Mashimo ya Mfalme Suleiman

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
75,488
158,139
UTANGULIZI
Hadithi hii ilipigwa chapa kwa lugha ya Kiingereza katika mwaka 1885. Katika mwaka 1905 Bwana H. Rider Haggard aliandika maneno haya: 'Sasa katika mwaka 1905 naweza kuzidisha maneno yangu kwa kusema ya kuwa nimefurahishwa sana kuona hadithi yangu inadumu kuwapendeza wasomaji wengi. Hayo yaliyobuniwa yamedhibitishwa kuwa ni kweli: Mashimo ya Malme Sulemani niliyokuwa nikiyafikiri sasa yamegunduliwa nayo sasa yanatoa dhahabu tena, na kwa habari zilizotoka hivi karibuni hata almasi pia hutoka.'

MASHIMO YA MFALME SULEIMAN

SURA YA KWANZA

Kukutana na Bwana Henry Curtis

Ni ajabu sana kwa mtu aliyefika umri wangu, yaani miaka hamsini na tano, kushika kalamu na kuanza kuandika kitabu, kama hivi ‘nifanyavyo mimi sasa. Sijui habari hizi zitakuwaje nikiisha kuzitunga, yaani nikijaliwa kufika mwisho wa safari yangu salama, maana ingawa nimefanya mambo mengi katika maisha yangu, lakini sijawahi kujaribu kuandika kitabu. Tokea utoto wangu nimeshughulika na kazi ya biashara na kuwinda, kupigana na kuchimba dhahabu, na tangu kupata utajiri huu nilionao ni miezi minane tu.



Sasa nina mali nyingi sana, hata jumla yake siijui, lakini nadhani nisingekubali kuvumilia tena hayo yote niliyoyavumilia katika miezi kumi na tano iliyopita hata kama ningejua kwa hakika kuwa nitatoka salama pamoja na mali nyingi pia. Mimi ni mtu mtaratibu, sipendi ghasia, na tena nimechoka kabisa kusafirisafiri na kupambana na mambo ya ajabu. Sijui kwa nini naandika kitabu hiki, maana uandishi si kazi yangu. Mimi si mwana chuoni ingawa napenda sana kusoma vitabu. Hebu kwanza nijaribu kuandika sababu zangu za kutunga kitabu hiki, ili muone kama kweli ninazo sababu.

Sababu ya kwanza ni kuwa Bwana Henry Curtis na Bwana Good wameniomba nikitunge. Sababu ya pili ni kuwa nimebaki hapa Durban kwa kuwa mguu wangu wa kushoto waniuma sana. Tangu nilipoumwa na simba ninapata maumivu, na hasa siku hizi yanazidi, hata siwezi kwenda vizuri. Nadhani haikosi meno ya simba yana sumu na kama sivyo majeraha yangeisha pona kabisa na yasinge rudi tena, na hasa ajabu ni kuwa yanarejea mwezi ule ule niliyong’atwa. Ni ajabu sana kuwa baada ya kuua simba sitini na tano na labda zaidi, Yule wa sitini na sita aliniuma mguu. Jambo hili limeharibu mipango yangu ya desturi yote, na kwa kuwa mimi ni mtu wa kufuata taratibu na mipango naona dhiki kabisa. Lakini hayo hayamo katika habari za kitabu hiki.

Sababu ya tatu ni kuwa nataka mwanangu Harry anaesoma katika chuo cha utabibu, awe na mazungumzo ya kumfurahisha na kumpendeza. Asifanye upumbavu. Kusomea utabibu si kazi rahisi, na kazi ya kuvumbua habari za mwili vile vile inachosha. Habari zilizomo katika kitabu hiki si kama zile zinazotokea kila siku, kwa hivyo labda zitamfurahisha kwa muda kidogo.

Sababu ya nne na ilivyo ya mwisho ni kuwa nataka kusimulia hadithi ya ajabu kupita zote ninazozijua. Labda itakuwa ajabu kweli kwa kuwa hapana mwanamke aliyetajwa katika hadithi hii, ila Foulata. Lakini ngoja kwanza! Nilitaka kumsahau Gagula, lakini sina hakika kama alikuwa mwanamke au shetani. Lakini kwa umri wake ulizidi miaka mia moja na kwa kuwa: haoleki, basi simhesabu kuwa mwanamke. Basi afadhali nijifunge kibwebwe. Kazi ni ngumu nami naona kama nimekwisha yavulia nguo maji. Lakini kama wasemavyo wajuzi, ‘Pole pole ndio mwendo,’ Basi sasa naanza.

‘Mimi Alan Quatermain, mzaliwa wa Durban, Natal, naapa na kusema …’Hii ndiyo namna nilivyoanza kusema mbele ya kadhi nilipokuwa natoa habari za kufa kwa Khiva na Ventvogel, lakini naona kuwa hii siyo namna ya kuanza kutunga kitabu. Basi, je, mimi ni muungwana? Muungwana ni nini? Sijui hakika. Maisha yangu yote nilikuwa nikifanya kazi ya biashara na kuwinda tu. Nimejaribu daima kuwa muungwana, basi wewe usomaye utanihukumu. Mungu ajua kuwa nimejaribu. Ama kweli katika maisha yangu nimeua watu wengi, lakini sikuu mtu bure wala sikuua mtu asiye na hatia, ila kwa kujilinda mwenyewe tu. Mwenyezi Mungu alitupa maisha, nadhani nia yake ni kwamba tujilinde, nami siku zote nimeshikilia hivyo ; natumaini kwamba hayo hayatanitia hatiani siku ya kuhukumiwa itakapowadia.

Lakini dunia ina ukali na maovu, na ingawa mimi ni mtu taratibu na mwoga kidogo nimeona mauaji mengi. Lakini naweza kusema kuwa sijaiba, ingawa mara moja nilimdanganya mtu mmoja nikachukua kundi la ng’ombe wake. Lakini yeye alikuwa amenifanyia mambo mabaya kabisa na hata hivyo, tangu siku ile ninajuta kwa vitendo vyangu nilivyovifanya.

Toka nilipokutana na Bwana Henry Curtis na Bwana Good mara ya kwanza, imepita miezi kumi na nane, na namna tulivyokutana ilikuwa hivi: Nilikwenda kupita Bamangwato ili kuwinda ndovu. Nikawa na bahati mbaya sana katika safari hiyo, na juu ya hayo nilishikwa na homa kali. Nilipopona nikasafiri mpaka kunakochimbwa almasi, nikauza pembe zangu zote nilizokuwa nazo pamoja na gari la ng’ombe, nikawapa ruhusa wawindaji wangu, na mimi mwenyewe nikapanda gari niende Captown. Baada ya kukaa Captown kwa muda wa jumaa moja niliona kuwa gharama za hoteli zinazidi sana, tena nilikuwa nimekwisha ona yote niliyoyataka kuyaona, basi nikanuia kurudi Natal kwa meli iitwayo Edinburg Castle inayotoka Ulaya.

Basi nikaenda kukata tiketi nikaingia melini, na jioni ile ile meli ikang’oa nanga tukasafiri. Katika abiria walioingia melini niliona wawili niliowatazama sana. Mmoja alikuwa mtu mwenye umri kadiri ya miaka thelathini, kifua kipana na mikono mirefu kushinda watu wote niliowahi kuwaona. Nywele zake zilikuwa za rangi ya kimanjano na alikuwa na ndevu nyingi za rangi ile ile, na macho yake yalikuwa ya rangi ya kijivujivu tena yameingia ndani. Wala nilikuwa sikupata kuona mtu mzuri kumpita yeye. Halafu nikajua kuwa huyu ni Bwana Henry Curtis. Yule mtu mwingine aliyekuwa akiongea na Bwana Henry alikuwa mfupi tena mnene, kisha mweusi kidogo, na sura yake ilikuwa haikufanana hata kidogo na ile ya Bwana Henry. Halafu nikajua kuwa anaitwa Bwana Good.

Basi jioni nilipokuwako sitahani nilisikia sauti, mara nikageuka kuangalia, nikaona kuwa ni Yule Bwana Good. Hata tulipokwenda chini kula chakula tulimkuta Bwana Henry amekwisha kaa mezani, na mara tukaanza kuongea habari za kuwinda na mambo mengineyo. Akaniuliza maswali mengineyo. Akaniuliza maswali mengi sana, nami nikamjibu kadiri nilivyoweza. Halafu yake tukaanza kuongea habari za ndovu, na mtu mmoja aliyekuwa karibu yetu akasema, ‘Ee bwana, kama ukitaka mtu hasa anayeweza kukwambia kweli habari za ndovu, ni mwindaji Quatermain.’ Bwana Henry Curtis aliposikia hivi, akashtuka na akasema kwa sauti ya upole, ‘Niwie radhi bwana, jina lako wewe ni Allan Quatermain?’ Nikamwambia, ‘Ndiye mimi.’

Tulipokwisha kula, tukawa tunatoka mezani, na Bwana Henry akanijia kunikaribisha niende chumbani kwake tukavute tumbako, nami nikakubali. Mradi tulikuwa watu watatu, na mara Bwana Henry Curtis akasema, ‘Bwana Quatermain, nadhani miaka miwili iliyopita ulipata kuwako mahali panapoitwa Bamangwato katika nchi ya Transvaal,sivyo? Kusikia hivyo nikaona ajabu sana yeye kujua habari za safari zangu. Nikamwambia, ‘Ndiyo nilikuwako’, Bwana Good akauliza, ‘Ulikuwa ukifanya biashara sivyo?’ Nikajibu, ‘Ndiyo, nilichukua gari la bidhaa nikapiga kambi nje ya mji, nikakaa huko mpaka nilipokwisha kuuza zote .’ Bwana Henry aliyekuwa amekaa katika kiti kukabili kiti changu, akaniuliza, ‘Ulipata kukutana na mtu mmoja jina lake Neville?’ Nikajibu, ‘Ndiyo, tulipiga kambi zetu karibu kwa muda wa siku kumi na nne, na baada ya miezi michache nikapokea barua kutoka kwa Mwana Sheria ya kuniuliza habari zake kama namjua alipo, nami nikapeleka majibu kueleza habari zake kama nilivyoweza.’

Bwana Henry akasema, ‘Najua, maana barua yako ililetwa kwangu. Ulisema kwamba mtu aitwaye Neville alitoka Bamangwato mwanzo wa mwezi wa Mei akasafiri kwa gari pamoja na watu wake na mwindaji mtu mweusi mmoja jina lake Jim, naye alisema kuwa anakwenda mpaka Inyati ambao ndio mji wa mwisho katika nchi ya Mtabele ; akifika hapo atauza gari lake aende kwa miguu. Kisha ulisema kuwa kweli aliuza gari lake kwa sababu uliliona tena baada ya miezi sita, na mtu uliyemwona nalo alikuwa ni Mreno mfanya biashara aliyekwambia kuwa amelinunua Inyati kwa mtu mweupe mmoja, ambaye jina lake amelisahau ila anafikiri kuwa yeye pamoja na boi wake amekwenda mwituni kuwinda.’ Nikajibu, ‘Hayo ni kweli.’ Basi tukanyamaza kidogo, kisha, Bwana Henry Curtis akasema, ‘Naona ya kuwa hujui vema habari hizo. Huwezi kukisia sababu zake za kusafiri kwenda kaskazini na mahali gani alipokwenda?’ Nikamjibu, ‘Nilisikia kidogo.’

Na kwa kuwa sikutaka kusema naye zaidi juu ya habari hizi nikanyamaza kimya. Bwana Henry na Bwana Good wakatazamana, kisha Bwana Good akatikisa kichwa kwa kumfanyia ishara Bwana Henry, akasema, ‘Bwana Quatermain nitakusimulia hadithi yangu, halafu unipe shauri na msaada wako. Yule wakili wangu aliyeniletea barua yako aliniambia kuwa wewe ni mtu wa heshima sana na watu wote wanakustahi, na kwa hiyo naweza kukuamini. Basi nikainamisha kichwa kwa haya kwa vile nilivyosifiwa na Bwana Henry akaendelea kusema, ‘Huyo Bwana Neville ni ndugu yangu.’ Niliposikia hivi nikastuka sana, maana sasa nalifahamu sababu ya kumtazama sana nilimwona mara ya kwanza, kwa kuwa wamefanana sana.

Basi Bwana Henry akaendelea kusema, ‘Yeye ni mdogo wangu, na mpaka miaka mitano iliopita nadhani hatukupata kuachana hata kwamuda wa mwezi mmoja. Lakini katika mwaka ule wa mwisho tulioonana tulipatwa na msiba kama wanavyopatwa watu wote mara kwa mara. Maana tuligombana sana hata nilimtenda mambo yasiyo ya haki kwa ajili ya hasira zangu. Haikosi unajua kuwa mtu akifa na kama mali yake ni mashamba tu, wala naye hakuacha wosia wowote, kwa sheria ya Uingereza mrithi huwa ni Yule mtoto mwanaume mkubwa, yaani aliyezaliwa kwanza, ndiye anayechukua mali yote. Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa. Na wakati ule tulipokuwa tukigombana baba yetu alifariki naye hakuwahi kuandika wosia. Basi kwa hivyo ilionekana kuwa mdogo wangu hakuwa na urithi.

Kusema kweli ilikuwa ni wajibu wangu kumsaidia na kumtunza, lakini kwa ule uchungu wa ugomvi jinsi ulivyokuwa mwingi sana, hata sasa naona aibu kukiri kuwa sikufanya jambo. Sikuwa na nia ya kumnyima haki yake, ila nilitaka yeye aje kwangu’ kuomba suluhu, naye hakuja. Nasikitika sana kukuudhi kwa habari hizi zangu, lakini naona sina budi kukueleza waziwazi mambo yote, sivyo Bwana Good?’ Bwana Good akajibu, ‘Ndivyo, nami najua kwa hakika kuwa Bwana Quatermain atayasitiri yote moyoni mwake.’ Nikajibu, ‘Vema,’ Maana mimi natafakari sana kuwa si mtu wa kupayuka.

Halafu Bwana Henry akasema, ‘Mdogo wangu alikuwa na fedha kidogo na bila kunishauri alitoa fedha zote alizokuwa nazo katika banki, na kuchukua jina lingine la Neville, akafunga safari kwenda kuchuma Afrika ya Kusini. Nikakaa kwa muda wa miaka mitatu bila kupata habari zake wala salamu zake, ingawa mimi nilimwandikia barua nyingi. Labda zilikuwa hazimfikii. Lakini baadaye nikaanza kuwa na wasiwasi, maana mtu haachi kumpenda ndugu yake.’
Nikasema, ‘Hayo ni ya kweli. ‘Maana nilikuwa nikimkumbuka mtoto wangu. Bwana Henry akawa anaendelea kusema, ‘Nikahisi kuwa hata nusu ya mali yangu yote nitatoa ili nipate kujua yaliyompata mdogo wangu, maana ni mmoja tu aliyebaki katika ukoo wangu. Basi siku zilipozidi kupita nami nikazidi kuwa na wasiwasi, nikatamani sana kupata habari zake. Ndipo nikaanza kuulizauliza, hata nikapata ile barua. Basi mpaka sasa habari ni nzuri, maana zaonyesha kuwa yu hai mpaka sasa. Na nilitia nia kwenda mwenyewe kumtafuta, na Bwana Good amenifurahisha sana kwa kufuatana nami.’ Basi Bwana Good akasema, ‘Ndiyo na sasa Bwana, labda utatwambia habari zote ujuazo za Yule mtu aitwaye Neville.’

SURA YA PILI

Basi kabla sijaanza kumjibu Bwana Good, nilitia tumbako katika kiko changu, na Bwana Henry akauliza, ‘ Ulisikia habari gani juu ya safari ya ndugu yangu ulipokuwako Bamangwato?’ Nikamjibu, ‘Nalisikia hivi, ya kuwa anakwenda kutafuta Mashimo ya Sulemani. Na tangu siku hiyo hata hivi leo, sijamwambia mtu habari hizo.’ Wote wawili wakauliza pamoja, ‘Mashimo ya Sulemani! Yapo wapi?’ Nikajibu, ‘Mimi sijui, lakini najua mahali ambapo watu husema kuwa yapo. Siku moja niliona vilele vya milima inayopakana nayo, lakini baina ya mahali hapo nilipokuwa mimi na milima hiyo palikuwa na jangwa la upana wa maili mia moja na thelathini, nami sijapata kusikia kuwa Mzungu yeyote amepata kuvuka jangwa hilo, isipokuwa mtu mmoja tu.



Lakini nadhani itakuwa vizuri zaidi nikisimulia habari hizo, yaani kama nilivyopokea kutoka kwa wenyeji, za Mashimo ya Sulemani kwa kadiri ninavyojua, ikiwa mtaahidi kuwa mtazisitiri mioyoni mwenu na kutomwambia mtu yeyote bila ya idhini yangu. Je, mtakubali sharti hilo?’ Bwana Henry akainamisha kichwa, na Bwana Good akaitikia, ‘Naam, naam.’ Basi, nikaanza kutoa hadithi yangu: ‘Kwa kawaida mwajua kuwa wawindaji wa ndovu ni watu wasiotamani anasa za dunia, wala hawashughuliki na mambo ila ya kweli ya dunia. Lakini pengine mwaweza kumkuta mtu mmoja mmoja anajitia katika mambo ya kuandika hadithi na kujaribu kutunga habari za zamani za watu wa kale. aliyeniambia maneno haya alikuwa ni mtu wa namna hiyo, na tangu aliponiambia maneno haya umepita muda wa miaka thelathini. Ilikuwa hivi: katika safari yangu ya kwanza nilikwenda kuwinda ndovukatika nchi ya Matabele. Mtu mmoja aliyeitwa Evans ndiye aliyeniambia maneno hayo, naye masikini aliuawana nyati mwaka wa pili yake, akazikwa mahali palipokuwa karibu na maporomoko ya maji yam to wa Zambezi. Nami nakumbuka sana kuwa siku moja nilikuwa nikizungumzia habari za kulungu na pofu katika mtaa mmoja wa Transvaal.’

Evans akasema, ‘Ndiyo, lakini mimi nitakutolea hadithi iliyo ya ajabu zaidi kupita habari za wanyama.’ Akaendelea kuhadithia jinsi alivyopata kuvumbua magofu ya mji wa zamani sana ambao aliamini kuwa ni mji ule uliokuwa ukiitwa Ophir uliotajwa katika Agano la Kale,na tangu siku hizo, watu wengi wenye maarifa kuliko yeye marehemu Evans wamesema hivyohivyo. Mimi nikakaa kusikiliza sana, maana wakati ule mimi nilikuwa bado kijana, na hadithi zile za kale zilinipendeza sana, na mara akasema, ‘je, mwanangu, umepata kusikia habari za milima ya Sulemani iliyo upande wa kaskazini wa nchi ya Mashukulumbwe?’’ , Nikamwambia, ‘Sijapata kusikia .’Akasema, ‘Basi, haidhuru, hapo ndipo mashimo ya Sulemani yalipo, yaani mashimo ya almasi.’ Nikamuuliza, ‘Je, wewe umejuaje?’ Akajibu, ‘Najuaje! Najua kwa jina lake lilivyo, na tena niliambiwa na mwanamke mmoja mchawi wa kabila la Isanusi katika nchi ya Manika. Alisema kwamba watu wanaokaa upande wa pili wa milima ile ni wa ukoo wa Amazulu, wanasema lugha inayofanana na Kizulu, ila wao ni wakubwa, tena wazuri zaidi ya Amazulu. Lakini kuna wachawi wenye nguvu nyingi wanaokaa humo na walikuwa na siri ya shimo la ajabu lenye mawe yale yanayong’aa.’ Nilicheka sana niliposikia hadithi hii, nikaipuuza, lakini ilinipendeza sana, maana wakati ule mashimo ya almasi yalikuwa bado hayajavumbuliwa. Lakini Yule marehemu Evans aliuawa, nami nikakaa muda wa miaka ishirini bila kufikiri tena jambo hili.

Baada ya miaka ishirini, na huo ni muda mrefu sana, maana mwindaji wa ndovu ana shida kuishi miaka ishirini katika kazi yake, nikasikia habari zaidi juu ya milima ya Sulemani na nchi iliyo upande wa pili yake. Hapo mimi nilikuwa katika nchi ya Manika, mahali paitwapo KwaSitanda, napo ni mahali pabaya sana, maana sikuweza kupata chakula wala wanyama hakuna. Nilishikwa na homa kali mno hata hali yangu ikawa dhaifu sana, na siku moja akafika Mreno mmoja pamoja na mwenziwe mmoja suriama. Tukaongea kidogo pamoja, maana yeye aliweza kusema Kiingereza kidogo, nami pia nilijua kusema Kireno kidogo, akaniambia kuwa jina lake ni Jose Silvestre, na tena ana shamba karibu na Delagoa Bay. Lakini siku ya pili yake aliondoka pamoja na mwenziwe. Katika kuniaga akasema ‘Bwana, tukionana tena natumai mimi nitakuwa tajiri kuliko watu wote duniani, nami nitakukumbuka.’ Nikacheka kidogo, maana nilikuwa mnyonge kwa homa na kwa hivyo sikuweza kucheka sana; nikamwona akienda kuvuka lile jangwa kwenda upande wa magharibi. Nikadhani kuwa ana wazimu, kwani anakwenda kutafuta nini huko? Baada ya juma moja, nikapona, na jioni nilipokuwa nimekaa nje ya hema langu dogo, nikitafuna paja la kuku wa mwisho niliyemnunua kwa mtu mmoja kwa bei ya kitambaa kimoja kilichonipatia kuku ishirini, nikitazama jua jinsi lilivyokuwa jekundu linavyoshuka nyuma ya jangwa hilo, mara nikaona kitu kama mzungu amevaa koti akiteremka mteremko uliokuwako kiasi hatua mia sita, mbele yangu.

Kwanza mtu huyo alitambaa kwa magoti na mikono, kisha akasimama na kupepesuka hatua chache mbele, tena akaanguka na kutambaa. Mradi nikaona kuwa ni mtu aliye taabani. Nikapeleka mmoja wa wawindaji wangu kwenda kumsaidia, na baadae kidogo akaja nae. Je, wadhani alikuwa ni nani? Alikuwa ni Yule Jose Silvetre, kwa kweli, mifupa yake ilikuwa dhaifu, tena alikuwa amekonda kabisa. Uso wake ulikuwa manjano, uking’aa kwa homa aliyokuwa nayo, nayale macho yake meusi makubwa yalionekana kama yaliyotokeza nje, maana alikuwa hana nyama kabisa .. Ngozi yake ilikuwa imekauka, na nywele zake zilikuwa zimegeuka rangi zikawa nyeupe, na mifupa imemtoka. Akawa anaugua huku akisema, ‘Nipeni maji! Jamani.

Nikaona kuwa midomo yake imepasuka na ulimi ulikuwa mweusi tena umevimba. Nikampa maji yaliyochanganyika na maziwa kidogo, akayabugia. Nikamzuia kusudi asinywe zaidi. Na mara homa ilimshika tena na kuanza kupayuka na kusema habari za milima ya Sulemani, na almasi na jangwa. Nikamchukua na kumweka hemani mwangu nikamtunza kama nilivyoweza; lakini nilijua kuwa atakufa. Kama saa tano ya usiku akatulia kidogo, nami ndipo nilipopata usingizi kidogo, nikalala. Kulipopambazuka nikaamka, nikamwona namna alivyokuwa amekonda sana amekaa na kulikodolea jangwa macho. Baadae kile kianga cha kwanza chajua kilionekana mawinguni, kikaangaza jangwa mpaka kufika kilele kirefu katika milima ya Sulemani, masafa ya maili mia moja na zaidi. Mara Yule mgonjwa akanyosha mkono wake mwembamba kuelekeza kileleni na huku akisema kwa Kireno, ‘Ndipo, ndipo papo hapo, lakini mimi sitawahi kupafikia kamwe. Wala hapana atakayepafikia kwamwe!’ Mara akakaa kimya kidogo kama mtu anayewaza jambo moyoni, halafu akanigeukia akasema, ‘Rafiki bado ungalipo? Ama sasa naona macho yangu yanaingia giza,’ Nikajibu, ‘Ndiyo, nipo hapa hapa.

Lakini sasa afadhali ulale upumzike.’ Akasema, ‘Ndiyo nitapumzika sasa hivi; tena nitakuwa na wasaa mwingi wa kupumzika, hata milele. Nisikilize, ninakufa! Wewe umenitendea mema. Nitakupa hati. Labda utaweza kupafikia ikiwa utaishi na kuvuka jangwa ambalo limemuua mtumishi wangu na mimi!’

Akapapasapapasa katika mfuko wake akatoa kitu nilichokidhania kuwa kikoba cha kuwekea tumbako kilichofanywa kwa ngozi ya mnyama. Kikoba hicho kilifungwa kwa uzi wa ngozi naye alijaribu kukifungua asiweze. Akanipa akisema, ‘Fungua.’Nikakifungua nikatoa kipande cha kitambaa kikuukuu cha katani kilichokuwa kimeandikwa maneno, na ndani ya kitambaa hicho mlikuwamo karatasi. Kisha akasema kwa sauti ya kufifia, maana alizidi kudhofu, akanena, ‘Juu ya hiyo karatasi kumeandikwa yote yaliyoshindikwa juu ya kitambaa na hivyo ilinibidi kufanya kazi miaka hata kuweza kuisoma. Sikiliza: Babu yangu ambaye ilimlazimu kuutoka mji wa Lisbon alikuwa katika Wareno hao wa kwanza waliofika katika nchi hii.

Aliandika maneno hayo wakati alipokuwa akifa katika milima ile ambayo hapana hata Mzungu mmoja aliyepata kuikanyaga kwa miguu yake mpaka hivi leo. Jina lake lilikuwa Jose da Silvestre, naye aliishi miaka mia tatu, nyuma. Mtumishi wake aliyekuwa akimngojea upande huu wa milima aliona kuwa amekwisha kufa, nae ndiye aliyeleta maandishi haya mpaka Delagoa. Na tokea wakati huo yametunzwa na warithi wake, lakini hapana aliyetaka kuyasoma, mpaka mimi nilipofaulu. Nami nimepoteza maisha yangu kwa ajili yake, lakini labda mtu mwingine ataweza kufaulu na kuwa tajiri kupita watu wote duniani. Lakini usimpe mtu mwingine bwana, wewe nenda mwenyewe!’ Akaanza kuugua tena, na baada ya saa moja akafa. Mungu amrehemu. Nilimzika katika kaburi la kwenda chini sana, nikaweka na mawe makubwa juu ili kusudi asifukuliwe na fisi. Kisha nikaondoka pale.

Bwana Henry akauliza, na sauti yake ilionyesha jinsi alivyokuwa akisikiliza maneno yangu, ‘Ehe, lakini hiyo hati iko wapi? Naye Bwana Good akaongeza, ‘Hati hiyo iko wapi sasa, iliandikwa habari gani?’ Nikasema, ‘Mkitaka nitawasimulia habari zake. Nami sijamwonyesha hata mtu mmoja ila Mreno mmoja mfanya biashara aliyekuwa amelewa wakati alipoitafsiri, tena hakosi’ kuwa alikuwa amekwisha sahau habari zake ulevi ulipomtoka. Hicho kitambaa chenyewe nimekiweka kwangu Durban pamoja na hiyo karatasi aliyoifasiri marehemu Jose, lakini hapa ninayo tafsiri ya Kiingereza na nakala ya ramani iliyokuwamo, nayo ni hii:’

Mimi Jose da Silvestre nipo hapa ninakufa kwa njaa ndani, ya pango dogo katika upande wa kaskazini mwa titi la mlima ulio upande wa kusini wa milima miwili ambayo nimeipa jina la Maziwa ya Sheba. Naandika haya kwa kipande cha mfupa na wino wa damu yangu mwenyewe katika mwaka 1590. Ikiwa mtumishi wangu atakuja na kuiona na kuichukua mpaka Delagoa, nataka rafiki yangu (Na hapo katika hati, jina lake limefutika.) ampashe habari mfalme ili alete jeshi la askari watakaoweza kuvuka jangwa hili na kuwashinda hawa Wakukuana walio majabali sana na wenye uchawi mwingi. Lakini kwa sababu ya hila na udanganyifu wa Mchawi Gagula sikuweza kuleta kitu cha ushahidi, tena hata maisha yangu nayo nimeyaokoa kwa shida nyingi. Na huyu atakayekuja na afuate ramani, apande theluji ya ziwa la kushoto la Sheba mpaka afike penye titi, ambapo kwa upande huo wa kaskazini pana njia kuu iliyotengenezwa na Sulemani. Kutoka hapo ni mwendo wa siku tatu kufikia jumba la Mlalme. Basi na amwue Gagula. Nawe niombe dua.

Kwaheri. Jose da Silvestre.

Nilipokwisha soma barua na kuonyesha ile nakala ya ramani iliyoandikwa na Yule mzee kwa damu ya mkono wake, wakanyamaza kimya kwa ajili ya kustaajabu kwao. Baadae Bwana Good akasema, ‘Lo! Nimezunguka dunia mara mbili, tena nimefika bandari nyingi lakini sijapata kusikia hadithi kama hii hata vitabuni.’ Bwana Henry akasema, ‘Ni hadithi ya ajabu Bwana Quatermain. Natumai unajaribu kutuhadaa! Najua kwamba watu hudhani kuwa si vibaya kumhadaa mjinga.’ Niliposikia hivi nikaudhika, nikatwaa karatasi nikaiweka mfukoni, maana sikupenda kudhaniwa kuwa ni mmoja wa wale wapendao kusimulia uwongo na kuwahadithia wageni habari za kuwinda na mambo mengine ambayo hayakutokea kamwe. Basi nikajibu, ‘Kama unafikiri hivyo basi mambo yaishe hapa hapa. Nikasimama nikataka kwenda zangu. Bwana Henry akaniwekea mkono wake begani pangu akasema, ‘ Kaa, Bwana Quatermain, niwie radhi, usiudhike; kwani naona kuwa hupendi kutuhadaa, lakini hadithi yenyewe ni ya ajabu mno hata kwanza niliona vigumu kuisadiki.’

Basi ndipo nilipoanza kutulia kidogo, maana nilipofikiri niliona kuwa si ajabu kuwa yeye hawezi kusadiki hadithi, nikamwambia, Tutakapojaliwa kufika Durban utaona ramani ya asili na maandishi yake. Lakini bado sijakwambia habari za ndugu yako. Nilimjua Yule Jim aliyekuwa pamoja naye. Yeye ni Mbechuana, mwindaji hodari, tena na mtu mwenye busara. Siku hiyo Bwana Neville alipoanza safari yake nilimwona Jim amesimama karibu na gari langu akisokota tumbako yake, nikasema, ‘Jim, safari hii unakwenda wapi? Kuwinda ndovu?’ Akajibu ‘La! Tunakwenda kutafuta kitu kinachotafutwa sana zaidi ya pembe za ndovu.’ Mimi nikazidi kumdadisi, nikamuuliza, ‘Je, kitu hicho chaweza kuwa nini? Ni dhahabu? Akacheka akajibu, ‘siyo Bwana, ni kitu kinachotakiwa zaidi ya dhahabu.’

Basi sikumuuliza neno tena, maana sikupenda kuonekana kuwa ni mdaku. Baada ya Jim kuisha kusokota tumbako yake, akasema ‘Bwana, sisi tunakwenda kutafuta almasi.’ Nikasema, ‘Almasi! Lakini mbona unafuata njia ambayo si njia ya kwendea huko; kwa nini hufuati njia inayoendelea kwenye mashimo?’ Akajibu, ‘ Bwana, umepata kusikia habari za mlima wa Sulemani?’ Nikamjibu, ‘Ndiyo.’ Akaniuliza, ‘Umesikia habari za almasi zilizoko huko?’ Nikwamwambia, ‘Ni upuuzi tu.’ Akanena, ‘Si upuuzi,? Wana maana, namjua mwanamke aliyetoka huko, naye alifika Natal pamoja na mtoto wake, akaniambia; lakiniamekufa sasa.’

Nikamjibu, ‘Wewe na bwana wako mkijaribu kufika nchi ya Sulemani, hamkosi mtaliwa na tai.’ Akacheka, akasema, ‘Labda, bwana . Mtu amezaliwa naye atakufa; nami ningependa kutembea katika nchi ngeni; maana ndovu wanakwisha katika nchi hii.’ Nikasema, ‘Haya, tutaona.’ Baada ya nusu saa nikaona gari la Neville likitoka. Na baadae kidogo Jim akarudi mbio akasema, ‘Kwaheri bwana, kwani sikupenda kuanza safari bila kuagana nawe. Ninaona labda umesema kweli ya kuwa hatutasafiri kwenda kusini tena.’ Nikamuuliza, ‘Je, Jim, wasema kweli? Bwana wako amesema kuwa anakwenda mlima wa Sulemani, au sivyo?’ Akasema, ‘Ni kweli bwana maana aliniambia kuwa imempasa ajaribu kuchuma mali kwa njia yoyote; basi ni afadhali ajaribu kutafuta hiyo almasi.’ Nikasema, ‘Vema Jim, lakini ngoja kwanza, nataka uchukue barua hii, lakini lazima uahidi kuwa hutampa mpaka nifike Inyati.’ Kufika Inyati ilikuwa ni mwendo wa maili kama mia. Basi akaahidi. Nami nikachukua karatasi nikaandika maneno haya: ‘Kwa huyo atakayekuja ..apande theluji ya ziwa la kushoto la Sheba mpaka afike penye titi, ambapo kwa upande huo wa kaskazini pana njia kuu iliyotengenezwa na Sulemani.’

Basi nikampa, kisha nikamwambia, ‘Sasa utakapompa bwana wako barua hii, mwambie afuate sana shauri lililomo. Wala usimpe sasa barua hii kwa sababu sipendi arudi kuja kuniuliza maswali mengi ambayo sitaweza kuyajibu. Haya nenda.’ Basi Jim akaitwaa barua akaenda zake. Na hayo ndiyo yote ninayoyajua juu ya ndugu yako, Bwana Henry; lakini nachelea sana ya kuwa.. ‘Bwana Henry akasema, ‘Tazama, Bwana Quatermain, mimi ninakwenda kumtafuta ndugu yangu; nitamtafuta hata mlima wa Sulemani, hata nitaupita ikiwa ni lazima, mpaka hapo nitakapomwona au mpaka hapo nitakapo hakikisha ya kuwa amekufa; je, utafuatana nami?’

Nimekwisha sema kuwa mimi ni mtu wa taratibu , kweli na pengine ni mwoga kidogo, na haya yalinitia hofu. Maana safari kama hiyo iliyokusudiwa nilibaini kuwa ni kufa tu. Na tena juu ya hivyo nina mtoto anaenitegemea mimi kwa hivi sipendi nife. Basi nilijibu, ‘Hapana bwana, ahsante sana lakini naona ni afadhali nisiende. Sasa mimi ni mzee siwezi kusafiri safari ya kubahatisha hivyo, na tena naona mwisho wetu utakuwa kama ule wa rafiki yetu Silvestre. Mtoto wangu ananitegemea mimi, basi kwa hivyo sina haki ya kujitia katika hatari.’

Basi hapo wote wawili, yaani Bwana Henry na Bwana Good wakahuzunika sana, na Bwana Henry alisema, ‘Bwana Quatermain, mimi ni tajiri sana, nami nimenuia kusafiri ili nimtafute ndugu yangu, na kadhalika waweza kutaja mshahara wowote uutakao nami nitakupa kabla ya kuanza safari. Tena nitausia kuwa tukipatikana na ajali, mtoto wako atazamwe. Mradi sasa naona kwa maneno hayo utaweza kutambua jinsi tunavyo kuhitaji wewe ufuatane pamoja nasi. Tena ikiwa kwa bahati tutavumbua mahali pale palipo na almasi, basi hizo zitakuwa shirika wewe na Bwana Good, mimi sizitaki. Vile vile ikiwa tutapata pembe za ndovu. Waweza kutoa shauri na kufanya mapatano yoyote yanayokupendeza, na tena gharama zote za safari ni juu yangu mwenyewe.’ Nikajibu, ‘Bwana Henry, maneno yako ni mema kweli kweli, lakini lazima niyafikiri kwanza, maana mimi sina mali nyingi, pili kwa sababu najua kuwa ni kazi kubwa sana, basi nipe nafasi nipate kuyafikiri zaidi. Nitakupa jibu kabla hatujafika Durban.’ Bwana Henry akasema, ‘Vema.’ Nikamwambia kwa heri, nikaenda kulala, na nilipolala nilimwota Yule marehemu Silvestre na almasi!

SURA YA TATU UMBOPA AMEINGIA KAZINI

Kutoka Capetown mpaka Durban ni mwendo wa siku nne au tano kwa kadiri ya mwendo wa meli ulivyo, na hali ya baharini na upepo ilivyo. Pengine meli inacheleweshwa East London muda wa saa ishirini na nne ikiwa mawimbi ni makubwa na bahari imechafuka. Lakini safari hii hatukuwekwa kwa sababu mawimbi yalikuwa si makubwa ila ya kadiri tu, na matishari yaliletwa mara moja kuja kuteremsha shehena. Basi kwa muda huo wote tuliokuwa tukisafiri kwenda Natal nilikuwa nikifikiri sana maneno ya Bwana Henry. Hatukupata kuongea juu ya safari muda wa siku mbili tatu, ingawa nilimsimulia visa vingi vya safari zangu za kuwinda, na hivyo vyote vilikuwa vya kweli kabisa.

Basi siku moja jioni katika mwezi wa January, tulipita bara ya Natal, tukitarajia kuingia bandari ya Durban kabla ya kuchwa. Lakini tulikuwa hatukupima wakati vizuri, maana jua lilikuwa limeshuka kabisa wakati tulipotia nanga nje ya rasi, tukasikia mzinga wa kuonya watu wa Durban kuwa meli ya Kiingereza imekwishafika. Tulichelewa kuingia bandarini usiku ule, kwa hivi baada ya kuteremsha mifuko ya barua katika mashua, tulikaa mezani tukala kwa raha bila ghasia. Tulipopanda tena juu sitahani, mwezi ulikuwa umetoka na kung’aa vizuri juu ya bahari kadiri ya kufanya taa ya mnara kama si kitu. Kutoka pwani upepo ulileta, harufu nzuri ya matunda iliyonitia hamu ya kuimba nyimbo za dini kwa jinsi zilivyokuwa nzuri, na huko katika madirisha ya nyumba za pwani, taa kwa mamia zilitoa mwangaza.

Tukasikia sauti za mabaharia waliokuwa katika meli nyingine wakijitayarisha kung’oa nanga ili wawe tayari kushika majira yao. Sisi watatu, yaani Bwana Henry Curtis na Bwana Good na mimi tulikwenda karibu na usukani tukakaa kimya kwa muda, Na badae kidogo, bwana Henry akasema, ‘Je, Bwana Quatermain umekwisha yafikiri maneno yangu?’ Na Bwana Good akasema, ‘Ndiyo, waonaje Bwana Quatermain? Natumai kuwa utapenda kusafiri pamoja nasi mpaka Mashimo ya Sulemani, au popote alipofika Yule mtu jina lake Neville.

Nikaondoka nikagonga kiko changu ili kukikongoa tumbako. Nalikuwa bado sijakata shauri, mradi nikataka nafasi ya dakika moja nipate kukata shauri kabisa. Basi dakika ile ilinitosha, nikakaa tena nikasema, ‘Vema nitakwenda, na kama mkinipa ruhusa nitawaambia sababu zangu za kwenda, na vile vile nitawaambia kwa mapatano gani. Kwanza mapatano ni haya:
Utalipa gharama zote, na pembe za ndovu zozote na vitu vya thamani vyovyote vingine tutakavyo pata vitakuwa shirika kati ya Bwana Good na mimi, Yapili, unipe pauni mia tano mshahara wangu kabla ya kuanza safari, nami nitaahidi kukutumikiavema mpaka siku utakapoazimu kuacha safari, au mpaka tutakapofaulu, au mpaka tutakapofikwa na ajali.

Ya tatu, kabla ya kuanza safari utaandika hati ya kuahidi kumpa mtoto wangu anaeelimishwa katika hospitali ya London, pauni mia mbili mwaka kwa muda wa miaka mitano, wakati huo ndipo atakapoweza kufanya kazi mwenyewe, akiwa ana akili zake timamu. Basi ni haya tu, na labda utaona ninataka mengi.’
Bwana Henry akajibu, ‘Sidhani kuwa unataka mengi, nami nakubali kwa furaha hayo yote. Mimi nimekaza nia kwenda safari hiyo, nami nilikuwa tayari kukulipa zaidi, ili nipate msaada wako, maana maarifa uliyonayo wewe si ya kawaida, watu wengine hawana.’basi nikasema, ‘Wanifanya kusikitika kwa kuwa sikutaka zaidi! Lakini haidhuru, mimi siwezi kuvunja ahadi yangu.

Na sasa tumekwisha patana, nitakwambia kwa nini nimekubali kwenda. Kwanza, siku hizi zilizopita nilikuwa nikiwatizama sana nyinyi watu wawili, na ikiwa hamtaudhika, nitasema kuwa ninawapenda na tena nadhani kuwa tutapatana vema pamoja. Tena kupatana huku si jambo dogo katika safari ya siku nyingi kama hii tunayokusudia kufanya.

Na sasa kuhusu safari yenyewe, nasema waziwazi kuwa naona hatutarudi salama, yaani, kama tukijaribu kuvuka milima ya Sulemani. Kumbukeni yaliyompata mzee Silvestre miaka mia tatu nyuma, tena yaliyompata Yule mtu mmoja wa ukoo wake miaka ishirini iliyopita! Na sasa yapi yaliyompata ndugu yako? Nitakwambieni waziwazi kuwa mimi nadhani ajali yao itakuwa ndiyo yetu.’

Kisha nikawatazama kuona nini watakayoyafikiri wakisikia maneno yangu. Bwana Good akageuka uso kidogo, lakini Bwana Henry akawa imara kabisa, akasema, ‘Liwalo na liwe, lazima tubahatishe.’Mimi nikaendelea kusema, ‘ Labda utaona ajabu ya kuwa mimi ingawa nimesema maneno hayo, lakini nimekubali kwenda safari hii? Lakini nina sababu mbili. Kwanza, mimi ninaamini ya kuwa mwanadamu hana hiari, yalioandikwa yameandikwa. Ikiwa ajali yangu imefika itakuwa tu bila shaka. Ikiwa nilazima niende safari ya milima ya Sulemani na kuuawa, basi nitakwenda na kuuawa. Haikosi, Mungu mwenyewe anajua nia yake juu yangu, nami sina haja ya kushughulika juu yake.

Na sababu ya pili, ni kuwa mimi si tajiri. Yapata miaka arubaini nimefanya biashara na kuwinda bila kupata kitu isipokuwa riziki tu. Nyinyi mnajua ya kuwa watu huhesabu maisha ya mwindaji ndovu kuwa miaka minne, au mitano tu. Hivyo nimeishi vizazi saba vya watu wanaoshika kazi ninayofanya, nami naona kuwa wakati wangu wa kufariki hauwezi kuwa mbali sasa. Na sasa namna ninavyoishi, ikiwa nitapatwa na ajali yoyote, sina kitu chochote cha kumwachia mwanangu arithi. Lakini tokea sasa atatazamwa kwa muda wa miaka mitano. Basi hizo ndizo sababu zinazonivuta niende.’

Bwana Henry alisikiliza sana maneno yangu, kisha akajibu, ‘Bwana Quatermain, zile sababu ‘ulizotaja za kukubali safari hii, ingawa unafikiri kuwa mwisho wake ni kufa, zaonyesha kuwa wewe ni mtu thabiti kabisa. Kama yale unayoyafikiri yatatokea kuwa kweli itaonekana baadae. Lakini ikiwa yatatokea kuwa kweli au si kweli, mimi nimenuia kuendelea mpaka nione mwisho wake, ukiwa mtamu au ukiwa uchungu. Ikiwa ndiyo tutakufa, basi mimi naona ni afadhali na tupate furaha ya kuwinda kwanza, sivyo Bwana Good? Bwana Good akajibu, ‘Ndivyo, ndivyo. Sisi sote watu watatu tumezoea tangu zamani kuingia katika hatari za namna nyingi na kustahamili mashaka makuu.’

Basi tukashuka chini tukalala. Siku ya pili tulishuka kwenda pwani nikamchukua Bwana Henry na Bwana Good mpaka nyumba yangu ndogo niliyokuwa nimejenga huko Durban zamani. Yule mtu aliyekuwa akitunza nyumba na bustani ni mtumishi aitwae Jack. Alikuwa mtu wangu wa zamani. Aliwahi kuvunjwa paja na nyati katika nchi ya Sikukuni tulipokwenda kuwinda, nae hawezi kuwinda tena. Lakini anaweza kufanya kazi kidogo kidogo katika bustani.

Bwana Henry na Bwana Good walilala katika hema katika bustani yangu kwa sababu hapakuwa na nafasi ndaniya nyumba. Lakini lazima niendelee kusimulia hadithi yangu usije ukachoka. Mara niliponuia kwenda safari hiyo nilianza kutengeneza kila kitu tayari. Kwanza niliandikisha hati ile ya mapatano ili mwanangu apate haki yake ikiwa nitapatwa na ajali. Kisha nikapata zile pauni mia tano. Kisha nikafanya hivi, nikanunua gari na ng’ombe wa kulivuta. Gari lilikuwa refu sana, lina namna ya hema iliyofunika nusu ile ya gari iliyo nyuma, na mbele nafasi ilikuwapo ya kuwekea mizigo yetu. Katika hema ile palikuwa na kitanda kikubwa likichotosha watu wawili, na tena mahali pa kuwekea bunduki na vitu vingine. Kisha nilinunua ng’ombe wa Kizulu ishirini waliokwisha zoea magonjwa ya humo. Kwa kawaida kumi na sita wanatosha, lakini nilichukua wane zaidi kwa tahadhari ikiwa wengine wata kufa.

Kisha kufanya hivi ilikuwa kazi ya kufikiri namna ya chakula na dawa za kuchukua katika safari. Kwa bahati Bwana Good alikuwa amekwisha elimishwa kidogo katika elimu ya utabibu, nae alikuwa na kasha lake la dawa za kila namna. Kisha, tulitengeneza mipango ya bunduki na risasi za kufaa safarini, tukazichagua kwa uangalifu sana, maana kila mwindaji anajua kuwa bunduki na risasi ni jambo muhimu sana. Sasa tukaanza kuchagua watu watakaofuatana nasi katika safari yetu, na baada ya mashauri mengi tukachagua watano, mtu mmoja wa kuchunga ng’ombe, kiongozi mmoja, na watumishi watatu. Yule mchungaji na kiongozi tukawapata upesi, walikuwa Wazulu wawili, na majina yao yalikuwa Goza na Tom; lakini kupata watumishi ilikuwa taabu kidogo. Ilikuwa lazima kuwachagua watu waaminifu na hodari, maana pengine labda maisha yetu yatategemea walivyo.

Mwisho tulichagua wawili, mmoja alikuwa kabila la Hottentot jina lake Ventvogel, maana yake ‘Ndege wa upepo,’ na Yule wa pili alikuwa Mzulu mdogo aliyeitwa Khiva, naye alijua Kiingereza sana. Nilimjua Ventvogel, tangu zamani, alikuwa mtu hodari wa kusaka wanyama, akiweza kufuata nyayo zao kwa namna ya ajabu kabisa, tena alikuwa hachoki kabisa. Sasa tulikuwa tumekwisha chagua wawili, lakini wa tatu hatukuweza kumpata, tukanuia kuanza safari yetu na kujaribu kutafuta mwingine njiani.

Lakini siku moja kabla ya kuondoka, wakati wa jioni, Yule Mzulu Khiva aliniambia kuwa yupo mtu mmoja anataka kuonana nami. Basi tulipokwisha kula, nilimwambia Khiva amlete. Baadae kidogo mtu jamili mwenye umri wa kama miaka thelathini aliingia. Alikuwa mwekundu kuliko Wazulu walivyo. Aliingia akaniamkia kwa kuinua rungu lake, akakaa kitako katika pembe ya chumba.

Niliona ya kuwa alikuwa mtu mwenye cheo, maana kichwani alivaa methali ya taji iliyong’aa, ambayo inavaliwa na Wazulu wakiisha kupata umri fulani, au cheo Fulani. Tena nikaona kama ninamtambua sura yake. Baada ya kitambo, nilimuuliza, ‘Je, jina lako nani? Akajibu, ‘Umbopa.’ Na sauti yake ilikuwa nene na alitamka polepole. Nikasema, ‘Nadhani tumekwisha onana mahali zamani.’ Akajibu, ‘Ndiyo, umeniona katika mahali paitwapo ‘Isandhlwana’ (maana yake ni ‘Mkono mdogo’) siku ile iliyotangulia vita.’
Ndipo nilipomkumbuka.

Mimi nilikuwa mmoja wa viongozi wa Jemedari mmoja katika vita vya Wazulu, na yeye alikuwa mkubwa katika kikosi kidogo cha wenyeji, na siku moja aliniambia ya kuwa alifikiri kuwa kambi letu lina hatari. Mimi nikaona uchungu kidogo, nikamwambia afadhali na uwaachie mashauri kama hayo wakubwa wenye akili kupita zake; lakini baadae niliona kuwa maneno yake yalikuwa ya kweli. Basi nilimwambia, ‘Ndiyo, sasa nakukumbuka. Je, unataka nini?’ Akajibu, ‘Ni hivi Makumazahn (hilo ndilo jina walilonipa wenyeji, na maana yake ni ‘ Akeshaye usiku’. Nasikia ya kuwa unasafiri kaskazini pamoja na mabwana hawa waliotoka Ulaya. Je, ni kweli?’ Nikamwambia, ‘Ni kweli.’ Akasema, ‘Nimesikia ya kuwa utapita mto wa Lukanga ulio safari ya mwezi mmoja kupita nchi ya Manika. Ni kweli, Makumazahn?’
Nikaona ajabu, maana habari za safari yetu tulifanya kuwa ni siri, nikamuuliza, ‘Kwa nini unauliza habari za safari yetu?’ Akajibu, ‘Kwa sababu hata na mimi nataka kufuatana nanyi.

Jina langu ni Umbopa. Mimi ni Mzulu lakini si Mzulu. Ukoo wangu unatoka katika nchi ya kaskazini kabisa. Wametoka huko zamani, miaka elfu nyuma. Wazulu walipokuja hapa, zamani sana kabla ya kutawala Chaka. Mimi sina nyumba. Nimetembeatembea kwa muda wa miaka mingi. Nilikuwa mtu wa Setewayo katika kikosi cha Nkomabakosi, nilikuwa chini ya Umslopogaas (maana yake, ‘Mwenye shoka’) naye ndiye aliyenifundisha kupigana. Baadae nilikimbia kutoka nchi ya Wazulu kwa sababu nilitaka kuona mambo ya watu weupe. Kisha nilimpigania Setewayo katika vita. Na tangu wakati ule nimefanya kazi katika Natal na sasa nimechoka, nataka kurudi kaskazini tena. Hapa si kwangu. Sitaki mshahara , lakini mimi ni mtu hodari nami nadhani ninastahili kupewa nafasi katika safari yako.’ Kwa namna alivyosema nilitambua kuwa anasema kweli. Lakini nilikuwa na shaka kidogo kwa kuwa alitaka kuja bila ya kupata mshahara. Basi nikawaeleza Bwana Henry na Bwana Good, nikawataka wakate shauri.

Bwana Henry akamwambia asimame. Umbopa akasimama akavua koti kubwa alilokuwa kavaa, akasimama amevaa ngozi kiunoni tu na makucha ya simba shingoni. Hakika alikuwa mtu aliyeumbika kabisa wala sijaona mtu aliyependeza kupita yeye. Urefu wake ulikuwa futi sita na inchi tatu, nae alikuwa mpana kwa kadiri ya urefu wake. Alikuwa mwekundu wala si mweusi sana, isipokuwa alikuwa na makovu ya majeraha aliyopata katika vita. Bwana Henry akasimama karibu nae akamtazama usoni, akasema kwa Kiingereza, ‘Napenda watu walio kama wewe Umbopa, utakuwa mtumishi wangu.’ Umbopa akafahamu maneno yale, akasema, ‘Vema.’ Akamtazama namna alivyokuwa mkubwa na mpana, akasema, ‘Sisi ni wanaume, wewe na mimi.’
 
SURA YA NNE
Si nia yangu kueleza habari zote za safari yetu mpaka kufika mji wa Sitanda ulio karibu na mahali inapoungana mto Lukanga na mto Kalukwe. Maana ni safari ya zaidi ya maili elfu moja kutoka Durban, na sehemu ya mwisho wa safari, yaani mwendo wa maili mia tatu hivi tulikwenda kwa miguu kwa kuwa chafuo wengi wapo na ng’ombe wakiumwa nao hufa.

Tulitoka Durban mwisho wa mwezi wa Januari, na tulipofika Sitanda na kupiga kambi yetu, ilikuwa katikati ya mwezi wa Mei. Mambo yaliotokea ni kama yale yanayotokea katika kila safari katika nchi hii ya Afrika, ila jambo moja, na hilo nitaeleza baadaye. Tulipofika Inyati, ulio mji wa mwisho wa biashara katika nchi ya Matabele inayotawaliwa na Lobengula, tuliacha gari letu bila ya kutaka. Katika wale ng’ombe ishirini tulionunua, kumi na mbili tu walibaki. Mmoja aliumwa na nyoka, watatu walikufa kwa njaa na kiu: mmoja alitembeatembea akapotea, na watatu wengine walikufa kwa kula majani yenye sumu. Watano wengine waliugua kwa kula majani hayo hayo lakini tuliweza kuwaponya.

Basi tuliacha gari letu katika mikono ya Goza na Tom, yaani mchungaji na kiongozi, tukamwomba mtu wa Mission aliyekaa karibu aende kuwaangalia mara kwa mara, tukaanza safari yetu ya hatari pamoja na Umbopa, na Khiva, na Ventvogel na wapagazi sita tuliowaandika pale pale. Nakumbuka ya kuwa sote tulikuwa kimya kabisa tulipoanza safari hiyo. Nadhani sote tulikuwa tukifikiri labda hatutaliona gari lile tena; na mimi kwa hakika sikutumai kuliona tena. Kwa muda kidogo tulitembea kimya kabisa mpaka Umbopa aliyekuwa katangulia kidogo alianza kuimba wimbo wa Kizulu kuhusu watu hodari waliokuwa wamechoka kukaa hivi hivi tu, wakaanza safari ili watafute mambo mapya. Na kumbe, walipokuwa wamesafiri mbali sana katika jangwa waliona kuwa si jangwa ila ni mahali pazuri mno penye wanawali wazuri na ng’ombe walionona , na wanyama wa kuwinda porini, na adui wa kupigana nao. Basi sote tulianza kucheka tukaifanya kuwa ni njozi njema.

Umbopa alikuwa mcheshi na wakati mwingine alikaa akijisemea tu mwenyewe, nae aliweza kutuchangamsha sana kwa fikira zake. Sote tulimpenda sana. Na sasa lazima nisimulie habari za jambo nililotaja. Baada ya kupita juma mbili kutoka Inyati tulifika mahali pazuri katika mwitu. Miti mingi ya namna nyingi ilikuwa ikiota juu ya vilima, na miti mingi ilikuwa ikizaa matunda wanayopenda sana ndovu. Tukaona alama ya kuwa kweli wapo ndovu, maana wengine wameng’oa kabisa miti wapate kula matunda yake ndovu ni mlaji mharibifu sana.

Jioni moja, baada ya kufanya safari ndefu, tulitokea mahali pazuri chini ya kilima penye mto wa maji matamu kabisa. Mara tulipoingia katika mto tukaona kundi la twiga wakitoka: mbio’ kwa mwendo wao wa kuchekesha, na mikia yao imeinuka juu. Walikuwa mbali, hatua mia nne hivi na kwa hivyo ilikuwa mbali kuweza kuwapiga bunduki, lakini Bwana Good aliyekuwa katangulia hakuweza kujizuia, akaona lazima ajaribu kuwapiga.

Akaelekeza bunduki yake na kwa bahati alimpiga mmoja aliyekuwa nyuma kidogo. Risasi ikampiga shingoni akaanguka kichwa chini, kama sungura tu. Basi ustadi wa Bwana Good ulihakikishwa tokea siku ile, lakini kwa kweli alikuwa hana shabaha hata kidogo. Ikawa baadae kila mara alipomkosa mnyama, tulimsamehe kwa sababu ya kumpiga Yule twiga. Basi tukawatuma wapagazi watengeneze riyama ya Yule twiga, nasi tukaanza kutengeneza kambi yetu. Kambi yenyewe ilikuwa boma la miiba, na katikati tulitandaza majani makavu ya kulalia, tukakoka moto mwingi wa kuzunguka kambi.

Basi tulipokuwa tumekwisha tengeneza kambi, mwezi ukatoka na chakula chetu cha nyama ya twiga na mafuta ya mifupa yake kilikuwa tayari. Tulifurahi sana kula mafuta yale ya twiga, lakini ilikuwa kazi kuivunja jinsi ilivyokuwa migumu. Nadhani hapana chakula kitamu kama mafuta ya mifupa ya twiga, ila labda moyo wa ndovu.

Tulikula chakula chetu kwa mwangaza wa mbalamwezi, na mara kwa mara tulimsifu Bwana Good kwa shabaha yake; kisha tukakaa tukavuta tumbako na kusimuliana hadithi. Ungalituona ungalistaajabu tulivyokaa. Mimi nywele zangu zaanza kuwa na mvi, na Bwana Henry zake zilizo na rangi ya kimanjano zaanza kuwa ndefu na hatukufanana hata kidogo. Maana yeye ni mrefu, mweupe mpana, na mzito; lakini mimi ni mfupi, mweusi, mwembamba na mwepesi. Lakini labda aliyekuwa mcheshi zaidi ni Bwana Good. Alikaa juu ya mfuko wa ngozi kama ndiyo kwanza amerudi kutoka safari ya kuwinda kwao Ulaya, maana alikuwa maridadi sana, safi kabisa; nae amevaa vizuri. Alikuwa amevaa nguo za kizungu, na kofia vile vile iliyopatana na nguo zake, tena amenyoa vizuri na amevaa miwani yake ya jicho moja.

Basi tulikaa sisi watatu tukizungumza huku tukiwatazama watu wetu waliokuwa wamekaa karibu wakivuta tumbako yao, hata wakaanza mmoja mmoja kujifunika blanketi na kulala penye moto, ila Umbopa aliyekaa mbali kidogo peke yake kashika tama anafikiri. Niliona kuwa hachanganyiki kabisa na wenzake. Baadae kidogo kwa nyuma yetu tulisikia sauti, ‘Woof, Woof!’ Nikasema kuwa huyu ni simba, tukakaa tunasikiliza na mara kutoka mahali penye mto tulisikia sauti ya ndovu. ‘Unkungunklovo! Ndovu!’ Kikasisikia watu wetu wakinong’ozana, ‘Ndovu! Na baadae kidogo tukamwona wameandamana kama vivuli vikubwa wakitoka penye maji wanakwenda mwituni. Mara moja Bwana Good aliruka akataka kuwafuata. Nadhani labda alifikiri kuwa kumpiga ndovu ni sawasawa na kupiga twiga, lakini nilimshika mkono nikamwambia, ‘Waache waende zao.’ Basi Bwana Henry akasema, ‘Naona ni pahali pazuri hapa pa kuwinda wanyama, ni afadhali na tukae siku mbili tatu tuwinde.’ Nikasema, ‘ Vema, nadhani tunataka kujiburudisha kidogo, lakini sasa na tulale tuamke asubuhi na mapema na labda tutawaona wale ndovu kabla hawajaenda mbali.’

Tukajifunika na mablanketi yetu, tukalala. Mara nilisikia kishindo, nikashtuka na sote tuliruka na kutazama kwenye moto. Tukasikia kelele nyingi na mingurumo mingi sana kama nyama wanavutana. Tulijua kuwa hapana ila simba anayeweza kunguruma hivyo, tukazidi kutazama. Macho yalipozoea giza, mara tuliona mchanganyiko wa vivuli vyeusi na vya kimanjano vinatujia. Tukashika bunduki zetu tukavaa viatu vyetu tukatoka kambini kutazama kunanini. Sasa mchanganyiko wa vivuli ulianguka chini ukagalagala na tulipofika pale ulilala kimya.

Sasa tuliweza kuona ni kitu gani. Pale chini tuliona kulungu amekufa kabisa, na juu ya pembe zake amechomeka simba dume mkubwa naye vile vile amekwisha kufa. Nadhani yaliyotokea ni hivi: Yule kulungu alikuja kunywa maji, na Yule simba alikuwa pale akimvizia, akamrukia na akanaswa na pembe zake. Sasa Yule simba hakuweza kujitoa, lakini akageuka na kumuuma Yule kulungu mgongoni na shingoni, naye kulungu alikimbia mbio mpaka akaanguka na kufa.

Tulipokwisha tazama, tuliwaita watu wetu wawavute wanyama wale mpaka kambini, tukalala tena mpaka asubuhi. Kulipopambazuka tu! Tuliondoka tukafunga safari kwenda kuwinda. Tulichukua bunduki kubwa tatu na risasi nyingi, tukaweka chai baridi katika viriba vyetu vya maji. Baada ya kufungua kinywa kwa haraka, tuliondoka tukafuatana na Umbopa na Khiva na Ventvogel.

Tuliwaacha watu wengine kambini kuchuna ngozi ya Yule simba na kukatakata nyama ya Yule kulungu. Hatukuona shida kufuata nyayo za ndovu, na Ventvogel alikisia kuwa walikuwa ndovu ishirini au thelathini katika kundi lile, na wengi ni dume wakubwa. Tulikwenda mbali sana, na ilipopata karibu na saa tatu tulikuwa tumelowa jasho, lakini tulijua kuwa sasa hawako mbali. Tulifahamu hivyo kwa sababu ya miti iliyovunjika na kwa sababu mavi yao yalikuwa bado moto.

Baadae tukaliona kundi, tukaona kuwa kweli wapo ishirini au thelathini, nao wamesimama katika bonde wamekwisha kula, wanapunga masikio yao makubwa. Ilikuwa shani kubwa kuwaona, maana walikuwa karibu, kadiri ya hatua mia mbili na hamsini tu. Nikainama nikatwaa majani makavu kidogo nikayatupa juu hewani ili nipate kujua upepo unatoka upande upi; maana nilijua kuwa wakisikia harufu yetu watakimbia nasi hatutapata nafasi kuwapiga.

Basi nikaona kuwa upepo unatoka kwao, tukatambaa chini na kwa kuwa majani yalikuwa marefu tuliweza kuwakaribia mpaka kufika kiasi hatua hamsini hivi. Pale mbele yetu ndovu wakubwa dume wenye pembe kubwa sana walikuwa wamesimama. Nikanong’ona kumwambia Bwana Henry amlenge ‘yule wa upande wa kushoto, na Bwana Good achague Yule wa upande wa kulia, na mimi nikamlenga Yule wa katikati.

Nikasema , ‘Piga.’ Na mara bunduki zote tatu zikalia pamoja, na ndovu wa Bwana Henry alianguka amekufa, risasi imempenya moyo. Ndovu wangu aliangukia magoti, nikafikiria kama anakufa, lakini mara akasimama tena akaja mbio akanipita kabisa, lakini alipokuwa akinipita, nilimpiga risasi ya mbavu akaanguka. Basi nilimkaribia nikampiga ya kichwa kummaliza kabisa na kukomesha maumivu yake. Kisha niligeuka nimtazame Bwana Good, maana nilipokuwa nikimpiga ndovu wangu nilisikia ndovu akilia kwa hasira na maumivu. Nilipomfikia Bwana Good nilimwona ameingiwa na wasi wasi kabisa. Ikaonekana kuwa mara alipopiga ndovu wake ndovu huyo akaja mbio kumtafuta, nae Bwana Good alikuwa na shida ya kujiokoa. Kisha ndovu alikwenda mbio akifuata njia ya kwendea kambi yetu. Huku nyuma kundi zima lilikimbilia porini.

Kwa muda kidogo tulifikiri, tufuate kundi au tumfuate Yule aliyejeruhiwa, ndipo tulipokata shauri kufuata kundi, tukafikiri kuwa hatutamwona tena Yule ndovu mkubwa. Na toka siku ile ninatamani laiti kwamba tusingalimwona tena. Ilikuwa kazi nyepesi kufuata kundi, maana njia walimopita ilikuwa wazi kabisa kwa jinsi walivyokimbia.

Lakini kuwafikia tena ilikuwa kazi, tukafanya kazi ngumu kwa muda wa saa mbili kabla ya kuwafikia tena. Wote walikuwa wamesimama pamoja ila dume mmoja, nao kwa namna walivyoinua mikonga yao mara kwa mara kunusa nikajua kuwa wamefahamu kuwa hatari ipo karibu. Yule dume alikuwa amesimama yapata hatua hamsini kutoka kundi na hatua sitini kutoka sisi tulipo, akawa amesimama kama analinda zamu.

Nikadhani labda tukikaribia zaidi atasikia harufu yetu,. Basi nikawaambia wenzangu afadhali sote tumpige pamoja. Tukapiga na mara moja akaanguka amekwisha kufa. Basi lile kundi likashtuka likakimbia, lakini walifuata njia iliyowaongoza katika bonde, na mwinuko wa upande wa pili ulikuwa umekwenda juu sana. Basi tulipofika karibu tukawakuta wameshangaa kabisa na kusukumana na kupigana na kupiga kelele wakitafuta njia ya kuokoka.

Basi sasa tulipata wasaa; tukawapiga tukawaua watano. Kisha wakatoka kwa njia nyingine nasi kwa kuwa tumekwisha choka hatukuwafuata tena, maana ndovu wanane kwa siku moja walitosha kabisa. Baada ya kupumzika kidogo, watu wetu waliwakata ndovu wawili wakachukua mioyo yao kuwa chakula cha jioni, tukarudi kambini tukifurahiya kazi za mchana, na tukakusudia kupeleka watu kutoa pembe zote asubuhi. Tulipopita mahali pale tulipopiga wale ndovu wa kwanza, tuliona kundi la wanyama wengine, lakini hatukuwapiga, maana nyama tuliyokuwa nayo ilitosha kabisa. Lakini Bwana Good alitaka kuwakaribia ili awatazame vizuri maana alikuwa bado hajaona namana yao, akampa Umbopa bunduki yake, naye alifuatana na Khiva akaingia mwituni na sisi tulikaa tukiwangoja.

Jua lilikuwa linaanza kutua, likawa jekundu kabisa na Bwana Henry na mimi tukakaa tukitazama uzuri wake, na mara tulisikia ndovu analia, tukamwona anakuja mbio kabisa, mkonga na mkia juu hewani. Tena tukaona jambo jingine, tukaona Bwana Good na Khiva wanakuja mbio na Yule ndovu anawafuata. Tukaona kumbe ni Yule mkubwa aliyejeruhiwa na Bwana Good.

Kwa muda tulishangaa, maana hatukuweza kupiga bunduki kwa kuogopa kuwapiga Bwana Good na Khiva. Hapo jambo la kutisha sana likatokea, Bwana Good aliteleza akaanguka pale pale mbele ya miguu ya Yule ndovu.
Roho zilikuwa si zetu kwa hofu, tukamkimbilia tulivyoweza. Katika muda wa nukta tatu, mambo yangalikuwa yamekwisha, lakini hayakutokea kama tulivyodhania. Maana, Khiva mara alipoona kuwa Bwana Good ameanguka akageuka akatupa mkuki wake usoni pa ndovu, ukampiga mkonga.

Yule ndovu akalia kwa maumivu, akamshika Khiva akamtupa chini, akaweka mguu mmoja juu yake, akamzungushia mkonga wake akamvunja sehemu mbili. Sisi tulishikwa kama na wazimu kwa chuki, Yule ndovu tukampiga bunduki tena na tena, na mwishowe akamwangukia Yule mtu aliye muua. Bwana Good akaondoka akatikisa mikono yake juu ya Yule mtu hodari aliyemwokoa kwa kujitolea maisha yake, na hata mimi niliyezoea sana mambo ya hatari niliona kwikwi ikinipanda kooni. Umbopa akasimama akatazama maiti ya ndovu mkubwa na vipande vya maiti ya maskini Khiva, na baadae kidogo akasema, ‘Amekufa, lakini amekufa kiume!’
 
SURA YA TANO
SAFARI YETU YA JANGWANI
Tulikuwa tumeua ndovu tisa, ikachukua kazi ya siku mbili kutoa pembe zao. Tulipokwisha kuzitoa tulizileta kambini tukachimba shimo chini ya mti mkubwa tukaziweka humo tukafukia shimo. Pembe zilikuwa nzuri kabisa, nadhani sijaona namna yake, maana zile za Yule mkubwa aliyemuua Khiva zilikuwa yapata ratili mia na sabini, kadiri tulivyoweza kukisia. Na marehemu Khiva tulimzika katika kaburi pamoja na sagai lake kama ilivyo desturi, yaani apate kujitetea katika safari yake ndefu kwenda ahera. Siku ya tatu tuliondoka tukafunga safari yetu tukitumaini kuwa tutarudi salama na kuchimbua pembe zetu. Baada ya safari ndefu ya kuchosha tulifika mji wa Sitanda karibu na mto wa Lukanga, na hapo kwa kweli ni mwanzo wa safari yetu. Nakumbuka sana siku ile tuliyofika huko.

Kwa upande wa kulia zilikuwa nyumba chache zimetawanyika pamoja na mazizi ya ng’ombe, na karibu na mto yalikuwapo mashamba ya wenyeji. Kupita mashamba hayo ni mwitu wenye majani marefu umejaa wanyama wa porini. Upande wa kushoto palikuwa jangwa lile kubwa. Hapo paonekana kwamba ni mwisho wa ardhi inayofaa kuoteshwa vitu, siwezi kujua kwa sababu gani, lakini ndivyo ilivyo.

Upande wa chini ya kambi yetu maji yalitiririka katika mto mdogo, na ng’ambo yamto palikuwa mteremko wenye mawe mengi. Huu ndio ulikuwa mteremko ule ule nilipomwona Yule Silvestre akitambaa kwa mikono na magoti miaka ishirini nyuma, yaani aliporudi katika safari yake ya kutafuta Mashimo ya Sulemani. Na kupita mteremko huo ni jangwa lile lisilo na maji, jangwa la ukiwa kabisa.

Tulipo piga kambi yetu ilikuwa ni jioni, na jua lilikuwa likizama, mfano wa mpira mkubwa mwekundu. Mishale ya nuru ya rangi mbali mbali ilitoka ikaenea jangwani. Bwana Henry na mimi tulimwacha Bwana Good atengeneze kambi, nasi tulipanda mteremko ule tukasimama tukitazama jangwa.

Mbingu zilikuwa nyeupe kabisa, na mbali sana tuliweza kuona milima ya Sulemani kama vivuli vikubwa, na wakati mwingine kuona theluji juu ya vilele vyake. Basi nikasema, ‘Kule ndipo upo ukuta unaozunguka Mashimo ya Sulemani, lakini anaejua kama tutaweza kuupita ni Mungu tu.’ Bwana Henry akasema, ‘Nadhani ndugu yangu yupo, na ikiwa yupo basi tutaonana, lazima.’ Nikasema, ‘InshaIlah.’

Tukageuka turudi kambini, nikaona kuwa sisi hatupo pekee yetu, maana nilimwona Umbopa amesimama nyuma yetu na macho yake ameyakodolea milima ile ya mbali. Umbopa alipoona tumemwona, akamwambia Bwana Henry, ‘Je, Inkubu, ile ndiyo nchi unayotaka kufika?’ (na jina la Inkubu ndilo jina walilomwita wenyeji, nadhani maana yake ni ‘ndovu’).

Basi Bwana Henry, akajibu, ‘Ndiyo ile nchi ninayokwenda.’ Umbopa akasema , ‘Inkubu, jangwa ni pan asana, tena hapana maji kabisa, milima ni mirefu sana na vilele vyake vimefunikwa na theluji, na mwanadamu hawezi kukisia kuna nini pale nyuma pale linaposhukia jua; utafika huko kwa njia gani, na kwa nini unataka kwenda?’

Basi nilimtafsiria maneno yale yote, na Bwana Henry akasema, Mwambie ya kuwa na kwenda kumtafuta ndugu yangu aliyenitangulia.’ Umbopa akasema, ‘Inkubu, ni kweli: maana njiani nilikutana na mtu mmoja kabila lake Hottentot akaniambia kuwa miaka miwili nyuma Mzungu mmoja alianza kuvuka jangwa amefuatana na mtumishi mmoja, nao hawakurudi.’ Bwana Henry akamuuliza, ‘Je, waona ya kuwa huyo ni ndugu yangu?’
Umbopa akajibu, ‘La, bwana sijui, ila nilipomuuliza Yule mtu yu wanamna gani, akajibu kuwa ana macho kama yako, lakini ndevu zake ni nyeusi, na tena amefuatana na mtumishi mmoja Mbechuana jina lake Jim.’

Basi nilipotafsiri maneno haya nikasema, ‘ Ndhani ‘ndiye bila shaka, maana mimi namjua Jim tangu zamani.’ Basi Bwana Henry akatikisa kichwa akasema, ‘Mimi nilijua hakika, maana ndugu yangu akitia nia yake kutenda jambo atalitenda. Ikiwa alitaka kuvuka milima ya Sulemani basi amekwisha kuivuka isipokuwa amezuiwa na jambo.

Na kwa hivi lazima tumtafute upande wa pili.’ Umbopa alifahamu Kiingereza ingawa hakukisema ila mara chache, akasema, ‘Inkubu, ni safari ndefu.’ Bwana Henry akajibu, ‘Ndiyo ni mbali, lakini hakuna jambo duniani asiloweza kufanya ‘mwanadamu ikiwa amedhamiria kulifanya.

Umbopa, ikiwa mapenzi yanamvuta mtu naye yu tayari kukosa maisha yake kama kwamba si kitu, hakuna jambo asiloweza kulitenda, hakuna milima asiyoweza kuipanda, hakuna jangwa asiloweza kulivuka, ila mlima mmoja na jangwa moja ambalo wewe hulijui.’ Nilipoyatafsiri maneno hayo , Umbopa alijibu, ‘Maneno makubwa, baba yangu, maneno yanapovuma kweli yanayostahili kusemwa na mwanaume. Umesema kweli, Inkubu baba yangu.

Sikiliza! Maisha ni kitu gani? Ni unyoya, ni mbegu ya majani, ikipeperushwa huko na huko, pengine huzaa na kujizidisha na ikisha kufanya hivyo hufa, pengine huchukuliwa mawinguni. Lakini ikiwa mbegu ni njema na nzito, huenda itasafiri kidogo katika njia ambayo inataka. Ni vizuri kujaribu kusafiri katika njia yako na kushindana na ajali. Kila mtu ameandikiwa kufa. Kama mambo yamezidi, basi hufa upesi kidogo zaidi tu. Baba yangu, nitafuatana nawe kuvuka jangwa na milima mpaka nitakapozuiwa na ajali njiani
 
Hapo alinyamaza kimya kidogo, na baadae akaendelea kutoa hotuba yake kama ilivyo desturi ya Wazulu. ‘Maisha ni kitu gani? Niambieni, Ee Wazungu, nyinyi wenye busara, nyinyi mjuao siri za dunia, na dunia ya nyota, na dunia iliyo juu na kuzunguka nyota; nyinyi mpelekao maneno yenu mbali bila kutumia sauti; niambieni, Ee nyinyi Wazungu, siri ya maisha yetu ni nini huenda wapi, hutoka wapi? Hamwezi kunipa jawabu; hamjui! Sikilizeni, nitawaambia. Maisha ni mkono tunaotumia kukinga mauti.

Ni kimulimuli kinachong’aa wakati wa usiku; ni kama pumzi nyeupe za ng’ombe zinazoonekana wakati wa baridi; ni kivuli kidogo kile kinachokimbia katika majani na kupotea katika jua hapo linaposhuka.’

Bwana Henry akasema, ‘Wewe Umbopa ni mtu wa ajabu.’ Umbopa akacheka kidogo akasema, ‘Huoni kuwa wewe na mimi tumefanana sana. Huenda hata na mimi nakwenda kuvuka milima ile ili kumtafuta ndugu yangu!; Nikamtazama sana nikamuuliza, ‘Je, maneno gani hayo, maana yake ni nini? Wewe unajua habari gani ya ile milima? Akajibu, ‘Kidogotu, kidogo sana.

Ni nchi ngeni kabisa, nchi ya uchawi na vitu vizuri; nchi ya watu hodari na miti na vilele vya theluji na njia nyeupe kubwa. Nimesikia habari zake, lakini iko faida gani kusema.? Sasa giza linashuka. Wale watakaoishi kuona wataiona.’ Nikamtazama tena, maana ilinibainika kuwa anajua habari zaidi. Alifahamu ninayoyafikiri, akasema, ‘Usiniogope, Makumazahn, mimi sitegi mitego upate kutegwa.

Mimi sifanyi hila. Ikiwa tutajaaliwa kuvuka milima ile iliyo nyuma ya jua, nitakwambia yote ninayoyajua. Lakini mauti yamekaa juu ya milima ile. Uwe na busara, urudi nyuma, nendeni mkawinde ndovu, mabwana. Nimesema.’

Na bila kusema neon jingine, aliinua sagai lake kutuaga akageuka akarudi kambini, na baadaye tulimkuta huko anasafisha bunduki kama wale watu wengine, Bwana Henry akasema, ‘Mtu huyu wa ajabu sana.’ Nikasema, ‘Ndiyo, nampenda kama simpendi.

Ajua neno lakini hataki kulisema. Lakini ya nini kugombana naye! Safari yetu ni ya ajabu na Mzulu wa ajabu hawezi kuzidisha ajabu yake.’ Siku ya pili tulifanya vitu vyote tayari kuanza safari yetu. Hatukuweza kuchukua bunduki nzito tukaziacha pamoja na vitu vingine kwa wapagazi wetu, tukafanya shauri kuwaacha katika nyumba ya mtu mmoja aliyekaa karibu.

Sikupenda kabisa kuviacha vitu hivyo, maana Yule mtu alivitazama kwa macho ya uroho sana, lakini nilifanya hila. Kwanza nilishindilia bunduki zote, nikaziweka tayari kupigwa, nikamwambia kuwa akizigusa hata kidogo, basi zitalia.

Yeye hakusadiki, na mara ile akashika moja, na kama nilivyomwonya, ikalia, na risasi ikampiga ng’ombe wake mmoja, na vile vile kishindo chake kikamwangusha chini. Akainuka upesi ameshtuka kabisa tena anaona uchungu kwa kupata hasara ya ng’ombe wake, akataka nimlipe, lakini hakutaka kabisa kugusa tena bunduki.

Akasema, ‘Weka shetani wale katika majani ya paa la nyumba au zitatuua sote.’ Nikamwambia kuwa tutakaporudi nikiona kuwa moja imepotea nitamuua yeye na watu wake wote kwa uchawi; na ikiwa haturudi naye akijaribu kuiba bunduki, basi vivuli vyetu vitakuja kumfuata na kuwatia wazimu ng’ombe wake, na kuharibu maziwa yao kabisa, mpaka maisha yake yatakuwa na udhia mtupu! baada ya hayo, akaapa kuwa atazitunza awezavyo.

Basi tukisha kuweka vitu vyetu salama, tulifunga mizigo midogo, tukawachagua Umbopa na Ventvogel wafuatane nasi, tukawa watano, yaani, Bwana Henry, Bwana Good, mimi na Umbopa na Ventvogel. Hatukuchukua vitu vingi, tulipunguza mzigo kadiri tulivyoweza. Tulichukua bunduki tano na bastola tatu, na viriba vya maji vitano, na mablanketi matano, na nyama kavu na shanga za kutoa zawadi, na dawa.

Tena tukachukua visu vyetu na vitu vidogo vidogo kama vile dira na vibiriti na tumbako. Basi vitu hivyo pamoja na nguo tulizokuwa tukivaa ndivyo tulivyo chukua, basi, Siku ya pili hatukufanya kitu, tulipumzika tu, na jua liliposhuka tuliamka tukala, tukafunga vitu vyote tayari, tukalala tena kungojea mbalamwezi.

Yapata saa tatu mwezi ukatoka ukaangaza nchi nzima na mbele yetu tukaona lile jangwa kubwa la kutisha sana. Tukaondoka, na baada ya dakika chache tukawa tayari, lakini hata sasa tulisita kidogo kama ilivyo desturi, ya kibinadamu ikiwa anaanza safari ya hatari. Sisi watu watatu tulisimama pamoja.

Umbopa akasimama mbele kidogo ameshika sagai lake mkononi na bunduki ameweka begani analitazama sana jangwa; na Ventvogel na watu watatu waliokubali kufuatana nasi kuchukua vibuyu vya maji kwa safari ya siku ya kwanza wakasimama pamoja nyuma yetu.

Basi Bwana Henry akasema, ‘Rafiki zangu, sasa tu tayari kuanza safari yetu ya ajabu. Labda hatutafaulu. Lakini sisi ni watu watatu, nasi tutashirikiana katika mambo mema na maovu mpaka mwisho, Na sasa kabla hatujaanza, na tumwombe Mungu anayeumba na kuandika ajali za wanadamu, ambaye tangu zamani amekwisha amuru njia zetu, atuongoze miguu yetu kama apendavyo.’

Akavua kofia yake na Bwana Good pia akavua yake, wakasimama kimya kwa muda. Mimi si mtu wa kuomba, nadhani wawindaji wachache sana huwa wa namna hiyo; wala sijamsikia Bwana Henry akisema namna hiyo lakini nadhani katika moyo wake ni mtu wa dini. Bwana Good vile vile ni mtu wa dini. Lakini siwezi kukumbuka hata siku moja niliyoomba kama nilivyoomba siku ile. Na lazima nikiri kuwa niliona faraja kwa kuomba hivyo.

Maana yaliyo mbele yetu hatukuyajua, na siku zote mambo yanayotisha na yasiyojulikana huvuta wanadamu wamkaribie Muumba wao. Kisha Bwana Henry akasema, ‘ Haya twendeni!’ Tukaanza safari yetu.

Hatukuwa na kiongozi ila milima ya mbali na ile ramani aliyoandika mzee Jose da Silvestre, na kwa kuwa iliandikwa na mtu aliyekuwa akifa juu ya kipande cha kitambaa miaka mia tatu iliyopita, haikuwa kiongozi cha kutia moyo sana.

Lakini hii ndiyo iliyokuwa tama yetu kufaulu. Tukikosa kuliona ziwa lile la maji machafu ambayo alama yake ilionyesha kuwa ni katikati ya jangwa, basi haikosi tutakufa kwa kiu.
Na nilifikiri kuwa bahati ya kuliona haiwezi kutumainiwa sana.

Na hata ikiwa Yule mzee da Silvestre alipima sawasawa na kufanya alama barabara katika ramani, je, baada ya miaka hii yote iliyopita sip engine limekauka,au labda wanyama wa porini wamekwisha kuyakanyaga maji mpaka yamekwisha, au labda yamekwisha kufunikwa na mchanga uliyopeperushwa na upepo? Basi tukaenda, tukaenda, usiku tukikanyaga mchanga na majani yale yaliyosokotana sokotana yalitunasa miguuni, na mchanga uliingia katika viatu vyetu ikawa mara kwa mara kusimama tupate kuutoa.

Basi hivi hivi tulisafiri, na Bwana Good alijaribu kututia moyo kwa kupiga mbinja, lakini sauti yake ilizidi kututia huzuni tu, akaacha. Baadae kidogo jambo lilitokea lililotushtua sana kwanza, lakini kisha lilituchekesha mno. Tulikuwa tukifuatana mmoja mmoja na Bwana Good ametangulia, mara nilisikia sauti yake inafifia kabisa, na tena tukasikia kelele na ghasia, na mkoromo na mguno na vishindo vya miguu. Katika giza tuliweza kuona kama vivuli vinakimbia vimefichwa kidogo kwa mavumbi ya mchanga.


Bwana Henry na mimi tulisimama tumeshangaa; na mshangao wetu ulizidi tulipoona Bwana Good anakwenda mbio kuelekea milima, juu ya kitu tulichodhani kuwa ni kama farasi, akipiga makelele moja kwa moja. Mara tulimwona ametupa mikono juu, tukamsikia akianguka chini kwa kishindo. Ndipo nilipotambua kuna nini; tulikuwa tumetokea kwenye kundi la punda milia waliokuwa wamelala, na Bwana Good alianguka juu ya mgongo wa mmoja ambaye aliamka akamchukua mgongoni mwake.


Nikawaambia watu wetu wasiogope, nikamkimbilia Bwana Good nikichelea kuwa labda ameumia, lakini nilifurahi nilipoona kuwa amekaa kitako juu, ya mchanga ameshangaa na kuogopa sana. Lakini hakuumia, Baada ya hayo tulikwenda bila ya kupatwa na jambo jingine mpaka saa saba hivi, tukapumzika kidogo tukanywa maji kidogo na baada ya kupumzika kwa muda wa nusu, ambaye mpaka sasa alikuwa akituchekesha mara kwa mara alinyamaza tu.


Basi ilipopata saa nane, tukafika kwenye kile kilima kidogo, tumechoka kabisa, na hapo tulikaa na kwa sababu kiu kilituzidi, tulimaliza maji yote. Tena hayakutosha . Basi tukalala, Nilipokuwa katika kusinzia, nilisikia Umbopa akisema peke yake, ‘Kama hatupati maji kesho kabla mwezi haujapanda mawinguni, basi tutakuwa maiti.’ Joto lilikuwa jingi sana, lakini hata hivyo nilitetemeka kama mtu aliyeshikwa na baridi. Maana kutarajia mauti si vizuri, na hasa mauti ya namna ile. Lakini hata fikira za mauti hazikuweza kunizuia nisipatwe na usingizi, nikalala.
 
SURA YA SITA


Ilipopata saa kumi za usiku niliamka baada ya kulala kwa muda wa saa mbili tu, na sasa haja ya kwanza ya mwili, yaani kupumzika, imetimizwa. Maumivu yale mengine ya kiu yalianza kuniudhi, nami sikuweza kupata usingizi tena.

Kabla ya kuamka nilikuwa nikiota ndoto ya kuwa ninaoga katika mto wa maji mazuri yanayopita, na kando ya mto miti mizuri inaota, Kumbe! Niliamka kujiona katika jangwa la ukiwa, kavu kabisa, nakumbuka yale maneno aliyosema Umbopa kuwa kama hatupati maji leo tutakufa kifo kibaya. Hapana mwanadamu aliyeweza kuishi katika nchi ya joto kama lile jangwa bila maji ya kunywa.

Nilikaa nikasugua uso wangu uliokuwa mchafu kwa mikono yangu iliyokuwa mikavu kabisa. Midomo na kope zangu zilikuwa zimegandamana kabisa, nikaweza kuyafumbua macho kwa shida. Mapambazuko yalikuwa karibu, lakini baridi ile tunayozoea kuona asubuhi haikuwapo kabisa, na hewa ilikuwa nzito na nene jinsi nisivyoweza kueleza.
Wenzangu walikuwa wamelala.

Baadaye kukaanza kupambazuka, na ili nipate kusahau kiu yangu, nilitoa kitabu kidogo nilichozoea kuchukua mfukoni mwangu, nikaanza kusoma, na kwa bahati maneno niliyosoma yalikuwa haya: ‘Kijana mzuri ajabu alishika kombe la nakshi, Limejaa maji matamu na safi..’ Niliposoma maneno yale nilimeza mate au kwa kweli nilijaribu kumeza. Hata kufikiri maji kulitaka kunifanya niwe na wazimu.

Hapo nadhani nilishikwa na kichaa kidogo, maana nilianza kucheka, na sauti yangu iliwaamsha wenzangu, na wao wakaanza kusugua nyuso zao chafu, na kufungua midomo na kope zao zilizogandamana.

Mara tulipoamka kabisa tukianza kuzungumza juu ya shida yetu. Hapana hata tone la maji. Tulipindua viriba vyetu tukalamba kingoni, lakini wapi! Vikavu kabisa. Bwana Henry akasema ‘Tusipopata maji tutakufa.’ Nikasema, ‘Kama ile ramani ya Yule mzee ni sahihi, maji yapo karibu tulipo sasa.’ Lakini maneno yangu hayakufariji mtu, maana ilikuwa dhahiri kuwa hatuwezi kuitumai sana ile ramani.

Sasa ikaanza kuwa kweupe kidogo kidogo, tukakaa tunatazamana tu, nikamwona Ventvogel, Yule Hottentot, akiondoka na kuanza kwenda macho chini, na mara akafanya sauti kama ya kukoroma, akaonyesha chini katika mchanga.

Tukashtuka tukasema, ‘Nini, nini? Tukaondoka sote tukamwendea tukitazama chini. Akasema, ‘Wako wanyama wengi kama paa hapa. Tazameni nyayo zao.’ Nikamuuliza, ‘Je, hata kama paa ni wengi hapa hilo linatufaa nini? ‘ Akajibu, ‘Paa hawatembei mbali na maji.’

Nikasema, ‘Kweli, nilisahau, Alhamdulilahi.’ Basi jambo hilo lilitutia uzima tena; ni ajabu sana ya kuwa ‘kama watu wamo katika shida tama ya faraja hata ndogo huwafurahisha. Maana katika usiku wa giza hata nyota moja ni bora kuliko kutokuwa na nyota kabisa.
 
Huko nyuma Ventvogel alikuwa akiinua pua yake akinusa hewa ile yenye moto kama anavyonusa paa mzee anayeshuku hatari. Mara akasema, ‘Nasikia harufu ya maji.’ Ndipo tulipozidi kufurahi, maana tulifahamu namna watu walio zoea kukaa porini wanavyojua kutumia fahamu zao kwa jinsi ya ajabu.

Mara ile jua likatoka likaangaza pote kwa fahari likatufunulia shani iliyotusahaulisha kwa muda ile kiu kali iliyotusumbua. Mbele yetu kadiri ya maili arubaini au hamsini tuliona vilele vya milima viitwavyo, ‘Maziwa ya Sheba’ viking’aa kama fedha katika mianga ya jua la asubuhi, na kila upande, mpaka upeo wa macho kwa maili mia nyingi, mlima wa Sulemani ulienea.

Hapo nilipo sasa siwezi kueleza fahari na utukufu wa shani ile ya ajabu, maana maneno yananipotea kabisa.
Hata kuikumbuka hunitia ububu. Mbele yetu tuliona milima mirefu sana, na nafasi ya katikati ya milima ilikuwa kama mwendo wa maili kumi na mbili.

Milima hiyo ilifanana sana na maziwa ya mwanamke, na mara kwa mara ukungu na kivuli cha chini kilifanana na mwanamke aliyelala amefunikwa kwa namna ya ajabu katika usingizi wake.

Chini ya milima pameinuka kwa taratibu kutoka jangwa, na kutoka mbali huonekana kama juu yake imeviringana na laini; na juu ya kila mlima kiko kilima kidogo kilichofunikwa na theluji na umbo lake ni kama titi la ziwa la mwanamke.

Kwa muda mdogo mianga ya jua ikacheza juu ya theluji na ukungu uliokuwa chini, na mara mawingu na ukungu zikazidi kuwa kama pazia kubwa yakatufichia milima mpaka tukaweza kuona alama tu ya milima ikitokeza katika pazia la mawingu.

Mara yale maziwa ya Sheba yalipotoweka, tukakumbuka tena kiu na taabu yetu. Twaona vilele vya milima viitwavyo ‘Maziwa ya Sheba’ vinang’aa kama fedha.
Ni kweli ya kuwa Ventvogel alisema anasikia harufu ya maji, lakini kila mahali tulipotazama hatukuona hata dalili ya maji. Pote tuliona mchanga mkavu na majani yale ya jangwa mpaka upeo wa macho.

Tulitembea tukazunguka kilima tukitafuta kila upande, lakini hatukuona dalili ya ziwa wala kisima, wala chemchem. Nikasema, ‘wewe Ventvogel, wewe ni mpumbavu kabisa; hapana maji hata kidogo.’ Lakini yeye alizidi kuinua pua na kunusa hewa akasema, ‘Bwana, nasikia harufu ya maji. Najua maji yapo.’ Bwana Henry akapapasa ndevu zake akafikiri, akasema, ‘Labda maji yapo juu ya kilima.’ Bwana Good akasema, ‘Upuuzi tu,! Nani aliyewahi kusikia maji hukaa juu ya kilima!?’


Nikasema, ‘Haya twendeni tukatazame.’ Tukaondoka tukapanda kilimani na Umbopa akatangulia. Mara alisimama kama amepagawa, akaita, ‘Maji! Maji!Maji!’ Tulikwenda kwa haraka, na hakika tuliona maji yako katika shimo. Namna yalivyokuwa katika mahali pale hatukungojea kuulizana, wala hatukusita kwa sababu yalikuwa meusi. Mara tukayarukia tukaanza kunywa.

Lo!jinsi tulivyokunywa! Tulipokwisha kunywa, tukavua nguo zetu zilizokuwa zimekauka kabisa.

Baadaye kidogo tuliondoka tukiwa tume burudika kabisa, tukala nyama kavu, maana kwa muda wa saa ishirini na nne tulishindwa kula, tukashiba. Kisha tulivuta tumbako tukalala mpaka saa sita, kando ya maji yale yaliyotuponya.

Siku ile tulikaa tukapumzika karibu na maji, tukishukuru ya kuwa ilikuwa bahati yetu kuyaona. Maana ingawa si mazuri lakini yalitufaa. Wala hatukumsahau Yule marehemu Silvestre aliyeandika alama sahihi ya mahali pale juu ya kitambaa kile. Ni jambo la ajabu kuwa maji yale yalikaa hivi, nami nadhani kwamba haikosi iko chemchemi chini ambayo maji yake yanapanda juu.

Basi tulipokwisha shiba na kujaza viriba maji, nyoyo zetu ziliburudika, na mwezi ulipotoka tulianza safari yetu tena, usiku ule tulikwenda mwendo wa maili ishirini na tano, lakini hatukuona maji tena, ila mchana tulipata kivuli chini ya vichuguu. Jua lilipotoka tena tukaona Maziwa ya Sheba, na sasa yalikuwa mazuri kupita jana.

Jioni tuliondoka tukashika safari na kulipopambazuka tukaona tumefika kwenye mwinuko wa chini ya Ziwa la kushoto la Sheba, maana ndipo tulipoelekea kutoka mwanzo wa safari. Na sasa maji yametuishia tena, na kiu kimetushika, wala hatukuona mahali pa kupata maji mpaka kufika kwenye theluji ya juu.

Baada ya kupumzika muda wa saa moja, ilitubidi kwenda mbele tena kwa sababu ya kiu, tukazidi kupanda kwa kujikokota mlimani. Ilipopata saa tano tulikuwa tumechoka, nasi hali yetu ilizidi kuwa mbaya. Chini palikuwa kokoto nyingi na miguu yetu ilituuma mno, basi tulikaa chini ya mwamba mmoja tukiuguzana.

Tulipokuwa tumekaa hivi nilimwona Umbopa akiondoka na kujikokota kwenye mahali penye majani kidogo, mara nilimwona yeye aliyekwenda pole pole na kwa taratibu, akirukaruka na kupiga kelele kama mtu aliyeshikwa na wazimu, na huku anatikisa kitu katika mkono wake.

Tuliondoka kwa haraka tukamfuata upesi tulivyoweza, tukitumai kuwa ameona maji. Nikamwita, ‘Je, una nini, Umbopa, una nini?’ Akaitikia, ‘Ee Bwana Makumazahn, ni maji na chakula pia.’ Akazidi kutikisa kile kitu chenye rangi ya kijani kibichi.

Ndipo tulipoona amevumbua kitu gani. Lilikuwa tikiti, nae amegundua konde la matikiti mengi mno, nayo yote yalikuwa mabivu. Mara tukaanza kuyala. Nadhani kila mmoja alikula matikiti sita hivi! Lakini ingawa yalituliza kiu yetu lakini tuliona njaa ya chakula. Tukajaribu kula nyama kavu, lakiniilikuwa tumeikinai.
 
Hapo kwa bahati niliona kundi la ndege wakubwa wanaruka juu, nikaona kuwa ni namna inayofaa kuliwa. Nikatwaa bunduki yangu, na kwa bahati tena nilipiga mmoja. Sasa tukafanya moto kwa majani makavu ya matikiti tukamwoka ndege, tukala chakula namna tusiyokula kwa juma zima.

Tulikula ndege Yule wala hatukusaza kitu ila mifupa ya miguu yake na mdomo wake, tukaona nafuu.

Usiku ule mwezi ulipotoka tukaendelea katika safari yetu. Tulichukua matikiti kadiri tulivyoweza. Tulipopanda kidogo tuliona hewa inaanza kuwa baridi na tuliona raha, maana tulikuwa karibu kufika kwenye theluji, ulibaki mwendo wa maili kumi na mbili tu. Na hapo tuliona matikiti mengine, basi hatukuona taabu ya kiu, na tena tulijua kwamba mara tukifika kwenye theluji shida yetu ya maji itakwisha.

Lakini sasa mlima ulianza kwenda juu sana na kwa hivyo mwendo wetu ulikuwa wa kobe tu. Usiku ule tulikula nyama iliyobaki, na mpaka sasa hatujaona kiumbe chenye uhai ila wale ndege, wala hatujaona chemchemi wala mto wa maji, tukafikiri kuwa ni ajabu , maana theluji ikiisha yeyuka lazima maji yake yateremke mahali.

Lakini baadaye tulijua kuwa mito yote iliteremka kwa upande wa pili wa mlima. Sasa tulianza kufikiri habari za njaa. Tumenusurika kufa kwa kiu, lakini ilionekana kuwa tutakufa kwa njaa. Habari zilizotokea katika siku tatu za taabu zilizofuata zimeandikwa katika kitabu changu kama hivi:

21 Mei: ‘’Tulianza safari saa tano mchana, hewa ilikuwa baridi tukaweza kusafiri mchana huku tumechukua matikiti. Tulijikokota mpaka jioni lakini hatukuona matikiti mengine. Naona kama tumekwisha pita mahali yanapositawi. Hatukuona mnyama yeyote, Jua liliposhuka tulipumzika, na kwa kuwa hatujala kwa muda wa saa nyingi tulisumbuka sana. Na hasa kwa sababu ya baridi ya usiku.’

22 Mei: ‘Mara kulipopambazuka tulianza safari tena, lakini tulikuwa dhaifu sana. Safari ya kutwa ilikuwa mwendo wa maili tano tu.

Tuliona theluji kidogo kidogo tukaila, lakini hatukula kitu kingine, Tulifanya kambi yetu usiku chini ya mwamba. Baridi ni kali mno. Tulikunywa mvinyo kidogo tukajifunika na mablanketi yetu tusife kwa baridi. Sasa tumo taabuni kabisa kwa sababu ya baridi na njaa. Nilifikiri kuwa Ventvogel atakufa usiku.’

23Mei: ‘Mara jua lilipopanda tukashika safari tena, tukaota jua. Sasa tu taabani kabisa kabisa, nadhani ilikuwa ni safari ya mwisho tusipopata chakula.
Mvinyo umebaki kidogo sana. Bwana Good na Bwana Henry na Umbopa wanavumilia namna ya ajabu, lakini Ventvogel yu karibu kufa. Kama walivyo Hottentot wote, yeye hawezi kuvumilia baridi.

Maumivu ya njaa si mabaya sana, lakini naona kama tumbo limekufa ganzi. Wenzangu wasema hayo hayo, sasa tumefika juu yam lima ule unaoungamana na matiti ya Sheba na chini pote ni pazuri ajabu. Nyuma yetu jangwa linalong’aa katika jua limeenea mpaka upeo wa macho, na mbele yetu theluji inaonekana kwenda juu kwa taratibu mpaka kufika kwenye matiti ya Sheba.

Hapana kitu chenye uhai kinachooneka. Mungu atusaidie nahofu ya kuwa hatima yetu ipo karibu.’ Na sasa nitaacha habari zilizoandikwa katika kitabu nishike hadithi yangu tena. Siku ile ya 23 Mei, kutwa tulijikokota mbele tukapanda mwinuko ule wa theluji na mara kwa mara tulilala tukapumzika.

Nadhani watu wangalituona wangalifikiri tu watu wa ajabu, maana tumekonda, tumechoka na tulikuwa tunavuta miguu kwa shida sana, na macho yetu yana dalili ya njaa kali nayo yamekodoka mbele kabisa.


Siku ile tulikwenda maili saba tu, na jua lilipokuwa karibu kushuka tukajiona chini ya titi la kushoto la Sheba, nalo lilikwenda juu sana kama mlima mrefu wa theluji. Ingawa tulikuwa dhaifu sana lakini tuliyoyaona tulihisi ajabu na shani, maana mianga ya jua ilitia theluji rangi ya damu, na juu yake ilikuwa kama taji la theluji nyeupe inayong’aa.

Hapo Bwana Good alisema akitweta, ‘Nadhani tuko karibu na lile pango alilotaja Yule mzee katika hati yake.’ Nikasema, ‘Ndiyo, yaani iwapo pango liko.’ Bwana Henry akasema, ‘Haya, Bwana Quatermain, usiseme hivyo, mimi namwamini sana Yule mzee; hukumbuki namna tulivyoona yale maji? Haikosi tutaona na lile pango upesi.’ Nikasema, ‘Tusipoliona kabla ya giza kuingia, sisi ni maiti, hivi ndivyo ninavyojua mimi.’

Basi tulijivuta tulivyoweza mpaka kufika kwenye shimo na hakika tuliona kuwa ni kinywa cha pango, na haikosi ni pango lile alilotaja Yule mzee Silvestre katika hati yake. Kwa bahati tulifika kwa wakati unaofaa, maana mara tulipofika jua likatua na giza likaingia upesi sana.

Basi tukatambaa tukaingia katika pango na kila mtu alikunywa mvinyo kidogo ukaisha kabisa, tukasongana pamoja tupate kujitia joto, tukajaribu kusahau taabu zetu katika usingizi. Lakini kwa kuwa baridi ilikuwa kali mno hatukuweza kupata usingizi. Basi hapo tulikaa tukiona baridi inatuumiza, kwanza katika vidole, na tena miguu na usoni, Tulisongana pamoja , lakini wapi! Ilikuwa bure tu, maana miili yetu ilikuwa haina joto hata kidogo.

Mara kwa mara mmoja wetu alipata usingizi kwa muda kidogo, lakini mara aliamka tena, nami naona kuwa tungalipatwa na usingizi kamili hatungeamka tena, tungekufa pale pale. Nadhani iliyotuponya ilikuwa ni nia yetu tu.

Ilipokuwa karibu kupambazuka nilimsikia Ventvogel akiugua, na meno yake yaliyokuwa ya kitetemeka kwa baridi yakatulia. Nikafikiri kama ameshikwa na usingizi. Mgongo wake uliokuwa unaniegemea mimi ukazidi kuwa baridi mpaka ukawa kama barafu.

Baadaye kulianza kuwa kweupe kidogo na mishale ya jua ilikuwa kama mishale ya dhahabu ikipenya mote katika pango, imetuangaza, ikamwangaza na Ventvogel aliekaa katikati yetu, amekwisha kufa! Masikini, si ajabu ya kuwa mgongo wake ulikuwa baridi.
Nilipomsikia anaugua alikuwa ana kata roho, na sasa mkavu kabisa. Tulishtuka sana tukaondoka upesi tukamwacha pale amekaa na mikono yake imekumbatia miguu yake..

Ni ajabu namna wanadamu wanavyoona woga katika mahali penye maiti! Baadaye jua lilipanda kukawa kweupe kabisa ndani ya pango.

Mara nilisikia mmoja wetu akipaaza sauti yake kwa hofu, nikageuka nikatazama. Haya ndiyo niliyo yaoona: Pale mwisho wa pango niliona maiti mwingine, amekaa na kichwa chake kimeinamia kifuani,’ na tena nikaona kuwa maiti mwenyewe ni Mzungu. Na wenzangu pia wakamwona, na kuona kuliwatia woga sana. Kila mmoja akatoka pangoni upesi alivyoweza.
 
SURA YA SABA


Tulipofika nje ya pango tulisimama tumepumbaa. Bwana Henry akasema, ‘Mimi nitaingia ndani tena.’ Bwana Good akamuuliza kwa nini? naye akajibu, ‘Kwa sababu labda Yule tuliyemwona ndiye tunayemtafuta labda ni ndugu yangu.’

Basi tukaingia ndani tena ili tushuhudie. Tulipoingia kwanza hatukuweza kuona vizuri sababu ya kiwi cha macho kilichofanywa na mwangaza wa nje lakini tuliposimama mwisho wa pango niliona maiti mwingine amekaa, kichwa chake kimeinamia kifuani. Baada ya kuzoea giza tulimkaribia Yule maiti, na Bwana Henry akapiga magoti karibu naye akamtazama usoni, akasema, ‘Namshukuru Mungu, huyu si ndugu yangu.’

Basi ndipo nilipomkaribia mimi nikamtazama. Huyu marehemu alikuwa mtu mrefu, mtu mzima na pua ya upanga, na nywele zake zilianza kuwa na mvi, na alikuwa na masharubu marefu.

Ngozi yake ilikuwa imekauka kabisa nayo imetanda juu ya mifupa yake. Alikuwa hana nguo ila shingoni alifungwa msalaba wa pembe. Nikasema, ‘Marehemu huyu alikuwa nani?’

Bwana Good akasema, ‘Je, huwezi kubahatisha?’ Nikatikisa kichwa, akasema, “Huyo si mzee Jose da Silvestre’ Nikasema, ‘Haiwezekani, maana yeye alikufa miaka mia tatu iliyopita.’ Bwana Good akajibu, ‘Na hapa kuna nini cha kuzuia asikae bila kuoza kwa miaka elfu tatu? Maana ikiwa ni baridi mno, nyama inaweza kukaa bila kuoza kwa muda mrefu sana.

Na hapa joto la jua haliingii kabisa; Wala wanyama hawaji kumrarua na kumharibu. Haikosi Yule mtumishi wake aliyemtaja katika maandishi yake alimvua nguo na kumwacha hapa.

Tazama, huu ndiyo mfupa aliotumia kama kalamu kuandikia ile ramani yake.’ Akainama chini akaokota mfupa mdogo uliopasuliwa ncha. Tukatazama tumeshangaa, na katika kutazama ajabu hii tulisahau shida na taabu zetu.

Bwana Henry akasema, ‘Ndiyo kweli, na hapa ndipo mahali alipotoa wino wake.’ Akaonyesha kijeraha kidogo katika mkono wa Yule maiti.

Basi sasa hatukuwa na shaka tena, maana tumekwisha shuhudia. ‘’Huyu maiti ni Yule mtu aliyeandika yale maelezo vizazi kumi nyuma ambayo yametuongoza hapa. Huu mkononi mwangu ni mfupa ule aliotumia kuwa kalamu, na hapo shingoni upo msalaba alioubusu wakati alipokuwa akifa.’’

Baadaye kidogo Bwana Henry alisema, ‘Haya twendeni, lakini ngoja kwanza nimpe mwenzie akae pamoja naye.’ Akamwinua Yule marehemu Ventvogel akamweka karibu na maiti ya Yule mzee, kisha akainama akatoa ule msalaba katika shingo ya Yule mzee kuwa ni ukumbusho. Nadhani anao hata sasa.

Mimi nilichukua ule mfupa, ninao hata sasa napengine nautumia kama kalamu, Basi tuliwaacha wale maiti wawili pamoja, walinde zamu katikati ya theluji inayodumu milele, tukatoka katika pango na kuingia katika mwangaza wa jua.

Tukaendelea katika safari yetu tukiwaza mioyoni ni baada ya saa ngapi na sisi tutakuwa kama wao walivyo sasa. Tulipokwisha kwenda yapata nusu saa tulifika, kwenye ukingo wa mlima uliokuwa kama meza.

Yaliyokuwa mbele yetu hatukuona kwa sababu ukungu ulifunika nchi kama mawimbi ya bahari. Lakini ukungu ulipoinuka kidogo tuliona kwa mbele yetu yapata hatua mia tano mahali padogo penye majani mwisho wa theluji, na katika majani hayo tuliona mto wa maji unapita.

Wala hayo si yote, maana pale katika majani tuliona wanyama wakubwa kumi au kumi na tano wamekaa wanaota jua.
Hatukuweza kuona ni wa namna gani, lakini nyoyo zetu zilijaa furaha tena, tukafanya shauri la kuwapiga.

Basi nilitwaa bunduki na Bwana Henry na Bwana Good vile vile wakatwaa bunduki zao tukamwambia Umbopa atupe ishara na sote tukapiga pamoja. Basi tukajiweka tayari na Umbopa akasema ‘Piga’ na sote tulipiga pamoja, na moshi wa bunduki ulipoinuka tuliona mnyama mkubwa amekufa.

Tulipiga kelele za furaha kwa kuokoka, hatutakufa kwa njaa. Ingawa tulikuwa dhaifu sana tuliruka katika theluji mpaka pale penye mnyama na kabla haijapita dakika kumi temekwisha mkatakata mnyama.

Na moyo na maini yake yalikuwa yamewekwa mbele yetu. Lakini sasa tukatambua shida nyingine, maana hatuna kuni, na kwa hivi hatuwezi kukoka moto wa kupikia nyama. Basi tukatazamana katika shida yetu, Bwana Henry akasema, ‘‘Watu wenye njaa hawawezi kuwa wachaguzi, lazima tule nyama mbichi’’ basi hapakuwa na njia nyingine ya kutoka katika shida yetu, na njaa. Yetu ilikuwa kali mno.

Basi tulifukia moyo na maini katika theluji kwa muda kidogo ili kuyapoza, kisha tuliyaosha sana katika maji ya mto, tukayala mabichi.

Kwa kweli sijaonja nyama tamu kama ile nyama mbichi. Baada ya robo saa tulikuwa na hali nyingine kabisa, maana uzima wetu ulirudi pamoja na nguvu, na damu ilizunguka katika mishipa yetu.

Lakini hatukusahau habari za hatari ya kula sana, maana matumbo yetu yalikuwa dhaifu, tukaacha kula kabla ya kushiba. Bwana Henry akasema, ‘’Tushukuru Mungu, Yule mnyama ametuokoa maisha yetu. Je, Quatermain, ni mnyama gani?’

Niliondoka nikaenda kumtazama, lakini nilikuwa sina hakika. Baadaye nilikuja kujua kama watu wa huko walimwita Inko. Tulipokwisha kula tulikaa tukatazama pote. Palikuwa pazuri mno. Tulipokuwa tumekaa hivyo, Bwana Henry alisema, ‘Je, katika ile ramani haikuandikwa habari za Njia kuu ya Sulemani?’ Nikatikisa kichwa na nikaendelea kutazama ardhi mbele yetu.

Akaelekeza mkono upande wa kushoto akasema, ‘Basi, tazama, ni ile!’ Tukatazama tukaona njia pana uwandani imetambaa kama nyoka. Hatukusema mengi, maana tulianza kuzoe mambo ya ajabu. Bwana Good akasema, ‘’Nadhani si mbali; afadhali na tufuate njia, haya tuondoke.’’

Basi tulipokwisha nawa katika mto tuliondoka tena. Kwa mwendo wa maili moja tulisafiri juu ya miamba na theluji, na tulipokwisha panda kilima kidogo tuliona njia tukaifuata.

Njia ilikuwa imara ya ajabu mno, na upana wake ulipata kadiri ya hatua thelathini, lakini haikuendelea, maana tulitembea hatua mia moja tukaona imefifia kabisa, imefunikwa kwa miamba.
 
Bwana Henry akaniuliza, ‘Je, imekuwaje sasa?’ nikatikisa kichwa tu. Bwana Good akasema, ‘Mimi najua.

Nadhani njia ilipita huku lakini mchanga umepeperusha na kuifunika, na huko juu nadhani imefunikwa kwa mawe yaliyotoka juu mlimani.’ Basi tukaona kuwa labda maneno yake ni ya kweli, tukaanza kuteremka mlimani.

Sasa safari yetu ilikuwa nyepesi wala si kama ile ya kupanda mlima tulipokuwa tunaona njaa kali. Kama tungaliweza kuwasahau masikini Ventvogel na Yule mzee pangoni nadhani tunaliona furaha kabisa, ingawa hatukujua hatari inayoweza kutokea kwa mbele. Kila tukiteremka tuliona hewa inazidi kuwa nzuri, na nchi yenyewe ilikuwa nzuri kabisa.

Njia ilikuwa ya ajabu mno, pengine ilivuka misingi mirefu juu ya daraja yenye matao, na pengine ilipanda mlima kwa kuzunguka zunguka, na pengine ilipenya ndani yam lima wenyewe. Ukuta wa tundu lile lililopenya mlima ulichorwa picha.

Bwana Henry akazitazama akasema, ‘Watu wanaita njia hii njia ya Sulemani lakini mimi nafikiri kama ni kazi ya watu wa Misri walipofika hapa kabla ya watu wa Sulemani. Maana, kazi hii kama si kazi ya Wamisri, nadhani imefanana sana nayo.’

Ilipopata saa sita tulikuwa tumekwisha teremka na kufika mahali penye miti mingi. Mara Bwana Good akasema, ‘Ah! Hapa tunaweza kupata kuni; na tukae hapa kidogo tuchome nyama iliyobaki; maini yale mabichi yamekwisha shuka tumboni.’

Basi tuliacha njia tukaenda kwenye mto wa maji safi tukakaa, na upesi tuliwasha moto. Sasa tulikata nyama ya Inko tuliyoleta tukaioka. Tulipokwisha shiba, tukavuta tumbako tukaaa tumefurahi, na raha yetu tulipoilinganisha na taabu iliyotupata ilikuwa kama ni raha ya peponi.

Baadaye kidogo sikumwona Bwana Good, nikatazama kuona umekwenda wapi. Nikamwona amekaa karibu na mto amekwisha oga. Sasa amevaa shati lake tu na tabia yake ya umaridadi ikadhihirika; maana amekunja suruwali na koti, naye anatikisa kichwa kwa kuona namna zilivyoraruka kwa miiba ya njiani. Kisha akatwaa viatu vyake akavisugua kwa majani, kisha akatwaa kipande cha mafuta ya nyama akaanza kuvisugua kwa mafuta.

Kisha akavitazama kwa miwani yake, maana alivaa siku zote miwani yenye kioo kimoja tu, akavivaa. Sasa alitoa kioo kidogo na kitana akajitazama uso na tena akatikisa kichwa, akachana nywele zake, lakini hakuwa radhi.

Akapapasa ndevu zake, maana hakuweza kunyoa kwa muda wa siku kumi, akatwa kile kipande cha mafuta akakiosha katika maji, kisha akasugua ndevu zake kwa mafuta, akatwaa wembe katika mfuko wake akaanza kunyoa ndevu zake.

Lakini niliona akiumia sana, maana niliweza kumsikia akiguna, nikacheka sana. Maana niliona kuwa ni ajabu kuwa mtu anakubali kuvumilia maumivu ya kunyoa kwa mafuta katika mahali tulipo sisi, yaani porini pasipo na watu. Basi alizinyoa ndevu zilizokuwa nyingi sana, kwa upande wa kulia wa uso wake, na mara nilishtuka sana nikaona mshale wa nuru unampitia kichwani.
 
Bwana Good akaruka ameshtuka sana, na mimi vile vile nikaruka nikatazama, na haya ndiyo niliyoona.

Pale yapata hatua ishirini kutoka nilipokuwa nimesimama mimi, na hatua kumi kutoka alipokuwako Bwana Good, niliona watu wamesimama. Wote walikuwa warefu na weusi, lakini wekundu kidogo kama rangi ya shaba nyekundu, na wengine walivaa manyoya marefu meusi na ngozi za chui; basi haya ndiyo niliyoona kwanza.

Mbele niliona kijana mwenye umri wa miaka kumi na saba amesimama kama ndiyo kwanza autupe mkuki. Mshale ule wa nuru niliouona ulikuwa mwangaza uliomulikwa na mkuki alioutupa.

Nilipokuwa nikitazama, mzee mmoja aliyekuwa kama askari akaja mbele akamshika mkono Yule kijana akasema naye, kisha wote wakatujia.
Bwana Henry na Bwana Good na Umbopa wote walishika bunduki zao wakaelekeza. Lakini wale watu wakazidi kutujia.

Basi niliona kuwa hawa kujua bunduki ni kitu gani, maana wangalijua wasingezi dharau hivyo. Basi nikawaambia waweke bunduki zao chini, maana watambue kuwa usalama wetu u katika kutafuta suluhu.


Wakafanya nilivyotaka, kisha nikaenda mbele kuonana na wale watu, nikamwambia Yule mzee kwa Kizulu. Maana nilibaatisha tu, lakini nilipoona kuwa wanafahamu maneno yangu nilistaajabu.

Yule mzee akaitikia, lakini maneno yake yaliachana kidogo na maneno ya Kizulu ila si sana, na mimi na Umbopa tuliweza kuyafahamu mara. Yule mzee akauliza, ‘Mmetoka wapi? Nyinyi ni nani? Kwa nini sura za nyinyi watatu ni nyeupe na huyu wanne ni kama sura zetu?’


Akapeleka mkono kumwonyesha Umboka. Nikamtazama Umbopa na nikajua kuwa anasema kweli. Sura yake ilikuwa kama sura za watu wale waliokuwa wamesimama mbele yetu, na maungo vile vile yalifanana nao. Nikamjibu, ‘sisi ni wageni tumekuja kwa amani, na mtu huyu ni mtumishi wetu.’
Akasema, ‘’Unasema uwongo, wageni hawawezi kuvuka ile milima.

Lakini uwongo wenu utafaa nini? Ikiwa nyinyi ni wageni lazima mtakufa, maana wageni wowote hawana ruhusa kuishi katika nchi hii ya Wakukuana. Hii ndiyo amri ya Mfalme. Basi mjiwekeni tayari kufa, e nyinyi wageni’’ Niliposikia maneno hayo nilifadhaika, na hasa nilipoona mikono ya wale watu inashuka na kushika visu vikubwa vilivyofungwa viunoni mwao. Bwana Good akauliza, ‘Je, mtu huyu anasema nini?’ Nikamjibu, ‘Anasema kuwa tutauawa .’

Bwana Good akaghumia, na kama ilivyokuwa desturi yake anapokuwa kwenye shida yeyote, alitia vidole kinywani akashika meno yake akayavuta chini, kisha akayaacha yarudi juu tena kwa kishindo. (Maana alikuwa ametiwa meno yaliyotengenezwa, kwa kuwa meno yake yameng’olewa).

Jambo hilo lilituokoa, maana mara walipoona hivyo, wale watu wakashtuka wakapiga kelele kwa hofu, wakaruka nyuma hatua mbili tatu. Nikasema, ‘Je, kuna nini?’ Bwana Henry akaninong’oneza akasema, ‘Ni meno ya Bwana Good nadhani alipoyavuta chini; wale watu wameona ni ajabu.

Haya, Bwana Good, yatoe kabisa.’ Basi akayatoa akayaficha upesi katika mkono wa shati lake.

Basi wale watu sasa walishikwa na udadisi wakasahau hofu yao kidogo, wakaja mbele, sasa ile habari ya kutuua waliisahau.

Yule mzee akaelekeza mkono wake kumwonyesha Bwana Good, naye amesimama amevaa shati na viatu tu, na tena amenyoa upande mmoja tu wa uso wake, akasema, ‘Ee nyinyi wageni, imekuwaje kuwa huyu mnene amevaa nguo maungoni ila miguu ni mitupu, na pia ndevu zaota kwa upande mmoja tu wa uso wake, naye, analo jicho moja ambalo linapenya nuru? Imekuwaje anaweza kuyatoa meno yake nakuyarudisha apendavyo?’


Nikamwambia Bwana Good, ‘Funua kinywa chako.’ Akafunua midomo yake kama mbwa mkali, wakaona kuwa hana meno kabisa, waliouona ni ufizi tu. Basi wale watu wakashtuka sana, wakasema, ‘Meno yake yako wapi sasa? Tulioyaona kwa macho yetu sasa hivi!’

Basi Bwana Good akageuza kichwa chake kidogo akainua mkono wake akayaweka meno ndani kwa siri, kisha akacheka. Kumbe! Kinywa chake kimejaa meno tena. Basi walipoona hivyo, Yule kijana alijiangusha chini akalia kwa hofu; na magoti ya Yule mzee yaligongana kwa kuogopa, akasema, na sauti yake ilitetemeka.

‘Naona kuwa nyinyi ni mizuka, maana hapana mtu aliyezaliwa na mwanamke mwenye ndevu upande mmoja tu wa uso, wala jicho moja linalopenya nuru, wala meno yanayotoweka na kuonekana tena. Ee mabwana, mtuwie radhi.’

Basi nikaona kama ni bahati yetu tena, nikamjibu kwa sauti kali, ‘Basi, msiogope; nitawataarifu habari za kweli. Sisi ni wanaume kama nyinyi lakini tumetoka katika ile nyota kubwa inayozidi kung’aa usiku.

Tumekuja kukaa pamoja nanyi kwa muda kidogo na kuwaleteeni neema. Mnaona rafiki zangu, nimejifunza lugha yenu ili niwe tayari.’

Wakaitika, ‘Ni kweli, ni kweli.’ Nikaendelea nikasema, ‘Na sasa, rafiki zangu, labda mnaogopa, mnafikiri kuwa tutamuua Yule kijana aliyemtupia mkuki huyu mwenzetu mwenye meno yanayotoka na kurudi tena. Maana mmetupokea vibaya baada ya safari ndefu tuliyoifanya ili kufika hapa.’

Yule mzee akasema, ‘Mabwana, mtusameheni nawasihi, maana yeye ni mwana wa mfalme na mimi ni mjomba wake. Akidhurika lazima mimi nitauawa.’ Yule kijana akaitikia, akasema, ‘Ndiyo, hayo ni kweli kabisa.’

Nikasema, ‘Labda mnafikiri kuwa hatuna nguvu za kujilipiza kisasi, lakini nitakuonyesheni. Haya wewe (nikamwita Umbopa kwa ukali sana) nipe mwanzi wangu wa uchawi unaosema.’ (Nikamwashiria anipe bunduki yangu).

Umbopa alitambua mara moja niliyotaka, akanipa bunduki yangu huku akiinamisha kichwa, na akasema, ‘Ni huu, bwana wa mabwana.’ Basi kabla sijamwambia anipe bunduki niliona swala amesimama juu ya mwamba kadiri ya mwendo wa hatua mia moja, nikanuia kumpiga.

Basi niliwaonyesha huyo swala, nikasema, ‘Niambieni kama yupo mtu aliyezaliwa na mwanamke anayeweza kumuua Yule mnyama kwa mshindo tu!
Yule mzee akajibu, ‘Hapana mtu, wala haiwezekani kabisa.’ Nikajibu, ‘Lakini mimi nitamuua.

Nikaelekeza bunduki yangu, Yule mnyama alikuwa mdogo lakini nilijua kuwa ni lazima nimpige. Nikavuta pumzi nikakaza mtambo wa bunduki kwa taratibu. Yule swala alisimama kimya kabisa. Bunduki ikalia, na mara Yule swala akaruka juu, akaanguka juu ya mwamba amekwisha kufa.


Basi, hapo wale watu waliguna kwa hofu, nikasema, ‘Haya, mkitaka mnyama nendeni mkamchukue huyo.’ Yule mzee akamwashiria mtu mmoja, na akaenda akamleta mnyama, wakamzungukia wakatazama tundu iliyoingia risasi.

Nikasema, ‘Kama hamsadiki hata sasa, basi mtu mmoja asimame mwambani nimfanye kama nilivyomfanya huyo swala. Hapo mtafahamu kuwa mimi sisemi maneno ya bure.’
Hapana aliyetaka kufanya hivyo mpaka Yule mwana wa mfalme aliposema, ‘Umesema vema. Wewe, mjomba wangu, nenda ukasimame mwambani, Uchawi ule umeua mnyama tu, hauwezi kumuua mtu.’

Lakini Yule mzee hakupenda shauri lile, akaudhika, akasema, ‘Hapana! Hapana! Macho yangu ya kizee yameona mambo ya kutosha. Watu hawa ni wachawi wa kweli kweli. Tuwachukue kwa mfalme.

Lakini ikiwa mmoja wenu anataka ushuhuda zaidi, basi na yeye asimame mwambani na ule mwanzi wa uchawi utasema naye.’

Hapo wote wakaanza kukataa. Na mmoja akasema, ‘Hapana, uchawi wa namna hiyo usipotee bure kwa ajili yetu. Sisi tumeridhika. Uchawi wote wa watu wetu hauwezi kufanya jambo kama hilo.’

Yule mzee akasema, ‘Ni kweli. Bila shaka ni kweli. Na sasa nyinyi watoto wa nyota, sikilizeni, nyinyi watoto wenye macho yanayong’aa, meno yanayotoweka, nyinyi mnaonguruma kwa ngurumo inayoweza kuua kwa mbali. Mimi ni Infadus, mwana wa Kafa, aliyekuwa mfalme wa watu wa Kukuana.


Huyu kijana ni Skraga, mwana wa Twala aliye mfalme mkuu wa Kukuana, Mlinzi wa Njia Kuu, Mtishaji wa adui zake, Mwenye elimu ya uchawi, Jemedari wa askari mia elfu, Twala mwenye chongo, Mweusi, Mtishaji.’

Nikasema kwa maneno ya dharau, ‘Mn, basi na tuongoze kwa Twala. Sisi hatutaki kusema na watu wanyonge na wadogo.’

Yule mzee akajibu, ‘Vema, mabwana wangu. Sisi tunawinda muda wa siku tatu kutoka mji wa mfalme, lakini mabwana muwe na subira na sisi tutawaongozeni.’ Nikajibu, ‘Vema, wakati wote upo mikononi mwetu, maana sisi hatufi.

Tu tayari mtuongoze. Lakini wewe Infadus, na wewe Skraga, angalieni! Msitudanganye, msijaribu kututega, maana tutatambua fikra zenu duni kabla hazijaingia katika akili zenu, na hatutakosa kujilipiza kisasi.

Nuru ile inayotoka katika jicho la Yule mwenye miguu mitupu na ndevu upande mmoja tu wa uso, itakuaribuni, itapita katika nchi yenu. Meno yake yanayotoweka yatajibana mikononi mwenu na yatakuleni nyinyi na wake zenu na watoto wenu; mianzi ya ajabu itasema nanyi kwa sauti na itawafanyeni kuwa kama takataka.

Angalieni.’ Basi maneno yangu yaliwatisha sana, na yule mzee alijibu, ‘Koom! Koom!’
Baadaye nilipata kufahamu ya kuwa yale maneno ndiyo wanayoyatumia kwa kumwamkia mfalme.

Akageuka akawaamuru watu wake, na mara upesi wakashika vitu vyetu ili wavichukukue, ila bunduki hawakushika, maana waliziogopa. Hata na nguo za Bwana Good wakazishik, naye alipoona hivi akataka kuzitwaa, ‘Ee, Bwana mwenye jicho linalong’aa na meno yanayoyeyuka, usitwae nguo, maana watumishi wako watazichukua.’

Bwana Good akasema kwa Kiingereza, ‘Ndiyo, lakini nataka kuziva.’ Umbopa akatafsiri maneno yake, na Infadus akajibu, ‘Hapana Bwana, usifiche miguu yako mizuri iliyo meupe tusiione tena? Tokea sasa lazima uvae shati na viatu na miwani yako tu basi.’

Na mimi nikaongeza, ‘Ndiyo, na tena lazima uache ndevu upande mmoja tu wa uso wako. Ukijibadili kwa namna yoyote watu hawa watafikiri kuwa tunawadanganya. Nakusikitikia, lakini kweli, lazima ufanye hivyo. Kama wakishuku habari hizi si za kweli, basi maisha yetu yatapotea kabisa.’

Bwana Good akasema, ‘Je, unasema kweli?’ Nikamjibu, ‘Ndiyo, nasema kweli kabisa, maana miguu yako meupe mizuri na miwani yako imekuwa ni umbo lako na lazima uvumilie tu.’ Akavumilia lakini hakuzoea, mpaka baada ya kadiri ya siku kumi, kwenda akivaa nguo chache hivi.
 
SURA YA NANE

Mchana kutwa tulisafiri na tulifuata njia ile nzuri. Infadus na Skraga walifuatana nasi, lakini watu wao walitangulia.

Baadaye kidogo nilimuuliza Infadus, ‘Nani aliyetendeneza njia hii? Akajibu, ‘Ilitengenezwa zamani sana na hayupo anayejua wakati gani au kwa namna gani ilivyotengenezwa, hata Kizee Gagula aliyeishi kwa vizazi kumi hajui.

Hapana anayeweza kutengeneza njia kama hii sasa.’Nikamuuliza, ‘Na maandishi na picha zile katika pango lile nani aliye chora?’

Akajibu, ‘Bwana wangu, mikono iliyotengeneza njia hii ndiyo iliyochora picha zile. Hatujui nani aliyechora.’ Nikamuuliza tena, ‘Wakukuana walikuja katika nchi hii wakati gani?’ Akajibu, ‘Bwana wangu, kabila hili lilikuja kama kuvuma kwa dhoruba zama za kale miaka elfu na elfu nyuma.

Walitoka nchi ile iliyo kaskazini, Babu zetu walisimulia kama hawakuweza kwenda mbele zaidi kwa sababu ya milima mirefu inayozunguka nchi.

Na Kizee Gagula, mwanamke mwenye busara, anasema hivyo hivyo. Nchi hii ilikuwa ya neema, basi wakakaa wakazaana wakapata nguvu, na sasa hesabu yetu ni kama punje za mchanga wa pwani, na mfalme Twala akiwaita askari wake wakutanike, huenea huwandani mpaka upeo wa macho.’

Nikamuuliza, ‘Je, na kama nchi imezungukwa na milima, majeshi watapigana na adui gani?’ Akajibu, ‘Nchi yetu imezungukwa na milima ila upande wa kaskazini, na mara kwa mara adui hutoka upande huo kama mawingu kutoka nchi tusioijua, nasi tunawaua. Tokea vita vya mwisho miaka ishirini tu imepita, na elfu nyingi za watu walikufa, lakini tuliwaua wale waliokuja kutula sisi.

Basi tangu siku hizo hakujakuwa na vita tena.’ Nikasema, ‘Basi ikiwa ni hivi Infadus, askari wenu watakuwa wamechoka kwa kukaa bure tu!’ Akajibu, ‘La, bwana, tangu vita vile, vita vingine viliingia vilivyokuwa vikali, lakini vilikuwa vita kati yetu sisi wenyewe; yaani mbwa kula mbwa.

Ikawa hivi: Ndugu yangu aliyekuwa mfalme alikuwa na ndugu yake waliyozaliwa pamoja, yaani, walikuwa pacha. Katika nchi yetu ni desturi tusiwaache wote wawili waishi, Yule aliye dhaifu huuawa.

Lakini mama alimficha Yule mtoto aliyekuwa dhaifu ambaye alizaliwa mwisho, maana alimpenda sana, na Yule mtoto ni Twala, mfalme wa sasa.

Mimi mdogo wake nilizaliwa na mama mwingine. Baba yetu aliitwa Kafa, naye alipofariki, ndugu yangu Imotu alitawala mahali pake, akazaa mtoto. Yule mtoto alipopata umri wa miaka mitatu, ukawa wakati ule wa mwisho wa vita vikubwa.

Wakati huo watu hawakupata nafasi kulima, na njaa kali iliingia katika nchi na watu wakaanza kunung’unika, wakageuka kama simba watafutao kitu cha kurarua. Ndipo alipotokea Yule mchawi mwanamke Gagula ambaye hafi kabisa, akasema, ‘Huyu mfalme Imotu si mfalme.’

Na wakati huo Imotu alikuwa amelala anaugua majeraha, amekaa katika nyumba yake hajiwezi kabisa.

Basi Gagula alikwenda katika nyumba akamtoa Twala, ndugu yake, ambaye alimficha katika mapango na miamba tokea wakati aliozaliwa, akamvua shuka akawaonyesha Wakukuana alama tukufu ya nyoka aliyochanjwa kiunoni, alama ambayo amechanjwa mwana wa kwanza kuzaliwa na mfalme, akapaaza sauti yake na kusema, ‘Tazameni, huyu ni mfalme wenu, nimemwokoa mpaka hivi leo kwa ajili yenu!’

Basi, watu ambao walikuwa kama wana wazimu kwa sababu ya njaa wakapiga kelele, ‘Mfalme! Mfalme!’Lakini mimi nilijua ya kuwa siyo mfalme, maana Imotu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa katika wale pacha, naye ndiye mfalme wa kweli.

Basi kelele zilipozidi, mfalme Imotu akatoka nyumbani ingawa alikuwa mgonjwa, ameshikwa mkono na mke wake, naye amefuatwa na mtoto wake mdogo, Ignosi, yaani kwa tafsiri yake ni ‘Umeme

Akauliza, ‘Kelele hizo za nini? Mbona mnaita ‘Mfalme! Mfalme!’ Basi hapo Twala aliyekuwa ndugu yake waliozaliwa na mama mmoja pacha, akamkimbilia akamshika nywele na kumchoma kisu cha moyo.

Na watu wote walipiga makofi na kelele, ‘Twala ni mfalme, sasa tunajua kuwa Twala ndiye mfalme’ maana walikuwa dhaifu kabisa.

Nikamwuliza Infadus. ‘Je, na Yule mke wake na mtoto Ignosi, Twala aliwaua vile vile?’ Akajibu, ‘Hapana, bwana wangu. Malkia alipoona kuwa bwana wake ameuawa alimshika mkono mtoto wake akakimbia huku analia.

Baada ya siku mbili alikwenda nyumba moja akaomba chakula, lakini kwa vile bwana wake aliyekuwa mfalme amekwisha kufa hapana aliyekubali kuwapa chakula wala maziwa.

Lakini usiku ulipoingia, mtoto mmoja mdogo mwanamke akatoka akampa chakula, mama akamshukuru Yule mtoto, akashika safari kwenda milimani kabla jua halijapanda mbinguni, na humo hakosi alipotea, maana hapana aliyemwona yeye wala Yule mtoto Ignosi mpaka leo hivi.’ Nikasema, ‘Basi, na kama huyo mtoto Ignosi yu hai, ndiye Mfalme wa kweli wa Wakukuana?

Akajibu, ‘Naam, bwana, nyoka mtukufu amechanjwa kiunoni mwake. Kama yu hai, yeye ndiye mfalme. Lakini amekufa zamani.

Tazama bwana, nyumba ile ni nyumba ambayo mke wa Imotu alionekana mara ya mwisho pamoja na mtoto Ignosi. Ndipo tutakapolala usiku, yaani ikiwa nyinyi mabwana mnalala duniani.’

Basi nikajibu, ‘Rafiki yangu Infadus, tunapokaa pamoja na Wakukuana, basi tutafuata desturi za Wakukuana.’

Basi hapo niligeuka kuongea na Bwana Good aliyekuwa anafuata nyuma amechukia sana kwa kuvaa shati tu, maana lilikuwa likipeperuka katika upepo. Nikashtuka, maana niligongana na Umbopa, nikaona kuwa alikuwa akinifuata karibu sana ili asikie maongezi ya Infadus na mimi, nikaona uso wake kama mtu anayejaribu sana kukumbuka mambo yaliyokwisha pita.
 
Kabla hatujaondoka, Infadus alikuwa amepeleka mtu kutangulia amepeleka mtu kutangulia apeleke habari mjini.

Mtu huyu alikwenda mbio sana, maana watu wote wa kabila lile walizoezwa kwenda mbio sana, Sasa tukaona matokeo ya habari alizopeleka, maana tulipokaribia mjini, tuliona vikosi vingi vya askari wakitoka katika milango ya mji.

Bwana Henry akanishika mkono akasema kuwa labda tutapokewa vibaya. Lakini sauti yake ilimwonyesha Infadus kuwa tuna shaka, akasema, ‘Mabwana wangu, msiwe na hofu, hapana hila katika moyo wangu.

Hivyo vikosi ni askari wangu mimi, nao wanataka amri yangu ili wawapokee kwa heshima.’ Tulipokaribia zaidi tuliona kuwa vikosi vimejipanga kwa safu. Kila kikosi kilikuwa na watu mia tatu, na vilikuwa vikosi kumi na mbili. Ilikuwa vizuri sana kuwatazama askari namna walivyokuja mbio na kujipanga kwa nidhamu katika mahali pao.

Tulipofika kwenye kikosi cha kwanza tuliona namna walivyokuwa wanaume. Wote walikuwa watu wazima, na hapana mmoja aliyepungua urefu wa futi sita, na wengine walikuwa futi sita na inchi nne.

Walikuwa wamejipamba na manyoya marefu meusi vichwani, na kiunoni na chini ya goti la kulia walikuwa wamefungwa mikanda meupe ya ngozi ya ng’ombe na katika mkono wa kushoto wameshika ngao ndogo ya duara. Ngao hizo zilitengenezwa kwa namna ya ajabu sana, maana viunzi vyake vilikuwa vya chuma, na juu yake imetandwa ngozi ya ng’ombe nyeupe.

Silaha zao zilikuwa mikuki mifupi, na visu vyao vilikuwa vipana kadiri ya shubiri moja. Mikuki hii haitupwi, ila hutumika kwa kumchoma adui wanapopigana karibu karibu. Tena kila mtu alikuwa na visu vikubwa vitatu.

Kisu kimoja kilichomekwa katika mkanda uliofungwa kiunoni, na viwili vingine vilichomekwa kwa nyuma ya ngao. Askari aliye hodari aliweza kuvitupa kadiri ya hatua sitini kwa shabaha kamili.

Ni desturi kuwatupia adui mfululizo wanapokaribiana.
Watu wa vikosi vyote walisimama imara kama masanamu mpaka tulipowafikia, na mara mkubwa wao aliyevaa ngoziya chui alitoa amri, na kila mtu aliinua mkuki wake na wote wakasema kwa sauti kubwa, IKoom.’

Na mara tulipokwisha pita walifuata nyuma yetu. Basi ikawa vivyo hivyo mpaka tulipokwisha kupita vikosi vyote na vyote vilifuata nyuma yetu wakikanyaga nchi mpaka ikatetemeka.

Tulipofika kwenye mji tuliona kuwa umezungukwa na handaki pana, na ng’ambo ya handaki boma la miti minene yenye nguvu limejengwa. Daraja ya kupitia iliwekwa mlangoni mwa mji, nayo iliweza kuinuliwa na kushushwa tena..

Basi tuliona kuwa mlinzi wa mlango amekwisha shusha daraja tayari, tukapita ndani. Mji ulikuwa umetengenezwa kwa mpango mzuri, maana katikati ilikuwepo njia pana na kila upande wa njia nyumba zilipangwa kwa miraba, na kila mraba ni wa kikosi kimoja.

Nyumba zilikuwa za udongo nazo ziliezekwa vizuri kwa majani. Kila nyumba ilizungukwa na baraza upana wake hatua sita, na chini ilipigiliwa na chokaa mpaka kuwa ngumu kabisa.

Wanawake wengi walikuwa wamejipanga kila upande wa njia wamekuja kututazama. Walikuwa wazuri sana. Wote walikuwa warefu na wenye maumbo mazuri. Nywele zao zilikuwa fupi za kuviringana, si za kipilipili, na midomo yao haikuwa minene sana.

Basi tulipofika katikati ya mji, Infadus alisimama mbele ya nyumba kubwa iliyozungukwa na nyumba ndogondogo, akasema, ‘Ingieni, Wana wa Nyota, mpumzike katika nyumba ndogo yetu.

Chakula kidogo kitaletwa ili msiwe na haja ya kukaza mikanda yenu kwa ajili ya njaa, asali kidogo na maziwa, na ng’ombe wawili watatu; si kingi, Mabwana wangu, lakini ni chakula.’

Nikamjibu, ‘Ahsante, Infadus, tumechoka kwa kusafiri katika dunia zilizo angani; na sasa tupumzike.’ Basi tuliingia ndani ya nyumba tukaona kuwa imetengenezwa vizuri ili kutupokea kwa heshima. Vitanda vyenye ngozi laini vilikuwa tayari, na maji ya kuoga yalikuwa yamewekwa tayari.

Baadaye kidogo tulisikia sauti za watu nje, tukaenda mlangoni na tukaona wanawali wakileta maziwa na bisi na asali katika vyungu.

Na nyuma ya wanawali tuliona vijana wanaume wanaleta ng’ombe aliyenona sana. Tulipokea zawadi, na mara kijana mmoja akatwaa kisu chake akamchinja Yule ng’ombe, na katika muda wa dakika kumi alikuwa tayari amechinjwa na kugawanywa vizuri.

Nyama iliyo bora iliwekwa mbali, na iliyobaki niliwapa askari waliokuwepo, nao wakaitwaa wakaigawanya wakasema kuwa ni ‘Zawadi ya mabwana weupe.’

Umbopa alianza kutupikia chakula katika chungu cha udongo, na mwanamwali mzuri alimsaidia. Chakula kilipokuwa tayari tulipeleka mtu kuwakaribisha Infadus na Skraga waje wale pamoja nasi. Wakaja tukakaa juu ya viti vidogo, maana Wakukuana hawakai chini kama wanavyokaa Amazulu.

Yule mzee alitupendeza sana namna alivyotuheshimu, lakini tuliona kuwa Yule kijana alitushuku, akawa anatutilia shaka.

Yeye pamoja na wenzake alistaajabu alipoona weupe wetu na uchawi wetu; lakini alipoona kuwa tuna kula na kunywa na kulala kama wanavyofanya wanadamu wengine, basi hofu aliyokuwa nayo ilianza kumtoka kidogo.

Tulipokuwa tukila, Bwana Henry akaniomba nijaribu kuwauliza kama wanazo habari za ndugu yake; lakini nilifikiri ni afadhali tungoje mpaka wakati mwingine. Baada ya kula tulikaa tukavuta tumbako, na Infadus na Skraga wakashangaa, maana Wakukuana hawakuwa na habari za matumizi ya tumbako. Tumbako inaota katika nchi yao lakini hawavuti, hunusa tu.

Halafu nilimuuliza Infadus tutaendelea lini na safari yetu? Akaniambia ya kuwa safari imekwisha fungwa nayo itakuwa asubuhi siku ya pili na tarishi amekwisha tangulia kumpa habari mfalme Twala ya kuwa tunakwenda.

Twala alikuwa anakaa katika mji wake mkubwa ulioitwa Loo. Naye alikuwa akitayarisha karamu kubwa ya siku kuu iliyokuwa katika mwezi wa juni.

Katika karamu hiyo ni desturi kwa jeshi zima kuhudhuria mbele ya Mfalme ila wale tu wanaolinda miji, na tena ndio wakati wanapohudhuria wachawi wote walio katika nchi, lakini nitasimulia habari zake zote baadaye.


Infadus alitwambia kuwa tutaondoka kutakapo pambazuka tu, na njiani tutalala usiku mmoja tu, yaani ikiwa mito haina maji mengi.

Alipokwisha kutwambia hayo, akatuaga; nasi tulilala, ila tulimweka mtu mmoja akeshe atulinde tusishambuliwe kwa ghafla. Tukajitupa vitandani tukalala usingizi mtamu.
 
SURA YA TISA

Hapana haja ya kusimulia habari za mambo yote yaliyotokea katika safari yetu mpaka kufika mji wa Loo.

Ilikuwa mwendo wa siku mbili kufuata Njia Kuu ya Sulemani iliyopita katikati ya nchi ya Wakukuana. Yatosha kusema kuwa tulipozidi kuingia katika nchi tuliona kuwa inazidi kuwa nzuri, na mashamba na nyumba zilizidi kuwa nyingi.

Miji yote ilijengwa kufuata taratibu ile iliyotumiwa katika kujenga lile kambi la askari, na kila mji ulilindwa na kikosi cha askari.

Maana katika nchi yao Wakukuana hufuata desturi ile wanayofuata Amazulu, na Wadachi, na Wamasai, yaani kila mtu mzima ni askari, na kwa hivyo nguvu zote za taifa ni tayari wakati wa vita, vikiwa vya kushambulia au kujitetea. Tulipokuwa tukisafiri tuliona askari elfu nyingi wanakwenda mbio Loo kwenye siku kuu ile ya mwaka, nao walikuwa wa kupendeza sana.

Jioni ya siku ya pili tulipumzika kidogo juu ya kilima, tukatazama chini na tukaona mji’ wa Loo katika uwanda.

Mji ulikuwa mkubwa na kuuzunguka ni mwendo wa maili tano, na kwa nje miji midogo iliyotumika kwa askari wakati wa siku kuu ilionekana. Mji ulikaa vizuri sana, na katikati yake mto ulipita uliogawanya mji sehemu mbili.

Infadus aliona kuwa tunatazama mji akasema, ‘Njia inaishia huko kwenye milima ile mitatu inayoitwa Vichawi Vitatu.’ Akaonyesha` kwa mkono mahali penyewe, Nikamuuliza, ‘Mbona inaishia hapo?’ Akajibu, ‘Nani anayejua? Milima imejaa mapango na katikati lipo shimo linalokwenda chini sana.

Ndipo wale watu wa zamani waliokwenda kupata waliyojia kuyapata, ndipo tunapowazika wafalme wetu sasa, yaani ni Mahali pa Mauti.’ Nikamuuliza, ‘Wale watu walikuja kutafuta nini?’ Akajibu, ‘Sijui, nyinyi mabwana mlioshuka kutoka nyotani hamkosi kujua.’

Akanitazama macho upande. Nadhani alijua mambo zaidi lakini hakutaka kuniambia. Nikajibu , ‘Ndiyo, umesema kweli, katika nyota twafundishwa mambo mengi. Nimesikia kuwa wazee wale wenye busara wa zamani walikuja hapa milimani ili watafute mawe yanayong’aa, mawe mazuri mno, na chuma chenye rangi ya kimanjano.’

Akasema, ‘Bwana una akili nyingi. Mimi ni mtoto tu, siwezi kuongea nawe juu ya mambo hayo. Afadhali useme na Kizee Gagula katika jumba la Mfalme, ndiye mwenye akili kama zako bwana.’ Akaondoka na mara niliwaonyesha wenzangu ile milima nikasema, ‘Mashimo ya Almasi ya Sulemani ni kule.’

Umbopa aliyekuwa kasimama anafikiria kama ilivyokuwa desturi yake, alisikia maneno yangu akasema, ‘Ndiyo, Makumazahn, almasi zipo kweli, nawe utazipata maadam nyinyi watu weupe mnapenda michezo na fedha.’

Nikamuuliza , ‘Unajuaje hayo Umbopa?’
Alicheka akasema, ‘Niliota ndoto usiku.’ Akageuka akaondoka.

Bwana Henry akasema, ‘Je, rafiki yetu ana nini? Yeye anajua mambo mengi lakini hapendi kuyasema. Hayo ni dhahiri. Lakini, Quatermain, ulimuuliza kama amesikia habari za ndugu yangu?’ Nikajibu, ‘Hajasikia hata kidogo, amemuuliza kila mtu anayemjua lakini wote wanasema kuwa hapana mtu mweupe aliyefika katika nchi hii.’


Bwana Good akasema, ‘Unadhani kama alifika hapa? Maana sisi tulifika kwa miujiza tu; yeye angaliwezaje kufika hapa bila ramani?’ Bwana Henry akasema, ‘Sijui, lakini nadhani tutamwona.’ Na sauti yake ilionyesha huzuni.

Basi jua lilishuka na giza likafunika nchi kama wingu, lakini giza halikuficha nchi kwa muda mrefu, na mara mwezi ulitoka na mbalamwezi ikazagaa kila mahali.

Tulisimama tukatazama nchi namna ilivyokuwa nzuri mno, na Infadus akaja akasema, ‘Ikiwa mabwana mmekwisha pumzika tushike safari yetu kwenda Loo, ndipo kulipotengenezwa nyumba ya kukaa usiku huu. Sasa mbalamwezi inaangaza nchi hamwezi kujikwaa njiani.’

Tukakubali, na baada ya saa moja tulikuwa tumefika mpaka wa mji, na mioto ya kambi ilikuwa haihesabiki kwa wingi wake.

Tulifika upesi kwenye daraja ya kuvukia, tukaona askari analinda zamu. Infadus alitaja neno la kujulisha kama tu rafiki, tukapita katika njia kuu ya katikati ya mji.

Baada ya mwendo wa nusu saa tulipokuwa tukipita katika majumba, Infadus alisimama mbele ya mlango uliokuwa umekabili nyumba chache zilizopangwa kuzunguka kiwanja kilichopigiliwa mawe na chokaa, akatuambia ya kuwa hizo ni nyumba zetu.
Tuliingia tukaona kuwa kila mtu amewekewa nyumba yake.

Nyumba hizo zilikuwa bora kuliko nyumba zozote tulizo ziona. Katika kila nyumba kilikuwamo kitanda kilichotandikwa ngozi zilizolainishwa na majani mabichi.

Chakula kilikuwa kimepakuliwa tayari, na mara tulipokwisha nawa mikono, wanawali wazuri walituletea nyama iliyookwa, na bisi zilizowekwa vizuri juu ya sahani za mbao, wakatupa kwa unyenyekevu.

Tukala tukanywa, kisha tukaagiza vitanda vyetu tuhamishiwe katika nyumba moja, tukajitupa vitandani tukalala usingizi wa watu waliochoka kabisa. Tulipoamka tuliona kuwa jua limekwisha panda mbinguni, na wanawali wako nje tayari wameamrishwa kuja kutusaidia tukijitayarisha kuvaa.


Bwana Good akasema, ‘Kujitayarisha nitawezaje nami nina shati moja na viatu tu! Bwana Quatermain, tafadhali waombe waniletee suruali zangu.’ Nikaomba, lakini niliambiwa kuwa zimekwisha chukuliwa kwa mfalme, naye anataka kutuona adhuhuri. Basi tuliwatoa nje wanawali wale tukajitengeneza kadiri tulivyoweza.
 
Bwana Good akanyoa tena upande wa uso wake, lakini tulimwambia asinyoe upande wa pili, maana sasa ndevu nyingi zimekwisha ota.

Tulioga tukachana nywele. Nywele za Bwana Henry zikawa ndefu sana , sasa hata zikafika kwenye mabega yake.

Tulipokwisha kufungua kinywa, tukavuta tumbako, na baadaye kidogo Infadus akaja akatwambia kuwa mfalme Twala yu tayari kutupokea. Lakini tulimwambia kuwa sisi hatuna haraka, tutangoja mpaka jua lipande juu kidogo.

Tulifanya hivi ili asije akafikiri kuwa anaweza kutuita apendavyo yeye. Basi tulikaa muda wa saa nzima tukitengeneza zawadi katika vitu tulivyokuwa navyo, yaani bunduki ile iliyokuwa ya marehemu Ventvogel, na shanga kidogo.

Ile bunduki na risasi zake tulinuia kumpa mfalme, na shanga zile tulitaka kuwapa wake zake na wafuasi wake.

Tulikuwa tumekwisha wapa Infadus na Skraga kidogo wakafurahi sana, maana hawajaona shanga namna zile. Basi baadaye kidogo tulisema kuwa sasa tupotayari, tukaongozwa na Infadus, na Umbopa aliyechukua bunduki na shanga. Baada ya kutembea hatua mia na hamsini tulifika kwenye kiwanja kama kile tulichopewa sisi lakini kikubwa zaidi.

Nyumba nyingi zilipangwa kuzunguka boma la nje, nazo lilikuwa nyumba za wake zake mfalme, Jumba kubwa lilikabili mlango wa kiwanja, nalo ndilo jumba la mfalme. Katikati ya kiwanja kulikuwa wazi yaani hapana nyumba, ila kulijaa vikosi vya askari, na askari walipata elfu saba au nane.


Askari hao walikuwa wamesimama kimya kama masanamu.
Tukapita katikati yao. Siwezi kueleza jinsi walivyokuwa wazuri. Wote walivaa manyoya vichwani, na mikononi walikuwa wameshika ngao ndogo na mikuki iliyong’aa katika mwangaza wa jua.

Palikuwa na nafasi mbele ya jumba na viti vimepangwa tayari. Infadus alituashiria, tukakaa vitini na Umbopa alisimama nyuma yetu. Infadus alisimama mbele ya mlango wa jumba.

Muda wa dakika kumi tulikaa hivi kimya kabisa, lakini tulijua kuwa macho elfu yalitutazama na ikawa ni hali ya kutisha mno, lakini tulifanya kama si kitu.

Halafu mlango wa jumba ulifunguliwa na jitu kubwa sana, likatoka. Lilikuwa limevaa ngozi ya chui begani na limefatwa na Yule kijana Skraga na kitu kilichoonekana kuwa kama nyani kimefunikwa nguo za ngozi yenye manyoya.

Lile jitu lilikaa kitini, na Yule kijana Skraga alisimama nyuma yake, na kile kitu kama nyani kikakaa kitako; ikawa kimya kabisa.

Sasa Yule mtu mkubwa alisimama akavua ngozi ile ya chui, akawa wa kutisha mno. Alikuwa mkubwa kabisa na sura yake ilichukiza kupita sura zote tulizoziona. Midomo yake ilikuwa minene mno, pua yake imebonyeka, na alikuwa na jicho moja tu linalong’aa. Jicho lingine hana ila tundu tu.

Sura yake ilionyesha ukali na uovu kupita kiasi. Kichwani alivaa manyoya ya mbuni marefu meupe, na mwilini nguo za minyororo miembamba ya chuma iliyofumwa pamoja, na kiunoni na magotini amefungwa mikia meupe ya ng’ombe.

katika mkono wa kulia ameshika mkuki mkubwa sana, na shingoni amevaa mkufu wa dhahabu, na juu ya kipaji cha uso almasi kubwa iliyong’aa sana ilikuwa imefungwa.
Hata sasa ilikuwa kimya; lakini si kwa muda mrefu, Mara Yule mtu, maana ndiye mfalme, akainua mkuki wake.

Mara ile mikuki elfu nane iliinuliwa na sauti nene nane elfu zikajibu amkio la mfalme, ‘Koom.’ Mara tatu walisema hivi, na kila mara sauti ilifanya nchi kutetemeka. Ikawa kama mlio wa ngurumo.

Ndipo tuliposikia sauti kali iliyotoka kwa Yule aliyekuwa kama nyani, ‘Mfalme Mtukufu, ni Mfalme.’ Na mara sauti kubwa zilitoka kwa askari wale elfu nane, ‘Ni Mfalme, Mfalme Mtukufu, ni Mfalme.’

Ikawa kimya kabisa tena, lakini mara askari mmoja aliyesimama upande wa kushoto ngao yake ilimtoka mkononi, ikapiga chini kwa kishindo . twala akamgeukia na kumwambia, ‘Njoo hapa wewe.’

Kijana mzuri akaja akasimama mbele yake. Twala akasema, ‘Mbwa wewe usiyeangalia, ngao yako ndiyo iliyoanguka? Wataka kuishusha heshima yangu mbele ya wageni hawa waliotoka kwenye nyota? Je, unalo la kusema?’ Yule kijana alisawajika akasema kwa sauti ndogo, ‘Sikukusudia, Ee Ndama wa Ng’ombe Mweusi .’


Twala akasema, ‘Umenifanya mpumbavu mbele za watu hawa; jiweke tayari kufa.’
Akajibu kwa sauti ndogo, ‘Mimi ni ng’ombe wa mfalme .’ Twala akasema kwa sauti kubwa, ‘Skraga, hebu nione ustadi wako wa kutumia mkuki.

Niulie huyu mbwa.’ Skraga akasimama mbele huku kakenua, akainuka mkuki wake. Yule masikini kijana akaweka mkono mbele ya macho yake, akasimama kimya. Na sisi tulikuwa kama tumegeuka mawe.
 
Skraga akapunga mkuki wake mara moja, mara ya pili, akapiga. Aah! Umempiga, umetoka upande wa pili kadiri ya futi moja.

Akanyosha mikono yake juu akaanguka, akafa. Basi yamekwisha; pale maiti amelala, nasi bado hatujatambua vema mambo yaliyotokea. Bwana Henry akaruka juu na kupiga ‘Lahaula,’ lakini mara alikaa tena, maana kila mtu alikaa kimya.

Mfalme akasema, ‘Lilikuwa pigo zuri sana. Haya, mwondoe.’ Na watu wanne wakatoka katika kikosi wakamwinua Yule mtu aliyeuawa wakamchukua. Hapo tulisikia ile sauti ndogo tena ya Yule kama nyani, ‘Futeni alama ya damu, futeni. Amri ya mfalme imetekelezwa.’

Mwanamwali mmoja akatoka amechukua chokaa katika kapu akainyunyiza juu ya alama ya damu. Huku nyuma Bwana Henry alishikwa na ghadhabu kuu; nikamzuia kwa shida asisimame, nikamnong’oneza, ‘Kaa, kaa usisimame au tutapoteza maisha yetu.’ Akakubali akakaa.

Twala alikaa kimya mpaka alama zile za damu zimekwisha futwa, ndipo aliposema, ‘Watu weupe mmetoka wapi, mmekuja kutafuta nini?’ Nikajibu, ‘Tumetoka katika nyota, usituulize kwa namna gani, Tumekuja kutazama nchi hii.’

Akasema, ‘Mmesafiri kutoka mbali ili kuja kutazama kitu kidogo. Je, na Yule ametoka katika nyota vile vile?’ (akamwonyesha Umbopa.) Nikamjibu, ‘Hakika hata watu wa rangi uliyonayo wewe wapo mbinguni; lakini Mfalme Twala haifai kuuliza mambo ambayo huwezi kuyafahamu.’

Akajibu, na sauti yake iliyochukiza sana, ‘Nyinyi watu wa nyota mnasema kwa sauti na maneno ya kiburi sana, afadhali mkumbuke kuwa nyota ziko mbali, na nyinyi mpo hapa. Je, itakuwaje nikikufanyeni kama Yule waliye mchukua?’

Nikacheka sana, lakini katika moyo wangu sikuwa na kicheko, nikajibu, ‘Ee Mfalme, tahadhari sana, nenda pole pole juu ya mawe ya moto usije ukaunguza nyayo zako; uushike mkuki kwenye mpini usije ukakukata mkono.

Ukigusa hata unywele mmoja wa vichwa vyetu utaangamia papo hapo. Je, huyu Infadus na Skraga hawajakwambia sisi ni watu gani? Umepata kuwaona watu kama sisi?’ (Nikamwonyesha Bwana Good, maana nilijua hakika kuwa hajaona mtu kama yeye.) Mfalme akamtazama Bwana Good akasema, ‘Ni kweli, sijaona.’


Basi nikaendelea nikasema, ‘Hawajakwambia namna tunavyoweza kuwaua watu kwa mbali?’ Mfalme akajibu, ‘Wameniambia, lakini sisadiki. Nataka nione kwa macho yangu ukimuua mtu. Muue mtu Yule anayepita kule, nami nitasadiki.’ Akaonyesha mtu aliyekuwa akipita upande mwingine wa mji.

Nikajibu, ‘La, sisi hatumwagi damu ya watu wasio na hatia lakini ukitaka kuona, basi amuru mtu alete ng’ombe, na kabla hajaenda hatua ishirini nitamuua Yule ng’ombe.’ Mfalme akacheka, akasema, ‘Hapana, ukimuua mtu ndipo nitakapo sadiki.’

Nikajibu, ‘Vema’ wewe nenda upite uwanjani na kabla hujafika mlangoni utakuwa maiti; au kama hupendi kwenda wewe mwenyewe, basi mpeleke mwanao Skraga.’ Basi kusikia hayo tu, Skraga akalia sana akaondoka akakimbilia nyumbani. Twala akakunja uso akasema, ‘Leteni ng’ombe.’


Mara watu wawili walikwenda mbio kuleta ng’ombe, nikamwambia Bwana Henry, ‘Sasa Bwana Henry ni juu yako kumpiga ng’ombe, maana nataka mfalme ajue kuwa si mimi tu ninayeweza kupiga bunduki.’

Basi tukakaa kimya kidogo, halafu tukaona ng’ombe anakuja mbio, na mara alipoona wale watu wengi, akasimama.

Nikamwambia Bwana Henry. ‘Haya sasa piga.’ Na pale pale akaelekeza bunduki akapiga. Mara ile ile ng’ombe alilala kafa. Basi hapo watu wote walishangaa wakazuia pumzi; nikageuka nikamwambia mfalme, ‘Je, mfalme nimesema kweli?’
Mfalme akajibu, na sauti yake ilikuwa ya mtu anayeogopa sana, ‘Ndiyo, mtu mweupe, umesema kweli.’

Basi nikaendelea nikasema, ‘Sikiliza, Twala. Umeona sasa unaweza kusadiki kuwa sisi tumekuja kwa amani wala si kwa vita. Tazama.’ Nikamwonyesha ile bunduki tuliyomletea.
‘Huu ndio mwanzi utakaokupa nguvu kuua kama sisi tunavyoua, lakini naweka sharti hii, usimuue mtu. Ukiielekeza kumpiga mtu, utajiua wewe mwenyewe.

Ngoja, nitakuonyesha. Mwambie mtu mmoja apime hatua arubaini kisha achomeke mkuki katika ardhi na bamba lake lituelekee sisi.’

Akaamuru ikafanywa, nikasema, ‘Sasa tazama utaona kuwa nitalivunja nikapiga bunduki.

Risasi ikalipiga lile bamba la mkuki likavunjika vunjika vipande. Tena watu wote walizuia pumzi kwa kushangaa, nikasema, ‘Sasa Twala, twakupa mwanzi huu, na baadaye nitakufundisha namna ya kuutumia, lakini uangalie sana usiutumie uchawi huu wa nyota kumdhuru mtu wa duniani.’


Nikampa ile bunduki. Mfalme akaitwaa kwa kuiogopa akailaza miguuni pake. Alipokuwa akiiweka, Yule kama nyani akatamani kutoka kivulini mwa nyumba. Alitambaa kwa miguu na mikono, lakini alipofika mahali alipokuwa kakaa mfalme, akasimama, akafunua uso wake ambao ulikuwa wa kutisha mno.

Alikuwa mwanamke kizee sana sana, na uso wake umekunjika mno kwa uzee hata kuwa kama uso wa mtoto mchanga wenye mikunjo mingi.

Kinywa chake kilikuwa kama ufa katika mikunjo hiyo, na chini ya ufa, kidevu chake kilitokeza kama ncha. Alikuwa na pua ndogo na kama macho yake yasingelioneka , uso wake ungalikuwa kama uso wa maiti iliyokauka kwa kuwekwa juani.


Lakini macho yake yaling’aa kama mwenye akili nyingi. Kichwa chake kilikuwa kipara, hana nywele kabisa, na ngozi ya utosini iliyokunjana ikimeta kama ngozi ya nyoka.
Mtu huyu alitufanya kutetemeka kwa hofu.

Alisimama kimya kidogo, kisha akaweka mkono wake uliokuwa na makucha marefu sana, juu ya bega la mfalme Twala, akasema kwa sauti nyembamba na kali, ‘Sikiliza, Ee Mfalme! Sikilizeni, Ee Mashujaa!


Sikilizeni, Ee milima na nyanda na mito, na nchi ya Wakukuana! Sikilizeni, Ee mbingu na jua, Ee mvua na dhoruba na ukungu! Sikilizeni, Ee wanaume na wanawake, Ee vijana na wanawali, na nyinyi watoto msiozaliwa bado! Sikilizeni, vitu vyote vyenye uhai vitakavyokufa! Sikilizeni, vitu vyote vilivyokufa vitakavyofufuka na kufa tena! Sikilizeni, nami nitabashiri. Sasa nabashiri, nabashiri!’

Sauti yake ilififia na watu wote walishikwa na hofu kuu. Kizee huyu alitisha mno. Akaendelea. ‘Damu! Damu! Damu! Mito ya damu; damu pote pote. Naiona, naisikia, naionja ina chumvi! Ni nyekundu juu ya nchi! Inanyesha kutoka mawinguni. Nyayo! Nyayo! Nyayo! Nyayo za watu weupe watokao mbali. Zinatikisa nchi; nchi inatetemeka mbele ya bwana wake.


Damu ni njema, damu nyekundu hung’aa; hakuna harufu kama harufu ya damu iliyomwagwa kwa kiasi. Simba watailamba na kunguruma, tai wataoshea mbawa zao ndani yake na watalia kwa furaha.


Mimi ni mzee! Mimi ni mzee! Nimeona damu nyingi; ha,ha.! Lakini nitaona nyingi zaidi kabla sijafa, nitafurahi. Baba zenu walinijua, na baba zao walinijua, na baba za baba zao. Nimeona watu weupe, ninajua tama zao. Mimi mzee, lakini milima hii imenipita kwa uzee. Nani aliyetengeneza Njia Kuu, niambieni?’


Nani aliyechora sanamu zile juu ya miamba, niambieni? Nani aliyeumba wale Watatu walio kimya wanaotazama shimo, niambieni?’

Akaelekeza mkono wake kuonyesha kwenye milima ile mirefu. Akaendelea, ‘Hamjui, lakini mimi najua. Walikuwa watu weupe waliowatangulieni nao watakuja hapo nyinyi mtakapokwisha kutoweka, watawaleni na kuwaaharibuni.


Ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Na hao watu weupe walijia nini? Wenye kutisha, Wenye elimu ya uchawi na maarifa yote, wenye nguvu wasiochelea! Ee Mfalme, lile jiwe linalong’aa katika kipaji chako ni nini? Mikono ya nani ilifuma nguo hizo za minyororo unazovaa kifuani, Ee mfalme?

Hujui!, ila mimi najua. Mimi, mzee, mimi mwenye busara, mimi Isanusi, Kichawi.’ Akatugeukia akasema, ‘Nyinyi watu weupe wa Nyota mnatafuta nini? Mnatafuta mmoja wenu aliyepotea?


Hayupo. Hapana mguu mweupe uliokanyaga nchi hii tangu vizazi na vizazi vilivyopita ila mara moja tu, naye alipoondoka hapa aliondoka kwenda kufa tu.

Mmekuja kuchuma mawe yanayong’aa; najua, najua; damu itakapokwisha kukauka mtayaona; lakini je, mtarudi mtokako au mtakaa na mimi?


Ha!ha!ha! Na wewe, wewe mwenye ngozi nyeusi, mwenye udaha, nani wewe, unatafuta nini? Wewe hutafuti mawe yanayong’aa wala chuma cha dhahabu, hayo unawaachia watu weupe watokao kwenye Nyota.

Nadhani nakujua; nadhani naweza kusikia harufu ya damu iliyo katika moyo wako. Haya uvue mkanda ..

Basi hapo Yule kizee akawa amepandwa na pepo akaanguka chini na povu likamtoka kinywani, akachukuliwa ndani ya nyumba.

Mafalme akasimama anatetemeka, akapunga mikono. Mara moja vikosi vyote vikaanza kutoka kwa taratibu, na baada ya dakika kumi hapakuwa na mtu ila sisi na Mfalme na watumishi wachache.

Mfalme akasema, ‘Watu weupe, ‘ninayo nia ya kuwauweni, Gagula amesema maneno ya ajabu juu yenu. Mnasemaje?’ Nikacheka nikasema, ‘Angalia, Ee Mfalme, sisi si wepesi wa kuuawa.

Umeona kufa kwa Yule ng’ombe; wataka kuwa kama alivyo Yule ng’ombe?’
Mfalme akakunja uso akasema, ‘Si busara kujaribu kumtisha mfalme.’
Nikasema, ‘Hatujaribu kukutisha, tunayoyasema ni ya kweli.

Ukijaribu kutuua basi utatutambua’ Yule mfalme akaweka mkono kichwani akafikiri, kisha akasema, ‘Nendeni kwa amani.


Usiku wa leo kuna ngoma kuu. Mtayiona. Msiogope na kudhani labda nitajaribu kuwanasa. Kesho nitafikiri juu ya habari zenu.’ Nikajibu, ‘Vema, Ee mfalme.’ Kisha tukaondoka, tukafuatana na Infadus tukaenda nyumbani kwetu.
 
SURA YA KUMI

Tulipofika nyumbani nilimwashiria Infadus aingie pamoja nasi, nikamwambia, ‘Infadus, tunataka kusema nawe.’ Akajibu, ‘Semeni, mabwana zangu.’ Nikasema, ‘Tumeona kuwa huyu Mfalme Twala ni mtu katili.’ Akajibu, ‘Ni kweli, mabwana zangu.

Nchi yote inalalamika kwa sababu ya ukatili wake. Usiku huu mtaona. Itakuwapo ngoma kuu ya kutambulisha wachawi na wengi watatambuliwa kuwa ni wachawi na kuuawa. Hapana mtu anayeweza kusema kuwa maisha yake yapo salama.

Mafalme akiwatamani ng’ombe wa mtu, au mke wa mtu, au akishuku kuwa atawashawishi watu kumwasi basi Yule Gagula mliyemwona au wanawake wengine katika wanawake wanaotambulisha wachawi, watamchagua usiku huu naye atauawa. Wengi watakufa kabla ya mwezi kufifia usiku huu.


Kila mara ni hivyo. Labda hata na mimi nitauawa. Mpaka sasa nimeokoka kwa kuwa ni hodari katika vita, nami napendwa sana na askari; lakini sijui hesabu ya siku zangu za uhai.

Nchi inaugua kwa ajili ya ukatili na maovu ya Mfalme Twala; imechoka naye na mambo yake ya kumwaga damu.’

Nikamuuliza, ‘Infadus, kwa nini watu hawamwondoi? Akajibu, ‘Mabwana zangu, yeye ndiye mfalme, na akiuawa, Skraga atatawala mahali pake na moyo wa Skraga akitawa nira itakayowekwa shingoni mwetu itakuwa nzito kuliko ile ya Twala.


Ingalikuwa Imotu hakuuawa, au Ignosi mwana wake angalikuwepo, ingalikuwa bora; lakini wote wawili wamekufa.’ Hapo tukasikia sauti; tukageuka tukaona kuwa ni Umbopa, akasema, ‘Unajuaje kuwa Ignosi alikufa?’ Yule Infadus akasema, ‘Je, namna gani we mtoto? Nani aliyekupa ruhusa ya kusema?’


Akajibu, ‘Sikiliza, Infadus, nami nitakwambia hadithi. Zamani, wakati alipouawa Mfalme Imotu katika nchi hii, mke wake alikimbia pamoja na mtoto Ignosi, sivyo?’ Akajibu, ‘Ndiyo.’
Umbopa akasema, ‘Ilisemwa kuwa mwanamke huyo na mtoto wake walikufa katika milima, sivyo?’ Infadus akasema, ‘Ndiyo.’


Umbopa akaendelea, ‘Basi ilivyo ni kuwa Yule mama na mtoto Ignosi hawakufa. Walivuka milima wakaongozwa na kabila la watu wanaotembea tembea jangwani mpaka kufika katika nchi yenye maji na majani na miti.’

Infadus akauliza, ‘Je, unajuaje hayo?’ Umbopa akajibu; ‘Sikiliza. Walisafiri mbali kwa muda wa miezi mingi mpaka kufika nchi ya watu waitwao Amazulu, nao ni ukoo mmoja na Wakukuana.

Watu hawa kazi yao ni vita, Wakakaa nao miaka mingi mpaka mama mtu akafa. Basi alipokufa, Yule mtoto Ignosi akawa msafiri tu, akasafiri katika nchi za ajabu wanapokaa watu weupe, akakaa nao miaka mingi, akajifunza maarifa yao.’


Yule Infadus akasema kwa sauti ya kutosadiki, ‘Ni ‘hadithi nzuri, lakini ya nini?’ Basi Umbopa akaendelea, akasema, ‘Miaka mingi alikaa akifanya kazi ya utumishi na uaskari, lakini katika moyo wake alikumbuka yote aliyoambiwa na mama yake juu ya nchi yake, alitamani sana namna ya kufika tena katika ile nchi, ili apate kuwaona watu wake na nyumba ya baba yake, kabla hajafa.


Miaka mingi alikaa akingoja, na halafu alipata nafasi, maana alionana na watu weupe waliokusudia kutafuta nchi ile isiyojulikana, akafuatana nao. Wale watu weupe walisafiri wakaenda mbele tu wakimtafuta mtu mmoja tu aliyepotea.


Walivuka jangwa lenye joto, wakavuka milima yenye theluji, wakafika nchi ya Wakukuana, na pale ndipo walipokuona wewe, Ee Infadus.’

Yule Infadus akashangaa, akasema, ‘Kweli, wewe, una wazimu kusema hivyo.’ Umbopa akasema, ‘Unafikiri tu hivyo; tazama nitakalokuonyesha, Ee wewe mjomba wangu. Mimi ni Ignosi, Mfalme wa haki wa Wakukuana!’

Basi hapo alifungua nguo yake akasimama uchi mbele yetu, akasema, ‘Tazameni, hii ni nini?’ Akaonyesha kiunoni mwake amechanjwa alama ya nyoka anayezunguka kiuno. Infadus akatazama, na macho aliyakodoa kwa kushangaa, kisha akampigia magoti akasema, ‘Koom!Koom!

Ndiye mtoto wa ndugu yangu; ndiye mfalme.’ Umbopa akasema.’ Umbopa akasema, ‘Ee mjomba wangu, sikukwambia hayo? Inuka; mimi sijawa mfalme, lakini kwa msaada wako pamoja na msaada wa hawa watu weupe mashujaa walio rafiki zangu, nitakuwa mfalme.


Lakini Yule kichawi Gagula alisema kweli, yaani nchi italowa kwa damu kwanza, naye damu yake italowesha nchi pia, yaani ikiwa anayo damu, kwani ndiye aliyemuua baba yangu kwa maneno yake, ndiye aliyemfukuza mama yangu. Na sasa wewe Infadus, imekupasa uchague. Utakubali kuweka mikono yako katika mikono yangu uwe mtu wangu?


Wewe utakubali kushirikiana nami katika hatari zilizo mbele yangu, na’ kunisaidia nimwangushe huyo jeuri na muuaji, au huwezi kukubali? Chagua.’


Yule mzee alikamata kichwa akafikiri, kisha akaondoka akamjia Umbopa, yaani Ignosi, akapiga magoti mbele yake akamshika mkono, akasema, ‘Ignosi, mfalme wa haki wa Wakukuana, naweka mikono yangu katika mikono yako, nami ni mtu wako mpaka kufa.


Ulipokuwa mtoto nilikupakata nakakulea, na sasa mkono wangu ulio dhaifu utapigana kwa ajili yako na uhuru.’


Umbopa akajibu, ‘Vema, ewe Infadus. Nikishinda wewe utakuwa mtu mkubwa katika ufalme wangu chini ya mfalme mwenyewe.

Nikishindwa, hapana ila kifo, na wewe tangu hapo si mbali na kufa sasa. Simama, mjomba wangu. Na nyinyi watu weupe, mtanisaidia? Je yale mawe meupe sitaweza kuwapa? Hakika nikishinda yale mawe meupe mtayaona na kuchukua kwa kadiri ya nguvu zenu. Je, mtakubali?

Nikatafsiri maneno yake, na Bwana Henry akajibu, ‘Mwambie kuwa hafahamu tabia ya Mwingereza. Mali ni njema, nayo ikitujia tutaiokota; lakini mungwana hajiuzi kwa mali. Lakini mimi binafsi nasema haya:

Tokea mwanzo nilimpenda Umbopa, na kwa kadiri ya nguvu zangu nitamsaidia. Nitafurahi sana kujaribu kumtia adabu Yule shetani mwovu Twala.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom