Zanzibar. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwasili mjini hapa jana baada ya kumaliza ziara ya kichama katika mataifa mbalimbali ya Magharibi.
Katika ziara ya takriban wiki mbili, Maalim Seif na ujumbe wake akiwamo Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, walitembelea Canada, Marekani na Umoja wa Mataifa, jijini New York.
Maalim Seif aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, Kisauni mjini hapa saa 11 za alasiri na kupokewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.
Katika salamu zake fupi, Maalim Seif alisema ripoti ya uchaguzi iliyowasilishwa juzi kwa Rais John Magufuli na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haiwezi kuwa na jawabu la mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, kwani waliosaidia kuuvuruga ndio walewale waliojidai kuwasilisha ushahidi, jambo ambalo haliwezi kukubalika.
Alisema tatizo la Zanzibar bado lipo na dawa yake ni kuirejesha haki ya kidemokrasia ya wananchi walioamua kupitia masanduku ya kura ya Oktoba 25, 2015.
“Hili, chama cha CUF kilikwishalitolea maamuzi kupitia maazimio ya Baraza Kuu, kama mnakumbuka, nayo ni pamoja na kutoitambua Serikali ya Dk Shein na kuendelea kuikataa kwa vitendo na nafsi na pia kuendelea kudai haki ya maamuzi ya wananchi hadi pale itakapopatikana,” alisema.
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali iliyopita alisema; “kwa hili watawala wasijisumbue, wananchi hawajalala na katu hawatorudi nyuma, wewe wacha watoe tu hizo ripoti zao... msimamo wetu upo palepale”.
Kuhusu ziara yake, Maalim Seif alisema ilikuwa ya matumaini na mafanikio makubwa katika kufanikisha juhudi za kutetea na kupigania haki ya kidemokrasia ya wananchi na kwamba muda ukifika ataweka bayana zaidi mafanikio hayo.
Katika ziara hiyo Maalim Seif aliwasilisha mada ya ‘Chaguzi za Zanzibar: Haki iliyocheleweshwa’, katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa taasisi za kimataifa za taaluma za siasa, stratejia na demokrasia za NDI, IRI na CSIS za Marekani.
Vijana wa CUF walaani
Jumuiya ya Vijana wa CUF (JUVICUF), imelaani vitendo ilivyoviita vya ukiukaji wa haki visiwani Zanzibar.
Katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika jana katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF Vuga mjini hapa, vijana hao walieleza kukerwa na mkakati wa kutisha raia na kuwanyamazisha ili kupunguza kasi ya kudai haki yao ya kidemokrasia.
“Sisi Jumuiya ya Vijana ya CUF tunamuahidi Maalim Seif Sharif Hamad na ulimwengu mzima kuwa tuko pamoja naye na hatutorudi nyuma katika kuhakikisha maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya kupitia njia za kidemokrasia tarehe 25 Oktoba 2015 yanaheshimiwa,” alisema Katibu Mtendaji wa JUVICUF, Mahmoud
Sorce:Mwananchi