtaridhika?’ Yule mkubwa akajibu, ‘Ndiyo, bwana wangu, mkifanya hivi sisi tutaridhika kabisa.’

Nikajibu, ‘Vema, itafanyika; sisi watatu tumesema, nayo yatafanyika. Umesikia, Infadus?’
Infadus akasema, ‘Nasikia bwana wangu, lakini ni jambo la ajabu uliloahidi litafanyika, yaani kuzima mwangaza wa mwezi ulio mama wa dunia.’

Nikasema, ‘Ni ajabu kweli, lakini nakwambia kuwa tutafanya.’
Infadus akasema, ‘Vema, bwana wangu, kesho saa mbili baada ya kushuka jua, mfalme Twala atawaita nyinyi mabwana zangu ili mwende mkatazame ngoma ya wanawali, na baada ya saa moja kutoka kuanza ngoma, Yule mwanamwali anayedhaniwa na Twala kuwa mzuri kupita wenzake wote atauawa na Skraga, mwana wa mfalme, awesadaka ya Wale Watatu wanaokaa kimya wakiangalia milima.’


Akaonyesha vile vilele penye mwisho wa Njia Kuu ya Sulemani, ‘Basi, ndipo mabwana zangu watie mwezi giza na kuokoa maisha ya mwanamwali, na kweli ndipo watakaposadiki watu wote.’


Yule mzee akasema, ‘Ndiyo, kweli ndipo watakaposadiki watu wote. ‘ Akacheka kidogo. Infadus akaendelea akasema, ‘Mwendo wa nusu saa kutoka mji wa Loo upo mlima uliokaa mfano wa upinde au mwezi mpya, nao ni kama boma, ndipo vilipowekwa vikosi vitatu vyangu na vikosi vitatu vingine vya wakubwa hawa.

Kesho asubuhi tutafanya shauri la kupeleka vikosi viwili au vitatu vingine.


Na ikiwa nyinyi mabwana wangu mtafaulu kutia giza mwezi, basi tutaungana mikono na nitawaongoza kumpiga vita mfalme.’ Nikajibu, ‘Vema, na sasa tuache tupumzike kidogo tufanye tayari ishara yetu.’


Walipokwisha kwenda, Umbopa, yaani Ignosi, akasema, ‘Rafiki zangu, mnaweza kufanya jambo hilo la ajabu, au mlikuwa mnasema maneno ya bure?’

Nikajibu, ‘Tunadhani kuwa tunaweza kulifanya, Ignosi.’ Akasema, ‘Tukiwa hai baada ya mambo haya, hakika nitawalipa.’

Bwana Henry akasema, ‘Ignosi, nakutaka uahidi neno moja.’ Ignosi akacheka, akajibu, ‘Hata kabla sijasikia neno lenyewe nitaahahidi nini?’

Akajibu, ‘Ni hili: ukijaliwa kuwa mfalme, ahidi kuwa utakomesha desturi hii tuliyoona ya kuwafichua wachawi na kuwaua watu bila kuwahukumu kwa haki.’

Ignosi akafikiri kidogo kwanza na baadaye akasema, ‘’Desturi za watu weusi si kama za watu weupe. Lakini nitaahidi. Nikipata nguvu nitazuia wasifichue tena wachawi, tena watu hawatauawa bila kuhukumiwa kwa haki kwanza.’

Basi Bwana Henry akasema, ‘Basi sasa tumekwisha patana, tulale tupumzike.’
 
Basi Bwana Henry akasema, ‘Basi sasa tumekwisha patana, tulale tupumzike.’


Tulilala upesi sana, maana tulichoka sana, wala hatukuamka mpaka Ignosi alipotuamsha saa tano. Tuliondoka tukaoga tukala. Baadaye tulitoka nje tukatazama namna nyumba zilivyojengwa, na desturi za watu.

Halafu Bwana Henry akasema, ‘Natumaini kuwa kweli mwezi utapatwa usiku.’ Nikajibu, ‘Kama haupatwi basi tumekwisha kabisa, maana haikosi wakubwa wengine watamweleza mfalme habari zote na hatima yetu itatatufika upesi.’

Basi tukarudi nyumbani tukala chakula cha mchana tukakaa tukizungumza na watu waliokuja kutuamkia. Jua liliposhuka tulikaa muda wa saa mbili tukifikiri, na saa mbili na nusu tarishi akaja kutoka kwa mfalme Twala kutukaribisha kwenye ngoma ya wanawali usiku huo huo.

Tukafanya haraka tukavaa nguo zile za minyororo ya chuma chini ya nguo zetu, tukatwaa bunduki zetu na risasi ili tuwe tayari ikilazimu kukimbia mambo kama ya kienda ovyo. Tukatoka kama mashujaa, lakini katika mioyo yetu tulitetemeka kabisa.

Tulipofika katika kiwanja kile mbele ya jumba la mfalme, tuliona ni namna nyingine kabisa. Badala ya safu za askari, tuliona makundi ya wanawali, na kila mmoja amejipamba na amevaa maua kichwani, na katika mkono mmoja ameshika kuti kama lile la mtende, na katika mkono wa pili ameshika ua kubwa jeupe.

Katika nafasi ya katikati iliyoangazwa na mbalamwezi, mfalme Twala amekaa na Gagula amekaa kitako miguuni pake, na kijana Yule Skraga amesimama nyuma pamoja na askari kumi na mbili. Wakubwa ishirini walikuwapo, nikawatambua wale waliotujia usiku wa jana.

Twala alituamkia kwa urafiki lakini niliona kama alimtazama Umbopa kwa uchungu mwingi, akasema, ‘Karibuni, nyinyi watu weupe mliotoka katika nyota.

Leo mtaona mambo mengine si kama yale mliyoona usiku wa jana, lakini si mazuri kama yale ya jana. Wanawali ni wazuri mno nao wanafurahisha, maana wasingekuwepo na sisi tusingekuwepo; lakini wanaume ni bora. Maneno ya wanawake ni matamu naya kupendeza, lakini kishindo cha mikuki ya mashujaa na harufu ya damu ni tamu zaidi.


Lakini karibuni, mabwana, na wewe mtu mweusi, karibu; Kama Gagula angalifanikiwa alivyotaka, wewe ungali kuwa maiti sasa. Una bahati kuwa na wewe vile vile umetoka katika nyota. Ha!Ha!’

Ignosi akajibu kwa upole sana, ‘Nitakuua wewe kabla ya kuniua mimi, nawe utakuwa mkavu kabla viungo vyangu havijaacha kujimudu.’

Twala akashtuka akasema kwa sauti kali, ‘Maneno yako ni makubwa, wewe kijana, usinikasirishe zaidi.’ Umbopa akajibu, ‘anayesema kweli ana haki ya kusema maneno makubwa. Kweli ni mkuki mkali unaopiga shabaha kila mara. Hii ndiyo habari ninayokupa kutoka nyotani Ewe Mfalme.’

Twala akakunja uso wake asiseme neno. Halafu alisema, ‘Haya, ngoma ianze sasa.’
Na mara wale wanawali waliopambwa na maua waliondoka wakaanza kucheza, wakaimba nyimbo nzuri.

Wakacheza, wakacheza, pengine walizunguka wakakutana katikati, wakafanya mfano wa vita, tena wakaenda mbele na kurudi nyuma tena.

Ndipo alipotokea mmoja mzuri sana akacheza mbele yetu kwa namna ya ajabu. Alipokwisha akarudi nyuma na mwingine akaja mbele akacheza, hivyo hivyo.

Walipokwisha cheza hivyo, mfalme akainua mkono akasema, ‘Je nyinyi watu weupe, nani mzuri kupita wote?’ Mimi nikajibu bila kufikiri sana, nikasema, ‘Yule aliyekuja kwanza kucheza .’

Mara nikakumbuka alivyotwambia Infadus kuwa Yule mzuri kupita wote lazima auawe ili kuwa sadaka, nikasikitika na nikajuta kwa maneno yangu.

Basi mfalme akasema, ‘Unavyofikiri wewe, ndivyo ninavyofikiri mimi. Yeye ni mzuri; na hayo ni huzuni kwake maana lazima afe.’

Gagula akaitikia, ‘Ndiyo, lazima afe.’ Akamtazama Yule masikini mwanamwali aliyekuwa kasimama hajui ajali inayomngojea.

Nikajizuiya nilivyoweza, nikamuuliza, ‘Ewe mfalme, kwa nini afe, Yule mwanamwali aliyecheza vizuri akatupendeza sana? Tena ni mzuri mno; ni vibaya kumlipa kwa kumuua.’

Twala akacheka akajibu, ‘Ni desturi yetu, maana wale watatu wakaao huko lazima wapate haki yao.’ Akaonyesha penye vilele vile vya mlima. ‘Nisipomuua Yule msichana mzuri, kisirani kitaniangukia nyumbani kwangu.

Haya ndiyo yaliyobashiriwa zamani. Ikiwa mfalme ataacha kumuua mwanamwali aliye mzuri katika siku ya ngoma ya wanawali awe sadaka kwa Wale Watatu wakaao huko, basi ataanguka yeye na nyumba yake.

Tazameni, watu weupe, ndugu yangu aliyetangulia kutawala, hakutoa sadaka kwa sababu ya machozi ya mwanamke, basi akaanguka yeye na nyumba yake vile vile, nami nilishika utawala wake.
Yamekwisha, lazima afe!
 
Akawageukia askari akasema, ‘Haya, mlete hapa; na wewe Skraga, unoe tayari mkuki wako.’ Basi watu wawili wakaja mbele na walipomkaribia Yule mwanamwali, ndipo kwanza alipofahamu ajali yake, akalia sana, akageuka apate kukimbia. Lakini wale askari wawili walimshika wakamleta analia na kujaribu kuwatoka.


Gagula akamuuliza, ‘Jina lako nani, wewe mwali? Je, hutaki kunijibu? Je, mwana wa mfalme afanye kazi yake sasa?

Kusikia hayo, Skraga alionekana kuwa mwovu kupita kiasi, akajongea hatua moja, akainua mkuki wake, na mara niliona mkono wa Bwana Good unashika bastola, na Nuru ya bastola ilimpata machoni Yule mwali, akanyamaza kimya.

Akaacha kushindana, akafumbata mikono yake akasimama anatetemeka toka kichwa hata miguu.

Skraga akacheka, akasema, ‘Tazama anajikunyata kuona mchezo wangu, hata kabla hajaiona.’ Akapapasa mkuki wake. Nikamsikia Bwana Good anasema kimoyomoyo, ‘Lo! Nikipata nafasi utajuta maneno yako, Mbwa we!’

Basi, sasa Gagula akamfanyia dhihaka , akasema, ‘Sasa umekwisha tulia, tuambie jina lako nani? Mpenzi wangu. Haya sema, usiogope.’


Yule mwali akatetemeka, akajibu, ‘’Ewe mama, jina langu naitwa Foulata, na ukoo wangu ni Suko. Ewe mama, kwa nini sina budi kufa? Mimi sikufanya makosa au ubaya wowote!’


Gagula akajibu, ‘Usifadhaike, lazima ufe uwe sadaka kwa Wale Wazee wakaao huko, lakini ni afadhali kulala usiku kuliko kufanya kazi mchana; ni afadhali kulala usiku kuliko kufanya kazi mchana; ni afadhali kufa kuliko kuishi, nawe utakufa kwa mkono wa mwana wa mfalme.’


Yule mwali Foulata akajiuma vidole vyake kwa huzuni akalia, ‘Ole wangu, huu ndio ukatili kweli! Mimi ni kijana! Nimefanya nini nisipate kuona jua likitoka katika giza la usiku huu, nisione tena nyota zikifuata majira ya jioni, nisipate kuchuma maua katika umande wala kusikiliza nyimbo za mteremko wa maji?


Ole wangu, sipati tena kuona nyumba ya baba yangu, wala kuona tena mapenzi ya mama yangu, wala kuchunga wana wa kondoo! Ole wangu, sitapata mwanaume wakunipenda na wala sitazaa wana! Ukatili! Ukatili!’

Tena akajiuma vidole kwa huzuni akageuka akatazama juu na machozi yalionekana yakimtoka machoni, akawa wa kusikitisha kabisa hata kuleta huruma kwa mtu yeyote, ila wale mashetani waliokuwa wamekaa mbele yetu hawakujali kabisa.

Na wala haikuvuta huruma kwa Gagula, wala bwana wa Gagula, ila niliona dalili ya huruma na huzuni katika sura za walinzi wale, na katika sura za wale wakubwa waliokuwapo; na Bwana Good alijizuia kwa shida tu, akafanya kama anakwenda kumsaidia.


Basi kwa akili ya kike, Yule mwali alitambua fikira zake, na mara akaruka akajitupa mbele yake akamshika miguu akalia, ‘Ewe baba mweupe uliyetoka katika nyota, nifunike kwa nguo yako ya ulinzi, nitambae katika kivuli cha nguvu zako nipate kuokoka.


Niokoe katika mikono ya watu waovu hawa wasio na huruma!’ Bwana Good akamshika mkono akasema, ‘Vema, mimi nitakulinda.’ Akainama akamshika mkono akasema, ‘Haya ondoka, mwanangu.’


Twala akageuka akamwashiria mwanawe, naye akajongea mbele ameshika mkuki juu.
Bwana Henry akasema akinong’oneza, ‘Sasa huu ndiyo wakati unaofaa; unangoja nini? Nikajibu kwa sauti ndogo, ‘Mimi nangoja kuona dalili ya mwezi kupatwa kwanza.


Nimeutazama kwa nusu saa hivi, lakini sioni dalili ya kupatwa.’
Akajibu, ‘Sasa lazima tubahatishe au huyu mwanamwali atauawa, maana naona Twala anaanza kuchoka.’

Basi nikatambua kuwa asemavyo ni kweli, nikatazama mwezi mara moja tena nisione hata dalili ya kupatwa, nikajikaza nikasimama mbele, nikajongea katikati ya Skraga na yule mwanamwali, nikasema, ‘Mfalme jambo hili halitakuwa; sisi hatutavumilia jambo hili; mwanamwali na aende zake salama.’


Twala akaghadhibika mno, akasimama katika kushangaa kwake, na askari wake waliokuwapo na wanawali nao walishangaa.


Na mfalme Twala akasema, ‘Halitakuwa! Wewe mbwa mweupe aliaye mbele ya simba katika pango lake; halitakuwa! Wewe una wazimu? Angalia sana usije ukapatwa na ajali ya kifaranga huyo, na wale waliopo pamoja nawe vile vile.

Je, wawezaje kumwokoa au kujiokoa mwenyewe? Nani wewe ujitiaye katikati ya mimi na matakwa yangu? Kaa upande, na wewe Skraga muue!


Haya, askari wangu, washike watu hawa.’ Basi hapo askari wengi wakatoka kwa nyuma ya jumba walikofichwa. Bwana Henry na Bwana Good na Umbopa wakasogea karibu nami, wakaelekeza bunduki zao.


Nikasema kwa sauti kuu lakini moyo wangu haukwepo kabisa, ‘Acheni! Twacheni sisi watu weupe tuliotoka katika nyota, tunasema kuwa halitakuwa.

Mkikaribia hata hatua moja tu, tutauzima mwezi, na sisi tukaao katika nyumba yake tunaweza kufanya hivi, tutaitia nchi yote katika giza tupu, nanyi mtaonja uchungu wa nguvu zetu.’

Basi maneno yangu yaliwastua; watu wakasimama, na Skraga akasimama kimya mbele yetu, ameshika mkuki wake juu.

Gagula akasema, ‘Msikieni! Msikieni! Msikieni asemavyo uwongo. Basi na afanye anavyosema na mwanamwali ataachiliwa. Afanye au auawe pamoja na mwanamwali na wale walio pamoja naye.’


Nikatazama mwezi tena, na sasa: nilifurahi, maana niliona kuwa alama nyeusi inaanza kuonekana katika mwezi.

Ndipo nilipoinua mkono wangu kwa taratibu sana nikaonyesha juu mbinguni, na Bwana Henry na Bwana Good wakafanya vile vile, tukaanza kusema maneno yoyote tuliyoweza kuyakumbuka.

Pole pole na kwa tara-tibu, kivuli kilianza kufunika mwezi, na kilipozidi kuja nikasikia watu wanaanza kuvuta pumzi juu, nikasema,
‘Tazama, Ewe Mfalme! Tazama, Gagula!

Tazameni nyinyi wakubwa, na watu wote, mwone kama watu weupe waliotoka katika nyota wametimiza maneno yao au kama ni uwongo mtupu! Mwezi unafunikwa mbele ya macho yenu; na sasa hivi itakuwa giza tupu.

Mmeomba ishara nasi tumeifanya. Ee mwezi, ufunikwe uwe giza tupu! Uzime mwangaza wako, Ee wewe mtakatifu; ulete ule moyo wa kiburi hata mavumbini, Ee mwezi, ule dunia kwa vivuli vyako.’

Basi watu wote waliguna kwa hofu. Wengine walisimama kama wamegeuka mawe, na wengine walijitupa chini wakapiga magoti wakalia kwa sauti kubwa.


Na mfalme mwenyewe alikaa kimya, uso umembadilika.
Gagula tu hakunyamaza, akasema, ‘Giza litapita, nimeyaona kama haya zamani; hapana mtu anayeweza kuzima mwangaza wa mwezi; msiogope; mkae kimya na giza litapita.’


Nikasema, ‘Ngojeni mtaona. Ee Mwezi!Mwezi! Mwezi!’ na sisi wote watatu tukazidi kusema maneno ya ovyo ovyo tu! na kwa muda wa dakika kumi tukaendelea hivyo hivyo.

Giza likazidi, na watu wote walikodoa macho yao kutazama juu, na walikaa kimya kabisa. Sasa dunia ikaanza kujaa vivuli vya ajabu, na kila kitu kilikuwa kimya kama mauti.

Wakati ulipita na pamoja giza likazidi kushika mwezi. Ikawa ajabu mno, maana kwanza ikawa kama mwezi unakaribia dunia na kuzidi kuwa mkubwa.

Sasa uligeuka rangi ukawa mwekundu kama damu, na halafu tuliona alama zile zilizo katika mwezi zinang’aa katika wekundu wake.

Pole pole giza likatambaa; sasa limefika nusu ya ule wekundu kama damu. Likazidi kuenea hata hatukuweza kuona sura za watu waliokuwa karibu. Sasa kila mtu alikuwa kimya kabisa, nasi hatukusema neno.


Mara Yule kijana Skraga alilia kwa hofu, ‘Mwezi unakufa. Wachawi weupe hawa wameuwa mwezi. Tutaangamia katika giza.’ Naye alishikwa na wazimu kwa hofu akainua mkuki wake akampiga Bwana Henry kwa nguvu zake zote.

Lakini alikuwa amesahau habari za nguo zile za chuma alizotupa mfalme, na mkuki ukapinduka bila kuzipenya.


Kabla hajapata nafasi kupiga tena, Bwana Henry akashika ule mkuki akampiga kifuani. Skraga akaanguka maiti! Basi watu walipoona hivyo, na kwa sababu ya hofu waliyokuwa nayo kufikiri kuwa mwezi unakufa, wakaanza kutawanyika, wakapiga mbio na kulia.


Na hata mfalme na walinzi wake na Gagula wakaondoka mbio wakakimbilia majumbani, na baada ya dakika chache tukajiona tupo peke yetu pamoja na Foulata, Yule mwanamwali tuliyemwokoa, na Infadus, na wakubwa wengine waliotujia usiku, na maiti ya Skraga mwana wa mfalme.


Nikasema, ‘Wakubwa, tumewaonyesha ishara mliyotaka. Kama mmeridhika, basi twendeni upesi mahali mlipotaja. Hatuwezi sasa kukomesha kitendo chetu.

Giza litaendelea kwa muda wa saa moja na nusu. Haya, na tujifiche kwa giza hili.’
Infadus akasema, ‘Twendeni.’ Akageuka akaenda, na wakubwa wale walimfuata, na sisi na yule mwanamwali tulifuatana nao.


Kabla hatujalifia lango la mji, mwezi uliliwa kabisa na nyota nyingi zikaonekana katika mbingu nyeusi. Tukashikana mikono tukajikokota katika giza.
 
SURA YA KUMI NA MBILI


Ilikuwa bahati yetu kuwa Infadus na wakubwa wale walivijua vema vinjia katika mji, na kwa hivyo ingawa ilikuwa giza tuliweza kwenda upesi.

Kwa muda wa saa moja hivi tulikwenda, mpaka mwezi ulianza kutoa mwangaza wake tena.

Tukautazama na mara tuliona mshale wa nuru unatoka na kuangaza, na baada ya dakika tano nyota zikaanza kutoweka tena na mwangaza ulitosha kutuwezesha kuona mahali tulipo.

Tukajiona kuwa tumekwisha toka mjini na sasa tunakaribia kilima ambacho juu yake ni sawa sawa kama meza. Kilikwenda juu yapata futi mia mbili hivi, na juu yake palikuwa na nafasi kwa kambi la skari wengi sana.

Tukaambiwa kuwa kwa kawaida vikosi vitatu vinafanya kambi hapa, lakini nafasi iliyopo inatosha kwa vikosi vingine pia. Tukakipanda kilima, tukaona kuwa vikosi vingine vipo tayari.

Tukaona watu wamesongana, wameamshwa katika usingizi na sasa wanatetemeka kwa hofu. Tukapita katikati bila kusema neno, tukafika kwenye nyumba moja, na hapa tulistaajabu, maana watu wawili walikuwa wakitungojea wamekisha leta vitu tulivyoviacha tulipotoka mjini.


Infadus akasema, ‘Mimi nilipeleka watu wavichukue, na hata hivi vile vile.’ Akamwonyesha Bwana Good suruali yake.

Bwana Good akacheka sana na katika furaha yake akashika suruali yake akaivaa pale pale.

Infadus alijaribu kumshauri asiivae na kuficha miguu yake, lakini Bwana Good hakukubali.

Basi Infadus alitwambia kuwa ameamuru vikosi vikusanyike jua likitoka tu ili awaeleza askari sababu ya kumwasi mfalme na kuwaonyesha mfalme wao wa haki, Ignosi.

Basi jua lilipochomoza wakakusanyika watu wapatao ishirini elfu walio bora katika askari wa Kukuana, wakajipanga katika kiwanja kikubwa; tukaenda kuwatazama.

Sasa Infadus akawaita wakubwa na baada ya kukaa kimya kidogo akaanza kueleza habari zote, naye alikuwa msemaji hodari. Alieleza habari za baba yake Ignosi na namna alivyouawa bila haki na Twala aliye mfalme wa sasa, na namna mke wake na mtoto wake walivyofukuzwa, wafe kwa njaa.


Kisha akaeleza kuwa watu weupe waliotoka katika nyota waliitazama nchi hii kutoka kwao juu wakaona dhuluma na taabu zilizopo, basi wakaja kwa taabu nyingi wapate kuwasaidia watu wa nchi; na ya kuwa walimshika Ignosi mfalme wa haki wa Wakukuana wakamwongoza kutoka nchi ngeni alipokuwako na kumleta kuvuka milima.


Tena akaeleza kuwa walikuwa wamekwisha ona vitendo viovu vya Twala na kwa hivyo waliwaonyesha ishara wale wasiosadiki, wakamwokoa Yule mwanamwali, wakazima mwangaza wa mwezi na kumuua Skraga; na sasa wapo tayari kutusaidia katika vita vya kumwondoa Twala na kumweka Ignosi, aliye mfalme wa haki, katika mahali pake.


Infadus alipomaliza kusema maneno yake, Ignosi, akasimama mbele, na baada ya kusema tena yote aliyosema Infadus mjomba wake, akasema, ‘Ee wakubwa, askari, na watu wote, mmesikia maneno yangu.


Sasa lazima mchague baina ya mimi na yeye anayekaa sasa katika kiti cha enzi, Yule mjomba wangu aliyemuua ndugu yake akamfukuza mtoto wa ndugu yake ili afe katika baridi ya usiku.

Ni kweli kuwa mimi ni mfalme wa kweli, na hawa wakubwa wanaweza kuwaambieni kuwa wamekwisha ona nyoka aliyechanjwa kiunoni mwangu.
 
Kama mimi si mfalme, je, watu weupe hawa wangetetea upande wangu kwa nguvu za uwezo wao?

Msitetemeke, wakubwa na askari na watu wote! Lile giza mliloona usiku ambalo, lililetwa kusudi kumfadhaisha Twala, mmekwisha kulisahau?

Si liko mbele ya macho yenu hata sasa? Mimi ni mfalme.’ Akasimama akajinyosha akainua shoka lake la vita juu kichwani, akasema, ‘Kama yupo mtu mmoja asiyekubali,
Basi atoke mbele nami nitapigana naye sasa na damu yake itakuwa dalili ya kuwa nisemayo ni kweli.’

Akatikisa shoka likang’aa katika mwangaza wa jua. Lakini hapana mtu aliyetoka mbele, akaendelea tena akasema, ‘Mimi ni mfalme wa kweli, na wote watakaosimama upande wangu watafuatana nami kwa heshima na fahari kama tukishinda.

Nitawapa ng’ombe na wanawake, nanyi mtakuwa wa kwanza katika vikosi vyote; na ikiwa tutashindwa, basi na mimi nitashindwa pamoja nanyi.

Na tazameni, nitatoa ahadi ya kuwa nikiisha kukaa juu ya kiti cha enzi cha babu zangu, kumwaga damu ya bure kutakoma.

Watambuzi wa wachawi hawatatafuta tena watu na kuwaua. Hapana mtu atakayeuawa ila atakayekosa sheri zetu.

Miji na nyumba zenu hazitaingiliwa tena, na kila mtu atalala salama katika nyumba yake bila hofu, na haki itazagaa katika nchi yetu yote.

Je, mmekwisha kuchagua nyinyi wakubwa na askari na watu wote?
Wakaitikia, ‘Tumechagua, Ee mfalme.’

Akajibu, ‘Vema. Geukeni mtazame matarishi wa Twala wanavyotawanyika kwenda mashariki na magharibi na kaskazini na kusini ili kukusanya jeshi kubwa wapate kuniua mimi na nyinyi na hawa rafiki zangu na walinzi wangu.

Kesho au labda kesho kutwa atakuja pamoja na watu wake wote kupigana nasi. Ndipo nitakapoona kweli walio watu wangu, watu wale wasio na hofu kufa kwa ajili ya yale wanayoamini; nami nakwambieni ya kuwa hamtasahauliwa katika wakati wa ngawira.

Wakubwa na askari na watu wote sasa nendeni nyumbani mkajitayarishe kwa vita.’
Basi ikawa kimya mpaka mmoja wa wakubwa wale akainua mikono yake akaita neno lile la kumwamkia mfalme, ‘Koom,’ ikawa ishara ya kuwa askari wamemkubali Ignosi kuwa mfalme wao. Wakatoka kwa taratibu za kiaskari, wakaenda zao.

Baada ya nusu saa tukafanya mkutano wa vita na wakubwa wote wakahudhuria. Ikawa dhairi kuwa kabla ya kupita muda mwingi tutashambuliwa na askari wengi kupita hesabu tuliyo nayo. Maana tuliona majeshi ya askari wanakuja kutoka kila mahali, na matarishi wa mfalme wanakwenda pote.

Kwa upande wetu tulikuwa na askari kadiri ya ishirini elfu wa katika vikosi saba vilivyo hodari katika nchi.

Infadus aliniambia kuwa Twala atakuwa na askari kadiri ya thelathini au thelathini na tano elfu, akasema kuwa watakuwepo Loo tayari, na kabla ya kufika saa sita kesho ataweza kuhudhurisha elfu tano zaidi.

Ilikuwa dhahiri kuwa lazima tujiweke tayari tuwezavyo kufanya vita, maana wao walikuwa wakijiweka tayari, na hata sasa makundi ya askari walikuwa wakizunguka kilima kwa chini, na dalili nyinginezo za vita zilionekana.
 
Basi tulianza kufanya imara mahali petu jinsi tulivyoweza. Kila mtu alifanya kazi nyingi sana.

Vinjia vyote vya kupandia kilima tuliviziba kwa chungu za mawe, tukakusanya chungu za mawe makubwa sana tayari kuyaangushia adui wakijaribu kupanda kilima.

Jua lilipokaribia kushuka tulipumzika kidogo tukaona kundi dogo la watu wanatujia kutoka mji wa Loo na mmoja alikuwa amechukua jani mkononi ili iwe dalili ya kutufahamisha kuwa yeye ni tarishi aliyetumwa.

Alipokaribia Ignosi na Infadus na wakubwa wawili watatu walishuka kumlaki. Tarishi huyo alikuwa mtu mkubwa shujaa, amevaa ngozi ya chui. Alipofika karibu alisema, ‘Salamu za mfalme kwa wale wanaompiga vita. Salamu za simba kwa wale fisi wanaovitafuna visigino vyake.’

Nikasema, ‘Haya sema utakayo.’ Akaendelea, ‘Haya ni maneno ya mfalme; mjitoe katika mikono ya mfalme kabla hamjapatwa na maafa. Bega la fahali mweusi limekwisha pasuliwa, na mfalme anamtembeza kambini huku linatoka damu.’ (Desturi hii inafuatwa katika makabila mengine ya Afrika ikiwa ni mwanzo wa vita au mwanzo wa jambo kubwa jingine).

Nikamuuliza, ‘Je, na mapatano ya mfalme yatakuwaje.?’ Akajibu, ‘Mapatano ya mfalme ni ya huruma na rehema, yaliyo stahili mfalme Twala.

Haya ndiyo maneno ya Twala, Mwenye chongo, Mume wa wake elfu, Bwana wa Wakukuana, Mlinzi wa Njia Kuu, Mpenzi wa Wale Watatu wakaao kimya juu ya milima ile, Ndama wa Ng’ombe Mweusi, Ndovu ambaye akikanyaga nchi ardhi hutetemeka.


Kitisho cha watenda maovu, Mbuni ambaye miguu yake hula jangwa, Mkubwa, Mweusi, Mwenye busara, Mfalme kutoka karne hata karne!

Haya ndiyo maneno ya mfalme Twala: Nitakuonyesheni rehema, nitaridhika kwa damu kidogo tu.

Mmoja katika kila kumi atakufa, wengine watapata msamaha; lakini Yule mtu mweupe aliyemuua Skraga, Yule mtu mweusi mtumishi wake anayejidai mfalme, na Infadus ndugu yangu anayefitinisha watu wangu, hawa watakufa kwa maumivu na mateso, wawe sadaka ya Wale Watatu wakaao kimya. Haya ndiyo maneno ya huruma ya Twala.’

Basi nikazungumza kidogo na wenzangu, kisha nikasema, kwa sauti kubwa ili wale askari wote wasikie, nikasema. ‘Rudi kwa Twala, wewe mbwa, rudi kwa aliyekuleta, ukamwambie kuwa:

Sisi,na Ignosi mfalme wa kweli wa Wakukuana, na sisi watu weupe wenye hekima tuliotoka katika nyota, tutiao mwezi giza, na Infadus wa ukoo wa ufalme, na Wakubwa na askari na watu waliokusanyika hapa tunampa jawabu na kusema: hatutajitoa kabisa katika mikono ya Twala; na kabla jua halijashuka mara mbili, Twala atalala maiti mkavu mbele ya mlango wake wa ikulu, na Ignosi, ambaye baba yake aliuawa na Twala, atatawala katika mahali pake! Sasa nenda, tusije tukakufukuza kwa mijeledi, nawe uangalie sana usiinue mkono wako kupigana na watu kama sisi.’


Yule tarishi akacheka akasema, ‘Huwezi kunitisha kwa maneno makubwa yanayovuma sana. Mjionyeshe kuwa mashujaa kesho, nyinyi mnaotia giza mwezi. Muwe mashujaa, mpigane kwa furaha kabla kunguru hajachambueni nyama mbali na mifupa yenu, mpaka ikawa meupe kuliko sura zenu zilivyo.


Kwaherini; labda tutaonana tena vitani, nawaombeni msiruke kwenda juu katika nyota tena bila ya kuningojea mimi.’

Basi alipokwisha kusema maneno hayo ya kutudharau, akatoka akaenda zake, na punde jua lilishuka. Usiku ule tulikuwa na kazi nyingi, maana ingawa tulichoka mno ikawa lazima kutengeneza vitu vyote tayari kadiri tulivyoweza tusiache jambo hata moja, na matarishi walikuwa wakija na kutoka mahali petu pa mashauri.


Basi yapata saa tano usiku, mambo yote tuliyoweza kuyatengeneza yalikwisha kuwa tayari, na kambi ikawa kimya kabisa ila kwa sauti za watu ‘Yaliokuwa wakishika zamu.


Mimi na Bwana Henry tukashuka kilimani pamoja na Ignosi na mkubwa mmoja tukazunguka kila mahali pa mbele penye mlinzi, tukaona kuwa wote wapo macho. Kisha tukarudi tena tukipita katikati ya askari maelfu waliolala usingizi ambao wengi wanalala usingizi wa mwisho duniani.

Nikamwambia Bwana Henry, ‘Mimi nimo katika hali ya woga kabisa. Mimi nafikiri kuwa hapana mmoja katika sisi atakayekuwa mzima usiku wa kesho. Tunashambuliwa na askari wengi kabisa kupita askari wetu.’

Bwana Henry akasema, ‘Tutafanya jitihada. Tutaonyesha ushujaa wetu lakini mambo haya ni makubwa mno, na kweli si haki yetu kuingia katika shughuli hii, lakini tumekubali na kwa hivyo lazima tufanye tuwezavyo.

Mwenyewe nimechagua kufa katika vita kuliko kufa kwa namna nyingine, na sasa nimeona kuwa hatuwezi kumwona ndugu yangu tena, basi kufa kwangu si kugumu.

Lakini kila mara hutokea kuwa mashujaa wana bahati, na labda tutawashinda. Liwalo naliwe lakini vita vitakuwa vikali nasi lazima tuwe katikati kabisa ya vita.’

Alisema maneno haya kwa sauti ya huzuni kabisa, lakini niliona macho yake yaking’aa sana nikatambua kuwa Bwana Henry kwa kweli alipenda vita.

Baada ya haya tulilala usingizi muda wa saa mbili. Ilipokuwa karibu na mapambazuko tuliamshwa na Infadus aliyekuja kutuarifu kuwa kwa upande wa mji wa Loo kuna shughuli nyingi, naya kuwa askari wengine wa Twala wanawafukuza askari wetu waliowekwa mahali pa mbele kulinda.

Tukaondoka tukavaa tayari kwa vita, tukavaa zile nguo za chuma ndani ya nguo zetu za kila siku, tukashukuru sana kuwa nazo.

Tulipokwisha kuvaa tulikula kwa haraka tukatoka kutazama mambo yanavyoendelea. Mahali pamoja juu kilimani palikuwa mwamba mkubwa, tukafanya kuwa ngome yetu na mahali pa kutazamia chini pote.

Hapa tuliona Infadus amezungukwa na kikosi chake kilichoitwa Wajivu, na bila shaka askari hao walikuwa bora kupita wote katika jeshi la Wakukuana.

Kikosi hicho kilikuwa na askari elfu tatu na mia tano, nacho kiliwekwa hapa kuwa kama akiba, na askari walikuwa wamelala chini wakitazama askari wa Twala wakitoka mji wa Loo, wakitambaa kama siafu.

Ilikuwa kama kwamba mistari hiyo ya askari wa Twala haina mwisho, nayo ilikuwa mistari mitatu na kila mstari ulikuwa na askari kadiri ya elfu mbili.


Walipokwisha toka mjini walijipanga. Jeshi moja likachagua njia ya kulia, na jingine njia ya kushoto, na jingine njia ya katikati.

Basi Infadus akasema, ‘Ah! Watatushambulia kutokea pande tatu kwa mara moja.’
Hii ilikuwa habari mbaya, maana mahali petu pa juu ya kilima palikuwa kama duara na urefu wa duara ile ulikuwa hadiri ya mwendo wa saa nne, na kwa kuwa eneo lake lilikuwa refu na askari wetu ni wachache, ikawa lazima tusongane kadiri tulivyoweza.


Lakini kwa kuwa hatukuweza kutambua hasa namna watakavyo tushambulia ikawa lazima tufanye tuwezavyo, tukapeleka habari kwa vikosi vyote kila mtu awe tayari kujitetea katika mashambulio.
 
SURA YA KUMI NA TATU

Pole pole bila haraka, majeshi yale matatu yalitambaa kutujia.

Walipofika karibu kadiri ya mwendo wa hatua mia sita, jeshi lile la katikati lilisimama chini ya kilima kungojea majeshi yale mawili mengine yatuzunguke mfano wa duara. Yaani walikusudia kutushambulia kutoka mahali patatu kwa mara moja.


Bwana Good akasema, ‘Laiti ningekuwa na bomu ningelifuta eneo lote hili katika muda wa dakika ishirini.’ Bwana Henry akajibu, ‘Kweli, lakini hatuna bomu, basi ya nini kulililia!

Wewe, Quatermain, afadhali ujaribu kumpiga Yule mtu mrefu, nadhani ndiye mkubwa wao.’

Basi nilitwa bunduki yangu, nikangoja hata Yule mtu amejitenga na watu wake akawa pamoja na mtumishi wake tu; nikalala nikaegemeza bunduki juu ya mwamba nikapiga, nikitumai kumpiga kifuani.


Lakini moshi ulipo inuka nilimwona amesimama salama ila mtumishi wake amelala amekwisha kufa. Basi Yule mkubwa mara akastuka akawakimbilia wenzake. Bwana Good akasema,’Una shabaha, bwana! Umewatisha sana.’


Basi nilichukizwa, maana sipendi kukosa shabaha mbele za watu, nikainua bunduki tena, nikaelekeza kwa Yule mkubwa tena, nikapiga. Mara akatupa juu mikono yake akaanguka kifudifudi.

Askari wetu walivyo ona hivyo walipiga makelele ya furaha, maana walifanya kama ni ishara njema kubashiri kwamba tutashinda, na jeshi lile la mkubwa Yule aliyeuawa wakarudi nyuma wamefadhaika.

Sasa Bwana Henry na Bwana Good wakatwaa bunduki zao wakaanza kupiga na kwa kadiri tulivyoona nadhani tuliua askari sita au wanane kabla hawajatoka katika eneo la bunduki zetu.

Mara tulipoacha kupiga tulisikia makelele makubwa yanatoka upande wa kushoto, na mara tukasikia makelele yanatoka upande wa kulia vile vile, tukajua kuwa majeshi yale mawili mengine yanatushambulia.

Wale adui waliokuwa mbele yetu walitawanyika kidogo waliposikia makelele hayo wakashika njia ya kuja kilimani, wakienda mbio kidogo na huku wakiimba kwa sauti ya kiume naya mkazo.

Tulipiga bunduki zetu kwa taratibu wakati walipokuwa wakija, na Ignosi vile vile akapiga bunduki mara kwa mara, tukawaua wengine.

Lakini hatukuweza kuwazuiya, ikawa kama; mtu apigaye bahari kujaribu kuzuia mawimbi.

Walizidi kuja na huku wanapiga kelele na kufanya vishindo kwa mikuki yao; sasa walikuwa wakiwafukuza watu wetu tuliowaweka mbele katika miamba chini ya kilima huku wakipanda pole pole wasije wakachoka.

Safu ya kwanza ya watu wetu wa mbele iliwekwa katikati ya kilima, na safu ya pili ilikuwa nyuma yao kadiri ya hatua sitini, na safu ya tatu ilikuwa katika ukingo wa kilima kwa juu.

Wakazidi kuja mbele wakiitana kilio chao cha vita, ‘Twala!Twala!Twala! Pigeni! Pigeni!’
Na watu wetu wakaitika, Ignosi!Ignosi! Pigeni! Pigeni!’

Wakawa karibu sasa, wakaanza kutupiana visu, vikameremeta nyuma na mbele, na mara kwa kelele kubwa, wakakutana.

Huku na huku mashujaa walipambana wakapigana, na watu wakaanguka kama majani ya miti wakati wa kiangazi; lakini kwa haraka nguvu za wale adui waliokuwa wakitushambulia zilisukuma nyuma safu yetu ya kwanza mpaka walikutana na safu ya pili.
 
Hapo vita vilikuwa vikali sana, lakini tena watu wetu walisukumwa nyuma, mpaka baada ya dakika ishirini tu toka mwanzo wa vita, safu yetu ya tatu ilikuwa katika vita.

Lakini sasa adui zetu walikuwa wamechoka, na tena wamepata hasara kubwa ya watu waliouawa na waliopata majeraha, nao hawakuweza kuvunja ukuta ule wa mikuki ya safu yetu ya tatu. Kwa muda kidogo askari wote wakapambana huku na huko katika vita, na mwisho wake hautambulikana.
Bwana Henry akatazama vita huku macho yake yaking’aa, ndipo alipojitosa katikati ya vita bila kusema neno, na Bwana Good akamfuata.

Mimi nilikaa pale pale . Askari walimwona Bwana Henry akiingia vitani wakaanza kuitana, ‘Ndovu ameingia! Pigeni!Pigeni!’

Kutoka hapo mwisho wa vita ulijulikana. Wale waliokuwa wakishambulia walisukumwa nyuma hatua kwa hatua kushuka kilima mpaka wakawakimbilia wale waliowekwa nyuma kuwasaidia, huku wamefadhaika sana.

Na mara tarishi alifika kutuarifu kuwa jeshi lile lililoshambulia kwa upande wa kushoto vile vile limesukumwa nyuma.

Nilianza kufurahi na kufikiri kuwa tumeshinda, kumbe, tukaona watu wetu wa upande wa kulia wanafukuzwa, nao wanatujia kwa kasi wakisukumwa nyuma na adui, ikawa kama maadui wameshinda upande huo.

Ignosi aliyekuwa kasimama karibu nami, alitambaua hali ya mambo ilivyo mara moja, akatoa amri upesi sana.

Mara vikosi vya Wajivu, waliokuwa wamewekwa kama akiba, vikajipanga. Ignosi akatoa amri nyingine na mara nikajiona nimo katikati ya vita vikali kuwashambulia maadui wanaotujia.nilijificha nyuma ya mwili mkubwa wa Ignosi kadiri nilivyoweza, nikafuata.

Katika muda kidogo tulikuwa tukipita kwa nguvu katikati ya askari wetu waliokuwa wakikimbia, nao mara walijipa moyo wakajipanga tena nyuma yetu, na hapo sijui nini kilichotokea.

Ninachoweza kukumbuka ni kusikia kelele kubwa na kuona jitu kubwa sana mbele ya macho yangu, linanijia na mkuki wake juu umetapakaa damu.

Lakini nilikuwa tayari, maana nilitambua kuwa nikisimama tu lazima nitauawa, basi nilijitupa chini kwa ghafla, na kwa kuwa alikuwa akija kwa nguvu hakuweza kujizuiya, akajikwaa akaanguka.

Kabla hajaweza kuondoka tena nilikuwa nimekwisha nyanyuka na nikampiga kwa bastola yangu.

Baada ya kitambo kidogo niliangushwa na mtu nikawa sina habari tena ya shambulio hilo. Nilipoteza fahamu tena nilijiona nimelala kilimani tena na Bwanab Good ameniinamia akininyunyuzia maji, akaniuliza, ‘Je, rafiki, sasa waonaje?’ Nikanyanyuka nikajipapasa kabla ya kumjibu, nikasema, ‘Sasa naona nafuu.’

Akasema, ‘Alhamdulilahi! Nilipoona wanakuchukua nilijiskia uchungu sana; nilifikiri kuwa umekwisha kufa.’ Nikamuuliza vita vimekwendaje, akaniambia, ‘Maadui wamesukumwa nyuma kila mahali.

Lakini hasara ni kubwa mno. Watu wa upande wetu waliokufa na kujeruhiwa wapata elfu mbili, na kwa upande wao nadhani hawapungui elfu tatu. Tazama huko!

Nikatazama nikaona mistari mirefu ya watu wanakuja wanne pamoja. Nikaona kuwa wale waliojeruhiwa wamechukuliwa katika machela.
 
Basi tuliondoka hapo kwa haraka tukapita upande wa pili wa kilima, tukamwona Bwana Henry ameshika shoka lake la vita mkononi, na Ignosi na Infadus na wakubwa wachache wengine wanasemezana na kushauriana.


Bwana Henry akasema, ‘Ah, nimefurahi umekuja. Ignosi anataka kufanya mambo nami sifahamu maneno yake.

Nadhani kuwa ingawa tumekwisha kuwashinda maadui kwa sasa, lakini askari wengine wengi wanaletwa kumsaidia Twala, naye anadhani anawaweka watuzunguke ili tusipate chakula, na Infadus anasema kuwa maji yetu yapo karibuni kuisha.’


Infadus akasema, ‘Ndiyo, kweli. Chemchem haitoki maji ya kutosha watu wengi, na sasa yanapungua. Kabla ya kuingia usiku, wote tutaona kiu. Sikiliza, Makumazahn, wewe ndiye mwenye akili, pengine umeona vita vingi katika nchi nyingine, yaani ikiwa wanafanya vita katika nyota.

Twambie tufanye nini? Twala ameleta watu wengi kuchukua mahali pa wale waliokufa. Twala amekwisha pata akili.

Mwewe hakufikiri kukuta kuku tayari! Lakini tumekwisha muuma kifua; ana hofu kutupiga tena. Lakini hata na sisi tumejeruhiwa naye atangoja hapo mpaka tufe; atatuzunguka kama anavyofanya chatu anapokamata swala. Naye atapigana vita vya kusubiri tu.’
Nikasema, ‘Vema nimekusikia.’


Basi akaendelea, akasema, ‘Basi Makumazahn, waona sisi hapa hatuna maji, na chakula tulichonacho ni kidogo tu, nasi lazima tuchague kukaa na kufa kama simba anayekufa katika pango lake kwa njaa, au kujaribu kutoka kwa njia ya kaskazini au tumrukie Twala na kumshambulia kwa nguvu zetu zote.


Ndovu (yaani Bwana Henry ) ni shujaa, maana leo amepigana kama nyati aliyetegwa, na askari wa Twala walianguka mbele yake kama mtama mchanga unaopigwa na mvua yam awe; yeye asema ni afadhali tuwarukie; lakini ni desturi ya ndovu kushambulia.


Je, wewe Makumazahn, wasemaje? Wewe sungura mwerevu aliyekwisha ona mambo mengi na kupenda kumumiza adui kutoka kwa nyuma. Shauri la mwisho ni Ignosi aliye mfalme, maana ni hiari ya mfalme kupigana vita, lakini na tusikilize shauri lako, Ee Makumazahn.

Na vile tusikilize shauri la Bougwan, yeye mwenye jicho linalong’aa’. (Maana hilo ni jina walilomwita Bwana Good.)

Nikamuuliza Ignosi, ‘Je, Ignosi, wasemaje?’ lakini yeye, ambaye alikuwa mtumishi wetu lakini sasa amevaa kiaskari na kuonekana kuwa mfalme kabisa, akajibu, ‘Hapana, tafadhali wewe sema, nami niliye mtoto tu kwako kwa akili zangu, nitasikiliza maneno yako.’


Basi kuombwa hivyo, nikashauriana na Bwana Henry na Bwana Good, kisha nikawapa kauli yangu. Ikawa ya kuwa sisi tumekwisha tiwa mtegoni, na tena maji yanatupungukia, ni afadhali tuwashambulie askari wa Twala.


Tena nikashauri kuwa yafaa kuanza shambulio mara moja kabla ya kukauka majeraha yetu, na tena kabla askari wetu hawajakata tamaa kwa kuona wingi wa askari wa Twala.

Nikasema kuwa tukingoja, huenda wakubwa wengine wa upande wetu wakaghairi na kwenda kufanya suluhu na Twala, na hata kututia katika mikono yake.

Basi kauli yangu ikapokewa kwa furaha; na Wakukuana walipendezwa sana na shauri langu. Lakini neno la mwisho likawa kwa Ignosi aliye mfalme, tukamgeukia tusikilize asemavyo.

Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu kidogo akifikiri , alisema, ‘Rafiki zangu watu weupe; na Infadus mjomba wangu, na wakubwa wangu; nimekaza moyo wangu. Nitampiga Twala leo hivi na kubahatisha nguvu zetu.


Sikilizeni, hivi ndivyo namna nitakavyowapiga. Sasa ni saa sita na watu wote wanakula na kupumzika baada ya vita. Baadaye kidogo jua linapoanza kushuka, wewe mjomba wangu pamoja na jeshi lako uende pamoja na jeshi lingine hata pale penye mteremko, na mara Twala atakapowaoneni ataleta jeshi lake kupigana.


Lakini njia hii nyembamba na kwa hivyo jeshi linaweza kuja kikosi kikosi; na kwa hivyo wataangamizwa kikosi kikosi, na macho ya askari wote wa Twala yatakuwa yanatazama vita hivi vikali.

Na rafiki yangu Ndovu (yaani Bwana Henry) atafuatana nawe, na Twala akiona shoka lake kubwa linang’aa na kumeremeta katika safu ya kwanza ya Wajivu, moyo wake utafifia.


Mimi nitafuatana na jeshi la pili litakalokufuata wewe, yaani, ikiwa wewe utaangamizwa , basi mfalme atabaki, na watu watapigana kwa ajili yake. Na Makumazahn ataandamana pamoja na mimi.’

Infadus akasema, ‘Vema, Ewe Mfalme.’ Ignosi akaendelea tena akasema, ‘Na hapo askari wote wa Twala wanapotazama vita vikali, nataka jeshi la tatu lililobaki ligawanyike sehemu tatu.

Sehemu moja itatambaa kwenda kwa upande wa kushoto wa adui na kuwarukia, na sehemu ya pili watatambaa kwenda upande wa kulia, nami nikiona kuwa askari wa pande zote mbili wako tayari kuwarukia watu wa Twala, basi mimi nitashambulia kwa katikati, na tukiwa na bahati, tutashinda.


Nasi kabla jua halijashuka kabisa tutakuwa tumekaa kwa amani na raha katika mji wa Loo.

Na sasa tule tujiweke tayari, na wewe, Infadus, utengeneze mambo yote tusije tukasahau hata kitu kimoja, na Bougwan (yaani Bwana Good) yeye na aandamane na wale watakaokwenda kwa upande wa kulia apate kuwatia wakubwa nguvu kwa jicho lake linalong’aa.’

Basi matengenezo hayo yote yakafuatwa kwa upesi sana, yakaonyesha ustadi wa uaskari wa Wakukuana. Katika muda wa saa moja, watu wote walikuwa wamekwisha kula na majeshi yaligawanyika tayari.

Baadaye kidogo Bwana Good akatujia mimi na Bwana Henry akasema, ‘Kwaherini, rafiki zangu. Mimi nakwenda kwa upande wa kulia, na sasa nimekuja ili tupeane mikono maana labda hatutaonana tena.’ Basi tukapeana mikono kwa kimya sana na uzuni.
 
SURA YA KUMI NA NNE

Baada ya kupita muda kidogo zile sehemu mbili zilizoamrishwa kwenda pande za kushoto na kulia za kilima zilikuwa zimekwisha kwenda kwa hadhari sana zisije kuonekana na wapelelezi wa Twala. Tukakaa kwa muda wa nusu saa ili kuwapa nafasi ya kufika mahali pao.


Ndipo jeshi lile liitwalo Wajivu na jeshi lile lingine lililoamrishwa kuandamana nalo, yaani lililoitwa Wanyati, yakaondoka.

Watu wa majeshi yote mawili walikuwa wazima kabisa na wenye nguvu, maana Wajivu hawakuingia katika vita mpaka mwisho walipowafukuza maadui, na wale Wanyati vile vile walikuwa wamewekwa nyuma katika vita asubuhi, na kwa hivyo hawakuingia katika vita.


Infadus alikuwa mkubwa wa askari wa zamani sana, naye alitambua sana faida ya kuwatia moyo watu wake, wakati wa shida; basi akatoa hotuba kwa maneno mazuri ya mashahiri ya vita, aka waeleza namna walivyopewa heshima kwa kuwekwa wa kwanza katika vita, na kwa kupewa Yule mtu weupe aliyetoka katika nyota afuatane nao.


Akaahidi kuwapa zawadi kubwa ya ng’ombe na kuwapandisha vyeo wote watakaotoka salama katika vita, ikiwa majeshi ya Ignosi yatashinda .


Kazi ya jeshi hili ilikuwa kupigana na kikosi baada ya kikosi cha askari wa Twala katika ile njia nyembamba chini mpaka waishe kuangamizwa kabisa, au mpaka wale waliozunguka wapate nafasi ya kuwarukia maadui.


Lakini hawakufadhaika hata kidogo wala sikuona dalili ya hofu katika sura zao. Walikuwa wakienda kukutana na mauti kwa hakika, walikuwa wakitoka katika nuru ya mchana kwa milele, nao walikuwa na nguvu za kwenda bila kutetemeka.


Basi Infadus alimaliza hotuba yake akasema, ‘Tazameni mfalme wenu! Nendeni mkapigane na kufa kwa ajili yake, maana huu ndio wajibu wa mashujaa wanaume, na yeye atakayeogoba kufa kwa ajili ya mfalme wake, na yeye atakayempa kisogo adui yake, na alaniwe na kufedheheshwa.


Nyinyi wakubwa na askari tazameni mfalme wenu! Sasa nyenyekeeni mbele ya nyoka mtukufu, mnifuate mimi na Ndovu (yaani Bwana Henry), nitawaonyesha njia mpaka tufike katika moyo wa majeshi ya Twala.’

Kwanza ikawa kimya kabisa kwa kiasi cha dakika moja, kisha sauti ikatoka askari waliposongana mbele yetu, ikawa kama sauti ya mawimbi ya bahari yakivuma kwa mbali, na ilikuwa sauti ya vishindo vya mikuki ikigongana na ngao.


Pole pole sauti ikazidi na kuzidi mpaka ikawa kama ngurumo inayozunguka katika milima, ikajaza hewa yote kwa mawimbi makubwa ya sauti.

Kisha ikapungua pole pole tena, ikapungua mpaka ikafa, ndipo wakapaaza sauti kuu ya kumwamkia mfalme.


Ignosi akapokea kuamkia kwao kwa kuinua juu shoka lake la vita, na Wajivu wakajipanga wakatoka kwa taratibu ya watatu watatu, na kila mstari ulikuwa na askari elfu moja, wakubwa wao mbali.

Walipokuwa wamekwisha kwenda hatua mia sita, Ignosi akajiweka mbele ya Wanyati nao wakajipanga hivyo hivyo wakatoka, nami niliandamana nao.


Tulipofika ukingo wa kilima, Wajivu walikuwa wamekwisha teremka nusu ya kilima, nao wanakaribia ile njia nyembamba. Watu wa kambi la Twala sasa wakaanza kushughulika sana, na kikosi baada ya kikosi wakaja mbio wapate kufikia ile njia kabla Wajivu hawajawahi.


Wajivu walipokwisha kufika kwenye mahali palipokuwa papana kidogo, wakasimama kimya, nasi, yaani Wanyati, tulisimama nyuma yao kadiri ya hatua mia moja tuwe tayari kuwasaidia.


Sasa tulipata nafasi kutazama jeshi la Twala, tukaona kuwa hawajapata wengine wa kuwasaidia tangu vita vya asubuhi.


Askari wa Twala walipofika karibu na kupanda kwenye njia ile nyembamba, wakasita, maana waliona kuwa kikosi kimoja tu kinaweza kupita kwa mara moja, na tena waliona Wajivu mashujaa na watukufu wa majeshi yote ya Wakukuana wamesimama juu ya miamba isiyopitika wanangoja tayari kuwazuia.


Kwanza walisita, kisha wakasimama; hawakuwa na moyo wa kuonana na kupigana na Wajivu waliosimama thabiti hivi.

Lakini mkubwa mmoja akatoka amevaa manyoya marefu ya mavazi ya mkubwa wa jeshi, amefuatana na wakubwa wengine na watumishi, nikamdhania kuwa ndiye Twala mwenyewe.
 
Akatoa amri, na kikosi cha kwanza wakatoa sauti kubwa wakawashambulia Wajivu, na wao walisimama kimya tayari kuwapokea mpaka walipofika karibu kadiri ya hatua arobaini wakaanza kutupiana visu vyao vikubwa.


Ndipo wakawarukia kwa kishindo kikubwa huku mikuki juu, na majeshi wakaonana na kupigana vita vya kufa, Mara kishindo cha ngao zikigongana kilikuwa kama ngurumo , na uwanda wote ukameremeta kwa mianga ya nuru iliyotoka mikuki iliyong’aa.

Huku na huku wakapambana, wakachomana chomana mikuki yao, lakini si kwa muda mrefu.

Pole pole ikawa kama wale wanaoshambulia wanapungua, ndipo kwa jitihada kuu Wajivu wakawakanyaga kama wimbi kubwa linavyopanda juu ya mwamba baharini.

Kikosi kile kiliangamizwa kabisa, lakini katika Wajivu, mistari miwili tu ilibaki, mmoja umekwisha, yaani theluthi ya kikosi iliangamizwa.


Basi wakajipanga tena wakasongana pamoja, na tena walisimama kimya wakangojea adui kushambulia. Huku nyuma sisi tulijongea mbele tukasimama juu ya mahali walipokuwa wamekwisha pigana, ikawa pamefunikwa kwa watu elfu nne, wengine maiti, wengine wanakufa, na wengine wamejeruhiwa, na ardhi ikawa nyekufundu kwa damu.


Igosi akatoa amri kuwa wale maadui waliojeruhiwa wasiuawe kabisa, na kwa kadiri nilivyoona, watu wakafuatana amri hiyo. Lakini sasa kikosi kingine kikaja, na watu wake walivaa manyoya meupe na ngozi nyeupe, wakawa na ngao nyeupe.


Wakaja kushambulia wale Wajivu elfu mbili waliosalia, nao wakasimama kimya kabisa mpaka maadui walipofika karibu kadiri ya hatua arobaini, ndipo walipojitupa kwa nguvu zisisowezekana kuzuiwa.

Tukasikia tena kishindo kile cha ngao zao, na tena tukaona mambo yale yale. Lakini sasa mambo hayakuisha upesi sana, maana wale adui walikuwa vijana, wakapigana kwa ukali mno, na kwanza ikawa kama watashinda na kuwasukuma nyuma Wajivu.

Mauaji yalikuwa mengi mno, na mamia walianguka kila dakika, na katika vilio na kuugua kwa wale wanaokufa na waliojeruhiwa na vishindo vya mikuki kugongana na ngao, tulisikia sauti ya ‘S’gee!S’gee!’ Hii ndiyo sauti aliyofanya kila mtu alipomchoma mkuki adui yake.

Lakini utii mkamilifu na ushujaa usiobadilika huleta miujiza, maana tulipodhani kuwa Wajivu tayari wameshindwa sisi tukajiweka tayari kuingia katika mahali pao, nikasikia sauti kubwa ya Bwana Henry akiita katika vita, nikaona shoka lake juu.

Ndipo tulipoona mambo yanabadilika. Wajivu wakaacha kurudi nyuma, wakasimama imara kama mwamba, na mawimbi ya maadui yakawarukia tena na tena wasiweze kuwavunja ila walirudishwa nyuma kila mara.

Sasa Wajivu wakaanza kujongea tena, lakini sasa wakijongea mbele; na kwa kuwa hawana bunduki hapakuwa na moshi, kwa hivyo tuliweza kuona kila kitendo katika vita. Baada ya dakika moja, vita vikaanza kufifia tena.

Ignosi akaita, ‘Ah!Kweli hawa ndio wanaume; watashinda tena, tazama vita vimekwisha!
Mara adui walioshambulia walikimbia kama moshi kutoka kinywa cha mzinga, na manyoya meupe yao yalipeperuka katika upepo, wakawaacha Wajivu wameshinda kabisa.

Lakini hawakuwa jeshi tena. Katika mashujaa elfu tatu walioingia katika vita, mia sita tu walibaki, wametapakaa damu; wengine wameanguka chini.


Lakini hata hivyo wakapiga makelele kwa furaha na badala ya kurudi nyuma kama tulivyofikiri kuwa watafanya, waliaanza kuwafukuza adui wale wanaokimbi, na tena, Alhamdu-lilahil nilimwona Bwana Henry yu salama amesimama pamoja na rafiki yetu Infadus.

Tena majeshi ya Twala wakashambulia, na tena wakawa katikati ya vita. Sasa kwa mara ya kwanza katika maisha yangu niliona moyo wangu unatamani vita.

Nikageuka nikamuuliza Ignosi, ‘Je, tusimame hapa mpaka tuote mizizi? Mpaka Twala awameze ndugu zetu wote huko?’ Ignosi akajibu, ‘Hapana, Makumazahn, tazama, sasa wakati umewadia, twendeni!’


Alipokuwa akisema, jeshi lingine lilitoka kwa upande likaanza kushambulia kundi lile dogo, basi Ignosi akainua shoka lake la vita akatoa amri, na mara moja Wanyati waliruka mbele kama wimbi la bahari.

Yaliofuata mimi siweze kusimulia. Ninayo ya kumbuka ni haya: shambulio la nguvu lililotikisa nchi, kisha kishindo kikubwa, na makelele mengi ya watu, na mifululizo ya mikuki niliyoona katika ukungu uliokuwa mwekundu kamadamu.
 
Nilipopata fahamu tena nikajiona nimo katikati ya wale Wajivu waliobaki nimesimama nyuma ya Bwana Henry mwenyewe.

Sijui namna nilivyofika huko lakini baadaye Bwana Henry akanieleza kuwa nilichukuliwa kwa nguvu za shambulio la kwanza la Wanyati, nikaachiliwa huku waliporudiswa nyuma tena, naye akaruka, akanishika, akanivuta ndani.


Nani anaweza kusimulia habari za vita vilivyofuata? Adui walitushambulia tena na tena kama mawimbi ya bahari, na tena tuliwasukuma nyuma.

Lakini mara tulisikia mlio, ‘Twala, ni Twala!’ Na katika msongamano Twala akaruka amechukua mkuki na shoka, akaita, ‘Upo wapi.

Wewe Ndovu, wewe mtu mweupe uliyemuua mwanangu Skraga, njoo ujaribu kuniua mimi!

Na hapo alimtupia Bwana Henry kisu kikubwa, naye akakiona kinakuja akakikinga kwa ngao yake.

Basi ndipo Twala akapika ukelele mkuu akamrukia akampiga shoka kwa nguvu hata nguvu ya pigo ilimwangusha Bwana Henry, akaangukia magoti, ingawa alikuwa mtu mwenye jiramu na nguvu .

Lakini sasa jambo hilo halikuendelea, maana tulisikia sauti ya mshangao, tukatazama tukaona sababu yake. Kwa mkono wa kulia na wa kushoto vile vile uwanda ulikuwa kama u hai kwa jinsi walivyokuja askari wenye kupambwa na manyoya.


Walikuwa ni askari wetu waliokwenda kuzunguka, na sasa wamefika hapa.

Tena wamefika kwa wakati unaofaa sana, maana kama alivyobashiri Ignosi, askari wote wa Twala walikuwa wamekodoa macho yao kutazama vita vikali vilivyoshika baina ya Wajivu na Wanyati, wala hawakuona askari wetu waliotokea pembezoni mpaka wamekaribia sana kuwashambulia.


Na sasa kabla hawajawahi kujipanga, askari wetu wamewarukia kama mbwa anavyorukia windo lake.

Katika muda wa dakika tano, mwisho wa vita ukatambulikana, maana wale askari wa Twala walishambuliwa kwa pande zote mbili, nao wali fadhaika kwa mauaji waliyofanya Wajivu na Wanyati, walianza kukimbia, na kwa upesi uwanda wote katikati ya mahali tulipo na mji wa Loo ulitapakaa makundi madogo madogo ya askari wakijaribu kujiokoa.


Na wale askari waliokuwa wakiwashambulia Wajivu na Wanyati nao wakayeyuka kama wemeyeyushwa kwa uchawi, na sisi tuliachiliwa tumekaa kama mwamba ulioachiliwa na bahari iliyokupwa.


Lakini tuliachiliwa jinsi gani! Kote kote wamelala wale waliokufa, na wale wanaokufa, na wale wenye majeraha, na katika Wajivu, waliobaki ni tisini na tano tu.


Zaidi ya elfu tatu na mia nne wameanguka katika jeshi hilo, na wengi wao wameanguka wala hawaamki tena. Infadus akawa anajifunga jeraha mkononi mwake, akawaambia watu wake, ‘Watu wangu, leo hivi mmethibitisha kabisa sifa ile ambayo watu waliwapeni tangu zamani.

Habari za vita vya leo zitasimuliwa na watoto wa watoto wenu.’

Kisha akageuka akamtazama Bwana Henry akampa mkono akasema, ‘Wewe Ndovu, wewe ni shujaa kweli kweli, nimeishi maisha marefu yangu katikati ya askari na mashujaa, nami nimemwona mashujaa wengi, lakini sijaona mtu kama wewe.’

Basi hapo Wanyati waliobaki walikuwa wakipita kwenda mji wa Loo, na walipokuwa wakipita tukapata habari ya kuwa Ignosi alitaka Infadus na Bwana Henry na mimi tukaonane naye.

Basi tukawaamuru Wajivu waliobaki wakusanye wenye majeraha nasi tukaenda kumtafuta Ignosi.

Tulipomwona alitwambia kuwa anatangulia Loo kwenda kujaribu kumkamata Twala, maana ndipo vita vitakapokwisha kabisa.

Kabla hatujaenda mbali tulimwona Bwana Good ameegemea kisiki cha mti mbali kidogo, na karibu naye tulimwona maiti tuliyedhani ni Mkukuana.
 
Bwana Henry akafadhaika akasema, ‘Nafikiri amejeruhiwa.’

Na hapo aliposema hayo, Yule tuliyefikiri kuwa ni maiti Mkukuana akaruka akampiga Bwana Good kichwani akamwangusha chini, akaanza kumchoma mikuki, Tulimkimbilia Bwana Good, na tulipomkaribia tulimwona Yule Mkukuana anampiga na kumpiga tena kwa mkuki, na kila alipopiga mikono na miguu ya Bwana Good ikaruka juu.


Yule Mkukuana alipotuona tunakuja, akazidi kumpiga kwa nguvu, akapiga kelele, ‘Haya, wewe mchawi nimekuua.’ Akakimbia. Bwana Good akalala kimya wala hakuweza kujimudu hata kidogo, tukafikiri kuwa rafiki yetu tayari amekufa.


Tulimkaribia kwa huzuni, tukashangaa tulipoona anacheka ingawa amegeuka rangi kwa maumivu, akacheka na miwani bado ipo katika jicho lake, akasema, ‘Hizi nguo za chuma ni nzuri sana, naona kuwa Yule Mkukuana amestaajabu.’

Na mara akazimia. Tulipomtazama tuliona kuwa amejeruhiwa vibaya mguu mmoja kwa pigo la kisu kikubwa, lakini nguo zile za chuma zimemlinda asiumizwe zaidi na Yule Mkukuana. Ikawa ameokoka kwa rehema ya Mungu.

Hatukuweza kumtibu wakati ule basi tukamweka juu ya ngao akachukuliwa pamoja nasi. Tulipofika penye lango la Loo tukaona kikosi cha askari wa upande wetu wamesimama kulinda zamu kwa amri za Ignosi.

Vikosi vingine viliwekwa penye milango mingine ya mji.
Yule mkubwa wa kikosi alipomwona Ignosi, alimwamkia kwa amkio la kifalme, akamwambia kuwa askari wa Twala wamejificha katika mji, na Twala mwenyewe vile vile yumo mjini, lakini alifikiri kuwa watu watajitoa, maana wame fadhaika kabisa.


Basi aliposikia hayo Ignosi alituma tarishi kwa kila mlango wa mji kuwaamuru walio ndani wafungue milango, naye aliahidi kuwa wote watakaojitoa na kutoa silaha zao watapata msamaha.

Basi habari hii ikapokewa, na mara tulisikia makelele na milango ikafunguliwa. Tukaingia katika mji, lakini tuliangalia sana tusije tukaghafilika.

Katika njia zote tulikuta askari wamesimama na vichwa kuinamia chini, na silala na ngao zao zimewekwa chini miguuni pao, na Ignosi alipokuwa akipita walimwamkia kwa amkio la kifalme.

Tukaenda mbele mpaka jumba la Twala, Tulipofika kwenye kiwanja kile tulichokwenda juzi juzi kutazama ngoma, tulikiona kipo wazi kabisa, lakini si wazi, maana pale mbele ya mlango wa jumba lake, Twala mwenyewe alikaa, pamoja na mtu mmoja tu, naye alikuwa Gagula.

Ilisikitisha kumwona vile alivyokaa, na shoka lake na ngao yake vimewekwa chini ubavuni pake, na kichwa chake kainamisha kifuani, na mtu mmoja tu amekaa kumfariji.


Na ingawa tulikumbuka ukatili wake, hatukuweza kujizuia kuto kumsikitikia.

Hapana hata askari mmoja katika maelfu ya askari wake; hapana hata mfuasi mmoja katika wale wengi walionyenyekea mbele yake, hapana hata mke mmoja aliyesalia kumfariji katika uchungu wa yaliyomfika. Masikini!

Tulipita mlango wa kiwanja tukaenda mpaka mbele ya Twala, na huku Gagula anatutukana vibaya.

Tulipokaribia, Twala akafanya kutuona, akainua kichwa chake kilichovikwa manyoya marefu, akamtazama Ignosi kwa jicho moja lake, likang’aa kama ile almasi iliyofungwa katika kipaji chake cha uso, akasema kwa sauti yenye uchungu na dharau, ‘Hujambo, Ewe mfalme, wewe uliyekula chakula changu, na sasa kwa msaada wa uchawi wa watu weupe umewashawishi askari wangu kuniasi!

Niambie, ajali yangu ni nini, Ewe mfalme?’

Ignosi akajibu kwa ukali, ‘Ajali yako ni ile ile uliyompa baba yangu, ambaye kiti chake umekikalia kwa miaka hii yote.’ Twala akasema, ‘Vema, nimekubali. Nitakuonyesha njia ya kufia, ili nawe ukumbuke wakati wako utakapowadia.

Tazama, jua linazama, ni vizuri na jua langu lizame pamoja nalo. Na sasa, ewe mfalme, mimi tayari kufa, lakini nataka haki ya mfalme wa Wakukuana, yaani nife nikipigana. Huwezi kunikatalia; ukikataa hata wale waoga waliokimbia leo, hata na wao watakwita mwoga.’

Ignosi akajibu , ‘Nimekubali. Chagua, utapigana na nani? Mimi mwenyewe siwezi kupigana nawe, maana mfalme hupigana katika vita tu.’


Jicho la Twala likatutazama, na kwa dakika moja nilimwona ananitaza mimi tu, na baadaye akasema, ‘Ndovu, wasemaje, tumalize yale tuliyoanza leo, au nikwite kwa jina la mwoga?’

Ignosi akasema kwa haraka, ‘La, huna ruhusa kupigana na Ndovu.’ Twala akajibu, ‘Vema, kama anaogopa, sipigani naye.’ Basi Bwana Henry alifahamu maneno hayo, na uso ulimwiiva akasema, ‘Nitapigana naye, naye ataona kuwa siogopi.’


Nikamsihi, ‘Nakuomba usipigane naye, usijitie katika hatari ya bure, maana huyu anajua lazima afe. Kila mtu aliyekuona leo anajua kuwa wewe ni shujaa, si muoga.’

Akajibu, ‘Lazima nipigane naye. Hapana mtu atakayeniita muoga na kuishi. Sasa mimi ni tayari.’ Akashika shoka lake akasimama mbele. Nilipoona kuwa amekwisha azimia, wasiwasi uliniingia, lakini sikuweza kumzuia asipigane.

Ignosi akaweka mkono juu ya bega lake kwa upole, akamwambia, ‘Rafiki, ndugu yangu mweupe, usipigane naye. Vita uliyopigana leo inatosha kabisa, na ukidhurika, moyo wangu utakuwa mzito sana.’

Bwana Henry akasema, ‘Ignosi, lazima nitapigana naye .’ Akaijibu, ‘vema, Ndovu, wewe ni shujaa kweli kweli. Tazama, Twala, Ndovu yu tayari kupigana nawe.’

Twala akacheka kicheko kikubwa, akasimama akamtazama Bwana Henry. Kwa muda kidogo wakasimama hivi na mwangaza wa jua lililokuwa likishuka ukawaangaza ukaonyesha maungo yao namna yalivyokuwa mazuri.

Kisha wakaangaza kuzungukiana, na mashoka yao juu.

Mara Bwana Henry akaruka mbele akajaribu kumpiga Twala kwa nguvu zake zote, lakini Twala aliepa.

Nguvu za pigo zilikuwa nyingi hata alitaka kuanguka, basi adui yake akawa tayari akapungu shoka lake kichwani, akapiga kwa nguvu nyingi kabisa. Moyo wangu ulisita, nikafikiri kuwa yamekwisha. Lakini sivyo;

Bwana Henry akaweka mkono wake juu kwa upesi akalikinga shoka. Mara Bwana Henry akapata nafasi kupiga mara ya pili, lakini Twala akakinga kwa ngao yake.

Basi ikaendelea hivyo, pigo kwa pigo, na kila pigo lilikingwa. Sasa watu wote waliokuwako wakaanza kusongana katika mshangao wao, wakapiga kelele au kuguna kwa kila pigo.

Hapo Bwana Good aliye kuwa amezimia, akapata fahamu tena, na mara akasimama akaanza kurukaruka huku akimtia moyo Bwana Henry.

Basi hivyo hivyo wakapigana, hata kwa bahati mbaya Twala akapata nafasi ya kulipiga shoga la Bwana Henry likamtoka mkononi, likaanguka chini.

Sasa wote waliugua kwa mashaka na huzuni, na Twala akainua shoka lake juu akamrukia huku akipiga kelele. Nikafumba macho.

Nilipofumbua macho tena, niliona ngao ya Bwana Henry imelala chini, naye amemkumbatia Twala kiunoni.

Huku na huku waliminyana, huku wamekamatana kwa nguvu zao zote. Twala akajitahidi sana, akamwinua Bwana Henry juu, wakaanguka chini wote pamoja, na Twala alijaribu kumpiga shoka la kichwa, na Bwana Henry akajaribu kumpiga Twala kisu.


Ikawa shindano kuu kabisa, na hapo Bwana Good alipiga ukulele, ‘Shika shoka lake!’ Na labda Bwana Henry alisikia, maana alitupa kisu chake akashika shoka la Twala wakaanza kupinduana chini wakipigana kama paka wa mwitu wanavyopigana, huku wakitweta kwa nguvu.

Mara tuliona kuwa ngozi iliyofungiwa shoka kwenye mkono wa Twala imekatika, na Bwana Henry ametengwa naye na amepata shoka hilo. Mara akaruka juu, na damu inamtoka usoni pale alipojeruhiwa na Twala, na mara ile Twala naye akaruka juu.


Basi sasa ikawa kupigana tena, mpaka Bwana Henry akajitahidi akapiga shoka kwa nguvu zote, akampiga la shingo.

Hapo watu waliokuwapo waliguna kwa pamoja maana kichwa cha Twala kikaanguka kikabiringika mpaka kikafika kwenye mguu wa Ignosi kikasita.


Kwa dakika hivi kiwiliwili chake kilisimama wima, kisha kikaanguka kwa kishindo, na pale pale Bwana Henry alizimia, naye akaanguka juu ya maiti ya Twala.


Basi tulimwinua tukammwagia maji akafumbua macho yake. Hakufa, nami, jua lilipokuwa likishuka, nikasimama mbele, nikafungua ile almasi iliyofungwa juu ya kipaji cha uso wa Twala, nikampa Ignosi, nikasema, ‘Itwae Ignosi, mfalme wa haki wa Wakukuana, mfalme kwa ‘kuzaliwa, na mfalme kwa kushinda.’

Ignosi akaifunga juu ya kipaji chake, akaja mbele akaweka mguu wake juu ya kiwiliwili cha Twala, akaanza kuimba wimbo wa ushindi, hivi:

Sasa uasi wetu umemezwa katika ushindi, na vitendo vyetu viovu vimegeuka kuwa haki kwa nguvu. Asubuhi wadhalimu waliamka wakajitikisa; walijifungia manyoya wakajiweka tayari kwa vita. Waliamka wakashika mikuki yao: askari waliwaita wakubwa wao, ‘Njooni mtuongoze.’

Na wakubwa walimwita mfalme, ‘Utuongoze vitani.’ Wakaondoka na kiburi chao, watu ishirini elfu na tena ishirini elfu.

Manyoya yao yalifunika nchi kama manyoya ya ndege yanavyofunika tundu lake; walitikisa mikuki yao kwa vigelegele.

Ndiyo, walirusha mikuki yao katika mwangaza wa jua; wakatamani vita wakafurahi.
Wakanishambulia; wenye nguvu wao eakanijia mbio waniue, wakipiga kelele,’ Hal Ha! Ni kama aliyekwisha kufa.’ Ndipo nilipovuma juu yao, na pumzi zangu zikawa kama upepo wa tufani, na tazama! Wakatawanyika .


Umeme wangu uliwachoma; nililamba nguvu zao kwa umeme wa mikuki yangu; niliwapeperusha kwa ngurumo ya kulia kwangu.

Walivunjika, walitawanyika, walitoweka kama ukungu wa asubuhi.
Sasa wamekuwa chakula cha kunguru na fisi, na mahali pa vita pamenona kwa damu yao.

Wa wapi wale walioamka asubuhi na nguvu zao?
Wa wapi wale wenye kiburi waliotikisa manyoya yao wakasema ‘Ni kama aliyekwisha kufa:’

Wameinamisha vichwa lakini si katika kusinzia; wamejinyosha, lakini si katika usingizi.
Wamesahauliwa; wametoweka gizani nao hawatarudi; ndiyo, watu wengine watawachukua wake zao, na watoto wao hawatawakumbuka tena.


Na mimi, mimi? Mimi ni mfalme. Kama tai nimeona tundu langu.

Tazama! Nilitembea mbali wakati wa usiku, lakini nimewarudika makinda yangu wakati wa mapambazuko.

Ingieni nyinyi kwenye kivuli cha mabawa yangu, ee nyinyi watu, nami nitawafariji, nanyi hamtafadhaika tena.

Huu ndiyo wakati wa neema, huu ndio wakati wa kuteka. Ng’ombe walio bondeni ni wangu, wanawali pia walio mjumbani ni wangu.

Taabu imepita, neema imefika. Sasa uovo utafunikwa uso wake, na Huruma na Furaha watakaa katika nchi.

Furahini, furahini, watu wangu!

Dunia yote ifurahi kwa kuwa jeuri imekanyagwa, na mimi ndiye mfalme.


Ignosi akanyamaza, na kutoka katika giza lililokuwa limeingia, jibu likaja kama ngurumo kutoka milimani, ‘Wewe ndiye mfalme!’

Hivyo yale niliyombashiria Yule tarishi yalitimia, na katika muda wa saa arubaini na nane, kiwiliwili cha Twala kimelala kikavu mbele ya mlango wa jumba lake.
 
SURA YA KUMI NA TANO

Baada ya mapigano kuisha, Bwana Henry na Bwana Good walichukuliwa na kuwekwa katika jumba la Twala, nami nilikwenda pamoja nao.

Wote walikuwa dhaifu kabisa kwa kuchoka na kwa kutokwa na damu, na hata mimi hali yangu ilikuwa hivyo hivyo.

Lakini mimi ni mwembamba kama uzi wa simu, yaani sichoki upesi: lakini usiku ule kwa kweli nilikuwa nimechoka kabisa.

Kwa hakika sote tulikuwa katika hali dhaifu, tukawa tukijifariji kwa kukumbuka kuwa tu hai wala si kama wale waliolala wakavu katika uwanda ule wa vita.

Kwa msaada wa Foulata aliyejifanya kuwa mtumishi wetu, tulizivua nguo zile za chuma ambazo kwa yakini zimetuokoa hivi leo. Lakini tulipozivua tuliona kama tumechubuka sana, maana ingawa zilitulinda tusichomwe na silaha hazikuzuia tusipate machubuko.

Foulata akaleta majani ya dawa yalionukia vizuri na ambayo yalipunguza maumivu yetu. Lakini maumivu yangu hayakuwa kama yale ya Bwana Henry na Bwana Good.

Bwana Good alikuwa amejeruhiwa mguuni maana mkuki ulipenya hata upande wa pili akatokwa na damu nyingi; na Bwana Henry alikuwa na majeraha mengi, na hasa moja kubwa usoni pale alipopigwa shoka na Twala.

Lakini kwa bahati Bwana Good alikuwa mganga wa kutosha akatuganga sote kwa dawa zilizokuwa katika kasha lake. Huku nyuma Foulata alitupikia mchuzi wa kututia nguvu, maana tulikuwa tumechoka hata hatukuweza kula.


Kisha baada ya kunywa mchuzi tukajitupa juu ya ngozi zilizokuwa katika jumba la Twala tukalala. Lakini ilikuwa vigumu kupata usingizi vizuri baada ya kazi za mchana, kwa sababu sauti za kuagana za wale wanaokufa, na vilio vya wale.

Waliofiwa zilizagaa kote. Kutoka kila upande tulisikia vilio vya wanawake waliofiwa na wanaume, wana na ndugu katika vile vita vikali.

Na kwa hakika walikuwa na haki ya kulia, maana katika jeshi la Wakukuana, karibu elfu kumi na mbili waliangamia katika vita vile.

Ilituathiri sana kusikia vilio vile vya huzuni walivyowalilia wale ambao hawarudi tena; vikanikumbusha sana kazi ya kutisha iliyotendeka siku ile kwa ajili ya kutekeleza tamaa za wanadamu.

Lakini ilipofika kiasi cha saa sita, vilio vilipungua, na baadaye kidogo ikawa kimya ila kwa sauti tuliyosikia ikitoka kwa nyuma ya jumba, tukafahamu baadaye kuwa alikuwa Gagula akimlilia mfalme Twala.



Baada ya saa sita nililala kidogo, lakini mara kwa mara nilishtuka nikafikiri kuwa nimo katika vita tena, na katika ndoto zangu nilipigana vita vyote tangu mwanzo.

Basi usiku ulipita, kukapambazuka; nikaona kuwa hata na wenzangu vile vile hawakulala vizuri.

Bwana Good alikuwa na homa kali sana, na akili zilimruka; pia akaanza kutema damu, maana nadhani Yule Mkukuana aliyejaribu kumchoma mkuki alimuumiza vibaya kwa ndani. Lakini Bwana Henry alipata nafuu ingawa alijimudu kwa shida bado kwa namna alivyokuwa ameumia.


Ilipofika kama saa mbili Infadus akaja kutuamkia, naye alikuwa kama hakuwamo katika vile vita vya jana, jinsi alivyokuwa mzima. Alifurahi sana kutuona tena, akatupa mikono na kututikisa kwa nguvu sana, lakini akamsikitikia sana Bwana Good.
 
Lakini niliona kuwa siha zake kwa Bwana Henry zilikithiri, baadaye tulikuja kujua kuwa askari hawakumfananisha Bwana Henry na mwanadamu wa kawaida.

Walisema kuwa hapana mwanadamu aliyeweza kupigana na Twala kama yeye alivyopigana naye, na hasa baada ya siku ya vita kama vile, maana Twala alisifiwa kuwa si mfalme tu lakini ni askari shujaa kupita wote.

Na pigo lile alilompiga hata kumkata kichwa likawa kama methali, yaani pigo lolote lililozidi nguvu likiitwa, Pigo la Ndovu.


Infadus akatuarifu kuwa askari wote wa Twala wamejiweka chini ya amri ya Ignosi, na wale waliokaa mbali wanafika sasa kujitoa. Kufa kwake Twala kwa mkono wa Bwana Henry kumemaliza kabisa vita katika nchi, maana Skraga aliyekua mrithi hata yeye amekufa.


Baadaye Ignosi akaja kutuamkia amevaa ile almasi ya kifalme juu ya kipaji cha uso. Nikamtazama alipokuwa akija, nikajaribu kumfananisha na Yule aliyekuja kwetu, akiomba tumpe kazi miezi michache nyuma.


Basi alipokaribia nikanyanyuka nikasema, ‘Hujambo, Ewe mfalme!’
Akajibu, ‘Sijambo, Makumazahn, mimi ni mfalme kwa nguvu za mikono yenu.’ Akatuarifu kuwa mambo yote yanaendelea vizuri, naye alitumaini kufanya karamu baada ya juma mbili apate kuonekana mbele ya watu wake.


Nikamuuliza atamfanya nini Yule Gagula, akajibu, ‘Yeye ni kama waziri mwovu katika nchi, na lazima nimuue, pamoja na wachawi wote.


Ameishi sana duniani, hata hapana anayejua miaka mingapi, naye ndiye aliyewafundisha wachawi wote na kufanya nchi iwe mbaya mbele ya Mungu.’
Nikajibu, ‘Kweli, lakini anayo maarifa mengi, na ni rahisi kuharibu maarifa kuliko ‘kuyapata!’


Akajibu, ‘Kweli, ni yeye peke yake ajuaye siri ya Wale Watatu Walio Kimya, na palipozikwa wafalme.’ Nikasema, ‘Ndiyo, na usisahau kuwa almasi zipo. Usisahau, Ignosi, yale uliyoahidi kuwa utatuongoza mpaka mashimo ya almasi, hata kama itakulazimu umwache Gagula aishi.’ Akajibu, ‘Mimi siwezi kusahau, Makumazahn, nami nita yafikiri maneno uliyosema.’


Ignosi alipoondoka nilikwenda kumtazama Bwana Good, nikamkuta ameshikwa na homa kali sana. Kwa siku mbili tulifikiri kuwa lazima atakufa, tukawa na mioyo mizito sana, lakini Foulata hakukubali, akasema kuwa lazima atapona.


Usiku wa tano wa ugonjwa wake nilikwenda kumtazama usiku kabla ya kwenda kulala, nikaingia chumbani pole pole sana, na kwa mwangaza wa taa nilimwona Bwana Good, lakini hakuwa akigaagaa kama siku zote, alilala kimya kabisa. Basi nilifikiri huu ndio mwisho, na nilikaribia kulia kwa uchungu.


Mara nilisikia sauti, ‘Sh! Sh!’ Nikatambua nikaenda karibu nikaona kuwa amelala usingizi wala hakufa, Alilala hivyo kwa muda wa saa kumi na nane, na wakati huo wote ameshika mkono wa Foulata, naye hakuweza kuondoka kwa sababu aliogopa atamwamsha.

Akakaa hivi bila kujinyosha na bila kula; lakini kwa kweli alipoamka ikawa lazima kumchukua, maana hakuweza kwenda kwa sababu viungo vyake vilikufa ganzi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom