Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma timu ya wanasheria watakaokuwa Mkoani Arusha kwa siku kumi kuanzia Ijumaa Machi 28, 2025 kwaajili ya kusikiliza na kutatua migogoro ya kisheria kwa wananchi wa wilaya zote zinazounda Mkoa wa Arusha.
Akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ufadhili wa Wanasheria hao, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda wakati wa Kongamano la Miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Mkoani Arusha leo Machi 24, 2025, amesema Wanasheria hao kupitia kwenye Ofisi za Wakuu wa wilaya watahudumia wananchi wa Wilaya zote kwa gharama za Rais Samia Suluhu Hassan hivyo hakuna mwananchi atakayetozwa gharama zozote.
Kulingana na Makonda, Ujio wa wanasheria hao wa Rais Samia Suluhu Hassan unatokana na mwamko mkubwa wa wananchi waliojitokeza wakati wa Wiki ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, iliyofanyika Machi 1-7, 2025 mkoani hapa, ambapo uchunguzi unaonesha kuwa bado wapo wananchi wanyonge na wale wa pembezoni ambao bado wanaokabiliwa na migogoro na masuala mbalimbali yenye kuhitaji msaada wa kisheria.