KUKANUSHA TAARIFA YA KUKAMATWA KWA MWANDISHI DICKSON NG'HILY NA MKUU WA WILAYA YA UBUNGO
Kumekuwa na taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kumkamata mwandishi wa habari ambaye pia ni Mhariri wa biashara na Mkuu wa Kitengo cha Mtandaoni (digital) Ndugu Dickson Ng'hily kutoka Gazeti la The Guardian.
Taarifa hiyo imeeleza pia mwandishi huyo alipigwa sana na kuumizwa kwenye mkono na simu yake kuvunjiwa kioo huku sababu ikielezwa kuwa ni kupiga picha wanafunzi wa Shule ya Msingi Kwembe waliokuwa wanasoma chini ya mti. Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa mwandishi huyo alipelekwa ofisi ya Serikali ya Mtaa na baadaye kushikiliwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo anapenda kukanusha taarifa hiyo iliyoleta tahahuruki kwa wananchi na waandishi wa habari. Ukweli ni kwamba mwandishi huyo hakupigwa na mtu yeyote isipokuwa aliulizwa na Mwalimu Mkuu kwa nini anapiga picha bila ridhaa yao wala kujitambulisha.
Baada ya mwandishi huyo kukataa kutoa ushirikiano alipelekwa Ofisi ya Serikali ya Mtaa na baadaye akapelekwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kujiridhisha kama kweli ni mwandishi na ana kibali cha kufanya kazi hiyo.
Hata hivyo leo Julai 10, 2024, Mhe. Mkuu wa Wilaya alikuwa kwenye ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mburahati na hivyo hakuhusika wala kutoa amri yoyote kuhusu kukamatwa kwa mwandishi huyo.
Aidha, ni kweli kuwa wanafunzi walikuwa nje ya madarasa yao kwa ajili ya programu maalumu ya kufanya masahihisho ya mtihani wa Utamilifu (mock) Mkoa, hivyo kimsingi shule haina wanafunzi wanaosomea nje kwa kukosa madarasa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo inathamini na kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari katika kufanikisha kazi yao muhimu ya kuhabarisha Umma juu ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo, ni muhimu Waandishi wa Habari kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo katika kutimiza haki yao ya kutafuta, kuchakata na kusambaza habari.
Joina Nzali
KAIMU MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
Taarifa za nyuma kuhusu tukio hili soma bofya hapa:
~ THRDC yakemea Mwandishi wa Habari kukamatwa kwa kupiga picha Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kwembe wakisoma chini ya mti
~ Mwandishi wa Habari wa The Guardian anadai amepigwa na Walimu baada ya kupiga picha Wanafunzi wakisoma chini ya miti