Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,617
- 13,320
TAARIFA YA KUPINGA KUFUNGIWA KWA CHOMBO CHA HABARI CHA MWANANCHI DIGITAL
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania, (UTPC) unapinga vikali kitendo cha Serikali, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufungia kwa muda wa siku 30 leseni za huduma za maudhui mtandaoni za kampuni ya Mwananchi Communications Limited.
Hatua hii imezuia machapisho ya kidigitali ya gazeti la Mwananchi kuchapishwa mtandaoni kitendo ambacho kinakwenda kinyume na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata taarifa.
UTPC inaungana na wadau wengine wa habari hapa nchini kupinga vikali matumizi ya sheria zinazoruhusu taasisi moja au mtu mmoja kutoa hukumu bila kuzingatia haki ya msingi ya kusikilizwa kwa upande wa pili. Mwananchi walipaswa kupewa haki yao ya kujitetea mbele ya chombo huru cha kisheria kabla ya uamuzi wa kufungia chombo hiki kutekelezwa.
UTPC inaamini kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya kuchochoa ukuaji wa demokrasia na utawala bora na kwa maana hiyo uhuru wa vyombo vya habari unapaswa kulindwa kwa nguvu zote. Vyombo vya habari vina jukumu la kuelimisha, kuburudisha, na kuibua mijadala yenye tija kwa jamii. Kukandamiza vyombo vya habari ni kurudisha nyuma juhudi za waandishi wa habari kuuhabarisha umma lakini pia kudidimiza haki ya wananchi kupata taarifa.
Tunatoa wito kwa Serikali na TCRA kufuata taratibu za kisheria zinazotoa fursa ya chombo cha habari kujitetea mbele ya chombo huru kabla ya kutoa hukumu. Pia, tunashauri kufanyika kwa majadiliano baina ya Serikali na Mwananchi Communications Limited kwa nia ya kulinda amani na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kulinda uhuru wa vyombo vya habari.
UTPC na Press Clubs zake itaendelea kusimama kidete kutetea haki za waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini Tanzania kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa. Pamoja na hayo, UTPC inawaomba wadau wa habari wote nchini kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha tasnia ya habari inabaki kuwa salama wakati wote na waandishi wetu wanajivunia kazi wanayofanya.