Doctor Mama Amon
JF-Expert Member
- Mar 30, 2018
- 2,056
- 2,605
Papa Francis, Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani
Papa Francis, katika mahubiri yake mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu mnamo Oktoba 10 2021, Mjini Roma, Vatican, alikazia mambo makuu matatu mintarafu Liturujia ya Neno la Mungu: Kukutana, Kusikiliza na Kung’amua.
Katika Dominika ya tarehe 10 Oktoba 2021 akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alizindua rasmi Sinodi kwa Ibada ya Misa Takatifu.
Maadhimisho haya ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu isemaayo “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”
Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu zinazoanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2023.
Awamu ya kwanza, ambayo ni kwa ajili ya parokia zote katika Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki, ni kuanzia tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi Aprili 2022.
Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi, ambayo ni kwa ajili ya Kanisa katika ngazi ya Mabara, ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023.
Awamu ya Tatu, kwa Kanisa la Kiulimwengu, itakayofanyika Vatican, ni kuanzia mwezi Oktoba 2023.
Papa Francis katika mahubiri yake mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu alikazia mambo makuu matatu mintarafu Liturujia ya Neno la Mungu: Kukutana, Kusikiliza na Kung’amua.
Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 28 ya Mwaka B wa Kanisa ilimwonesha kijana tajiri aliyemwendea Kristo Yesu mbio na kumpigia magoti, akitaka nafasi ili, aweze kusikilizwa kutokana na yale yaliyokuwa yanamsumbua moyoni mwake.
Hiki ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu anasafiri pamoja na waja wake, ili aweze kuzima kiu ya maisha na mahangaiko yao ya ndani.
Kwa waumini, uzinduzi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni muda muafaka wa kujiuliza ikiwa kama, Jumuiya ya Wakristo inamwilisha ndani mwake ule mtindo wa maisha wa Mungu wa kusafiri na wengine, au wana wasiwasi na mashaka ya kusafiri pamoja na wengine.
Huu ni wakati wa kubadili maisha na utume wa Kanisa kwa kuondokana na tabia ya kufanya mambo kwa mazoea!
Sinodi maana yake ni kutembea katika njia moja, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu alipokutana na kijana tajiri, akamsikiliza kwa makini na hatimaye, akampatia vigezo vya kufanyia mang’amuzi ili kuurithi uzima wa milele.
Kristo Yesu alikutana na kijana tajiri akiulizia jinsi ya kupata maisha ya uzima wa milele. Yesu akaonesha ari na mwamko wa kumsikiliza, kama kielelezo cha ujenzi wa ujirani mwema.
Akamwangalia, akasikiliza historia ya maisha tangu ujana wake na hatimaye, akampatia ushauri wa kufanyia mang’amuzi, ili kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha.
Injili ni mahali pa kukutana na Kristo Yesu, ili kumwinua, kumganga na kumponya mwamini!
Papa Francis anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujizatiti kikamilifu ili waweze kuwa ni wajenzi wa sanaa ya watu kukutana.
Huu ni muda muafaka wa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu. Ni wakati wa Sala, Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa kwa nyakati hizi.
Ni wakati wa kukutana na kutajirisha kutokana na karama, miito na utume. Ni makutano yanayohitaji ukweli na uwazi, ujasiri na uwepo ili kukutana na wengine.
Huu ni mwelekeo mpya unaowataka waamini kutoka katika ubinafsi na mazoea yao, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu ambaye yuko na anatembea pamoja nao katika ukweli na uwazi!
Makutano ya kweli anasema Papa Francis yanafumbatwa katika sanaa ya kusikiliza kwa makini kama alivyofanya Kristo Yesu kwa yule kijana aliyekuwa na kero kubwa moyoni mwake kuhusu maisha ya uzima wa milele.
Ni mfano wa kuweza kusikiliza kwa moyo, ili ushauri unaotolewa uweze kumweka mtu huru, baada ya kutembea naye katika safari ya maisha tangu ujana wake.
Kijana tajiri akahisi moyoni mwake kwamba, amekubalika mbele ya Kristo Yesu na wala hakumhukumu na badala yake akamwachia fursa ya kusimulia maisha yake ya kiroho! Je, Wakristo wanao ujasiri wa kusikiliza kwa moyo? Je, waamini wanatoa nafasi kwa wengine kusafiri katika imani hata katika magumu ya maisha yao?
Kila mwamini ajitahidi kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa bila kuwekewa vizingiti, kukataliwa au kuhukumiwa.
Ni wakati wa kusiliza Neno la Mungu na waamini kusikilizana wao kwa wao!
Ni muda wa kumsikiliza Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunulia njia na lugha mpya, ili kuzama katika ukweli wa mambo.
Roho Mtakatifu anawataka waamini kusikiliza maswali ya watu waliokata tamaa, matumaini ya watu na Makanisa mahalia! Mkazo ni sanaa ya kusikiliza kwa kwa makini.