Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,854
- 13,608
Mchoraji wa katuni maarufu nchini Tanzania na kimataifa ambaye pia ni mbunifu na mtangazaji wa vipindi vya redio na televisheni vyenye mvuto mkubwa kwa jamii, Bw. Ally Masoud Nyomwa anayejulikana zaidi kwa jina la Masoud Kipanya (KP), amafungua mashitaka Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Ndogo ya Dar es Salaam) dhidi ya Bw. Burton Mwemba Mwijaku anayemtuhumu kumkashifu, kumshushia hadhi na heshima yake kupitia maandishi kwenye mitandao ya kijamii.
Mahakama Kuu imepokea na kuisajili kesi hiyo tarehe 05 Agosti 2024 ikiwa ni Petitition No. 18911 of 2024 ambayo amepangiwa Mheshimiwa Jaji David Ngunyale atakayeisikiliza kuanzia tarehe 03 Septemba 2024 ambapo mdaiwa au mlalamikiwa (Bw. Burton Mwijaku) ameshapelekewa wito wa kuitwa mahakamani (summons to file written statement of defence) na kutakiwa kuwasilisha maelezo ya utetezi ndani ya siku 21 tangu alipopokea huo wito au samansi.
Bw. Masoud Kipanya amemshitaki Bw. Burton Mwijaku kwa kumkashifu kwa maandishi mnamo tarehe 04 Juni 2024 kupitia ukurasa wake wa Facebook wenye utambulisho namba 108657908847651 na kwenye akaunti yake ya Instagram aliyoandika maneno ya uongo, yenye nia ovu na kumfedhehesha yakiwemo kwamba yeye KP anafanya biashara haramu inayoharibu maisha ya vijana wengi nchini.
Aidha, Bw. Masoud Kipanya anaeleza katika hati yake ya mashitaka kwamba Bw. Burton Mwijaku aliandika kwenye akaunti za mitandao tajwa kwamba yeye KP huwazodoa na kuwadhalilisha viongozi wa nchi na serikali hususani marais kwa kuhongwa.
Bw. Masoud Kipanya amesema maneno hayo ya uongo na yenye nia ovu yaliyochapishwa mitandaoni na kusomwa na watu wengi ndani ya jamii ya Tanzania na dunani kote, yametafsiri kwamba yeye KP ni sio mtu mwenye tabia nzuri wa kupewa heshima yoyote kwani hafai, anajihusisha na biashara haramu kama dawa za kulevya au nyara za serikali au magendo. Hivyo, kipato chake kinatokana na biashara hiyo haramu na sio uchoraji katuni, utangazaji, ubunifu, ubalozi wa masuala ya jamii, ukurugenzi wa bodi za taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa.
Bw. Masoud Kipanya kupitia mawakili wake wa kampuni yenye wanasheria wazoefu wa masuala ya habari na haki za binadamu Haki Kwanza Advocates amechambua katika vipengele 15 akifafanua maana ya maandishi ya Bw. Burton Mwijaku kwa tafsiri ya watu wa kawaida ndani ya jamii kwamba yeye KP anaonekana ni mla rushwa, jambazi, tapeli, laghai, asiyeaminika, chanzo cha vijana walioharibiwa maisha yao, na kwamba hapaswi kuhusishwa katika masuala yoyote ya kijamii ikiwemo kupewa fursa na kufanya kazi na taasisi za serikali ambazo amekuwa akijihusisha nazo hasa katika elimu na malezi ya vijana mashuleni na mitaani.
Kutokana na maandishi ya kashfa ya maneno ya uongo ya Bw. Burton Mwijaku aliyenukuliwa pia kukiri kufanya hivyo mbele ya vyombo vya habari mnamo tarehe 13 Juni 2024 alipoomba radhi bila kuchukua hatua ya dhati ya kumsafisha kimaandishi Bw. Masoud Kipanya, imemuathiri kiajira, kibiashara, kimahusiano ndani ya jamii ya Tanzania kuanzia kwenye familia yake, kisaikolojia na kumshushia hadhi na heshima aliyoijenga kwa "jasho na damu" kwa zaidi ya miaka thelathini na tano (35).
Bw. Masoud Kipanya anaiomba mahakama imuamurua Bw. Burton Mwijaku nafuu kumi na mbili (12) ikiwa ni pamoja na kumuamuru Bw. Burton Mwijaku amlipe fidia ya madhara halisia (specific damages) atakayothibitisha kwa ushahidi mahakamani kutokana na kashfa hiyo ya shilingi milioni mia tano (500,000,000/-) na fidia ya madahara ya jumla (general damages) yatakayopimwa na kuridhiwa na mahakama kwa mamlaka yake ya shilingi bilioni tano (5,000,000,000/-).
KP ameomba pia malipo ya kiadhabu kwa mdaiwa yaani punitive damages na kwamba malipo ya fidia ya madhara halisia yaambatane na riba ya asilimia thelathini na moja (31%) tangu kashfa ilipotolewa yaani tarehe 04 Juni 2024 hadi utekelezaji wa hukumu utakapokamilika.
Aidha, mdai Bw. Masoud Kipanya anaiomba mahakama katika hukumu yake itamke kwamba maneno yaliyoandikwa na kusambazwa na Bw. Buton Mwijaku yalikuwa ni ya uongo, yenye nia ovu na kuharibu hadhi na heshima yake. Mahakama imuamuru Bw. Mwijaku kuomba radhi bila masharti yoyote na kuondoa mitandaoni maneno ya kashfa yaliyoandikwa na kusambazwa.
Mahakama itamke na kumuamuri mdaiwa Bw. Burton Mwijaku, mawakala. wake, wasaidizi wake na mtu mwingine yeyote aliye katika mamlaka yake kutosambaza maneno hayo ya uongo na kashfa dhidi ya mdai Bw. Masoud Kipanya ambaye ameomba pia kulipwa gharama ya kesi ikwemo ya kuajiri mawakili na nafuu nyingine ambazo mahakama itaona ni haki na zinafaa apewe.
Pia soma
- Masoud Kipanya amfungulia Mwijaku Kesi ya Madai ya Tsh. Bilioni 5 kwa kumtuhumu kufanya biashara haramu
- Mwijaku amuomba msamaha Masoud Kipanya baada ya kumtuhumu kuwa “anafanya biashara haramu” na kutukana Viongozi akiwemo Rais
----