Kujenga Utajiri kupitia Ardhi na Akiba

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,818
3,116
Rafiki yangu mpendwa,


Karibu kwenye mwendelezo wa masomo ya NJIA KUMI ZA KUJENGA UTAJIRI kutoka kitabu kinachoitwa THE TEN ROADS TO RICHES kilichoandikwa na Ken Fisher.


Kwenye masomo yaliyopita tumejifunza njia nane kati ya 10 za kujenga utajiri. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza njia ya tisa na ya kumi katika njia 10 za kujenga utajiri. Karibu ujifunze.


ARDHI-NA-AKIBA.jpg


NJIA YA TISA; ARDHI NA MAJENGO


Kama unapenda kujenga majengo na kukusanya kodi, basi unaweza kuwa bwana nyumba na kujenga utajiri kwa njia hiyo.


Kuwa mmiliki wa ardhi na majengo ni moja ambazo zimekuwa zinatumika na wengi kujenga na kutunza utajiri.


Hii siyo njia rahisi na wanaofanikiwa sana ni wachache kwa sababu inataka zaidi ya umiliki tu wa majengo. Lazima mtu awe na uwezo mzuri wa kibiashara ili kuendesha njia hii kama biashara.


Ukweli ni kwamba marejesho ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo siyo makubwa sana ukilinganisha na njia nyingine.


Hivyo faida pekee kwenye njia hii ya ardhi na majengo inatokana na kutumia nyenzo, yaani fedha za wengine kwenye kuwekeza na kuzalisha faida.


Hivyo yeyote anayetaka kutumia njia hii kwa mafanikio, anapaswa kuwa anapenda kutumia mikopo na fedha za wengine. Hicho ni kitu hatari ambacho wengi hawawezi wala hawapendi kutumia.


Kwa kutumia nyenzo, unaweka fedha yako kidogo na kuwezeshwa kiasi kingine, lakini faida unapata kwenye thamani nzima.


Kufanikiwa kwenye njia hii unapaswa kuwa mpiga dili mzuri na uweze kuleta vitu vitatu kwa pamoja; jengo, wapangaji na fedha. Ukiweza kuwa na njia nzuri ya kuleta vitu hivyo vitatu pamoja, yaani ukaweza kupata jengo ambalo lipo eneo zuri, ukawa na wapangaji ambao wanahitaji na ukapata fedha za kuwezesha kupata jengo hilo, umefanikiwa kwenye njia hii.


Faida kubwa ya njia hii inapatikana kwa kuweza kupangisha jengo na kuingiza fedha nyingi kuliko zinazotoka. Japo wengi huhangaika zaidi na kununua na kuuza kwa muda mfupi, lakini gharama na makato huwa ni kubwa hivyo faida inakuwa ndogo.


JINSI YA KUTUMIA NJIA HII.


Kama unapenda njia hii ya ardhi na majengo kwenye kujenga utajiri, chukua hatua zifuatazo;


1. Chagua eneo ambalo lina ukuaji wa uchumi, ambapo watu wengi wanahamia kuliko kuondoka.


2. Nunua majengo ambayo bei yake ni ya chini, ila yanaweza kuingiza fedha haraka yakiboreshwa.


3. Tumia kiasi chako kidogo cha fedha na nyenzo kuweza kununua majengo unayopata.


4. Pata wapangaji kwa wingi na hakikisha fedha inayoingia ni nyingi kuliko inavyotoka.


5. Usiuze haraka, bali shikilia kwa muda mrefu. Tumia fedha unazopata kukopa na kununua zaidi.


6. Rudia huo mtiririko kwa muda mrefu bila ukomo, ukiendelea kukuza mapato na nyenzo.


7. Endelea kutafuta wawekezaji na kukua zaidi.


NJIA YA KUMI; KUWEKA AKIBA NA KUWEKEZA KWA MUDA MREFU.


Kama upo tayari kujenga utajiri kwa njia ya taratibu, isiyokuwa na mbwembwe na ambayo ni ya uhakika, njia ya akiba na uwekezaji itakufaa sana.


Hii ndiyo njia inayotumiwa na wengi, njia inayotoa fursa kwa kila mtu kuweza kujenga utajiri, bila ya kujali ukubwa wa kipato chake.


Njia hii inahitaji muda mrefu sana ili kujenga utajiri. Japo haitoi matajiri wanaoingia kwenye orodha mbalimbali, inawawezesha watu kufikia uhuru wa kifedha kwenye maisha yao.


Hii ni njia ya ubahili na juhudi, inayotaka mtu kuwa na nidhamu kali sana ndiyo aweze kufanikiwa.


Njia hii ina hatua kuu mbili;


Moja ni kuweka akiba, hii ni lazima, kwa sababu bila akiba mengine hayawezekani.


Mbili ni kuwekeza maeneo ambayo yana ukuaji wa wastani, ambao ni wa uhakika na wenye hatari kidogo.


Kwa mtu kuzingatia hatua hizo mbili na kujipa muda mrefu, ambapo kanuni ya riba mkusanyiko inafanya kazi, kujenga utajiri kunakuwa kwa uhakika.


Kuharakisha njia hii unapaswa kuwa unaongeza kipato chako na kuongeza kiasi cha akiba na uwekezaji unachofanya.


Njia hii inawafaa watu wote ambao wanaingiza kipato kwa njia yoyote ile, iwe ni kuajiriwa, kujiajiri au kufanya biashara.


Uzuri hii ni njia ambayo inaweza kuambatana na njia nyingine katika 10 zilizoelezewa kwenye kitabu. Kwa kuingiza kipato kwenye hizo njia nyingine, kisha sehemu kubwa ya kipato hicho kuweka akiba na kuwekeza.


Kufanikiwa kwenye njia hii lazima uwe muuzaji bora na kufanya kazi kwa juhudi kubwa.


Njia hii inamtaka mtu kuanza mapema na kuwekeza kwa muda mrefu bila kuacha. Na kama mtu amechelewa, anapaswa kuwekeza kiasi kikubwa ili kufidia muda ambao mtu hakuwekeza.


Maeneo ya kuwekeza ili kunufaika na njia hii ni kwenye masoko ya mitaji. Hapo inahusisha kuwekeza kwenye HISA, HATIFUNGANI na MIFUKO YA PAMOJA. Masoko ya mitaji, hasa hisa, yana ukuaji mzuri kwa kipindi cha muda mrefu.


Katika aina zote za uwekezaji, ni uwekezaji wa hisa ndiyo wenye ukuaji mkubwa na wa uhakika zaidi kwa kipindi cha muda mrefu. Yaani zaidi ya miaka 10.


Kwa sababu ya changamoto zilizopo kwenye uwekezaji, mtu hashauriwi kuingia kwenye soko na kuwekeza moja kwa moja. Badala yake anashauriwa kufanya uwekezaji usio wa moja kwa moja kwa kutumia mifuko ya gharama nafuu inayowekeza kwenye soko zima.


Kwa kuwa uwekezaji ni wa muda mrefu, marejesho ya wastani kwa muda mrefu yanajenga utajiri mkubwa. Unapaswa kuepuka uwekezaji unaoahidi kulipa marejesho makubwa huku hatari yake ikiwa kubwa. Tumia muda mrefu kunufaika na uwekezaji wenye marejesho ya kawaida na hatari ndogo.


JINSI YA KUTUMIA NJIA HII.


Hii ni njia ya kutumiwa na watu wote, hata kama tayari unatumia njia nyingine ambazo tumeshajifunza. Ili kutumia vizuri njia hii, fuata hatua hizi;


1. Kuwa na njia ya kukuingizia kipato ambayo unaifanyia kazi na kila wakati kazana kuongeza kipato chako.


2. Dhibiti sana matumizi yako na sehemu kubwa ya kipato chako weka akiba.


3. Chagua mifuko ya pamoja yenye gharama nafuu na inayowekeza kwenye soko zima (low cost index funds) kisha wekeza kwenye mifuko hiyo.


4. Acha uwekezaji wako ukue bila ya kuuingilia, jipe muda mrefu wa uwekezaji huo kukua


5. Endelea na shughuli zako kuku, kuza kipato chako na ongeza kiwango unachoweka akiba na kuwekeza. Rudia hivyo mpaka utakapofikia uhuru wa kifedha kwa kadiri ulivyopanga.


STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA.


Kutokana na mafunzo ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI ambayo tumeendelea kuyapata, tunaona uhitaji mkubwa wa mtu kuwa na mkakati sahihi anaoufanyia kazi ili kufikia utajiri na uhuru wa kifedha.


Ni kupitia hitaji hilo tumeandaa huduma maalumu ya STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA ambayo inakupa mwongozo na usimamizi hatua kwa hatua mpaka mtu kufikia uhuru wa kifedha kwa uhakika.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Karibu uweze kusikiliza kipindi hicho ujifunze mengine mengi ambayo yapo kwenye kitabu ila hapa hayajapata nafasi. Pia usikie maoni ya wengine juu ya njia hizi za kujenga utajiri.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.


Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,


Kocha Dr. Makirita Amani,


Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi


+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com


MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 
Unajua kiongozi. Kuna sehemu moja nimesoma umeandika pia nilishaona pahala. Watu wakafanya kwa staili hiyo wamefika mbali.
 
Back
Top Bottom