Stories of Change - 2022 Competition

Davidy Sabas

New Member
Sep 10, 2022
1
1
Kutatua mapengo ya kijinsia katika TEHAMA ni muhimu kwa mustakabali endelevu

"Kuwawezesha wasichana kuchagua taaluma za TEHAMA sio tu nzuri kwa wasichana na familia zao, inaweza kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ngazi ya kitaifa." - Brahima Sanou, Mkurugenzi, Ofisi ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU.

Siku moja nilipokuwa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dodoma, nilikwenda maktaba ya ndaki ya Elimu ya TEHAMA, msichana alinijia na kukaa karibu yangu na kusema kompyuta yangu haifanyi kazi, unaweza kunitengenezea? Nilipoiangalia, niligundua kuwa kuna tatizo kwenye programu ya mfumo wa uendeshaji (Operating system). Nilimsaidia na baada ya masaa kadhaa kupita aliaga na kuondoka, aliweza pia kuniachia namba yake ya simu.

Kwa kipindi kifupi tulikuwa marafiki na kugundua kwamba alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu akichukua shahada ya kwanza ya afya katika mfumo wa Habari. Nilijiuliza ni vipi mwanafunzi wa mwaka wa tatu anashindwa kusakinisha programu ya mfumo endeshi (Windows installation) kwenye kompyuta. Pia niliona kwamba idadi ya wasichana wanaosoma TEHAMA ni chini ya idadi ya wasichana katika vyuo vingine. Miaka miwili baadaye, nilienda kusoma kozi ya muda mfupi ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Computing Center (UCC), mbaya zaidi kulikuwa na mwanamke mmoja tu katika darasa la wanafunzi 15. Hali hii ilinifanya nijiulize kwanini wanawake wako nyuma sana katika elimu ya TEHAMA. Niligundua kwa namna fulani kuna tatizo mahala fulani.

Ingawa TEHAMA ni kichocheo kikuu cha ajira kwa wanawake na uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi, wasichana wengi nchini Tanzania bado hawajajumuishwa katika maendeleo ya digitali. Kama Tanzania ingekuwa na wanawake wengi walio na elimu ya TEHAMA, taifa hili sasa lingeweza kuwa lenye maendeleo makubwa. Kwa kasi ya wimbi la mapinduzi ya kiteknolojia kwa miaka ijayo, ni muhimu kwamba tujifunze kutoka kwa somo hili na kujenga nguvu kazi ya wanawake ya TEHAMA.

Hata hivyo, kuna changamoto kubwa, kwani upatikanaji wa TEHAMA na elimu inasalia kuwa ya mijini, isiyohusisha jinsia na ya gharama kubwa. Tafiti nyingi za vitabu mbalimbali vya kuhitimu vyuo vikuu nchini Tanzania zinaonyesha kuwa kiwango cha wanawake wanaohitimu kutoka vyuo vikuu na digrii zinazohusiana na TEHAMA ni cha chini sana.

Jambo hili linaonyesha taswira hasi ambayo wanawake na wasichana hawaendelei katika masomo yanayohusiana na TEHAMA, na hivyo kuishia katika uwakilishi mdogo katika taaluma za TEHAMA. Viwango vya chini vya kuhitimu huchangia idadi ndogo ya wanawake wanaostahiki kazi katika elimu ya TEHAMA, ikizingatiwa kwamba waajiri wengi wataajiri tu wataalam wa teknolojia ya dijitali ambao wana digrii ya chuo kikuu, licha ya ukweli kwamba idadi kubwa ya wahitimu wanakuwa ni wanaume.

Kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika TEHAMA nchini Tanzania ni sehemu ya tatizo la dunia nzima. Ripoti ya Jukwaa la Kiuchumi la Dunia la 2021, ilibainisha kuwa ni takriban asilimia 26 tu ya wataalamu wa akili bandia (AI) duniani kote ni wanawake, na ripoti ya UNESCO ya 2021 ilibainisha kukosekana kwa usawa wa kijinsia duniani kote kuhusiana na uwakilishi wa wanawake katika nyanja za STEM-na haswa zaidi katika Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara.

Tofauti za kijinsia katika taaluma zinazohusiana na TEHAMA nchini Tanzania zinaweza kuathiri kwa urahisi usawa wa kijinsia na juhudi za uwezeshaji wa kiuchumi katika sehemu nyingi za kazi. Maendeleo ya haraka katika teknolojia ya kidijitali yanamaanisha kuwa wahasiriwa wa kwanza ni wanawake haswa wale wenye ujuzi mdogo katika teknolojia ya kidijitali, kwa kuzingatia kwamba tayari kuna uhaba wa wanawake duniani kote katika maeneo ya kazi ya teknolojia ya kidijitali, ni wazi kuwa kuhamia kwa uchumi wa kidijitali kutasababisha kuongezeka kwa viwango vya ukosefu wa ajira miongoni mwa wanawake nchini.

Serikali ya Tanzania imeanzisha mipango mikakati kadhaa ambayo inataka kuvutia haswa wasichana zaidi kwenye kozi zinazohusiana na TEHAMA, kwa kushirikiana na shirika la Don Bosco serikali ilianzisha elimu ya kidijitali kwa kutumia kompyuta za mkononi katika shule chache za msingi kupitia mradi wa Profuturo.

Sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Wasichana katika TEHAMA ya mwaka 2022 ya “Ufikiaji na Usalama,” mipango hii nchini Tanzania inaonyesha jinsi mashirika ya ndani yanavyoweza kukuza upatikanaji salama na wa kuaminika wa intaneti, zana za kidijitali, na ukuzaji ujuzi wa TEHAMA na hivyo kuwawezesha wasichana na wanawake kustawi katika Elimu ya STEM. Mipango hii itasadia kupunguza tofauti zilizopo za kijinsia na, muhimu zaidi, kukuzaji ujuzi wa TEHAMA na hivyo kuwawezesha wasichana na wanawake kustawi kitaaluma na kiuchumi.

Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa kike katika TEHAMA 2022, Muungano wa Umoja wa Mataifa wa Mawasiliano (ITU) uliangazia haja ya kukuza nafasi za kazi kwa wasichana na wanawake katika sekta hii inayokua kwa kasi zaidi duniani. Huku dunia ikikabiliwa na upungufu wa ujuzi wa wanawake katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ndani ya miaka mitano ijayo, ITU inatarajia kutoa msukumo kwa serikali na sekta binafsi kutafuta mbinu za kuwawezesha wasichana na wanawake vijana. ujuzi wanaohitaji ili kuwa wataalamu wa TEHAMA.

Sayansi, teknolojia, na uvumbuzi ni vichochezi muhimu vya jamii yetu inayozidi kukua kimataifa na kidigitali. Hivyo basi Africa na dunia kwa ujumla zinahitaji kuungana ili kutatua mapengo ya kijinsia katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) na matumizi ya teknolojia na mgawanyiko wa kidijitali katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ili kufikia mustakabali ulio sawa na endelevu.

Iwapo mataifa kwa ujumla yatanufaika na wimbi la mapinduzi ya kiteknolojia, basi maslahi, ufikivu, na ujuzi lazima uongezeke miongoni mwa watu wote hasa wasichana wenye umri wa miaka 12- 35. Umoja wa Mataifa na washikadau nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla lazima waimarishe uwekezaji na washirikiane na mashirika ya ndani yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kiraia yaliyo katika hali nzuri ili kushughulikia masuala yaliyounganishwa ya umaskini na kanuni za kijamii za kijinsia ambazo zinazuia upatikanaji na matumizi ya TEHAMA kati ya wanawake hasa wasichana wenye umri wa miaka 12- 35.

BY: David Sabas
davidysabas@gmail.com
Tel: 0625292653
 

Attachments

  • KUWAWEZESHA WANAWAKE KUPITIA TEHAMA.pdf
    291.7 KB · Views: 1
Back
Top Bottom