Copy and paste kwa wapenda historia:
Titanic—“Meli Maarufu Zaidi katika Historia”
APRILI 10, 1912: Meli ya
Titanic inaondoka Southampton, Uingereza, ikielekea New York, Marekani.
APRILI 11: Baada ya kuwachukua abiria huko Cherbourg, Ufaransa, na huko Queenstown (ambayo sasa inaitwa Cobh), Ireland,
Titanic inaelekea kwenye Bahari ya Atlantiki.
APRILI 14: Saa 5:40 hivi usiku,
Titanic inagonga mwamba wa barafu.
APRILI 15: Saa 8:20 usiku, Titanic inazama, watu 1,500 hivi wanakufa.
MELI ya
Titanic ilikuwa ya aina gani? Ni nini kilichoifanya izame? Tunapata majibu tunapotembelea Jumba la Makumbusho la Ulster Folk and Transport, karibu na Belfast huko Ireland Kaskazini.
Titanic—Kwa Nini Ilikuwa Meli ya Pekee?
Kulingana na Michael McCaughan, aliyekuwa msimamizi wa Jumba la Makumbusho la Ulster Folk and Transport,
Titanic ilikuwa ndiyo “meli maarufu zaidi katika historia.” Lakini meli ya
Titanic haikuwa ya kipekee. Kati ya meli tatu kubwa zilizojengwa katika viwanda vya kutengenezea meli vya Harland and Wolff huko Belfast,
Titanic ilikuwa ya pili kwa ukubwa.
* Titanic ilikuwa moja ya meli kubwa zaidi za wakati huo, ikiwa na urefu wa mita 269 na upana wa mita 28.
Kampuni ya meli ya White Star iliagiza meli hizo kubwa zitengenezwe ili iweze kutawala biashara ya usafiri kwenye Bahari ya Atlantiki Kaskazini. Kampuni hiyo ya White Star Line haingeweza kuishinda kampuni ya Cunard Line katika usafiri wa kasi. Kwa hiyo, ilikazia fikira hasa kujenga meli kubwa na zenye starehe ili kuwavutia watu maarufu na matajiri.
Lakini meli ya
Titanic ilikuwa na uwezo wa kutimiza jambo lingine vilevile. “Wahamiaji 900,000 hivi waliingia Marekani kila mwaka kati ya 1900 na 1914,” anasema William Blair, msimamizi wa Majumba ya Makumbusho ya Ireland Kaskazini. Kampuni za kuwasafirisha watu kwenye Bahari ya Atlantiki zilipata pesa nyingi zaidi kwa kuwasafirisha wahamiaji hao kutoka Ulaya hadi Marekani, na
Titanic ilitumiwa kwa kusudi hilo.
Msiba
Kapteni wa
Titanic, E. J. Smith, alijua hatari zilizotokezwa na barafu kwenye Bahari ya Atlantiki Kaskazini. Alikuwa amesafiri kupitia njia hiyo mara nyingi akitumia meli ya
Olympic. Meli nyingine zilitoa maonyo mara kadhaa kwamba kuna miamba ya barafu, lakini huenda kapteni alipuuza au hakupokea maonyo hayo.
Ghafula, wenye kushika doria kwenye
Titanic walitoa onyo kwamba kuna mwamba wa barafu mbele—lakini ilikuwa kuchelewa mno! Ofisa aliyekuwa akisimamia alifaulu kuepuka kuugonga mwamba huo moja kwa moja lakini hangeweza kuzuia ubavu mmoja wa
Titanic usikwaruze mwamba huo. Hilo liliharibu ubavu wa meli hiyo na maji yakaanza kujaa ndani ya vyumba kadhaa vya mbele. Punde si punde, Kapteni Smith akaelezwa kuwa meli hiyo ilikuwa hatarini. Akatuma ujumbe wa dharura na akaagiza kwamba mashua za kuokoa uhai zishushwe.
Meli ya
Titanic ilikuwa na mashua 16 za kuokoa uhai na mashua nyingine nne za kujazwa upepo. Mashua hizo zikiwa zimejaa kabisa zingeweza kutoshea watu 1,170 hivi. Lakini meli yote ilikuwa na watu 2,200! Zaidi ya hayo, mashua nyingi ziliondoka kabla ya kujaa kabisa. Na nyingi hazikuwatafuta waokokaji waliokuwa wameruka ndani ya maji. Mwishowe, ni watu 705 tu waliookolewa!
Baada ya Msiba
Baada ya msiba wa
Titanic, wenye mamlaka wanaosimamia usafiri wa baharini waliweka sheria zilizoboresha usalama baharini. Sheria moja ilihakikisha kwamba kuna mashua za kutosha za kuokoa uhai ndani ya meli.
Kwa miaka mingi watu waliamini kwamba
Titanic ilizama haraka sana kwa sababu ilikuwa na shimo kubwa sana kwenye upande ambao uligonga mwamba. Lakini katika mwaka wa 1985, baada ya
Titanic kupatikana chini ya bahari, wachunguzi walifikia mkataa tofauti—kwamba maji yenye barafu yaliharibu vyuma vya meli hiyo na kufanya vyuma hivyo vivunjike kwa urahisi. Katika muda usiozidi saa tatu baada ya meli hiyo kugonga mwamba, ilivunjika na kuwa vipande viwili kisha ikazama, na kwa sababu hiyo, huo ukawa mojawapo ya misiba mikubwa zaidi katika usafiri wa baharini.
*