Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,885
Kwa ufupi
- Akizungumza juzi na waandishi wa habari jijini Washington nchini humo, Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Heather Nauert alizitaja nchi hizo kuwa Tanzania, Cambodia na Ufilipino akisema zimekuwa na matukio ya kufungia vyombo vya habari.
Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imetaja nchi tisa duniani ikidai zinanyanyasa vyombo vya habari na waandishi wa habari na kutoa wito kwa dunia kuruhusu uhuru wa maoni na utawala wa demokrasia.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari jijini Washington nchini humo, Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Heather Nauert alizitaja nchi hizo kuwa Tanzania, Cambodia na Ufilipino akisema zimekuwa na matukio ya kufungia vyombo vya habari.
Alizitaja pia nchi za Afghanistan, Burma, Cuba, Uturuki, Misri na China kwa unyanyasaji wa waandishi wa habari.
“Waandishi wa habari wanakamatwa kutokana na kazi zao katika maeneo ya Burma, Uturuki, Misri na China. Wanafamilia nao wamekuwa wakikamatwa kutokana na kazi za ndugu zao,” alisema na kuongeza:
“Mifano hii inaonyesha jinsi usalama na uhuru wa waandishi wa habari na vyombo vya habari na mazingira yao wanavyotishiwa. Tungependa kusisitiza umuhimu wa usawa na uwepo wa demokrasia ya wazi na uhuru wa maoni.”
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ndiye msemaji mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas hakupatikana kuzungumzia madai hayo kwani simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokewa. Pia, ujumbe wa maandishi kwa simu aliotumiwa haukujibiwa.
Mbali na Dk Abbas, si Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe wala msaidizi wake, Juliana Shonza waliopatikana kuzungumzia suala hilo.
Kauli hiyo ya Marekani ilitolewa Mei 3, katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo hapa nchini, wadau wa habari waligusia matukio ya utekaji wanahabari, kufungiwa vyombo vya habari na kutozwa faini kubwa kwa vyombo hivyo.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, suala la kutoweka kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda nalo lilichukua nafasi kubwa.
Azory aliyekuwa akifanya kazi wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani alichukuliwa na watu wasiojulikana wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser Novemba 2017 na hajaonekana hadi leo.
Miongoni mwa taasisi zilizotoa matamko ni pamoja na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (Misa- Tan), Muungano wa Klabu za Habari Tanzania (UTPC), Bazara la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema Serikali imefungua milango ya majadiliano na wanahari kuhusu changamoto zao.
Alisema ingawa Serikali imetoa haki ya kupelekwa mahakamani mashauri kuhusu sheria ambazo zimepitishwa, bado kuna fursa nzuri ya kufanya mazungumzo miongoni mwa wadau.